Kiswahili Questions and Answers - Form 2 Mid Term 1 Exams 2023

Share via Whatsapp
Maagizo:  
 • Jibu maswali yote katika karatasi hii.
 1. INSHA (ALAMA 20)
  Andika insha itakayodhihirisha maana ya methali kuwa mpanda ngazi hushuka.
 2. UFAHAMU (ALAMA 15)
  Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yote.

  “Mimi nilizaliwa  Dodoma,” Amina alianza kusimulia kale yake. “Babangu alikuwa mtu mwenye nafasi yake.  Alikuwa na cheo na ulwa katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Kila alipoenda sisi aila yake tulienda naye. Tulikuwa tumetononoka si haba mpaka adawa ilipozuka baina ya wazee wetu.”
  Kimya kikapita kitambo huku akianza kusonga nywele. Alikuwa nadhani anavuta kumbukizi za awali yake. “Nini kisa na maana ya adawa hiyo?”  Nikauliza.  “Mama hakudiriki kumzalia baba mtoto wa kiume,” aliendelea Amina. “Tulikuwa mabinti watano. Basi ugomvi ukashitadi. Mwishowe baba alipohamishwa toka Tanga hadi  Kampala, mtengo ukajiri. Baba akaoa mke mwingine na dada zangu wote wakaenda naye. Mimi nilistahabu kufuatana na mama hata Dodoma. Huko naye akaolewa na jitu jingine.”
  “Wamwita jitu kwani?”   “Jibaba la kambo hili!” Amina alisema kwa hamaki. Akaamka na kuanza kuduruduru chumbani. “Lilikuwa fedhuli na lenye ukware wee! Nakwambia lilinikalia mguu wa kausha katika kila jambo.” Amina akarudi kuketi. “Hivi unionavyo ningekuwa nimeolewa, tena kwa nemsi,” aliendelea.
  “Nilikuwa nimempata mchumba mmoja Mkenya. Tulipendana chanda na pete. Alikuwa mwalimu wa lugha ya Kiingereza katika sekondari moja kule Dodoma. Nakwambia alikuwa anautema Umombo kama ambaye kazaliwa huko kwenyewe. Basi wacha lile jitu liupinge uchumba wetu. Likadai ati haikuhalisi niolewe na mtu wa kabila na taifa jingine.  Mchumba wangu Onyango akarudi kwao Ukwala. Nasikia alipata nyumba huko.” Amina alisita kusonga nywele akaanza kufikicha macho. Haikosi kajitonesha kidonda.
  “Siku moja,” Amina alisema kwa sauti iliyopwelewa na huku kashika tama kwa jitimai, “Mama alienda safari Sumbuwanga kumwona kakake. Akaniacha nyumbani na lile jitu. Nilikuwa tunda bichi sijadokolewa hata na ndege. Lile afriti lenye vitimbi vishindavyo vya Firauni! Usiku ulipoingia likajitoma chumbani mwangu. Kuzinduka usingizini n’kakuta limejitupa kitandani. N’kajaribu kufurukuta lakini wapi! Likanilazimisha kutenda tendo lisilofikirika. Wallahi siwezi kulisamehe hapa duniani wala akhera.” Machozi yalianza kumchirizika.
  “Lo! Alibwaga zani huyo bwana,” nilidakia.  “Pole Amina pole.”  “Niliingiwa na wazimu au mahoka sijui,” alisema Amina baina ya kwikwi za kilio. “Lo! Mama na binti kukaangiwa kwenye kaango moja! Maisha yalikosa maana. Yakawa sawasawa na ganda tupu la yai. Matumaini hakuna. Heshima hakuna. Miiko hakuna. Unyama umewatoka wanyama na kuwaingia wanadamu. Hakuna asokuwa mbwa koko au pakashume. Nikaamua kuja hapa Mombasa kuishi unionavyo hivi. Pana ajabu gani? Kwani bahari mimi nimeitia chumvi?”
  Amina alikuwa sasa mtenzi wa yote katika mchezo mbaya usiojua mipaka wala staha. Lakini nilivyompima nilimwona hakufaa kuingia katika uwanja huo. Alikuwa na moyo wa huruma na utu wema. Kama si kwa fadhila zake nisizoziamkia wala kuzilalia, mambo yangeniendea tenge chomboni. Kisha akaamua kunikirimia na kunipa mahali pa kulala hadi keshoye. Alikuwa mwema. Alinidokezea kuwa alikuwa hajawahi kurudi Dodoma kwa miaka mitatu mtawalia. Aliingia ukahaba akiwa mdogo hata ubwabwa haujamtoka shingoni. Halafu akasikia habari ya kifo cha babake wa kambo aliyemtenda kitendo.
  Maswali
  1. Kwa mujibu wa kifungu taja matatizo yanayowakumba vijana. (al 5)
  2. Ni nii maana ya “Unyama umewatoka wanyama na kuwaingia wanadamu” kwa kurejelea kifungu ulichosoma. (al 2)
  3.  
   1. Je, baba mzazi wa Amina alidhamini watoto wa jinsia gani? (al 1)
   2. Fafanua jibu lako. (al 2)
  4. Eleza maaana ya msamiati ufuatao kama ulivyotumika katika kifungu (al 2)
   1. Aila
   2. Adawa
  5. Vifungu vifuatavyo vina maana gani kwa mujibu wa kifungu. (al 3)
   1. Tulipendana chanda na pete
   2. Kajitonesha kidonda
   3. Tunda bichi sijadokolewa hata na ndege
 3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
  1. Taja  vipasuo viwili vya mdomo (alama 2)
  2. Taja sifa tatu bainifu za sauti zifuatazo. (alama 3)
   1. /o/
   2. /sh/
  3. Andika maneno yenye miundo ifuatayo ya silabi (alama 2)
   1. I-I
   2. KKKI-KI
  4. Weka nomino zifuatazo katika ngeli mwafaka (alama 2)
   1. Ukuta
   2. Manukato
  5. Ainisha viambishi katika neno lifuatalo. (alama 3)
   Amekuchezea
  6. Eleza maana ya mzizi (alama 2)
  7. Tunga sentensi kudhihirisha dhana tatu za kiimbo (alama 3)
  8. Weka shadda katika maneno yafuatayo. (alama 2)
   1. Darasani
   2. Pazuri
  9. Kanusha sentensi  ifuatayo; (alama 2)
   Waliwapiga na kuwafukuza.
  10. Sahihisha sentensi ifuatayo katika njia tatu. (alama 3)
   Huko alipoenda mna utulivu.
  11. Akifisha sentensi ifuatayo (alama 3)
   nitawapa kazi leo alasiri mwalimu alisema
  12. Andika sentensi ifuatayo katika wakati ujao. (alama 1)
   Wewe ulifanya kazi kwa bidii.
  13. Taja kwa kigezo cha muundo aina tatu za sentensi. (alama 3)
  14. Tumia ‘o’ rejeshi katika sentensi zifuatazo. (alama 2)
   1. Somo ambalo hupendwa nchini ni Kiswahili.
   2. Ufisadi ambao unachunguzwa umezidi.
  15. Tunga sentensi mbili  kuonyesha matumizi ya ritifaa. (alama 2)
  16. Tambua nomino katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
   Baba yangu atawania uongozi mwezi wa Agosti.
  17. Andika sentensi ifuatayo kwa udogo. (alama 2)
   Ng’ombe wa nyumba yetu amekula mboga.
 4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
  1. Eleza dhima ya lugha ya Kiswahili. (alama 5)
  2. Taja na kufafanua kwa kifupi kaida tano za lugha. (alama 5)
 5. FASIHI SIMULIZI (ALAMA 15)
  1. Taja vipera vitano vya utanzu wa hadithi (alama 5)
  2. Taja sifa za mtambaji bora wa hadithi.  (alama 5)
  3. Tofautisha kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi (alama 5)


MARKING SCHEME

 1. INSHA (ALAMA 20)
  Mpanda ngazi hushuka.
  Hii ni insha ya methali.
  Mtahiniwa anapaswa kutunga kisa ambacho kinaoana na maana ya methali hii.
  Maana ya methali hii ni kuwa mtu anaweza kuwa amepanda ngazi kimaisha halafu baadaye akaporomoka. Kwa mfano, mtu anaweza kuwa na cheo kikubwa kazini lakini hatgimaye akaporomoka kihadhi.
  Kisa kionyeshe pande mbili za methali.
  Mtahiniwa atoe maelezo ya kutosha kuonyesha kwamba mhusika fulani kweli alipanda ngazi, yaani alipata cheo kikubwa. Pia atoe maelezo ya jinsi mhusika huyo alivyoshuka ngazi, kwa mfano, akafutwa kazi.
  Kisa kinaweza kuonyesha hali zifuatazo:
  1. Kuwa tajiri mkubwa lakini baadaye ukwasi kuisha na kuwa mkata.
  2. Kupanda mamlaka lakini baadaye kushushwa hadhi.
 2. UFAHAMU (ALAMA 15)
  Majibu
  1. Kwa mujibu wa kifungu taja matatizo yanayowakumba vijana. (al 5)
   1. Kukosa malezi ya wazazi wanapotalakiana
   2. Kubakwa na baba wa kambo
   3. Wachumba wao kukataliwa na wazazi
   4. Kupoteza matumaini na kujikosea heshima
   5. Dhiki za kisaikolojia baada ya dhuluma
   6. Kufiwa na wazazi
   7. Kufanya kazi ya ukahaba
  2. “Unyama umewatoka wanyama na kuwaingia wanadamu” (al 2)
   • Baba wa kambo kumbaka binti yake. Ikawa mama na binti wamekaangiwa kwenye kaango moja.
  3.  
   1. Je, baba mzazi wa Amina alidhamini watoto wa jinsia gani? (al 1)
    • Kiume
   2. Fafanua jibu lako. (al 2)
    • Anamtaliki mkewe kwa kukosa kumzalia mtoto wa kike. Alikuwa na mabinti watano, mwishowe anaoa mke mwingine Uganda.
  4. Eleza maaana ya msamiati ufuatao kama ulivyotumika katika kifungu (al 2)
   1. Aila. - Familia
   2. Adawa  - doa/dosari
  5. Vifungu vifuatavyo vina maana gani kwa mujibu wa kifungu. (al 3)
   1. Tulipendana chanda na pete – Tulipendana sana
   2. Kajitonesha kidonda – kajikumbusha machungu ya awali yaliyomuumiza
   3. Tunda bichi sijadokolewa hata na ndege – hawahi kuguswa/ alikuwa bikira
 3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
  1. Taja  vipasuo viwili vya mdomo (alama 2)
   • /p/ na /b/
  2. Taja sifa tatu bainifu za sauti zifuatazo. (alama 3)
   • /o/ nyuma kati viringwa
   • /sh/ kikwamizo, si ghuna cha kaakaagumu
  3. Andika maneno yenye miundo ifuatayo ya silabi (alama 2)
   1. I-I  u-a
   2. KKKI-KI mbwe-ha
  4. Weka nomino zifuatazo katika ngeli mwafaka (alama 2)
   1. Ukuta U-ZI
   2. Manukato YA-YA
  5. Ainisha viambishi katika neno lifuatalo. (alama 3)
   Amekuchezea
   • A-me-ku – viambishi awali
   • Chez – mzizi
   • e-a – viambishi tamati
  6. Eleza maana ya mzizi (alama 2)
   • Ni sehemu ya kimsiingi katika neon yenye kubeba maana kuu na ambayo haibadiliki.
  7. Tunga sentensi kudhihirisha dhana tatu za kiimbo (alama 3)
   • Taarifa.  Mama ameenda sokoni.
   • Swali . Utarudi saa ngapi?
   • Mshangao. Kumbe, wewe ni polisi!
   • Ombi. Tafadhali nipe maji.
  8. Weka shadda katika maneno yafuatayo. (alama 2)
   1. Dara’sani
   2. Pa’zuri
  9. Kanusha sentensi  ifuatayo; (alama 2)
   Waliwapiga na kuwafukuza.
   • Hawakuwapiga wala kuwafukuza
  10. Sahihisha sentensi ifuatayo katika njia tatu. (alama 3)
   Huko alipoenda mna utulivu.
   • Huko alikoenda kuna utulivu.
   • Hapo alipoenda pana utulivu
   • Humo alimoenda mna utulivu
  11. Akifisha sentensi ifuatayo (alama 3)
   • “Nitawapa kazi leo alasari,” mwalimu alisema.
  12. Andika sentensi ifuatayo katika wakati ujao. (alama 1)
   Wewe ulifanya kazi kwa bidii.
   • Wewe utafanya kazi kwa bidii
  13. Taja kwa kigezo cha muundo, aina tatu za sentensi. (alama 3)
   1. Sentensi sahili
   2. Sentensi ambatano
   3. Sentensi changamano
  14. Tumia ‘o’ rejeshi katika sentensi zifuatazo. (alama 2)
   1. Somo ambalo hupendwa nchini ni Kiswahili.
    • Somo lipendwalo nchini ni Kiswahili
   2. Ufisadi ambao unachunguzwa umezidi.
    • Ufisadi uchunguzwao umezidi
  15. Tunga sentensi mbili  kuonyesha matumizi ya ritifaa. (alama 2)
   • Kuonyesha sauti king’ong’o: Ng’ombe Yule atakamuliwa jioni.
   • Kuonyesha silabi iliyoachwa: Mtoto ‘meenda kulala
   • Kuonyesha silabi iliyotiliwa mkazo: Ka’lamu hiyo ni yangu
  16. Tambua nomino katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
   Baba yangu atawania uongozi mwezi wa Agosti.
   • Baba- kawaida
   • Uongozi - dhahania
   • Mwezi- kawaida
   • Agosti - pekee (zozote tatu 1x3)
  17. Andika sentensi ifuatayo kwa udogo. (alama 2)
   Ng’ombe wa nyumba yetu amekula mboga.
   • Kigombe cha kijumba chetu kimekila kiboga
 4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
  1. Eleza dhima ya lugha ya Kiswahili (alama 5)
   1. Hutumiwa katika mawasiliano
   2. Kiswahili hutambulisha jamii
   3. Huhifadhi utamaduni wa jamii
   4. Husaidia kutatua mizozo
   5. Hutumiwa katika biashara hivyo hukuza uchumi
   6. Hutumika katika maendeleo ya dini, kama katika mahubiri
   7. Hutumiwa katika sanaa, kuleta burudani/ huburudisha
   8. kuimarisha utangamano katika jamii/ Linguafranka
   9. Humaliza ukabila
  2. Taja  kaida tano za lugha. (alama 5)
   1. Cheo
   2. Tabaka
   3. Mada
   4. Madhumuni au lengo
   5. Muktadha wa mazingira
   6. Hali ya mtu
   7. Idadi ya lugha azijuazo mtu
   8. Uana/jinsia
   9. Malezi
   10. Uhusiano baina ya wahusika
   11. Wakati
   12. Mandhari (zozote tano)
 5. FASIHI SIMULIZI (ALAMA 15)
  1. Taja vipera vitano vya utanzu wa hadithi (alama 5)
   1. Ngano za mazimwi
   2. Hurafa
   3. Hekaya
   4. Ngano za mtanziko
   5. Ngano za usuli
   6. Ngano za mashujaa
   7. Ngano za kimafumbo
   8. Mighani
   9. Visakale
   10. Visaasili (zozote tano)
  2. Taja sifa za mtambaji bora wa hadithi.  (alama 5)
   1. Awe na uwezo wa kutumia lugha kwa ufasaha
   2. Awe mcheshi
   3. Awe mfaraguzi
   4. Ashirikishe hadhira 
   5. Huelewa utamaduni na lugha ya hadhira yake
   6. Matumizi mazuri ya jukwaa
   7. Uwezo kubadilisha toni na kiimbo kulingana na hali tofauti anazoigiza
  3. Tofautisha kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi (alama 5)
   1. Fasihi simulizi huhifadhiwa akilini ilhali fasihi andishi huhifadhiwa kwa maandishi
   2. Fasihi similizi huwasilishwa kwa hadhira hai ilhali fasihi andishi kwa maandishi. Hadhira haionani ana kwa ana na mtunzi
   3. Fasihi simulizi ina hadhira tendi ilhali fasihi andishi ina hadhira tuli
   4. Hadhira ya fasihi simulizi ni pana ilhali ya fasihi andishi ni finyu
   5. Fasihi simulizi hubadilika kimaudhui na kimtindo kutegemea fanani ilhali faishi andishi haina nafasi ya mabadiliko hadi toleo jipya likapotelewa.
   6. Fasihi simulizi ni kongwe kwani ilianza pamoja na binadamu ilhali fasihi andishi ilianza badaa ya kubuniwa kwa maandishi.
   7. Fasihi simulizi ni mali ya jamii husika ilhali fasihi andishi ni mali ya mtu binafsi. 

Download Kiswahili Questions and Answers - Form 2 Mid Term 1 Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Join our whatsapp group for latest updates
Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest