Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - MECS Cluster Joint Mock Examinations 2022

Share via Whatsapp

MASWALI

  1. UFAHAMU
    Soma taarifa ifuatayo kasha ujibu maswali yanayofuata
    Tumeshuhudia baadhi ya ndugu wa familia moja wakiishi bila maelewano na wakati mwingine kukata kabisa kabisa mawasiliano. Hivi leo kuna familia ambazo haziwezi kuketi pamoja na kumaliza matatizo yao, na badala yake huchukua njia za vita ugomvi na hata pengine mauaji kama suluhisho la migogoro yao. 
    Kawaida maisha sio mstari mnyoofu. Kuna milima, mabonde, kona na hata mashimo. Ndiposa migogoro ni sehemu ya maisha yetu! Mara nyingi haiepukiki, isipokuwa kuipitia na kupata suluhisho. Ipo migogoro baina ya ndugu ambayo huleta kutoelewana, kukosesha amani na hata pengine kupoteza kabisa mahusiano. Ni wazi kuwa mahali popote wanapoishi watu au kufanya kazi pamoja,hapakosekani migogoro kwani hata vikombe vinapokuwa kabatini, havikosi kugongana. 
    Ukweli ni kwamba sote tunazaliwa na tabia tofauti, uwezo tofauti wa kuvumilia na hata kuamua kutenda. Katika mazingira yoyote ya kutoelewana, kiasi kikubwa cha busara, upendo, amani na imani huhitajika ili kuiondoa migogoro hiyo. Isipotafutiwa suluhisho ama utatuzi wake ukatendeka kwa jazba na chuki, migogoro ya ndugu katika familia hukua na kuzaa madhara makubwa. 
    Kuanzia utotoni au hadi uzimani, kunaweza kuwa na sababu nyingi ambazo huweza kupelekea kuleta tofauti baina ya ndugu. Kwa ujumla, ndugu ni watu unaowaamini, ambao hawatakupa kisogo.  Walakini, hii sio wakati wote. Kwa bahati mbaya ukweli umetuonyesha kuwa kuna uhusiano wa kindugu ambao huisha vibaya. Sababu kubwa zikiwa ni mazingira ambayo ndugu wameishi ambayo wakati mwingine kuna upendeleo wa mzazi kwa mtoto au watoto fulani na kuwafanya wengine wahisi wivu, kutopendwa na kutengwa. 
    Zipo sababu za kiuchumi ambapo ndugu wengine katika familia wanafanikiwa zaidi kuliko wengine na kuwa na maisha bora zaidi kuliko wengine.  Hali hii pia inaweza kuleta mfarakano kwa wale ambao hali zao ni tofauti na wengine, hasa iwapo hakukuwa na mazingira ya utangamano katika familia tangu awali. 
    Ndugu wa familia moja huzaliwa wakiwa na tabia tofauti. Kila mshiriki wa familia ana haiba na mtazamo wake tofauti katika masuala mbalimbali.  Wengine hukasirika mara kwa mara, wengine ni wakimya sana, wapo walio wakorofi  na wengine wanaopenda amani, hivyo jambo hili ni muhimu  mno kulielewa mara inapotokea migogoro ili kutamua namna ya kupata suluhisho. 
    Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba migogoro hii wakati mwingine hupelekea kuvuruga mwelekeo wa maisha ya watoto hasa wakati wa ukuaji,kwani kulingana na tofauti zao, wapo wale wanaoamua kuondoka nyumbani wakiwa bado na umri mdogo na kuhamia mitaani.
    Pamoja na migogoro kuwepo katika familia zetu ni vyema wazazi ama walezi waelewe tofauti za kifamilia zinavyoweza kuchangia mfarakano baina ya ndugu wa familia moja. Kwamba mzazi ama mlezi anapompendelea mtoto mmoja na kutokuwa karibu na mwingine, anatengeneza mazingira ya tofauti baina ya watoto wake. Ni vyema kuweka uwiano sawa baina ya watoto na familia ili kuweza kupunguza tofauti zinazoweza kujitokeza.
    1. Onyesha athari tatu za migogoro miongoni mwa ndugu katika familia. (alama3)
    2. Eleza mambo matano yanayochangia kuwepo kwa watoto wanaorandaranda mitaani kwa kurejelea kifungu.(alama5) 
    3. Malezi yanachangia migororo baina ya ndugu. Thibitisha kwa kurejelea kifungu. (alama1)
    4. Taja na ueleze mbinu nne za kimtindo zilizotumika katika kifungu. (alama4)
    5. Andika visawe vya maneno yafuatayo kama yalivyotumika  katika kifungu. (alama2)
      1. haiepukiki
      2. haiba
  2. UFUPISHO (ALAMA 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali. 
     Serikali kupitia Wizara ya Elimu imetoa mwongozo wa karo ambao unastahili kuzingatiwa katika shule za upili kufuatia hatua ya shule mbalimbali kuongeza karo kwa viwango mbalimbali.  Hatua hiyo inadhamiriwa kumkinga mzazi dhidi ya kunyanyaswa kifedha na walimu hasa ikizangatiwa kuwa gharama ya maisha imepanda mara dufu. 
    Hata hivyo, ingekuwa bora ikiwa serikali ingefanya maamuzi kwa ushirikiano na walimu wakuu maana kwa hakika suala la karo linahusu matumizi ya fedha ambayo pia huja na gharama zake. Gharama hii inatokana na ununuzi wa vitabu vya kiada na vya mazoezi, karatasi za uchapishaji mitihani, kwa kuwa wanafunzi sharti wasome na waandike. 
    Vilevile, gharama hii inatokana na ununuzi wa kemikali za kutumiwa katika maabara.  Aidha kuna gharama ya kuendesha michezo na tamasha za muziki na drama.  Wanafunzi wa shule za malazi hula na kulala na kwa sababu hiyo maamuzi ya kifedha lazima yafanywe.
     Jambo ambalo linastahili kuangaliwa kwa makini ni viwango vya kupanda kwa gharama ya maisha.  Lazima tujiulize gharama hiyo imepanda kwa kiasi gani na wapi?  Kwa kweli haiwezekani kununua kilo moja ya mahindi kwa bei hiyo hiyo Kitale, Mombasa na Turkana.  Vile vile ni muhimu kujiuliza ikiwa shule husika ni ya mashambani au ya mjini?  Kwa hivyo sharti la kifedha ni muhimu katika kuamua karo ya shule na maeneo mbalimbali nchini. 
    Pili, hebu tuangalie ikiwa shule inayohusika ni ya kiwango cha kaunti ndogo, kaunti au cha kitaifa.  Hili ni muhimu kwa kuwa hali ya masomo katika shule hizo hutofautiana.  Tofauti kuu hutokana na miundomisingi na programu za masomo zinazoendeshwa. 
    Kwa mfano, programu za kitahini, kompyuta na zinazohusu ziara huhitaji fedha nyingi.  Shule ambayo ina masomo kama vile muziki, sanaa na sayansikimu sharti zitoze karo ya juu kwa kuwa masomo hayo huandamana na gharama ya kununua vyombo na vyakula? 
    Sasa mbona fedha za ziada? Wanaotetea kupunguzwa kwa karo wanapunguza mchango wa motisha katika ufanifu wa masomo.  Ndio, baadhi ya shule hutoza karo ya juu ili kuwamotisha walimu kwa vyakula na kwa zawadi ili kuwastahi wanapopata matokeo mema.  Hali hiyo huwafanya kujikakamua kazini na kutoa huduma ya hali ya juu. 
    Fedha za ziada vile vile, hutumiwa kuwaajiri walimu wa ziada ikizingatiwa kuwa serikali haijawaajiri walimu wa kutosha.  Pia katika baadhi ya shule, wanafunzi huandaliwa vyakula spesheli tofauti na mseto wa maharagwe na mahindi almarufu ‗ ‘maram’ uliozoeleka katika shule nyingi. Ikumbukwe kuwa lishe bora ni mojawapo ya haki za kimsingi kwa watoto ambayo sharti iheshimiwe. 
    Kwa marefu na mafupi yake, serikali haipaswi kuweka viwango sawa vya karo kwa kila shule kwa maana hilo huenda likazua mgogoro wa kiutawala katika shule nyingi.  Shinikizo za kupunguzwa kwa karo inayotozwa hasa katika shule za upili zinafaa kutetewa kimantiki wala si kihisia. 
    Mambo huenda yangekuwa tofauti ikiwa serikali ingewajibika kwa upande wake kwa kuwaajiri walimu wa kutosha, kuwaongeza walimu mshahara na kuwatambua kwa zawadi wanapofanya kazi nzuri na kuwapandisha vyeo.  Hata hivyo, mgala muue na haki umpe; hatua kali zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya walimu wanaowatoza wazazi karo ya juu kupindukia ili kuendeleza maslahi yao ya kibinafsi. 
    Naamini kuwa hatua ya Waziri wa Elimu kukutana na washikadau katika sekta ya elimu kuhusu karo na uteuzi wa wanafunzi wa kujiunga na shule za upili ni ya busara na inafaa kutoa mwelekeo mzuri kuhusu masuala tata yaliyopo kwa sasa. 
    1. Kwa maneno 65 – 70, eleza mambo muhimu yanayostahili kuzingatiwa katika kutathmini viwango vya karo katika shule za upili nchini Kenya. (alama 8, 1 ya mtiririko) 
    2. Fupisha aya tatu za mwisho.(maneno 40 – 45)  (alama 7, 1 ya mtiririko)
  3. MATUMIZI YA LUGHA. ( ALAMA 40)
    1. Andika neno lenye  kikwamizo  sighuna cha ufizi, irabu ya  mbele  wastani, nazali ya midomo na irabu ya chini kati. (alama2)
    2. Eleza muundo wa silabi katika neno mbilikimo. (alama2)
    3. Tambua hali katika sentensi ifuatayo.
      Vyungu vya aina hii vyafinyangwa na huyu.  (alama1)
    4. Tunga sentensi zifuatazo. (alama2)
      1. Arifu
      2. Rai.
    5. Tunga sentensi moja yenye kiwakilishi cha A-unganifu, kitenzi kishirikishi kipungufu na kijalizo. (alama2)
    6. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya udogo. (alama2)                                                              
      Mbuzi wake amekata kamba akaingia shambani na kula mahindi.
    7. Andika katika usemi wa taarifa (alama2)
      “Wanasiasa hawa wenu wakipigana hivi wataharibu  nchi” Rais alisema
    8. Changanua sentensi kwa jedwali. (alama4)
      Jirani aliyenisaidia juzi ataondoka mwakani.
    9. Onyesha yambwa katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
      Alawi alifumiwa mkeka mzuri na shangaziye kwa miyaa.
    10. Eleza tofauti ya kisarufi ya maneno yaliyopigiwa mstari. ( alama 2)
      1. Duka la mwalimu limechomeka.
      2. Duka la mwalimu limechomeka,
    11. Tunga sentensi  kuonyesha wakati ujao ,hali ya mazoea. (alama 2)
    12. Tumia neno pongezi katika sentensi kama (alama 2)
      1. Nomino
      2. Kihishi
    13. Eleza matumizi ya „na‟ katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
      Ridhaa  na  Mwangeka  walikuwa  wameketi  karibu  na  jumba  la  kifahari  walipoitwa  na Apondi.
    14. Andika sentensi zifuatazo upya kulingana na maagizo.                                                         
      1. Mwana mwadilifu huwaletea wazaziwe fahari.
        (Badilisha neno lilopigiwa mstari kuwa nomino.)
      2. Nyota wengi waliipamba anga usiku huo.
        (Tumia nomino ya jamii badala ya maneno yaliyopigiwa mstari.)
      3. Makokha ni mkakamavu.Onyango ni mkakamavu pia.
        (Unganisha iwe sentensi moja yenye kihusishi cha kulinganisha.)
      4. ‘Kibali, nionyeshe ulipoandika zoezi hilo.’ Mwalimu alisema.
        (Tumia kiwakilishi nafsi badala ya nomino pekee.)
    15. Kwa kutunga sentensi, onyesha ngeli mbili za neno ‘upwa’  (alama 2)
    16. Andika maana mbili zinazojitokeza katika sentensi hii.  ( alama 2)                                                                           
      Selume alimsimulia Ridhaa kisa chake. 
    17. Tunga sentensi moja kubainisha maana mbili za neno : (alama 2)
      kina  
    18. Rubani ni kwa ndege,………………..ni kwa meli na ……………..ni kwa matwana. ( alama 2)                                        
  4. ISIMU JAMII ( ALAMA 10)
    Wewe ni mtaalamu wa maswala ya usalama. Umepewa fursa kuhutubia warsha inayojumuisha maafisa wa usalama kutoka katika vikosi mbalimbali kuhusu jukumu lao katika kudumisha usalama,amani na maridhiano nchini.
    1. Taja sajili ambayo utatumia kisha ueleze sababu ya jibu lako. ( alama2)
    2. Andika huku ukifafanua vipengele vinane vya kimtindo utakavyotumia kufanikisha mazungumzo yako. (alama 8)


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

  1.      
    1.      
      1. kutoelewana
      2. kukosekana kwa amani
      3. kupoteza mahusiano kabisa
    2.      
      1. kukosa imani miongoni mwa ndugu
      2. mazingira wanamozaliwa
      3. mapendeleo ya wazazi kwa mtoto au watoto fulani yanayowafanya wengine kuwaonea wivu wenzao
      4. kutopendwa na wazazi
      5. kutengwa 
      6. tofauti za kiuchumi miongoni mwa ndugu kuzua mfarakano
      7. tofauti za kuzaliwa miongoni mwa ndugu 
    3. mzazi au mlezi hupendelea mtoto mmoja na kutokuwa karibu na mwingine hivyo kutengeneza mazingira ya tofauti kati ya watoto wake.
    4.    
      1. takriri – kabisa kabisa
      2. nidaa - ... maisha yetu!
      3. jazanda/sitiari – milima/mabonde/mashimo – kumaanisha mambo mbalimbali magumu ya maisha.
      4. msemo – vikombe vinapokuwa kabatini havikosi kugongana
      5. nahau – hawatakupa kisogo
      6. tanakuzi – utotoni hadi uzimani
    5.    
      1. haiepukiki- haikwepeki/ haihepeki
      2. haiba – tabia/ mwenendo/mzoea/desturi
  2.         
    1.      
      1. Kushirikiana na walimu wakuu. 
      2. Gharama ya vitabu, karatasi za uchapishaji wa mitihani.
      3. Ununuzi wa kemikali katika maabara. 
      4. Gharama za kuendesha michezo na tamasha za muziki.
      5. Gharama ya shule za malazi.
      6. Kupanda kwa gharama ya maisha. 
      7. Maeneo yapatikanapo shule.
      8. Kiwango cha shule.
      9. Programu za kitathmini shuleni / mfumo wa masomo katika shule husika 
      10. gharama ya kununua vyombo vinavyohitajika katika masomo haya
      11. Motisha ya walimu na wafanyakazi wengine. 
      12. Kuwaajiri walimu wa ziada. - Gharama ya lishe bora.     
        (hoja zozote 8, alama 8, 1 ya mtiririko) 
    2.      
      1. Serikali haipaswi kuweka viwango sawa vya karo kwa kile shule. 
      2. Hili huenda likazua mgogoro wa kiutawala. 
      3. Shinikizo la kupunguzwa karo katika shule ya upili zinafaa kutetewa kimantiki na wala si kihisia.
      4. Serikali ingewajibika kwa kuwaajiri walimu wa kutosha. 
      5. Walimu wangeongezewa mshahara, kuwazidi na kuwapandisha vyeo. 
      6. Hatua zichukuliwe dhidi ya walimu wanaowatoza wazazi karo ya juu.
      7. Hatua ya waziri wa Elimu kukutana na washikadau katika sekta ya elimu ni ya busara. 
      8. Hii inafaa kutoa mwelekeo mzuri kuhusu maswala tata yaliyopo kwa sasa. 
        (hoja zozote 5x1 = alama 5)
  3.    
    1. Sema ( 2/0)
    2. Mbi- kki, li-ki, ki-ki, mo-ki (2/0)
    3. Vyungu vya aina hii vyafinyangwa na huyu.  
      hali ya  a/ hali isiyodhihirika
    4.    
      1. Mama alininunulia kitabu cha Kiswahili.
      2. Tafadhali nipe hicho kikombe. (2X1)
    5. Wa mwalimu ni mchoyo(maneno yawe matatu pekee) (2/0)
    6. Kibuzi chake kimekata kikamba kikaingia kijishambani na kula vihindi
      au
      Kijibuzi chake kimekata kikamba kikaingia kijishambani na kula vijihindi (2/0)
    7. “Wanasiasa hawa wenu wakipigana hivi wataharibu nchi” Rais alisema
      Rais alisema kuwa/kwamba ½  wanasiasa hao ½  wao1/2  wangeendelea ½ kupigana hivyo1/2  wangeiharibu ½ nchi ( ½   x 6)
    8. Jirani aliyenisaidia juzi ataondoka mwaka ujao.
      S
      KN KT
      N s T E
      Jirani Aliyenisaidia juzi ataondoka Mwaka ujao
    9. mkeka mzuri-tendwa/kipozi, 
      Alawi-tendewa/kitondo, 
      miyaa-ala/kitumizi. 
    10.      
      1. La mwalimu- ni kivumishi
      2. la—kihusishi. ( 2x1)
    11. Mama atakuwa akipika chakula.( 1x2)
    12.    
      1. Alipewa pongezi nyingi aliposhida Tuzo.
      2. Pongezi! Mama alimwambia mwanawe. ( 2x1)
    13. Ridhaa  na  Mwangeka  walikuwa  wameketi  karibu  na  jumba  la  kifahari  walipoitwa  na Apondi.
      Ridhaa na Mwangeka—pamoja na/kiunganishi.
      Na jumba---- mahali/ kihusishi cha mahali
      Na apondi—Na ya mtenda ( 3x1)
    14.      
      1. (Badilisha neno lilopigiwa mstari kuwa nomino.)
        Uadilifu wa mwana huwaletea wazaziwe fahari.
        Mwadilifu huwaletea wazaziwe fahari.
      2. (Tumia nomino ya jamii badala ya maneno yaliyopigiwa mstari.)
        Thurea ya nyota iliipamba anga usiku huo.
      3. (Unganisha iwe sentensi moja yenye kihusishi cha kulinganisha.)
        Makokha ni mkakamavu kama/sawa na/zaidi ya/kuliko/ kumpiku/ kushinda Onyango.
      4. (Tumia kiwakilishi nafsi badala ya nomino pekee.)
        ‘Wewe,nionyeshe ulipoandika zoezi hilo.’Mwalimu alisema.
        (4x1)
    15.      
      1. upwa (U-U) : Upwa wake Mwangemi  ulimsalimisha mbele ya ami yake.
        upwa (U-ZI) : Upwa wa Ziwa Viktoria hauzuriki kwa kujaa maji yanayofurika.
      2. wapwa(A(yu) - WA) : Wapwa wake Juma walimnunulia gari
    16. Selume alimsimulia Ridhaa kisa chake.
      kisa cha Selume
      kisa cha Ridhaa  (zozote mbili 2 x 1=2)
      kisa cha Mtu mwingine
      ili Ridhaa asikilize
      kwa niaba ya Ridhaa
    17. kina 
      Kina-Urefu wa kwenda chini.
      Kina-silabi za sauti namna moja
      Kina-neno la kueleza watu wenye uhusiano wa kiukoo
      Kadiria sentensi ya mwanafunzi
    18. Wewe ni mtaalamu wa masuala ya usalama. Umepewa fursa kuhutubia warsha inayojumuisha maafisa wa usalama kutoka katika vikosi mbalimbali kuhusu jukumu lao katika kudumisha usalama,amani na maridhiano nchini.
  4.        
    1. Sajili ya kitaaluma/Mazungumzo rasmi
      Hotuba kwa wataalamu,maafisa wa usalama
    2.       
      1. Nitatumia msamiati maalum
      2. Nitatumia sentensi fupifupi/ndefu ndefu ili kutoa maelezo
      3. Nitatumia lugha rasmi ya Kiswahili
      4. Nitatumia lugha sanifu
      5. Nitatumia lugha ya heshima, mabibi na mabwana
      6. Nitatumia lugha shawishi
      7. Nitatumia lugha ya ushauri
      8. Nitatumia lugha ya tasfida kuficha makali ya msamiati
      9. Nitachanganya na hau kuhamisha msimbo
      10. Nitatumia msamiati wa kutoholewa/maneno ya kukopwa kuakisi maendeleo ya kiteknolojia na zana za kivita.
      11. Nitataja na kunukuu takwimu kwa kutoa ushahidi.
      12. Nitatumia ishara 
      13. Nitatumia lugha ya kuwapa matumaini. 
      14. Nitatumia takriri ili kusisitiza mambo muhimu.
      15. Nitatumia kiimbo kuhalisi hisia tofauti tofauti 
        Tanbihi:
        Ama mwanafunzi atoe ufafanuzi wa kina au mfano ili atuzwe alama 1 kwa kila hoja.
        Jumla hoja 8 x 1 = 8
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - MECS Cluster Joint Mock Examinations 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?