Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Form 3 End Term 2 Exams 2022

Share via Whatsapp

MASWALI

  1. UFAHAMU: (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yanayofuatia
    Mateso ya wanawakiwa ni suala la kijamii linalofaa kutazamwa kwa darubini kali. Hata hivyo wanaoathirika zaidi ni watoto ambao bado wako katika umri unaohitaji kulelewa na kupewa mahitaji ya msingi kama mavazi, malazi, elimu na mengine anuwai. Hali ya kuachwa na wazazi imekuwa ikizikumba jamii tangu enzi za mababu na kila itokeapo, wanajamii huipokea kwa mitazamo tofautitofauti, hivyo kuwafanya wanawakiwa kuathirika sana.
    Baadhi ya jamii zina imani za kijadi pamwe na mila zilizochakaa zinazozifanya kuamini kuwa baadhi ya vifo hutokana na laana. Wengine huchukulia kuwa mwendazake ameondolewa na ulozi. Imani kama hizi huifanya jamii kuwatia watoto walioachwa katika mkumbo ule ule, hivyo kuwaangalia kwa macho yasiyo ya kawaida. Hili husababisha dhana gande. Hali hii husababisha kuwachukulia watoto kama wanaotoka katika kizazi kilicholaaniwa. Jamii basi hukosa kuwapa watoto hawa stahiki yao. Hata wanapojitahidi kuiwania nafasi yao, waliowazunguka huwavunja mioyo. Jitihada zao huishia kuwa si chochote kwa kuwa jamii inawatazama kama waliolaaniwa.
    Punde baada ya mzazi mmoja au wote wawili waendapo wasikorudi, inatarajiwa kwamba aliyeachiwa mtoto, awe mzazi wake, mwanafamilia au jirani awajibike na kumtunza mwanamkiwa. Kunao kadha wa kadha wanaowajibika – ninawavulia kofia. Hata hivyo wengi hutelekeza jukumu hili walilopewa na Muumba. Si ajabu basi kuona kuwa idadi ya watoto wanaozurura mitaani inazidi kuongezeka kila uchao. Ukichunguza utakuta kuwa wengi wa watoto hawa ni waliopotelewa na wazazi wao. Inakera zaidi kugundua kuwa baadhi ya watoto hawa wana mzazi mmoja. Kwamba mke au mume wa mtu ameaga, au iwe kwamba mzazi mmoja alimzaa mtoto na kumwachia mwenzake mzigo wa ulezi, aliyeachiwa ana jukumu la kumpa mwanawe mahitaji ya msingi. Machoni pa Jalali, kila anayeupuuza wajibu huu ana hukumu yake siku ya kiama!
    Ni haki ya kila mtoto kupata elimu. Katika katiba ya Kenya mathalan, elimu ya msingi, yaani kuanzia shule ya chekechea had kidato cha nne ni ya lazima. Tangu hapo hata hivyo, jamii zimekuwa zikiwanyima wanawakiwa wengi elimu. Kwamba kunao wachache wanaowaelimisha baadhi ya wanawakiwa, ni kweli. Hata hivyo, wengi hukosa hata wa kuwapeleka katika shule ya chekechea, hivyo kuishia kutojua hata kuandika majina yao. Mfikirie mtu katika karne ya 21, asiyejua kusoma wala kuandika! Nani ajuaye, huenda huyo mwanamkiwa asiyepelekwa shuleni ndiye angalikuwa profesa, daktari, mwalimu, rubani au msomi mtajika na mtaalamu wa uwanja muhimu katika jamii!
    Kila mtoto ana haki ya kulelewa hadi kufikia utu uzima kabla ya kupewa majukumu mazito. Katika katiba ya Kenya, utu uzima, ulio umri wa kuanza kufanya kazi huanzia miaka 18. Wanaohakikisha watoto hawa wametimiza utu uzima kabla ya kufanyishwa gange ngumu wanafaa pongezi. Hata hivyo wanawakiwa wamekuwa wakitumiwa na wengi kama punda wa huduma. Wanaaila wengine huwachukua wanawakiwa kwa machozi mengi wazazi wao waagapo nakuapa kuwahifadhi na kuwatunza wana wale wa ndugu zao, kumbe ni machozi ya simba kumlilia swara! Hata kabla ya mwili wa mzazi mhusika kuliwa na viwavi, mateso kwa mtoto yule huanza, akawa ndiye afanyaye kazi zote ngumu. Utakuta watoto wao wamekaa kama sultan bin jerehe huku mwanamkiwa yule akiwapikia, kuwafulia nguo, kudeki, karibu hata awaoshe miili! Kazi kama zile za shokoa huwa za sulubu na aghalabu husindikizwa kwa matusi yasiyoandikika.
    Baadhi ya waja walionyimwa huruma huwahadaa wanawakiwa na kuwapeleka ng’ambo wakitumia vyambo, kuwa wakifika kule watapata kazi za kifahari. Maskini wale hushia kushikwa shokoa, wakawa watumwa katika nyumba za waajiri wao, bila namna ya kujinasua. Wengine hushia kutumiwa kama watumwa wa ‘kimapenzi’ katika madanguro, miili yao ikawa ya kuuziwa makahaba waroho wasiojali utu. Kujinasua kule huwa sawa na kujitahidi kuokoa ukuni uliokwishageuka jivu, maadamu wanawakiwa aghalabu hukosa watu wenye mioyo ya huruma ya kuwashughulikia. Wengi huitumia methali ‘mwana wa ndugu kirugu mjukuu mwanangwa’ kuwapuuzilia mbali wanawakiwa ambao hukimbiliwa tu wabinafsi hawa wanapofaidika wenyewe.
    1. Ipe taarifa hii anwani mwafaka. (alama 1)
    2. Eleza dhana ya mwanamkiwa kwa mujibu wa kifungu. (alama 2)
    3. Eleza imani za kijadi kuhusiana na wanawakiwa. (alama 2)
    4. Jadili masaibu yanayowakumba wanawakiwa. (alama 4)
    5. Eleza haki mbili za kikatiba zilizokiukwa kuhusiana na wanawakiwa. (alama 4)
    6. Eleza maana ya msamiati ufuatao kulingana na kifungu. (alama 2)
      1. Inakera
      2. Majukumu
  2. UFUPISHO (Alama 15)
    Tunapinga na kulaani vikali visa vya ugaidi vinavyoendelea kutetemesha usalama wa wananchi. Hivi ni vitendo vya kinyama vinavovyotekelezwa na watu waliokosa ubinadamu na utu kabisa. Inaghadhabisha kuona Wakenya wasio na makosa wakiteswa na kuuawa kinyama bila huruma na watu wasio na utu. Hatuogopi wala hatuna fedheha kuamba kuwa magaidi hawa wamelaaniwa na siku zao zimehesabiwa hapa duniani. Damu ya mwananchi asiye na makosa katu watailipia. Napinga vikali pale magaidi hawa wanapohusisha vitendo hivi kuwa vita vya kidini; vita hivi si vya kidini kwani hakuna dini yoyote iliyo na imani ya kumuua kinyama binadamu asiye na makosa.
    Kando na tishio la ugaidi, Wakenya pia wanakabiliwa na hatari za ujambazi, mauaji, unajisi, ubakaji na maovu mengine. Katika juhudi za kudumisha usalama, polisi wana jukumu la kutumia kila mbinu kuhakikisha kuwa haki za kikatiba za Wakenya kuhusu kulindwa kwa maisha na mali yao zimedumishwa. Lakini cha kusikitisha ni kuwa, mbinu ambazo polisi wamekuwa wakitumia hasa ile ya kufanya misako inayoishia kuwanasa mamia ya raia wasio na habari kuhusu kinachoendelea, inawaongezea Wakenya mateso. Hali hii inawaacha kwenye hatari ya kunaswa na majambazi ama polisi.
    Matumizi ya mbinu hii ya misako yameishia kunasa raia wengi wasio na makosa.Wanaponaswa, hurundikwa kwenye seli usiku mzima ama siku kadha na hata kama wanaaachiliwa huwa tayari wameteseka. Huu ni ukiukaji wa haki za raia. Kadhalika, mbinu hii inaonekana kama hila ya polisi kutaka kuonyesha wanafanya kazi lakini sio mwafaka kwani wanapokuwa wakiwanasa raia mijini na mitaani, magaidi na majambazi wanaendelea na shughuli zao.
    Badala ya kusaka wakora kwa kubahatisha kwenye umati, polisi wanapaswa kubuni njia ambazo zitawapa mwelekeo mwafaka zaidi kuhusu wahalifu ili waweze kuwafuatilia. Ushirikiano baina yao na majasusi uwepo. Hii itawezesha polisi kupata habari muhimu kuhusu vitisho vya uhalifu. Maafisa wa usalama pia wanaweza kupata habari muhimu kutoka kwa raia.
    1. Ni nini maoni ya mwandishi kuhusu suala la ugaidi (alama 7,1 utiririko) (maneno 60-70)
      Matayarisho:
      Nakala safi
    2. Kwa kutumia maneno yasiyozidi 50 fupisha aya mbili za mwisho. (alama 6, 1 utiririko)
      Matayarisho:
      Nakala safi
  3. SARUFI NA MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
    1. Tofautisha kati ya sauti /m/ na sauti /b/ . ( alama 1)
    2. Unda neno lenye muundo huu: Irabu+ Irabu+ Irabu ( alama 1)
    3. Weka kiimbo kwenye sentensi hii ili kuibua maana tatu. Musa amefariki ( alama 3)
    4. Weka maneno haya kwenye ngeli mwafaka. ( alama 2)
      1. Maiti __________________________________________
      2. Kipofu _________________________________________
    5. Eleza maana ya neno mofimu. ( alama 1)
    6. Tunga neno lenye viambishi vifuatavyo: ( alama 2)
      1. Kiima nafsi ya pili umoja
      2. Hali timilifu
      3. Mtendwa
      4. Mzizi
      5. Kauli ya kutendea
      6. Kiishio
    7. Tambua aina za maneno kwenye sentensi hii. ( alama 2)
      Baba yangu alienda kanisani.
    8. Changanua sentensi hii kwa matawi. Mtoto mdogo analia sana. (alama 3)
      1
    9. Tambua aina za vishazi kwenye sentensi hii. Utapita mtihani ukisoma kwa bidii. ( alama 2)
    10. Andika katika hali ya udogo wingi. Kiti cha mvulana huyu kimepotea. ( alama 2)
    11. Kwa kutolea mifano, onyesha matumizi mawili ya ritifaa. ( alama2)
    12. Tambua Kipozi, kitondo na ala katika sentensi. Okwero alimpikia Gitau chakula kwa sufuria. ( alama 3)
    13. Tambua aina mbili za virai kwenye sentensi hii. Kiatu change kiliraruka baada ya kushonwa. ( alama 2)
    14. Nyambua vitenzi hivi kwenye kauli zilizowekwa mabanoni. ( alama 3)
      1. Kimbia ( tendesha) ________________________________________________
      2. Choma ( tendua) _________________________________________________
      3. Ficha ( tendama) _________________________________________________
    15. Unda nomino kutokana na kitenzi Pika . ( alama 1) ___________________________________________
    16. Andika kinyume cha sentensi hii. Tajiri aliyebarikiwa ni huyu. ( alama 1)
    17. Tolea maana za misemo hii. ( alama 2)
      1. Vaa miwani _______________________________________________________________________
      2. Enda mbweu ______________________________________________________________________
    18. Tunga sentensi zenye vivumishi vinavyoleta dhana hizi: ( alama 3)
      1. Kumiliki
      2. Bila kuchagua
      3. Kuonyesha mbali sana
    19. Andika kwenye usemi wa taarifa. ( alama 3)
      “ Unaitwa nani?” Mwalimu alimuuliza. “ Naitwa Mahat. “ Akajibu.
    20. Tunga sentensi moja kuonyesha Kitenzi kishirikishi kipungufu. ( alama 1)
  4. ISIMU JAMII ( ALAMA 10)
    Jadili changamoto zozote tano zinazoikumba lugha ya Kiswahili. ( alama10)


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

  1.       
    1. Wanawakiwa/mateso ya wanawakiwa. (alama 1)
    2. Ni mtoto aliyefiwa na mzazi mmoja au wote. (alama 1)
    3.    
      1. Baadhi ya vifo hutokana na laana.
      2. Mwendazake ameondolewa na ulozi. 2x1=2
    4.      
      1. Wanatelekezwa na walioachiwa jukumu la kuwatunza hivyo kuishia kuwa watoto wanaozurura mitaani.
      2. Hawapelekwi shuleni
      3. Fanyishwa kazi ngumu
      4. Wanadaiwa na kupelekwa ng’ambo kuwa watapata kazi za kifahari lakini wanaishia kuwa watumwa wa kimapenzi
        4x1=4
    5.       
      1. Haki ya elimu ya msingi
      2. Kulelewa hadi kufikia utu uzima kabla ya kupewa majukumu mazito za kwanza 2x2=4 f)
    6.       
      1. Inaudhi/inakasirisha
      2. Kazi/wadhifa 2x1=2
        Adhabu
        Sarufi - ½ x 6 s=3
        Hijai - ½ x 6 h=3
  2. UFUPISHO (Alama 15)
    1. Ni nini maoni ya mwandishi kuhusu suala la ugaidi? (alama 7, 1 utiririko)
      1. Tunapinga na kulaani visa vya ugaidi
      2. Ugaidi ni kitendo cha kinyama kinachotekelezwa na watu waliokosa ubinadamu.
      3. Ugaidi hauna uhusiano na dini yoyote.
      4. Polisi wanazembea katika kuzuia matendo ya kigaidi.
      5. Polisi wabuni njia mbadala ya kukabiliana na ugaidi badala ya kunasa raia waio na hatia.
      6. Wakenya wasio na makosa huteswa na kuuawa kinyama.
      7. Magaidi watalipia matendo yao.
      8. Wakenya wana haki ya kulindwa.
        (Hoja zozote 7×1=7, alama 1 ya utiririko)
    2. Kwa kutumia maneno yasiyozidi 50, fupisha aya mbili za mwisho. (alama 6,1 ya utiririko)
      1. Raia wasio na hatia hunaswa.
      2. Hurundikwa kwenye seli na kuachiliwa huru kama wameteseka.
      3. Huu ni ukiukaji wa haki za binadamu.
      4. Hii ni hila ya polisi kujionyesha kuwa wanafanya kazi.
      5. Magaidi huendeleza shughuli zao.
      6. Polisi wanapaswa kubuni njia zitakazowapa mwelekeo mwafaka kuhusu wahalifu.
      7. Ushirikiano baina yao na majasusi uwepo.
      8. Maafisa wa usalama kupata habari muhimu kutoka kwa raia.
        (Hoja zozote 6×1=6, alama 1 ya utiririko)
        1. Ondoa ½ alama kwa kila kosa la sarufi hadi makosa sita kila litokeapo kwa mara ya kwanza.
        2. Ondoa ½ alama kwa kila kosa la hijai hadi makosa sita kila litokeapo kwa mara ya kwanza.
  3. SARUFI NA MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
    1. Tofautisha kati ya sauti /m/ na sauti /b/ . ( alama 1)
      /m/ ni king’ong’o ilhali /b/ ni kipasuo.
    2. Unda neno lenye muundo huu: Irabu+ Irabu+ Irabu ( alama 1)
      aua
      aoa
    3. Weka kiimbo kwenye sentensi hii ili kuibua maana tatu. Musa amefariki ( alama 3)
      Musa amefariki? SWALI
      Musa amefariki. TAARIFA
      Musa amefariki! HISIA
    4. Weka maneno haya kwenye ngeli mwafaka. ( alama 2)
      1. Maiti A-WA au I-ZI
      2. Kipofu A-WA
    5. Eleza maana ya neno mofimu. ( alama 1)
      Sehemu ndogo ya neno yenye maana na haiwezi gawika Zaidi.
    6. Tunga neno lenye viambishi vifuatavyo: ( alama 2)
      1. Kiima nafsi ya pili umoja
      2. Hali timilifu
      3. Mtendwa
      4. Mzizi
      5. Kauli ya kutendea
      6. Kiishio
        Umempikia
        ( Mwalimu akadirie jawabu la mtahiniwa)
    7. Tambua aina za maneno kwenye sentensi hii. ( alama 2)
      Baba yangu alienda kanisani.
      Baba- Nomino
      Yangu- kivumishi
      Alienda- kitenzi
      Kanisani- kielezi
    8. Changanua sentensi hii kwa matawi. Mtoto mdogo analia sana. (alama 3)
    9. Tambua aina za vishazi kwenye sentensi hii. Utapita mtihani ukisoma kwa bidii. ( alama 2)
      Utapita mtihani- kishazi huru
      Ukisoma kwa bidi- kishazi tegemezi
    10. Andika katika hali ya udogo wingi. Kiti cha mvulana huyu kimepotea. ( alama 2) vijiti vya vivulana hivi vimepotea.
    11. Kwa kutolea mifano, onyesha matumizi mawili ya ritifaa. ( alama2)
      Kwenye ving’ong’o m.f ng’ombe
      Kufupisha miaka 1999- ‘99
    12. Tambua Kipozi, kitondo na ala katika sentensi. Okwero alimpikia Gitau chakula kwa sufuria. ( alama 3)
      Chakula- kipozi
      Gitau- kitondo
      Sufuria - ala
    13. Tambua aina mbili za virai kwenye sentensi hii. Kiatu chake kiliraruka baada ya kushonwa. ( alama 2)
      Kiatu chake – RN
      Raruka – RT
      Baaya ya kushonwa – RH
      Chake - RV
    14. Nyambua vitenzi hivi kwenye kauli zilizowekwa mabanoni. ( alama 3)
      1. Kimbia ( tendesha) kimbiza
      2. Choma ( tendua) chomoa
      3. Ficha ( tendama) fichama
    15. Unda nomino kutokana na kitenzi Pika . ( alama 1)
      mpishi
      Kupika
      Mapishi
    16. Andika kinyume cha sentensi hii. Tajiri aliyebarikiwa ni huyu. ( alama 1)
      Tajiri aliyelaaniwa ni huyu .
    17. Tolea maana za misemo hii. ( alama 2)
      1. Vaa miwani - lewa chakari
      2. Enda mbweu – toa harufu mbaya kutoka kinywani
    18. Tunga sentensi zenye vivumishi vinavyoleta dhana hizi: ( alama 3)
      1. Kumiliki - Mtoto mwenye kikaragosi amefika. ( enye)
      2. Bila kuchagua mwanafunzi yeyote aje. ( o-ote)
      3. Kuonyesha mbali sana kiatu kile kimeanguka. ( -le)
    19. Andika kwenye usemi wa taarifa. ( alama 3)
      “ Unaitwa nani?” Mwalimu alimuuliza. “ Naitwa Mahat. “ Akajibu.
      Mwalimu alimuuliza aliitwa nani naye akajibu kuwa aliitwa Mahat.
    20. Tunga sentensi moja kuonyesha Kitenzi kishirikishi kipungufu. ( alama 1)
      Tunda li mtini.
      Kiatu ki sokoni.
      Wewe ni mwanafunzi.
      Mimi si mwizi. (Mwalimu akadirie jawabu la mtahiniwa)
  4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
    Jadili changamoto zozote tano zinazoikumba lugha ya Kiswahili. (alama10)
    1. Uhaba mkubwa wa wataalamu wa Kiswahili
    2. Athari kutoka kwa lugha ya kwanza.
    3. Watu kupenda lugha nyinginezo kama vile kiingereza, kijerumani.
    4. Imani potovu – lugha ya Kiswahili ni duni
    5. Uhaba wa walimu wa Kiswahili.
    6. Uhaba wa vitabu vya Kiswahili.
    7. Kutokuwepo kwa sera ya lugha kutoka kwa baadhi ya serikali za mataifa ya Afrika mashariki.
    8. Uhaba wa pesa za kutafiti.
    9. Nchi za Afrika za kutokuza wala kuendeleza Kiswahili.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Form 3 End Term 2 Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest