Wednesday, 19 April 2023 07:59

Kiswahili Questions and Answers - Grade 6 End Term 1 Exams 2023 Set 3

Share via Whatsapp

SEHEMU YA KWANZA   (Alama 5)

Kusikiliza na kuzungumza 

Soma mazungumzo yafuatayo kisha ujibu maswali. 

G6SwaT1TW23003P1

(Mama ameketi kochini akifuma sweta. Anaiwacha shughuli yake anapomwona Amara

Amara: (akimkaribia mama) Shikamoo mama? 
Mama:  (kwa tabasamu) Marahaba binti yangu! Umeshindaje shuleni?
Amara: Vyema mama! (kimya) Nikwambie tuliyoyasoma?
Mama:  Naam, niambie mwanangu
Amara: Tulifunzwa kuhusu mabadiliko ya hali ya anga. 
Mama:  Mafunzo mazuri sana. Ni kweli kuwa hali ya anga hubadilikabadilika na kuleta misimu mbalimbali. 
Amara: Lakini mama, sikuelewa vizuri kwa sababu nilikuwa nikisinzia kwa sababu ya mafua. 
Mama:  Pole! Nitajaribu kukuelezea. Kwanza kuna msimu wa kiangazi ambao huwa na jua kali. Hali hii huleta ukame.
Amara: Je, kuna kipupwe? 
Mama:  Naam mwanangu. Hukupitwa na kila kitu. Kipupwe ni majira ya baridi kali. Wakati huu watu wanafaa kuvaa mavazi                             mazito ili kupata joto. 
Amara: Ninaelewa mama. Nakumbuka pia kuna msimu wa mvua nyingi bali sikumbuki jina lake. 
Mama:  Msimu au majira haya huitwa masika. Sanasana wakati huu wakulima hupanda kwa sababu kuna maji ya kutosha. Isitoshe                  huwa kuna mafuriko na watu hufaa kutahadhari. 
Amara: Kuna msimu unaitwa kivuli? 
Mama:  Sio kivuli mwanangu. Ni vuli au mchoo. Wakati huu mvua huwa ndogondogo. 
Amara: (Kwa furaha) Umeelezea misimu minne na ninakumbuka mwalimu akisema kuwa angetufunza minne. 
Mama: Nina furaha kuwa nimeweza kukusaidia kuelewa zaidi yale mliyofunzwa shuleni leo. 
Amara: Asante mama! Hakika umenifaa sana. 

  1. Amara alipoulizwa na mama alivyoshinda shuleni alimjibu vipi? 
    1. Naam 
    2. Vyema 
    3. Shikamoo 
    4. Marahaba
  2. Maneno yafuatayo yametumiwa katika mazungumzo. Lipi halionyeshi adabu? 
    1. Pole 
    2. Naam
    3. Asante 
    4. Je 
  3. Ni jibu lipi linaloonyesha misimu ambayo mama alimfunza Amara?
    1. Kivuli, ukame, mchoo, masika 
    2. Ukame, kiangazi, masika, kipupwe 
    3. Kipupwe, kiangazi, vuli, masika 
    4. Masika, kivuli, kiangazi, kipupwe 
  4. Ni kauli gani si sahihi kulingana na mazungumzo haya? 
    1. Amara hakuelewa chochote darasani. 
    2. Amara alikuwa na ugonjwa wa malaria 
    3. Akina amara walifundishwa kuhusu misimu mbalimbali. 
    4. Mama yake Amara anaelewa misimu vizuri.
  5. Neno misimu limetumika katika mazungumzo kisawe chake ni gani?
    1. Anga 
    2. Majira 
    3. Ukame 
    4. Mabadiliko 

Swali la 6 hadi la 9 

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

G6SwaT1TW23003P2

Hospitali kuu ya Ubora inapatikana katika kaunti ya Kinga. Hii ni mojawapo ya hospitali nyingi katika kaunti hii. Hospitali hii imegawanywa katika sehemu tofauti kila moja ikishughulikia ugonjwa mmoja. Hospitali hii ni ya kipekee. Wagonjwa wengi huenda hapa wanapougua. 

Madaktari wa Ubora ni wenye bidii ya mchwa. Huwa wanashughulika kama nyuki mzingani. Kila mmoja huwa anahudumia wagonjwa wake kwa upendo na heshima. Wauguzi pia husaidiana na madaktari ili kuhakikisha wagonjwa wamepata tiba inayofaa na kwa haraka. Hakuna anayefanya uzembe kazini kisa na maana wanaamini kuwa bidii huleta ufanisi. Wapo wanaoshughulikia magonjwa ya kuambukiza, matatizo ya macho, shida za mifupa, ndwele za mfumo wa hewa, moyo na magonjwa mengineyo. Hakika, kila mmoja huwa na shughuli yake. 

Jitihada za wafanyakazi wa hospitali hii huwasaidia wagonjwa wengi kupata matibabu na kuwa na afya bora. Hakujawahi kuwa na visa vya wagonjwa kutohudumiwa vyema hapa. Magonjwa ya aina zote hukabiliwa. Isitoshe huwashauri watu kujikinga na maradhi kwani kinga ni bora kuliko tiba. Aidha huwatuma madaktari kufundisha umma kuhusu umuhimu wa afya bora na za kuzuia magonjwa. Kusema kweli hakuna hospitali nyingine katika kaunti ya Kinga inaishinda hii. 

  1. Ni jibu lipi sahihi kulingana na aya ya kwanza? 
    1. Katika kaunti ya Kinga kuna hospitali moja tu. 
    2. Magonjwa yote hutibiwa sehemu moja. 
    3. Hospitali ya Ubora hushughulikia magonjwa machache. 
    4. Hospitali ya Ubora ndiyo bora zaidi kauntini.
  2. Kulingana na aya ya pili ni sehemu gani ndani ya mwili huathiriwa na shida ya mfumo wa hewa? 
    1. Figo 
    2. Kibofu 
    3. Mapafu
    4. Moyo
  3. Ni njia gani madaktari. huwasaidia wananchi kujikinga na magonjwa?
    1. Kuwashauri kujikinga na maradhi.
    2. Kuwatibu haraka.
    3. Kushirikiana na wauguzi. 
    4. Kuwafundisha kuhusu lishe bora. 
  4. Ni Methali gani imetumika katika kifungu hiki?
    1. Bidii ya mchwa 
    2.  Kila mmoja huwa na shughuli yake
    3. Shughulika kama nyuki mzingani
    4. Kinga ni bora kuliko tiba 

Swali la 10 hadi la 12 

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali. 

G6SwaT1TW23003P3

Wanafunzi wa gredi ya sita katika shule ya msingi ya Busara wamegawanywa katika makundi manne.Makundi haya ni: Upendo, Amani, Subira na Umoja. Kila kikundi huwa na sehemu tatu za kutunza usafi kila juma. 

Tazama jedwali la juma hili kisha ujibu maswali. 

 VIKUNDI   JUMATATU   JUMATANO   IJUMAA 
 Upendo  darasani   chumba cha maakuli   msalani 
 Amani  msalani   majilisini  darasani 
 Subira  chumba cha maakuli   msalani   majilisini
 Umoja  majilisini  darasani   chumba cha maakuli 
  1. Ni kikundi kipi hakikusafisha darasa? 
    1. Subira 
    2. Amani 
    3. Umoja 
    4. Upendo
  2. Ni kikundi kipi hakikusafisha majilisi? 
    1. Subira 
    2. Umoja
    3. Upendo
    4. Amani
  3. Ni kikundi kipi hakikusafisha chumba cha maakuli
    1. Upendo
    2. Amani
    3. Subira 
    4. Umoja 

Swali la 13 hadi la 15 

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali. 

G6SwaT1TW23003P4

Ugali ni chakula kinachopendwa na watu wengi sana. Njia ya kupika si ngumu. Kwanza, lazima uwe na unga wa mahindi, maji, sufuria, mwiko na jiko la kupikia lenye moto. Pima kiasi cha maji unayohitaji na kuyatia kwenye sufuria safi. Injika sufuria. Yapatie maji muda yachemke. Tia unga kidogo kidogo ndani ya maji yanayochemka, huku ukikoroga kwa mwiko.Ongeza unga kulingana na unavyotaka ugali wako uwe. Ukitaka ugali mgumu, endelea kuongeza unga. Ngoja ugali uive kwa joto la wastani. 

Ugali huandaliwa kwa vitoweo vya aina mbalimbali kama vile: Maziwa yaliyochachuka, mboga za kiasili kama vile mchicha, samaki au nyama.Kusema kweli ugali ni chakula cha kipekee. 

  1. Hatua ya kwanza ya kupika ugali ni ipi? 
    1. Kuwa na vitu utakavyohitaji kupika ugali.
    2. Kuinjika sufuria yenye maji jikoni.
    3. Kuchukua mwiko na kuanza kukoroga.
    4. Kuwa na kitoweo ambacho unahitaji.
  2. Neno injika lina maana gani
    1. Kuosha 
    2. Kuweka sufuria jikoni
    3. Kuchoma 
    4. Kuchemsha
  3. Ugali humwongeza mtu ___________________________ mwilini.
    1. Udhaifu
    2. Urefu
    3. Unyonge 
    4. Nguvu 

Swali la 16 hadi la 20 

Soma kifungu kifuatacho. Kwa kila swali umepewa majibu manne. Chagua jibu lifaalo zaidi kati ya yale uliyopewa

Johari alishiriki ___16___ michezo tofauti tukiwa shuleni. Michezo ___17___ alipenda sana ni kandanda na kuogelea. ___18___ na timu ya mchezo wa kandanda alipoingia gredi ___19___nne. Alifanya bidii na kuiletea timu yake ushindi. Alifahamu kuwa ___20___.

   A   B    C   D 
 16.   kwa   kwenye   katika   ndani ya 
 17.  ambapo   ambayo   ambazo   ambako 
 18.  Alikuunga   Aliwaunga   Alijiunga   Alituunga 
 19.  ya  wa  la  za
 20.  kidole kimoja hakivunji chawa   mtaka cha mvunguni sharti  ainame    asiyesikia la mkuu huvunjika  guu   mtoto umleavyo ndivyo  akuavyo 

Swali la 21 hadi la 30 

Chagua jibu sahihi. 

  1. Kiungo hiki cha mwili kinaitwaje?
    G6SwaT1TW23003P5 
    1.  Figo
    2.  Ini
    3. Moyo
    4. Pafu
  2. Nomino hizi ni za aina gani? Wingu la nzige, pakacha la matunda, bunda la noti na robota la pamba. 
    1. Kawaida 
    2. Wingi
    3. Makundi
    4. pekee
  3. Chagua wingi wa: Ukuta mrefu umejengwa na fundi mzuri. 
    1. Kuta ndefu zimejengwa na mafundi wazuri. 
    2. Kuta ndefu zimejengwa na fundi wazuri.
    3. Ukuta mrefu zimejengwa na fundi wazuri.
    4. Kuta ndefu zimejengwa na mafundi wabaya.
  4. Tenda ni kwa tendea, chora ni kwa _____________________ 
    1. Choresha 
    2. Chorea 
    3. Choreshwa 
    4. Choreshea 
  5. Ni kauli gani sahihi kuhusu bendera ya Kenya?
    1. Ina rangi tano
    2. Katikati imechorwa mkuki na ngao 
    3. Rangi ya juu ni kijani
    4. Rangi ya chini ni nyeusi
  6. Kati ya Maneno haya gani si la adabu? 
    1. Asante
    2. Tafadhali
    3. Karibu
    4. Ninataka
  7. Chagua ukubwa wa sentensi ifuatayo: Mlango wa nyumba yake unapendeza. 
    1. Lango la jumba lake linapendeza.
    2. Mlango wa jumba lake linapendeza. 
    3. Lango la nyumba yake linapendeza.
    4. Mlango wa nyumba yake linapendeza.
  8. Chagua jibu lisilo sahihi.
    1. Watano ni kivumishi cha idadi
    2. Mimi ni kiwakilishi cha nafsi
    3. Huyu ni kivumishi kiashiria
    4. Gani? ni kivumishi cha sifa 
  9. Ni nini maana ya msemo kupiga chafya
    1. Kuchemua.
    2. Kukohoa. 
    3. Kutema. 
    4. Kupenga.
  10. Sentensi hii imetumia tamathali gani ya lugha. Bawabu wetu ni mkali kama simba. 
    1. Istiara 
    2. Methali
    3. Tashbihi
    4. Kitendawili

INSHA

Andika insha ya kusisimua kuhusu mada ifuatayo: 

SIKU YA MICHEZO SHULENI MWETU 

MARKING SCHEME

  1. B
  2. D
  3. C
  4. B
  5. B
  6. D
  7. C
  8. A
  9. D
  10. A
  11. C
  12. B
  13. A
  14. B
  15. D
  16. C
  17. B
  18. C
  19. A
  20. B
  21. C
  22. C
  23. A
  24. B
  25. B
  26. D
  27. A
  28. D
  29. A
  30. C

 

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Questions and Answers - Grade 6 End Term 1 Exams 2023 Set 3.


Tap Here to Download for 30/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students