Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Form 3 End Term 2 Exams 2022

Share via Whatsapp

MASWALI

SEHEMU A: USHAIRI
Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali yafuatayo

  1. Mkata ni mkatika, harithi hatoridhiwa
    Sina ninalolishika, wala ninalochukuwa
    Mlimwengu kanipoka, hata tone la muruwa!
    Mrithi nini wanangu?
  2. Sina ngo’mbe sina mbuzi, sina konde sina buwa
    Sina hata makaazi, mupasayo kuyajuwa
    Sina mazuri makuzi, jinsi nilivyoachwa
    Mrithi nini wanangu?
  3. Sina kazi sina bazi, ila wingi wa shakawa
    Sina chembe ya majazi, mno nikukamuliwa
    Nakwa’cheni upagazi, ngumu kwenu ku’tuwa
    Mrithi nini wanangu?
  4. Sina sikuachi jina, mkata hatasifiwa
    Hata nifanye la mana, mno mi kulaumiwa
    Poleni wangu sana, sana kwenu cha kutowa
    Mrithi nini wanangu?
  5. Sina leo sina jana, sina kesho kutwaliwa
    Sina zizi sina shina, wala tawi kuchipuwa
    Sina wanangu mi sina , sana la kuacha kuraduwa
    Mrithi nini wanangu?
  6. Sina utu sina haki, mila yangu meuliwa
    Nyuma yangu ili dhiki, na mbele imekaliwa
    N’nawana na miliki, hadi nitakapofukiwa
    Mrithi nini wanangu?
  7. Sina ila kesho kwenu, wenyewe kuiongowa
    Muwane kwa nyinyi mbinu, mwende pasi kupumuwa
    Leo siyo kesho yenu, kama mutajikamuwa
    Mrithi nini wanangu?
  1.    
    1. Taja mambo yoyote mawili ambayo mtunzi angewarithisha wanawe. (alama 2)
    2. Eleza sababu ya mtunzi kutoweza kuwarithisha wanawe. (alama 3)
    3. Andika ubeti wa nne kwa lugha nathari. (alama 4)
    4. Dondoa mifano miwili miwili ya : (alama 2)
      1. Inkisari
      2. Tabdila
    5. Chambua shairi hili kwa upande wa :
      1. Dhamira (alama 2)
      2. Muundo (alama 4)
    6. Eleza maana ya vifungu vifuatavyo kama vilivyotumiwa katika shairi. (alama 3)
      1. Mlimwengu kanipoka
      2. Sina konde sina buwa.
      3. Wingi wa shakawa.
  2. SEHEMU B: TAMTHILIA YA KIGOGO (Pauline Kea)
    ‟ Wamenimaliza… Wamenigeuka…″
    1. Weka dondoo hili katika muktadha wake. (Alama 4)
    2. Eleza namna msemaji amemalizwa na kugeukwa? (Alama 4)
    3. Eleza umuhimu wa msemaji. (Alama 4)
    4. Eleza jinsi wahusika wengine walivyomaliziwa katika tamthilia. (Alama 8)
  3.    
