KISWAHILI PAPER 3 - 2019 KCSE STAREHE MOCK EXAMS (QUESTIONS AND ANSWERS)

Share via Whatsapp

MAAGIZO

  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la lazima
  • Maswali hayo mengine yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki, yaani: tamthilia, fasihi simulizi, hadithi fupi na riwaya.

SEHEMU YA A: SHAIRI -SWALI LA LAZIMA

  1. S.Khatib:Fungate ya Uhuru
    Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali yanayofuata
    Maendeleo ya umma
              Sio vitu maghalani
               Kama tele vimesaki
               Lakini havishikiki
    Ama havikamatiki
    Ni kama jinga la moto
    Bei juu
    Maendeleo ya umma

    Sio vitu gulioni
               Kuviona madukani
               Kuvishika mikononi
               Na huku wavitamani
    Kama tamaa ya fisi
    Kuvipata ng’o
    Maendeleo ya umma

    Sio vitu shubakani
               Dhiki ni kwa mafakiri
               Nafuu kwa matajiri
               Ni wao tu washitiri
    Huo ni ustiimari
    Lo! Warudia
    Maendeleo ya umma

    Ni vitu kumilikiwa
               Na wanyonge kupatiwa
               Kwa bei kuzingatiwa
               Bila ya kudhulumiwa
    Na hata kuhadaiwa
    Hiyo ni haki
    Maendeleo ya umma

    Dola kudhibiti vitu
             Vijapo nchini mwetu
               Na kuwauzia watu
               Toka nguo na supatu
    Pasibakishwe na kitu
    Huo usawa
    Maendeleo ya umma

    Watu kuwa na kauli
               Katika zao shughuli
               Vikaoni kujadili
               Na mwisho kuyakubali
    Maamuzi halali
    Udikteta la
    Maendeleo ya umma

    Watu kuwa waungwana
               Vijakazi na watwana
               Nchini kuwa hakuna
                Wote kuheshimiwa
    Wazee hata vijana

    Maswali
    1. Huku ukitoa mifano, toa ithibati kuwa hili ni shairi huru     (alama 5)
    2. Mtunzi wa shairi hili alidhamiria nini?          (alama 1)  
    3. Bainisha matumizi mawili ya tamathali za usemi katika shairi hili.              (alama 2)  
    4. Andika ubeti wa nne kwa lugha ya kawaida       (alama 4)
    5. Eleza mambo yanayodhihirisha kuwa nchi imepiga hatua kiuchumi kwa mujibu wa shairi hili.       (alama 4)                                       
    6. Eleza kwa kutoa mfano mbinu ambayo mtunzi wa shairi hili ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi katika ubeti wa sita. (alama 2)                                  
    7. Eleza aina ya urudiaji unaojitokeza katika ubeti wa pili na uonyeshe umuhimu wake katika shairi hili.  (alama 2)

SEHEMU YA B: RIWAYA
Assumpta K. Matei: chozi la Heri
Jibu swali la 2 au la 3.

  1. Riwaya ya Chozi la Heri inasawiri adha zinayozikumba nchi za Kiafrika. Thibitisha kwa kutoa mifano mwafaka.        (alama 20)
  2. “Vijana hawapaswi kungojea kufanyiwa kila kitu. Tumewapa nyavu za kuvulia, nao wanaona wangoje kuletewa samaki!”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili                                                                                    (alama 4)
    2. Fafanua maudhui yanayodhihirika katika dondoo hili                                                  (alama 2)
    3. Tambua na ueleze mbinu mbili za kimtindo zinazojitokeza katika dondoo hili           (alama 4)
    4. Eleza maafa yaliyomwandama msemaji wa kauli hizi                                                  (alama 4)
    5. Taja na ueleze sifa sita za msemewa                                                                             (alama 6)

SEHEMU YA C: TAMTHILIA
Kea: Kigogo
Jibu swali la 4 au la 5

  1. Tamthilia ya Kigogo imesheheni mambo ya kukatisha tamaa. Thibitisha huku ukitoa mifano inayofaa.   (alama 20)
  1. “Walikuwa wanataka kukukanganya tu ili usiweze hata kuwakisia waliokudhuru”
    1. Eleza umuhimu wa msemaji katika dondoo hili                                                          (alama 4)
    2. Ni maudhui yapi yanayodhihirika katika dondoo hili?                                              (alama 2)
    3. Msemewa na wenzake ambao wanapigania ukombozi pamoja walikumbana na vizingiti anuai. Eleza kwa kutoa mifano (alama 14)

SEHEMU YA D: HADITHI FUPI
A.Chokocho na D. Kayanda: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine
Jibu swali la 6 au la 7. 

