Kiswahili Paper 3 Questions And Answers - Form 3 Term 2 Opener Exams 2021

Share via Whatsapp

KISWAHILI
KARATASI YA TATU
MTIHANI WA KWANZA WA MUHULA
MUHULA WA PILI

MAAGIZO

  • Jibu maswali Manne pekee. Swali la kwanza ni la Lazima.
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki, yaani; Fasihi Simulizi, Riwaya na Ushairi.
  • Usijibu maswali Mawili kutoka Sehemu moja.
  • Maswali yote yajibiwe kwa lugha ya Kiswahili.
  1. SEHEMU YA A:TAMTHILIA
    Lazima: K. Pauline, Kigogo
    1. Majoka alitumia njia nyingi kudhibiti uongozi wake. Thibitisha ukweli huu. (alama 20)

  2. SEHEMU B: RIWAYA
    K.Matei: Chozi la Heri
    Jibu swali la 2 au 3
    1. Wanawake wamesawiriwa kwa mtazamo chanya katika jamii ya chozi la Heri. Jadili ukweli huu kwa kutoa ithibati mwafaka. (alama. 20)
    2. “Ni mara ngapi mimi na babako husafiri na kukupagaza ulezi wa ndugu zako hawa? …umeweza kumuelekeza… katika kipindi hiki ambacho anatafuta utambuaji. Wewe pekee ndiwe dawa ya hasira … ya kivolkano. Bila wewe malezi ya hawa wadogo wako yangekuwa magumu.”
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      2. Tambulisha mbinu tatu za sanaa zilizotumika katika dondoo hili. (alama 3)
      3. Eleza sifa sita za mhusika “babako” aliyerejelewa katika dondoo hili. (alama 6
      4. “Ulezi ni ujima”. Thibitisha kauli hii kwa kurejelea dondoo hili na riwaya yote kwa jumla. (alama 7)

  3. SEHEMU YA C: USHAIRI
    Jibu swali la 4 au 5

    1. Soma shairi hili kisha ujibu maswali.

      Jicho, tavumiliaje, kwa hayo uyaonayo?
      Kicho, utasubirije, maonevu yapitayo
      Kwacho, lijalo na lije, nimechoka vumiliyo
      Naandika!

      Moyo, unao timbuko, maudhui tuyasikiayo
      Nayo, visa na mauko, wanyonge wayakutayo
      Kwayo, sina zuiliko, natoa niyahisiyo
      Naandika!

      Hawa, wanotulimiya, dhiki wavumiliayo
      Hawa, mamiya mamiya, na mali wazalishayo
      Hawa, ndo wanaoumiya, na maafa wakutayo
      Naandika!

      Hawa, sioni wengine,kwao liko angamiyo
      Hawa, uwapa unene, watukufu wenye nayo
      Hawa, bado ni wavune, kwa shida waikutayo
      Naandika!

      Bado, wawapo mabwana, wenye pupa na kamiyo
      Bado, tafauti sana, kwa pato na mengineyo
      Bado , tuling’owe shina, ulaji pia na moyo
      Naandika!

      Maswali
      1. Shairi hili laweza kuwekwa katika bahari zipi? Thibitisha kila jibu lako (ala4)
      2. Eleza dhamira ya mshairi (ala2)
      3. Onyesha mifano miwili ya uhuru wa kishairi jinsi ulivyotumika katika shairi (ala2)
      4. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari. (al.4)
      5. Tambulisha kwa mifano mbinu zozote mbili za sanaa katika shairi. (ala2)
      6. Fafanua sifa za kiarudhi zilizotumika katika ubeti wa tano. (al.3)
      7. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika shairi. (ala3)
        1. Zuiliko
        2. Wavune
        3. Wenye pupa na kamiyo.

    2. Soma shairi hili kisha ujibu maswali.

      Amka!
      Uondoe utandu machoni
      Uone mtandao duniani
      Uchawi wa karne hii
      Uunganishavyo watu.

      Amka!
      Uwe mtu mpya
      Uabiri mtandao ulimwenguni
      Ukuvushe milima na mabonde
      Ujuane na watu.

      Amka!
      Uwe na yako anwani
      Udhibiti wavuti mkononi
      Uone na uonekane kote
      Uzungumze na watu
      Ufurahie malimwengu

      Amka!
      Uone huu ulimwengu
      Ulivyofanywa mdogo sasa
      Ulivyopea kimawasiliano
      Unganike na watu.

      Amka!
      Ukalie tarakilishi
      Uangaze usioyajua
      Uwasiliane kwa meme
      Uunganike na watu.

      Amka!
      Uone nukulishi
      Ubebe yako rununu
      Useme na ulimwengu
      Useme na watu

      Maswali
      1. Lipe shairi hili anwani mwafaka. (al. 2
      2. Shairi hili ni la aina gani? Thibitisha. (al.2
      3. Andika maneno manne yanayotaja teknolojia ya kisasa. (al.2
      4. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha ya nathari. (al.4
      5. Eleza toni ya shairi hili. (al.2
      6. Tambulisha nafsi neni na nafsi nenewa. (al.2
      7. Tambulisha kwa mifano mbinu mbili za lugha katika shairi hili. (al.2
      8. Ni nini maana ya vifungu vifuatavyo kama vilivyotumika katika shairi. (al.4 )
        1. Uchawi wa karne katika shairi
        2. Ukavushe milima na mabonde

  4. SEHEMU YA D: FASIHI SIMULIZI
      1. Eleza sifa nne za kimtindo zinazopatikana katika methali za Kiswahili. (alama 8)
      2. Eleza mbinu tatu ambazo hutumiwa kuzua misimu. (alama 6)
      3. Ni jukumu la jamii kudumisha fasihi simulizi. Dhihirisha. (alama 6)

MARKING SCHEME

MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

  1. Njia alizotumia Majoka kudhibiti uongozi wake
    1. Majoka anatumia vyombo vya habari kufanya matangazo yake: mwezi mzima wa kusherehekea uhuru pamoja na kuzaliwa kwake bila kujali watu watakula nini wasipofanya kazi.
    2. Majoka anapanga mauaji ya wanaompinga. Ajali iliyosababisha kifo cha jabali, kiongozi wa chama cha Mwenge, (Uk. 35).
    3. Majoka anatumia Vyombo vya dola( askari) kuwafurusha waandamanaji pamoja na kuwaangamiza. Vijana watano waliuawa wakati wa maandamano.
    4. Anatangaza kuwa maandamano ni haramu huku akiwataka polisi kutumia kutumia nguvu zaidi. Kenga anasema, “Tangaza kuwa maandamano ni haramu, kisha uwaamuru maafisa wa polisi watumie nguvu zaidi.”
    5. Anapanga kutumia wahuni kunyamazisha watetezi wa wachuuzi wa Sagamoyo. Kenga anataka kumwangamiza Tunu anaposema, “Lazima tuwawekee vidhibiti mwendo na hatimaye tuwakomeshe kabisa.”
    6. Anatoa amri ya kuwazuia wahisani wa wapizani wake kwa kudai kuwa Sagamoyo ina uwezo wa kujitegemea. Majoka anasema, “Na hawa wafadhili wao nao lazima wavunje kambi zao. Sagamoyo twajiweza.”
    7. Majoka anatoza kodi zaidi ya inavyohitajika. Wachuuzi wanalipa kodi na kitu juu yake. Anaongeza mishahara ya walimu na wauguzi lakini anaongeza kodi kwa asilimia kubwa.
    8. Wasamoyo hawapewi uhuru wa kumchagua kiongozi wanaomtaka. Anapanga kuwa mtoto wake Ngao Junior atatangazwa kuwa mrithi wake.
    9. Majoka anazima uhuru wa vyombo vya habari. Anatoa amri ya kufungwa kwa Runinga ya Mzalendo kwa kutangaza moja kwa moja maandamano yaliongozwa na Tunu.
    10. Anawaamrisha askari kuwatawanya waandamanaji kwa vitoa machozi na risasi.
    11. Anamrisha lini watu watazikwa:Majoka anaagiza Chopi kuhakikisha maiti ya Ngurumo imezikwa siku hiyo hiyo kabla ya jua kutua kwani hataki kilio wakati wa sherehe.
    12. Majoka anafuga chatu, nyoka hatari na wenye sumu kali ambao huzunguka na hata kuwaangamiza Wasagamoyo ovyo. Ngao Junior na Ngurumo wanaangamizwa na chatu.
    13. Kutoa amri za kikatili:Katika siku ya kusherehekea uhuru, Majoka alimtaka mkuu wa polisi, Bwana Kingi kuwapiga risasi Tunu na Sudi kwa kuandaa mkutano nje la Soko la Chapakazi.
    14. Propaganda:Nyimbo za kizalendo zinachezwa katika redio baada ya matangazo maalum ni njia mojawapo ya kuwafumba macho Wanasagamoyo. Nyimbo hizi zinalenga kuwafanya wananchi kuona kuona kuwa Majoka anaendeleza demokrasia.
    15. Kutumia vikaragosi: Ngurumo pamoja na walevi wenzake wanaimba wimbo wa kumsifu Majoka kule mangweni.
    16. Kutumia uongo:Jamii ya Majoka inaeneza uongo kuwa wapinzani wote ni watu ambao si wazaliwa wa jimbo la Sagamoyo na wanapaswa kuhama. (Uk 51-52).
    17. Kutoa chatu kama kafara: Baada ya kifo Ngurumo, Majoka anamweleza Chopi kuwa lazima chatu mmoja atolewe kafara ili watu wajue kuwa usalama upo.
    18. Kutumia wahuni kueneza uvumi:Majoka anatumia wahuni kueneza uvumi kuwa Sudi na Ashua ndio wanaowinda nafsi ya Tunu.
    19. Kuchagua mashauri kutoka familia: Mashuri wake mkuu Bwana Kenga alikuwa ni binamu yake. Alikuwa nanamtumia kushawishi wasagamoyo kama Sudi ili wakubali matakwa yake.
    20. Kumia vitisho:Alitishia Tunu, Sudi na Ashua walipoenda ofisini mwake.
    21. Kupanga mauaji ya wapinzani: Majoka anapanga njama ya kuua Tunu ingawa kwa bahati yake Tunu, Chopi aliyepewa maagizo hakuyatimiza ipasavyo. Majoka na Kenga wanakubaliana kumuua Chopi ili asitoe siri zao.
    22. Kuwaua wapizani wake: Majoka alishiriki kwenye njama za kumuua Jabali ambaye aliuawa kwa ajali.
    23. Kuwazawadi wafuasi wake: Kenga alikuwa amegawiwa kipande cha ardhi katika soko la chapakazi. Mkewe Ngurumo mama Pima alipewa kibali cha kuuza pombe haramu.(Zozote 20x1)

  2. Mtazamo chanya wa wanawake
    1. Amekengeuka: Terry anamwonya Ridhaa mumewe kutoshiriki imani za kishirikina maana zilimtia wasiwasi bure.
    2. Wasomi: Wanawake waliosoma ni kama: Apondi, Neema, Bi.Tamasha, Tamira, Umulkheri, mamake Zohali.
    3. Wapenda masomo: Tila, Chandachema, Mwanaheri, Tuama, Rehema, Pete. Hata kama wengine hawakuweza kuendelea na masomo.
    4. Wavumilivu:Mwekevu kustahimili matusi ya wanaume na kutengwa na wanawake alipokuwa anapigania uongozi. Chandachema kuvumilia mengi baada ya kifo cha nyanyake.Neema alivumilia kero za wanajamii waliomwonea kwa kukosa mtoto.
    5. Faraja katika ndoa/mwamba katika ndoa: Licha ya mwangeka kuwa na jumba kubwa na kuishi na babake alihitaji mtu “…alihitaji mtu wa kumpembeja, kumliwaza…mwenzi katika uzazi na malezi (uk.110). Ridhaa anamhimiza Mwangeka kuoa tena. Kiriri alimsihi Annete asiondoke na kumwacha pweke. Lunga alikufa baada ya mwaka mmoja wa kuachwa na Naomi.
    6. Mwenye bidii kazini: Mwekevu alitia bidii kazini mwake akiwa mkurugenzi wa shirika la Chemichemi. Kwa bidii yake watu walipata maji ya visima.
    7. Mwenye bidii masomoni: Umulkheri alitia bidii masomoni na kuwa mhandisi. Wengine kama Neema, Apondi walitia bidii masomoni na kupata ajira.
    8. Mwenye bidii ya kupata riziki na kukimu familia: Mamake Kairu alifanya biashara yake ya kuuza samaki. Halua mkewe Shamsi licha ya ugumu wa maisha alijibidiisha kupata riziki.
    9. Amewajibika kama mzazi: Mamake Tindi na Lemi aliwaruhusu kwenda matembezini lakini akawaonya wasichelewe kurudi nyumbani. Walipokosa kurudi alienda kuwatafuta. Mamake Kairu alihakikisha mtoto wake ako shuleni na kusoma licha ya ukosefu wa fedha.
    10. Amewajibika kazini: Selume hangeondoka hospitalini baada ya zamu yake kabla ya kumtembeza muuguzi mwenzake (Meko) kwa wagonjwa.
    11. Amewajibika katika kuwadhibu watoto: Mamake Mwangeka na mamake Mwangemi waliwadhibu wana wao kwa kumuiga babu yao.
    12. Mcha Mungu: Wanawake katika makundi mbalimbali ya kidini walihusika pakubwa katika ugavi wa chakula cha msaada kwa wahasiriwa wa vita vya baada ya uchaguzi. Walikuwa wa CWA, Women’s Guild, Mothers Union. Lily Nyamvula alikiri kuwa mwokovu (born again) na hakutaka mumewe kufanya kazi ya uanajeshi.
    13. Watumishi wa Mungu kwa kuwa watawa: Mtawa Pacha, Cizarina na Anastacia ni watawa waliotumikia Mungu kila siku bila kuolewa.
    14. Wakarimu/wahisani:Wanawake wajane walikuwa wameanzisha makao ya watoto mayatima ya Jeshi la Wajane wa Kristu. Waliwapa hifadhi watoto wenye mahitaji kama Chandachema.
    15. Viongozi: Mwekevu alichaguliwa kama kiongozi wa Wahafidhina. Tamasha alikuwa Mwalimu mkuu wa shule ya Kilimo. Mamake Zohali alikuwa mwalimu mkuu wa shule ya upili.
    16. Msiri: Mamake Kipanga hakumweleza mwanawe kuhusu babake. Mamake Sauna hakumwambia kwa muda mrefu kuwa Maya hakuwa babake mzazi.
    17. Jasiri: mamake Kairu aliongoza wanawe kumzika mwanawe aliyefia mgongoni. Mwekevu alipigania uongozi kwa ujasiri mkubwa.
    18. Mwenye utu: Wanawake kadhaa wameonyesha utu kwa kuwasaidia waliokuwa na mahitaji. Wao ni kama: Nyanyake Chandachema, Neema, Apondi, Mwalimu Dhahabu n.k.
    19. Msamehevu: Umulkheri pamoja na nduguze walimsamehe mama yao Naomi na kuamua kumtafuta.
    20. Hatibu mzuri: Rachel Apondi alitoa hotuba nzuri ili kuwahimiza walinda usalama kuwajibika zaidi.
    21. Wenye adabu njema/busara: Selume aliongea akiwa mbali kabla ya kuingia kibanda cha Kaizari kwenye kumjulia hali mkewe na binti zao. Alijua kuwa vibandani hakukuwa na faragha.(Zozote 20x1)
  3.    
    1. Muktadha (al. 4)
      1. Maneno haya yalisemwa na Rachel Apondi. Alikuwa akimwambia mtoto wake wa kupanga Umulkheri. Walikuwa katika hoteli ya Majaliwa walipokuwa wakisherehekea siku yake Umu ya kuzaliwa. Apondi anamshukuru Umulkheri kwa kuchangia katika ulezi wa dadake Sophie aliyekuwa mwepesi wa hasira.
    2. Mbinu tatu za lugha (al.3
      1. Swali la balagha “…kukupagaza ulezi wa ndugu zako hawa?”
      2. Istiari-Ndiwe dawa ya hasira
      3. Utohozi-Kivolkano (volcano) (3x1)
    3. Sifa za Mwangeka (al. 6
      1. Mcha Mungu: Anashukuru Mungu baada ya kupata Umu ambapo anaona ni binti wa kufidia mwanawe Becky aliyekufa kwa ajali ya moto.
      2. Mvumbuzi:Anavumbua gari kwa jina Ngokoo ambalo Mwangeka anadai ndilo lilikuwa ka kwanza la Kiafrika.
      3. Mwenye ukiwa na upweke: Anaishi kwa ukiwa na upweke nyumbani kwake kutokana na kifo cha mkewe na mtoto.
      4. Mwenye msimamo thabiti:Licha ya kushawishiwa na mkwewe aache kazi ya uanajeshi kwa kuwa inahusisha uuaji, haachi kamwe.
      5. Mzalendo:Anadhihirisha uzalendo wake kwa kutaka kuwahudumia watu wengi katika udumishaji wa amani kama mwanajeshi katika Mashariki ya kati.
      6. Mwenye bidii:Anasoma kwa bidii mpaka akajiunga na chuo kikuu na kusomea shahada ya uhandisi.
      7. Mwenye mapenzi ya dhati kwa babake na mtoto wake wa kupanga Umulkheri: Anamkumbatia babake kwa mapenzi baada ya kuwasili kwa ndege katika uwanja wa kimataifa wa Ndege wa Rubia.
      8. Mtambuzi: anatambua kwamba babake amezeeka zaidi na kushabihiana na babu yake Mwangeka, Mzee Msubili.
      9. Mtundu: Kwa utundu wa kitoto ananyang’anywa babake stethoskopu na kuitia katika shingo ya yeye Mwangeka, kisha anamlaza babake kama mgonjwa ili amtibu.
      10. Mwenye wasiwasi alipokuwa mdogo: Ana mashaka na udhaifu kutokana na kutokuwepo na babake Ridhaa alipokuwa ameenda katika shughuli za kimatibabu.
      11. Mlezi Mwema: Akishirikiana na Mke wake Apondi wanamlea Umulkheri, Sophie na Ridhaa na kumsomesha hadi anafanikiwa.
      12. Mkarimu: alionyesha ukarimu mkubwa sana kwa Umulkheri. Aidha baada ya Dick naye kupatikana, Mwangeka na mkewe walimtunza pia kama mwana wao.
      13. Mdadisi: Kabla ya kujenga jumba lake alifanya utafiti wa kutosha kuhusu ardhi aliyotaka kununua. (6x1)
    4. Ulezi ni ujima
      1. Ulezi ni ujima inamaanisha kuwa ulezi ni wa watu wengi wakishirikiana; kwa ujumla si wa mtu mmoja au wazazi pekee. Yaani kila aliyewajibika anapaswa kuchangia. ( Tanbihi:Mwanafunzi aonyeshe isipokuwa mzazi mtoto alilelewa na watu wengine)
      2. Umulkheri alilelewa na mamake Naomi kwanza. Baadaye anachukuliwa kama mtoto wa kupanga na Mwangeka na Rachel Apondi ambao wanamlea na kumsomesha.
      3. Umulkheri aliwalea dadake Sophie na kumshauri wakati wazazi wake walikuwa wamesafiri. Ulezi huu ulisaidia kudhibiti hasira za Sophie.
      4. Chandachema alilelewa na jirani Satua kwa muda mfupi. Baadaye akatunzwa na nyanyake. Nyanyake alipoaga akajikuta akillelewa na Tenge na mke wake Kimai. Mwishowe alijipata katika makao ya watoto ya Jeshi la Wajane wa Kristu akilelewa na wasimamizi wa shirika hilo.
      5. Zohali alilelewa na wazazi wake na alipotoroka nyumbani alilelewa na Mtawa Pacha aliyemtoa katika aibu ya kukaa mitaani.
      6. Sauna alilelewa na mamake na baba wa kambo Maya bila kujua kuwa si babake mzazi.
      7. Mwaliko alilewa na dadake Umu baada ya mamake kuondoka.Baadaye akalelewa na watawa wa Benefactor kama Anastacia. Mwishowe akalelewa na Mwangemi na mkewe Neema.
      8. Mwangeka na Mwangemi waliadhibiwa na babu yao Mwimo msubili kwa sababu ya kumuiga. Babu anahusika na malezi ya wajukuu wake na kuwaadabisha.
      9. Mwalimu Dhahabu alichangia kaika ulezi wa mwanafunzi wake Umu. Alimshauri awe makini darasani. Pia alimkutanisha na wazazi wake wa kupanga.
      10. Pete alilelewa na nyanyake baada ya wazazi wake kutengana kwa sababu baba alisingizia kuwa si mtoto wake kwani hafanani naye.
      11. Cynthia analelewa na Neema baada ya wazazi wake kufariki. Anamlea kama mtoto wake.
      12. Riziki Immaculata, kitoto kilichookotwa na Neema kikiwa kimetupwa njiani kinapelekwa katika makao ya watoto ya Benefactor na kuanza kulelewa na Mtawa Cizarina. (7x1).
  4. Ushairi
    1. Tarbia -Lina mishororo minne katika kila ubeti
      Msuko -Kibwagizo kimefupishwa
      Ukara -Vina vya nje vinatiririka katika beti zote ilhali vya ndani havitiririki.
      Kikwamba -Katika beti 3-5 neno moja ndilo linaanza kila mshororo.
      Sakarani -Kuna bahari kadhaa katika shairi.
    2. Kuwahimiza watu (hasa wanyonge) wainuke na kupinga maovu na maonevu wanayofanyiwa na matajiri wenye uwezo.
    3. Inkisari km vumuliyo-kuvumilia manaandika.
      Mazida kurefusha k.m angamiyo,vumiliyo n.k
      Tabdila k.m mamiya dadala ya mamia
    4. Hawa wanaotulimia wanavumilia dhiki
      Wao ni wengi na ndio huzalisha mali.
      Wao ndio wanaoumia na kupata mateso/taabu
      Wanayokumbana nayo.Ninaandika /ninasema
    5. Takriri-hawa,bado,mamiya.
      Balagha-uyaonaje?
      Inkisari-Hawa,ndo
      Kinaya watukufu wenye nayo
    6. Kuna mishororo minne
      Kuna vipande vitatu katika mishororo ya kwanza mitatu na kimoja katika kibwagizo
      Vina vinatiririka/vinafanan
      Mizani
      2,-6-8
      2-6-8
      2-6-8
      4
    7.    
      1. Cha kunizuia /kizuizi/kizingiti/uogozi/hofu/pingamizi
      2. Wachovu/dhaifu/hafifu
      3. Walio na tama kubwa /walafi/mabwanyenye
  5. Ushairi
    1. Anwani mwafaka:
      • Teknolojia
      • Teknolojia ya kisasa
      • Njia mpya ya mawasiliano
      • Usasa katika kuwasiliana
    2. Shairi hili ni huru kwani halizingatii arudhi: (2x1)
      • Mishororo imetofautiana katika beti mbalimbali. Mf. Ubeti 3 unamishororo 6
      • Mizani inatofautiana katika mishororo katika beti mbalimbali
    3. Andika maneno manne yanayotaja teknolojia ya kisasa:( 4x1/2)
      • Mtandao
      • Wavuti
      • Tarakilishi
      • Nukulishi
      • Rununu
      • Meme
    4. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha ya nathari.
      • Mshairi anasema kuwa tuzinduke tupate kunufaika kwa matumizi ya nukulishi. Tubebe simu za mikononi ili tuwasiliane na ulimwengu wote wa watu uliomo.
    5. Eleza toni ya shairi hili. (al.2
      • Toni ya kuamrisha. Anaarisha watu wazinduke na kutumia teknolojia.
    6. Eleza nafsi neni na nafsi nenewa. (al.2
      • Nafsi neni-mweledi wa teknolojia/mwenye ujuzi wa teknolojia ya kisasa.
      • Nafsi nenewa-mtu mpya/asiye na ufahamu mpana wa teknolojia
    7. Mbinu za lugha
      • Jazanda-Uchawi wa karne(uvumbuzi wa ajabu)
      • Takriri-Amka, useme
    8. Maana ya vifungu vifuatavyo:
      • Uchawi wa karne -uvumbuzi/ uundaji wa mambo mapya ya kiteknolojia katika karne hii.
      • Ukavushe milima na mabonde-Uweze kuwasiliana na wengine ulimwengu kote (pembe zote za dunia/walio mbali)
      • Uwasiliane kwa meme-Uwasiliane kwa barua iitwayo meme kwa kutumia mtambo wa talakilishi.
  6. Fasihi simulizi
    1. Eleza sifa nne za kimtindo zinazopatikana katika methali za Kiswahili.(alama 8)
      1. Takriri:urudiaji wa maneno
        • Bandu bandu huisha gogo
        • Haraka haraka haina Baraka
      2. Taswira (picha)
        • Njia mbili zilimshinda fisi
        • Paka akiondoka panya hutawala
      3. Sitiari:mithilisha kitu kimoja na kingine moja kwa moja
        • Mgeni ni kuku mweupe
        • Ujana ni moshi
      4. Kejeli/dhihaka
        • Uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti
        • Maskini akipata matako hulia mbwata!
        • Balagha:maswali yasiyohitaji jibu kwa vile jibu ni bayana
        • Umekuwa mumumenye kuharibikia ukubwani?
        • Pilipili usiyoila yakuashiani?
        • Angurumapo samba mchezo ni nani?
      5. Tashbihi:ulinganisho kwa kutumia kilinganishi
        • Mapenzi ni kama majani popote penye rotuba hujiotea.
        • Jambo usilolijua ni kama usiku wa kiza.
      6. Kweli kinzani:hali inayopingana
        • Mpanda ngazi hushuka.
        • Kuinamako ndiko kuinukako
      7. Chuku:maneno yasiyo ya kweli
        • Polepole za kobe hufikisha mbali.
        • Ukiwa makini utayaona macho ya konokono
      8. Kinaya;kinyume na matarajio
        • Ngoja ngoja huumiza matumbo
      9. Tashihisi/uhaishaji/uhuishaji
        • Sikio la kufa haliskii dawa
        • Siri ya mtungi muulize kata {Zozote 4x2.sifa alama 1mfano1
    2. Eleza mbinu tatu ambazo hutumiwa kuzua misimu. (alama 6)
      1. Kutumia tanakali-neno mtutu-Bunduki/ hali ya kuachilia risasi
      2. Utohozi wa maneno
        • Gava - Government.
        • Hedi - Head
        • Fadhee - Father
      3. Maneno ya kawaida kupewa maana mpya
        • Toboa - faulu
        • Chuma - Bunduki
      4. Matumizi ya tabdila
        • Njaro - Ndaro
      5. Kufupisha maneno
        • Kompyuta - komp.
      6. Kutokana na umbo/rangi ya kinachorejelewa
        • Mfano Blue - Noti ya kitambo ya shilingi ishirini
        • Tangi - Mtu mwenye umbo nane
      7. Kutumia isitara au jazanda
        • Golikipa - nyani
        • Mtu mlafi - Fisi
      8. Kuunda maneno mapya kabisa;. mfano
        • Kuhanya - Usherati
        • keroro - Pombe
        • Kusikia ubao - Hisi njaa
        • Ni kubaya - hali si nzuri [ 3x2]
    3. Ni jukumu la jamii kudumisha fasihi simulizi. Dhihirisha. (alama 6)
      1. Kuendelea kufundisha Fasihi Simulizi shuleni
      2. Kufanya Fasihi Simulizi kuwa hai kiutendaji kupitia shehere na hafla tofauti za kiserikali
      3. Kuhifadhi tanzu mbalimbali ili vizazi vijavyo viweze kuzifahamu mfano kwa kurekodi
      4. Kufanya utafiti wa kina kuhusiana na tanzu za Fasihi simulizi.
      5. Kuhakikisha kuwa lugha za kiasili hazififii kwa vile ndizo chanzo cha Fasihi simulizi
      6. Kuonyeshwa kwa fani mbalimbali za Fasihi simulizi kwenye vyombo vya habari kama kama runinga.
      7. Kuhimiza wanajamii hususan viongozi kuwasilisha ujumbe wao kwa kutumia fani za Fasihi simulizi kwa mgano hotuba, ulumbi, mawaidha nk.
      8. Kuhimiza wanajamii kuionea fahari jadi hii na kushiriki kikamilifu katika matumizi ya fani mbalimbali mfano nyimbo.
      9. Kusisitiza uendelezwaji wa fani zake katika mashindano ya shule na hata baina ya shule tofauti kimaeneo na kitaifa. [6x1]
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions And Answers - Form 3 Term 2 Opener Exams 2021.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest