Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Form 3 End Term 2 Exams 2023

Share via Whatsapp

MAAGIZO KWA MTAHINIWA

  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote yaandikwe katika nafasi zilizoachwa katika kijitabu hiki cha maswali.
  • Tumia hati safi.

KWA MATUMIZI YA MTAHINI PEKEE

Swali

Jumla

Tuzo

1

15

 

2

15

 

3

40

 

4

10

 

JUMLA

80

 


MASWALI

  1. UFAHAMU (Alama 15)
    Soma makala yafuatayo kasha ujibu maswali

    Huku ulimwengu unapoingia katika teknologia ya tarakilishi na sera ya utandaridhi, ukweli wa mambo ni kuwa akina mama wamezinduka. Suala la usawa wa kijinsia limeanza kushamiri kote duniani na ole wake mwanamume yeyote ambaye hajawa tayari kutembea na majira. Lakini hebu tuchunguze jambo hili kwa makini zaidi.

    Usawa wa jinsia ni nini? Usawa wa kijinsia ni usawa wa binadamu wote; wawe wake au waume. Usawa huu unapaswa kudhihirika katika kugawa nafasi za kazi, utoaji wa elimu, nafasi za uongozi na nyanja nyinginezo zozote za maisha.

    Ubaguzi wa aina yoyote ile hasa dhidi ya mwanamke ni jambo linalokabiliwa na vita vikali sana ulimwenguni kote.

    Dahari na dahari, hasa katika jamii za kiafrika, kumekuwa na imani isiyotingisika kuwa mwanamke ni kiumbe duni akilinganishwa na mwanaume. Kwa hivyo mwanamke amekuwa akifanyiwa kila aina ya dhuluma ikiwepo kupigwa, kutukanwa, kudharauliwa, kunyimwa haki zake, kunyimwa heshima na mambo kama hayo. Lakini je, ni kweli kuwa mwanamke ni kiumbe duni asiyefaa kutendewa haki?

    Tukichunguza jamii kwa makini tunaweza kuona mara moja kuwa hivyo ni imani potofu isiyo na mashiko yoyote. Ukiimulika familia yoyote ile iliyopiga hatua kimaendeleo, uwezekano mkubwa ni kuwa mume na mke wa familia inayohusika wana ushirikiano mkubwa. Mume anamthamini mke wake na hadiriki kufanya maamuzi muhimu yanayoweza kuathiri maendeleo ya familia bila kumhusisha mke. Mume kama huyo huketi na mkewe, wakishauriana na kufikia uamuzi bora.

    Tukitoka katika muktadha wa kifamilia na kumulika ulimwengu wa kazi iwe ni katika afisi za kiserikali au kwenye makampuni binafsi, ukweli ni kwamba kiongozi yeyote yule aliyefaulu katika usimamizi wake mara nyingi huwa na mke nyumbani ambaye wanashauriana kila uchao kuhusu kazi anayofanya hata kama mke hafanyi kazi mahali pale. Hisia na mawaidha anayotoa mke kwa mume wake ni tunu na huenda asiyapate kwingineko kokote hata katika vitabu vya kupigiwa mifano. Hii ni mojawapo ya sababu ambayo huwafanya viongozi wa nchi mbalimbali kupenda sana kuwatambulisha wake na familia zao waziwazi kwa vile wanajua kuwa jamii inathamini sana msingi wa jamii. Kiongozi ambaye hana mke au familia au yule ambaye mke wake hatambuliki, hutiwa mashaka na jamii hata kama ni kiongozi aliye na azma ya kushikilia kazi ngumu ya kuongoza umma.

    Tukirudi nyuma kidogo na kupiga darubini mataifa ya mbali, tunaweza kuwaona wanawake mashuhuri walio uongozini ambao hadi waleo unapigiwa mfano. Wanawake mashuhuri waliotoa uongozini ambao hadi waleo unapigiwa mfano. Wanawake hao walisimamia mojawapo ya mataifa yenye uwezo na ushawishi mkubwa zaidi duniani. Ingawa wengi wao sasa wameng’atuka, uongozi wao bado unakumbukwa hata baada ya miaka mingi ya wao kuamua kupumzika, Mifano ni kama: Bi Margaret Thatcher aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza, Bi Bandranaike wa Sri Lanka, Golda Meir wa Israel na wengine wengi katika mataifa kama Indonesia, Ufilipino, Bangladesh, Pakistani na kwingineko.

    Katika kufikia tamati, tunapozungumza kuhusu jinsia, hatuna budi kugusia kitafsili masuala nyeti. Kwanza, imani ya kushikilia kikiki tamaduni zisizofaa, ni jambo linalofaa kuchunguzwa kw makini. Kwa mfano, kuna badhi ya jamii ambazo humlazimu mke kurithiwa baada ya kifo cha mumewe. Vile vile baadhi ya jamii za kiafrika zinashikilia kuwa mwanamke hana haki ya kurithi. Kutokana na imani hii, wanawake wengi huishi maisha ya taabu baada ya kutengana na waume zao kwa vile hawana haki ya kurithi chochote kutoka kwa wazazi wao hata kama wazazi hao wana mali nyingi kupindikukia. Mali ya wazazi ni haki ya watoto wa kiume wala si watoto wa kike! Hili ni jambo la kusikitisha mno.

    Isitoshe, wanawake hukumbwa na kizingiti kingine wanapojaribu kumiliki mali ya waume zao baada ya waume hao kukata kamba. Sababu ni kuwa, baada ya hao wenda zao kuwekwa kaburini, vita vya umiliki wa mali huanza mara moja na mwishowe yule mke maskini hujikuta hana hata mahali pa kulala sembuse mali waliyochuma na mali yake yote kunyakuliwa na aila ya mumewe . Jambo hili linaonyesha namna tulivyoachwa nyuma na uhalisia wa mambo. Ni lazima jamii izinduke na itoke kwenye kiza hiki chenye maki nzito.
    MASWALI
    1. Ina maana gani kusema kuwa wanaume hawana budi “kutembea na majira?” (alama2)
    2. Kabla ya uzinduzi huu kuhusu usawa wa kijinsia, wanawake wamekuwa wakitendewa dhuluma za kila aina. Taja tatu. (alama 3)
    3. Je, ni kwa nini viongozi wengi hupenda kujitambulisha na familia zao? (alama 2)
    4. Je, unaamini kuwa hisia na mawaidha anayotoa mke kwa mume wake ni tunu na huenda yasipatikane kwingineko? Fafanua (alama 2)
    5. Je licha ya kunyimwa haki yake ya kujiamulia, ni matatizo yapi mengine yanayoweza kumukumba mke anayelazimishwa kurithiwa? (alama 3)
    6. Eleza maana ya maneno yafuatayo jinsi yalivyotumiwa katika muktadha. (alama 3)
      1. Kushamiri
      2. Hulka
      3. Azma
  2. MUKHTASARI (Alama 15)
    Soma taarifa ifuatayo kasha ujibu maswali yatakayofuata.

    Binadamu hupenda kujivika vilemba vingi mno.Tunapenda kuheshimiwa na kutukuzwa na kila mtu. Tunapenda kuombwa ushauri na wote ambao wanahitaji ushauri! Tunapenda kutambuliwa popote tuendapo.

    |Watu wengi hukataa kufanya jambo la halali kwa kuhofia kuitwa wajinga. Mfano mzuri ni pale ambapo mtu amekosea kidogo katika kutenda jambo; utaona kuwa mtu huyo anaona ugumu wa kuomba radhi au samahani ati kwa sababu ataonekana mjinga.

    Je, ni mara ngapi mkurugenzi ameita mkutano na katika barua yake akatisha kuwaadhibu watakaochelewa na mwishowe ni yeye mwenyewe anayechelewa? Tena huwa haombi msamaha. Ataulaumu usingizi uliomchukua, au gari lililomleta.

    Aghalabu tunapowakuza watoto wetu, tunawafunza maadili mema. Tunawahimiza wale wadogo kwamba ni vizuri kuomba radhi kwa wakubwa wako unapowakosea. Lakini kumbuka kwamba kukosea ni kwa binadamu wote. Mtu anaweza kukukosea kwa makusudi au kwa bahati mbaya. Kwa hivyo tunapaswa kufahamu kwamba, tunapofanya makosa ni lazima tuombe msamaha, iwe ni kwa wakubwa au kwa wadogo, ili kuondoa kero.

    Waja wengi huogopa kusimama mbele za watu na kuwasilisha au kutenda jambo fulani. Kisa na maana, mtu hataki kutenda jambo fulani halafu akosee. Hajiamini na anaogopa kuwa huenda watu wakaona kasoro yake. Lakini kumbuka, kukosa njia ndiko kuijua.

    Huenda ikawa watu wanajadili maswala ibuka kama vile ufisadi, kuavya mimba, matumizi ya dawa za kulevya, ukimwi, uzuiaji wa kizazi na kadhalika... labda huyaungi mkono maoni ya watu wengine kwa sababu ya imani na maadili yako. Hata hivyo, hutaki kusimama ukatoa msimamo wako mbele za watu ingawa dhamiri yako imekwazika. Baadaye utasikika ukiwalaumu watu wengine ilhali ulikataa kusimama na kutetea msimamo wako.

    Wengi wetu hujichukua kuwa watu muhimu sana. Wanaona kuwa sherehe au mkutano wowote hauwezi kufaulu ikiwa wao hawako. Wanapokuwa kwenye hiyo mikutano wao hutaka watambuliwe. Hupenda majina yao yatajwe. Haya huwaridhisha , lakini swali ni je, kuwepo kwao ni muhimu kiasi hicho? Kumbuka kwamba mkutano ungeendelea vizuri bila kuwepo kwao. Kwa hivyo, tusiwe watu wa kutaka kutambuliwa kila tunapoenda mahali. Pia, tusilalamike ikiwa hatukuhusishwa katika jambo fulani.

    Unaposhuhudia jambo fulani, kama wizi au ajali, usiwe na woga wa kutoa usaidizi kwa kutoa ushuhuda. Wengine hata huogopa kutoa usaidizi huo, hata kwa manusura wa ajali za barabarani, eti kwa sababu wanahofia kuitwa mahakamani kutoa ushuhuda. Kuna shida gani kuenda kusema yale uliyoyashuhudia bila kuongeza au kutoa chochote?

    MASWALI
    1. Bila kupoteza maana, fupisha aya ya kwanza hadi ya nne.(maneno 60) (alama 7)
      Nakala chafu:
      Nakala safi:
    2. Fupisha aya nne za mwisho. (maneno 50) (alama 8)
      Nakala chafu.
      Nakala Safi.
  3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
    1. Taja tofauti iliyopo kati ya sauti /f/ na /v/ (alama 1)
    2. Andika sentensi ifuatayo ukitumia kinyume cha neno lililoandikwa kwa herufi ya mlazo: (alama 1)
      Binadamu hawezi kumuumba mwenzake.
    3. Andika sentensi ifuatayo upya ukizingatia kisawe cha neno lililopigwa mstari: (alama 1)
      Mtoto mwenye hamaki hawezi kuelewa maagizo.
    4. Andika kwa usemi halisi: (alama 3)
      Yule mshukiwa aliyekamatwa na polisi alisema kuwa papo hapo ndipo alipoficha ule mkufu.
    5. Tunga sentensi inayoshirikisha nomino uliyopewa pamoja na vipashio vifuatavyo vya sarufi: kivumishi kisisitizi, kitenzi kishirikishi, kitenzi, na kielezi cha wakati.(alama2)
      Pinde
    6. Sahihisha sentensi zifuatazo :
      1. Ndegwa alipeana kalamu yake kwa mwanafunzi. (alama 1)
      2. Siku hizi mahitaji imezidi na pesa haitoshi. (alama 1)
    7. Tunga sentensi mbili kubainisha maana mbili tofauti za neno: rudi. (alama 2)
    8. Akifisha: (alama 2)
      Mtume asimame nusura aingie kwenye shimo la taka
    9. Unda nomino kutokana na kivumishi:refu (alama 1)
    10. Onyesha chagizo katika sentensi ifuatayo: (alama 1)
      Watu wanne walipeperushwa juu kwa juu na upepo mkali.
    11. Tunga sentensi ukitumia: isije ikawa (alama 2)
    12. Andika upya sentensi ifuatayo ukitumia virejeshi vya tamati: (alama 2)
      Mwanafunzi anayefanikiwa maishani ni yule anayesoma kwa bidii na pia anayewatii wazazi wake.
    13. Ainisha viambishi awali na tamati katika sentensi: Anikumbukaye (alama 2)
    14. Kanusha kwa udogo: Mwizi aliiba kikapu na ng’ombe. (alama 2)
    15. Andika umoja wa sentensi: (alama 1)
      Kwato za wanyama hutufaidi.
    16. Andika kwa wingi : (alama 4)
      Wimbi hilo la maji lilimhofisha mvuvi akashindwa kutupa wavu wake majini.
    17. Andika katika hali ya kutendewa: (alama 2)
      Kuku hawa wamemsumbua Sabina kwa muda mrefu.
    18. Tumia sentensi moja moja kubainisha tofauti kati ya sentensi sahili na sentensi ambatano (alama 2)
    19. Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya mistari au mishale:
      Mwanasiasa aliyewapuuza wanaeneo bunge lake amekomelewa. (alama 4)
    20. Andika katika usemi wa taarifa. (Alama 2)
      “Karibu Bakari, tafadhali kaa”, Maimuna alisema. “Asante, je, habari za nyumbani?” Bakari aliuliza.
    21. Taja aina ya yambwa iliyopigiwa mstari katika sentensi uliyopewa: (alama 1)
      Mpishi amempikia mgeni wali vizuri.
  4. ISIMU JAMII (Alama 10)
    1. Taja nadharia zozote mbili zinazohusiana na chimbuko la lugha ya Kiswahili. (alama 2)
    2. Kwa kutolea mifano, eleza sifa zozote nne za kimsingi za sajili inayoweza kutumika darasani. (alama 8)

MWONGOZO WA KUSAHISHA

UFAHAMU

  1. Lazima wakubali mabadiliko / kuwa swala la mabadiliko kuhusu jinsia haliwezi kupuuziliwa mbali (alama 2)
  2.  
    1. Kutukanwa
    2. Kudharauliwa
    3. Kunyimwa
    4. Hakikunyimwa heshima
    5. Kunyimwa nafasi za ajira, elimu, uongozi (zozote 3x1=alama 1)
  3.  
    1. Jamii inathamini sana misingi ya familia/ mume na mke wa familia inayohusika wanaushirikiano mkubwa
    2. Kiongozi ambaye hana mke au familia au Yule ambaye mke wake hatambuliki, hutiwa mashaka na jamii hata kama kiongozi aliye na azma ya kushikilia kazi ngumu ya kuongoza umma. (alama 2)
  4.  
    1. Kwa sababu yatalenga mafanikio ya familia na mume
    2. Kiongozi aliyefaulu katika usimamizi wake mara nyingi huwa na mke ambaye wanashauriana
    3. Tunaweza kuwaona wanawake mashuhuri waliotoa uongozi ambao hadi waleo unapigiwa mfano. (3x1alama 3)
  5.  
    1. Kukosa urithi
    2. Maisha ya dhiki
    3. Kubaguliwa
    4. Magonjwa yanayoweza kuangamiza k.v. ukimwi
  6.  
    1. Kushamiri-kunawiri
    2. Hadiriki- hafai/ hastahili
    3. Azma- Nia/ kusudi

MUKHTASARI
Swali (a)

  1. Binadamu hupenda kujivika vilemba vingi kama vile kutukuzwa na kuheshimiwa, kuombwa ushauri na kutambuliwa
  2. Wengi hukataa kufanya jambo la halali kwa kuhofia kuiwa wajinga/ wanapokosa huona ugumu wa kuomba radhi/ samahani kwa sababu ataonekana mjinga
  3. Mara nyingi mkurugenzi huita mkutano na kutisha kuadhibu watakaochelewa na mwisho yeye mwenyewe akachelewa
  4. Huwa haombi msamaha (bali) hulaumu usingizi au gari
  5. Aghalabu tunapowakuza watoto, tunawafunza maadili mema/ tunawafunza umuhimu wa kuomba radhi wanapokosea wakubwa
  6. Kukosea ni kwa binadamu wote (na) huweza kuwa kwa makusudi au bahati mbaya
  7. Tunapofanya makosa ni lazima tuombe msamaha ili kuondoa kero (1x7)

Swali (b)

  1. Waja wengi huogopa kusimama mbele za watu na kuwasilisha/ kutenda jambo fulani
  2. Huwa hataki kukosea/ hajiamini/ huenda watu wakaona kasoro yake
  3. Hawajui  kuwa kukosa njia ndiko kuijua
  4. Wanaweza kujadili maswala ibuka na pengine huyaungi  mkono maoni ya wengine kwa sababu ya imani/maadili (nawe) hutaki kutoa msimamo ingawa dhamiri yako imekwazika na baadaye hulaumu wengine ilhali ulikataa kusimama na kutetea msimamo wako.
  5. Wengi hujichukuwa watu muhimu  sana na huona mkutano/sherehe hauwezi  kufaulu ikiwa hawako/hutaka watambuliwe/majina yao yatajwe
  6. Tusiwe watu wanaotaka kutajwa au wanaolalamika ikiwa hatukuhusishwa kwenye jambo
  7. Unaposhuhudia jambo, usiogope kutoa usaidizi au ushahidi   (1x zozote 7)
    a - 7
    b - 7
    ut - 1
    Jumla = 15
    Makosa
    1. Ondoa makosa ya sarufi hadi alama 5 (makosa 10 x ½ alama)
    2. Ondoa makosa ya hijai hadi alama 3 (makosa 6 x ½ alama)
      (makosa ya sarufi yaadhibiwe yanapotokea mara ya kwanza tu; kwa kila aina ya kosa la sarufi, addhibu makosa mawili tofauti)

MATUMIZI YA LUGHA

  1. /f/ - konsonanti hafifu/sghuna (al.1)
    /v/ - konsonanti ghuna
  2. Binadamu hawezi  kumuumba mwenzake (alama 1)
    (akipata kitahiniwa bila kutunga sentensi – al.½)
  3. Mtoto mwenye hasira/ghadabu hawezi kuelewa maagizo (al.1)
  4. Yule mshukiwa aliyekamatwa na polisi alisema, “papa hapa ndipo nilipoficha huo mkufu.”
    “papa hapa ndipo nilipoficha huo mkufu,” Yule mshukiwa aliyekamatwa na polisi alisema.   (al.3)
  5. Pinde zizi hizi ndizo zilizonunuliwa jana jioni. (al.2)
    (sentensi iwe na mantiki na ihusishe sehemu zote)
  6.  
    1. Ndegwa alimpa mwanafunzi kalamu yake. (al.1)
    2. Siku hizi mahitaji yamezidi na pesa hazitoshi (al.1)
  7. Rudi: 
    1. Njoo tena/rejea (al.1)
    2. Rekebisha tabia/kanya/adhibu/adilisha- hasa motto (al.1)
  8. Mtume! Asimame, nusura aingie kwenye shimo la taka (al.2)
  9. – refu : urefu (al.1)
  10. Chagizo : juu kwa juu na upepo mkali (al.1)
  11. Isije ikawa – sawa na ‘isitokee kuwa’ k.m. isije ikawa yeye ndiye alitenda kitendo hicho. (al.2) (sentensi sahihi, asibadilishe kiunganishi)
  12. Mwanafunzi afanikiwaye√ maishani ni Yule asomaye√  kwa bidii na pia awatiiye √ wazazi wake  (‘O’ tamati  ½ x 3 + ½ ya sentensi = al.2) (bila ‘O’ ya tamati asipate)
  13. Anikumbukaye  a-, -ni- (viambishi awali );√  -a-, -ye- (viambishi tamati) √
    a - Kiambishi  cha nafsi ya tatu, umoja (mtenda) √
    -ni-  kiambishi cha nafsi ya kwanza umoja (mtendwa)√
    -a- kiishio√
    -ye- kirejeshi√
  14. Kijizi hakikuiba kijikapu na kigombe/kijigombe (al.2)
    (swali lizingatiwe kwa ujumla, akikosa kutahiniwa chochote – 0)
  15. Ukwato wa mnyama hunifaidi (al.1)
  16. Mawimbi hayo ya maji yaliwahofisha wavuvi wakashindwa kutupa nyavu zao majini (al.4)
  17. Sabina amesumbuliwa na kuku hawa kwa muda mrefu (al.2)
  18. Sahili : sentensi yoyote sahihi yenye kitenzi kikuu kimoja/wazo moja kuu. (al.1)
    Ambatani : sentensi sahili mbili zilizounganishwa (al.1)
  19. S _________________ KN + KT√
    KN ________________N + S √√
    N _________________ Mwanasiasa√
    S _________________Aliyewapuuza wanaeneo lake√
    KT _________________ T
    T __________________amekomelewa.  (al. ½ x 6 =3) (sita kutuza anapokosea, asipopata mwanzo-sifuri)Maimuna
  20. alimkaribisha Bakari na kumuomba/sihi akae (naye) Bakari akamshukuru na kumuuliza/kutaka kujua habari za nyumbani. (al.2)
  21. Mgeni – yambwa tendewa (al.1)
    Makosa
    1. Hijai 6 x ½ = 3h
    2. Sarufi makosa yote
      *mwanafunzi asiadhibiwe makosa ya sarufi zaidi ya nusu ya alama  alizopata katika kila kisehemu.

ISIMUJAMII

  1. Nadharia :
    1. Kiswahili kama lugha ya mseto/mchanganyiko wa lugha tofauti za kigeni na za dkiafrika. Ni zao la kuingiliana kwa lugha za kigeni kama kihindi, kiarbu, kiajemi na lugha za makabila ya wenyeji
    2. Kiswahili kama tokeo la ndoa baina ya wanawake wa pwani ya afrika mashariki na waarabu/lugha ya vizalia wa ndoa kama hio.
    3. Kiswahili ni lugha  ya kibantu kulingana na ushahidi wa kiisimu na kihistoria (alama 1 x 3 =3)
  2. Sifa za kimsingi za sajili ya darasani :
    1. Lugha sanifu
    2. Mwingiliano wa kisarufi hudumishwa
    3. Msamiati huegemea kwenye mada husika/maneno ya taaluma mbalimbali hutumika
    4. Urudiaji/takriri – ili kuhakikisha kuwa hoja imeeleweka
    5. Majibizano – kati ya mwalimu na waxnafunzi wanapouliza na kujibu maswali
    6. Sentensi huweza kuwa fupi/ndefu kutegemea mada husika
    7. Imejaa ufafanuzi – wahusika wanapoelezea hoja ili ieleweke vyema
      (mtahiniwa atoe maelezo au mifano, akitaja hoja tu – al 1)
      (zozote 4 za kwanza x 2 =8)
      Makosa
      1. Hijai 6 x ½ = 3h
      2. Sarufi 6 x ½ =3s
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Form 3 End Term 2 Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest