Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Maranda High School Mock Exams 2023

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki Riwaya, Tamthilia, Ushairi na Fasihi Simulizi.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Maswali yote ni sharti yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU A: HADITHI FUPI

D. W. Lutomia na Phibiana Muthama( Wah.): Mapambazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

  1. Lazima
    1. Clara Momanyi: Mapambazuko ya Machweo
      “Poko! Ukiumwa na nyuki haina haja ya kujitwika jukumu la kuharibu mizinga yote ya asali. Hujui faida ya nyuki ulimwenguni? Uliamua kurina asali ya nchi.”
      1. Eleza muktadha wa maneno haya. (alama 4)
      2. Tambua tamathali mbili za usemi zilizotumika katika dondoo hili. (alama 2)
      3. Onyesha matokeo ya kuharibu mizinga yote ya asali ukirejelea hadithi Mapambazuko ya Machweo. (alama 7)
    2. Rayya Timammy: Ahadi ni Deni
      Fafanua mikakati saba anayotumia Fadhumo kufanikisha azma yake maishani ukirejelea hadithi Ahadi ni Deni. (alama 7)

SEHEMU B: RIWAYA

Assumpta K. Matei: Chozi la heri

Jibu swali la 2 au 3

  1. “Mama na baba, nawashukuru sana kwa hisani yenu. Nimetembea kwingi katika umri wangu mdogo huu lakini sijapata kuwaona waja wenye utu kama nyinyi…”
    Huku ukirejelea riwaya Chozi la Heri, jadili mchango wa wazazi na walezi katika:
    1. Kujenga familia (alama 10)
    2. Kusambaratisha familia (alama 10)
  2. “Na wewe Mungu kakupa siha na uzima, unaweza ukajitegemea, una kisomo”
    1. Bainisha mazaji yanayojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)
    2. Eleza nafasi ya kisomo katika maisha ya Wahafidhina ukirejelea riwaya Chozi la Heri.    (alama 11)
    3. Fafanua umuhimu wa mandhari ya dondoo hili katika kujenga riwaya Chozi la Heri (alama 7)

SEHEMU C. TAMTHILIA
T. Arege: Bembea ya Maisha
Jibu swali la 4 au 5

  1. “Maji yangekuwa yamewafika Shingo basi wangeshindwa kuishi pamoja. Ndoa ni bembea. Kuna wakati itakuwa juu na wakati itakuwa chini. Hizo juu-chini chini-juu ndizo utamu wake. Ni kama maisha kwa jumla. Yana pandashuka ndiyo lakini pandashuka hizo ndizo hutupa kuridhika hatimaye tunapozishinda. Maisha yangekuwaje bila hali kubadilika?”
    1. Eleza vipengele sita vya kimtindo vinavyojitokeza katika dondoo hili. (alama 6)
    2. Fafanua umuhimu wa mazungumzo kati ya Luka, Beni na Yona katika kujenga tamthilia Bembea ya Maisha. (alama 14)
  2. "Bembea inapolika na kukatika haiwi mwisho wa michezo. Huungwa na mchezo kuanza tena."
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa kutolea mifano mwafaka katika tamthilia Bembea ya Maisha. (alama 10)
    3. Tathmini mchango wa msemaji wa maneno haya katika kufanikisha ploti ya tamthilia Bembea ya Maisha. (alama 6)

SEHEMU D: USHAIRI

Jibu swali la 6 au 7

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

    Unganambia ni mui, katu siuwati wema,
    Wewe ndiwe wangu bui, nilousiwa na mama,
    Neno kwamba siujui, ni kupotosha heshima,
    Siati kutenda wema, kaandama uadui.

    Wema nambiwa ni ndia, kwayo maisha salama,
    Hayo niliyasikia, wao wahenga wa zama
    Penye wema tajitia, nipate taadhima,
    Siati kutenda wema, japo munganinunia.

    Na iwe kupawa mali, ya kuhadaa mtima,
    Niandame ufedhuli, nitengane nao wema
    Hilo sitokubali, hata waja wangasema.
    Siati kutenda wema, ujapokuwa ni ghali.

    Sitomcha kabaila, nganiteuza nache wema,
    Munganitia na jela, kisa imefanza huruma,
    Haragwe lenu talila, pamoja na yenu sima,
    Siati kutenda wema, japo tagoni talala.

    Haufi mungaufisha, au hamipo karima
    Mola atauhusha, weleleapo kuzama,
    Mimi ni huo maisha, hadi siku ya kiama,
    Siati kutenda wema, nganitia mshawasha.

    Wema ingawa mchungu, tajaribu kutotema,
    Tautenda nende zangu, niache wanaosema,
    Malipo yangu kwa Mungu, hayo yenu si lazima
    Siati kutenda wema, kigharimu roho yangu.
    1. Nafsineni katika shairi hili ana msimamo thabiti. Thibitisha kwa hoja sita. (alama 6)
    2. Taja na ueleze bahari ya shairi hili ukizingatia vigezo vifuatavyo: (alama 4)
      1. Vina
      2. Vipande
      3. Idadi ya mishororo
      4. Mshororo wa mwisho
    3. Fafanua jinsi mtunzi wa shairi hili alivyotumia uhuru wake. (alama 3)
    4. Eleza umuhimu wa aina za takriri zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 4)
    5. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari. (alama 3)
  2. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

    Wewe,
    Utazame mlolongo wa,
    Waja wanaoshika njia giza likiwapo;
    Unaofuata pembe za barabara zisokuwepo,
    Kwenda kuisaka auni,
    Kuitafuta kazi inayowala chenga.

    Itazame migongo ya wachapa kazi,
    Watokwao na jasho kapakapa na,
    Wanaotafunwa uhai na jua liso huruma:
        Wakiinua vyuma na magunia,
        Wakiinua makontena,
        Wakichubuka mashambani,
        Wakiumia viwandani,
        Wakiteseka makazini,
    Halafu,
    Uangalie ule ujira wa kijungu meko,
         mshahara usokifu haja,
         nguo zisizositiri miili dhaifu,
         kilio chao kisichokuwa na machozi,

    Na
    Ujiangalie
    Mwenyewe:
           Mwili wako unaomeremeta ujana na ufanisi,
           Gari lako la kifahari lililozibwa vioo,
           Jumba lako la kujishasha kama uwanja mdogo,
           Malaki ya pesa unayomiliki
    Ujiitapo mwajiri kwa raha, hunusi usaha wa hali yao?
    1. Linganua hali mbili zinazosawiriwa katika shairi hili. (alama 5)
    2. Chambua muundo wa shairi hili. (alama 4)
    3. Tambua toni inayojitokeza katika shairi hili (alama 2)
    4. Bainisha jinsi mshairi alivyotumia vipengele vifuatavyo katika shairi hili:
      1. Aina za taswira (alama 2)
      2. Usambamba (alama 3)
    5. Tambulisha hulka za nafsinenwa katika shairi hili. (alama 2)
    6. Toa mifano na uonyeshe umuhimu wa mishata katika shairi hili. (alama 2)

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

  1. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali

    Hapo zamani za kale Nyani alikuwa rafiki wa kufa kuzikana na Bafe. “Mjukuu wangu sijui kama umewahi kuwazia urafiki wa aina hii; ule wa mmoja wao akijikwaa dole anayeuhisi uchungu wenyewe ni mwenzake.”

    Wanyama hawa waliishi pamoja kwa amani na upendo. Walisaidiana wakati wa dhiki na wakati wa furaha. Walisaidiana na wakati wa masika na wakati wa kiangazi. La Nyani lilikuwa la Bafe na la Bafe lilikuwa la Nyani. Ulifika wakati ambapo wanyama wote walikumbwa na ngambi ya chakula kutokana na kiangazi kilichoselelea nchini mwao kwa takribani miezi minane.

    “Njaa hii itatusafirisha jongomeo,” akasema Nyani akiwa ameshika tama.

    “Usiwe na wasiwasi ndugu!” akasema Bafe, “Nina hakika kwamba Mwenyezi Mungu hatatuacha tuangamie pamoja na aila zetu.”

    Kutokana na uchechefu huu wa chakula, Nyani na Bafe pamoja na vikembe wao walikula hadi chakula kile walichokuwa wameweka akiba na kukimaliza. Sasa kuiona kesho ilibaki mikononi mwa Mungu alivyokuwa ametakadamu kusema Bafe kwa maana wanyama walianza kupukutika mmoja baada ya mwingine kama majani makavu msimu wa kiangazi. Msitu wote ulijaa nyamafu.

    Nyani alipoona kuwa huenda akakata kamba aliamua kula mayai ya sahibuye Bafe wakati alipokuwa ameenda kuhemera ili angalau apate chakula cha kupunguza mng’ato wa njaa. Bafe aliporudi, Nyani alimpiga mafamba kwamba kuchakuro aliyavamia mayai yake na kuyala lakini Bafe hakuridishwa na jibu hili. Aliona hila katika jibu la Nyani na kutaka kubaini ukweli kwani ukweli unapodhihiri uongo hujitenga.

    Nyani alipomwona Bafe akimkaribia ili kukinusa kinywa chake, alianza kutoroka bila kukimbizwa na yeyote. Kutoroka kwake kulimthibitishia Bafe kuwa Nyani ndiye aliyekula mayai yake, hivyo akaamua kumfuata unyounyo akiwa amepandwa na kiruu mithili ya Mbogo aliyejeruhiwa usasini. Nyani alikimbia na kujibanza kwenye jiti aina ya bobo liliokuwa karibu na jito lililojaa Ngwena na Viboko.

    Bafe aliutumia uwezo wake wa kunusa na kugundua alikojificha Nyani. Nyani alipomwona Bafe akiukwea mti, alishikwa na mtapo na kuanza kutetemeka kama dondoo aliyevamiwa na siafu. Alitamani kuchupa na kupiga kachombe kwenye yale maji male ili atorokee ng’ambo ya pili lakini akagundua kwamba Mamba walikuwa wamekenua meno yao wakimsubiri. Alipotaka kuchupia mti wa msonobari uliokuwa karibu naye, pia chui watatu walikuwa wamelalama kwenye matawi ya mti huo wakimsubiri mithili ya golikipa anayeusubiri mpira ili audake. Alipotamani kushuka, aligundua kwamba naye Bafe alikuwa akiupanda mti kwa kasi akiwa amefunua kinywa tayari kummeza. Je, ungekuwa Nyani, ungefanya nini?
    1. Huku ukitolea ithibati, ainisha ngano hii:
      1. Kimaudhui (alama 2)
      2. Uhusika (alama 2)
    2. Tambua na ufafanue umuhimu wa mbinu za utambaji zilizotumika kufanikisha uwasilishaji wa ngano hii. (alama 6)
    3. Eleza manufaa ya kutumia mbinu ya mahojiano kukusanya data ya fasihi simulizi. (alama 5)
    4. Fafanua njia tano ambazo kwazo jamii ya kisasa inaendeleza utanzu wa hadithi. (alama 5)

MARKING SCHEME

  1. Lazima
    1. Mapambazuko ya Machweo-Clara Momanyi
      "Poko! Ukiumwa na nyuki haina haja ya kujitwika jukumu la kuharibu mizinga yote ya asali. Hujui faida ya nyuki ulimwenguni? Uliamua kurina asali ya nchi."
      1. Eleza muktadha wa maneno haya.  (alama 4)
        • Maneno ya Makucha kwa Makutwa mgodini baada ya MAkutwa kukamatwa kwa kosa kufuja raslimali ya nchi.
          4 x 1=4
      2. Tambua tamathali tatu za usemi zilizotumika katika dondoo hili. (alama 2)
        • Taswira fiche. Ukiumwa na nyuki-kuajibishwa kwa kuhujumu uchumi wa nchi.
        • Dhihaka. kujitwika jukumu la kuharibu mizinga yote ya asali.
        • Jazanda. Uliamua kurina asali ya nchi -kuhujumu uchumi wa nchi    2x1=2
      3. Onyesha matokeo ya kuharibu mizinga yote ya asali ukirejelea hadithi Mapambazuko ya Machweo.    (alama 7)
        • Makutwa anafanya biashara ya kimagendo ya kuchimba vito katika mgodi kisiri. Hii ni raslimali ya serikali ambayo mtu anafaa kupata leseni ya kuchimba
        • Ukoloni Mamboleo. Mzee Makutwa anawasomba ijana kwenda kuwafanyisha kazi ya kusaka vito vya thamani katika mgodi wake. Wanafanya kazi hii katika mazingira mabovu na kufungiwa mle ndani, wasiwe na nafasi ya kutokea.
        • Makutwa analipoka taifa nguzo yake muhimu kwa kuwachukua vijana mabarobaro na kwenda kuwatumikisha katika mgodi wake. Vijana hawa wanafaa kuwa wakiendesha shughuli nyingine muhimu za kujenga jamii.
        • Ajira ya watoto. Vijana kadhaa, ikiwemo watoto wadogo wanafanya kazi ya kudondoa vijiwe vidogo vidogo vinavyong'aa. Wanasimamiwa na wanyapara wanaowaamrisha kwa sauti za kutisha.
        • Mazingira mabovu ya utendakazi. Vijana mgodini wanakumbwa na hali ngumu ya
          kimaisha, kwani huko wanakoishi hakuna hali nzuri. Hewa si safi na kazi wafanyazo ni za sulubu.
        • Ukosefu wa ajira. Sai na Dai pia wanawakilisha hali ya vijana ambao baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu, hawajapata kazi wala hawana matuamini. Wanashinda kuzurura mitaani.
        • Wafanyakazi kutimuliwa bila fidia. Mzee Makucha anafanya kazi na shirika la reli ambalo linamtimua kwa ajili ya kupunguza idadi ya wafanyakazi wake. Baadaye linasambaratika, hivyo anakosa marupurupu yake.
        • Umaskini. Mzee Makucha anaanguka kwenye lindi la umaskini baada ya kuachishwa kazi katika shirika la reli bila marupurupu, kwani shirika hilo linasambaratika pia.
        • Kazi duni. Makucha analazimika kuchuuza vitafunio kando ya barabara kujipatia riziki. Mkewe naye anauza kaimati na vitumbua kwenye veranda ya nyumba yao.
        • Kukimbilia ndoa. Riziki, anawatoroka wazaziwe na kuolewa na Mhindi ili kuepuka urumo.    7x1=7
    2. Ahadi ni Deni-Rayya Timammy
      Eleza mikakati sita anayotumia Fadhumo kufanikisha azma yake maishani. (alama 6)
      • Elimu. Fadhumo anatoa ahadi kwa babake kuwa atasoma kwa bidii kwa ajili ya kuboresha maisha yake mwenyewe na ya familia.
      • Fadhumo anatimiza ahadi ya moyo wake. Anarejea masomoni baada ya miaka sita kutimiza ahadi yake kwa babake.
      • Kushikilia utu uadilifu. Jamaa wa babake anapomtaka awe kimada wake ili aweze kumlipia karo anakataa. Hawezi kukubali kuuza utu wake. Anahiari kuolewa na Adan badala ya kuwa kimada.
      • Ndoa. Fadhumo anakubali kuolewa na Adan ili awakidhi ndugu zake.
      • Kuweka mkataba/Maagano, Fadhumo na Adan wanaweka mwafaka baina yao kabla ya kuona. Adan analazimika kutimiza ahadi yake kwa Fadhumo. Anawakimu nduguze na kuwapeleka shule baada ya kumwoa Fadhumo. Fadhumo anapopata hamu ya kuendelea na elimu, Adan yuko tayari kumsaidia kwa kila hali.
      • Bidii maishani, Fadhumo anaanza cimu baada ya miaka sita. Licha ya changamoto tele anazopitia, anatia bidii. Anapata alama ya C-.
      • Taaluma na ajira. Anajiunga na koleji ya kufunza watoto wadogo na kujipatia astashahada inayomwezesha kupata kazi ya kufunza kwenye shule moja. Hatimaye anajiunga na masomo ya stashahada.
      • Maamuzi ya busara. Jamaa wa babake anapomtaka awe kimada wake ili aweze kumlipia karo anakataa. Hawezi kukubali kuuza utu wake. Anahiari kuolewa na Adan badala ya kuwa kimada.
      • Ukakamavu. Anajiunga na shule ya upili maarufu kaunti nzima. Hata baada ya kuolewa, anarejea masomoni na kujipa vyeti vya astashahada na stashahada.
      • Msimamo imara. Anaamua kurudi masomoni hata baada ya miaka sita nje. Anakataa katakata rai ya kuwa kimada kwa jamaa anayemtaka kukidhi mahitaji ya nduguze.
      • Uwajibikaji. Anaacha masomo kuwakidhi wadogo zake wazazi wao wanapofariki. Anakidhi majukumu anayotakiwa katika ndoa.
      • Mapenzi ya dhati. Anampenda mumewe Adan na anamkidhia mahitaji yote kama mumewe. Anamwambia kuwa yuko tayari kumpa watoto zaidi. Hili linafanya mumewe kutimiza ahadi yake. Za kwanzax 1=7
  2. "Mama na baba, nawashukuru sana kwa hisani yenu. Nimetembea kwingi katika umri wangu mdogo huu lakini sijapata kuwaona waja wenye utu kama nyinyi..."
    Huku ukirejelea riwaya Chozi la Heri, jadili mchango wa wazazi na walezi katika:
    1. Kujenga familia   (alama 10)
      • Familia ya Ridhaa na Terry inayowalea watoto wao vizuri na kuwapa elimu.
      • Katika ndoa ya Mwangeka na Apondi wanawalea watoto wao vizuri kwa kuwapa elimu na mashauri. Dick na Umu wanashukuru kwa malezi yao.
      • Apondi anamshukuru Umu kwa malezi mazuri ya wadogo wake aghalabu anapokuwa mbali nao. Kutuliza hasira za Sophie.
      • Mwangemi na Neema walimpanga Mwaliko ambaye wamemlea vyema kwa kumpa elimu na kusoma hadi kitengo cha uzamili katika isimu na lugha.
      • Kangata alimuoa Ndarine na kubarikiwa na; Lunga Kiriri, Lucia Kiriri na Akelo Kiriri. Waliwalea vyema kwani waliweza kuwapa elimu iliyowasaidia.
      • Familia ya Mzee Mwimo Msubili inawadhibu Mwangemi na Mwangeka ili kuwarekebisha kitabia.
      • Mamake Kairu anamwendeleza kielimu.
      • Mamake Ridhaa anazungumza na mwalimu, Ridhaa anapobaguliwa shuleni hali iliyompelekea kupaa katika anga za elimu.
      • Maelekezo ya Ridhaa kwa Mwangeka kuhusu kuingia katika ndoa tena kunamfanya kuridhia ndoa tena na kumwoa Apondi.
      • Dick kupata wazazi Mwangeka ana Apondi waliweza kumpa ushauri uliomsaidia kibiashara.
      • Songoa anaclimishwa na Kiriri na hata kughuria Ngambo na kuwekeza huko.
      • Mashirika ya kidini yanaungana pamoja kuwasaidia wakimbizi kwa kuwapa chakula katika kambi mbalimbali.
      • Mumewe Selume kushughulikia mahitaji ya mwanawe baada ya Selume kuondoka. Lunga kuwalea wanawe baada ya Naomi kuondoka.
      • Neema kumtunza mpwake Cynthia baada ya wazazi wake kufariki kutokana na maradhi fulani.
      • Shule ya Tangamano iliwasaidia wanafunzi kama vile mwalimu Dhahabu anamwambia Umu arudi darasani anapoona amekumbwa na mawazo.
      • Mamake Kairu ni maskini kwamba kulipa karo ni jambo linalomtatiza ila anaongea na mwalimu mkuu wa Shule ya Tangamano kumruhusu mtoto wake asome akilipa kidogo kidogo.
      • Mwalimu Dhahabu anajishughulisha kuwatafutia mayatima na wanafunzi wake wasiokuwa na familia wazazi wa kuwapanga - Umu.
      • Nyanyake Chandachema
    2. Kusambaratisha familia  (zozote 10 x 1-10) (alama 10)
      • Kutoroka - Naomi anawahini wanawe malezi anapomtoroka mumewe kwa kutaka kukimbia umaskini wanaishia kulelewa na kijakazi Sauna/ Subira/Mama yake Pete/ Rehema
      • Wanaendeleza ndoa za mapema - Mama ya Pete anashirikiana na wajomba wake kumwoza mapema licha ya rai ya bibi/nyanya yake kwamba wamwache aendelee na masomo.
      • Wanaendeleza ulanguzi wa binadamu - Sauna anawateka nyara Dick na Mwaliko na kuwatenganisha na Umu.
      • Wanaendeleza ubaguzi Mavyaa ya Subira anambagua kwa kusema Subira ni msichana wa Bamwezi; anamwita mwizi na kumfanya Subira aondoke.
      • Wanachangia kuvunjika kwa ndoa. Mayyaa ya Subira anamsimanga Subira hadi Subira anaondoka/Wazazi wake Rehema wanakataa aolowe na Fumba
      • Wanaendeleza mauaji - Subira,mkewe Kaizari anapatikana amejifia chumbani akiwa na chupa ya kinywaji kikali. Wanawe wanakosa malezi yake.
      • Kuwanyima waume zao ushirika wa watoto wao - Mkewe Kiriri anahamia ng'ambo na watoto.
      • Wazazi wake Zohali hawamsaidii binti yao baada ya kupachikwa mimba na kufukuzwa shuleni hawampi ushauri-nasaha wa kumsadia kuikabili hali yake mpya.
      • Amize Lucia wanawakandamiza watoto wa kike, kwa mfano,wanamkataza Kangata kumwelimisha mwanawe Lucia kwa sababu ya kuwa msichana
      • Wanasababisha dhiki za kisaikolojia - Mkewe Kiriri anamwachia Kiriri upweke na kuenda ughaibuni/ Naomi anamwacha Lunga na kusababisha kuugua kwake kisha anafariki/Kaizari.
      • Wanawanyima waume zao haki ya unyumba - Naomi anamwacha Lunga/Annette anamtoroka Kiriri.
      • Kuwanyamazisha wanao/kuwanyima haki ya kusema- k.m Mamake Sauna anamwambia Sauna asimpake Maya tope. Baadaye Sauna anatoroka kwao.
      • Baba Kairu anamtelekeza Kairu kwa kumwacha kulelewa katika maisha ya kimaskini kwa sababu mamake hakujiweza kiuchumi; hii ni kwa sababu alimzaa nje ya ndoa
      • Baba Zohali na mama Zohali wanamdhalilisha na kumsimanga Zohali na kumfanya kijakazi wao.Zohali anaishia kutoroka nyumbani.
      • Fumba anamtelekeza mwanawe Chandachema kwa mamake bila kumpa pesa za matunzo yake. Inawabidi dadaze Fumba kumtumia mama yao pesa za kumtunza Chandachema,
      • Fumba anaoa mke mwingine na kuhamia ughaibuni na kumwacha Chandachema akiteseka katika hali ya umaskini.
      • Babake Kipanga anamkana Kipanga kuwa mwanawe wa kuzaa, hali inayomchochea kutoroka nyumbani na kuanza kunywa pombe, hivyo kuishia kuacha shule.
      • Babake Pete anamkataa Pete kuwa mwanawe akidai kwamba hawafanani. Pete anaishia kulelewa na nyanyake.
      • Wazazi wa Pete wanamkatizia masomo kwa kumwoza kwa Mzee Fungo ili wapate mahari.
      • Mzee Maya anambaka mwanawe wa kambo Sauna na kumpachika mimba.
      • Wazazi wa Mwangemi na Mwangeka wanawahini mwangemi na Mwangeka chakula kama njia ya kuwaadhibu kwa kumuiga babu yao, badala yao ya kuwazungumzia ili kuwaonya dhidi ya kitendo hicho.
      • Mzee Fungo anamfurusha Pete na mwanawe bila kuwazia hatima ya mtoto huyo kwa maana Pete alikuwa angali kikembe katika malezi,
      • Wazazi wengine wanapalilia ukabila miongoni mwa wanao kwa mfano, Lucia anakatazwa na amize kuolewa katika ukoo wa Waombwe
      • Satua anamdhulumu Chandachema akielewa kuwa hana mlezi baada ya kifo cha nyanyake aliyekuwa mleziwe Chandachema anapohamia kwake, anaanza kulalamikia matumizi ya sukari na sabuni hiyo kumfanya Chandachema kumtoroka.
      • Tenge anafanya uasherati/uzinifu machoni pa wanawe, hivyo kuwaachia dhiki za kisaikolojia.
      • Pete anakunywa dawa ya kuulia panya ili afe bila kuwazia maisha ya wanawe wawili wakiwa hai.
      • Zohali anakiuka haki ya mwanawe Nasibu kwa kukataa kumjulisha kuwa ana babu na   nyanya.    (zozote 10 x 1-10)
  3. "Na wewe Mungu kakupa siha na uzima, unaweza ukajitegemea, una kisomo" (alama 2)
    1. Eleza mazaji yanayojitokeza katika dondoo hili. ;
      Matumaini - Sclume anapewa ushauri kutumia kisomo chake kujiendeleza swala linalozua matumaini kwa msomaji. (1x2-2)
    2. Eleza nafasi ya kisomo katika maisha ya Wahafidhina ukirejelea riwaya Chozi la Heri    (alama 11)
      • Ni njia ya kutoa ushauri nasaha/ uelekezaji - Mabinti Umu, Zohali, Mwanaheri, Kairu na Chandachema wanaamua kuufuata ushauri wa Mwalimu Dhahabu wa kuandama elimu kama njia ya kuwawezesha kuleta mabadiliko katika jamii na njia ya kujijengea mustakabali mzuri maishani.
      • Elimu inamfanya mtu kupata mali na ukwasi na kuishi kwa furaha. Ridhaa anazamia masomo kwa bidii hadi anafuzu kuwa daktari wa upasuaji. Kupitia taaluma hii anafanikiwa kuwa na maisha mazuri.
      • Ni njia ya kutunza mazingira - Lunga Kiriri-Kangata alipokuwa shuleni alikuwa amirijeshi wa uhifadhi wa mazingira. Alikuwa mwasisi wa Chama cha Watunza Mazingira Wasio na Mipaka.
      • Kupitia elimu mtu anaweza kujikwamua kutoka kwa masaibu anayoyapitia. Zohali, Kairu, Chandachema, Mwanaheri na Umu wanaamua kutilia maanani ushauri wa Mwalimu Dhahabu wa kuandama elimu kama njia ya kujinyanyua maishani.
      • Elimu inasaidia kudumisha amani. Mwangeka alisoma akahitimu katika uhandisi na kujiunga na jeshi. Taaluma yake ndiyo iliyompelekea kwenda kudumisha amani Mashariki ya Kati. Elimu na ujuzi aliokuwa nao ulimsaidia kujijengea jumba la kifahari.
      • Elimu inawasaidia vijana wa mtaani kujiokoa kutokana na kinamasi cha uvutaji gundi na matumizi ya mihadarati. Serikali inajenga makao ambapo vijana hawa wanasaidiwa na kupewa mbinu za kukabiliana na maisha. Hazina alipelekwa shuleni akasoma, akabahatika kujifunza upishi na huduma za hotelini na sasa anafanya kazi kama mhudumu katika hoteli. Sasa maisha yake yanachukua mkondo mpya.
      • Elimu inakuza kilimo. Lunga alisomea kilimo. Anatumia ujuzi wake kustawisha kilimo. Awali alikuwa ameajiriwa kama afisa wa kilimo nyanjani. Alikuwa akiwaelimisha raia kuhusu mbinu bora za kilimo kama vile watu wasilime karibu na mito, watu wachimbe mitaro kuzuia mmomonyoko wa udongo na watu wapande miti inayostahimili ukame. Lunga alikuja kuwa mkulima stadi na kutononoka si haba.
      • Masomo yanamwezesha mtu kuweza kutoa huduma kwa jamii. Selume na Meko walisomea uuguzi na kuhitimu. Wanawahudumia wagonjwa kwenye hospitali ya  Mwanzo Mpya. Ridhaa kupitia elimu na ujuzi wa udaktari aliweza kuwahudumia watu wengi.
      • Elimu inamwezesha mtu kuacha uhalifu. Dick ana kisomo katika nyanja ya teknolojia na mawasiliano. Anaamua kuacha biashara ya ulanguzi wa mihadarati na kuingilia biashara ya kuuza vifaa vya simu.
      • Elimu inakuza utangamano. Zohali, Kairu, Chandachema na Umu wanakutana shuleni na wanasimuliana masaibu yao na kuliwazana na hivyo kudumisha umoja baina yao.
      • Kupitia elimu mtu anapata kuzinduka. Tila anapata kujua changamoto zinazowakumba Waafrika. Elimu inamfanya kujua mengi kuhusiana na siasa, ukoloni na sheria. Anaazimia kuwa jaji ili kutetea haki za wanyonge.
      • Elimu inamwezesha mtu kupata ajira. Songoa anasomea ughaibuni, anafuzu na kuajiriwa huko. Kaizari alikuwa msomi. Alipotoka katika Msitu wa Mamba anapata kazi ya Afisa wa Matibabu. Selume alikuwa na ujuzi wa uuguzi. Awali alifanya kazi katika hosptali ya umma. Baada ya kutoka Msitu wa Mamba alifanya kazi kama Muuguzi Mkuu wa kituo cha afya cha Mwanzo Mpya. Neema, mkewe Mwangemi, ameelimika. Anafanya kazi katika Hazina ya Kitaifa. Rachel Apondi ni msomi aliyefanya kazi katika idara ya vijana.
      • Humwezesha mtu kuchangia katika maendeleo ya kitaifa. Kuzinduka kwa Ridhaa kunamfanya alibadilishe eneo la Msitu wa Heri ambalo awali lilikuwa limepewa lakabu ya Kalahari.
      • Elimu inamfanya mtu aweze kujitegemea. Hazina anachukuliwa na kuelimishwa na serikali hadi anafuzu kuwa mhudumu wa hoteli. Maisha yake yanakuwa mazuri sasa.
      • Kupitia elimu mipaka ya kikabila imeweza kuvunjwa. Wanafunzi wenzake Ridhaa walimtenga hapo awali lakini baada ya mwalimu kuwaelimisha kuhusu umoja, kulikuwa na utulivu na hapo ndipo maisha ya heri yakamjia Ridhaa.
      • Walimu husaidia kuwakutanisha watu waliokuwa wamepoteleana. Umu anakutana na ndugu yake Dick alipokuwa akitaka kuabiri ndege kuelekea ughaibuni kwa masomo zaidi.
      • Elimu huwakutanisha watu na wahisani wao. Umu alipokuwa akisoma katika shule ya Tangamano, aliweza kupata wazazi wa kupanga Apondi na Mwangeka ambao walimfanya aishi vizuri na akaja akawa mtu wa maana.
      • Kupitia elimu ubaguzi wa kijinsia uansitishwa. Tila anamwambia babake yale ambayo alifunzwa na mwalimu kuwa kiongozi anaweza kuwa mwanamume au mwanamke bora tu awajibike. (zozote 11 x1 = 11)
    3. Fafanua umuhimu wa mandhari ya dondoo hili katika kujenga riwaya Chozi la Heri.  (alama 7)
      • Kuibua maudhui mbalimbali k.m maudhui ya ukatili - jinsi Lime na Mwanaheri walivyabakwa.
      • Kuchimuza tabia za wahusika - k.m utu wa jiraniye Tulia; tabia za mwanzi kama katili kwani tunaambiwa Selume kuishi na wakimbizi kuliko kwenye kasri la dhuluma za mumewe.
      • Kuonyesha wakati wa kutukia kwa matukio- tandabelua baada ya uchaguzi
      • Huchangia kuibua toni na hali ya kijumla - mandhari haya yanaibua toni ya uchungu na masikitiko.
      • Huibua dhamira ya mwandishi mandhari ya kambi ya wakimbizi yanaibua dhiki za wakimbizi baada ya ghasia za baada ya uchaguzi.
      • Hutambulisha wahusika - tunabainishiwa wahusika kama Subira, Lime, Mwanaheri, Ridhaa, nk..
      • Kudokeza migogoro - baina ya wafuasi wa Bi.Mwekevu na mpinzani wake mkuu.
      • Husaidia kulinganua hali za matabaka- k.m. aliyekuwa waziri, familia ya Bw. Kute
      • Kuonyesha mahali pa tukio k.m Lime na Mwanaheri wanabakiwa nyumbani kwao
      • Huibua taharuki - Kaizari akisimulia jinsi gari lao lilivyoishiwa na petroli taharuki inajengwa.
      • Kuendeleza ploti k.m Wakimbizi wanapofurushwa kutoka makwao na kuanza maisha upya katika kambi ya wakimbizi / Msitu wa Mamba.    (zozote 7x1-7)
  4.  
    1. Eleza vipengele sita vya kimtindo alivyotumia msemaji kufanikisha uwasilishaji wa ujumbe.      (alama 6)
      • Sitiari-Ndoa ni bembea. Swali ya balagha- 
      • Msemo-Maji yangekuwa yamewafika Shingo
      • Tashhisi - Maji yangekuwa yamewafika Shingo
      • Jazanda - Ndoa ni bembea.
      • Kinaya
      • Tanakuzi - Kuna wakati itakuwa juu na wakati itakuwa chini, Juu chini, chini juu
      • Takriri - Hizo juu-chini chini-juu ndizo utamu wake.
      • Taswira - Hizo juu-chini chini-juu ndizo utamu wake
      • Ukweli kinzani - Ni kama maisha kwa jumla. Yana pandashuka ndiyo lakini pandashuka hizo ndizo hutupa kuridhika hatimaye tunapozishinda.
      • Balagha - Maisha yangekuwaje bila hali kubadilika?RR.
      • Tashbihi - kama.      (za kwanza 6x1 = 6)
    2. Fafanua umuhimu wa mazungumzo kati ya Luka, Beni na Yona katika kujenga tamthilia ya "Bembea ya Maisha" (alama 14)
      • Yanaonyesha sifa ya Luka kuwa ni mkarimu -anawakaribisha wenzake kwake nyumbani kwa chakula cha mchana na kinywaji..
      • Kuonyesha mila na utamadumi - Luka anadokeza kuwa kitendo cha kula pamoja kwa wazee kilikuwa kinafanywa na wazee wao kwani mavuno ya kwanza huonjwa na wazee na kutoa baraka. (uk. 58) / mabadiliko
      • Yanachimuza ukengeushi -Beni anasema kuwa tatizo la watu siku hizi ni kuzitupa mila zao kabisa. (uk.58) Wajukuu wa Yona hawafahamu lugha yao ya asili. (uk-59)
      • Yanadhihirisha mchango wa dini - Yona anaeleza dini,imechangia watu kuona mila kuwa chafu. (uk.58)
      • Yanaonyesha mabadiliko katika malezi - Yona anaambia wazee wenzake kwa malezi cule mjini yameachiwa kina yaya. (uk.59)
      • Yanaonyesha jinsi mila na tamaduni zilikuwa kandamizi kwani hazikuruhusu mtoto wa kike kuenda shule au kuridhi kitu - kulingana na Luka.(u.k 60) ndoa
      • Yanadhihirisha jinsi hao kina Luka walivyomshinikiza Yona kuoa mke mwingine apate mtoto wa kiume.(u.k 60)
      • Yanadhihirisha sifa za Beni jinsi ana wivu kwa watoto wa Yona kwani hataki Luka awataje katika mazungumzo yake.
      • Yanachimuza ufanisi wa watoto wa Yona - Luka anasema walikuwa nyota ya jaha. Neema anarudi kijijini akiwa na gari.
      • Yanaonyesha thamani ya mtoto wa kike ilivyopanda na nafasi yake kupanuka kwani zamani walikuwa wakiwategemea waume zao laikini sasa hali ni tofauti(u.k.60)
      • Yanaonyesha maudhui ya uhafidhina - Luka anamuona Neema kama si wao tena baada ya kuolewa.
      • Yanachimuza hekima ya Luka - Luka anamuuliza Beni kuwa lipi muhimu kati ya tiba au mtu kuja kumpikia mwenzake? (uk.61)
      • Yanaonyesha sifa za Yona hapo awali kuwa alikuwa mualimu mwenye bidii - Yona anasema angefika kazini majira ya alfajiri, kiboko mkononi, siku nzima kazi tu, aliweza kufunga vitabu kwenye baskeli kwenda kuvisahihisha wikendi. (uk. 62)
      • Yanadhihirisha mabadiliko katika nyanja ya elimu - Yona anasema siku hizi huwezi tena kumnyoosha mtoto kwa kiboko. (uk.62)
      • Yanachimuza athari za pombe - jinsi pombe ilivyomfanya Yona kuwa mtumwa akashindwa kuishi bila kulewa (uk62)
      • Yanaonyesha uvumilivu au stahamala za Sara wakati Yona alipokuwa mlevi. Yona anasema Sara alimsaidia kulea na kusomesha watoto na kwamba bila yeye chombo kingezama. (uk-62)
      • anaonyesha jinsi Yona alivyoanza kutumia tembo alipokuwa chuoni! Wenzake walimpa mvinyo kumrai kuonja. (uk. 62)
      • Yanadhihirisha uongo wa Beni-kuwa mtoto wake ni fundi wa mitambo na wala si injinia. (uk. 63)
      • Yanaendeleza ploti- tunatambulishwa kuwa Luka, Beni na Yona ni marafiki na walishiriki vileo pamoja.   (,zozote  14 x 1=14)
  5. "Bembea inapolika na kukatika haiwi mwisho wa michezo. Huungwa na mchezo kuanza tena."
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili    (alama 4).
      • Msemaji ni Sará
      • Msemewa ni Neema
      • Walikuwa nyumbani kwa Neema
      • Sara anamshauri Neema kuhusu maisha.   (4x1=4)
    2. Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa kutolea mifano mwafaka katika tamthilia "Bembea ya Maisha"   (alama 10)
      • Neema nusura apoteze uhai wake katika ajali Lakini Bunju akamnusuru kwa kumpeleka hospitalini.
      • Neema na Bunju baada ya kugombana kuhusu mchango wake Bunju katika matibabu ya Sara, Neema anaamua kumuelewa Bunju hivyo ndoa yao kuendelea vyema.
      • Baada ya changamoto ya kutopata watoto iliyoyumbisha ndoa baina ya Sara na Yona, hatimaye walijaliwa watoto watatu.
      • Maradhi ya moyo yalipomlemea Sara kiasi cha kukata tamaa na maisha, Neema anajitolea kuhakikisha mamaye amepata matibabu murua hivyo kumrejeshea matumaini. Japo Yona na Sara walikosa mwana wa kiume na kusimangwa na wanajamii, mabinti zao wanakuwa wembe masomoni hivyo kuwapa furaha katika ndoa yao.
      • Neema alipoonekana kukata tamaa kutokana na kile alichokiona kuwa ni ubahili wa Bunju, Sara alimpa wosia úliompa nguvu zaidi katika ndoa yake.
      • Yona baada ya kugundua kuwa ulevi wake unaangamiza familia yake, anaapa kutolewa tena na kumhudumia mkewe Sara.
      • Yona na Beni walipotofautiana kuhusu watoto wao, Luka anafaulu kutuliza hali na wazee hawa kuendelea na sherehe zao.
      • Baada ya kumsababishia mkewe maradhi ya moyo, Yona anamwomba Sara msamaha kwa kuwa hakujua upeo wa ugonjwa wa moyo.
      • Mgogoro baina ya Sara na Neema kuhusu Yona unaisha Neema anapogundua upendo wa Yona Kwao anapoacha utamaduni wa kutopika chakula.
      • Mgogoro baina ya Sara na Yona unaisha. Yona anapoachana na mila na tamaduni za kutopika kwa mwanaume.
      • Tatizo la Sara la kushindwa kumpikia mkewe linasuluhishwa na jiraniye Dina anapokuja kumsaidia.  (zozote 10 x 1=10) 
    3. Eleza umuhimu wa msemaji katika kuendeleza ploti ya tamthilia hii.     (alama 6)
      • Sara ametumiwa kuonyesha athari ya migogoro katika ndoa. Maradhi ya moyo anayogangua ni tokeo la mzozano baina yake na mumewe Yona
      • Kupitia mazungumzo baina yake na Asna, yanamsawiri Asna kama kijana aliyekengeuka kiasi cha kutotaka kuingia katika ndoa.
      • Kupitia kwake tunaelezwa kuhusu usuli wa matukio. Sara alisemwa na kutukanwa na wanajamii kwa sababu ya kuwapata watoto wa kike pekee. Hii ilipelekea Yona kuingilia ulevi.
      • Baadhi ya matukio katika maisha ya wahusika fulani yanaangaziwa katika nyumba yake. k.m Dina anaangaziwa kama mwenye utu kwani anaenda kumpikia kwa kuwa alikuwa mgonjwa.
      • Kuchimuza matukio fulani. Kupitia mazungumzo baina yake na Yona, junapata kujua kuwa Neema ndiye aliyewasomesha wanuna wake hadi chuo kikuu. elimu
      • Kupitia mazungumzo baina yake na Neema na Asna tunapata kujua kuhusu tofauti baina iza ya hospitali za mjini na kijijini. Huduma za hospitali mjini ni mzuri lakini za kijijini zinalinganishwa na seli na wahudumu hawana mlahaka mwema. 
      • Hatima ya mgogoro baina ya Sara na Yona. Yona anaachana na mila na tamaduni za kutopika kwa Mwanaume.
      • Anaonyesha jinsi utamaduni ulivyowakandamiza wasichana -Sara anamwambia Asna kuwa siku zao elimu ya wasichana ilifanyiwa bezo na kuwa Sara aliachia darasa la saba.
      • Kuonyesha mustakabali wa Sara wa kumsamehe, Yona-Yona anamwomba Sara msamaha kwa kuwa hakujua upeo wa ugonjwa wa moyo. (zozote 6x1-6)
  6. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali
    1. Nafsineni katika shairi hili ana msimamo thabiti. Thibitisha kwa hoja sita.    (alama 6)
      • Anaambiwa wema ni mui, lakini anaushikilia.,
      • Anashikilia kuwa kuwachilia wema ni kupotosha heshima,
      • Hawezi kuwacha kutenda wema, kaandama uadui.
      • Haachi kutenda wema, japo mungamnunia.
      • Hata akapewa mali ya kuhadaa mtima hawezi kukubali kuaacha wema
      • Hawachi kutenda wema, ujapokuwa ni ghali.
      • Hawezi kumcha kabaila,
      • Anakataa kishawishi cha kuwacha wema 
      • Mungamtia na jela, hachi kutenda wema,
      • Wema wake haufi mungaufisha na ana imani Mola bado atauhusha, 
      • Wema ingawa mchungu, atajaribu kutotema,
      • Haachi kutenda wema, kigharimu roho yake
      • Pande mbili zijitokeze bila atuzue =0     (za kwanza 6 x 1=6)
    2. Taja na ueleze bahari ya shairi hili ukizingatia vigezo vifuatavyo: (ala 4)
      1. Vina
        • Ukara - vina vya mwisho vinatiririka ilhali vya ndani vinabadilikabadilika.  (1x1 = al 1)
      2. Vipande
        • mathnawi: kuna vipande viwili (ukwapi, utao)    (1x1 = al 1)
      3. Idadi ya mishororo
        • Tarbia/unne-mishororo minne minne katika kila ubeti.        (1x1 = al 1)
      4. Mshororo wa mwisho
        • sabilia: mshororo wa mwisho unabadilikabadilika     (1x1 = al 1)
    3. Fafanua jinsi mtunzi wa shairi hili alivyotumia uhuru wake.   (alama 3)
      • Inkisari: Unganambia -unganiambia, kaandama - nikaandama, tajitia -nitajitia 
      • Vikale: mui - mbaya, taadhima - heshima, mtima - moyo, Mola
      • Lahaja: siuwati- siuwachi, ndi
      • Kuboronga sarufi: Wewe ndiwe wangu bui - Wewe ndiwe bui wangu Haragwe lenu talila, japo tagoni talala.
      • Udondoshaji wa maneno: Hayo niliyasikia - mambo Hayo niliyasikia
      • Tabdila: kupawa - kupewa mali, sitokubali- sitakubali.
      • Kuchopeka maneno: Munganitia na jela-Munganitia jela, Unganambia
        zozote 3x1-al 3. Mbinu na mfano na kibadala -1)
    4. Eleza umuhimu wa aina za takriri zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 4)
      • Takriri neno- neno wema. Kusisitiza dhamira ya nafsineni kuhusu wema.
      • Takriri silabi-silabi ma. Kuleta ridhimu.
      • Takriri muundo/Usambamba wa kimuundo - Siati kutenda wema. Kuonyesha msimamo thabiti wa nafsineni.
        2x2=4, aina na mfano = 1, umuhimu = 1
    5. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari.   (alama 3)
      • Mshairi anaweka azma ya kushikilia wema hata kama ni mchungu na atatenda wema bila kujali yanayosemwa na watu kwani malipo yake ni kwa Mungu. Anasema haachi kutenda wema hata kama utaigharimu roho yake.  3x1=3
  7. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali   (alama 5)
    1. Tofautisha hali mbili zinazosawiriwa katika shairi.
      • Kuna tabaka la juu la waajiri na la tabaka la chini la waajiriwa
      • Maskini wanaenda kwa miguu huku matajiri wakienda kwa gari la kifahari lililozibwa vioo
      • Maskini wanatafuta kazi inayowala chenga huku matajiri wakiwa ndio waajiri. • Maskini wanapata ujira wa kijungu meko, mshahara usokifu haja, Huku matajiri wanamiliki malaki ya pesa
      • Waajiriwa wanavalia nguo zisizositiri miili dhaifu, huku mwaajiri Mwili wake unameremeta ujana na ufanisi,
      • Mwajiri anaishi kwa raha, waajiriwa maisha yao ni magumu / usaha wa hali (zozote 5 x 1= 5)
        Pande mbili zijitokeze
        bila tuza = 0
    2. Chambua muundo wa shairi hili.    (alama 4)
      • Shairi lina beti nne.
      • Shairi lina kipande kimoja/ kina kimoja,
      • Kuna idadi tofauti tofauti ya mishororo betini.
      • Kila mshororo una idadi tofauti tofauti ya mizani.
      • Shairi halina urari wa vina.
      • Kuna mishata/mistari mishata              (zozote 4 x 1= 4)
    3. Bainisha toni inayojitokeza katika shairi hili    (alama 2)
      • Huzuni - Ujiitapo mwajiri kwa raha, hunusi usaha wa hali yao?
      • Maudhi - Ujiitapo mwajiri kwa raha, hunusi usaha wa hali yao?
      • Masikitiko mshahara usokifu haja, nguo zisizositiri miili dhaifu, kilio chao kisichokuwa na machozi,
        1x2. Kutaja = 1, kufafanua / mfano = 1
    4. Tambulisha hulka za nafsinenwa katika shairi hili.   (alama 3)
      • Mchoyo-anatoa mshara usokifu haja
      • Katili-hajali hali ya maisha ya waajiriwa wake
      • Mwenye bidii anamiliki kiwanda
      • Mwenye mapuuza-hazingatii hakli ya maishaya waajiriwa wake.   (zozote 3x1=3)
    5. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari. (alama 4)
      • Mshairi anamkumbusha mwajiri kutafakari hali yake ya ufanisi, mali na utajiri hali iliyo tofauti na ya mwajiriwa. Anashanga kwa nini anapofurahia haya yote mbona hawazii hali duni ya waajiriwa.   (zozote 4 x 1= 4)
    6. Taja mifano miwili ya mishata katika shairi hili.    (alama 2)
      • Wewe,
      • Utazame mlolongo wa,
      • Watokwao na jasho kapakapa na,
      • Halafu,
      • Na  (zozote 2x 1=2)
  8. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali
    1. Huku ukithibitisha, ainisha ngano hii:
      1. Kimaudhui    (alama 2)
        • Mtanziko; Mhusika hulazimika kuchagua kati ya hali mbili ambazo ni ngumu kuamua ili kupata suluhu.
        • Chui watatu walikuwa wamelalama kwenye matawi ya mti huo wakimsubiri Nyani na alipotamani kushuka, aligundua kwamba naye Bafe alikuwa akiupanda mti kwa kasi akiwa amefunua kinywa tayari kummeza.
          1x2. Kutaja = 1, kufafanua / mfano = 1
      2. Uhusika   (alama 2)
        • Hurafa; wahusika wanyama: nyani, bafe, chui
          1x2. Kutaja = 1, kufafanua / mfano = 1
    2. Tambua na ufafanua umuhimu wa mbinu za utambaji zilizotumika kufanikishauwasilishaji wa ngano hii.  (alama 6)
      • Dayalojia za wahusika - Njaa hii itatusafirisha jongomeo
      • Kuzungumza moja kwa moja na hadhira - mjukuu wangu sijui kama umewahi kuwazia
      • Upenyezi wa utambaji - mjukuu wangu sijui kama umewahi kuwazia
      • Kujenga taswira-kutetemeka kama kondoo/shikwa na mtapo
      • Tashbiha-tetemeka kama kondoo/wakimsubiri mithili ya golikipa anayeusubiri mpira
      • Kushirikisha hadhira kwa kuuliza maswali - ungekuwa Nyani ungefanya nini?
      • Matumizi ya lugha sahili
      • Matumizi ya fomyula ya ufunguzi - hapo zamani za kale
      • Taharuki/lugha inayojenga taharuki.
      • Muundo sahili wa hadithi.
      • Matumizi ya nahau-alimpiga mafamba.    (zozote 6 x 1-6)
    3. Eleza manufaa ya kutumia mbinu ya mahojiano kukusanya data ya fasihi simulizi    (alama 5)
      1. Kuweza kung'amua wakati mhojiwa anatoa habari zisizo za kweli.
      2. Kuweza kufafanulia mhojiwa maswali ili kuweza kupata habari sahihi zaidi.
      3. Kuweza kupata sifa za uwasilishaji kama toni/kiimbo, ishara na kadhalika.
      4. Ni rahisi kurekodi kama kwa vinasa sauti, video na kadhalika.
      5. Kupata habari za kutegewa na kuaminika.    (zozote 5 x 1= 5)
    4. Fafanua njia tano ambazo kwazo jamii ya kisasa inaendeleza utanzu wa hadithi. (alama 5)
      1. Utambaji wa hadithi hasa katika sehemu za mashambani
      2. Kukusanya / Kuhifadhi data kuhusu ngano za jamii mbalimbali Simulizi ili isipotee
      3. Kuirekodi ili kuiendeleza kwa kuirithisha kwa vizazi vijavyo.
      4. Kufunza na kutahini utanzu huu shuleni na vyuoni
      5. Mbinu za kisasa za uhifadhi data-sidi, tepurekoda na tarakilishi.      (zozote 5x 1=5)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Maranda High School Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?