Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Sukellemo Joint Mock 2020/2021

Share via Whatsapp

MTIHANI WA PAMOJA WA SUKELLEMO
KISWAHILI
KARATASI YA 3
FASIHI
Muda: Saa 2 ½

MAAGIZO

  • Jibu maswali manne pekee
  • Swali la kwanza ni la lazima
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki yaani; Riwaya, Hadithi Fupi, Ushairi na Fasihi Simulizi
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja
  • Majibu yote yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili sanifu

  1. SEHEMU A: TAMTHILIA P. Kea: Kigogo
    Swali la lazima
    1.  
      1. Mmesikia? Hamtatuletea wazimu wenu hapa! Nendeni kama mmekuja kutuhasimu.
        1. Eleza muktadha wa maneno. (alama 4)
        2. Jadili umuhimu wa msemaji kwa hoja nne. (alama 4)
        3. Fafanua mbinu ya lugha iliyotumika. (alama 2)
      2. Kenga alichangia pakubwa msiba wa Wanasagamoyo. Thibitisha kwa hoja zozote kumi. (Alama 10).

  2. SEHEMU B: RIWAYA Assumpta Matei: Chozi la Heri
    Jibu swali la II au III

    1. ‘…familia yake bado inamiliki mashamba ya michai na mibuni pamoja na mashirika mengi…’
      1. Weka dondoo hili katika muktadha wake. (alama 4)
      2. Kwa kurejelea mifano minane, eleza umuhimu wa msemaji katika kujenga riwaya hii. (alama 8)
      3. Jadili kwa hoja nane suala la ukoloni mambo leo lilivyoshugulikiwa katika riwaya. (alama 8)

        Au

    2. Tathmini umuhimu wa mbinu zifuatazo katika kuijenga riwaya ya Chozi la Heri
      1. Nyimbo (alama 10)
      2. Barua (alama 10)

  3. SEHEMU C: HADITHI FUPI; CHOKOCHO NA D. KAYANDA: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine
    Jibu swali la IV au V

    1. NDOTO YA MASHAKA
      "...dunia imenikunjulia mikono kunifariji baada ya kunicharaza fimbo yake aushi yangu yote."
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili (al.4)
      2. Tambua na ueleze mbinu ya lugha iliyotumiwa katika dondoo.(al.2)
      3. Eleza jinsi dunia ilimcharaza fimbo msemaji kwa kutolea hoja kumi na nne. (al.14)

        AU

    2. Kwa kurejelea hadithi ya Mapenzi ya Kifaurongo, Mame Bakari, Nizikeni Papa Hapa , Mtihani wa Maisha na Mkubwa, eleza changamoto zinazowakumba vijana. (al.20)

  4. SEHEMU D: USHAIRI
    Jibu swali la VI au VII

    1. SOMA SHAIRI LIFUATALO KISHA UJIBU MASWALI. (alama 20)

      Pana haja ya kupima, neno tuzowele –angu
      Tusizowee kusema , hili ni teuo langu
      Huenda huji mapema , -angu huja kuwa tungu
      Ikaja kukusakama, na kukuposha kwa Mungu
      Pana haja ya kupima.

      Neno huwa ni la kwako, likiwa ndani moyoni
      Lakini katu si lako, likishavuka menoni
      Kwa hivyo likutokako, liweke kwenye mizani
      Linaweza kuwa cheko, ama tusi kwa wendani
      Pana haja ya kupima.

      Vivyo hivyo kwa lebasi , huwa yako kisutuni
      Hivyo nina wasiwasi, wambe yako sebuleni
      Itavutiya matusi, ya wenzio insane
      Wakakuchoma nafusi, kwa mishale ya lisani
      Pana haja ya kupima.

      Mwana ujuwe ni wako, punje ukiimezele
      Lakini katu si wako, nde ukimuletele
      Akiwa yu ndani yako, ni wa duniya vivile
      Ukishishilia ni wako, muavye takakuole
      Pana haja ya kupima.

      Maisha nayo si wako, utabaradi milele
      Ungayaishi ja yako, ni tunu ya maumbile
      Mgawa si kufu yako, mshindane hili lile
      Akupapo akupoko, utaishi palepale
      Pana haja ya kupima.

      Ni chetu chako si chako, ulimwengu huwa vile
      Juhudi zingawa zako, wa kufaidi ni wale
      Ikifika siku yako, nyono zikukae mbele
      Ulichosema ni chako , huwabakiya wawale
      Pana haja ya kupima.

      Kaseme na moyo wako , Ubaini haya yale
      Ukiambacho ni chako , kisikupe mageule
      Kitu utajacho chako , huenda kiwe cha wale
      Na usemacho si chako, kiwe chako ndicho kile
      Pana haja ya kupima.

      MASWALI
      1. Eleza dhamira ya shairi hili. (alama 2)
      2. Eleza bahari zozote tatu za shairi hili. (alama 6)
      3. Andika ubeti wa nne kwa lugha tutumbi. (alama 4).
      4. Dhihirisha kwa kutoa mifano mitatu matumizi ya uhuru wa mshairi . (alama 3)
      5. Tambua (alama 2)
        1. Nafsi nenewa
        2. Toni
      6. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika shairi . (alama 2)
        1. Lebasi
        2. Punje ukiimezele

          AU

    2. SOMA SHAIRI LIFUATALO KISHA UJIBU MASWALI. (alama 20)

      1. Nikiwa na njaa na matambara mwilini
        Nimehudumika kama hayawani
        Kupigwa na kutukanwa
        Kimya kama kupita kwa shetani
        Nafasi ya kupumzika hakuna
        Ya kulala hakuna

      2. Ya kuwaza hakuna
        Basi kwani hili kufanyika
        Ni kosa gani lilotendeka
        Liloniletea adhabu hii isomalizika ?

      3. Ewe mwewe urukaye juu angani
        Wajua lilomo mwangu moyoni
        Niambie pale mipunga inapopepea
        Ikatema miale ya jua
        Mamangu bado angali amesimama akinisubiri?
        Je nadhari hujitokeza usoni
        Ikielekea huku kizuizini?
        Mpenzi mama , nitarudi nyumbani
        Nitarudi hata kama ni kifoni
        Hata kama maiti imekatikatika
        Vipande elfu , elfu kumi
        Nitarudi nyumbani

      4. Nikipenya kwenye ukuta huu
        Nikipitia mwingine kama shetani
        Nitarudi mpenzi mama
        Hata kama kifoni

        Maswali
        1. Taja mambo manne anayoyalalamikia mshairi. (alama 4)
        2. Fafanua dhamira ya shairi hili. (alama 2)
        3. Eleza mbinu nne za kimtindo. (alama 4)
        4.    
          1. Hili ni shairi la aina gani? (alama 1)
          2. Thibitisha jibu la i hapo juu. (alama 4)
        5. Tambua katika shairi ; (alama 3)
          1. Nafsineni
          2. Nafsi nenewa
          3. Toni
        6. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika shairi.(alama2)
          1. Hayawani
          2. Nadhari

  5. SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI (alama 20)

    1.         
      1. Fafanua sifa tano za hekaya. (Alama 5)
      2. Eleza maana ya; (alama 5)
        1. Vitanza ndimi.
        2. Tahalili
        3. Vivugo
        4. Matambiko
        5. Maapizo
      3. Jadili mifano mitano ya ngomezi za kisasa. (al 5)
      4. Eleza kwa hoja tano udhaifu wa hojaji kama njia ya kukusanya Fasihi Simulizi. (al 5)

MARKING SCHEME

  1. SEHEMU A: TAMTHILIA P. Kea: Kigogo
    Swali la lazima
      1. Mmesikia? Hamtatuletea wazimu wenu hapa! Nendeni kama mmekuja kutuhasimu.
        1. Eleza muktadha wa maneno. (alama 4)
          • Ni maneno ya Ngurumo (al 1)
          • Kwa Tunu (al 1)
          • Wakiwa Mangweni (al 1)
          • Asiya/ Mamapima alikuwa amekasirika baada ya mteja mmoja kuondoka na kuwafukuza akina Tunu kwa kuwapa dakika moja waondoke ndipo Ngurumo akauliza Tunu iwapo wamesikia kuwa waondoke wakiwa na Sudi. Tunu alikuwa amesema hapo mbeleni kuwa ni hatia kuuza pombe haramu na kuwa katiba imezifafanua sheria za uuzaji na unywaji pombe
        2. Jadili umuhimu wa msemaji kwa hoja nne. (alama 4)
          (Ngurumo)
          • Anaendeleza maudhui ya ulevi; kijana anayejulikana kwa uraibu wa vileo
          • Anaendeleza maudhui ya taasubi ya kiume; kusema kuwa afadhali apigie paka kura kuliko mwamamke.
          • Anaendeleza maudhui ya uzinizu; kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mamapima ilhali ana mume.
          • Kielelezo cha usaliti ; anasaliti Wanasagamoyo kwa kuunga mkono uongozi dhalimu.
          • Anaonyesha ukatili wa Majoka; anauawa na chatu (kundi la Majoka) licha ya kuunga mkono utawala wa Majoka.
          • Anaonyesha ujinga wa Boza; Boza hagundui kuwa Boza ana uhusiano wa kimapenzi na mkewe licha ya kuwa mlevi mwenzake.
          • Kielelezo cha vijana ambao hawachangii katika maendeleo; anatumia wakati mwingi huko mangweni na hana mwelekeo.
        3. Fafanua mbinu ya lugha iliyotumika. (alama 2)
          • Kinaya; akina Tunu hawakuwa hasimu bali walitaka tu kuita watu kwa mkutano wa kusukuma viongozi wafungue soko na kuonyesha uvunjaji wa sheria katika kuuza pombe haramu.
          • kejeli; hamtatuletea wazimu wenu hapa. (yoyote moja)
      2. Kenga alichangia pakubwa msiba wa Wanasagamoyo. Thibitisha kwa hoja zozote kumi. (Alama 10).
        • Kutoa ushauri mbaya kwa Majoka km kufunga soko na watu wengi walilitegemea.
        • Kuzorotesha usalama- alihutubia wahuni pale chini ya mbuyu na aliwatumia kuvuruga usalama. Alikuwa akipanga njama fulani.
        • Kupiganisha raia/ kufunga raia bure. Anamwambia Majoka aite Husda ofisini ili pakitokea vurugu kati ya Husda na Ashua, asingizie Ashua na kumtia ndani.
        • Kupendekeza wanaharakati wadhulumiwe- wanaharakati wawekewe vidhibiti mwendo na basi Majoka akawafukuza wafadhili na hivyo kulemaza upiganiaji haki.
        • Kupendekeza polisi watumie nguvu dhidi ya waandamanaji. Majoka basi akaamuru polisi watumie nguvu zaidi na kukatokea vifo.
        • Kupendekeza mauaji – ya wapinzani kama vile Jabali. Ya wanaharakati Tunu na Sudi kwa kupinga uongozi mbaya wa Majoka./ ya Chopi kwa sababu Majoka alisema Chopi anajua mengi kuliko inavyostahili.
        • Anaunga mkono udikteta- Majoka anapotaka kumrithisha Ngao Junior uongozi, Kenga anasema jambo hilo linafaa nah ii inanyima raia nafasi ya kuchaguana.
        • Kupendekeza runinga ifungwe na iadhibiwe kwa kupeperusha maandamano ya raia jambo amabalo lingeharibia sifa uongozi wa Majoka. Anasema Runinga ya Mzalendo ichukuliwe hatua lakini kituo cha Sauti ya Mashujaa kibakie.
        • Kutopinga miradi isiyo na faida na hata kuisimamia. Anafanikisha mradi wa kuchonga ambao unafilisi nchi na raia watalazimika kulipa deni kwa miaka mingi.
        • Kukubali kugawiwa ardhi ya umma. Majoka anamgawia kipande cha ardhi cha soko la Chapakazi alichonyakua.
        • Kufanikisha ubomoaji wa vibanda sokoni Chapakazi. Alisimamia ubomoaji bila kujali raia waliotegemea soko kwa mapato yao.
        • Kukubali ajira kwa njia ya mapendeleo- alikuwa binamuye Majoka na basi kuendeleza unasaba badala ya kupatia mtu ambaye angetoa ushauri mwafaka wa kuleta maendeleo.
        • Kuharamisha maandamano na basi kunyima raia haki ya kupigania haki yao ya kufunguliwa soko. Anamshauri Majoka kuyaharamisha.
          10x1 (kadiria hoja yoyote nyingine ambayo ni sahihi)

  2. SEHEMU B: RIWAYA Assumpta Matei: Chozi la Heri
    Jibu swali la II au III
    1. ‘…familia yake bado inamiliki mashamba ya michai na mibuni pamoja na mashirika mengi…’
      1. Weka dondoo hili katika muktadha wake. (alama 4)
        • Maneno ya Chandachema
        • Akiwaambia Umu, Zohali na Mwanaheri.
        • Wakiwa katika bweni la wasichana ya Shule ya Tangamano.
        • Alikuwa akiwaeleza usuli wa uwepo wake katika shule hiyo.
          1X4 = 4
      2. Kwa kurejelea mifano minane, eleza umuhimu wa msemaji katika kujenga riwaya hii. (alama 8)
        • Mmoja kati ya wasimulizi wa hadithi ya Chozi la heri ndiye anayesimulia kuhusu maisha ya wahusika kama vile Fumba na Tenge.
        • Kupitia kwake, mwandishi anasisitiza umuhimu wa familia katika malezi.
        • Baba anamtelekezea kwa nyanyake baada ya kifo cha nyanya, anaishi katika familia ya jirani yao Satua, na hatimaye kwa Tenge. Hawa wote wana mchango katika malezi yake.
        • Mwandishi amemtumia kukashifu ukiukaji wa haki za kibinadamu. Baba yake anamtunga mwanafunzi wake mimba na baadaye kumtelekeza mtoto -Chandachema.
        • Chandachema anaendeleza ajira ya watoto. Anafanya kazi katika shamba la chai kwa malipo kidogo.
        • Anachimuza umuhimu wa mashirika ya kidini katika kutetea haki za kibinadamu. Makao ya Jeshi la wajane Wakristo yanawahifadhi watoto waliotupwa na wazazi pamoja na wale wazazi wahitaji.
        • Ni kielekezo cha vijana wasiokata tamaa. Anawaambia akina Umu kuwa atajitahidi masomoni ili ahitimu kuwa mwanasheria au afisa wa maslahi ya kijamii na kuweza kutetea haki za kibinadamu.
        • Anaendeleza maudhui ya elimu na kuonyesha jinsi elimu inachangia kuleta mustakabali mwema wa msomi siku za usoni. Chandachema angependa kuwa Mwanasheria au Afisa wa maslahi ya Kijamii na kuweza kutetea haki za binadamu
        • Kupitia kwake, dhiki zinazowapata wafanyikazi wa kima cha chini zinaangaziwa.
        • Anafunza mbinu-ishi ya uvumilivu. Anavumilia maisha ya taabu baadaya kifo cha nyanyake hadi anapopata ufadhili na kujiunga na shule yaTangamano.
        • Anajenga tabia za wahusika. Kupitia kwake, tunaona utu wa Waridi anayemsomesha, ukatili na ukosefu wa uwajibikaji wa Fumba ambaye anamuacha Chandachema kulelewa na nyanya yake, Fumba mwenyewe akihamia ng’ambo na familia nyingine.
        • Uzinifu wa Bwana Tenge kunakusababisha dhiki ya kisaikolojia kwa wanawe na Chandachema
      3. Jadili kwa hoja nane suala la ukoloni mambo leo lilivyoshugulikiwa katika riwaya. (alama 8)
        • Watoto wa walowezi wa kikoloni kumiliki mashamba yaliyomilikiwa na familia zao-shamba la Tengenea,wazungu wanamiliki mashamba ya michai na mibuni pamoja na mashirika ya utengenezaji wa mazao ya mimea nchini.
        • Baadhi wa Wahafidhina wanamiliki mashamba huku Waafrika wengine wakiwa maskwota au wafanyikazi-Kangata anafanya kazi na kuishi katika shamba la Kiriri.Watoto wa Kangata hata wanajitambulisha kwa jina la Kangata.
        • Wahafidhina inaendeleza umilikinafsi wa ardhi ulioanzishwa na mzungu.
        • Wageni kuamua kitakachokuzwa Wahafidhina.
        • Unyonyaji-wenyeji kukuza zao na kuwapa wageni kuwasagia huku wakiwauzia kwa bei ghali.
        • Mifumo kandamizi ya utawala- uongozi unatuma vyombo vya dola kudhibiti upinzani
        • Utegemezi. Wanahafidhina wanawategemea washiria wa kimaendeleo wakati mikasa inapotokea. Kudhibitiwa na malengo ya kimataifa- Tila anamwambia Ridhaa kwamba wangependa kufikia Malengo ya Kimilenia. Haya ni matakwa ya kimataifa ambayo nchi hujifunga kutimiza.
        • Kampuni za kigeni kuchimbua madini katika sehemu za mashambani na fedha kuwaendea hao hao wageni. Raia wanaoajiriwa kuchimbua madini kulipwa mshahara duni.Tila analalamikia haya.
          (Hoja zozote 8)
          Au

    2. Tathmini umuhimu wa mbinu zifuatazo katika kuijenga riwaya ya Chozi la Heri
      1. Nyimbo (alama 10)
        • Wimbo wa Shamsi unaonyesha ukengeushi,
          1. licha ya elimu aliyo nayo, Shamsi ameshindwa kukabiliana na changamoto za maisha. Anaingilia matumizi mabaya ya pombe.
        • Unabainisha ukosefu wa uwajibikaji, badala ya kutafuta mbinu ya kukabiliana na hali duni ya maisha, analalamika kwamba wenye nguvu hawakumpa kazi walizoziahidi.
        • Unakashifu unyakuzi wa ardhi za wanyonge. Shamba la kina Shamsi linachukuliwa na Bwana Mabavu.
        • Unachimuza ufisadi – Bwana Mabavu anawaonyesha hati miliki bandia na kuwafukuza shambani mwao
        • Unaendeleza maudhui ya ukoloni mamboleo – Mabavu anamiliki shamba la Baba ya Shamsi na kuwageuza kuwa maskwota.
        • Unaangazia ukiukaji wa haki za binadamu – Shamsi na wenzake wanafutwa kazi kwa kuwazia kugoma.
        • Inaonyesha umaskini wa familia ya Shamsi – Babake Shamsi anakufa kwa kula mizizi mwitu wenye vijaasumu
        • Unakashifu unyonyaji wa wafanyikazi – Shamsi na wenzake wanalipwa mishahara duni.
        • Unasawiri tatizo la matumizi mabaya ya vileo- Shamsi anaingilia ulevi baada ya kufutwa.
        • Wimbo wa Shamsi unaoghaniwa na Ridhaa
        • Wimbo wa majigambo unaosawiri tabia ya Shamsi – anajivunia na kusema kuwa anaogopwa kwa kutoka katika jadi tukufu.
        • Unamfanyia tashtiti Shamsi kwa kujisifu kwa kuzua mikakati ya kukabiliana na hali ya uhitaji na hali mwenyewe ni mlevi.
        • Unaonyesha uovu wa jamii – wauza pombe wanatia vijaasumu ili iwe tayari haraka bila kuwazia madhara ya watumia wayo.
      2. Barua (alama 10)
        • Barua ya Lunga
          1. Barua ya kustaafishwa kwa Lunga inaonyesha dhuluma kwa wafanyikazi. Lunga anafutwa kwa kutetea wanyonge dhidi ya kuuziwa mahindi hatari kwa afya.
          2. Inaonyesha uadilifu wa Lunga anavyosema Afisa Mkuu Mtendaji
          3. Inakashifu ukatili wa waajiri – Lunga anafutwa bila hali yake kuwaziwa
          4. Inaonyesha mbinu-hasi za uongozi – Viongozi wanawaangamiza wanaowapinga njama zao za kiufisadi.
          5. Kuonyesha uongo/ unafiki wa waajiri- kusingizia kuwa shirika linapunguza wafanyikazi kutokana na changamoto za kifedha kutokana na gharama ya uzalishaji mali ilhali Lunga anafutwa kwa kukashifu kutaka kuuza mahindi yaliyoharibika. (hoja 5)
        • Barua ya Subira
          1. Inaonyesha ukosefu wa uwajibikaji wa Subira – anaondoka bila kuwazia hali ya baadaye ya watoto wake.
          2. Inadokeza maudhui ya malezi – Subira anamuusia Mwanaheri amtunze mnuna wake na pia wamtii baba yao.
          3. Inakashifu ubaguzi – Subira analalamikia kubaguliwa na mavyaa Inaonyesha uwajibikaji wa mzazi kwa watoto wake japo Subira anaondoka anawaachia wanawe ujumbe kwamba ameondoka na kuwashauri
          4. Anakashifu ukiukaji wa haki za kibinadamu – anasimangwa na kuitwa mwizi.
          5. Inajenga tabia ya wahusika – imesawiri udhaifu wa nia wa Kaizari. Hamtetei mkewe dhidi ya dhuluma ya mavyaa. Inakuza ukatili wa mavyaa kwa kumwita muuki na mwizi. (hoja 5)

  3. SEHEMU C: HADITHI FUPI; CHOKOCHO NA D. KAYANDA: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine
    Jibu swali la IV au V
    1. NDOTO YA MASHAKA
      "...dunia imenikunjulia mikono kunifariji baada ya kunicharaza fimbo yake aushi yangu yote."
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili (al.4)
        • Maneno ya Mashaka .
        • Katika ndoto .
        • Yumo chumbani mwake.
        • Anaota kuhusu kurudi kwa ua lake baada ya kupotea kwa karne moja.
      2. Tambua na ueleze mbinu ya lugha iliyotumiwa katika dondoo.(al.2)
        • Tashihisi -  dunia kunikunjulia mikono kunifariji baada ya kunicharaza
      3. Eleza jinsi dunia ilimcharaza fimbo msemaji kwa kutolea hoja kumi na nne. (al.14)
        • Mamake Mashaka kufariki punde tu baada ya kumkopoa.
        • Babake pia anafariki punde tu baada ya mamake.
        • Kuambulia mama mlezi maskini.
        • Kuanza kufanya kazi za kijungu jiko kujikimu yeye na mama mlezi.
        • Licha ya bidii yao mara kwa mara walikosa ikamlazimu Kidebe kutumia akiba yake.
        • Kufiwa na mama mlezi.
        • Kufungishwa ndoa ya mkeka na Mzee Rubeya.
        • Kudharauliwa na wazazi wa Waridi kwa sababu ya umasikini wake.
        • Kuishi katika mtaa duni.
        • Chumba chake ni duni - kinavuja paa inyeshapo.
        • Alikosa samani chumbani – hana meza,viti,kitanda wala godoro.
        • Kazi ya usiku.
        • Mshahara duni .
        • Kukopoa pacha mara tatu.
        • Kulazimika kuomba nafasi ya malazi ya wana kwa jirani.
        • Mazingira yenye harufu mbaya ya chooni.
        • Mke na wana kumkimbia. Zozote 14
          AU

    2. Kwa kurejelea hadithi ya Mapenzi ya Kifaurongo, Mame Bakari, Nizikeni Papa Hapa , Mtihani wa Maisha na Mkubwa, eleza changamoto zinazowakumba vijana. (al.20)
      1. Mapenzi ya Kifaurongo.
        • Ukosefu wa karo -wazazi wa Dennis kufanya kazi kwa majirani kudunduiza karo yake.
        • Ukosefu wa hela za matunzo – Dennis hana cha kupika ila uji mweupe bila sukari.
        • Mapenzi shuleni – wanafunzi wa Chuo kikuu cha Kivukoni wanahusiana kimapenzi.
        • Masomo magumu – wanafunzi hawaelewi anayofunza Dkt. Mabonga.
      2. Mame Bakari
        • Ubakaji – Sara anabakwa na jana dume.
        • Kuavya mimba – Sara anatupilia mbali wazo la kuavya.
        • Kujitia kitanzi – Sara alilikataza wazo la hili likome hata kumpitikia.
        • Kutengwa –Alijiona akitengwa na jamii kwa jumla.
      3. Nizikeni Papa Hapa
        • Mapenzi ya kiholela - Otii kuhusiana na Rehema bila kujali ushauri wa mwendani wake.
        • Ukimwi – Otii anaugua gonjwa lenye dalili zote za UKIMWI.
        • Kuumia kazini – Otii anaumia mguu akiichezea timu yake ya Bandari.
        • Kutelekezwa na waajiri wao – anapoumia timu yake haikumjali wala kumfidia.
      4. Mtihani wa Maisha
        • Kutembea kwenda shule – Samueli anatembea kilomita sita kila siku kwenda shuleni.
        • Ukosefu wa karo – babake Samueli analazimika kuuza ng`ombe ili kulipa karo.
        • Mapenzi shuleni – Samueli anahusiana na Nina.
        • Kufeli mtihani wa kitaifa – Samueli anafeli mtihani wake.
      5. Mkubwa
        • Umaskini- Mwavuli wa Mubwa umetoka mistari mitatu.
        • Matumizi ya dawa za kulevya – vijana wengi vichochoroni anakopitia Mkubwa wanatumia dawa hizi.
        • Ufisadi – wanafunzi wa profesa wanahongwa kumpigia Mkubwa kura.
        • Kufungwa – vijana wanaotumiwa kulangua dawa na wanaozitumia wanapokamatwa hutiwa kizuizini.

  4. SEHEMU D: USHAIRI
    Jibu swali la VI au VII
    1. SOMA SHAIRI LIFUATALO KISHA UJIBU MASWALI. (alama 20)

      Pana haja ya kupima, neno tuzowele –angu
      Tusizowee kusema , hili ni teuo langu
      Huenda huji mapema , -angu huja kuwa tungu
      Ikaja kukusakama, na kukuposha kwa Mungu
      Pana haja ya kupima.

      Neno huwa ni la kwako, likiwa ndani moyoni
      Lakini katu si lako, likishavuka menoni
      Kwa hivyo likutokako, liweke kwenye mizani
      Linaweza kuwa cheko, ama tusi kwa wendani
      Pana haja ya kupima.

      Vivyo hivyo kwa lebasi , huwa yako kisutuni
      Hivyo nina wasiwasi, wambe yako sebuleni
      Itavutiya matusi, ya wenzio insane
      Wakakuchoma nafusi, kwa mishale ya lisani
      Pana haja ya kupima.

      Mwana ujuwe ni wako, punje ukiimezele
      Lakini katu si wako, nde ukimuletele
      Akiwa yu ndani yako, ni wa duniya vivile
      Ukishishilia ni wako, muavye takakuole
      Pana haja ya kupima.

      Maisha nayo si wako, utabaradi milele
      Ungayaishi ja yako, ni tunu ya maumbile
      Mgawa si kufu yako, mshindane hili lile
      Akupapo akupoko, utaishi palepale
      Pana haja ya kupima.

      Ni chetu chako si chako, ulimwengu huwa vile
      Juhudi zingawa zako, wa kufaidi ni wale
      Ikifika siku yako, nyono zikukae mbele
      Ulichosema ni chako , huwabakiya wawale
      Pana haja ya kupima.

      Kaseme na moyo wako , Ubaini haya yale
      Ukiambacho ni chako , kisikupe mageule
      Kitu utajacho chako , huenda kiwe cha wale
      Na usemacho si chako, kiwe chako ndicho kile
      Pana haja ya kupima.

      MASWALI

      1. Eleza dhamira ya shairi hili. (alama 2)
        • Umuhimu wa kuchuja mambo kabla ya kuyatekeleza
      2. Eleza bahari zozote tatu za shairi hili. (alama 6)
        • Msuko - kibwagizo kina mizani michache / kimefupishwa
        • Mathnawi - kila mshororo una vipande viwili
        • Ukaraguni - Kila ubeti una mpangilio wake wa vina
      3. Andika ubeti wa nne kwa lugha tutumbi. (alama 4).
        • Mshairi anasema kuwa mwana ni wako wakati wa kupata himila.Anasisitiza kuwa mwana si wako akisha kuzaliwa.Hata akiwa tumboni mwako ni wa jamii /dunia.Anaongeza kusema kwamba ukishikilia kuwa mwana ni wako ujuaribu kuavya mimba uonekane.Mshairi anamaliza kwa kusema kuwa ni vyema kuchunguza tunayoyafanya.
      4. Dhihirisha kwa kutoa mifano mitatu matumizi ya uhuru wa mshairi . (alama 3)
        • Lahaja
          1. tungu - chungu
          2. nde - nje
        • Mazida
          1. ukiimezele - ukiimeza
          2. ukimletele ukimleta
        • Inkisari
          1. Vivile – vilevile
        • Tabdila
          1. tusizowee – tusizoee
          2. ujuwe - ujue
          3. duniya -dunia
        • kufinyanga sarufi
          1. wambe yako sebuleni – wambe sebuleni yako
      5. Tambua (alama 2)
        1. Nafsi nenewa - binadamu/asiyepima asemacho au afanyacho
        2. Toni - Kutahadharisha
      6. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika shairi . (alama 2)
        1. Lebasi - mavazi/ nguo
        2. Punje ukiimezele - unapopata ujauzito / himila
          AU

    2. SOMA SHAIRI LIFUATALO KISHA UJIBU MASWALI. (alama 20)
      1. Nikiwa na njaa na matambara mwilini
        Nimehudumika kama hayawani
        Kupigwa na kutukanwa
        Kimya kama kupita kwa shetani
        Nafasi ya kupumzika hakuna
        Ya kulala hakuna
      2. Ya kuwaza hakuna
        Basi kwani hili kufanyika
        Ni kosa gani lilotendeka
        Liloniletea adhabu hii isomalizika ?
      3. Ewe mwewe urukaye juu angani
        Wajua lilomo mwangu moyoni
        Niambie pale mipunga inapopepea
        Ikatema miale ya jua
        Mamangu bado angali amesimama akinisubiri?
        Je nadhari hujitokeza usoni
        Ikielekea huku kizuizini?
        Mpenzi mama , nitarudi nyumbani
        Nitarudi hata kama ni kifoni
        Hata kama maiti imekatikatika
        Vipande elfu , elfu kumi
        Nitarudi nyumbani
      4. Nikipenya kwenye ukuta huu
        Nikipitia mwingine kama shetani
        Nitarudi mpenzi mama
        Hata kama kifoni

        Maswali

        1. Taja mambo manne anayoyalalamikia mshairi. (alama 4)
          • kufungwa
          • Njaa
          • Kufukuzwa
          • Kutopewa nafasi ya kupumzika
          • Kuvaa matambara
          • Kufanyizwa kazi kama mnyama
        2. Fafanua dhamira ya shairi hili. (alama 2)
          • Mshairi anakashifu mateso watendewayo wafungwa na kumpa mamake matumaini kuwa siku moja atatoka kizuizini
        3. Eleza mbinu nne za kimtindo. (alama 4)
          • Takriri -neno “ nitarudi” limerudiwarudiwa
          • Tashbihi – Kupitia mwingine kama ibilisi/ kama hayawani
          • Swali balagha - Ni kosa gani lilotendeka liloniletea adhabu hii isomalizika?
          • Kejeli
          • Taswira- nikipenya kwenye ukuta/ nikiwa na njaa na matambara mwilini
        4.    
          1. Hili ni shairi la aina gani? (alama 1)
            • Huru
          2. Thibitisha jibu la i hapo juu. (alama 4)
            • Lina mishororo mishata - kupigwa na kutukanwa
            • Idadi ya mishororo katika kila ubeti inabadilikabadilika
              k.m ubeti wa1 ni sita na wa 2 ni minne .
            • Mishororo imejisimamia kivina.
            • Idadi ya vipande ni tofauti katika beti km beti 3 mshororo wa 8 una vipande viwili na mshororo wa kwanza ubeti huo una kimoja.
            • Idadi ya mizani ni tofauti katika mishororo. Km ubeti 1 mshororo 1 una 14 na wa pili una 12.
        5. Tambua katika shairi ; (alama 3)
          1. Nafsineni - mfungwa aliye kizuizini
          2. Nafsi nenewa - mamake mfungwa
          3. Toni - matumaini

        6. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika shairi.(alama2)
          1. Hayawani - mnyama
          2. Nadhari - fikira

  5. SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI (alama 20)
    1.         
      1. Fafanua sifa tano za hekaya. (Alama 5)
        • Huhusu mhusika mmoja anayetumia ujanja kujinufaisha.
        • Wahusika ni wanyama na/au binadamu
        • Kwa kawaida mhusika mkuu huwa mdanganyifu
        • Huwa fupi
        • Hazihusiani na tukio lolote la kihistoria na wala wahusika wake si watu walioishi
        • Visa vingi tofauti humhusu mhusika mkuu
        • Sana sana mhusika huyo huwa ni sungura
        • Mnyama huyo huepuka kiujanja hali fulani ambayo inamshinda labda kwa kuwa inahitaji nguvu
        • Ujanja huo huficha ujinga wa wanyama wengine wakubwa
        • Huonyesha nguvu si hoja bora akili
        • Wahusika wakuu wajanja huibuka washindi
      2. Eleza maana ya; (alama 5)
        1. Vitanza ndimi. - Maneno ambayo hutatanisha wakati wa kutamka kwa sababu ya kuwepo kwa sauti zinazofanana/Ni mchezo wa maneno ambapo kuna maana fiche katika huo mchezo. Ni vifungu vya maneno ambavyo humtatiza msemaji kuvitamka kutokana na maneno yanayokaribiana kimaana na kimatamshi.
        2. Tahalili - Ni nyimbo za maafa / matanga. Huimbwa wakati wa matanga /kilio ili kuomboleza
        3. Vivugo - Ni maonyesho ya kujisifu, kujitapa na maringo kutokana na ufanisi wa kutenda jambo lisilo la kawaida. Huonyesha kuwa yeye ni bora kuliko wengine
        4. Matambiko -  Sadaka au ada inayotolewa kwa Mungu, mizimu, pepo au miungu ili wasaidie binadamu kutatua mambo magumu, kuomba radhi au kutoa shukrani. Matatizo ni kama vile ukame, magonjwa, kukosa watoto, mafuriko au janga lolote lililomshinda binadamu nguvu na uwezo.
        5. Maapizo - Ni maombi maalum ya kumtaka Mungu kumwadhibu mhusika hasidi au mwovu au msaliti.
      3. Jadili mifano mitano ya ngomezi za kisasa. (al 5)
        • Kengele katika lango/ mlango kuashiria kuna mtu anataka kufunguliwa.
        • Mlio wa saa; kuamsha mtu au kukumbusha jambo
        • Mlio wa simu; simu inapigwa, ujumbe mfupi au kumbusho la shughuli fulani.
        • Mlio wa ambulensi; kutaka kupishwa kwa sababu kuna mgonjwa ndani au mgonjwa anaendewa mahali.
        • Kengele; km shuleni; kuashiria mwisho au mwanzo wa kipindi a shughuli fulani.
          Zozote 5x1
      4. Eleza kwa hoja tano udhaifu wa hojaji kama njia ya kukusanya Fasihi Simulizi. (al 5)
        • Huenda watu wakakosa kujaza hojaji kwa kikamilifu kutokana na hofu ya kulaumiwa au kukataa tu.
        • Maswali yenye utata husababisha fasiri mbalimbali ambazo hufanya matokeo yasitegemeke.
        • Sifa za uwasilishaji kama vile toni havipatikani kwani mtafiti hapatani ana kwa ana na mhojiwa.
        • Huenda walio na habri muhimu hawajui kusoma na kuandika. Husaidiwa na huenda wasaidizi wasiandike kila kitu.
        • Hojaji zinaweza kuchelewa kufikia wahojiwa na basi ujumbe usiopatikane kwa wakati ufaao.
        • Huenda wahojiwa wasiandike ukweli na mtafiti hawezi kuthibitisha kwa urahisi iwapo habari ni za ukweli.
        • Huenda wahojiwa wakakataa kujaza hojaji ikiwa ndefu.
        • Uchanganuzi huchukua muda mrefu hasa hojaji wazi.
          Zozote 5x1
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Sukellemo Joint Mock 2020/2021.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest