Thursday, 22 June 2023 11:51

Kiswahili Questions and Answers - Class 8 Mid Term Exams Term 2 2023 Set 1

QUESTION

Soma vifungu vifuatavyo. Vina nafasi 1 mpaka 15. Kwa kila nafasi umepewa majibu manne hapo. Jaza kila pengo kwa kuchagua jawabu lifaalo zaidi.

Nikikueleza jinsi __1__ kabla__2__maishani, hutaamini nitakayokueleza. Nilipitia shida baada ya __3__tangu nilipokuwa mtoto mchanga.__4__ tu nilipozaliwa, mama na baba yangu __5__. Mama aliamua kujiondoa akarudi nyumbani kwao. Nilibaki katika mikono ya baba aliyekuwa na __6__. Kila alipokasirika, alinipa kichapo cha mbwa. Maji yalipozidi unga, __7__ katika makao ya mayatima ya Jitunze. __ 8__ , maisha yangu yalibadilika na kuchukua mkondo mpya. Hata nilipokuwa katika darasa la nane, nilikuwa mwangalifu zaidi nisije nikapotoka. Nilikumbuka ya wahenga kuwa __9__.

   A   B   C   D 
 1.   nilipotesa   nilivyotesa   nilipoteseka   nilivyoteseka 
 2.  ufanisi  nifaulu  kufaulu   sijafaulu 
 3.  mingine  ingine  nyingine  mengine
 4.  Pindi  Namna   Lakini   Pia 
 5.  hawakupikika katika chungu kimoja   hawakuwa maji na mafuta   hawakuwa Lila na Fila   hawakubaidika kama mbingu na ardhi 
 6.  moyo thabiti  moyo mgumu   moyo mkunjufu   moyo mdogo 
 7.  nilihamishwa  nilihama  nilitorokea   nilijitosa 
 8. Huyo  Huko  Huo  Huyu
 9. mgaagaa na upwa hali wali mkavu mumunye huharibikia ukubwani kinga na kinga ndipo moto uwakapo papo kwa papo kamba hukata jiwe


Uamuzi wa mwanafunzi katika maisha __10__ mambo mengi mno. __11__ mwalimu na mzazi huweza __12__ kuhusu hili na lile, uamuzi wa kufuata ushauri au kuutupilia mbali huwa ni __13__ Lile analofaa __14__ ni kuwa akifanya uamuzi mzuri, atafurahia maisha. Uamuzi mbaya __15__na kilio na majuto.

   A   B   C   D 
 10.   huathiriana   huathiria   huathiriwa   huathiri 
 11.  Maadamu  Ingawa   Ikiwa  Ila 
 12.  kumwelekeza   kujielekea   kujielekeza   kumwelekea 
 13.  wake mwenyewe   yake yenyewe    wake wenyewe    yake mwenyewe 
 14.  kutilia maana  kutilia maanani   kutia maanani   kutia maana 
 15.  hutenga  huandama   huandamwa   hutengana 

 

Kuanzia nambari 16 hadi 30 jibu kulingana. na maagizo.

  1. Sentensi gani inayoonyesha kusudi la kufanyika kwa jambo?
    1. Nilienda nikamwona daktari. 
    2. Fanya mazoezi ulivyoambiwa.
    3. Nimekuja nikamwone mgonjwa. 
    4. Wanaimba kwa furaha.
  2. Ndege ni kwa 'kiota' kama vile kipepeo ni kwa ________________________________
    1. kiwavi
    2. utando
    3. kifukofuko
    4. kombe
  3. Sentensi 'Amechukua chake' ina maana gani?
    1. Amechukua anachomiliki, amechukua kinachomilikiwa na wengine
    2. Amechukua wanachomiliki, amechukua kinachomilikiwa na wengine
    3. Amechukua anachomiliki, amechukua kinachomilikiwa na mwingine
    4. Wamechukua wanachomiliki, wamechukua kinachomilikiwa na wengine
  4. Tambua jibu lililotumia 'm' kama mtendwa.
    1. mlionewa
    2. mlifagiliwa
    3. wampigia
    4. nilimchora
  5. Onyesha matumizi ya 'na' kwenye sentensi ifuatayo.
    Alikuwa na furaha alipojionea ng'ombe aliyenunuliwa na baba.
    1. umilikaji, pamoja na
    2. hali, mtendaji
    3. hali, pamoja na
    4. umilikaji, mtendaji
  6. Jibu gani lililo na kitenzi kutokana na nomino?
    1. imani - amini
    2. cheka - mcheshi
    3. tulia-mtulivu
    4. imani - mwaminifu
  7. Ulinganisho upi usio sahihi?
    1. pora- tembe
    2. jimbi - koo
    3. njeku - mori
    4. nzao - fahali
  8. Onyesha ukanusho wa;
    Wallowasili mapema wamekuwa uwanjani.
    1. Waliowasili mapema hawajawa uwanjani.
    2. Wasiowasili mapema hawajawa uwanjani.
    3. Wasiowasili mapema hawajakuwa uwanjani.
    4. Waliowasili mapema hawajakuwa uwanjani.
  9. Tambua aina za maneno yaliyopigiwa mistari.
    Wewe utaletewa hiyo mwakani
    1. kiwakilishi, kivumishi, kielezi
    2. kiwakilishi, kiwakilishi, nomino
    3. kiwakilishi, kiwakilishi, kielezi 
    4. kivumishi, kivumishi, kielezi
  10. Kifaa gani kitumikacho kupimia usawa wa unyookaji wa ukuta?
    1. pimamaji
    2. timazi
    3. fuawe
    4. bisibisi
  11. Sentensi ipi ambayo ni sahihi?
    1. Huyo mwenye anacheza ni mzuri.
    2. Miti yao yamepandwa yakanawiri.
    3. Mikunga mikubwa wamevuliwa.
    4. Matoto hayo yalitibiwa vizuri.
  12. Neno gani lililo na silabi ya sauti changamano?
    1. chama
    2. kamba
    3. maktaba
    4. fua
  13. Chagua umoja wa;
    Tutawasaidia wenye mafua.
    1. Nitawasaidia wenye mafua. 
    2. Nitamsaidia mwenye fua.
    3. Nitawasaidia mwenye mafua.
    4. Nitamsaidia mwenye mafua.
  14. Onyesha sentensi iliyo katika hali ya mazoea.
    1. Wachezao kwa bidii ndio wale.
    2. Hujafa hujaumbika.
    3. Huku ndiko kulikofyekwa.
    4. Hungenisaidia singefaulu. 
  15. Methali gani isiyokuwa na maana sawa na zingine?
    1. Mwanzo wa ngoma ni lele.
    2. Mwanzo wa mkeka chane mbili tu.
    3. Safari ndefu huanza kwa hatua moja.
    4. Mwanzo wa mvua mawingu.

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yanayofuata.

Kwa muda huo wote, sikujua kuwa angeweza kunifaa kwa lolote. Hata hivyo, siku moja nilielewa ukweli wa kauli kuwa jambo ulisolijua ni kama usiku wa giza. Siku hiyo, nilikuwa nimetulia tuli nje ya kijumba chetu cha msonge. Kijumba hicho kilijiinamia kwa majonzi na sikitiko ungedhani kuwa kingeanguka pu kama kidaka cha mnazi. Hakika, kuwa ndani na nje hakukuwa na tofauti yoyote. Wakati huo, nilikuwa hoi bin tiki kutokana na maradhi yaliyonifyonza nguvu na kuiguguna mifupa yangu daima dawamu. Aisee, ni wazi kama meno ya ngiri kuwa nilikuwa maskini wa nyama na tajiri wa mifupa. Nilikuwa dhaifu kama mkufu. Nzi angetua juu yangu, bi la shaka ningeanguka mithili ya mgomba uliokatwa.

Nilipokuwa papo hapo, nilifungua dafina ya ubongo wangu na kukumbuka nilivyoanza kuugua. Japc husemwa kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo, mimi nilishikilia kikiki kuwa mavi ya kale hayaachi kunuka, ashakum si matusi. Nilikumbuka siku niliyowasili hospitalini ili nimsaili tabibu chimbuko la madhila yaliyonisibu na kuniletea masaibu chungu nzima. Daktari alinipasulia mbarika kuwa niliugua maradhi ya figo. Afanalek! Nilipigwa na butwaa chakari, nikabaki kinywa achama kama spana. Ukweli usiopingika ni kuwa nilidhani kwamba masikio yangu yalikuwa yakinichezea shere. Ghafla kama mawingu, nilianza kukonda na kukondeana kama ng'onda. Nilitembea kwa takilifu na kupepesuka ungedhani kuwa ni mlevi. Maadamu tulikuwa maskini wa sina sinani, sikuwa na jingine ila kusubiri siku yangu ya kufumwa na mvi wa manaya. Chambilecho wataalam na watalamidhi wa lugha, sililo budi hubidi. Wengine husema, mkono usioweza kuukata ubusu.

Nilizinduliwa kutoka mawazoni na michakacho kwenye majani yaliyokuwa karibu nami kama pua na mdomo. Nilipoangalia kwa makini, nilishangaa mshangao wa shilingi kuzama na pantoni kuelea. Aliyesimama mbele yangu alikuwa Zumbukuku, kijana tuliyesoma naye katika darasa moja. Sawa na jina lake, alikuwa mbumbumbu asiyeweza kuongeza moja kwa moja akapata mbili. Yakini yakinifu, asingeweza kutofautisha mbu, umbu na mbung'o. Takribani kila mwanafunzi katika darasa letu alimdhalilisha na kumtweza ungedhani kuwa ni tambara bovu. Kila tulipofanya mtihani, Zumbukuku aliongoza kutokea nyuma. Yeye ndiye aliyeburura mgwisho katika kila somo. Katika hali hiyo ya kupigwa na bumbuwazi kenyekenye, Zumbukuku alinijuza kiini cha mjo wake. Alinifahamisha kuwa baada ya kutoniona shuleni kwa siku kadhaa, alikata shauri kuwauliza wanafunzi wengine. Aliamini ya wajuzi wa lugha kuwa kuuliza si ujinga, ni kutaka kujua.

Wakati huo wa jua kuaga miti, alikuja kunieleza kwa mapana na marefu kuwa alikuwa amesemezana na wavyele wake kuhusu hali yangu. Alikuwa amewarai kuhusu haja yao ya kunifaa. Aliwakumbusha kuwa ndugu ni kufaana si kufanana. Nilishangaa mithili ya mja aliyeona jua likiwaka usiku aliponifahamisha kuwa wazazi wake walikuwa wamekubali kugharimia matibabu yangu. Aidha, yeye alihiari kutolewa figo moja katika upasuaji huo. Je, nilikuwa katika ndoto ama huo ndio uliokuwa ukweli kamili? Iweje kijana niliyedhani kuwa asingemfaa yeyote kwa lolote wala chochote anipige jeki na kuniaviza kwa kiwango hicho? Hewaa! Umdhaniaye siye kumbe ndiye. Ni nani asiyejua kuwa dau la mnyonge huendeshwa na Mungu?

Siku ya kufanyiwa upasuaji ilipofika, nilikuwa na wasiwasi wa mwasi. Nilitetemeka temtem mithili ya kuku mwenye manyoya haba msimu wa kipupwe. Mtima wangu nao ulidunda kwa jazba nusura ukivunje kifua changu. Hata hivyo, nilipiga moyo konde nisikonde. Nilijitia moyo kwa kauli ya wenye lisani za uhenga kuwa maji ukiyavulia nguo ni lazima uyaoge. Nasaha za mwalimu wangu wa Kiswahili kuwa mja hatindi rehema ali hai duniani zilijiradidi katika masikio yangu wakati huo wote. Baada ya saa kadhaa katika harakati za kufanyiwa upasuaji, niliyafungua macho yangu. Zumbukuku naye alikuwa yu salama salimini. Hali ya kila mmoja wetu ilikuwa shwari bila shari.

  1. Aya ya kwanza inaonyesha kuwa mhusika;
    1. hakujua kuwa maisha yake yangefaa kwa lolote.
    2. aliketi nje ya nyumba baada ya kufanyiwa upasuaji.
    3. alikuwa amekonda sana kutokana na maradhi.
    4. alikuwa amechoka hoi bin tiki.
  2. Maneno 'nzi angetua juu yangu, bila shaka ningeanguka' yanaonyesha kuwa;
    1. alikuwa mdogo kushinda nzi
    2. alikuwa dhaifu
    3. alikuwa mwembamba
    4. alikuwa asiye na umuhimu
  3. Chagua maana ya neno 'nimsaili' jinsi lilivyotumika katika kifungu.
    1. nimwulize
    2. nimweleze
    3. nimwonyeshe
    4. nimchunguzie
  4. Kwa nini msimulizi alidhani kuwa masikio yake yalikuwa yakimchezea shere?
    1. ujumbe alioupata ulikuwa wa kushangaza
    2. mambo aliyoyaona yalikuwa yasiyoaminika
    3. tatizo la figo liliathiri masikio yake
    4. mambo aliyoyakumbuka yalimletea huzuni
  5. Jambo gani hasa lililofanya mhusika asitafute matibabu zaidi?
    1. kukosa matumaini ya kupona 
    2. kukosa pesa za matibabu
    3. kukosa tiba ya ugonjwa wake
    4. ukosefu wa madaktari wenye ujuzi
  6. Chagua jibu lisilo sahihi kulingana na kifungu.
    1. Zumbukuku alidharauliwa na kila mwanafunzi katika darasa lao.
    2. Zumbukuku ndiye aliyevuta mkia katika darasa lao katika mitihani yote.
    3. Zumbukuku alikuwa mwenye wema wa moyo.
    4. Wazazi wa Zumbukuku walikuwa matajiri.
  7. Kutibiwa kwa msemaji kulitokana na;
    1. utu aliotendewa na madaktari na wazazi Zumbukuku
    2. wema aliotendewa na Zumbukuku na madaktari
    3. utu aliotendewa na Zumbukuku na wazazi wake
    4. wema alioonyeshwa na wanafunzi na Zumbukuku
  8. Wasiwasi aliokuwa nao mwandishi katika aya ya mwisho ulitokana na nini?
    1. Kutetemeka kama kuku mwenye manyoya haba.
    2. Kudunda kwa moyo wake kifuani.
    3. Furaha ya kufaulu kwa upasuaji huo.
    4. Kutojua ikiwa upasuaji ungefaulu au la.
  9. Methali 'mja hatindi rehema ali hai duniani' inatoa ushauri gani ilivyotumika katika kifungu?
    1. Kufa moyo ni jambo la kawaida maishani.
    2. Mtu hafai kuwa na wasiwasi maishani.
    3. Mtu hafai kuwa mwoga katika maisha.
    4. Si vyema kupoteza matumaini maishani.
  10. Kichwa gani kinachoweza kutumika kuwa ujumbe wa kifungu hiki?
    1. Gae huwa chombo wakatiwe.
    2. Baniani mbaya kiatu chake dawa.
    3. Ndugu mui heri kuwa naye.
    4. Mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe.

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yanayofuata.

Ufisadi ni kati ya matatizo yanayolihangaisha taifa letu siku nenda siku rudi. Ufisadi wenyewe umekita mizizi sio tu nchini humu bali pia katika bara zima la Afrika. Umekuwa mithili ya dondandugu lililokataa katakata kusikia dawa. Sijui niseme kuwa juhudi zetu zimeshindwa kulimaliza au nieleze kuwa hakuna mwenye haja ya kulimaliza dudu hili. Kabla ya kuingia uongozini, utawasikia watu mbalimbali wakila yamini kuwa watakabiliana na ufisadi kwa jino na ukucha. Shani hutokea watu hao wanapochukua hatamu za uongozi. Watu walewale walioulaani ufisadi hutokea kuwa mafisadi wakubwa. Wao huwa mithili ya mja aliyeonjeshwa utamu wa asali. Baada ya kuichovya, akaamua kuishi palipo na mzinga ili kutimiza la wahenga kuwa mchovya asali hachovi mara moja. Kadri tunavyozidi kulibembeleza jitu hili, ndivyo taifa letu linavyozidi kuzama katika lindi la dhiki na mashaka. Nchi yetu haipigi hatua kimaendeleo. Inachechemea, inapepesuka isijulikane inakoelekea.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde, idara ya polisi ndiyo inayoongoza kwa ufisadi. Ufisadi katika idara hii umekithiri kiasi cha maafisa wa trafiki kupokezwa hongo mchana wa jua. Jambo la kuatua moyo ni kuwa maafisa hao wa trafiki wamechukulia hongo hiyo kama haki yao. Madereva na makondakta huwa hawana jingine isipokuwa kuwakabidhi hela hizo shingo upande. Kwa kuelewa kuwa mpiga ngumi ukuta huumiza mkonowe, huwa hawaoni haja ya kushindana na mwenye nguvu. Si walisema wajuao kusema kuwa mwenye nguvu mpishe!

Swali ambalo pengine unajiuliza ni je, madhara ya ufisadi ni gani? Madhara ya ufisadi katika taifa letu yarhekithiri. Ufisadi una madhara makubwa sana kwa uchumi wetu. Maendeleo hurudi nyuma kwa kuwa walio na uwezo wa kihela pekee ndio wanaopata huduma. Inapotokea kuwa watu wawili wanahitaji huduma kutoka katika afisi yoyote, yule aliye na pesa za kutoa hongo ndiye anayepewa huduma huku maskini akiwa ameshika tama kwa masikitiko makuu. Serikali nayo hukosa ushuru wa kutosha kwa kuwa walipa ushuru hukwepa kulipa ushuru kupitia ufisadi. Badala ya kulipa shilingi milioni moja kama ushuru, mtu hupendelea kutoa hongo ya shilingi laki mbili. Serikali hukosa pesa za kufanyia maendeleo na hivyo kuididimiza nchi katika lindi la ufukara. Wawekezaji nao hawawezi wakaanzisha miradi ya maendeleo katika nchi iliyoathirika na ufisadi. Katika nchi kama hiyo, mtu hulazimika kutoa hongo kwa kila jambo. Utoaji huo wa hongo hufanya wawekezaji kujiepusha na nchi kama hiyo.

Ufisadi nao huongeza kiwango cha maovu katika nchi. Wahalifu hufanya matendo yao maovu bila kujali iwapo watashikwa. Wanafahamu kuwa hata wakifumaniwa katika matendo yao ya uhalifu, watatoa hongo na kuachiliwa huru. Mara kwa mara, utaliona gari lililobeba abiria kupita kiasi likipita mbele ya polisi wa trafiki na kumpokeza polisi huyo shilingi hamsini au mia moja. Polisi hulifumbia jicho uovu huo na kuutuliza mfuko wake pesa za hongo. Ni mara ngapi umesikia kuwa mhalifu fulani amekuwa akitiwa mbaroni na kuachiliwa mara kwa mara? Ni kutokana na ufisadi ambapo kiwango cha wizi, ulanguzi wa mihadarati, uporaji na mauaji kimeongezeka.

Jambo jingine ni kuwa ufisadi umeongeza unyanyasaji katika jamii. Umewahi kusikia mtu anayejiona kuwa na uwezo mkubwa akimwuliza mwenzake "Utanipeleka wapi?". Huwa haina maana kuwa mwovu huyo hajatenda kosa. Huwa amemkosea mwenzake lakini hajali. Hajali kwa kuwa hata akishtakiwa, ana uhakika kuwa atatumia pesa zake kuwarambisha asali maafisa wa polisi na kuachiliwa. Ufisadi umejenga jamii ya mnyonge mnyongeni. Aghalabu tunaishi maisha ya 'mnyonge kupata ni mwenye nguvu kupenda". Wajane na mayatima wanapokonywa mali bila kujali. Maskini wanaojaribu kufungua biashara hukandamizwa na matajiri wanaotumia pesa zao ili wajiimarishe zaidi. Si shani kupata visa vya maskini wanaopokonywa mashamba na matajiri wenye tamaa.

Pendekezo langu ni kuwa serikali ijitolee mhanga kuhakikisha kuwa uovu huu umepotea. Maafisa wa kupambana na ufisadi wakae ange na kuchapa kazi usiku na mchana. Wahalifu wa ufisadi wanapotiwa mbaroni, kesi zao zifuatiliwe na kuhakikisha kuwa wameadhibiwa kwa njia inayofaa. Hili litakuwa funzo kwao na kwa wengine wenye nia kama zao. Raia nao wanafaa kukataa njia za mkato. Wafuate njia zinazofaa ili kupata kile wanachohitaji. Vita dhidi ya ufisadi ni vita vya jamii nzima. Vivyo hivyo, faida ya jamii isiyokuwa na ufisadi ni ya kila mmoja wetu.

  1. Kwa mujibu wa aya ya kwanza, ni kweli kuwa;
    1. ufisadi ni dondandugu lililokataa kusikia dawa nchini.
    2. Kenya ndiyo nchi katika bara la Afrika inayotatizwa na ufisadi.
    3. yapo matatizo mengi ambayo yanalisumbua bara la Afrika.
    4. Kenya inakumbwa na ufisadi pamoja na matatizo mengine.
  2. Chagua jibu lililo sahihi kulingana na aya ya pili.
    1. Madereva na makondakta hutoa hongo ili wasihangaishwe na maafisa wa trafiki.
    2. Maafisa wa trafiki hutoa hongo kwa kuwa mwenye nguvu mpishe.
    3. Madereva na makondakta wamechukulia hongo hiyo kama haki yao.
    4. Inadhaniwa kuwa idara ya polisi ndiyo inayoongoza kwa ufisadi.
  3. Maelezo yanayotolewa na kifungu yanaashiria kuwa ufisadi ukiisha katika jamii;
    1. kiwango cha ulanguzi wa mihadarati kitapungua.
    2. hakutakuwa na uovu katika jamii.
    3. maovu katika jamii yatakuwa machache.
    4. maafisa wa polisi hawatakuwa na kazi nyingi.
  4. Kauli 'watu walewale walioulaani ufisadi nhutokea kuwa mafisadi wakubwa' inaonyesha fani gani ya lugha?
    1. chuku 
    2. kinaya
    3. istiara 
    4. tasfida
  5. Nahau 'wakila yamini' ina maana gani jinsi ilivyotumika katika kifungu?
    1. wakiapa
    2. wakijaribu
    3. wakisema
    4. wakieleza
  6. Maneno 'ameshika tama' yanaonyesha kuwa;
    1. amezubaa.
    2. amehuzunika.
    3. ameudhika.
    4. amechanganyikiwa.
  7. Mtu anapomwuliza mwenzake kuwa "Utanipeleka wapi?" huwa;
    1. anadhani kuwa hakuna anakoweza kupelekwa.
    2. ana uhakika kuwa hatua itakayochukuliwa na mwenzake haitamwathiri.
    3. huwa ametoa hongo na hivyo hawezi akapelekwa popote.
    4. hana uhakika iwapo mwenzake anajua haki zake.
  8. Kwa mujibu wa aya ya tano, ufisadi una madhara hasa kwa;
    1. jamii kwa jumla
    2. serikali yetu
    3. wasiokuwa na uwezo
    4. wenye uwezo
  9. Mwandishi ana maana gani anapotumia maneno 'si shani'?
    1. si ajabu
    2. ni nadra
    3. ni muhali
    4. si kawaida
  10. Kwa mujibu wa maelezo katika aya ya mwisho, yawezekana kuwa;
    1. wahalifu wa ufisadi hawajawa wakitiwa mbaroni.
    2. hakuna maafisa wa kutosha wa  kupambana na ufisadi.
    3. wahalifu wa ufisadi huwa hawapati mafunzo ya kutosha.
    4. wapo raia wasiofuata njia zinazofaa wanapohitaji jambo fulani.

INSHA

Endeleza kisa kifuatacho. ukifanye cha kusisimua uwezavyo

Kila mmoja alikuwa amenyamaza kinya huku akisikiliza kwa makini. mara niliposikia jina langu likitajwa..................................................

MARKING SCHEME

  1. D
  2. D
  3. C
  4. A
  5. A
  6. B
  7. C
  8. B
  9. B
  10. D
  11. B
  12. A
  13. A
  14. B
  15. C
  16. C
  17. C
  18. C
  19. D
  20. B
  21. A
  22. D
  23. A
  24. C
  25. B
  26. D
  27. B
  28. D
  29. A
  30. D
  31. C
  32. B
  33. A
  34. A
  35. B
  36. A
  37. C
  38. D
  39. D
  40. A
  41. D
  42. A
  43. C
  44. B
  45. A
  46. B
  47. B
  48. C
  49. A
  50. D
Read 656 times Last modified on Monday, 26 June 2023 08:04