Dhamira na Maudhui Katika Bembea ya Maisha - Mwongozo wa Bembea ya Maisha

Share via Whatsapp

Menyu ya Urambazaji:

MAUDHUI NA DHAMIRA YA MWANDISHI

Maudhui ni masuala muhimu ambayo mwandishi anayachanganua Maudhui katika kazi yake; yale mambo muhimu anayoyaona katika jamii na anayotaka kuyaeleza kisanaa katika kazi yake, bila kujali utanzu anaotumia kumulikia masuala hayo. 

Dhana kuu ya mwandishi kwa hadithi hii ni kuonyesha jinsi maisha ya ndoa , familia na jamii yalivyo. Amehakikisha kwamba ameonyesha dhana yake kwa wale wahusika aliowaweka. Wausika wote wanaouhusiano wa kifamilia au kijamii. Mwandishi anataka kutuonyesha tofauti ya maisha haya yalivyo katika kijiji na katika mji, au katikavizazi vilivyopita na vizazi vya sasa.

Vizazi vilivoypita vinaangazia tamaduni zao kwa ukaribu ila ya sasa yamekiuka mila kwa maeneo mengine, mengine yakibaki kuangazia. Mwandishi pia anang’ang’ana kuonyesha changamoto na faida za itikadi zote, za kisasa na vya kale kuhusu familia, ndoa na malezi bila kuegemea sana kwa upande mmoja.

Tunaweza sema kwa kuzingatia jinsi bembea inavyofanya, anaonyesha yaliyo mazuri na yaliyo mabaya kwa itikadi zote. Hakuna kile kilicho sawa kamili ila vyote vinavyo changamoto vyake, ambavyo havionekani kuisha kwa kikamili.

Nafasi ya mwanamke katika jamii

Haya ni maudhui yanayonyesha namna mwanamke amesawiriwa katika tamthilia ya Bembea ya Maisha.

  • Mwanamke amesawiriwa kama mwerevu na mwenye maarifa, hekima na busara. Kwa mfano, katika uk. 6 Kiwa anasema kuwa Sara amebarikiwa na watoto wenye akili nzuri. Wote wamehitimu vizuri na kuleta faraja. Tunaona Neema amesoma na kuhitimu Chuo kikuu na ana kazi nzuri. Asna na Salome vilevile wamefanikiwa kusoma hadi Chuo kikuu. Salome alipita mtihani kwa kupatafirst class. Alibahatika kwenda nwambo kuendeleza masomo yake (uk. 28).
  • Mazungunzo ya Sara katika tamthilia hii yanaonekana kuwa yenye wingi wa hekima na busara. Anatoa ushauri katika masuala mbalimbali kama vile: masuala ya ndoa, maisha, heshima na mengineyo.
  • Mwanamke anaonekana kama mzazi anayestahili kujifungua watoto wa kike na wakiume na hasa watoto wa kiume. Asipopata watoto wa kiume, anasutwa na kukejeliwa.
  • Tunaelezwa kwamba Sara alisutwa na kutukanwa na wanajamii kwa kukosa mtoto wa kiume hata baada ya kujaliwa na mabinti watatu baada ya muda mrefu bila watoto (uk. 6,7).
  • Mwanamke amesawiriwa kama mtu mvumilivu na anayestahili kuvumilia mateso na bughudha za ndoa. Kwa mfano, Sara anavumilia ndoa yake ambayo ilikuwa na changamoto nyingi. Aidha anavumilia mumewe Yona baada ya kumtesa na kumchapa kichapo cha mbwa.
  • Neema anapewa mawaidha na mama yake kuhusu kuzidi kuvumilia ndoa yake.
    Kudhihirisha suala hili la uvumilivu wa ndoa tunamwona
  • Neema akimweleza mumewe kwamba anakubaliana na wazo kuwa hawaishi katika ndoa ya raha mustarehe mia fil mia (uk. 48). Wazo hili linaonyesha kuwa Neema pia anavumilia ndoa yake na Bunju.
  • Mwanamke ameonyeshwa kama mtu anayestahili kujukumika katika majukumu ya nyumbani. Anasawiriwa kama mtu mwenye majukumu ya shambani, jikoni na nyumbani kwa jumla. Yona anapomkuta Sara ameketi, analalamika kuwa hajaandaliwa chochote. Inambidi Sara amtumie salamu Dina ili aje amsaidie kupika. Hali hii inaonyesha kuwa ni jukumu la mwanamke kupika na kuandaa chakula kwa mumewe.
  • Kizazi cha jana kimemsawiri mwanamke kama mtu asiyestahili kupata elimu. Sara anasema kuwa siku zao elimu ya wasichana ilifanywa bezo. Yeye aliachia darasa la saba (uk. 33).
  • Mwanamke amesawiriwa kama kiumbe dhaifu. Kiumbe ambacho hakifai kushindana na mwanamume. Sara anamwambia bintiye
  • Neema kuwa utamaduni ungali una nguvu na hawezi kushindana na mwanamume (uk. 66).
  • Wanawake katika tamthilia hii wameonyeshwa kama watu wenye msimamo dhabiti. Sara na binti zake wamesawiriwa kama wenye msimamo imara. Kwa mfano, Sara anasimama na familia yake hata baada ya kutukanwa na kukejeliwa na wanajamii. Hakuwacha familia yake, alisimama nayo hadi wakati wa mwisho. Asna pia ana msimamo wake kuhusu ndoa (uk. 53). Anashikilia msimamo kuwa ndoa ni taasisi inayomkandamiza mwanamke na kuwa haifai.
  • Sara anafanya kazi kwa bidii ili aelimishe watoto wake. Aidha anavumilia mateso mengi anayoyapitia ili kusimamisha ndoa yake isije ikasambaratika.
  • Neema anapata elimu bora,anakuwa msomi, mwenye bidii na anayewajibika kusomesha wanae na kugharamia matibabu ya mamake.

Katika mila na desturi ya wanakijijim, wanawake hawaangaliwi kama warithi.

  • Yona anaambiwa kwamba hana mrithi licha ya kuwa na watoto watatu kwa sababu wote ni wanawake. “Fimbo inarithi watoto wa kiume sio wa kike” (uk 2)
  • Nafasi na thamani ya mwanamke ipo chini ya mwanaume kulingana na mila na desturi zao. Yina anatajia haya akiwa na marafiki wake na kusema kwamba mambo yanabadilika na anaona thamani ya msichana imeanza kuongezeka
  • Mwanamke anapaswa kuangalia maswali ya bwana yake. Kulingana na Sara, alikuwa anaona amekaa mjini sana na kwamba wanakijiji watamwongelea Yona vibaya wakiona amenda kujitekea maji mtoni. 
  • Mschana akifikisha miaka ya kukomaa, anapaswa kuolewa. Kwa maneno ya Sara kwa mwanawe Asna, mwanamke hapaswe kuishi kibaleghe. 
  • Mwanamke ana jukumu kubwa ya kuiweka familia yake pamoja. Tunaelezwa kwamba baada tya Yna kupoteza kazi, Sara inabidi ashuguhulike zaidi kwa kuilea familia yake, huku Yoan amepotelea ulevini.
  • Mwanamke anapaswa kuwa mvumulivu kwa ndoa. Jambo hli ndilo linamfanya Sara abaki katika ndoa yake licha ya yote aliyopitia. Pia, ndio sababu Asna anaogopa ndoa kwa sababu anaona jambo hili kama utumwa.
  • Mwanamke anapaswa kuwa chini ya amri ya mumewe. Kwa maneno ya Bunju, yeye ndio kichwa na Neema shingo. Anamlaumu Neema kwa kutaka kukiuka amri kwa kukosa kumhusisha kwa yale wanayofanya.
  • Nafasi ya mwanamke aliyeolewa haipo kwao tena ila inabaidlika na kuwa kwa familia yake. Kwa maneno ya Yona tunaona kwamba pindi mwanamke anapoolewa, nafasi yake haipo kwao tena ndio maana hawezi rithi. 

Majukumu ya wanaume kwa jamii

Mwanamume ni mrithi. Katika jamii ya kina Yona, mtoto mvulana ndiye anayeweza kurithi mali.

  • Mwanamume ana jukumu ya kuwa kichwa cha familia. Yeye ndio anapaswa kuwa kiongozi. Bunju anamwambia Neema kwamba yeye ndio baba kwa hivyo ndio anapswa kuwa kichwa na Neema shingo.
  • Mwanamume ana jukumu ya kuishughulikia familia yake jinsi apasavyo. Bunju amejitolea kuwasomesha dada zake Neema, amelipia watoto wao shule, ndiye analipa kodi licha ya Neema kuwa anapata msharaha pia.
  • Mwanaume ndiye ana nafasi ya uongozi kwa jamii. Yona , Luka na Beni wanapoketi kwa kikao chao, wanabariki mvua na mimea na vizazi.
  • Mwanamume anapaswa kumwelewa na kuwa msaidizi kwa bibi yake. Yona anajitolea kumsaidia Sara anapoambiwa kwamba itabidi aishi kwa madawa aliyopewa. Bunju pia anajitolea kumsaidia Neem ahata baada ya kumweleza jinsi alivyofinyiliwa kifedha na madeni.

Umaskini

  • Kunao umaskini kwa familia ya Dina. Kiwa anamwambia mama yake kwamba ingekuwa ni yeye amekuwa mgonjwa hajui angeshika mti gani
  • Asna anaishi kwa upweke lakini amejikwamisha hapo kwa sababu ni mtaa wa kifahari.
  • Kwa mazungumzo ya asna na mama yake, tunaweza kuelewa kwamba pia kijijini kuna upweke lakini kwa maneno ya Asna, anaona heri upweke huu wake kuliko upweke wenyewe ulio kijijini.
  • Sara akimpa Neema maelezo ya maisha yao, anamwambia walipitia umaskini wa aina tatu:
    • Wa watoto – ambapo walikosa watoto.
    • Wa mrithi – walipopata mtoto lakini hawakuwa wa kiume
    • Wa kifedha – pale ambapo Yona alipoteza kazi.
  • Hali ya umaskini umefanya Asna na Neema kufananisha hospitali za kijijini kama jela.

Mabadiliko

Mabadiliko ni hali ya kutoka katika hali moja hadi nyingine.

  1. Mabadiliko yanajitokeza pale ambapo Yona anatueleza kuhusu maisha yake ya ujana alipokuwa mwalimu. Anatueleza namna alivyokuwa akiamka alfajiri na mapema kiboko mkononi na mwanafunzi aliyekuja baada yake angepokea kichapo. Anasema kuwa siku hizi huwezi kumnyoosha mtoto kwa kiboko. Suala hili linamaanisha kuwa kuna mabadiliko ya sheria na kanuni za shuleni (uk. 62).
  2. Suala la mabadiliko linadhihirika wakati Yona anakubaliana na Sara. Mtazamo wa Yona kwa Sara unabadilika. Alikuwa hana huruma kwa mkewe Sara alipokuwa mgonjwa. Katika onyesho la kwanza, Yona analalamika kwa sababu Sara alikuwa hajamwandalia chakula. Yona alikuwa hana huruma hata baada ya Sara kumwelezea kuwa alikuwa hajaandaa chakula kwa sababu ya maumivu (uk. 1).
  3. Mabadiliko yanajitokeza wakati Yona anaonekana kuhuzunishwa na maradhi ya mke wake. Anasema aliona hapo awali kama maradhi yale yalikuwa mchezo lakini sasa anatamani angeishi tofauti. Yona anasema hawezi kuendelea kuishi kama zamani, ni lazima angefuata mkondo mpya wa maisha. Anataka kuzitumia siku zake za uzee kumshughulikia mkewe (uk. 70). Anamwambia Sara pole na kusema kuwa taabu zake Sara zitakuwa taabu zake (uk. 74).
  4. Yona amesawiriwa kukuza maudhui ya mabadiliko. Mwanzoni, ameonyeshwa kama mtu mzuri, baada ya kusutwa na kudharauliwa kwa kukosa mtoto wa kiume anabadilika na kuwa mlevi na kupoteza upendo kwa familia yake. Tunamwona akimpokeza bibiye kichapo cha mbwa hadi kusababishia bibiye maradhi ya moyo. Yona anabadilika kutoka hali hiyo ya ulevi kwa kuamua kuchukuwa mkondo mpya wa maisha (uk. 70). Anasema kwamba pombe imemchezesha kama mwanasesere na kumnyima fursa ya kuilea familia yake.
  5. Kuna mabadiliko ya mitazamo ya utamaduni wa jamii ya kizazi cha jana na ya kizazi cha leo. Mabadiliko haya yanajidhihirisha kupitia suala la mtoto wa kike na mtoto wa kiume. Mtazamo wa mtoto wa kike katika kizazi cha jana umebadilishwa na utamaduni wa kizazi cha leo. Kizazi cha jana kinamwona mtoto wa kike kama mtoto asiyekamilika na asiyestahili kusomeshwa wala kurithi mali ya familia (uk. 60). Wazo hili linabadilishwa na kizazi cha leo ambacho kinamwona mtoto wa kike sawa na mtoto wa kiume. Kwa hivyo, kama mtoto wa kiume, yeye pia anaweza kurithi mali ya familia na vilevile kusomeshwa.
  6. Mabadiliko ya utamaduni pia yanajitokeza katika suala la ndoa. Sara anamweleza Asna kuwa zamani, wasichana walikuwa wakiozwa punde tu walipobaleghe (uk. 52). Mtindo huu unabadilika miongoni mwa kizazi cha leo kwani wasichana wanaolewa wakati watakapo.
  7. Mabadiliko ya utamaduni yanadhihirika kutoka kwa mhusika Yona ambaye, hapo awali, hangeweza kuingia jikoni kumpikia mkewe Sara. Baada ya kugundua kuwa hayo ni mambo yaliyopitwa na wakati, tunamwona akiandaa kiamshakinywa kwa familia yake. Pia, anamhakikishia Sara kuwa atamshughulikia kwani hali yake Sio nzuri (uk. 62).
  8. Kuna mabadiliko ya mitazamo au uonevu wa mambo katika tamthilia hii. Neema anabadilisha mtazamo wake kuhusu baba yake (uk. 72).
  9. Bunju pia anabadilisha mtazamo wake wa kutomsaidia Neema kugharamia matibabu ya mamake Sara. Anamwambia anaenda kukutana na mkurugenzi wa kampuni na kuwa akipata hela, atampiga jeki katika suala la matibabu ya mama yake (uk. 40).
  10. Tamthilia ya Bembeaya Maisha inaangazia mabadiliko ya maisha. Mabadiliko haya yanajitokeza kupitia familia ya Yona. Kwanza, maisha ya Sara, mkewe Yona, yanabadilika kutoka kuwa ya afya njema na kuwa yenye afya duni. Afya ya Sara inazorota kutokana na ugonjwa wa moyo ambao ataishi akimeza vidonge vya dawa maisha yake yote (uk. 71).
  11. Pia, mtazamo wa wanajamii kuhusu familia ya Yona unabadilika pia. Wanajamii sasa wanaiheshimu familia ya Yona ambayo ilikuwa imedharauliwa na kudunishwa hapo mbeleni. Familia hii haisutwi wala kutukanwa kwa sababu ya mafanikio na elimu ya mabinti wao. Jambo hili linadhihirishwa kupitia maneno ya Luka wakati walikuwa wakiongea na Beni na Yona.

Mabadiliko ya mtazamo kwa maisha ya kisasa (pointi za ziada)

  • Wanawake wanaweza someshwa na hata thamani na nafasi yao kwa jamii imepanda.
  • Malezi ya watoto jijini inatofautiana sana na kijijini kwa sababu ya kazi wazazi wanzofanya. Kulingana na Beni, yaya ndio wanaotawala nyumba.
  • Kwa kulelewa jijini, watoto wengi hawajui vizuri mila na desturi zao. Kulingana na Beni a Luka hata hawajui lugha zao za mama.
  • Asna ananishi tofauti sana na jinsi wanawake wanavyopaswa kuishi. Yeye haoni haja ya kuolewa.
  • Usafiri umerahisishwa na teknolojia. Safari ambayo ingewachukua siku ttau kuenda jijini imewachukua siku moja tu.
  • Yona anaonekana kuwa alibadilika kutokana na maneno ya wanajamii, kutoka kuwa mtu mzuri na kuingia ulevini n ahata kuanza kuchapa mkewe.
  • Pia, Yona anaonekana kubadilika tena pale anapokuja kuona hai ya bibi yake ilivyodhoofika.
  • Pia, mtazamo wa wanajamii kuhusu familia ya Yona unabadilika pia. Wanajamii sasa wanaiheshimu familia ya Yona ambayo ilikuwa imedharauliwa na kudunishwa hapo mbeleni. Familia hii haisutwi wala kutukanwa kwa sababu ya mafanikio na elimu ya mabinti Jambo hili linadhihirishwa kupitia maneno ya Luka wakati walikuwa wakiongea na Beni na Yona.

Ndoa

Mwandishi amesawiri suala la ndoa kupitia wahusika wafuatao:

  • Yona na Sara, Neema na Bunju na hata Asna. Kupitia ndoa za wahusika hawa masuala mengi ya mahusiano katika ndoa yanajadiliwa.
  • Ndoa ya Yona na Sara inasawiriwa kama ndoa ya kizazi cha jana.Inaonyesha matarajio ya ndoa kulingana na jamii yao. Inaakisi malezi, majukumu ya mke na mume na matarajio ya wanajamii kuhusiana na watoto. Inachora picha ya majukumu kama yalivyopangwa na jamii ya Yona na Sara.
  • Kulingana na jamii katika tamthilia ya Bembea ya Maisha, mwanamke anapoolewa anahitajika kuanzisha familia na mumewe. Anatarajiwa kujifungua watoto wa kike na vva kiume. Katika ndoa ya Yona na Sara, tunafahamishwa kuwa wanajamii waliwasema na kuwatafuna kama chingamu huku Yona akiitwa gumba na Sara kuitwa tasa. Hii ni baada ya kuoana na kukaa kwa muda mrefu bila kujaliwa na watoto (uk. 6). Ni wazi kwamba ndoa ya Yona na Sara imenyimwa hadhi katika jamii kwa kukosa mtoto wa kiume (uk. 7).
  • Kulingana na kizazi cha jana, mke anatarajiwa kujifungua watoto wa kike na wa kiume na hasa wale wa kiume. Ndoa ya Yona na Sara inasutwa na kukejeliwa na wanajamii kwa kukosa mtoto wa kiume ambaye aliaminika angekuwa mrithi wa Yona (uk. 8). Wanajamii walimtaka Yona kumwoa mke ambaye angemzalia watoto wa kiume. Kulingana nao, Sara alikuwa ameshindwa kumzalia mtoto wa kiume. Unyanyapaa huu ulimsukuma Yona kuupokea ulevi na kuanza kumpiga Sara kipigo cha mbwa kwa kuwa hakumzalia mtoto wa kiume (uk. 9-10).
  • Ni wazi kwamba ndoa ya Yona na Sara imenyimwa nafasi na hadhi katika jamii kwa kukosa mtoto wa kiume.
  • Ndoa pia imesawiriwa kama kitu chema ingawa chenye changamoto zinazoweza kuvumiliwa. Sara anasema kuwa ndoa ni uvumilivu na wala Sio watoto na hakuna ndoa isiyokosa doa. Sara anaivumilia ndoa yake na Yona. Anavumilia kuchapwa, kudharauliwa na kudhulumiwa. Sara anamvumilia mumewe hata baada ya dhiki hizo. Fauka ya hayo yote, anamshauri Neema aivumilie ndoa yake na Bunju. Vilevile, anamshauri Asna kumtafuta mume aolewe (uk. 33, 67).
  • Ndoa huakisi suala la malezi. Yona na Sara wanaonyesha malezi kwa kuwalea mabinti wao. Sara anawafurahia watoto wake na kujitahidi kuwalea ipasavyo.
  • Ndoa ya Neema na Bunju ni ya kizazi cha leo. Neema na Bunju wamesoma, wamehitimu na wameajiriwa na kuanza familia yao. Wanashirikiana katika masuala ya matumizi ya pesa. Bunju anashughulikia majukumu ya familia yake na Neema. Amemruhusu
  • Neema kutumia mshahara wake kuwasaidia wazazi wake. Ndoa katika tamthilia hii imesawiriwa kama uhusiano unaofaa kuleta heshima na uvumilivu. Bunju anamlalamikia Neema kwa kukosa kujulishwa kuwa mama mkwe wake anarejea kijijini bila yeye kujulishwa. Suala hili linamkera sana Bunju na kumuona Neema kama mke asiye na heshima (uk. 48).
  • Neema anasisitiza kuwa amempa mumewe heshima ya kutosha (uk. 49). Jambo la ndoa limesawiri majukumu ya mke na mume. Katika ndoa ya Bunju na Neema, mume ana majukumu ya kulipa karo, kulipa kodi ya nyumba na majukumu mengine. Jambo hili linaonyesha kuwa Bunju ni mume aliyewajibika. Kwa upande mwingine, Neema ana jukumu la kuwatunza wazazi wake.
  • Katika ndoa ya Sara na Yona, Yona anasawiriwa kuwa na jukumu la kuwasomesha wanawe. Hata baada ya Sara kwenda mjini kwa ajili ya matibabu, Yona anachukua majukumu nyumbani kama vile kushughulikia mifugo na kuondoa mtama shambani. Katika mwisho wa tamthilia, Yona anamwahidi Sara kuwa atayachukua majukumu yote kama mumewe na atamshughulikia katika kila hali. Yona pia anaonyeshwa kuwa na jukumu la kumjuza Sara kuhusu mikutano ya vyama vya kina mama.
  • Ndoa pia imesawiriwa kama jambo lililojaa bughudha. Kulingana na Asna, ndoa ina mateso na imejaa masharti mengi. Asna anaona ndoa ya dadake Neema imejawa na matatizo yasiyoweza kuvumilika. Anasema kuwa Bunju ni mchoyo na asiyetaka kumsaidia mtu (uk. 33, 45). Asna vilevile anaiona ndoa ya wazazi wake kama iliyojawa na mateso.
  • Anamweleza mamake kuwa amedhoofishwa na mateso aliyoyapata katika ndoa yake (uk. 53). Hali hii inamfanya Asna kusawiriwa kama msichana anayetaka kuyajenga maisha yake bila mume.
  • Katika sehemu ya kwanza tunapata Yona anaoa Sara na kuishi pamoja
    Ndoa ya Yona na Sara imejaa changamoto mbali mbali kama vile kukosa mtoto wa kiume , na vile vile kuteseka kutokana na maradhi ambayo imesababishwa na kuteseka na kuchapwa na mumewe kwa wakati mwingine,
    Tunapata Yona anashauriwa kutafuta mtoto wa kiume njee ya ndoa ama kuoa mke mwingine.
    Tunapata wasichana wa kisasi pia wanashiriki katika ndoa na kusahau mandugu yao
    Neema mtoto wake Sara anashiriki kwa ndoa na Bunju baada ya elimu yake na kuzaa watoto.

Ulevi

  • Maudhui ya ulevi yameangaziwa kupitia mhusika Yona. Tunaelezwa kuwa Yona alijiingiza katika ulevi baada ya kushinikizwa na wanajamii kumuoa mke mwingine atakayemzalia mtoto wa kiume. Shinikizo hili lilimfanya kuingilia ulevi kwa hali ya juu zaidi.
  • Kutokana na ulevi, alianza kumpa mkewe Sara kichapo cha mbwa (uk. 10).
    Tatizo hilo la ulevi linamwingiza kwenye matatizo chungu nzima.
  • Yona pia alifutwa kazi kwa sababu ya ulevi (uk. 56).
  • Ulevi uliyamega maadili ya Yona na kumpokonya uwajibikaji wa familia yake. Katika jamii yoyote ile, uraibu wa pombe uliopindukia unaweza kuwa chanzo cha matatizo mengi katika familia. Yona anafutwa kazi na kuingia katika limbi la uchochole.
  • Anaanza kumdhulumu mke wake hadi kumsababishia maradhi ya moyo. Kwa kifupi, pombe inayavuruga maisha yake kama mfanyakazi na kama mume aliyetegemewa na jamaa yake. 

Teknolojia na Maendeleo

  • Suala la teknolojia na maendeleo limeonyeshwa na mwandishi kupitia maelezo ya wahusika kama vile: Neema, Asna, Sara, Luka na wahusika wengineo.
  • Maendeleo ya mjini na kijijini yamedhihirishwa kupitia mazungumzo ya Neema na Sara. Sara alikuwa amewasili mjini kwa ajili ya matibabu.
  • Neema anasema kuwa maendeleo mjini ni ya hali ya juu. Anasema kuwa watu hufika mjini kutoka mashambani ili kupata jambo au kitu kizuri.
  • Anasema kwao maendeleo bado na yanakuja kwa kudoda (uk. 17). Hali kadhalika, maendeleo ya kijijini yamedorora kwa sababu ya ahadi zisizotimizwa. Sara anasema kuwa tangu wakiwa watoto maendeleo yamekuwa yakija hadi walipokuwa wazima na kujaliwa na watoto na ahadi hii ya maendeleo imebaki kuwa tu ahadi isiyotimizika wakati wa uhai wao (uk. 17).
  • Katika mazungumzo ya Dina na Sara pale jikoni, Dina anasema kuwa anasikia mjini kuna magari mengi, majengo makubwa, barabara nyingi na pia watu wengi (uk. 15). Mazungumzo hayo yanaonyesha namna mjini kulivyoendelea. Dina anasema kuwa anasikia watu wa mjini wameendelea sana hata wametengeneza magari yatembeayo hewani.
  • Maendeleo katika hospitali za mjini yamesawiriwa katika mazungumzo ya Sara. Anasema kwamba kwenye hospitali aliyokuwa amelazwa, huduma za huko ni nzuri sana mpaka anashindwa kuamini kama kweli yuko wodini. Anasema kuwa kuna kitanda kizuri, godoro nzuri na shiti nzuri zilizoplgwa pasi. Anasema kuwa madaktari hawakawii kuzibadilisha shiti hizo. Anasema hospitali za mjini si kama za kijijini ambazo amezisawiri kama seli na ukilazwa katika hospitali hizo tayari wewe ni kama mahabusu. Asna anasema kuwa hewa katika wodi za hospitali za kijijini huwa zimejaa harufu ya dawa, vitanda vimesalimu amri mpaka shiti zimekagura. Anasema kuwa hospitali hizo hazimpi mtu matumaini ya kutoka akiwa bora na kumbidi mtu kuweka tumaini lake katika sala (uk. 42).

Mawaidha au Wosia

  • Suala la mawaidha au wosia katika tamthilia ya Bembea ya Maisha linakuzwa na wahusika kama vile Luka, Yona, Sara na Neema. Sara anamwambia Neema kuwa asishindane na mwanamume hasa nyumbani ila wanaweza shindana kazini au hata masomoni. Sara anawapa Neema na Asna mawaidha kuwa ni vyema wamheshimu Bunju kama ndugu yao.
  • Sara anawapa mawaidha wanawe wamheshimu baba yao aliyewalea na kuwasomesha. Sara anawashauri Asna na Neema kuziheshimu na kuzitii mila na desturi za jamii yao. Luka anawashauri Beni na Yona kuhusu I-muhimu wa elimu ya mtoto wa kike katika jamii. Anadai kuwa tamaduni, mila na desturi zinazidi kubadilika na wanapoyapuuza hayo yote ni kazi bure (uk. 60). Luka awafundisha Beni na Yola kuhusu usawa kati ya watoto wa kike na wa kiume (uk. 60).
  • Kuna mawaidha Sara anayompa Neema kwa njia ya mafumbo kuhusiana na maisha. Sara anamweleza Neema kuwa hakuna kizuri kinachokuja kwa urahisi. Analinganisha maisha na mbegu iliyopandwa. Mbegu hiyo hukua na kutoa mche wenye umbo la kupendeza hata baada ya kuoza. Vivyo hivyo, maisha hukumbwa na pandashuka lakini huzidi kuendelea. Anawataka Neema na dada zake warudi kijijini kuotesha mbegu zingine zitakazokua na kuwa miche ya kupendeza kama wao (uk. 68).
  • Sara anampa bintiye Neema mawaidha ya jinsi ya kuelimisha wanakijiji na kuwapa maarifa ya kisasa. Anamwambia anaweza kuanza kwa kumshawishi baba yao badala ya kumkabili kumwelewa ndiposa aweze(uk. 69).

Malezi

  • Suala la malezi limejitokeza kupitia kwa wahusika Yona na Sara, Bunju na Neema na hata Bela.
  • Yona na Sara wanajikakamua kuwalea watoto wao kwa njia inayostahili. Wawili hao walikuwa hawajiwezi kiuchumi hasa baada ya Yona kufutwa kazi kutokana na ulevi. Wanajitahidi kuwasomesha watoto wao. Licha ya tamaduni zao, Yona na Sara wamejitolea kuwa somesha watoto wao wa kike ile waweze kujikimu kimaisha. Kifungua mimba wao, Neema, alisoma hadi Chuo kikuu na kupata shahada mbili. Wanawalea mabinti hao badala ya kuwaelekezea ndoa za mapema kama njia moja ya kutoroka uhitaji wa kiuchumi waliokuwa nao.
  • Neema na Bunju wanaonyesha malezi kwa kuwasomesha ndugu za Neema hadi kuhitimu Chuo kikuu. Bunju anasema kuwa waliishi na Salome huku wakimlipia karo ya shule ya upili na chuoni (uk. 28). Bunju na Neema vilevile wanamlea mtoto wao Lemi. Wanamsaidia kufanya kazi ya ziada ya shule.  Bunju na Neema pia wanang’ang’ana kumpeleka mtoto wao , Mina, shule ya malezi ilia pate elimu ya kiwango cha juu.
  • Bunju na Neema wanasawiriwa kama wazazi ambao hawajawajibika katika kuwalea watoto wao kikamilifu. Wanamwajiri Bela ili awasaidie katika ulezi wa Lemi na shughuli za pale nyumbani. Mtoto wao Mina anasoma katika shule ya bweni, kwa hivyo mara nyingi hayuko nyumbani bali yuko shuleni. Hii ina maana kuwa malezi ya Mina yanatekelezwa na walimu wake. Vilevile, Neema anahuzunishwa na jinsi anavyokosa muda wa kuonana na mwanawe Lemi. Mara nyingi akitoka asubuhi Lemi huwa amelala na akirudi vilevile huwa amelala (uk. 22).
  • Bunju anasema kuwa mara nyingi Neema hayupo nyumbani na kuwa yeye ndiye humsaidia Lemi kufanya kazi ya ziada (uk. 49). Kwa kuwa wameshikana na kazi zao, tunaelezewa kwamba Neema na Bunju huwa sana wanampata mtoto wao keshalala. Lemi kwa mara nyingi anapoamka humpata mama yake ameshaenda kazini. 
  • Bunju na Neema pia wanaonekana kujaribu wawezavyo kuwa na uhusiano mwema na mwanao Lemi. Haya wanafanya kwa kufanya naye kazi za ziada (homework) na hata kumpeleka nje mara kwa mara kujivinjari. Bunju na Neema wameshugulika kuwasaidia wazazi wa Neema, Yona na Sara kadri ya uwezo wao. Wameshugulikia kwa kumpeleka Sara hospitalini. Bunju amewasomesha dada zake Neema hadi wote wakahitimu shuleni. Ndugu zake wakubwa wa Bunju wanatajwa kuwa wamewashughulikia mahitaji wazazi wao. 
  • Bela anakuza maudhui ya malezi kwa sababu ameajiriwa kama mfanyakazi nyumbani kwa Neema. Bela ameiacha familia yake na kuja kuifanya kazi ya kumlea Lemi. Bela amezoeana sana na Lemi kuliko alivyozoeana na mamake Neema. Bela anamfahamisha Neema jinsi Lemi anavyoendelea. Anamwambia kuwa Lemi alikuwa amekula na keshalala kwa sababu ya uchovu uliotokana na mazoezi ya shuleni. Bela anasema kuwa kila baada ya kutoka shule, Lemi humwonyesha jinsi walivyocheza shuleni. Hii ina maana ya kuwa Bela ndiye aliyekuwa mlezi wa karibu wa Lemi. Bela anamweleza Neema kwamba yeye amefanya kazi akiwa mbali na nyumbani na hajaweza kuwalea watoto wake kwa ukaribu hadi wamekuwa wakubwa na wakahama, wote wana makwao.
  • Yona anamsifia Sara kwa kumsaidia katika kuwalea na kuwasomesha mabinti wao. Anasema alikuwa akiwaangalia ng'ombe shambani huku Sara akipeleka maziwa na kuuza bidhaa walizozalisha sokoni (uk. 62).
  • Malezi katika maisha ya mjini yanasawiriwa kama ya ajabu. Yona anasema kuwa malezi mjini ni magumu sana. Watu wa mjini huraukia vibarua na kurudi watoto wakiwa wamelala. Wanaishi wiki nzima hawajaonana na watoto wao. Malezi yameachiwa yaya. Yaya ambaye anaweza kumfundisha mtoto lugha au tabia aitakayo. Ulezi umejaa mashaka (uk. 59).

Taasubi ya Kiume

  • Taasubi ni hali ya jamii kuthamini jinsia moja kuliko nyingine. Jamii katika tamthilia ya Bembeaya Maisha imemthamini mwanamume kuliko mwanamke kwa njia zifuatazo.
  • Mwanamume amesawiriwa kama mtu anayeweza kurithi mali ya familia. Hii ni kuonyesha kuwa mwanamume tu ndiye mwenye uwezo huo (uk. 2).
  • Sara anasema fimbo hurithiwa na watoto wa kiume wala si wa kike. Jamii inamshinikiza Yona kuoa mke mwingine ili aweze kumzalia mtoto wa kiume ambaye atakuwa mrithi wa fimbo yake.
  • Mwanamume ameonyeshwa kama mtu asiyestahili kuhusika na kazi ambazo zinaaminika ni za mwanamke. Kazi kama vile kupika na kuteka maji kisimani ni kazi ambazo zinaamika kuwa kazi za wanawake.
  • Beni anamwambia Yona amekaa muda mwingi kama mkewe hayuko nyumbani. Beni anamuuliza Yona nani anayempikia muda wote huo kwani umri wake si wa kuingia jikoni kujipikia (uk. 61).
  • Sara naye anamkaripia mwanawe Asna ambaye anasema haoni ubaya wa baba yake kwenda kujitekea maji kisimani. Sara anasema kwamba itakuwa aibu kubwa na wanajamii watamtazama Yona kwa dharau (uk. 44-45).
  • Katika uk. 1, tunamwona Yona aliyekinai na kukasirishwa na Sara ambaye ameketi palepale ilhali hajamwandalia chakula. Yona hajali kuwa mkewe anaugua, haja yake ni chakula. Kwa sababu ya mila za jamii, Yona hawezi kuingia jikoni kuandaa chakula. Inamlazimu Sara kumwita Dina ili aje amsaidie katika maandalizi ya chakula. Suala hili limetiliwa mkazo katika mazungumzo ya Sara na Dina (uk. 14), kuwa mwanamume hawezi kusaidia katika kazi zozote za jikoni. 

Utamaduni

  • Utamaduni una nafasi muhimu katika jamii ya Sara na Yona. Wanajamii wanaamini kuwa kuna mafunzo mengi ambayo yanatokana na mila na desturi za jamii hiyo.
  • Katika jamii ya Yona na Sara, kuna msisitizo mkubwa kwamba kila familia sharti iwe na mtoto wa kiume. Familia zenye watoto wa kike peke yake zinadhihakiwa na kudharauliwa kama ilivyofanyiwa familia ya Yona na Sara. Luka anapinga mwelekeo huu na kuwathamini watoto wa jinsia ya kike (uk. 60).
  • Utamaduni unajitokeza katika baraza la wazee: Luka, Beni na Yona. Luka anawaalika wazee wenzake ili kunywa, kucheza na kufurahia mazao yao (uk. 64).
  • Luka anataja kuwa mavuno ya kwanza huonjwa na wazee na kutoa baraka (uk. 58).
  • Utamaduni unasawiriwa kama jambo lililopitwa na wakati kulingana na ulimwengu wa leo. Kwa upande mwingine, utamaduni unazidi kutiliwa mkazo katika ulimwengu wa jana. Bunju anakubaliana na utamaduni wa kutowakubali wazazi na wakwe zake kulala nyumbani kwake.
  • Bela na Neema kwa upande mwingine wanapinga mawazo hayo na kusema kuwa utamaduni huo umepitwa na wakati na kuwa hauna nafasi katika ulimwengu wa leo uliojaa mabadiliko ya kila aina (uk. 24, 29).
  • Asna anasema kuwa dunia imebadilika, ya zamani yamepita (uk. 36).
  • Mila na desturi za jamii huwa na mafunzo ya kudumu. Sara aliishi wakati wa jana na leo. Anatoa mafunzo kwa wanawe kuhusu utamaduni wa jana. Wakati Asna na Neema wanamwambia kuwa hakuna tatizo lolote anapolala nyumbani kwa Neema na Bunju, anadai kuwa mila zina mahali pake (uk. 36).
  • Kulingana na mila na desturi za kizazi cha jana, msichana akisha baleghe, sharti aozwe (uk. 52).
  • Mila na tamaduni za kizazi cha jana kinawajenga wanaume kama watu wasioweza kusaidia katika kazi za jikoni. Kazi zote za jikoni zimeachiwa wanawake. Hata mume anapomsaidia mkewe kazi hizo, anaonekana kushushwa hadhi yake (uk. 14).
  • Inasemekana kuwa watu watamcheka na kusema amekaliwa (uk. 66).
  • Mtoto wa kiume huwa kiungo kikubwa sana cha familia kulingana na utamaduni wa jamii za kiafrika.
  • Tunapata Sara anakosa kujaliwa mtoto wa kiume hali ambayo wanajamii wanaona si sawa hivyo basi wanaanza kumshauri Yona aoe mke wa pili ili amzalie mtoto wa kiume.
  • Aidha anashauriwa kutafuta mtoto wa kiume nje ya ndoa lakini anakataa kushaurika kisa na maana ana msimamo wake na hataki ushawishi wa watu kwenye ndoa yake.

Elimu

  • Suala la elimu limepewa kipaumbele katika tamthilia ya Bembea ya Maisha hasa na kizazi cha leo. Maudhui haya yamekuzwa na Yona, Mina, Lemi, Sara na watoto wa Dina.
  • Yona ni mwenye elimu kwa sababu alikuwa mwalimu. Yona anasema kuwa wakati alipokuwa mwalimu, alikuwa akienda skuli wakati wa majira ya alfajiri, kiboko mkononi. Anasema kuwa siku nzima ilikuwa kazi tu, jioni ni darasani tena.
    Alipotoka shule, alikuwa akivifunga vitabu kwenye baiskeli kwenda kuvisahihisha wikendi (uk. 62).
  • Yona amesoma hadi Chuo kikuu. Alikuwa mtu wa kwanza pale kijijini kufuzu kutoka chuoni.
  • Mabinti wa Yona na Sara wanasawiriwa kama watoto walio na elimu.
  • Elimu ya Neema inadhihirishwa tunapoambiwa kuwa amesoma hadi Chuo kikuu na kuhitimu shahada mbili. Bunju anasema kuwa Asna amesoma hadi Chuo kikuu alikohitimu digrii vilevile. Salome naye ameishi nyumbani kwa Bunju na Neema huku akisoma Shule ya upili.
  • Baadaye anafanikiwa kwenda Chuo kikuu alikopita na kupata first class. Alibahatika kupata ufadhili wa kwenda kuendeleza masomo yake ng'ambo (uk. 28).
  • Elimu imeonyeshwa kupitia watoto wa Neema na Bunju: Mina na Lemi. Mina anasemekana kuwa anasomea Shule ya bweni. Lemi naye anakuza elimu kwa jinsi anavyoshiriki katika kazi yake ya ziada baada ya kutoka shuleni. Bela anamweleza Neema jinsi Lemi hujinengua anapocheza nyimbo za shuleni. Elimu imesawiriwa kama nguzo ya ufanisi katika maisha ya leo. Wahusika waliosoma na kuhitimu kama vile Yona, Neema na Sara wanafanikiwa kupata kazi na kuwa mwanga wa kijijini.
  • Yona na Sara wanaelimisha watoto wao.
  • Mwanao Neema anafanikiwa kupata kazi nzuri inayomwezesha kujiendeleza kimaisha na vilevile kuweza kugharamia matibabu ya mamake.
    Isitoshe,anasalia kuelimisha watoto wake pia.
  • Anajaliwa mume mzuri pia kutokana na elimu alio nao,hii ni kulingana na Yona .

Migogoro

  1. Migogoro ni hali ya mvutano au kutoafikiana baina ya pande mbili au zaidi. Migogoro katika tamthilia huzuka kwa sababu ya mambo mbalimbali yanayokinzana. Katika tamthilia hii kuna migogoro ya kitamaduni kati ya wanausasa na wanakizazi cha jana, migogoro katika ndoa, maisha na maendeleo ya mjini na kijijini.
  2. Kuna mgogoro wa kitamaduni kati ya kizazi cha leo na kizazi cha jana kinachoshikilia imani zilizopitwa na wakati. Kwa mfano, Asna anamwona babake angali kijana na ana uwezo wa kutekeleza majukumu ya nyumbani kama vile kuteka maji kisimani. Wazo la Asna linaleta mvutano baina yake na mamake. Sara analiona wazo hilo kama bovu na lisiloweza kutekelezwa na mumewe kwa sababu ya jinsi wanajamii watakavyomchukulia. Sara anasema kuwa wanajamii watamshushia hadhi na watamtazama kwa sini ya dharau (uk. 44-45).
  3. Utamaduni unazua mgogoro kati ya Asna na Sara. Kulingana na Sara, utamaduni wa jamii unamtaka kila msichana aliyebaleghe aozwe.
  4. Asna anapinga utamaduni huo na kudai kuwa, hilo ni jambo lililopitwa na wakati. Asna anadai kuwa msichana anaweza kuolewa au kukosa kuolewa. Na anapotaka kuolewa, anaweza kuolewa kwa wakati autakao yeye bali Sio kwa wakati wanaotaka wanajamii.
  5. Mgogoro unajitokeza baina ya mawazo ya Bunju kuhusu mila zinazowakataza wazazi kulala nyumbani kwa mkwe na mawazo ya Neema, Asna na Bela. Neema anapinga mawazo hayo na kusema kuwa mila hizo hazina thamani wala nafasi tena katika dunia ya sasa (uk. 29). Asna naye anayapinga mawazo hayo kwa kusema kuwa dunia imebadilika (uk. 36). Bela vilevile anapinga wazo hilo kwa kusema kuwa hayo ni ya kale na kuwa watu wengi hawafuati mila hizo kwani ulimwengu umebadilika (uk. 24).
  6. Kuna migogoro ambayo inazuka katika asasi ya ndoa. Ndoa ya Sara na Yona ni yenye migogoro. Yona anasababisha mgogoro baina yake na Sara kwa kumchapa na kumkosea hadhi Sara kwa kukosa mtoto wa kiume.
  7. Mgogoro huu unasababisha Sara kupatwa na maradhi ya moyo na kumfanya mwanawe Asna kuona ndoa kama doa.
  8. Ndoa ya Bunju na Neema ina mvutano kuhusu suala la matumizi ya pesa na suala la malezi ya mtoto wao Lemi. Bunju ana msimamo wake kuhusu majukumu yake kwa familia yake na kusema gharama ya matibabu ya mamake Neema Sio jukumu lake.
    Neema anahisi kuwa
  9. Bunju anaweza kumsaidia katika matibabu ya mama yake. Wawili hao wanavutana kuhusu suala hilo. Wazo la Bunju linamfanya kumuona kama mkono birika na asiyetaka kuwasaidia.
  10. Neema na Bunju wanavutana vilevile kuhusu suala la kumpeleka Lemi kwenda kucheza na kuogelea na wenzake. Neema anamsihi Bunju ampeleke Lemi kujivinjari lakini Bunju anasema kuwa hawezi kwenda huko badala ya kwenda kuvuta riziki. Isitoshe, anadai kuwa michezo hiyo hununuliwa si kama ya zamani (uk. 48).
  11. Bunju anasema kuwa Neema anapenda kukana na lazima abishe jambo ambalo litamfanya kuonekana mbwa kasoro.
  12. Kuna mgogoro baina ya wanajamii na familia ya Yona. Mvutano unazuka wakati ndoa ya Yona na Sara inakosa kujaliwa na mtoto.
  13. Wanajamii wanaikejeli na kuisuta ndoa hii na kumuita Yona gumba na Sara tasa. Hata wanapopata watoto wasichana bado jamii inawasuta kwa kukosa mtoto wa kiume.

Maudhui ya kazi

  • Yona na Sara wanapata nafasi ya kuajiriwa kama wafanyi kazi wa nyumbani baada ya yule mfanyikazi wa kwanza kutoroka kwa kuzidiwa na kazi.
  • Tunapata kwamba kizazi ya sasa hawawajibiki kazini kisa na maana wanataka kutajirika haraka bila kufanya kazi inavyofaa. Hii ndio sababu ya wengi wao kutoroka kazi.
  • Sara anafanya kazi kwa bidii wakati anapolea wanawe.
  • Neema na mumewe nao wanawajibika katika kazi zao ili kujiendeleza kimaisha.

Maudhui ya maradhi

  • Sara anapatwa na maradhi ambayo yanasababishwa na mateso mengi anayoyapitia mikononi mwa bwanake Yona.
  • Maradhi haya yanaleta gharama zaidi katika nyumba ya Yona na Sara. Neema anawajibika katika kugharamia matibabu ya mamake.

Nafasi ya watoto katika ndoa

  • Watoto huonekana kuwa muhimu sana katika ndoa.
  • Na mara nyingi jamii huonea fahari ikiwa na mtoto wa kiume.
  • Katika tamthilia ya ‘Bembea ya Maisha’ tunaona mtoto kama mwokozi.
  • Neema ambaye ni mtoto wa sara anagharamia matibabu ya mamake anapougua kutokana na dhulma.

Changamoto ya maisha ya kisasa

  • Changamoto za malezi yanaonekana pale tunapoona kwamba wanaoishi mjini hawawezi kuwalea watoto wao kwa ukaribu
  • Changamoto za kazi –
    • Neema pia anahofia hali ya Bunju kwa sababu makampuni yamekuwa yakiwafuta kazi wafanyikazi wao kwa wingi.
    • Asna anamweleza mama yake kwamba wao wanaoishi mjini wanaishi kwa kushikilia lolote wanachopata.
  • Asna anaishi kwa upweke kwa mtaa wa kifahari. Kwake, bora watu wan je wameona anatoka mtaa wa kifahari na hawajui jinsi anavyoishi haoni shida.
  • Bunju anakiri kwa Neema kwamba anaishi kwa madeni ili aweze kuikimu familia yake. Anamwambia kwamba anazo shida nyingi lakini amejivalish tabasamu watu wasizweze kubaini shida zake.
  • Watoto wa vizazi vya sasa hawana uhusiano wa karibu na tamaduni na mila zao.
  • Kwa mazungumzo ya Kiwa na mamake Dina, tunaelewa kuwa bila elimu mtu hawezi pata faraja miashani. Kwa maneno ya Kiwa, dunia ya leo haithamini misuli il akili.

Dhamira ya mwandishi

Dhamira huelezwa kama lengo au shabaha ya mwandishi wa kazi ya fasihi.
Mwandishi wa tamthilia ya Bembea ya Maisha anadhamiria:

  • kuonyesha masaibu ya pombe katika maisha ya familia
  • kuonyesha kuwa ili kujenga jamii mpya, mapinduzi ni muhimu na ni lazima wanajamii wajitolee kupinga tamaduni zisizo na umuhimu wowote katika maisha ya wanajamii
  • kutuonyesha kuwa watoto wa jinsia zote ni sawa na hawafai
  • kutenganishwa kwa mila na tamaduni za jamii
  • kutuonyesha kuwa hakuna lililo na mwanzo lisilokuwa na mwisho.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Dhamira na Maudhui Katika Bembea ya Maisha - Mwongozo wa Bembea ya Maisha.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?