Wednesday, 25 October 2023 08:37

Kiswahili Questions and Answers - Grade 6 End Term 3 Exams 2023 Set 1

Share via Whatsapp

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yanayofuata.

G6SwaET3S12023Q1

Siku moja wakati wa likizo, nyanya alitusimulia kisa cha kuhuzunisha mno. Sote tulikusanyika karibu na moto na kutulia tuli. Kila mmoja alikuwa kwa hamu na hamumu ili kupata uhondo wa hadithi ambayo angetutambia.

Baada ya kutulia kama maji ya mtungi na kujikohoza kidogo, alianza hivi, "Hadithi, hadithi..."Sote tulijibu,
"Hadithi njoo." Kisha akaendelea, "Hapo zamani za kale, zama za kuumbwa kwa ulimwengu, binadamu walifaa kupewa ujumbe muhimu mno. Ujumbe huo ndio uliofaa kuamua iwapo wangekuwa wakifa au waishi milele. Wapo walioomba ili ujumbe mzuri uwafikie. Kila mmoja alisubiri akielewa kuwa subira huvuta heri. Kinyonga ndiye aliyepewa ujumbe wa uhai. Ndege naye alipewa ujumbe wa kifo. Yule ambaye angetangulia kufikisha ujumbe, ndiye ambaye angeamua hatima ya binadamu. Wote walipewa amri kuwa waondoke kuelekea kwa binadamu.

Kinyonga alikuwa kobe kama ilivyo desturi yake. Ndege naye alipaa angani kwa kasi kama umeme. Kufumba na kufumbua, binadamu walimwona ndege akiwasili na kifurushi cheusi tititi kama makaa. walikipokea huku nyoyo zao zikidunda dududu! Wote waliangua kilio kwa huzuni walipotambua kuwa kifurushi hicho kilikuwa kimebeba kifo. Kinyonga alionekana akijikokota kwa mbali akiwa na ujumbe wa uhai. Tangu siku hiyo, binadamu walianza kufa." Baada ya kisa cha nyanya, tulijikokota kwa huzuni tukienda kulala.

  1. Maneno 'kutulia kama maji ya mtungi' ni mfano wa fani gani ya lugha?
    1. nahau
    2. istiara
    3. tashbihi
    4. kisawe
  2. Hali ya kinyonga ilifaa kurekebishwa kwa methali gani?
    1. Haraka haraka haina baraka.
    2. Chelewa chelewa utapata mwana si wako.
    3. Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.
    4. Achanikaye kwenye mpini hafi njaa.
  3. Kulingana na kifungu, ni kweli kuwa;
    1. binadamu alianza kufa tangu alipoumbwa. 
    2. binadamu walianza kufa baada ya kupokea ujumbe wa kinyonga.
    3. ndege ndiye aliyepewa habari za uhai.
    4. kifo cha binadamu kilitokana na kupokezwa ujumbe wa kifo kwanza.
  4. Maneno 'nyoyo zao zikidunda dududu' yanaonyesha kuwa binadamu walikuwa na;
    1. wasiwasi
    2. woga
    3. hasira
    4. huzuni
  5. Mwandishi anaposema kuwa 'kinyonga alikuwa kobe', ana maana gani?
    1. Alijifunika kama gamba la kobe
    2. Alilemewa na uzito wa mzigo aliobeba
    3. Alishindana na ndege kwa kasi
    4. Alienda polepole kama kobe
  6. Unadhani kwa nini wajukuu walijikokota kwa huzuni wakielekea kulala?
    1. Walimhurumia kinyonga
    2. Walikasirishwa na haraka ya ndege 
    3. Hawakufurahia tukio lililosababisha kifo
    4. Walihuzunishwa na uzee wa nyanya

Soma ufahamu unaofuata kisha ujibu maswali yanayofuata.

G6SwaET3S12023Q2

Juma, Hekima, Hidaya na Malkia ni wafanyabiashara. Wao ni wafanyabiashara ambao hulipa ushuru wa mapato kila mwisho wa mwezi. Juma huuza
vipuri vya magari, magari yenyewe na pikipiki. Hekima huuza magurudumu ya magari, baiskeli za watoto na pikipiki. Hidaya naye huuza baiskeli za watoto, pikipiki, vioo vya magari na magurudumu. Malkia huuza bidhaa zote zinazouzwa na Juma pamoja na fanicha katika duka jingine.

Juma ana maduka katika miji ya Kisumu, Mombasa na Kericho. Ukitaka kupata maduka ya Hekima, utayapata katika miji yote iliyo na maduka ya Juma pamoja na Nairobi na Naivasha. Hidaya naye ana maduka katika miji ya Molo, Nakuru, Naivasha na Mombasa. Malkia ana maduka katika miji yote kunakopatikana maduka ya Hidaya pamoja na Nairobi na Kisumu.

  1. Bidhaa gani ambazo huuzwa na kila mwanabiashara?
    1. pikipiki
    2. baiskeli za watoto
    3. magurudumu
    4. magari 
  2. Ni nani aliye na maduka katika miji mitano?
    1. Juma
    2. Hekima
    3. Hidaya
    4. Malkia 
  3. Mji gani ambako maduka ya wafanyabiashara hawa wote yanapatikana?
    1. Nairobi
    2. Naivasha
    3. Kisumu
    4. Mombasa

Soma mazungumzo yafuatayo kisha ujibu maswali yanayofuata.
(Wanafunzi wawili wanaonekana uwanjani wakati wa jioni, baada ya masomo ya siku.)

NZOLA : Hujambo Njeri? Unaendeleaje? (Akimnyoshea mkono.)
NJERI:    (Anamwangalia kwa makini, akimsalimia.) Sijambo rafiki yangu Nzola. Ninaendelea vyema. Nimefurahia sana kipindi cha leo kuhusu                         usafi  wa kibinafsi.
NZOLA: Enhe! Niambie mwenzangu.
NJERI:   Nimebaini umuhimu wa vitu kama vile mswaki, taulo, hanchifu, sabuni na kadhalika.
NZOLA(Akitikisa kichwa kuonyesha kuelewa.) Nami vilevile nimeelewa kuwa sifai kutumia vifaa kama vile mswaki, taulo na hanchifu pamoja na                   watu wengine.
NJERI:   Ukweli, hivyo ni vifaa vya kibinafsi.
NZOLA:  Kuanzia leo nitahakikisha kuwa ninaangua kucha na kupiga mswaki bila kuchoka.
NJERI:    Aha! Nami sina budi kuoga na kuinawa mikono yangu kwa njia inayofaa.
NZOLA:  Hewala Njeri. (Mlio wa kengele unasikika.)
NJERI:    Twende nyumbani mwenzangu. (Wanaondoka.)

  1. Kulingana na mazungumzo, ni kweli kuwa;
    1. Njeri hakujua umuhimu wa baadhi ya vifaa vya usafi.
    2. Nzola alielewa faida ya kutumia vifaa vya usafi pamoja na wengine.
    3. Njeri alifahamu kuwa si vizuri kutumia vifaa kama vile hanchifu na wengine.
    4. Njeri alijua umuhimu wa baadhi ya vya usafi.
  2. Yawezekana kuwa wanafunzi hao walipokutana, jua lilikuwa upande gani?
    1. mashariki
    2. kaskazini
    3. kusini
    4. magharibi
  3. Mwandishi alimaanishi nini aliposema kuwa 'nami sina budi'?
    1. Ninajua umuhimu
    2. Ninalazimika
    3. Ninafahamu
    4. Nina hiari
  4. Nahau 'ninaangua kucha' ina maana gani jinsi ilivyotumika katika mazungumzo?
    1. Ninakata kucha
    2. Ninaosha kucha
    3. Ninapangusa kucha
    4. Ninalinganisha kucha
  5. Mazungumzo haya ni mfano wa;
    1. mazungumzo katika muktadha rasmi
    2. mazungumzo yasiyofuata sheria
    3. mazungumzo katika muktadha usio rasmi 
    4. mazungumzo yasiyo na manufaa
  6. Kipi si kifaa cha kibinafsi kati ya vifaa vifuatavyo kulingana na mazungumzo?
    1. hanchifu
    2. mswaki
    3. taulo
    4. sabuni

Jaza nafasi zilizoachwa kwenye kifungu kifuatacho kwa jibu linalofaa.

Kulipa ushuru kuna manufaa sio tu kwa mtu binafsi ___16___ kwa nchi yote. Taifa ___17___ wananchi wanaolipa ushuru. ___18___ hatua kimaendeleo kila siku. Kulipa ushuru ___19___ kuwa mtu huyo ni mzalendo. Ombi ___20___ kwa kila mmoja wetu ni kuwa tulipe ushuru bila kuchelewa ili kuimarisha Kenya.

   A  B  C  D
 16.  mbali pia  lakini pia  bali pia  wala tena 
 17.  yenye  lenye   chenye   zenye 
 18.  hupigwa  hupigia  hupiga  hupigisha
 19.  kunaonyesha  unaonyesha  anaonyesha  wanaonyesha
 20.  langu  yangu  wangu  changu


Jibu maswali yafuatayo kulingana na maagizo.  

  1. Soma ni kwa 'somea' kama vile fua ni kwa ______________________________
    1. fuliwa
    2. fuliana
    3. fuia
    4. fulia  
  2. Neno gani lililo na silabi nne?
    1. lima
    2. kimbiliwa
    3. mbio
    4. lia
  3. Sentensi gani iliyoakifishwa kwa usahihi? 
    1. Walikula matunda kadhaa: mananasi, machungwa na maparachichi.
    2. Salaala! kumbe anaupenda usafi kiasi hicho.
    3. Je! Mwalimu wenu wa Kiswahili ni nani?
    4. Ngombe yule wa mjomba atafungwa wapi?
  4. Chagua sentensi inayoonyesha hali ya masharti.
    1. Waliokuwa wakisoma wameenda kula. 
    2. Angali anamsaidia mzee huyo kuvuka mto.
    3. Amina na mwikali husoma mara kwa mara.
    4. Ukimsaidia kijana huyo utabarikiwa na Mungu.
  5. Sentensi ipi inayoonyesha istiara?
    1. Mwanafunzi mwenye bidii kama mchwa ametuzwa.
    2. Yeye anajua kuwa bidii hulipa.
    3. Tumia hanchifu unapopenga kamasi.
    4. Babu yangu ni kobe, hajafika nyumbani.
  6. Tambua wakati na hali ya sentensi inayofuata.
    Walikuwa wakiandika mvua ilipoanza kunyesha.
    1. wakati uliopita, hali endelezi
    2. wakati ujao, hali endelezi
    3. wakati uliopita, hali timilifu
    4. wakati ujao, hali timilifu
  7. Nomino zipi zinazopatikana katika ngeli moja?
    1. mafuta, maradhi, matunda
    2. minyoo, mikahawa, mirathi
    3. chai, damu, kahawa
    4. kunguru, kuimba, kutu
  8. Onyesha ukubwa wa sentensi inayofuata.
    Jicho la ndovu liliumizwa na miti hiyo. 
    1. Jijicho la dovu liliumizwa na jiti hilo.
    2. Jijicho la dovu liliumizwa na majiti hayo.
    3. Kijicho cha kidovu kiliumizwa na kijiti hicho.
    4. Jijicho la jidovu jiliumizwa na majiti hayo.
  9. Chagua kinyume cha sentensi inayofuata
    Buda alicheka aliponunuliwa pora na kijana mnene.
    1. Shaibu alilia alipouziwa tembe na mzee mwembamba.
    2. Ajuza alilia alipouziwa tembe na mzee mwembamba.
    3. Buda hakucheka aliponunuliwa pora na kijana mnene.
    4. Bikizee alilia alipouziwa tembe na msichana mkonde.
  10. Halima alianza safari saa mbili kasorobo, safari hiyo ilichukua muda wa saa moja na robo. Je, aliwasili saa ngapi?
    1. 9:00
    2. 3:00
    3. 3:30
    4. 9:30

INSHA

Andika insha ya kusisimua ukianzia kwa maneno haya:-

Kipenga kilipolia, wachezaji wa timu zote mbili walijitosa uwanjani

MARKING SCHEME

  1. C
  2. B
  3. D
  4. A
  5. D
  6. C
  7. A
  8. B
  9. D
  10. A
  11. D
  12. B
  13. A
  14. C
  15. D
  16. C
  17. B
  18. C
  19. A
  20. A
  21. D
  22. B
  23. A
  24. D
  25. D
  26. A
  27. C
  28. B
  29. B
  30. A
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Questions and Answers - Grade 6 End Term 3 Exams 2023 Set 1.


Tap Here to Download for 30/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students