Tuesday, 11 July 2023 14:04

Kiswahili Questions and Answers - Class 8 Mid Term 2 Exams 2023 Set 6

Share via Whatsapp

Soma vifungu vifuatavyo. Vina nafasi 1 mpaka 15. Kwa kila nafasi umepewa majibu manne. Chagua jibu lifaalo zaidi kati ya yale uliyopewa.

Ufugaji wa kuku ni njia mojawapo ya uwekezaji __1__sana na watu wengi __2__ kujiimarisha kiuchumi. Kuku hawa hufungiwa ̧__3__ na __4__ vyakula vinavyonunuliwa madukani. Kama __5__ wahenga __6__. Mfugaji __7__ ipasavyo hupata hasara kwani kuku huhitaji kutunzwa kwa makini nyakati __8__. Bila shaka shughuli hii ni __9__ njia za kukabiliana na uhaba wa nafasi za ajira nchini.

       A             B          C           D 
 1.   unaotumika   zinazotumika   inayotumika   unapotumika 
 2.  kwa minajili ya   mintaarafu ya   mithili ya   sambamba na 
 3.  mazizini  matunduni   viambazani   vizimbani 
 4.  kukulishwa  kulishwa   kulishiwa   kukula 
 5.  waliposema  waliosema   walivyosema   wangesema 
 6. mtaka cha mvunguni sharti ainame  mwenye pupa hadiriki kula tamu  kila chombo na wimbile  mtegemea nundu haachi kunona
 7.  asipowajibika  asiowajibika   asiyowajibika   akiwajibika 
 8.  yote  yoyote  wote  zote
 9.  baadhi ya  kati ya  fauka ya  dhidi ya

 

Maki alielewa vyema maana ya methali isemayo __10__ Japo alifanya kazi ya __11__, aliweka akiba __12__ hadi __13__ mtaji wa kuanzisha biashara __14__. Kwa njia hiyo, __15__hali yake ya maisha.

                      A                 B                        C   D 
 10.  tone na tone huwa mchirizi  chururu si ndondondo  kwendako hisani hurudi hisani  mgaagaa na upwa hali wali mkavu
 11.  msaragambo  kikoa   kijungujiko   shokoa 
 12.  dogodogo  kidogokidogo   vidogovidogo   mdogomdogo 
 13.  aliyopata  aliopata  alivyopata   alipopata 
 14.  yake yenyewe  lake mwenyewe   lake lenyewe   yake mwenyewe 
 15.  alimudu kuiboresha alijihimu kuyaboresha  alimudu kuyaboresha   alijihimu kuiboresha

 
Kutoka swali la 16 mpaka 30, jibu kila swali kwa kuchagua jawabu lifaalo zaidi.

 1. Andika usemi wa taarifa wa sentensi ifuatayo.
  "Mto huu una mamba wengi," Shindo alisema.
  1. Shindo alisema kuwa mto huo huwa na mamba wengi.
  2. Shindo alisema kwamba mto huo ulikuwa na mamba wengi.
  3. Shindo alisema kwamba mto huo ungekuwa na mamba wengi.
  4. Shindo anasema kuwa mto huo una mamba wengi.
 2. Jora ni kwa vitambaa kama vile kande ni kwa
  1. samaki
  2. maua
  3. vibarua
  4. mawele.
 3. Chagua maelezo yaliyo sahihi.
  1. Pimamaji ni kifaa cha kupimia usawa wa ukuta.
  2. Fuawe hutumiwa na maseremala kutobolea mbao.
  3. Mvukuto hutumiwa na wahunzi kupulizia moto.
  4. Timazi hutumiwa kupimia usawa wa sakafu.
 4. Andika sentensi ifuatayo kwa wingi.
  Wimbi ulipepetwa kwa uteo ule.
  1. Mawimbi yalipepetwa kwa teo zile.
  2. Wimbi ulipepetwa kwa teo zile. 
  3. Mawimbi yalipepetwa kwa teo ile.
  4. Wimbi ulipepetwa kwa teo ile.
 5. Tegua kitendawili kifuatacho.
  Mtoto wangu mvivu hapandi mlima
  1. Upepo
  2. Mvua
  3. Mto
  4. Kobe.
 6. Chagua sentensi yenye kiwakilishi cha pekee.
  1. Vijana wote walishiriki michezo lakini wale walicheza vizuri zaidi.
  2. Dawati langu lina vitabu vingi lakini lake lina vichache tu.
  3. Mji huu na umeme lakini ule hauna miundomsingi muhimu.
  4. Shule yetu ina walimu wa kutosha lakini nyingine zina wachache tu.
 7. Salwa ni mtoto wa dada yangu. Jina linalofaa zaidi kwangu kumtajia Salwa ni
  1. mpwa
  2. umbu
  3. mkoi
  4. mkazamwana.
 8. Tambua sentensi iliyoakifishwa ipasavyo zaidi.
  1. Mwezi uliopita Februari- kulikuwa na joto jingi.
  2. Tulihitaji viungo vifuatavyo: dania, iliki, karafuu na mdalasini.
  3. Mama aliniambia: usiwe mtu anayependa kustarehe.
  4. Maneno yote; yale yaliyoandikwa; yalikuwa sahihi.
 9. Kipande cha pili katika mshororo wa shairi huitwaje?
  1. Ukwapi
  2. Mwandamizi
  3. Utao
  4. Mloto.
 10. Baada ya hukumu kutolewa, mshatakiwa alituma ombi la kutaka hukumu ile ibatilishwe na kesi isikilizwe upya. Kwa hivyo mshtakiwa
  1. alikata rufaa
  2. aliruka kesi
  3. alitoa dhamana
  4. aliahirisha kesi.
 11. Chagua kitenzi kilichoundwa kutokana na kivumishi
  1. Maandishi - andika 
  2. Upishi-mapishi
  3. Mcheshi - kicheko 
  4. Mwangalifu - angalia
 12. Ni jozi ipi iliyo sahihi?
  1. Punda, nirihi 
  2. Bata, kiyoyo
  3. Paka, kilebu
  4. Ndovu, shibli.
 13. Bainisha matumizi ya kiambishi 'ki' katika sentensi ifuatayo.
  Kijana huyo akipewa nafasi atapambana kishujaa.
  1. Wakati, namna
  2. Kuendelea, jinsi
  3. Masharti, jinsi
  4. Udogo, masharti.
 14. Maelezo yapi hayaonyeshi maana ya neno 'changa'?
  1. Kukusanya fedha ili kutimiza haja fulani.
  2. Kupata maumivu ya viungo.
  3. Hali ya kitu kukosa kukomaa.
  4. Namna ya samaki wa baharini.
 15. Chagua methali yenye maana sawa na hii.
  Nazi mbovu ni harabu ya nzima.
  1. Nzi mmoja huoza ngombe.
  2. Samaki huanza kuoza kichwani.
  3. Mkataa pema pabaya panamwita 
  4. Mpiga ngumi ukuta huumiza mkonowe.

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu swali la 31 mpaka 40.

Mengi yamesemwa kuhusu ufisadi. Si wanasiasa, si mapadre, si mashehe, si viongozi wengineo wa jamii, wote wametoa mchango wao juu ya suala hili nyeti. Kila linaloenda mvange, sababuye ufisadi. Nchi haina ustawi, kiini ni ufisadi. Kusambaratika kwa miundomsingi asili yake ni ufisadi.

Je, hapo ulipo unaelewa ufisadi kuwa ni nini? Huenda umewahi kujituliza na kutafakari juu ya ufisadi. Unahusika vipi na ufisadi? Umewahi kuathirika na ufisadi, wewe binafsi au kupitia kwa aila na masahibu? Kila mzalendo halisi anastahili kujisaili nafsi yake kupitia kwa maswali haya.

Wakati unapoendelea kuzingatia maswali hayo hebu tuzame kwenye kina cha ufisadi. Kijelezi cha ufisadi ni ile hali ya kutenda au kushiriki mambo yanayosababisha uharibifu au uborongaji wa kanuni au taratibu zilizokubalika kutekeleza mambo. Katika hali hii, ufujaji na ubanangaji huwa vyombo vya ufisadi. Madhumuni yake ya jumla ni kubatilisha haki, kuvotana na haki na hatimaye kuifanya isifuate mkondo wake sahihi.

Mbegu ya ufisadi ni uchoyo; kimsingi, chimbuko la ufisadi ni ubinafsi uliokithiri. Dhana ya kujiwazia kibinafsi katika shughuli zote ndiyo humpa ubinafsi nishati ya kujiendeleza. Kila mja ana kiwango fulani cha ubinafsi. Hali hii ndiyo hupelekea kujitahidi kwa jino na ukucha ili kujihifadhi na kujiendeleza. Ubinafsi wa aina hii hauna kasoro kwani humpa binadamu msukumo wa kujishughulikia kwa lengo la kijipatia natija inayofaidi aila, jamii na hatimaye taifa kwa jumla.

Uchoyo wa mimi-hiki, mimi-hicho, mimi-kile na hatimaye mimi-kila kitu ni uchuro. Ufisadi nao ni uchuro. Ni dude, jinyama, jipweza lenye minyiri isiyohesabika. Minyiri hiyo imepenyeza katika nyanja zote za maisha ya mtu binafsi na ya taifa kwa jumla. Ufisadi umeshamiri na kuzagaa hadi kufikia kiwango cha kimataifa.

Vuta taswira hali ya waja wazito wawili ambao zao zimewadia. Mmoja anajiweza anawasilishwa hospitalini kwa gari. Wa pili hana mbele wala nyuma amefika kwa miguu au pengine kwa rukwama. Kisia mwenyewe ni nani atakayehudumiwa kwanza. Ukitafiti utagundua kuwa sababu ni ufisadi. Mmoja atatadarukiwa ilhali mwenzake . atakawilishwa. Haya pengine ni kutokana na matumaini ya kupewa bahashishi ambayo kwa kweli ni namna ya hongo. Kumbuka, wahudumu wawa hawa ni waajiriwa wapokeao mishahara mwisho wa mwezi.

Katika amali za biashara, uborongaji wa taratibu unadhihirika hasa katika utoaji wa zabuni za miradi mbalimbali ambapo suala kubwa ni kasma. Kiasi na jinsi ni baada ya kuhakikisha kuwa tenda imeliendea shirika fulani. Kasma lazima ipatikane! Si hoja kuwa pesa za kugharamia miradi hii zimetokana na ruzuku au mikopo kutoka kwa wafadhili. Ghushi za kila aina zitatumiwa ili kasma ipatikane. Katika hali kama hii, si ajabu matokeo ni kuharibika kwa miundomsingi katika sekta mbalimbali zinazohusika na usambazaji wa huduma kwa wananchi.

Ni dhahiri shahiri kuwa kila mmoja anapaswa kujumuika katika kitali hiki dhidi ya ubinafsi, ufisadi na ubanangaji. Sote tukianzia na viongozi, tunapaswa kujifunga nira kupambana na ufisadi. Wananchi wahamasishwe juu ya wajibu wao katika vita hivi vikali. Sote tuzinduke na kufahamu hicho kidogo cha ziada, hiyo fadhili, mapendeleo hayo ambayo msingi wake ni kuvuruga utaratibu yatatuponza. Changamoto kwa kila mmoja wetu ni: Tuko tayari kuziasa nafsi zetu ili zitambue athari za ubinafsi na hivyo kuzikabili vilivyo? Tutakapotambua kuwa waendelezaji wa ubinafsi ni mimi na wewe, hapo ndipo vita hivi vitakapoanza kufanikiwa.

 1. Kulingana na aya ya kwanza
  1. viongozi mbalimbali wa kijamii wamehusishwa na ufisadi
  2. ufisadi ni chanzo cha kuvurugika kwa mambo mengi katika jamii
  3. viongozi wamepuuza mchango wao katika vita dhidi ya ufisadi
  4. kuharibika kwa miundomsingi kumefanya watu wawe mafisadi.
 2. Si kweli kusema kuwa
  1. mwandishi ana hakika kwamba msomaji amewahi kuwazia ufisadi
  2. wakati mwingine ufisadi haumwathiri mtu moja kwa moja
  3. jamaa na marafiki wanapofikwa na madhara sisi huathirika pia
  4. mtu anayeipenda nchi yake anapaswa kuwaza kuhusu misingi ya ufisadi.
 3. Ufisadi hasa unahusu nini?
  1. Utoaji wa pesa kinyume na sheria. 
  2. Kutojua vizuri sheria za jamii yake.
  3. Njama za kubadilisha mkondo wa haki.
  4. Kujuana na walio katika nafasi za uongozi.
 4. Maana ya 'kujitahidi kwa jino na ukucha' ni 
  1. kuvumilia shida ili uweze kufanikiwa
  2. kushiriki njama ziletazo maangamizi 
  3. kupigana na wale wanaokiuka sheria
  4. kufanya bidii kwa vyovyote vile.
 5. Mwandishi anasema kuwa ubinafsi hauna shida ikiwa
  1. utamletea mtu manufaa anayotarajia
  2. haujagunduliwa na vyombo vya dola
  3. wanaoathirika na hulka hiyo ni wachache 
  4. utazalisha manufaa yatakayowafaidi wote.
 6. Taswira inayotolewa kuhusu hali iliyo hospitalini ni kuwa
  1. wagonjwa hufikishwa kwa njia ainati
  2. huduma zinatolewa kwa mapendeleo 
  3. ukabila unajitokeza katika kuwashughulikia wagonjwa
  4. wanaohudumiwa vizuri hawana shida ya kutoa bahashishi.
 7. Utoaji wa zabuni bila kuzingatia utaratibu ufaao
  1. umeathiri utoaji huduma kwa wananchi
  2. hutokana na juhudi za serikali kukomesha ufisadi
  3. umesababisha kupatikana kwa huduma bora zaidi
  4. haujaliathiri taifa wala watu binafsi.
 8. Ipi si njia ya serikali kupata pesa za kuendesha miradi yake?
  1. Ushuru
  2. Misaada
  3. Mikopo
  4. Rushwa.
 9. Wito wa mwandishi katika aya ya mwisho ni kuwa
  1. tuwatambue mafisadi ili tukabiliane na uovu huu
  2. kila mmoja ajitahidi kugundua madhara ya ufisadi
  3. vita dhidi ya ufisadi vianze kwa sisi wenyewe kujiasa
  4. tuendeleze ubinafsi ili kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.
 10. Neno jingine lenye maana sawa na 'kitali' ni
  1. uovu
  2. juhudi
  3. vita
  4. harakati.

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu swali la 41 mpaka 50.

Mzee Maganga alikuwa tajiri maarufu katika mtaa wa Shwari. Wakazi wengi walimstahi kutokana na idili na maarifa yake ya kuendesha biashara. Aidha mzee huyu asingejumuishwa katika orodha ya adinasi wenye mkono birika. Hakika mzee huyu alikuwa mkwasi wa mali na moyo kwani mbali na kuwakidhia wanawe mahitaji yao yote, aliwasabilia wanakijiji kwa mengi. Wapo waliopewa ruzuku za vyakula, karo za wanao ada ya matibabu na hata vibarua almradi waweze kuzikimu aila zao.

Maganga mwenyewe hakuzaliwa na asali mdomoni. Inasemekana baba yake alikuwa fukara fukefuke. Kwa bahati nzuri alipata msaada wa kanisa akawaelimisha maganga na nduguze hadi vyuo vikuu. Ndugu zake walipata kazi serikalini lakini Maganga ambaye alisomea elimu biashara aliamua kuanzisha kazi yake binafsi. Alikuwa na maduka kadhaa kuanzia yale ya vipuri, ya nafaka, ya vitabu na hata kiwanda cha kukobolea mpunga.

Makali ya umri sasa yalianza kumlemea Maganga. Alikuwa si yule Maganga aliyerauka mapema kuenda kukagua shughuli katika biashara zake. Kila mara alijihisi mnyonge huku mwili wake ukilemewa na maumivu ya viungo. Maganga alijawa na hofu sio kwa sababu ya hali hii mpya kwani alielewa kuwa hii ni ada ya kila mja. Moyo ulimwuma kutokana na hali ya mwanawe wa pekee kuandama anasa kila uchao. Majanga alihofia kuwa angeenda kaburini na biashara zake.

Siku moja, Maganga alimwita mwanawe akamshtakia hali. Alimweleza kinagaubaga kuwa utendakazi wake ulikuwa ukikaribia ukingoni. Kijana alionyesha huruma machoni lakini moyo ulimdunda kwa raha ya kurithi milki ya baba yake. Mzee mwenyewe aliliona hili waziwazi. Hata hivyo alijitia hamnazo. Alimwagiza mwanawe ampelekee shilingi laki moja, pesa taslimu alizozifanyia kazi yeye mwenyewe. Kijana alimweleza mamaye, naye akaahidi kumpa fulusi zile baada ya juma moja.

Baada ya kupokea kitita kile kutoka kwa mama yake, kijana alimwendea mzee Maganga chumbani alimokuwa akiota moto. Bila kuzihesabu pesa zile, mzee alizitupa motoni zikateketea huku kijana amejitazamia tu, akingoja mzee atimize ahadi kwani ahadi ni deni. Hapo mzee alimtazama kijana akasema, "Nenda uniletee shilingi laki moja; jasho lako hasa!”

Kijana alikereka moyoni, akatuhumu kuwa mama alikuwa amemsaliti. Aliwaendea marafiki zake waliozoea kustarahe pamoja. Vijana wale walichanga bia, wakampa kiasi kile akaondoka kwa furaha. "Sasa baba atatambua kuwa mimi pia nina uwezo wa kuchuma”, akajiambia huku akielekea kwa baba yake. Hata hivyo hali ilikuwa kama ile ile ya kwanza. Moyo ulimwuma kijana kwa ujeuri wa babaye akaondoka huku akilaani.

Hamu ya kupata urithi ilimtia kijana ari ya kutimiza matakwa ya baba yake. Alibeba nguo chache akafunga safari kuenda katika mji wa mbali. Alipata kazi ya utwana akaifanya kwa hamu huku akitunduiza kidogo alicholipwa kila mwezi. Kwa miaka miwili, hakuthubutu kununua mavazi mazuri wala kushiriki anasa. Pesa zilipotosha, aliwaaga waajiri kwa heshima akafunga safari ya kurudi nyumbani. Wakati huu, alikuwa na hakika kwamba mambo yake yangetengenea.

Kijana alipofika nyumbani, hali yake ilikuwa ya kuhuzunisha. Alimwendea baba yake akampa pesa kama awali. Baba naye alikirudia kitendo kilekile. Kwa hamaki kuu, kijana aliutia mkono motoni bila kujali majeraha aliyopata akazitoa pesa zile kabla hazijateketea. Alimweleza babaye kimasomaso kwamba hakujali kukosa urithi lakini asingekubali jasho lake litiwe motoni. Aliondoka akajifungia chumbani mwake.

Siku iliyofuata, Maganga aliwaita wasimamizi wa biashara zake. "Sasa naona mwanangu ametambua kuwa uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi. Ninampa usukani wa biashara zangu zote." Hapo ndipo kijana alipolifumbua fumbo la baba yake. Alimwangukia miguuni akamwomba radhi na kumshukuru kwa kumpa elimu isiyopatikana katika chuo chochote. Kijana aliendeleza biashara vizuri huku akijitenga na marafiki waliomshawishi kushiriki anasa. Hakika alifanikiwa hata kuliko baba yake. Akaiyeyusha hofu ya mzee Maganga

 1. Chagua jibu lililo sahihi.
  1. Wanakijiji walimheshimu Maganga kwa utajiri wake.
  2. Maganga alikuwa mja mwenye mkono wazi. 
  3. Wote waliomwendea Maganga walipata msaada wa chakula
  4. Wachache waliyafahamu maarifa ya Maganga katika biashara.
 2. Maisha ya utotoni ya Maganga yalikuwa
  1. ya starehe
  2. yenye dhiki tupu
  3. ya kutia moyo
  4. ya uhitaji.
 3. Maganga alitofautianaje na ndugu zake?
  1. Alikuwa bora zaidi yao masomoni.
  2. Maganga alipenda kusaidiwa kuliko nduguze.
  3. Kinyume na ndugu zake, hakupendelea kazi za ajira.
  4. Maganga alifanikiwa maishani kuliko ndugu zake.
 4. Kulingana na aya ya tatu, ni kweli kuwa
  1. umri ukizidi hudhoofisha utendakazi wa watu 
  2. ugonjwa unaweza kukwamisha ndoto zetu
  3. kufanya kazi kidindia husababisha maumivu ya viungo
  4. unyonge wa nafsi huunyima mwili nguvu zifaazo. 
 5. Hofu ya Maganga hasa ilitokana na
  1. mauti yaliyokuwa yakibisha hodi
  2. uwezekano wa kukosa mrithi afaaye 
  3. tamaa ya mwanawe ya kurihi mali yake 
  4. njama alizofanya mkewe na mwanawe.
 6. Ni kweli kusema kwamba
  1. kijana alimsikitikia baba yake kwa hali iliyomkabili
  2. Maganga hakutaka kumrithisha mwanawe mali
  3. janga la baba lilionekana kama neema na mwanawe
  4. mama hakutaka mwanawe arithishwe mali. 
 7. Haikuwa vigumu kwa mzee kutambua kwamba kijana hakusumbukia pesa mara ya kwanza na ya pili kwa kuwa
  1. zilipatikana kwa urahisi sana
  2. zilipatikana kwa haraka sana
  3. kijana alikasirika zilipoteketezwa
  4. kijana hakuathirika sana zilipoteketezwa.
 8. Mwanawe Maganga aliishi maisha gani katika mji wa mbali?
  1. Ya kujinyima
  2. Ya anasa
  3. Ya kitajiri
  4. Hatujaambiwa.
 9. Maana ya methali "Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi" kulingana na kifungu ni kuwa 
  1. ni mzazi pekee anayezijua dhiki za mwanawe
  2. anayejua thamani ya kitu ni yule aliyesumbuka kukitafuta
  3. mtoto akimkosea mzazi heshima atafikwa na maafa
  4. maovu ya mtoto humwathiri zaidi mzazi wake.
 10. Kijana alifanikiwa kuliko baba yake kwa kuwa
  1. aliwajibika zaidi
  2. alikuwa na maarifa zaidi 
  3. alipata mtaji mkubwa zaidi 
  4. alisaidiwa na watu wengi zaidi.

INSHA

Umepewa dakika 40 kuandika insha yako.

Andika insha isiyopungua kurasa moja na nusu ukifuata maagizo uliyopewa.
Ufuatao ni mwanzo wa insha. Iendeleze kwa maneno yako mwenyewe huku ukiifanya iwe ya kusisimua zaidi.

Ni kweli kuwa ibilisi wa mtu ni mtu. Ukweli wa methali hii ulibainika siku moja ambapo........................................................

MARKING SCHEME

 1. C
 2. A
 3. D
 4. B
 5. C
 6. A
 7. A
 8. D
 9. B
 10. A
 11. C
 12. B
 13. D
 14. D
 15. A
 16. B
 17. D
 18. C
 19. B
 20. C
 21. D
 22. A
 23. B
 24. C
 25. A
 26. D
 27. B
 28. C
 29. D
 30. A
 31. B
 32. A
 33. C
 34. D
 35. D
 36. B
 37. A
 38. D
 39. C
 40. C
 41. B
 42. D
 43. C
 44. A
 45. B
 46. C
 47. D
 48. A
 49. B
 50. A
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Questions and Answers - Class 8 Mid Term 2 Exams 2023 Set 6.


Tap Here to Download for 30/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students