    1. Fafanua jinsi mwandishi wa Kigogo alivyofanikisha matumizi ya Majazi. ( alama 10)
    2. Ukiukaji haki na uvunjaji sheria ni mambo yaliyokithiri katika jimbo la Sagamoyo. Thibitisha. (alama. 10)
  4. SEHEMU C: RIWAYA YA CHOZI LA HERI (ASSUMPTA K MATEI)
    Jadili ufaafu wa anwani Chozi la Heri katika Riwaya. ( alama 20)
    1. “… mwanaume hufumbika hisia. Machozi ya mwanaume hayapaswi kuonekana hata mbele ya majabali ya Maisha…”
    2. Eleza muktadha wa dondoo. ( alama 4)
    3. Tambua mbinu ya lugha kwenye dondoo hili. ( alama 2)
    4. Eleza maudhui yanayodhihirishwa na dondoo hili. ( alama 2)
    5. Fafanua sifa za msemewa wa dondoo. ( alama 12)
  5. SEHEMU D: FASIHI SIMULIZI
    1. Taja aina mbili za Fasihi ( alama 2)
    2. kwa kutolea hoja nane Tofautisha kati ya Fasihi ulizotaja hapo juu. ( alama 8)
    3. (Eleza maana ya Mighani. ( alama 2)
    4. Jadili umuhimu wa mighani. ( alama 8)
  6. Ewe kilizi
    Ulozowea kujificha
    Nyuma ya mama kujikinga, dhidi ya milio
    ya radi ilo juu mbinguni
    Jua kesho ni siku ya siku
    Siku ya kujua mbichi na mbivu
    Kutofautisha jogoo na vipora,
    Ngariba taposhika, chake kijembe
    Ndipo utakapojua bayani
    Ukoo wetu si wa kunguru
    Ikiwa hu tayari
    Kisu kukidhihaki
    Sithubutu kamwe, wanjani kuingia
    sije kuniaibisha miye, amiyo na akraba nzima!
    1. Huu ni wimbo wa aina gani? Toa sababu. ( alama 2)
    2. Wimbo huu unaimbwa na nani ? Toa idhibati. ( alama 2)
    3. Fafanua sifa nane za huu. ( alama 8)
    4. Je, nyimbo za aina hii zina dhima gani kwenye jamii. ( alama 8)

 

 

 

 



MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

  1. SEHEMU A: USHAIRI
    1.      
      • makazi mabovu
      • upagazi
      • kutothaminiwa
      • dhiki
      • kufanya kesho ya wengine nzuri
    2.      
      • ni maskini hohehahe / hana kitu
      • aliporwa kila kitu.
      • hana mifugo.
      • hana kazi yoyote.
      • hana sifa / umaarufu.
      • ana makazi mabovu.
    3.      
      • sina jina nitakawacha kwani maskini hasifiwi
      • hata nikifanya jambo la maana ninalaumiwa tu.
      • poleni sana wanangu kwa kuwa sina la kuwatolea.
      • mtarithi nini wanangu?
    4.        
      1. inkisari
        • Mana – maana
        • Meuliwa – imeuliwa
        • Nitapofukiwa – nitakapofukiwa.
      2. tabdila
        muruwa - murua
        kutowa -kutoa
        kuchipuwa -kuchipua
        kuiongowa - kuiongoa
        kupumuwa - kupumua
    5.    
      1. dhamira
        • Kuwahimiza watu kufanya bidii wakiwa vijana.
        • Kulalamika kwamba maskini hana haki / huonewa / hapewi nafasi.
      2. muundo
        • Shairi ni aina ya tarbia / unne.lina mishororo minne katika kila ubeti.
        • Mishororo ya kwanza mitatu imegawika katika sehemu mbili (ukwapi na utao).
        • Kila kipande kina mizani nane na kila mshororo una mizani kumi na sita.
        • Vina vya kati vinatofautiana kutoka ubeti mmoja hadi mwingine, lakini vina vya mwisho ni sawa katika shairi zima katika mishororo ya kwanza mitatu.
        • Shairi hili lina kibwagizo ambacho kimefupishwa.
          Mrithi nini wanangu?
        • shairi hili lina beti saba.
    6.    
      1. mlimwengu kunipoka - mlimwengu kanipokonya.
      2. sina konde sina buwa - sina shamba sina chochote.
      3. wingi wa shakawa – mashaka mengi.
  2. SEHEMU B: TAMTHILIA
    ‟Wamenimaliza… wamenigeuka…″
    1. weka dondoohilo katika muktadha wake (alama 4x1)
      1. Maneno ya mamapima yaani asiya
      2. Anamwambia tunu.
      3. Wako katika soko chapakazi
      4. Hii ni baada ya kupinduliwa kwa serikali ya majoka ambaye mamapima alikuwa mfuasi wake
    2. elezea namna msemaji amemalizwa na kugeukwa?
      1. Mambo yameaanza kumuendea segemnege (kinyume).
      2. Serikari iliyopinduliwa ilikuwa inamwinda ili imuue
      3. Anasema wamemgeuka hata kufika kuimwaga pombe yake
      4. Anaomba ulinzi kutoka kwa akina wanasogamoyo na tunu anamhakikishia usalama.
        hoja 4x1=4
    3. eleza umuhimu wa msemaji. (alama 4)
      1. Mamapima ni kielelezo cha wanawake wakware katika jamii hakuwa mwaminifu katika ndoa anatembea na ngurumo.
      2. Pia mamapima ni wanawake ambao wako tayari kupoteza utu wao kwa kugawa uroda tu ilimradi wajipatie kipato.
      3. Yeye anaendeleza maudhui ya ulevi ambao unadhuru wanajamii.
      4. Ni kielelezo cha wanajamii wenye ubinafsi, ananufaika kutokana na utawala mwovu wa majoka hivyo anapinga harakati za ukombozi
        hoja 4x1
    4. Eleza jinsi wahusika wengine walivyo maliziwa katika tamthilia. (alama 8)
      Tunu
      Mwanaharakati huyu alipigwa na kuvunjwa mguu. Mpango wa awali ulikuwa ni kumuua. Hata hivyo alipona kwa bahati tu
      Ngurumo
      Ngurumo ananyongwa na chatu hata baada ya kuwa na manufaa makubwa katika utekelezaji maasi katika uongozi wa majoka. Kijana huyu anajitolea kufanya kila analoambiwa na utwala lakini anaangamizwa kwa sababu aliua siri nyingi za uongozi
      Chopi
      Ni mlinzi wa majoka ambaye anateeleza maovu ya utawala kama vile mateso kwa kenga ipasavyo. Hivyo katika mwendelezo uo huo majoka na kenga wanakubaliana kumuua chopi ili asitoe siri zao
      Jabali
      Alikuwa mpinzani wa karibu sana wa majoka. Alifanyiwa njama akauawa kwa kile kilichoonekana kama ajali ya barabarani.
  3.      
    1. Fafanua jinsi mwandishi wa Kigogo alivyofanikisha matumizi ya Majazi. ( alama 10)
      Ni mbinu ya kuwapa wahusika au mahali majina kulingana na sifa zake
      MAJOKA- Ni Wingi Wa Neno Joka. Kwa Kawaida, Joka Huwa Na Sumu Inayoua
      • Utawala Na Matendo Ya Majoka Ni Kama Sumu/ Nyoka Kwa Raia,
      • K.M Wandamanaji Wanauawa, Kwa Mfano Baadhi Ya Raia Wanakufa Kutokana Na Sumu Ya Nyoka.
        TUNU -Hii Ni Tuzo Hidaya Au Zawadi.
      • unu Ni Kama Zawadi Kwa Wanasagamoyo Kwani Anatia Bidii Katika Kutetea Haki Zao, Wananchi Wanamtaka Kuwania Uongozi Wa Sagamoyo Ili Awe Kiongozi Wao
        SUDI~ Sudi Inamaanisha Bahati.
      • Ana Bahati Ya Kuwa Na Mke Mzuri , Mwenye Bidii Na Mtetezi Wa Haki, Ama Ana Bahati Ya Kuwa Na Kipaji Cha Uchongaji Wa Vinyago Vizuri Akilinganishwa Na Wachongaji Wengine.
        MAMAPIMA -Ni Mama Ambaye Anafanya Kazi Ya Kuuza Pombe Hivyo Jina Lake Limetokana Na Kuwapimia Walevi Pombe.
        SAGAMOYO-Kuusaga Moyo Ni Kuumiza Moyo Au Kupitia Katika Hali Ngumu Ya Mateso Makubwa Yanayosaga Mioyo Yao.
        NGURUMO -Ni Sauti Ya Kutisha.Matendo Ya Ngurumo Ni Ya Kutisha Kwa Mfano Kulewa Kupita Kiasi, Matusi, Na Hata Kushiriki Katika Kumvunja Tunu Mguu.
        CHAPAKAZI-Jina Hili Linamaanisha Bidii,
        Soko La Chapakazi Ni Mahali Ambapo Wachochole Huchapa Kazi Kwa Bidii Na Kujitafutia Riziki Yao.
        HUSDA - Linaashiria Au Kurejelea Neno Husuda Kwa Maana Ya Kuonea Gere. K.M Ana Husuda Dhidi Ya Ashua Kwa Kudhania Kuwa Anamchukua Mumewe Kimapenzi . Aidha Mumewe Anamtaja Kama Chui Katika Ngozi Ya Kondoo.
        SITI- Ni Jina La Heshima La Mwanamke,Siti Ni Binti Wa Heshima Anayetaka Haki Itendeke Katika Sagamoyo Ndipo Anashirikiana Na Wanaharakati Wengine Kuleta Heshima Ya Sagamoyo.
        PENDO-Ni Mwana Wa Sudi Na Ashua Wazazi Wake Wanampenda Kwani Ni Matokeo Ya Pendo La Wazazi Wake.
        KENGA - Maana Yake Ni Kudanganya Au Kulaghai Hivyo Kenga Anampa Majoka Ushauri Usiokuwa Wa Kweli Unaompotosha Hatimaye.
    2. Ukiukaji haki na uvunjaji sheria ni mambo yaliyokithiri katika jimbo la sagamoyo. Thibitisha. (alama. 10)
      Ukiukaji wa haki na uvunjaji wa sheria:
      1. majoka kuruhusu ukataji miti.
      2. majoka kupatiana kibali cha uuzaji wa pombe haramu.
      3. soko la chapakazi kufungwa.
      4. waandamanaji kupigwa bila kuleta ghasia (ni haki yao).
      5. kuamuru mkuu wa polisi (kingi) awapige watu risasi.
      6. ashua kufungiwa seli bila hatia.
      7. majoka kumfuta kingi kazi/chopi kutishwa atamwaga unga.
      8. jabali kuuawa/ngurumo
      9. tunu kuvamiwa/kuumizwa
      10. kutishiwa kuuawa km chopi alipangiwa kuuawa.
      11. sudi kushinikizwa achonge kinyago.
      12. babake tunu kuuawa katika kiwanda cha majoka.
      13. vijana watano kuuawa wakati wa maandamano.
      14. kuongeza bei ya vyakula maradufu
      15. kubomoa vioski katika soko la chapakazi.
      16. majoka kumtaka ashua kimapenzi
      17. wanafunzi shuleni kuadhibiwa watumie dawa za kulevya.
      18. uwanja wa soko kunyakuliwa.
      19. kutozwa kodi zaidi
      20. kutosafisha soko ilhali watu wanalipa kodi
      21. kufungwa kwa vituo vya habari
      22. ngurumo kuzikwa juu ya maiti wengine.
        (zozote 10 x 1 = alama 10)
  4. SEHEMU C: RIWAYA YA CHOZI LA HERI (ASSUMPTA K MATEI)
    Jadili ufaafu wa anwani Chozi la Heri katika Riwaya. ( alama 20)
    Mwandishi anatuleza kuwa Ridhaa alipokwenda shuleni siku ya kwanza alitengwa na wenzake kwani hawakutaka ashiriki michezo yao. Kijana mmoja mchokozi alimwita 'mfuata mvua' aliyekuja kuwashinda katika mitihani yote. Ridhaa alifululiza nyumbani na kujitupa mchangani na kulia kwa kite na shake. Mamake alimliwaza na kumhakikishia kumwona mwalimu keshoye. Tangu siku hii, huu ukawa ndio mwanzo wa maisha ya heri kwa Ridhaa kwani baada ya mwalimu kuzungumza na wanafunzi umuhimu wa kuishi pamoja kwa mshikamano, Ridhaa alipea kwenye anga ya elimu hadi kufikia kilele cha cha elimu na kuhitimu kama daktari.
    Ridhaa alipotoka kwenye Msitu wa Mamba alijiona nafuu kwani wapwa zake- Lime na Mwanaheri walikuwa wamepata matibabu. Dadake Subira alitibiwa akapona. Mwamu wake Kaizari amepona donda lililosababishwa na kuwatazama mabinti zake wakitendewa ukaini(kubakwa) na Vijana wenzao. Ridhaa anajua kuwa Kaizari ni afadhali kwa sababu hakuna aliyemtenga na mmoja kati ya jamaa zake. Ridhaa anapomfikiria Kaizari anajiambia heri nusu Shari kuliko Shari kamili.
    Ridhaa aliposikia sauti ya kike ikitangaza, tangazo lile lilimrudiSha katika mandhari yake ya sasa. Alijaribu kuangaza macho yake aone anakoenda lakini macho yalijaa uzito wa machozi ambayo alikuwa ameyaacha yamchome na kutiririka yatakavyo.
    Wakati Ridhaa alimkazia macho Mwangeka-waka Mwangeka alikuwa akijiuliza iwapo babake amekuwa mweh kwa kukosa kushirikiana na majirani kuchimba kaburi kuyazika majivu- matone mazito ya machozi yalitunga machoni mwake Mwangeka. Akayaacha yamdondoke na kumcharaz, yatakavyo. Uvuguvugu uliotokana na mwanguko wa macho: haya uliulainisha moyo wake, ukampa amani kidogo. Moyo wake ukajaa utulivu sasa kwa kujua kuwa wino wa Mungu haufutiki.
    Wakati Ridhaa alikuwa akimsimulia Mwangeka misiba iliyomwandama tangu siku alipoondoka kwenda kuweka amani Mashariki ya Kati, Ridhaa alisita akajipagusa kijasho kilichokuwa kimetunga kipajini mwake kisha akatoa kitambaa mfukoni na kuyafuta machozi yaliyokuwa yameanza kumpofusha. Uk 48
    Mwangeka alipokuwa ameketi mkabala na kidimbwi cha kuogelea, mawazo yake yalikuwa kule mbali alikoanzia Akawa anakumbuka changamoto za ukauji wake. Akawa kumbuka wanuna wake. Alipomkumbuka Annatila(Tila) mwili ulimzizima kidogo akatabasamu kisha tone moto la chozi: likamdondoka.
    Katika Msitu wa Simba kulikuwa na maelfu watu waliogura makwao. Kati ya familia zilizoguria humu ni familia ya Bwana Kangata. Kwa Kangata na mkewe Ndarine, hapa palikuwa afadhali kwani hawakuwa na pa kwenda kwa kuwa hata kule walikokuwa wakiishi awali hakukuwa kwao. Uk 57
    Wakati Dick walikutana kisadfa na Umu katika uwanja wa ndege, walikumbatiana kwa furaha. Machozi yaliwadondoka wote wawili na wakawa wanalia kimyakimya. Walijua fika kuwa jaala ilikuwa imewakutanisha na kwamba hawatawahi kutengana tena. Maisha sasa yalianza kuwa ya heri kwao.
    Baada ya miaka kumi ya kuuza dawa za kulevya, Dick alifaulu hatimaye kujinasua kutoka kwa kucha za mwajiri wake. Alianza biashara yake mwenyewe ya kuuza vifaa wa umeme. Sasa akaanza kujitegemea kwa kuwa amejiajiri. Alikuwa ameufungua ukurasa mpya katika maisha yake. Maisha yake sasa ni ya heri.
    Wakati Neema na Mwangemi walikabidhiwa mtoto wao wa kupanga na Mtawa Annastacia, Mwaliko alimkumbatia Neema na kumwita mama na kumwahidi kuwa ataenda naye. Neema alidondokwa na chozi la furaha na kumkumbatia Mwaliko kwa mapenzi ya mama mzazi. Hili lilikuwa ni chozi la heri kwa Neema.
    Dick alimweleza Umu kuwa siku waliokutana katika uwanja wa ndege na wakasafiri pamoja, hiyo ndiyo ilikuwa siku ya heri Zaidi kwake. Nasaha alizopewa na Umu zilimfunza thamani ya maisha. Kisadfa, huu ndio wakati Dick alikuwa ameamua kubadilisha maisha na kuishi maisha mapya yasiyokuwa ya kuvunja sheria.
    Dick aliposimulia namna wazazi wake wapya pamoja na Umu walivyomfaa maishani, kila mmoja katika familia hii alilia. Bila shaka yalikuwa machozi ya heri
    Baada ya Mwaliko kujitambulisha kwa Umu na Dick, umu na Dick hawakungojea amalize. Walikimbia wote wakamkumbatia ndugu yao, wakaanza kulia huku wakiliwazana. Haya yalikuwa machozi ya furaha kwao kwa kupatana tena wote wakiwa hai. Kwa kweli kila mmoja alitokwa na chozi la heri.
    Mwaliko alimwambia babake kuwa kuja katika hoteli ya Majaliwa kuliwaletea heri kwa kuwa familia yao sasa imepanuka. Sasa amekutana na watu aliokuwa tu anasikia wakitajwa. Maisha sasa ni afadhali.
    Dick alitoa shukrani tele kwa Umu kwa kuwa alimpa matumaini kuwa siku moja watampata ndugu yao Mwaliko. Mwaliko hata anapomtazama Umu, macho yake yakiwa yamefunikwa na vidimbwi vya machozi, anajua kuwa familia yao imerudiana japo katika mazingira tofauti.
    Siku ambayo Mwangeka alimwoa Apondi ilikuwa siku ya heri kwake kwani alimwaga chozi la heri. Tunaelezwa kuwa, Ridhaa alijua kuwa wakati ndio mwamuzi, ipo siku atakapotokeza hurulaini wake Mwangeka. Ataifungua kufuli kubwa iliyoufunga moyo wake na hiyo itakuwa siku ya kumwaga chozi la heri.
  5. “… mwanaume hufumbika hisia. Machozi ya mwanaume hayapaswi kuonekana hata mbele ya majabali ya Maisha…”
    1. Eleza muktadha wa dondoo. ( alama 4)
      Msemaji- mamake Ridhaa
      Msemewa- Ridhaa
      Sababu- Kumkanya Ridhaa dhidi ya kulia ovyo
      Mahali- nyumbani mwao
    2. Tambua mbinu ya lugha kwenye dondoo hili. ( alama 2)
      Jazanda- huu ni uwepo wa maana ya ndani iliyojificha. K.m majabali ya Maisha.
    3. Eleza maudhui yanayodhihirishwa na dondoo hili. ( alama 2)
      Taasubi ya kiume/ ubabedume- machozi hayahusishwi na wanaume.
    4. Fafanua sifa za msemewa wa dondoo. ( alama 12)
      Huyu ni mumewe Terry. Ni mhusika mkuu ambaye ana sifa kadhaa.
      Mshirikina- Uk 1,"Anakumbuka mlio wa kereng'ende na bundi usiku wa kuamkia siku hii ya kiyama. Milio hiyo ndiyo iliyomtia kiwewe zaidi kwani bundi hawakuwa wageni wa kikaida katika janibu hizi " Pia anamwambia mkewe Terry, "milio hii ni kama mbiu ya mgambo, huenda kukawa na jambo " Kwa hivyo Ridhaa ni mhusika aliyekuwa na imani katika mambo ya ushirikina. Uk 2 "Ninashangaa vipi daktari mzima hapo ulipo unajishughulisha na mambo ya ushirikina " Huu ni ushahidi mwingine wa kuonyesha kuwa Ridhaa alikuwa mshirikina.
      Mwepesi wa moyo- Ridhaa ni mwepesi wa moyo kwani anapopatwa na mawazo ya hapo awali ambayo ni ya kukatisha tamaa, analia kwa urahisi, kinyume na matarajio ya jamii kuwa mwanaume hafai kulia. UK 2,"machozi yaliturika uwezo wake wa kuona " Uk 3 "Ridhaa mwanangu, mwanamume hufumbika chozi ya mwanamume hayapaswi kuonekana hata mbele ya majabalia ya maisha. Huku ni kujiumbua hasa. Unyonge haukuumbiwa majimbi, ulitunukiwa makoo "
      Mwenye bidii. Uk 4,"Alikuwa amesafiri kwa shughuli za ujenzi wa taifa, kama alivyoziita safari zake za kikazi " Tunapata kuwa Ridhaa alikuwa ni mwenye bidii za mchwa katika kazi yake ya kila siku aliyoiita 'ujenzi wa taifa'.
      Mvumilivu. Aliweza kuvumilia matukio yaliyomkumba kijijini mwake, yakiwemo kutotakwa huko, na kufukuzwa, mali yake kuharibiwa na familia yake kuuliwa.Anapiga moyo konde kukabiliana na hall hiyo mpya (uk 25).
      Mwenye busara. Ridhaa anapozisikia sauti za hawa ndege, anajua kuwa kuna jambo ambalo lingeweza kutendeka na ambalo si la kupendeza. Pia anamwambia mkewe, uk 2,"wewe endelea kupiga hulu tu, lakini utakuja kuniambia " Baadaye tunapata kuona kuwa kuna janga linaloipata familia yake na kwa hivyo, Ridhaa alikuwa na uwezo wa kuhisi kuwa kuna jambo lisilokuwa la kupendeza litakaloifikia jamii yake.
  6. SEHEMU D: FASIHI SIMULIZI
  7.    
    1. Taja aina mbili za Fasihi ( alama 2)
      • Fasihi simulizi
      • Fasihi andishi
    2. kwa kutolea hoja nane Tofautisha kati ya Fasihi ulizotaja hapo juu. ( alama 8)
      • Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya mdomo ilhali fasihi andishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi.
      • Fasihi simulizi huhifadhiwa akilini ilhali fasihi aandishi huhifadhiwa kwa maandishi.
      • Fasihi simulizi ni mali ya jamii ilhali fasihi andishi ni mali ya mtu binafsi/mwandishi.
      • Fasihi simulizi ina wahusika wa kila aina k.v binadamu, wanyama na ndege, mazimwi na majitu, miungu, mizimu, mashetani na vitu visivyo na uhai k.v. mawe na miti ilhali fasihi andishi ina wahusika binadamu kwa kiasi kikubwa.
      • Fasihi simulizi ina tanzu nyingi kuliko fasihi andishi.
      • Uwasilishaji wa fasihi simulizi huweza kuandamana na utendaji k.v matumizi ya ishara, nyimbo, makofi, kuimba, kubeba zana katika majigambo n.k ilhali ule wa fasihi andishi hauandamani na utendaji isipokuwa inapowasilishwa mbele ya hadhira.
      • Fasihi simulizi huwasilishwa mbele ya hadhira ilhali fasihi andishi si lazima iwasilishwe mbele ya hadhira.
      • Fasihi simulizi huwasilishwa mahali maalum k.v jandoni, matangani, arusini, n.k ilhali fasihi andishi haina mahali maalum.
      • Fasihi simulizi huandamana na shughuli fulani ya kitamaduni ilhali fasihi andishi haiandamani na shughuli ya kitamaduni.
      • Fasihi andishi huhitaji muda kutunga ilhali baadhi ya fasihi simulizi huzuka papo hapo k.m. semi, maigambo.
      • Fasihi simulizi ina uwezo mkubwa wa kubadilishwa na fanani anapowasilisha ufaraguzi) bali fasihi andishi haibadiliki isipokuwa mwandishi aiandike upya.
      • Fasihi simulizi ina historia ndefu kuliko fasihi andishi kwa kuwepo tangu mwanzo wa maisha ya binadamu
      • Fasihi simulizi huwasilishwa wakati maalum k.v. usiku, kipindi fulani cha mwaka ilhali andishi haina wakati maalum.
    3. Eleza maana ya Mighani. ( alama 2)
      Hadithi za mashujaa/majagina wa jamii fulani k.m. Rwanda Magere wa Waluo, Fumo Liyongo wa Wapate, Koome Njue wa Wameru, Wangu wa Makeri wa Wakikuyu na Syokimau wa Wakamba.
    4. Jadili umuhimu wa mighani. ( alama 8)
      • Huhusu mashujaa wa jamii fulani.
      • Wahusika hupambana na hali ngumu inayosababishwa na maadui.
      • Wahusika hupewa sifa na uwezo usiokuwa wa kawaida k.v. ukubwa wa ajabu, nguvu katika kivuli, nguvu katika nywele, kutoulika n.k.
      • Wahusika hupigania haki za wanyonge.
      • Mhusika hukomboa jamii yake dhidi ya maadui.
      • Mhusika hufa kifo cha huzuni (tanzia) kwa kusalitiwa na mtu wa karibu k.v. mwanamke au jamaa zao.
      • Mashujaa huuliwa kwa njia ya ajabu kama vile kunyolewa nywele, kivuli kuchomwa mkuki, kuchomwa shindano ya shaba kitovuni
      • Mighani huzungumzia matukio ya kihistoria.
      • Kuna tabia ya kupiga chuku matukio yaliyo hadithini.
      • Mighani hurithishwa jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
      • Huchukuliwa na jamii kama hadithi zenye ukweli na jamii hujinasibisha na mighani hiyo.
      • Husimulia mambo ya kiimani na kidini.
  8.        
    1. Huu ni wimbo wa aina gani? Toa sababu. ( alama 2)
      Nyiso/Nyimbo za tohara- Ngariba taposhika, chake kijembe
    2. Wimbo huu unaimbwa na nani ? Toa idhibati. ( alama 2)
      Ami ya anayepashwa tohara- sije kuniaibisha miye, amiyo na akraba nzima!
    3. Fafanua sifa nane za nyimbo za aina hii. ( alama 8)
      • Huambatana na shughuli za jando (wavulana) na unyago (wasichana).
      • Huimbwa faraghani katika mazingira ya tohara pekee.
      • Huimbwa usiku wa kuamkia siku ya tohara.
      • Zilitoa sifa kwa waliotahiriwa, wazazi na wasimamizi wao.
      • Ziliimbwa kuwapa wavulana ujasiri wa kukabili kisu cha ngariba.
      • Zilitoa mafunzo kuhusu majukumu mapya baada ya kutahiriwa.
      • Hujumuisha watu maalum walioteuliwa kushiriki katika sherehe.
      • Huhusisha watu wa jinsia na umri fulani.
        Maudhui yake hutegemea jinsia.
    4. Je, nyimbo za aina hii zina dhima gani kwenye jamii. ( alama 8)
      • Kuonyesha vijana wamevuka kutoka utotoni hadi utu uzima.
      • Kuwaandaa vijana kwa uchungu watakaouhisi kupitia kijembe.
      • Kuhimiza ujasiri na ukejeli uoga.
      • Kusifu wahusika kwa ujasiri wa kukabili kisu na kuingia katika utu uzima.
      • Kuburudisha waliohudhuria shughuli ya jando au unyago.
      • Kuelekeza vijana kwenye matarajio mapya ya jamii.
      • Kufunza majukumu katika utu uzima.
      • Kukuza umoja na ushirikiano katika jamii kwa kuwaleta wanajamii pamoja.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Form 3 End Term 2 Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest