Thursday, 03 February 2022 12:30

Kiswahili Questions and Answers - Class 7 End Term 3 Exam 2022 Set 1

Share via Whatsapp

MASWALI

Soma vifungu vifuatavyo. Vina nafasi 1 mpaka 15. Kwa kila nafasi umepewa majibu manne hapo. Jaza kila pengo kwa kuchagua jawabu lifaalo zaidi.
Sherehe za kuukamilisha mwaka na kuanza mwaka____1__huwa na shamrashamra chungu nzima. Siku ya mwisho ya mwaka_ 2_huonyesha mwanzo wa sherehe hizo. Watu hukesha 3 wakiwa makanisani, katika vyumba vya burudani au maeneo mengine ya 4 Usiku, wakati wa saa sita kamili, watu__5_mwaka mpya kwa shangwe, hoihoi na vigelegele. Wengi huadhimisha mwaka mpya kwa njia tofauti. Wengine huvaa nguo mpya__6__ kupendeza huku wengine wakichinja kulingana na uwezo _7_ . Watu 8 , huamkuana kwa kutakiana heri njema na mwaka mpya wenye mafanikio _9_ .

  1.                    
    1. mingine
    2. ingine
    3. mwingine
    4. nyingine
  2.                    
    1. unayokamilisha
    2. unaokamilika
    3. unaokamilisha
    4. unayokamilika
  3.                        
    1. mchana kucha
    2. mchana kutwa
    3. usiku kucha
    4. usiku kutwa
  4.                    
    1. kujifurahisha
    2. kukufurahisha
    3. kumfurahisha
    4. kutufurahisha
  5.                    
    1. huyapokea
    2. hulipokea
    3. huipokea
    4. huupokea
  6.                
    1. za 
    2. ya
    3. la
    4. mwa
  7.                          
    1. wake
    2. wangu
    3. wako
    4. wao
  8.                      
    1. wamepokutana
    2. walipokutana
    3. wanapokutana
    4. wangepokutana 
  9.                    
    1. mingi
    2. tele
    3. haba
    4. nadra

Kila mzazi au mlezi__10_jukumu__11__ kumkuza mtoto kwa njia inayofaa. Ni lazima ahakikishe kuwa mtoto huyo anapata mahitaji ya 12 katika maisha. Mahitaji hayo ni kama vile___13_ .___14__, mzazi au mlezi anafaa kuwa kielelezo bora kwa mtoto. Ajue kuwa mtoto huiga tabia zake. Hii ndiyo sababu wahenga wakasema kuwa____15___.

  1.                      
    1. ana
    2. hana
    3. hawana
    4. wana 
  2.                      
    1. la
    2. ya
    3. wa
    4. kwa
  3.                  
    1. kijumla
    2. kitaifa
    3. kimsingi
    4. kijuujuu
  4.                          
    1. masomo, makao na malazi
    2. chakula, makao na mavazi
    3. malezi, elimu na
    4. usafiri matibabu, chakula na malezi 
  5.                
    1. Na 
    2. Hata hivyo 
    3. Mathalani
    4. Aidha
  6.                          
    1. asiyesikia la mkuu huvunjika guu
    2. mwana hutazama kisogo cha nina
    3. fimbo ya mbali haiui nyoka
    4. uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi
  7. Chagua udogo wa sentensi ifuatayo.
    Mtoto aliumiza uso wa mbwa. 
    1. Toto liliumiza juso la jibwa.
    2. Kitoto kiliumiza kijuso cha kijibwa.
    3. Kijitoto aliumiza kijuso wa kijibwa.
    4. Kimtoto kiliumiza kiuso cha kimbwa.
  8. Maelezo gani ambayo ni sahihi? 
    1. Watu wakiagana bila matumaini ya kuonana tena huambiana binuru.
    2. Ukitaka kupewa nafasi ya kupita utaomba kwa kusema simile.
    3. Shikamoo ni salamu za mtu mkubwa kwa mdogo.
    4. Sabalheri na masalheri ni mifano ya salamu za asubuhi.
  9. Sentensi gani iliyotumia 'po' kuonyesha mahali? 
    1. Wote walipowasili tulipiga makofi. 
    2. Mlipoegesha magari yenu pana kivuli.
    3. Usiposoma kwa bidii hutapita mtihani. 
    4. Nilipomwona nilijificha ndani ya nyumba.
  10. Tambua sentensi iliyoakifishwa kwa kutumia alama za mtajo.
    1. . Watapikiwa vyakula vingi: Wali, chapatti, nyama, samaki na kadhalika.
    2. Nimeamini kuwa asiyesikia la mkuu... 
    3. Mbung'o wanafonza damu ya ng'ombe.
    4. Nyote leteni madaftari yenu," mwalimu akasema.
  11. Wakati wa machweo jua huwa upande gani wa dira?
    1. Kusini
    2. Kaskazini 
    3. Magharibi 
    4. Mashariki
  12. Sentensi gani ambayo ni sahihi kisarufi?
    1. unga ambao uliomwagika ni huu.
    2. Gari lile jeusi lina abiria wengi.
    3. Angejua njia ya kwenda nyumbani hangepotea. 
    4. Hapo nyumbani kwao kutakuwa na sherehe.
  13. Orodha ipi yenye vivumishi vimilikishi?
    1. wangu, zao, chake
    2. lote, mwingine, yenyewe
    3. safi, mzuri, kitamu
    4. gani, yupi, wangapi
  14. Jibu gani halijaunganisha sentensi zifuatazo kwa usahihi?
    Dhahabu alipewa zawadi. Dhahabu hakufurahi. 
    1. Licha ya Dhahabu kupewa zawadi hakufurahi. 
    2. Dhahabu alipewa zawadi bali hakufurahi.
    3. Ingawa Dhahabu alipewa zawadi hakufurahi.
    4. Dhahabu hakufurahi maadamu alipewa zawadi.
  15. Jaza nafasi kwa jibu linalofaa.
    Kitanda ........................kilivunjika kitatengenezwa.
    1. chenye 
    2. kile
    3. chenyewe
    4. ambacho
  16. Ulinganisho upi ulio na kitenzi
    kilichoundwa kutokana na nomino?
    1. mwandiko - uandishi 
    2. kilio -- mlio
    3. ulinzi - linda
    4. mwalimu - elimu
  17. Petero alikuwa na nusu ya mkate, akawagawia watoto wake wanne vipande sawa. Kila mtoto alipata akisami gani ya mkate?
    1. ½
    2. ¾
    3. 1/6
    4. 1/8
  18. Chagua neno baki kwenye orodha ifuatayo. 
    1. Jogoo
    2. Koo
    3. Jimbi
    4. Kikwara
  19. Tambua nomino ambayo
    haijalinganishwa kwa usahihi na ngeli yake. 
    1. Kipepeo KI-VI 
    2. Moyo U-ZI
    3. Bustani PAKUMU
    4. Ukuti U-ZI
  20. 'Ungewasili mapema usingeadhibiwa' ndiko kusema kuwa
    1. uliadhibiwa kwa kuwa hukuwasili mapema.
    2. kuwasili mapema kulifanya hukuadhibiwa.
    3. kutowasili mapema kulifanya hukuadhibiwa.
    4. kuadhibiwa kwako kulitokana na kuwasili kwako mapema.
  21. Fundi wa kujenga nyumba kwa mawe huitwaje? 
    1. Seremala 
    2. Mwashi
    3. Mhunzi
    4. Malenga 

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 31-40.
Kama kuna kitu ambacho kila mtu hupata kwa kiwango sawa, ni wakati. Kila mtu hupata saa ishirini na nne kwa siku. Haijalishi kama yeye ni tajiri au maskini, wa kiume au wa kike, kijana au mzee. Tofauti kubwa hutokana na namna tunavyoutumia wakati wetu. Je, wewe mwanafunzi unafaa kuutumiaje wakati wako hasa wa likizo? Awali ya yote, utumie wakati wako kuujenga uhusiano wako na Mungu. Hakikisha kuwa unasoma mafundisho kuhusu Mungu na kupiga dua kila wakati ili Jalali akujaalie fanaka kochokocho katika maisha yako. Hakikisha kuwa unaenda maabadini na kushirikiana na wenzako kumpa Mola sifa na kumshukuru. Aisee, mwomba Mungu si mtovu. Mungu ndiye atakayekusaidia kufaulu maishani.
Vilevile, ni jambo la busara kuwasaidia wazazi wako katika shughuli zao. Ni vyema sana kumwaviza mama yako katika shughuli mathalani kuosha vyombo, kufua nguo na kuzipiga pasi, kucheza na wanuna wako na kadhalika. Ikiwa baba yako ana duka pale sokoni, enda dukani pale ili umpige jeki katika shughuli za uuzaji. Unaweza kumsaidia kuwapa wateja bidhaa na kupiga hesabu. Huko kuwasaidia kutakuimarisha katika njia anuwai. Hewaa! Utaelewa kuyafanya mambo mengi ambayo pengine hukuyajua. Usisahau kuwa masomo bado yanaendelea. Hata kama umekamilisha masomo ya shule ya msingi, kumbuka kuwa elimu ni bahari. Naam, elimu haina mwisho. Endelea kusoma vitabu, magazeti na majarida ili upate maarifa chungu nzima kama mchanga wa bahari. Ukipata vitabu vya kidato cha kwanza, viinamie kama mwanasheria atafutaye neno la ushindi katika daawa. Ni nani asiyefahamu kuwa mizizi ya elimu ni michungu lakini matunda yake ni matamu?
Licha ya hayo, shirikiana na watoto wenzako katika michezo kadhaa kijijini penu. Kila unapokamilisha shughuli zako, shirikianeni kama kiko na digali katika michezo kama vile kibe, kurusha tiara, kucheza kandanda na mingineyo. Michezo hii ina faida kochokocho katika maisha. Michezo haichangii kuimarisha tu afya bali pia hukuza maadili. Mnaposhiriki katika michezo, viungo vya mwili huimarika na afya kuwa thabiti. Kumbuka kuwa afya ni bora kuliko mali? Pia, ushirikiano na umoja ujengwao wakati wa michezo ni muhimu kama dhahabu katika maisha ya kila mja. Wahenga hawakutuchezea waliposema kuwa umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.
Aidha, jitolee mhanga na kujikaza kisabuni kuhakikisha kuwa uhifadhi wa mazingira unaendelezwa. Kuhifadhi mazingira kuna manufaa sio kwako tu bali pia kwa jamii nzima. Ukiwa na ndugu na marafiki zako, fanyeni juhudi za mchwa ili kupanda miti na kuitunza Pandeni mbegu za miti mbalimbali kisha msubiri ziote. Pandeni miche hiyo katika sehemu zinazofaa na kunyunyizia maji. Usafi wa mwili na mazingira nao una umuhimu usiopuuzika. Bidii zenu ni muhimu katika kuhakikisha kuwa mnaishi katika mazingira yaliyo safi kama msahafu. Vilevile ninakushauri uwaepuke marafiki wenye tabia mbaya. Marafiki kama hao wanaweza kukuingiza katika mtego wa utovu wa maadili. Kutangamana na watu wenye maadili ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa tabia zako zinakuwa za kuigwa. Hewaa! Mtu ni utu, asiye na utu ana kutu.
Yote tisa, kumi ni kuwa jiepushe na matumizi mabaya ya mtandao. Usiwe mwenye mazoea ya kutazama runinga usiku na mchana. Filamu, picha na video chafu nazo uziepuke kama ugonjwa wa korona. Kumbuka kuwa vitu uvitazamavyo na kuvisikiliza mara kwa mara huathiri tabia zako. Mihadarati nayo ni sumu kali mno. Usijaribu hata kuionja mihadarati hiyo. Wapo wengi walioanza kutumia mihadarati kimzaha tu. Sasa hivi wanajiuma kidole na kulia kilio cha mbwa mdomo juu. Kifo nacho kimewatanulia kinywa cha mamba na kuwakodolea macho ya bundi. Ukitaka kuishi kwa miaka na mikaka, epuka matumizi ya mihadarati.

  1. Kulingana na ufahamu, ni kweli kuwa kila mtu; 
    1. hutumia wakati wake kwa njia sawa na wengine.
    2. hufanya mambo yanayofanana na ya wengine katika wakati wake.
    3. hupata muda unaotoshana na wa wengine.
    4. hupewa wakati kulingana na bidii yake.
  2.  Aya ya kwanza inashauri kuwa mhusika;
    1. aende kanisani kila wakati na kumwomba Mungu.
    2. atumie wakati wake kujenga uhusiano.
    3. ahakikishe kuwa anasoma vitabu vya kutosha.
    4. ampe Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yake.
  3. Kupiga dua' ina maana gani jinsi ilivyotumika katika kifungu?
    1. kusali
    2. kufanya bidii
    3. kusoma
    4. kuendelea
  4. Jambo gani ambalo anayeshauriwa hawezi akafanya akiwa nyumbani kwao? 
    1. Kucheza na ndugu zake
    2. Kusoma
    3. Kuuza dukani
    4. Kufua nguo na kuzipiga pasi
  5. ...mizizi ya elimu ni michungu lakini matunda yake ni matamu...' ni maneno yenye maana gani? 
    1. Masomo yenyewe ni kama mizizi ikiwa pamoja na matunda.
    2. Faida za masomo hutokea baada ya kuvumilia hali ngumu tunaposoma 
    3. Matatizo ya masomo huwa mengi na yenye uchungu hadi mwisho. 
    4. Mazao ya mimea hayawezi yakawa matamu iwapo mizizi si michungu.
  6. Ufahamu unaeleza kuwa michezo huimarisha
    1. maadili na uchumi.
    2. umoja na viungo.
    3. afya na uhusiano.
    4. afya na tabia.
  7. Kulingana na aya ya nne, anayetaka kuwa na tabia nzuri anashauriwa kufanya nini? 
    1. Kufuata ushauri wa walimu na wazazi
    2. Kuandamana na marafiki watovu wa nidhamu
    3. Kutembea na marafiki wenye tabia nzuri
    4. Kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na tabia mbaya
  8. Aya ya mwisho inashauri kuwa;
    1. mhusika asitumie mtandao ili asiwe na tabia mbaya.
    2. mhusika asitazame runinga usiku wala mchana.
    3. mhusika aepuke ugonjwa wa Korona.
    4. mhusika awe mwangalifu anapotumia mtandao.
  9. Nini kinacholinganishwa na sumu katika ufahamu?
    1. mtandao
    2. dawa za kulevya
    3. uvivu
    4. tabia mbaya
  10. Kulingana na aya ya mwisho, mtu asiyetumia mihadarati 
    1. huishi bila magonjwa yoyote.
    2. huwa na marafiki wengi.
    3. huishi kwa muda mrefu.
    4. hufaulu maishani.

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 31-40.
Mathayo alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Eshikalame. Alikuwa mtoto mwerevu sana. Mungu alimjalia akili za sumaku. Alinasa kila kilichofundishwa na mwalimu yeyote. Alifaulu katika masomo mengi. Wanafunzi wengi walitamani sana kuwa kama yeye. Wengi walimwendea kwa ushauri na msaada wa kimasomo. Hata hivyo, Mathayo mwenyewe hakuishi maisha ya furaha. Umaskini wao kule nyumbani ulimuudhi. Alikuwa na mzazi mmoja pekee aliyefanya kazi za kijungujiko pale kijijini ili kukidhi mahitaji ya mwanawe wa pekee. Zaidi ya umaskini huo, kilichomkasirisha zaidi ni hali ya mama yake kimaumbile. Mama yake alikuwa na jicho moja tu, alikuwa chongo. Mathayo hakutaka kabisa kujihusisha na mama yake. Alidhani kuwa wenzake walimcheka kutokana na ulemavu wa mama yake.
Katika shule ya upili, Mathayo hakuwahi kumwita mama yake katika mkutano wowote wa wazazi shuleni. Wakati wa likizo, alienda tu nyumbani kwa kukosa mahali pengine pa kuelekea. Mama alipomuuliza kwa nini wazazi hawakwenda shuleni kwa mkutano wowote, alisema kuwa walimu walitaka kuutumia muda wao katika masomo ya wanafunzi badala ya kupoteza muda wakifanya mikutano na wazazi. Mathayo aliendelea kuwa mchwa katika masomo. Alitia fora katika kidato cha kwanza hadi cha nne. Kama hakuwa nambari ya kwanza, alikuwa ya pili au ya tatu. Katika mtihani wa kidato cha nne, alipata alama za kumezewa mate. Alijiunga na chuo kikuu katika jiji moja katika nchi hiyo. Katika chuo hicho hakulegeza kamba. Alipokamilisha masomo yake, alipata kazi iliyokuwa na mshahara mzuri. Matatizo aliyopitia kitambo aliyasau kabisa.
Ajabu ni kwamba Mathayo hakutaka kabisa kurudi kijijini kule ambako mama yake aliishi. Wanakijiji walishangaa walipomwona mama yule akiendelea kuteseka katika maisha ya umaskini. Ilipotokea kuwa Mathayo ameenda kijijini, japo kwa nadra sana, hakukaa kwa zaidi ya saa nne. Alimbagia mzigo wa bidhaa na kung'oa nanga kurudi kule mjini. Mkewe alipomwuliza kuhusu wazazi wake, alisema kuwa alikuwa yatima. Alimweleza kwamba alikuzwa na kusomea katika makao ya watoto wasiokuwa na wazazi.
Siku moja Mathayo alipata ujumbe kuwa mama yake alikuwa mgonjwa, hali mahututi kule nyumbani. Aliingia ndani ya shangingi lake na kutua kijijini. Mama alikuwa hajiwezi kutokana na ugonjwa. Hakujua aingiaye wala atokaye. Kwenye meza palikuwa na barua, "Kwa mwanangu Mathayo. Mimi ninaona ni kama nitaaga dunia kutokana na ugonjwa huu. Hata kama sijakuachia chochote cha maana, ninakuachia jicho langu. Ulipokuwa mdogo, uligongwa na kijiti mkicheza na wenzako. Jicho lako liliumia kiasi cha kutoweza kuona tena. Nilijitolea kulipeana jicho langu moja ili wewe mwanangu usiwe chongo bali uyaone maisha vizuri. Hii ndiyo sababu huwa sina jicho moja mwanangu. Kwaheri ya kuonana."
Mathayo alipigwa na butwaa nusura azimie. Kwa kasi ya umeme, mama yake aliingizwa katika gari na kukimbizwa hospitalini. Mathayo aliagiza afanyiwe matibabu ya hali ya juu zaidi hadi apate nafuu. Pale kwenye pambajio, Mathayo alilia kwa kite huku akimfafanulia mkewe kisa cha maisha yake tangu mwanzo hadi mwisho.

  1. Aya ya kwanza inaeleza kuwa;
    1. Mathayo alifaulu katika masomo yote shuleni.
    2. Mathayo alikuwa na mzazi mmoja baada ya kifo cha baba yake.
    3. Mathayo alichekwa na wenzake kutokana na ulemavu wa mama yake
    4. Mathayo hakupendezwa na umaskini wao na ulemavu wa mama yake.
  2. Kulingana na ufahamu, 'kazi za kijungujiko' ni kazi zenye;
    1. kutumia nguvu nyingi
    2. kufanywa kwa kulazimishwa
    3. kufanywa kwa ushirikiano
    4. malipo ambayo ni kidogo
  3. Katika shule ya upili,
    1. Mathayo aliongoza katika mitihani iliyofanywa 
    2. Walimu hawakutaka kupote wakifanya mikutano na wazazi. 
    3. Mathayo alifanya vizuri katika mitihani yote. 
    4. Mathayo aliwaambia wenzake kuwa alikuwa yatima.
  4. Maneno 'aliendelea kuwa mchwa' ni mfano wa fani gani ya lugha?
    1. Tashbihi
    2. Sitiari
    3. Nahau
    4. Tanakali
  5. Kifuungu hiki kinaonyesha kuwa Mathayo alikuwa na tabia gani?
    1. mwongo na mwenye bidii
    2. mjanja na mzembe
    3. mjanja na karimu
    4. mwenye bidii na mwaminifu
  6. Methali gani isiyoweza kurejelea ujumbe ulio mwishoni mwa aya ya pili? 
    1. Achanikaye kwenye mpini hafi njaa. 
    2. Dau la mnyonge huendeshwa na
      Mungu.
    3. Baada ya dhiki ni faraja.
    4. Damla mnyonge haliandi inshi
  7. Mathayo alikamilishia masomo yake katika kiwango gani? 
    1. Shule ya msingi
    2. Chuo kikuu
    3. Shule ya chekechea
    4. Shule ya upili
  8. Mama wa Mathayo alikuwa mzazi bora kwa kuwa
    1. alimuuliza mwanawe kwa nini wazazi hawakuitwa shuleni.
    2. alimwandikia mwanawe barua kabla ya kuaga dunia. 
    3. alijinyima na kujikosesha ili mwanawe aishi vizuri.
    4. alimlipia mwanawe karo katika shule nzuri zaidi nchini.
  9. Unadhani kwa nini Mathayo alikuwa akilia katika aya ya mwisho? 
    1. Hakutamani kulitumia jicho alilopewa na mama yake.
    2. Aliona aibu kumweleza mkewe kuwa huyo ndiye aliyekuwa mama yake.
    3. Alihuzunishwa na habari za kifo cha mama yake.
    4. Aliaibikia maovu aliyomtendea mama yake.
  10. Funzo kuu linalopatikana katika kifungu hiki ni lipi? 
    1. Tunafaa kuvithamini vilivyo vyetu hata vikiwa havipendezi. 
    2. Hatufai kuwasaidia watoto ambao baadaye watatudharau.
    3. Mtoto asiishi mjini baada ya kukamilisha masomo yake.
    4. Tunafaa kuoa mke wa kutoka katika kijiji chetu ili tusiwadharau wazazi. 

MWONGOZO WA KUSAHISHA

swa jhgadya

INSHA

Andika insha itakayokamilika kwa maneno yafuatayo.

.....................................................Hakika, siku hiyo ilikuwa ya furaha sana. Tuliwasili nyumbani tukiwa tumechoka huku tukicheka kwa furaha na kumshukuru Mungu.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Questions and Answers - Class 7 End Term 3 Exam 2022 Set 1.


Tap Here to Download for 30/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students