Ali A. Ali: Ndoto ya Mashaka

  1. “Na kwa nini hazitaki kuukemea mfumo huu wa maisha? Mfumo wa mwenye nacho kuendelea kupata na msinacho kuendelea kukosa?”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili                                                                        (alama 4)
    2. Fafanua maudhui mawili yanayodhihirika katika dondoo hili                          (alama 4)
    3. Tambua na ueleze sifa sita za msemaji                                                           (alama 6)
    4. Eleza athari ya “msinacho kuendelea kukosa” katika jamii husika                         (alama 6)
  1. Fafanua jinsi suala la elimu limeshughulikiwa katika Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine kwa kurejelea hadidhi zifuatazo:
    1. Mapenzi ya Kifaurongo                                                                             (alama 5)
    2. Shogake Dada ana Ndevu                                                                               (alama 5)
    3. Mtihani wa Maisha                                                                                         (alama 5)
    4. Mwalimu Mstaafu                                                                                           (alama 5)

SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI

  1. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali
       Hapo zamani za kale paliishi mtoto katika kisima kimoja. Siku moja mtoto huyu aliokota kijiwe karibu na soko kuu. Kijiwe kilikuwa kikimeremeta kwa rangi mbalimbali na kilizingirwa na pete ya dhahabu.
         Mtoto huyu na wenzake walianza kurushiana kijiwe hicho. Baada ya muda kilianza kuongezeka umbo na kuonekana kama kiwiliwili cha binadamu. Kikaanza kuwakimbiza wale watoto. Kutokana na ukelele wao, watu walikuja kutazama nini kilikuwa cha mno. Walipofika walikutana ana kwa ana na dubwana hilo. Lilizidi kuongezeka umbo na likawameza wote pamoja na mifugo wao. Wachache waliojaribu kukimbia liliwashika kwa mikono yake mipana na mirefu. Kwa bahati njema alikuwepo mama mmoja aliyeona hayo yote. Alikuwa mbali kiasi na hapo. Aliteremka kutoka kilele cha mlima na kuwapata wakulima makondeni na sawia akawajuza kuhusu kitendo kilichomwogofya sana. Wote wakaacha shughuli zao na wakatwaa silaha zao wakaelekea soko kuu.
             Dude sasa lilikuwa limejilaza baada ya shibe, wakulima wale walichagua watu sita ambao walijulikana kwa ushujaa wao. Pamoja walilinyemelea lile nyangarika na kulikata mara moja. Lilitoa mkoromo mkuu kabla halijakata kamba. Punde, wanakijiji kwa uangalifu mkubwa walitoboa tumbo lake wakitarajia kupata maiti za wapenzi wao pamoja na mifugo wao. Wote walijawa na furaha kuu walipoona wapenzi wao wakijichomoza kutoka tumboni, mmoja baada ya mwingine hadi akatoka yule wa mwisho. Mbuzi, kondoo na ng’ombe wote walitoka mmoja mmoja. Siku hiyo kuliandaliwa sherehe ya kumshukuru Muumba kwa wema wake. Watoto walishauriwa wasithubutu kuchezea vitu wasivyovijua.

    Maswali
    1. Ainisha kipera hiki cha hadithi                                                                                    (alama 1)
    2. Fafanua mambo manne yanayodhihirisha kuwa kipera hiki ni sanaa.                         (alama 4)
    3. Mwasilishaji bora wa kipera hiki anafaa kuwa na sifa gani? Eleza zozote nne.           (alama 4)                                                                          
    4. Onyesha mifano miwili ya fantasia katika hadithi hii.                                                 (alama 2)
    5. Eleza majukumu manne ya tungo hizi kwa wanajamii                                                 (alama 4)
    6. Eleza majukumu matano ya mtindo uliotumiwa kuanzisha hadithi hii.                       (alama 5)


MARKING SCHEME

  1. Swali la kwanza
    1. Lina urudiaji mwingi- mshororo “maendeleo ya umma”
      • Usambamba –urudiaji wa kimuundo katika ubeti wa pili
      • Lina uakifishaji-alama hisi katika ubeti wa tatu
      • Limekiuka sheria za kiarudhi kama vile urari wa mizani
      • Lina mishata-mishororo isiyokuwa kamili-mshororo wa kwanza katika beti za kwanza nne
    2. Kueleza mambo yanayodidimiza maendeleo
    3. Takriri-kuna mishororo iliyorudiwarudiwa
      Tashbihi-ni kama jinga la moto, kama tama ya fisi
      Kinaya-vitu kujaa maghalani lakini haviwanufaishi watu
    4. Maendeleo ya umma ni vitu kumilikiwa na wanyonge kupewa kwa bei ambayo wanaweza kumudu bila kuwadhulumu wala kuwadanganya kwani hiyo ndiyo haki.
    5. Wanyonge kupewa vitu kwa bei nafuu bila kudhulumiwa wala kudanganywa
      Dola inapodhibiti kila kitu kilichoagizwa nchini
      Watu kuhusishwa/ kuruhusiwa kutoa maoni katika shughuli bila udikteta
      Kuwepo kwa usawa wa watu wote
    6. Kuboronga sarufi-katika zao shughuli badala ya katika shughuli zao
    7. Usambamba-urudiaji wa kimuundo
      Kuviona madukani
    8. Kuvishika mikononi
      Huleta mdundo fulani katika shairi linapokaririwa
  2. Swali la pili
    • Ukabila-ukoo wa Anyamvua na Waombwe wanachukiana
    • Vita vya baada ya uchaguzi-vita vinazuka baada ya kutawazwa kwa kiongozi wa kike
    • Unyakuzi wa ardhi-katika hotuba ya Lunga, ni bayana kuwa viongozi hunyakuwa ardhi iliyotengewa misitu
    • Ukatili-wanawe Kaizari, Lime na Mwanaheri wanabakwa wakati wa vita vya baada ya uchaguzi
    • Uporaji wa mali-katika harakati za vita mali ya watu inaporwa
    • Uharibifu wa mazingira-mwandishi anaeleza kuwa wakimbizi wanaohamia Msitu wa Mamba wanaanza kukata miti na kuendeleza shughulu za kilimo
    • Ukosefu wa ajira-mja mmojawapo wa waliozua vurumai anasikika katika runinga akisema kuwa mtu anaweza kuwa na shahada kadha ilhali hana ajira
    • Taasubi zinadidimiza maendeleo-baada ya kiongizi wa kike kuapishwa vurumai zinaanza huku wengine wakidai kuwa huko ni kumkosea mwanamume heshima
    • Ufisadi-viongozi kunyakua ardhi ya umma na kujenga viwanda vyao
    • Tama ya uongozi-Mwanzi, mpinzani wa kiume wa kiongozi aliyeapishwa anachochea umma kuzua vurumai
    • Umaskini-tunaelezwa kuwa katika Msitu wa Mamba walikutania watu wa matabaka yoe mawili: tajiri na maskini
    • Matumizi mabaya ya vyombo vya dola-askari wanawashambulia wakimbizi wanaoishi katika Msitu wa Mamba na kuangamiza baadhi yao
    • Udanganyifu-ridhaa anamtahadharisha Mwangeta asije akauziwa ardhi ambayo tayari imeuzwa: jambo ambalo ni kawaida sana katika jamii hii
    • Ukiukaji wa haki za kibinadamu/watoto
      (zozote 10 × 2 = 20)
      Tanbihi : mtahini ambaye hatarejelea nchi za Kiafrika atuzwe sufuri
  3. Swali la 3
    1. Ridhaa anakumbuka akimweleza Tila katika dayalojia kati yao wakiwa nyumbani mwao baada ya Tila kurejea nyumbani kutoka shuleni na kumweleza waliyofunzwa na Mwalimu Meli
    2. Nafasi ya vijana katika jamii-anasema kuwa vijana wanafaa kutumia elimu waliyopewa kutafuta riziki
    3. Jazanda-neno nyavu kumaanisha ujuzi/ elimu, samaki kumaanisha riziki, kuvua-kutafuta riziki
      Kinaya –vijana kungoja wapewe mahitaji yao ilhali wamepewa uwezo wa kukidhi mahitaji hayo
      Kutaja-alama moja, mfano-alama moja
    4.  
      • Kuipoteza aila yake kwa moto katika vita vya baada ya uchaguzi
      • Kupoteza majumba yake yaliyobomolewa kwa madai kuwa yalikuwa yamejengwa kwenye sehemu iliyotengewa barabara
      • Kupoteza jumba alilokuwa amepangishia wafanyabiashara kufuatia mkasa wa moto
      • Nduguye-Makaa kufa katika Mkasa wa moto katika lori la kusafirisha mafutalililobingirika
      • Mwanawe Dede kufariki dunia akiwa na umri wa miaka sita
    5. Sifa za Tila
      • Msomi-alikwa mwanafunzi katika mojawapo wa shule
      • Mtambuzi-anatambua kuwa nchi yao haijapiga hatua kiuchumi anavyodai babake
      • Mshawishi-anawashawishi nguguze kuigiza mviga wa mazishi ya nduguye Dede aliyeaga dunia
      • Mbunifu-anabuni jeneza wanapoigiza mviga wa mazishi ya nduguye
      • Mwenye mtazamo pevu-anasema kuwa yu tayari kumchagua kiongozi anayefaa bila kuzingatia jinsia
      • Makini –anamakinika darasani kiwango cha kuweza kumhadithia babake waliyofunzwa na Mwalimu Meli
        (6×1=6)
  4. Swali la nne
    • Mauaji-jabali anauliwa na Mojoka kwa kuwa katika chama pinzani
    • Tamaa ya uongozi-Majoka anawashambulia wapinzani wake ili aendelee kutawala, kwa mfano Tunu
    • Uharibifu wa mazingira-Hashima anasema kuwa kigogo amefungulia ukataji wa miti
    • Ufisadi-Majoka anafunga soko ili ajijengee hoteli ya kifahari
    • Matumizi ya dawa za kulevya-Tunaelezwa kuwa Ngao Junior amekufa kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya
    • Ukosefu wa ajira-kuna watu walioelimika ilhali hawana elimu.Kwa mfano, Ashua
    • Umaskini –Ashua anaenda kwa Majoka ili kuomba msaada kwani wanawe hawana chakula
    • Udikteta-Majoka anaagiza kufungwa kwa soko bila kuzingatia maoni ya wafanyabiashara
    • Unyakuzi wa ardhi-Majoka ananyakua ardhi iliyokuwa imetengewa soko
    • Unyanyasaji-Majoka anamtia Ashua kifungoni bila hatia bayana
    • Matumizi mabaya ya vyombo vya dola-askari wanawashambulia wachuuzi walioandamana na kuangamiza baadhi yao
      (Zozote 10 × 2=20)
  5. Swali la tano
    1. Umuhimu wa Siti
      • Ametumika kudhihirisha maudhui ya unyanyasaji kwani kupitia kwake tunajua kuwa bei ya chakula katika kioski cha kampuni imeongezwa tangu kufungwa kwa soko
      • Anatumika kudhihirika sifa za Majoka-kupitia kwake tunajua kuwa Majoka ni mnyamnyasaji kwani anaongeza bei ya chakula katika kioski cha kampuni ilhali soko limefungwa
      • Ni kielelezo chema cha kuigwa kwani Ngurumo anaeleza kuwa hapo awali alikuwa mlevi lakini anaamua kubadilika na kuacha ulevi
      • Ametumika kuonyesha madhara ya uongozi mbaya kwani anatueleza kuhusu walivyoandamana
      • Anaendeleza mchezo kwani amehusika katika baadhi ya matukio
        (Zozo 4×1=4)
    2. Ujanja-wanajaribu kumkanganya Tunu ili adhani kuwa anaendewa kinyume na Sudi ilhali ni wahuni waliotumwa na Majoka
    3.  
      • Kuuliwa-wapinzani kama vile Jabali wanauliwa
      • Kuvamiwa-Tunu anavamiwa na vikosi vya kihuni vya Majika na kujeruhiwa mguu
      • Vitisho-Tunu anapomwonya dhidi ya mauaji Majoka anamwambia kuwa asimshawishi kumtia ndani
      • Dhihaka-Tunu anadhihakiwa na vijana huko Mangweni akiambiwa kuwa aolewe badala ya kujihusisha na siasa
      • Kutiwa gerezani-mke wa Sudi anatiwa gerezani ili kumshawishi Sudi kuchonga kinyago cha Mojoka
      • Kushambuliwa-wanaoandamana dhidi ya kufungwa kwa soko wanashambulia na askari na kujeruhiwa
      • Usaliti-wanaopigania ukombozi wanasalitiwa na watu kama vile Ngurumo ambao wanaunga uongozi mbaya mkono
        (zozote7 × 2=14)
  6. Swali la sita
    1. Mawazo ya Mashaka baada ya mkewe kumtoroka akiwaza kuhusu umaskini unaozikumba nchi za Kiafrika kama vile Kenya na Tanzania.
    2.  
      • Utabaka-anazungumzia mfumo wa mwenye nacho na msinacho kumaanisha matajiri na maskini.
      • Umaskini-kuna watu maskini ambao anawarejelea kama msinacho
      • Ubinafsi-kuna watu ambao wanaendelea kutajirika ilhali wengine wanaendelea kuselelea katika lindi la umaskini
        (Zozote mbili: kutaja-alama moja, kueleza alama moja)
    3.  
      • Mwenye bidii-anafanya vibarua anui ili kukidhi mahitaji yake na Bi. Kidebe
      • Msomi-anaelimika hadi chumba cha nane
      • Mwenye kutamauka –mkewe anapomtoroka anatamauka kwani anasema kuwa amechoka kungoja
      • Mwenye mapenzi-anampenda mkewe kwani anamlinganisha na ua la waridi
      • Mwenye tamaa-anatamani mabadiliko ya kumtoa katika hali yake ya umaskini
      • Mwenye mtazamo finyu-wanapata watoto wengi ilhali wanafamu kuwa hali yao ya kiuchumi haitawaruhusu kuwakimu
      • Mvumilivu-anavumilia hali yake ya umaskini kwa muda mrefu
        (Zozote 6×1=6)
    4. Athari ya umaskini:
      • Utengano –Waridi anamtoroka Mashaka kwa misingi ya kuwa maskini
      • Majuto-Mashaka anajutia hali yake ya umaskini na kutamani kuwa angekuwa tajiri kwani mkewe hangemtoroka
      • Aibu-Mzee Rubeya-babake Waridi anatorokea Yemeni kwa vile bintiye ameolewa na mtu maskini
      • Kukatiziwa elimu-Mashaka anaacha kundelea na masomo ya juu kwa kukosa pesa
      • Ajira ya watoto-Mashaka akiwa na umri mchanga analazimika kufanya ajira ya watoto ili apate mahitaji yake
      • Kutamauka-Katika ndoto, Mashaka anawaona wanyonge wakiandamana huku wakisema kuwa afadhali wafe
      • Hali duni ya maisha-tunaelezwa kuwa makazi ya watu wa Tandale yalivyochafuka na kwamba hakuna mfumo mwafaka wa kusafisha
      • Dharau-Mashaka anasema kuwa laiti angekuwa tajiri mkewe angemheshimu
        (Zozote 6×1=6)
  7. Swali la saba
    1. Mapenzi ya kifaurongo
      • Dennis anasema kuwa wazazi wake wamejitaabisha ili apate elimu
      • Dkt. Mabonga yumo ukumbini anasomesha somo la Fasihi
      • Dennis anasema kuwa wengi wa wanafunzi wenzake walisomea katika shule za mkoa na kitaifa
      • Mwanzoni mwa hadithi, wanafunzi wamo darasani wakifunzwa somo la Fasihi
      • Msimuli anaeleza kuwa kuna watu waliosoma sana kama Dkt. Mabonga
      • Elimu inatarajiwa kuwa nyenzo ya kuboresha maisha.Denis anatarajia kuwa akifuzu masomoni, Somo la Kiswahili litamfaa hasa kuwa mwandishi mtajika wa kazi ya fasihi
      • Dennis anapoenda kutafuta ajira anakutana na Shakila, msichana waliyekuwa wakisoma pamoja katika Chuo Kikuu cha Kivukoni
      • Katika jamii husika, elimu inatarajiwa kumwezesha mtu kupata ajira-Dennis anaenda kutafuta ajira akiwa na vyeti vyake vya elimu
    2. Shogake Dada ana Ndevu
      • Safia ni mwanafunzi anayetarajiwa kufanya mtihani ya kuingia kidato cha kwanza
      • Safia huibuka wa kwanza kabisa darasani- tunaelezwa kuwa ni hodari masomoni
      • Safia anawaomba wazazi wake ruhusa ya kumleta Kimwana nyumbani ili wadurusu pamoja
      • Wazazi wa Safia wanamshauri kuwa wawe wakifunga mlango kwa ndani wanapodurusu na Kimwana ili wasisumbuliwe na dadake mdogo
      • Kuna elimu ya dini-Bwana Masudi anasema kuwa Safia anatawaliwa na zile staha za kumwogopa Mungu kwa mujibu wa sheria, kanuni na amri zote alizoamrisha Mungu kupitia dini yao
    3. Mtihani wa Maisha
      • Samueli yuko kwenye foleni ya kuyaona matokeo yake ya mtihani wa kidato cha nne
      • Dada zake Samueli walipasi mitihani yao ya kidato cha nne kwenye Shule ya Upili ya Busukalala
      • Dadake Samueli, Bilha,ni mwanafunzi wa katika Chuo Kkuu cha Kenyatta naye Mwajuma ni mwanafunzi katika Chuo cha Ualimu cha Eregi
      • Elimu inatarajiwa kuwa nguzo ya kujikwamua kutoka kwa umaskini kwani mamake Smueli ana matumaini kuwa Samueli akifaulu masomoni basi hali yao ya maisha itakuwa bora
      • Samueli anapochukua matokeo yake wanafunzi ambao ndio mwanzo wamemaliza kipindi cha mwisho wanamzunguka wakitaka kujua alichopata
      • Kutofuzu katika elimu kunakatisha tamaa kwani babake Samueli anamhimiza ajitie kitanzi kwa sababu ameanguka mitihani
    4. Mwalimu Mstaafu
      • Mwalimu Mosi ni mwalimu mstaafu aliyewafunza wanafunzi wengi walioshia kufaulu maishani
      • Elimu ni mhimili mkuu katikakuboresha maisha kwani kuna wengi walioelimishwa na Mwalimu Mosi na sasa wana vyeo mbalimbali
      • Wanafunzi wa Mwalimu Mosi hawamsahau kwa nasaha, hekima na ustaarabu wake
      • Mwalimu Mosi hutaka kuandika tawasifu yake kuhusu maisha yake alivyosoma hadi chuo cha ualimu na kufundisha kwa zaidi ya miaka thelathini
  8. Swali la nane
    1. Ngano ya mazimwi
    2. Lugha imetumiwa kwa ufundi
      • Kina umbo maalum
      • Mandhari yamesawiriwa kwa ufundi mkubwa
      • Wahusika wamejengwakwa ufundi mkuu
    3.  
      • Awe mbunifu ili abuni hadithi upya
      • Ajue hadhira yake na mahitaji yake pamoja na kiwango cha elimu
      • Kuielewa na kumudu lugha ya hadhira yake
      • Kuyaelewa mazingira ya hadhira yake
      • Kuwa jasiri ili asimame mbele ya hadhira yake
      • Kuujua utamaduni wa hadhira yake asije akasema mambo ambayo huenda yakaudhi
      • Awe mfaraguzi ili aibuni upya kutegemea hadhira
      • Kuwa mcheshi ili hadhira ichangamke
      • Kuwa na uwezo wa kushirikisha hadhira yake kwa njia mbalimbali
      • Kuwa mbaraza ili kuingiliana vyema na hadhira yake
    4.  
      • Zimwi kuweza kumeza umati wa watu pamoja na mifugo
      • Watu na mifugo kutoka tumboni mwa zimwi wakiwa hai
    5.  
      • Hujaa uharibifu
      • Matumizi ya fantasia
      • Mazimwi kutenda mambo kama binadamu
      • Kipengele cha safari
    6.  
      • Kuvuta makini ya hadhira
      • Humtangaza mtambaji
      • Kuashiria mwanzo wa hadithi
      • Huweka mpaka kati ya ulimwengu halisi na ulimwengu wa hadithi
      • Kushirikisha hadhira na mtambaji
Join our whatsapp group for latest updates

Download KISWAHILI PAPER 3 - 2019 KCSE STAREHE MOCK EXAMS (QUESTIONS AND ANSWERS).


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest