Tuesday, 30 August 2022 06:56

Kiswahili Questions and Answers - KCPE 2022 Prediction Papers Set 2

Share via Whatsapp

Maswali

Soma vifungu vifuatavyo. Vina nafasi 1 mpaka 15. Kwa kila nafasi umepewa majibu manne hapo. Jaza kila pengo kwa kuchagua jawabu lifaalo zaidi.

Serikali     1    wananchi wote kutunza afya     2    . Wananchi wenye afya     3    kutekeleza shughuli mbalimbali za kuindeleza nchi kiuchumi     4    watapunguzia serikali gharama ya kushughulikia matibabu. Hata hivyo,    5    . Kufanikiwa kwa juhudi za serikali      6     kwa kiasi kikubwa jinsi wananchi wenyewe     7    kujitunza.
Miongoni mwa    8    iliyowekwa ni bima ya afya inayohakikisha kuwa wananchi wanapata matibabu bila malipo.

  A B C D
1  ingekuwa iliwahimiza   inakuwa ikiwahimiza   imekuwa ikiwahimiza   ilikuwa ingewahimiza 
2  zao  zenu  zake   yako
3  wanawez tu  hawawezi tu  hawawezi kamwe  wakaweza kamwe
4  kwani pia  bali pia  mbali na  ilhali
5  hakuna mchele ukosao ndume   kitanda usichokilalia hujui kunguni wake  penye miti hapana wajenzi  ukibebwa usilevyelevye miguu
6  inategemea  zinategemea  kunategemea  watategemea
7  wanavyojitahidi  wanaojitahidi  wanayojitahidi   wanapojitahidi
8  hatua  mikakati  lengo  mambo


Ziara yetu katika eneo la Bonde la Ufa     9    sana. Tulijionea    10    ya kupendeza kama vile Kasoko ya Long’onot, Ziwa Naivasha na ndege wa ziwani waitwao       11    . Walimu wetu       12     kwamba haya ni    13     muhimu sana kwa uchumi wetu. Huko Olkaria,       14    kuona umeme ukizalishwa kwa nguvu za mvuke      15    ardhini.

  A B C D
9  ilifaa   ilifana   ilifaana  ilifanana 
10  mandari  mazingara  mandhari  maajabu
11  chozi  nondo  bundi  heroe
12  walitujuza  wealitujulia  walitujulisha  waliwajulisha
13  rasilimali    malighafi  mazigazi  maliasili
14  tunaajabia  tukiajabia  tulijiabia  tungeajabia
15  zitokazo   itokayo  zitokapo  utokao


Kuanzia nambari 16 mpaka 30, jibu kulingana na maagizo uliyopewa.

 1. Chagua sentensi yenye kiwakilishi cha nafsi ya tatu.
  1. Wanaenda mashambani mwao.
  2. Nilikipata kijiko pale.
  3. Unataka nikusaidie vipi?
  4. Tutaanza kusoma moja kwa moja.
 2. Bainisha matumizi mwafaka ya ritifaa.
  1. Kuonyesha kuwa kuna orodha inayofuata.
  2. Kutambulisha sauti inayotamkiwa puani.
  3. Kuonyesha sauti ambayo ni ghuna.
  4. Kutambulisha maneno halisi yaliyotamkwa.
 3. Ni orodha ipi iliyo na kasoro?
  1. Nyigu, panzi, kumbikumbi.
  2. Kizibao, kanzu, bwelasuti
  3. Kitovu, shavu, kisigino.
  4. Ujira, ubwete, pete.
 4. Andika sentensi ifuatayo katika kauli ya kutendwa.
  Mtoto alikula chakula akashiba.
  1. Mtoto aliliwa chakula akashiba.
  2. Chakula kililiwa mtoto akashiba.
  3. Chakula kililiwa na mtoto akashiba.
  4. Mtoto alilishwa chakula akashiba.
 5. Tambulisha kihusishi katika sentensi ifuatayo.
  Mtama wote ulianikwa nje ya nyumba ile.
  1. ile
  2. nje ya
  3. wote
  4. nyumba ile
 6. Tamko lipi hutolewa na mtu anayetarajia kutamka maneno ambayo huenda yakaudhi hadhira yake?
  1. Ashakum
  2. Simile
  3. Samahani 
  4. Pole
 7. Tumia kiulizi kifaacho zaidi.
  Musila aliumia mguu_____?
  1. ipi
  2. mgani
  3. mbona
  4. lini
 8. Bainisha sentensi iliyo na ‘kwa’ kuonyesha sababu.
  1. Alitembea kwa madaha ya tausi.
  2. Wazee kwa vijana walifika hapo.
  3. Fundi alilipanda jengo kwa ngazi.
  4. Ulikemewa kwa utovu wa nidhamu.
 9. Kanusha sentensi ifuatayo.
  Mgeni akiondoka tutaanza shughuli nyingine.
  1.  Mgeni asipoondoka hatutaanza shughuli nyingine.
  2. Mgeni akiondoka hatutaanza shughuli nyingine.
  3. Mgeni asipoondoka tutaanza shughuli nyingine.
  4. Mgeni hataondoka wala hatutaanza shughuli nyingine.
 10.  Mahali jikoni penye bomba la kuoshea vyombo ni
  1. dohani
  2. karo
  3. kichaga
  4. shubaka.
 11. Chagua jozi iliyo na methali zenye maana moja.
  1. Aliye kando haangukiwi na mti.
  2. Usipoziba ufa utajenga ukuta.
  3. Cheche ya moto huchoma msitu.
  4. Tone na tone huwa mchirizi.
   1. (ii) na (iii)
   2. (i) na (iv)
   3. (iii) na (iv)
   4. (ii) na (iv)
 12. Korija moja hujumulisha vitu vingapi?
  1. Viwili
  2. Kumi na viwili
  3. Ishirini
  4. Mia.
 13. Chagua jibu sahihi.
  1. Mjusi alituuzia mchuzi mtamu.
  2. Doa yao haikuwa na doa hata kidogo.
  3. Alikaanga kanga vizuri tukafurahia.
  4. Danda alidadia lori lilipopita hapa.
 14. Shairi lenye mishororo miwili katika kila ubeti ni ______ ilhali shairi la majibizano huitwa _______.
  1. tarbia, utenzi 
  2. tathlitha, ngonjera
  3. mizani, utenzi
  4. tathnia, ngonjera
 15.  Ni sentensi gani iliyo na kiigizi sahihi?
  1. Aisee! Mambo usemayo ni ya kitoto.
  2. Hewala! Hilo usemalo haliwezekani.
  3. Oiyee! Tumefunga bao la ushindi.
  4. Kefule! Nitakusaidia utakavyo.

Yasome makala yafuatayo kisha ujibu maswali 31- 40.

Ulemavu ni hali ya kuwa na kasoro katika viungo vya mwili. Upungufu huu huchangiwa na mambo mbalimbali. Pengine mtu anaweza kushindwa kutekeleza baadhi ya shughuli za kawaida kama vile kuongea, kutangamana na wengine, kusoma au hata kujitegemea kwa mambo mbalimbali. Mara nyingi ulemavu huwa wa kudumu japo kuna ule uwezao kuisha baada ya kipindi fulani.

Baadhi ya watu hupata ulemavu kutokana na kasoro wakati wa kufanyika kuwa motto tumboni. Huenda mzazi akajifungua salama lakini baadaye akagundua kuwa mtoto wake amekosa kiungo fulani. Pia, mtoto anaweza kuendelea kukua bila kugunduliwa lakini mabadiliko yanayotarajiwa katika vipindi mbalimbali vya ukuaji yakakosekana. Hata hivyo, wakati mwingine mabadiliko yanaweza kuchelewa lakini mwishowe yakatokea tu.

Mbali na hayo, binadamu anapotangamana na mazingira yake, anaweza kuambulia ulemavu kutokana na majeraha ya viungo, ya ubongo au uti wa mgongo. Magonjwa kama vile kisukari na shinikizo la damu pia yanaweza kuchangia ulemavu. Baadhi ya watu waliokuwa wazima hivi majuzi tu wameambulia ulemavu kupitia ajali mablimbali. Ni vyema mtu ajizatiti kuepuka hali yoyote inayoweza kuhatarisha afya yake.

Unaweza kufikiria kuhusu siku uliyoteleza mlipokuwa mkicheza na wenzako, ukateguka mguu au mkono? Pengine unakumbuka namna ulivyoteseka kwa kushindwa kujifanyia mambo muhimu kama vile kuoga, kutembea kuenda haja au hata kula. Yamkini utaniambia kuwa lililokuuma zaidi ya uchungu wa jeraha hilo hilo ni kule kukosa fursa katika shughuli za kila siku. Hata wenzako walipokuzuru kukujulia hali, ulifurahi lakini ukavaliwa na ukiwa pindi tu walipokupa mgongo. Walemavu wengi hupitia hali kama hizi aushi yao yote.

Wakati mwingine watu huzitonesha nyoyo za ulemavu bila kujali hisia zao. Utamsikia mtu kwa mfano akisema, ‘Niitie huyo chongo nimtume’ au ‘Msaidieni huyo kiwete jamani.’ Sharti ieleweke kwamba walemavu ni binadamu wa kawaida na kila mtu anao ulemavu wa aina fulani. Hakuna aliye na wepesi wa kufanya kila kitu. Hata kuwa na moyo wa harara ni ulemavu mkubwa. Tukumbuke ya wahenga kuwa hucheka kovu asiyefikwa na jeraha. Watu hawa wana majina yao. Tusiwadhalilishe kwa kuwarejelea kwa maumbile yao.

Wapo wazazi wanaowaficha wana wao walemavu na hata kukosa kuwapeleka shuleni. Huu ni ukandamizaji wa hali ya juu. Mtu yeyote akipata nafasi ya kutangamana na mazingira yake ipasavyo, bila shaka atabuni njia ya kutekeleza shughuli zake kadri awezavyo. Walemavu wengine wameinukia kuwa watu wa kutegemewa sana na jamii, hata kiasi cha kuwafikia kuwafaa wale wasio na uatilifu wowote.

Kila binadamu ana haki zake. Ni vyema jamii ikubali kuwa waatilifu ni binadamu wanaohitaji huduma kama wengine wowote. Haki zao zitambuliwe na maumbile yasiwe kigezo cha kuwadhalilisha kwa vyovyote vile.

 1. Chagua maelezo sahihi kulingana na aya ya kwanza.
  1. Ulemavu ni hali ya mtu kushindwa kufanya jambo.
  2. Huenda mlemavu akashindwa kujihudumia ipasavyo.
  3. Ulemavu wowote ule huwa ni hali ya kudumu.
  4. Walemavu hushindwa kabisa kutekeleza shughuli muhimu maishani.
 2. Kipi si kiini cha ulemavu?
  1. Kuhusika katika ajali.
  2. Kasoro za kimaumbile.
  3. Mwili kukosa kuendelea ipasavyo.
  4. Uchelewaji kaitika kukua
 3. Waliokuwa wazima kulingana na makala haya ni wale
  1. ambao kasoro zao hazikuwa zimegunduliwa
  2. ambao si watoto kwani wamekomaa
  3. wasiokuwa na kasoro zozote za kimaumbile
  4. waliofikiria kuwa hawawezi kuathirika.
 4. Kulingana na aya ya nne
  1.  kuteleza kwa msimulizi kulimfanya mlemavu
  2. mwandishi ana uhakika kuwa msomaji aliteleza michezoni
  3. watoto waliopata majeraha hawaogi wala kutembea
  4. kushindwa kujumuika na wengine huathiri hisia zaidi.
 5. Ni hali gani ambazo mwandishi anasema walemavu wengi hupitia auishi yote?
  1. Hali ya upweke na kunyimwa nafasi ya kushiriki.
  2. Ukiwa baada ya marafiki waliozuru kuaga haraka
  3. Majeraha ya viungo na kulala siku nzima.
  4. Kupuuzwa na marafiki na kuhitajika kutoa msaada.
 6. Si vizuri kuwataja watu kulingana na kasoro zao kwani
  1. huku ni kuwaumiza hisia zao
  2. wana majina yanayojulikana na wote
  3. huenda wasijue maana ya majina hayo
  4. hata sisi ni walemavu kama wao.
 7. ‘Chongo’ kulingana na makala haya ni
  1.  mtu ambaye mboni za macho yake zimeelekea kombo
  2. mtu asiye na uwezo wa kuona kabisa
  3. mtu ambaye jicho lake moja limepofuka
  4. mtu mwenye nundu mgongoni pake.
 8. Wazazi huwanyima watoto wao walemavu haki zipi?
  1. Elimu na malezi.
  2. Utangamano na makazi.
  3. Mapenzi na makazi.
  4. Shule na hiari.
 9. Maana ya kuwa na ‘moyo wa harara’ ni
  1. kushtuliwa na mambo madogo
  2.  hali ya kukasirika upesi
  3. kutumia maneno makali kwa wengine
  4. kuwa na maradhi ya moyo.
 10. Kichwa kifaacho zaidi kwa makala haya ni
  1. Haki za walemavu.
  2. Vyanzo vya ulemavu.
  3. Aina mbalimbali za ulemavu.
  4. Ukarimu wa malemavu.

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 41 – 50.

Daktari Maluki alikaa katika chumba cha matibabu akijisikilizia muziki kwenye rukono yake. Alikuwa amefika kazini saa chache zilizopita. Akili zake zilikuwa mbali kidogo.Aliwaza kuhusu kima cha pesa na muda aliotumia kusomea taaluma hii. Akalinganisha na ‘ mshahara tonge’ aliopata kama alivyouita yeye, japo mshahara wenyewe ulikuwa wa kuliliwa ngoa na akina yahe. Aliona kweli kwamba dunia haina huruma. Alipiga darubini na kuwaona jinsi viongozi wakuu walivyojilimbikizia donge nono licha ya kuwa walifanya kazi kwa muda mfupi sana.

Baada ya kutia na kutoa, aliibuka na uamuzi aliohisi kwamba ungemfaa bila ‘kuwaathiri sana’ waliosaka huduma yake. Kwanza, yeyote aliyesaka huduma yake angelipa kifunguamkoba cha shilingi elfu mbili ili apate nafasi ya kumwona. Maadamu, alikuwa daktari mkuu, uamuzi wake haukupingwa sana pale hospitalini. Si kila mmoja anafahamu vyema kuwa mkono mtupu haurambwi? Tena yeye Daktari Maluki hakumwalika yeyote kuja kumwona. Si wanaletwa na shida zao tena kwa hiari yao?

Mradi huu ulifanikiwa sana na kumfurahisha Daktari Maluki. Sasa kipaji kilionekana kumnawiri wakati wote akiwa kazini. Aidha, aliiraukia kazi mapema sana ili aweze kuwahudumia wagonjwa wengi kadri ilivyowezekana. Kufanikiwa kwa mradi huu kulimfanya azuke na mwingine. Alifungua duka kubwa la dawa mkabala wa hospitali ile. Wagonjwa waliokuwa wakija kwa matibabu walikuwa wakipewa dawa dukani pale. Serikali ndiyo iliyolaumiwa kwa kukosa kuleta dawa hospitalini. Lakini sikwambii kuwa dawa zizo hizo zilizokuwa halali na haki yao ndizo walizozilipia pale dukani.

Daima dawamu mbio za sakafuni huishia ukingoni. Siku moja, wasamaria wema walikuja na mgonjwa aliyehusika katika ajali ya barabarani. Alikuwa akivunja damu sana hivyo basi alihitaji kushughulikiwa kwa haraka. Daktari aliitwa lakini hakubanduka pale kitini mwake. Alitaka kujua ni nani angegharamia matibabu. Wasamaria wema hawakutaka kufanya hiyo maadamu hawakuhusiana na mwele yule kwa damu wala usaha. Basi mgonjwa akaachwa kuendelea kuvunja damu.

Watu waliokuwepo walishauriana na kuafikiana kuchanga angaa kifungua mkoba ili mgonjwa ahudumiwe. Hata zilipotosha walimwendea mgonjwa ili wampeleke kwa daktari. Lo! Walishangaa walipogundua kuwa mwili wake ulikuwa u baridi tayari. Daktari alitia fulusi kibindoni na kuagiza aletwe. Alipompimapima, aligundua kuwa amekata kamba. Hata hivyo, alivutiwa na jingine. Ni uso wa mtu aliyemfahamu sana. ‘Haiwezekani......mama........ mam....’ Daktari akazirai.

Kumbe mamaye Maluki alikuwa amekuja kumzuru mwanawe mjini alipopigwa dafrau na gari kabla ya kufika kwa mwanawe. Sasa alikuwa kaenda jongomeo baada ya kunyimwa huduma na mwanawe aliyemzaa, akamlea na kumsomesha kwa shida. Ama kweli, kigumba ni kwa nguruwe, kwa binadamu ki uchungu.

 1. Kulingana na aya ya kwanza, Daktari Maluki
  1. aliketi ofisini kusikiliza muziki kwenye redio
  2. alizingatia sana muziki wa rukono yake
  3. hakuwa amekaa sana baada ya kufika kazini
  4. hakuwa na hamu ya kuwahudumia wagonjwa.
 2. Kwa nini Daktari Maluki alijipata akiwaza?
  1. Alihisi kuwa malipo yake hayakulingana na hadhi yake kikazi.
  2. Alitumia pesa na muda mrefu kusoma kuliko wenzake.
  3. Mshahara wake ulikuwa ukililiwa ngoa na kina yakhe.
  4. Alitaka kuwa kiongozi wa serikali apate donge nono.
 3. Kulingana na aya ya pili
  1. waliotafuta msaada kwa daktari hawakuathirika kwa uamuzi wake
  2. nafasi ya Daktari kazini iliufanya uamuzi wake kufuatwa bila swali
  3. mtu akiwa na shida hafai kupewa hiari ya kuwa na usemi wowote
  4. mtu akitaka msaada bila kutoa chochote hafai kuhudumiwa popote.
 4. Kunawiri kwa kipaji cha Daktari Maluki ni ishara kuwa
  1. watu sasa wameanza kuja kwake kwa hiari yao
  2. kuongezewa mshahara kazini kumempa raha aliyotamani
  3. huduma anayotoa kwa wateja ni bora kuliko awali
  4.  shughuli ya kifisadi aliyoanza inampa kipato alichotamani.
 5. Si kweli kusema kuwa
  1. Daktari alipofika kazini mapema aliwajali wagonjwa
  2. Daktari alianzisha biashara karibu na hospitali aliyofanyia kazi
  3. watu walilipia ada kwa sababu ya kukosa hiari
  4.  wagonjwa walipata baadhi ya dawa pale hospitalini.
 6. Chagua sifa za Daktari Maluki kulingana na makala haya.
  1. Mzingatifu na mkatili.
  2. Fisadi, asiye na utu.
  3. Katili na mwenye bidii kazini.
  4. Mlafi na anayetafuta kutambuliwa.
 7. Kwa nini Daktari hakubanduka kitini alipoitiwa mgonjwa?
  1. Alikuwa amezama mawazoni.
  2. Hakujua kuwa mgonjwa alikuwa hatarini.
  3. Hakuwa na hamu ya kazi siku ile.
  4. Mgonjwa hakuwa amelipiwa ada iliyohitajika.
 8. ‘Hawakuhusiana na mwele yule kwa damu wala usaha’ ina maana kuwa
  1. wasamaria wema hawakujuana na mgonjwa
  2. daktari hakutaka kujihusisha na Mjeruhiwa
  3. wasaidizi hawakuwa wa nasaba ya mjeruhiwa
  4. wasamaria wema hawakuwa na uhusiano na Daktari.
 9.  Kilichochangia kifo cha majeruhi ni
  1. kutelekezwa
  2. kukosa kufungua mkoba
  3. kuchelewa kufika hospitalini
  4. kupewa matibabu yasiyofaa.
 10. Aya ya mwisho imetufahamisha kuwa
  1. mtu anapoadhibiwa kwa makosa yake hafai kuhurumiwa
  2. mtu akitendewa dhuluma atendeazo wengine hawazii matendo yake
  3. mtu anapotendewa uovu uo huo aliozoea huona uchungu sana
  4. Mtu anaweza kufurahi anapowadhulumu wengine lakini adhulumiwapo hivyo huona uchungu.

INSHA
Umepewa dakika 40 kuandika insha yako.

Andika insha isiyopungua ukurasa mmoja na nusu ukifuata maagizo uliyopewa.

Umechaguliwa kutoa hotuba kwa niaba ya wanafunzi wenzako siku ya kutoa tuzo kwa wanafunzi waliotia for a katika tofauti tofauti. Andika hotuba yako.

Majibu

 1. C
 2. A
 3. B
 4. B
 5. D
 6. C
 7. A
 8. B
 9. B
 10. C
 11. D
 12. A
 13. D
 14. C
 15. D
 16. A
 17. B
 18. D
 19. C
 20. B
 21. A
 22. D
 23. D
 24. A
 25. B
 26. A
 27. C
 28. C
 29. D
 30. C
 31. A
 32. D
 33. C
 34. D
 35. A
 36. A
 37. C
 38. B
 39. B
 40. A
 41. C
 42. A
 43. B
 44. D
 45. A
 46. B
 47. D
 48. C
 49. A
 50. D
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Questions and Answers - KCPE 2022 Prediction Papers Set 2.


Tap Here to Download for 30/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students