Wednesday, 29 March 2023 13:58

Kiswahili Questions and Answers - Class 8 Mid Term Exams Term 1 2023 Set 11

Share via Whatsapp

Soma vifungu vifuatavyo. Vina nafasi 1 mpaka 15. Kwa kila nafasi umepewa majibu manne hapo. Jaza pengo kwa kuchagua jawabu lifaalo zaidi.

__1__ wakazi wa miji na majiji mbalimbali __2__ na changamoto __3__ kila aina, mathalani __4__uchafuzi wa mazingira, misongamano ya magari na uhalifu. __5__ mambo haya yote, utovu wa usalama __6__waja wengi wasiwasi zaidi. Nyakati za usiku,
giza __7__, wengi wao hutembea __8__. Mchango wa kila mkazi unahitajika katika kukabiliana na hali hii kwani __9__.

   A   B   C   D 
 1.   Almradi   Angaa   Aghalabu   Ilhali 
 2.  huangaliwa   huzongwa   huangaziwa   hukabidhiwa 
 3.  la  cha  ya  za
 4.  :  ,  ;  ---
 5.  Baadhi ya  Kati ya  Dhidi ya   Fauka ya
 6.  ndiyo inayowatia   ndio unayewatia   ndio unaowatia   ndilo linalowatia 
 7.  inapofungamana   unapofungamana     linapofungamana    kinapofungamana 
 8.  roho mkononi  maguu begani  ulimi mdomoni   moyo kifuani
 9.  Mbwa hafi maji aonapo ufuko   Mbio za sakafuni huishia ukingoni   Cheche ya moto huchoma msitu   Mkono mmoja hauchinji ng'ombe 


Shawe alitamani kuanzisha __10__ ya useremala, __11__ wazazi wake ili wampe __12__ aweze kutimiza haja yake. Baba yake alimpa __13__. Alianza kwa kununua vifaa vilivyohitajika ambavyo ni __14__. Biashara hii __15__ kwani katika muda mfupi,umaarufu wa samani alizoundia hapo ulizungumziwa karibu na mbali.

   A   B   C   D 
 10.   duka   karakana   kiwanda   maabara 
 11.  angewaendea   akiwaendea   anawaendea   akawaendea 
 12.  mtaji  ujira   dhamana   koto 
 13.   bumba la pesa   kipeto cha pesa    kitita cha pesa   kichala cha pesa 
 14.  mvukuto, randa na fuawe   parafujo, timazi na beleshi   tishali, msasana rukwama   jiriwa, bisibisi na msumeno 
 15.  ilichanua kama waridi  ilichipuka kama uyoga  ilinukia kama ruhani   ilijitia kati kama mchuzi

 

Kuanzia nambari 16 mpaka 30, jibu kila swali kulingana na maagizo uliyopewa.

  1. Chagua sentensi yenye kivumishi cha idadi.
    1. Mataifa mengi yametia sahihi mkataba wa amani.
    2. Wanane wamepokea vyeti vyao baada ya kuhitimu.
    3. Amani ameenda uwanjani tena akacheze.
    4. Shamba lile lina mitunda ya kila aina.
  2. Ni sentensi ipi iliyo sahihi kisarufi?
    1. Nyembe iliyonunuliwa inanyoa vizuri.
    2. Maji ambayo yaliyochemshwa ni salama kwa kunywa.
    3. Uovu ambao ulitekelezwa uliwahuzunisha wengi.
    4. Wimbi ambao ulitokea baharini ulikuwa mkubwa.
  3. Kipi ni kivumishi kilichoundwa kutokana na kitenzi.
    1. ubaya - baya
    2. samehe - samehevu
    3. andika --maandishi
    4. ucheshi - kicheko
  4. Andika sentensi ifuatayo bila kirejeshi amba. Wanafunzi ambao wamekuja ni wenye bidii.
    1. Wanafunzi wamekuja ni wenye bidii.
    2. Wanafunzi wakujao ni wenye bidii.
    3. Wanafunzi wameokuja ni wenye bidii.
    4. Wanafunzi waliokuja ni wenye bidii.
  5. Unganisha sentensi zifuatazo kwa usahihi:
    Wanafunzi wameandika insha.
    Wanafunzi wameagizwa na mwalimu.
    1. Wanafunzi wamemwandikia mwalimu insha.
    2. Insha imeandikiwa na wanafunzi kwa mwalimu.
    3. Mwalimu ameandikia wanafunzi insha.
    4. Mwalimu amewaandikisha wanafunzi insha.
  6. Mtu mwenye ujuzi wa kutengeneza visu huitwaje?
    1. Mjumu
    2. Sonara
    3. Mjume
    4. Mwashi
  7. Chagua sentensi iliyotumia kiambishi ki cha hali ya kuendelea
    1. Kiti hicho kikipanguswa kitakaliwa.
    2. Kikoba alichobeba kilikuwa kimejaa pesa.
    3. Mtoto huyo alishambuliwa na mamba akiogelea mtoni.
    4. Munga akifika tutaanza mkutano wetu.
  8. Tegua kitendawili kifuatacho:
    Daima nasuka mikeka lakini wanangu hulala chini.
    1. Kobe
    2. Mboga
    3. Mnazi
    4. Nyuni
  9. Aibu ni kwa fedheha kama vile bidii ni kwa 
    1. hamu
    2. shauku
    3. hamaki
    4. ari
  10. Kanusha:
    Mpunga uliopandwa umeotam
    1. Mpunga usiopandwa haujaota.
    2. Mkunga ambao haukupandwa haukuota.
    3. Mpunga uliopandwa haukuota. 
    4. Mpunga uliopandwa haujaota.
  11. Maelezo yapi ni sahihi kuhusu ukoo?
    1. Mjomba ni kaka wa baba.
    2. Ndugu wa kike na wa kiume huitana umbu.
    3. Mpwa ni mtoto wa shangazi,
    4. Mama na mke wa mwanawe huitana wifi.
  12. Andika usemi wa taarifa wa:
    Baba: Mwanangu, nitakufunza kulima kwa plau kesho.
    1. Baba alimwambia mwanawe kwamba angemfunza kulima kwa plau siku ambayo ingefuata. 
    2. Baba amemwambia mwanawe kwamba atamfunza kulima kwa plau kesho.
    3. Baba alimwambia mwanawe  kwamba angemfunza kwa plau
    4. "Kesho nitakufunza kulima kwa plau," baba alimwambia mwanawe.
  13. Maneno niliyoyasikia yamenikata ini. Sentensi hii imetumia tamathali gani ya usemi?
    1. Chuku
    2. Kinaya
    3. nahau
    4. Ishara
  14. Upi ni udogo wa sentensi:
    Kidole kidogo kimevishwa pete.
    1. Dole dogo limevishwa jipete
    2. Kidole kidogo kimevishwa kipete. 
    3. Kijidole kidogo kimevishwa pete. 
    4. Kijidole kidogo kimevishwa kijipete.
  15. Kupotea njia ndiko kujua njia ni methali ambayo huambiwa;
    1. wale wanaoogopa kufanya makosa wanapojifunza.
    2. wanaoshangazwa na ujuzi wa wengine katika jambo.
    3. wanaopuuza uwezo wa wenzao kwa kuwaona duni.
    4. wale wanaokata tamaa wakiwa karibu kufanikiwa.

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali kuanzia 31 mpaka 40

Siwezi kuyatia katika kaburi la mghafala yaliyotokea katika kaya yetu wakati wa likizo ya muhula wa pili. Mimi na mama yangu tulikuwa tumefanya kazi kondeni mchana kutwa. Hali hii ilinifanya niwc hoi kwa uchovu. Nilipopata chajio, nilianza kusinzia. Niliamua kujiegemeza kwenye kochi. Punde si punde, nilienda chumbani mwangu kulala. Sikuwa nimepata usingizi wa pono niliposikia kamsa. Niligutuka. Nilitulia tuli huku nikiyatega masikio ndi! Nilifanya hili kimaksudi ili niweze kusikia vizuri ulikotoka usiahi huo.\

Niliamka huku moyo wangu ukinipuma kifuani. Nilielekea mlangoni asteaste nikaufungua taratibu. Mkononi nilijihami kwa sime na rungu yangu. Ule ulegevu niliokuwa nao ulitoweka ghafla, Nilihakikisha kuwa sikuuacha mwenge wangu. Nilisimama tutwc huku nikisikiliza kwa utuvu na tuo angalau niweze kusikia tena ulikotoka unyende huo. Pindi si pindi, nilitambua kuwa usiahi huo ulitoka upande wa matlai ya mastakimu yetu.

Kwa mwia mrefu, wanakitongoji chetu walikuwa wamebughudhiwa na malusu. Nilikumbuka kilio cha wengi walioibiwa mali. "Wanakijiji wenzangu, hatuna budi kuungana ili kuangamiza majambazi hawa," alisema mmoja wa wanakijiji siku moja baada ya kuvamiwa. Nilikumbuka kauli ya wahenga ivumayo hivi: Kijinga na kijinga ndipo moto uwakapo.

Wanakijiji wengi walikuwa wameshakusanyika pamoja tayari kuanza msako wa majambazi hao. Kila mmoja alikuwa amejihami kwa zana za vita. Tulifuatana unyounyo kuelekea upande wa mashariki. Punde si punde, tulikaribia nyumba ya Karogo. Kamsa ile ilisikika tena lakini waziwazi. Tulitembea chapuchapu kuelekea chengoni mle. Tulipofika kwenye lango, tulimpata Kargo amesimama kidete, mkuki mkononi. Alitufahamisha kuwa majambazi walikuwa akimvamia jirani yake, Omondi.

Sote tulipandwa na wa kwetu. Hidaya kuvuta taswira namna majambazi hawa walivyokuwa wamewasafirisha jengombe wakazi wengi kitongojini mwetu. Tulikata shauri kupambana nao; liwe liwalo. Sote tuheckea lewa Omondi. Tulitembea kwa tahadhari kuu. Kiongozi wetu alitushauri tusiiwashe mienge yetu ili isitutilie mchanga kitumbua chetu. Sote tuliyazingatia mawaidha yale. Ajabu ni kuwa hakuna aliyesema lolote. Lakini kila mmoja aliweza kuusikia mpumuo wa mwenzake.

Mwia si ayami, tulikaribia nyumba ya Omondi. Malumbano makali yalitualika humo. Hatukufanya papara. Tulikaa ange kwa lolote. Jitu moja lilitoka nyumbani mwa Omondi likihema kama mnyama aliyekuwa akiwindwa. Lilikuwa limejihami kwa zana kali. Kwa nyota ya jaha, halikutuona. Nilifaulu kulitega. Lilianguka chini pu! Tulilivamia kituta. Hatimaye tulilifunga kifati kwa kamba ambayo haikujulikana ilikotoka. Baadaye tulijituma nyumbani ili tuweze kuona madhara liliyotekeleza.

Masalale! Omondi na mkewe walikuwa wakigaragara sakafuni. Lilikuwa limewajeruhi vibaya. Damu iliwatiririka tiriri. Hasira za mwizi zilimpata mmoja wetu ambaye alilipiga teke kifuani. Jitu lilianguka chini kwa kishindo. Wengine, kwa ghadhabu walitaka kulitoa roho. Wakati huo baadhi yetu walikuwa wameagiza gari la kuwapeleka wahasiriwa hospitalini. Walikuwa wakilia kwa uchungu huku michinzi ya machozi ikiwatiririka njia mbilimbili.

"Tuchunge kulima jitu hili katili ili litoe habari kuhusu washirika wake," nilishauri. Tuliafikiana katika hilo. Tulifululiza hadi kwenye kituo cha polisi. Jitu hilo lilikuwa likitetemeka kama ukuti wa mnazi. Askari walipotuona walikenua meno. "Siku za mwizi ni arubaini," afisa mmoja alisema. "Bila shaka pwagu hupata pwaguzi,'.niliongeza. Sote tulitazamana kwa ufurufu mzomzo.

  1. Chagua jibu sahihi kulingana na aya ya kwanza. Tukio lilitokea
    1. katika mwezi wa pili.
    2. katika mwezi wa nne.
    3. katika mwezi wa nane.
    4. mwishoni mwa mwaka.
  2. Kwa nini mwandishi alianza kusinzia?
    1. Ulikuwa wakati wa usiku. B
    2. Alikuwa na uchovu mwingi.
    3. Alikuwa amejilaza kochini.
    4. Ilikuwa ni baada ya kula chajio.
  3. Baada ya kusikia usiahi, msimulizi
    1. alitoka nje kwa kasi.
    2. alijawa na hofu isiyo kifani.
    3. aliendelea kujilaza kitandani.
    4. alitulia ili kubaini yaliyokuwa yakitendeka.
  4. Si kweli kusema kuwa;
    1. matukio ya aina hii hayakuwa ya kawaida kijijini.
    2. vitendo vya uhalifu vilikuwa vimekithiri kitongojini.
    3. mwandishi alikuwa na silaha nyumbani.
    4. usiahi ulitoka mashariki ya alikokuwa mwandishi.
  5. Zipi ni sifa za msimulizi wa makala haya?
    1. Jasiri, mwenye makini.
    2. Mwoga, anayewajali wengine. 
    3. Hodari, anayeheshimiwa na wengi.
    4. Katili, anayepinga uhalifu.
  6. Kulingana na kifungu,
    1. majambazi walitekeleza uhalifu nyumbani kwa Karogo.
    2. msako ulishirikisha raia na polisi. 
    3. kamba ya kumfunga mshukiwa ilitolewa kwa Omondi.
    4. mwandishi ndiye aliyechangia ari ya kukabiliana na wahalifu.
  7. Jambo lililowatia wananchi ari ya kukabiliana na wahalifu ni,
    1. silaha hatari walizokuwa nazo.
    2. maovu ainati yaliyotekelezwa kijijini.
    3. woga uliodhihirishwa na majambazi wenyewe.
    4. himizo kutoka kwa wale waliohasiriwa.
  8. Maana ya kukaa ange ni
    1. kuwa na woga.
    2. kuwa tayari kuondoka.
    3. kuwa mwangalifu.
    4. kuchukua hatua.
  9. Kwa nini msimulizi alishauri jitu lipelekwe kituoni mwa polisi? Ili
    1. lisidhulumiwe na wakazi wenye hamaki:
    2. liweze kuadhibiwa vikali na polisi.
    3. kuwasalimisha Omondi na mkewe.
    4. lisaidie uchunguzi wa kuwakamata wahalifu wengine.
  10. Methali 'pwagu hupata pwaguzi' imetumiwa kwa maana kuwa,
    1. mwizi hodari hunaswa na wezi wenye ujuzi zaidi.
    2. mtu mwenye maarifa hushindwa kwa mikakati iliyo bora zaidi. 
    3. anayewadhulumu wengine hukomeshwa kwa dhuluma zizo hizo.
    4. anayepuuza uwezo wa wengine hushtuka akiuona uhodari wao.

Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali kuanzia nambari 41 mpaka 50

Mwili wa binadamu hauna budi kufanyizwa mazoezi hususan kwa watu wenye kufanya kazi katika mazingira ya ofisi ambapo wanaketi mchana kutwa. Mazoezi haya ni muhimu kwa sababu mwili wa binadamu ulidhamiriwa kufanya mazoezi ya viungo kwa kutembea au kufanya kazi zenye kuhitaji misuli kupashwa moto. Si watu wengi wenye habari kwamba mazoezi yana faida tele.

Mosi, mtu anayefanya mazoezi huishi zaidi kuliko asiyefanya hivyo. Mtu kama huyu huwa katika hali nzuri ya siha kuliko wale ambao hawaishughulikii miili yao kwa mazoezi au kazi zinazohitaji utumiaji wa nguvu.

Si jambo la mjadala kuwa mazoezi huchochea kuundwa kwa seli mpya za ubongo. Hali hii humfanya mtu kukumbuka na kujifunza mambo vizuri. Hali hii hutokana na ukweli kuwa mazoezi husisimua schemu za ubongo. Ukosefu wa mazoezi huzifanya sehemu za ubongo kushindwa kukumbuka au kujifunza maarifa mapya. Aidha, imedhibitishwa kuwa watu wanaoshiriki shughuli zenye kuwahitaji kutumia nguvu hutia fora katika mambo yanayowahitaji kukumbuka, kufanya maamuzi pamoja na kusuluhisha matatizo.

Halikadhalika, mazoezi huimarisha siha ya binadamu. Mathalani, matatizo ya moyo yanaweza kukabiliwa kwa kufanya mazoezi ya viungo. Mazoezi ya mara kwa mara huufanya kuwa imara na kuuwezesha kutekeleza jukumu lake inavyofaa. Moyo wenye afya huweza kupiga kiasi kikubwa cha damu bila juhudi kubwa. Jambo hili humkinga binadamu dhidi ya kulemewa na kazi.
moyo

Pia, utulivu wa akili hupatikana kwa kufanya mazoezi. Ni ukweli usiopingika kuwa mazoczi hupunguza dalili za unyong'onyevu Pia humsaidia mtu kupata usingizi wa pono. Hivyo, pana haja ya kufanya mazoezi kwa angalau daika thelathini kwa muda wa kati ya siku tatu na tano kwa wiki.

Kunyooshanyoosha viungo nako huchangia kuufanya mwili kuwa imara na wenye kunyumbuka. Hali hii ya mwili upungua uwezekano wa kupata majeraha. Mwili usionyumbuka humfanya mtu ashindwe kutekeleza shughuli nyepesi zinazomhitaji kutumia nguvu. Si shani kupata kuwa kutekeleza shughuli ndogo tu humfanya mtu asiyeshiriki mazoezi ahisi maumivu.

Halikadhalika, mazoezi husaidia kujenga mifupa kadri binadamu anavyoshiriki katika shughuli kama vile kuruka, ndivyo anavyoimarisha mifupa yake. Amali kama hii huipa mifupa uzito unaoiwezesha mifupa kukua na kujengeka ikiwa na nguvu. Mazoezi pia hukawiza kudhoofika kwa mifupa.

Isitoshe, kushiriki mazoezi au shughuli zenye kutumia nguvu mara kwa mara huuweka mwili katika hali nzuri ya kupambana na maradhi. Shughuli zinazomhitaji mtu kutumia. nguvu, pamoja na kupunguza uzani na uzingatiaji wa lishe bora hupunguza uwezekano wa kuambulia maradhi ya kisukari. Mazoezi hayapunguzi tu shinikizo la damu bali pia hatari ya kupata kiharusi. Aidha, kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kudhibiti uzito na huvisisimua viungo vya mwili. Matokeo ya haya ni utendakazi wa hali ya juu bila kuchoka upesi.

Mbali na hayo, mwili unaofanya mazoezi haudorori. Umbo la mtu anayefanya mazoezi hupendeza. Fauka ya hayo, kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kujenga misuli yenye nguvu. Hili likifanyika, tunaweza kulifanya jambo kwa muda mrefu pasipo kuchoka sana. Moyo wa mtu anayeshiriki mazoezi hupiga damu kwa nguvu ili kueneza oksijeni na sukari kwenye viungo mahsusi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa oksijeni na sukari ndivyo viini vya nishati mwilini.

Mke ni nguo mgomba kupaliliwa. Nao mwili wa binadamu kama mgomba, unahitaji kushirikishwa katika mazoezi ili kuuwezesha kuwa na hamu ya kutenda kazi.

  1. Kulingana na aya ya kwanza,
    1. watu wanaoshiriki kazi za kiofisi hawachoki.
    2. kazi zinazofanywa ofisini huvinyima mwili mazoezi ya viungo.
    3. wanaofanya kazi ofisini pekee ndio wanaohitaji mazoezi.
    4. watu wengi wanajua umuhimu wa mazoezi ya viungo.
  2. Mtu akifanya kazi zinazomhitaji kutumia nguvu,
    1. anapaswa kushiriki mazoezi mengine.
    2. si sawa na anayefanya mazoezi ya viungo.
    3. huathiri mwili wake kwa ugumu wa shughuli hizo. 
    4. tayari huwa ameufanyisha mwili wake mazoezi.
  3. Si jambo la mjadala, ndiko kusema.
    1. inaeleweka waziwazi.
    2. jambo hilo halijulikani.
    3. ni jambo lenye ubishi.
    4. si suala lenye umuhimu.
  4. Kufanya mazoezi humsaidia mtu kwa yote haya ila,
    1. kufanya ubongo kuwa na seli mpya.
    2. kuimarisha uwezo wa kukumbuka mambo.
    3. kumwezesha mtu kuelewa hata yale asiyojifunza.
    4. kumwezesha mtu kusuluhisha mambo mbalimbali.
  5. Ili mtu aweze kufanya kazi ipasavyo; 
    1. moyo huhitajika kusukuma damu nyingi.
    2. moyo huhitajika kupiga damu kiasi tu.
    3. ubongo wake unafaa kuwa na seli mpya.
    4. lazima awe amepumzika kwa muda mrefu.
  6. Aya'ya tano inaonyesha kuwa,
    1. kufanya mazoezi huchangia mazoea ya kulala m ra kwa mara.
    2. kushiriki mazoezi huwezesha mwili kupata mapumziko yafaayo. C
    3. wanaofanya mazoezi huambulia usingizi wa mang'amung'amu.
    4. watu wasiofanya mazoezi hujikosesha usingizi.
  7. Kunyumbuka kwa viungo vya mwili,
    1. humwondolea mtu majeraha.
    2. husababisha maumivu ya viungo.
    3. huupa mwili nguvu zaidi.
    4. hupunguza uwezekana wa mtu kuumia.
  8. Ni maradhi yapi yanayodhibitiwa zaidi kwa kushiriki mazoezi ya viungo?
    1. Ya kuambukiza.
    2. Yasiyo ya kuambukiza.
    3. Ya kila aina
    4. yale ya zinaa.
  9. Mwito wa mwandishi wa kifungu ni kuwa,
    1. tushiriki mazoezi ili tukomeshe vikwazi mbalimbali vya afya.
    2. mke huhitaji kuvishwa lakini mgomba sharti upaliliwe ipasavyo.
    3. tujifunze umuhimu wa mazoezi ya viungo ili tuimarishe utendakazi watu..
    4. ukakamavu.
  10. Maneno si shani yanamaanisha si
    1. vigumu.
    2. muhali.
    3. ajabu.
    4. kawaida.

INSHA

Umepewa dakika 40 kuandika insha yako. Andika insha ya kusisimua zaidi itakayomalizika kwa maneno yafuatayo.

.............. Ushindi huo haukutujia vivi hivi. Bila shaka, tulijibiidisha na kushirikiana ipasavyo.

MARKING SCHEME

  1. C
  2. B
  3. D
  4. A
  5. B
  6. C
  7. C
  8. A
  9. D
  10. B
  11. D
  12. A
  13. C
  14. D
  15. B
  16. A
  17. C
  18. B
  19. D
  20. D
  21. A
  22. C
  23. B
  24. D
  25. D
  26. C
  27. A
  28. C
  29. D
  30. A
  31. C
  32. B
  33. D
  34. A
  35. A
  36. D
  37. B
  38. C
  39. D
  40. B
  41. B
  42. D
  43. A
  44. C
  45. A
  46. B
  47. D
  48. B
  49. A
  50. C
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Questions and Answers - Class 8 Mid Term Exams Term 1 2023 Set 11.


Tap Here to Download for 30/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students