Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kapsabet Mock Exams 2023

Share via Whatsapp
MAAGIZO:
  • Jibu maswali manne pekee
  • Swali la kwanza ni la lazima
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki yaani Tamthilia, Riwaya, Ushairi na Hadithi Fupi
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili

                                                                                       SEHEMU A: 

                                                                                   FASIHI SIMULIZI

                                                                                           LAZIMA

  1. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali
    Mimi ni Olichilamgwara
    Olichilamgwara mwana mbee wa Ojilong
    Ojilong wa Marukatipe
    Wazee waliposhindwa
    Nilivuka misitu milima na mito
    Ni mimi jabali
    Kipande cha jifya la mama
    Nilipokuwa nalisha mifugo
    Nilisikia baragumu inalia
    Baragumu ya wito
    Mifugo wa mtemi wamechukuliwa
    Nikachukua mkuki wangu
    Wenye kigumba cha mti
    Nikachukua upanga wangu
    Wenye makali kama mmweso wa radi
    Upanga uliopasua pembe za nyati kwa dhoruba moja
    Ndipo nilipofyatuka kasi kama umeme
    Kufumba kufumbua nikawakaribia nduli
    Kusikia vishindi vyangu wakaanza kubabaika
    Kuona kifua changu cha manyoya ya kanga wakatetemeka
    Macho yangu makali kama kaa la moto yalipowatazama wakakimbia
    Mkuki wangu ulipaa kama umeme
    Wote wakalala
    Mifugo wakanifuata…
    Mko wapi vijana
    Mmekuwa kama majivu baada ya moto kuzimika?

Maswali

  1. Tambua kipera ulichokisoma na udhibitishe jibu lako (al. 2)
  2. Tambua sifa za jamii zinazosawiriwa katika utungo huu (al. 2)
  3. Kwa kutoa mifano bainisha vipengele vine vya kimtindo vilivyotumiwa na nafsineni (al. 4)
  4. Fafanua sifa nne za kipera hiki (al. 4)
  5. Eleza mambo manne ambayo mtendaji wa kipera hiki anaweza kufanya ili kufanikisha utendaji wake. (al. 4)
  6. Fafanua mikakati ambayo jamii inaweza kutumia ili kuzuia tungo kama hizi kufifia            (al. 4)

                                                                                          SEHEMU B: 

                                                           TAMTHILIA: BEMBEA YA MAISHA, TIMOTHY AREGE

  1.  “Sima tayari. Ninaanda mchuzi…..”
    1. Weka dondoo hili katika muktadha wake (al. 4)
    2. Onyesha umuhimu wa msemewa wa maneno haya (al. 6)
    3. Tambua toni katika dondoo hili (al. 2)
    4. Eleza changamoto zinazokumba ndoa za kisasa kwa kurejelea tamthilia nzima (al. 8)
  2. “Masombo hufungwa kama walau mtu ametia kitu mdomoni. Pamoja na hali ngumu iliyopo, bado hatujafikia pa kukosa mlo wa kimsingi. Ndiyo hatumudu viliwa vya samli lakini hatuwezi kuishi kama kwamba tunazongwa na njaa. Tazama ulivyokonda unaelekea kushindana na ng’onda. Hii nafasi ya ng’onda unaitaka kwa nini?
    1. Weka dondoo hili katika muktadha wake (al. 4)
    2. Tambua mbinu mbili za kimtindo zilizomo kwenye dondoo (al. 2)
    3. Bainisha sifa nne za msemewa (al. 4)
    4. Jadili namna msemaji amechangia katika kuendeleza
      1. Ploti (al. 5)
      2. Maudhui (al. 5)

                                                                                               SEHEMU C: 

                                                                             RIWAYA:  Chozi la Heri la 4 au la 5

  1.  
    1. ….haya imekuandama tangu usiku ukimtongoza fulani, siku za kuchora ramani ya Afrika kwa vyanda vya miguu hadi sasa? Ama ni hizo mvi unaficha? Naskia ile mid-life crisis ikiwashika wazee ndiyo hivyo,
      1. Weka dondoo hili kwenye muktadha wake (al. 4)
      2. Tambua mbinu zozote tatu za kimtindo kwenye dondoo hii (al. 3)
      3. Jadili udhaifu wa msemewa (al. 4)
    2. Dhibitisha kauli kwamba ‘Kweli jaza ya hisani ni madhila’
      Kwa kurejelea wahusika tisa kwenye riwaya ya Chozi la Heri (al. 9)

                                                                                    RIWAYA: CHOZI LA HERI

  1.  “Nashangaa kinachompa kijana kama huyu, na wengine waliofariki jana, ambao wamesomea shahada za uzamili, kujihusisha na unywaji wa pombe haramu!
    1.  
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili (al. 4)
      2. Fafanua umuhimu wa msemaji katika dondoo hili (al. 4)
      3. Kando na maudhui ya elimu eleza maudhui mengine mawili katika dondoo hili (al. 2)
    2. Eleza jinsi mwandishi alivyofaulu kutumia mbinu zifuatazo katika kuijenga riwaya hii
      1. Hadithi ndani ya hadithi (al. 5)
      2. Mbinu rejeshi (al. 5)

                                                                                        SEHEMU D:USHAIRI

                                                                                                   USHAIRI

                                                                                         Jibu swali la 6 ay la 7

  1. Soma shairi lifuatalo kasha ujibu maswali
    Said A. Mohamed: Mbele ya Safari

    Ilipoanza safari, ilianza kwa dhiki
    Tulishikana kwa ari, kwenda safari ya haki
    Tukawa ni majabari, nyoyo zisitaharuki
    Tukajizatiti

    Njaa ikawa thabiti, na kiu kutamalaki
    Nasi tulitia dhati, tusijali kuhiliki
    Ingawa mbele mauti, dhila na mingi mikiki
    Tulijizatiti.

    Huu mwisho wa safari, tukaambiwa ni haki
    Shangwe kwetu na fahari, utumwa hatuutaki
    Kuwa mbele ya safari, juhudi iliyobaki
    Tulijizatiti.

    Ile ilikuwa ndoto, mwisho wake mafataki
    Nguvu zimechomwa moto, sahala ‘mmekuwa dhiki
    Wagombania kipato, utashi haukatiki
    Na kutabakari.

    Msafara ukasita, kwenye mlima wa haki
    Kijasho kinatuita, mlima haupandiki
    Basi soe ‘kajipeta, kukikwea kima hiki
    Twataka hazina.

    Tukiwa migongo wazi, tukainama kwa shaki
    Tukawa’chia ukwezi, kialeni wadiriki
    Wakapanda bila kazi, kuteremsha miliki
    Wakaitapia.

    Wakafikia makazi, ya pumbao na ashiki
    Huko wakajibarizi, kwenye raha lakilaki
    Wakaisahau ngazi, ya umma uliomiliki
    Mbele ya safari.

    Na hazina yetu sote, kuishusha hawataki
    Wamo wanatema mate, kwa umati halaiki
    Imezima nia yote, kiza hakitakasiki
    Mbele ya safari.

    MASWALI
    1.  Eleza safari inayorejelewa katika shairi hili (al. 2)
    2. Onyesha kinaya cha safari inayozungumziwa (al. 3)
    3. Taja na ueleze bahari mbili za shairi hili ukizingatia: (al. 2)
      1. Mizani
      2. Vina
    4. Andika ubeti wa saba kwa lugha ya nathari (al. 4)
    5. Eleza umuhimu wa aina mbili za uhuru wa kishairi zilizotumiwa katika ubeti wa sita (al. 2)
    6. Bainisha aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili (al. 2)
    7. Fafanua aina mbili za taswira zinazojitokeza katika shairi hili (al. 2)
    8. Kando na kinaya, bainisha vipengele vingine viwili vya kimtindo katika shairi hili (al. 2)
    9. Eleza toni ya shairi hili (al. 1)
  2. Soma shairi lifuatalo kasha ujibu maswali
    Ee mpwa wangu,
    Kwetu hakuna muoga,
    Uoga ukikufikia, huenda ni wa akina mamayo,
    Fahali tilichinja ili uwe mwanamume,
    Eewe mpwa wangu, kisu kikali ajabu!
    Iwapo utatingisa kichwa,
    Uhamie kwa wasiotahiri.

    Wanaume wa mbari yetu,
    Si waoga wa kisu,
    Wao hukatwa kuanzia macheo hadi machweo,
    Wewe ndiye wa kwanza,
    Iwapo utashindwa,
    Wasichana wote,
    Watakucheka,
    Ubaki msununu,
    Simama jiwe liwe juu
    Ndege zote ziangamie.

    Simu nimeipokea,
    Ngariba alilala jikoni,
    Visu ametia makali,
    Wewe ndiye wangojewa,
    Hadharani utasimama,
    Macho yote yawe kwako,
    Iwapo haustahimili kisu,
    Jiuzulu sasa mpwa wangu,
    Hakika sasa mpwa wangu,
    Hakika tutakusamehe, mwaka kesho unakuja.

    Asubuhi ndio hiii,
    Mama mtoto aamushwe,
    Upweke ni uvundo,
    Iwapo utatikisa kichwa.
    Iwapo wewe ni mme,
    Kabiliana na kisu kikali,
    Hakika ni kikali!

    Kweli ni kikali!
    Wengi wasema ni kikali!
    Fika huko uone ukali!
    Mbuzi utapata,
    Na hata shamba la mahindi,
    Simama imara,
    Usiende kwa wasiotahiri.

    Maswali
    1. Hili ni shairi la aina gani? Thibitisha (al. 2)
    2. Tambua anayeimba na anayeimbiwa shairi hili (al. 2)
    3. Toa ithibati kwenye shairi hili kuthibitisha kuwa msimulizi ana taasubi za kiume (al. 2)
    4. Taja kwa kutolea mifano mbinu zozote nne za uandishi katika shairi hili (al. 4)
    5. Taja shughuli zozote mbili za kiuchumi za jamii inayorejelewa katika shairi hili (al. 2)
    6. Eleza mbinu alizotumia mshairi kutosheleza mahitaji ya kiuarudhi (al. 4)
    7. Msamiati ufuatao umetumika kwa maana gani katika shairi hili? (al. 4)
      1. Mbari 
      2. Msununu 
      3. Ngariba 
      4. Uvundo
  3. SEHEMU E:
    HADITHI FUPI
    Harubu ya maisha Paul Nganga Mutua
    “Naja. Nakamilisha shughuli ndogo hapa kisha nianze safari…”
    1. Weka dondoo hili katika muktadha wake (al. 4)
    2. Eleza sifa sita za msemaji wa kauli hii (al. 6)
    3. Jadili changamoto wanazokumbana nazo waajiriwa kwa kurejelea hadithi hii  (al. 10)

                                                                                MWONGOZO

                                                                     SEHEMU A: FASIHI SIMULIZI (LAZIMA)

                                                                               MAJIBU YA FASIHI SIMULIZI

  1.  
    1.  
      • Ni majigambo / vivugo
      • Matumizi ya mimi ni….. (1x2)
    2.  
      • Ni wafugaji – nilipokuwa nalisha mifugo
      • Ni wezi wa mifugo – mifugo wa mtemi wamechukuliwa
      • Wanajihusisha na vita (2x1)
    3.  
      • Istiara (sitiari) Ni mimi Jabali
      • Tashbihi – Kasi kama umeme
                      − Ulipaa kama umeme
                      − Kama mmweso wa radi
      • Mdokezo – mifugo ikanifuata…
      • Swali la balagha – mmekuwa kama majivu baada ya jua moto kuzimika?
      • Chuku – upanga kupasua pembe za nyati kwa dhoruba moja
      • Msemo – kufumba na kufumbua
      • Urudiaji (takriri) nikachukua mkuki wangu
        Nikachukua upanga wangu
        Matumizi ya mishororo mishata m.f wazee waliposhindwa
        Nilipokuwa nalisha mifugo…
      • Uhuishi – mkuki kupaa
      • Usambamba – nikachukua mkuki wangu, nikachukua upanga wangu
    4.  
      • Anayejigamba hutunga kufuatia tukio mahususi katika maisha yake – anakumbuka alivyokomboa mifugo ya Mtemi kutoka kwa wezi
      • Huwa na matumizi ya chuku
      • Kwa kawaida hutungwa na kughanwa na wanaume
      • Hutolewa kwa nafasi ya kwanza m.f Nikachukua mkuki wangu
      • Anayejisifu huweza kutaja usuli wake wa kinasaba m.f Ochilamgwara mwana mbee wa Ojilong
      • Maudhui makuu ni ushujaa
      • Hutungwa kwa usanii mkubwa – sitiaru urudiaji tashbihi n.k
      • Avae maleba – mkuki, upanga ngozo
      • Atumie kiimbo na toni kupanda na kushuka kwa sauti yake
      • Atumie miondoko ya mwili
      • Atumie ishara za uso
      • Ashirikishe hadhira kwa kuuliza maswali ya balagha
                                      Kadiria hoja Zaidi (za kwanza 4x1=4)
    5.  
      • Kufanya utafiti Zaidi
      • Kuhifadhi kwenye kanda tepu rekodi video n.k
      • Kufunza shuleni
      • Kupanga mashindano kati ya jamii mbalimbali
      • Kuhifadhi katika maandishi
      • Kuhimiza watu kutunga tungo kama hizi
      • Sherehe mbalimbali
                                                                    SEHEMU YA B: TAMTHILIA
  2. “Sima tayari. Ninaanda mchuzi…..”
    1.  Weka dondoo hili katika muktadha wake (al. 4)
      • Msemaji : Bela
      • Msemewa : Neema
      • Mahali : Nyumbani kwa Neema
      • Tukio : Neema alikuwa amemuuliza kufahamu iwapo chakula kiko tayari kwa vile mamake Neema (Sara), sasa alikuwa akisubiri chakula
    2. Onyesha umuhimu wa msemewa wa maneno haya (al. 6)
      • Msemewa ni Neema
        Umuhimu wake
        1. Kielelezo cha uwajibikaji – Sara anamwambia Yona kuwa Neema amewafaa wanuna wake kwa hali na mali. Neema alilipia Asna karo ya chuo kikuu (uk. 28), Neema amemlea Lemi vizuri hadi akawa mtoto mwenye adabu (uk. 26), Neema yuko mezani akimsaidia Lemi katika masomo yake (uk. 47).
        2. Neema anachimuza sifa ya Bunju kama mwenye utu. − Neema anamwambia Yona kuwa hekaheka za Bunju zimewasaidia kulipia matibabu ya Sara (uk. 71), - Bunju alimletea Neema Flying Doctors kuokoa maisha yake alipohusika katika ajali na kugharamia matibabu ya Neema (uk. 51)
        3. Neema anachimuza sifa ya Yona kama mwenye Shukrani – Yona anamwambia Neema, ‘Mwanangu, asante kwa wema ulionifanyia mama yako. Umesimamia mji wangu vizuri...’ (uk. 71)
        4. Neema anachimuza sifa ya Yona kamamwerevu masomoni. Neema anasema, ‘Ninasikia hata pale chuoni imebaki kuwa rekodi ya idara. Inazungumziwa hadi leo hii’ uk. 73
        5. Kuchimuza sifa ya Bunju kama mwenye mapenzi. Neema ameshindwa kuendelea kusimulia jinsi Bunju alimwokoa kutoka kwenye ajali na kuanza kulia. Bunju anamkaribia, anampapasa na kumvuta Neema na kumrai awache kulia na kisha wanakumbatiana (uk. 51)
        6. Kuchimuza sifa ya Yona kama katili. Neema anaambia Sara kuwa ugonjwa wake wa moyo ulisababishwa na mivutano kati ya Yona na Sara hasa Yona alipompeleka Sara mbio. (uk. 46) (uk. 20). Yona aliwashikia watoto wake mkwaju. (uk. 19)
        7. Neema anachimuza kuwajibikakwa wauguzi wa hospital za mjini. Neema anasema kuwa hospitali alipolazwa Sara ni safi na wahudumu wote ni marafiki kwa wagonjwa.
        8. Neema anachimuza kuwajibikakwa Bunju kupitia kumpeleka Mina katika shule ya boarding school ya gharama ya juu/shule ya bweni. (uk.27)
        9. Neema anachimuza ukarimuwa Bunju kupitia Bunju kumlipia Salome karo katika shule ya upili na chuo kikuu (uk. 28) Bunju anamnunulia Neema gari (uk. 28), Bunju na Neema wamewajengea wazazi wa Neema nyumba.
        10. Neema anachimuza sifa ya Lemi kama mtoto mwenye adabu. Neema anamwambia Bunju kuwa Lemi anayaendesha mambo yake kwa udhu na adabu. (uk. 26)
        11. Neema anachimuza ulaghai/ufisadi wa wafanyabiashara. Neema anamwambia Sara kuwa wasiouwahi ulimaji watawapa wafanyabiashara fursa nzuri ya kuwauzia bidhaa kwa bei ya juu (uk. 16)
        12. Kuendeleza maudhui ya elimu. Asna anamwambia Sara kuwa Neema alikuwa hodari asiyeshindika darasani. Asna anamwambia Sara kuwa Neema ana digrii mbili. (uk. 35)
        13. Neema anachimuza sifa ya Lemi kuwa mdadisi. Neema anamwambia Lemi kuwa maswali yake huwa hayaishi. (uk. 30)
    3. Tambua toni katika dondoo hili (al. 2)
      • Toni ya kurai
    4. Eleza changamoto zinazokumba ndoa za kisasa kwa kurejelea tamthilia nzima (al. 8)
      1. Ukosefu wa watoto katika ndoa
      2. Ukosefu wa watoto wa kiume
      3. Mila na tamaduni
      4. Dhuluma katika ndoa
      5. Ulevi
      6. Kufutwa kazi
      7. Kutegemea watoto kwa malezi
      8. Majukumu ya nyumbani
      9. Uchochezi kutoka kwa watu wa nje
  3. “Masombo hufungwa kama walau mtu ametia kitu mdomoni. Pamoja na hali ngumu iliyopo, bado hatujafikia pa kukosa mlo wa kimsingi.Ndiyo hatumudu viliwa vya samli lakini hatuwezi kuishi kama kwamba tunazongwa na njaa. Tazama ulivyokonda unaelekea kushindarana na ng’onda. Hii nafasi ya ng’onda unaitaka kwa nini?
    1. Weka dondoo hili katika muktadha wake (al. 4)
      • Msemaji ni Dina
      • Msemewa ni Kiwa
      • Wakiwa nyumbani kwa Dina
      • Kiwa amefanya mazoea ya kula kidogo. Anasema kutokana na mabadiliko ni wakati wa kujifunga masombo.
    2. Tambua mbinu mbili za kimtindo zilizomo kwenye dondoo hii (al. 2)
      • Swali balagha – hiyo nafasi ya ng’onda unaitaka kwa nini?
      • Istiara – unaelekea kushindana na ng’onda
    3. Bainisha sifa nne za msemewa (al. 4)
      • Mvumilivu – Anakula chakula kidogo na anasema hali ya maisha imekuwa ngumu na kupata chakula kingi ni adimu basi amejifundisha kuvumilia maisha jinsi yalivyo.
      • Amewajibika – Anaenda kumwona mamake ili kujua hali yake
      • Mdadisi – Kiwa anamuuliza mama yake maswali mengi kuhusu familia ya Yona
      • Mwenye utu – Anahimiza Dina aende akamsaidie Sara kwake nyumbani
      • Mwenye heshima – Anamheshimu mama yake na kushirikiana naye licha ya pato dogo analopata
    4. Jadili namna msemaji amechangia katika kuendeleza
      1. Ploti (al. 3)
        1. Dina ndiye anayujuza maisha ya awali ya Sara yanayotusaidia kuelewa hali ya Sara ya sasa
        2. Kupitia kwa Dina tunatambua Sara na Yona walikosa watoto.
          Baadaye watasemwa sana
        3. Kupitia kwake tunatambua Yona hakuwa mlevi awali
          Anatusaidia kujua yaliyojira hadi Yona akawa mlevi chakari
        4. Kupitia kwake tunajua kiwango cha maradhi ya Sara kwani Sara hawezi kufanya lolote
        5. Kupitia kauli ya Dina wanajamii wa Kiafrika wanaonekana kama wambea. Anasema kuwa hao ndio hujua tatizo lenyewe.
      2. Maudhui (al. 5)
        1. Kupitia kwake tunapata kujua namna Sara na Yona walivyoanza ndoa yao na kuishi vizuri (maudhui ya ndoa)
        2. Kupitia kwa Dina tunatambua namna wanajamii walivyoweza kuwasema Sara na Yona kwa kukosa mtoto wa kuwarithi (maudhui ya utamaduni) kwani jamii inathamini mtoto wa kiume.
        3. Pia maudhui ya ulevi yamechimuzwa kwani Yona alisukumwa na maneno ya watu kwa kukosa mtoto wa kiume.
        4. Isitoshe anawapamba wanaume wa Kiafrika sifa za ubabedume, anasema wanaume wa Kiafrika hawawezi kusaidia wanawake hata kukiwa na shida (maudhui ya ubabedume yanajitokeza).
        5. Maudhui ya urafiki / ujirani mwema / mapenzi ya majirani, Dina anamsaidia Sara katika mapishi.
        6. Utu, Dina kuenda kumsaidia Sara ambaye alikuwa mgonjwa

                                                                             SEHEMU C: 
                                                        RIWAYA:  Chozi la Heri la 4 au la 5
  4.  
    1. ….haya imekuandama tangu usiku ukimtongoza fulani, siku za kuchora ramani ya Afrika kwa vyonde vya miguu hadi sasa? Ama ni hizo mui unaficha? Naskia ile mid-life crisis ikiwashika wazee ndiyo hivyo, 
      1. Weka dondoo hili kwenye muktadha wake (al. 4)
        • Msemaji ni Terry mawazoni mwa Ridhaa
        • Msemewa ni Ridhaa
        • Ridhaa yuko kwenye mawazoni uwanjani wa ndege wa Rubia
        • Anakumbuka maisha yake mkewe na aila yae huku akimngojea mwanawe mwangeka anayetoka ng’ambo
      2. Tambua mbinu zozote tatu za kimtindo kwenye dondoo hii (al. 3)
        • Taswira (mwono) − kuchora ramani ya Afrika
        • Maswali ya balagha − Hadi sasa? Ama ni hizo mvi unaficha?
        • Kuchanganya ndimi − Mid-life crisis
        • Mbinu rejeshi/Kisengere nyuma – Ridhaa kukumbuka yaliyopita
      3. Jadili udhaifu wa msemewa (al. 4)
        • Ridhaa ni mwepesi wa moyo kwani anapopatwa na mawazo ya makali anatokwa na machozi. Kwani anapotengwa na wanafunzi wenzake shuleni Analia kwa urahisi kinyume na matarajio ya jamii kwamba wanaume machozi yao hayafai kuonekana.
        • Ni mhusika aliyekuwa na Imani katika mambo ya ushirikina licha ya kuwa daktari mzima. (uk. 2). Terry anasema “Ninashangaa vipi daktari mzima hapo, ulipo unajishughulisha na mambo ya ushirikina.
        • Kutoondoa majivu baada ya aila yake kuchomewa na Mzee Kedi licha ya kuwa msomi anayeweza kutambua masharti ya jamii na itikadi. Kupitia mwangeka tunafahamishwa kuwa Ridhaa alikosa kuota majivu.
        • Anakosa kumpatia Shamsi ushauri nasaha kuhusu athari za ulevi licha ya kuwa daktari na kuelewa athari za pombe katika maisha ya binadamu.
    2. Dhibitisha kauli kwamba ‘Kweli jaza ya hisani ni madhila’
      Kwa kurejelea wahusika tisa kwenye riwaya ya Chozi la Heri (al. 9)
      • Ridhaa aliwatendea hisani wahafidhina kwa kupanda miti kwenye Kijiji na kusambaza maji ya mabomba, hatimaye alichukuliwa kama mgeni mahali hapo hata kuchomewa mali yake na familia yake kuuawa.
      • Selume hata baada ya kumpenda mumewe na kuishi vyema na wakweze, anafukuzwa nyumbani kwa kutofautiana nao kwa misingi ya kisiasa na kujipata kwenye msitu wa mamba.
      • Makaa – alijitolea mhanga kuwaokoa wananchi waliokuwa wakifyonza mafuta kwenye lori iliyoanguka. Mshahara wake ulikuwa kifo cha uchungu.
      • Lunga alitetea haki za wananchi wasije wakanunuliwa mahindi mabovu na mwishowe akapigwa kalamu kazini.
      • Mwekevu aliwajengea wananchi visima katika sehemu zilizokuwa na ukame. Hatimaye walimsaliti kwa kusema hawawezi kuongozwa na mwanamke na mwishowe kupigana na kusababisha maangamizi makubwa.
      • Kiriri alijizatiti kuwasomesha wanawe ugaibuni na hata mkewe, baadaye familia hiyo walikataa kurejea nyumbani na kumsababishia kihoro akafa.
      • Billy amjengea Sally kijumba ili waishi raha mstarehe, alipompeleka aone jumba, aliambiwa kuwa nyumba hiyo ilikuwa kama kiota cha ndege.
      • Babake Tuama alimshauri bintiye kutokeketwa na badala yake Tuama alikeketwa na kujipata katika hali mbaya hospitalini na kumsababishia aibu babake.
      • Zohari – baada ya wazazi wake kumkimu kwa mahitaji yake yote hadi kumpeleka shuleni, alijiingiza kwa mapenzi ya kiholela na kusababisha mimba ya mapema. Baadaye ana alifukuzwa shuleni na akatoroka nyumbani.

                                                                        RIWAYA: CHOZI LA HERI
  5. “Nashangaa kinachompa kijana kama huyu, na wengine waliofariki jana, ambao wamesomea shahada za uzamili, kujihusisha na unywaji wa pombe haramu!
    1.  
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili (al. 4) 
        • Msemaji – Selume
        • Msemewa – Meko
        • Mahali – kituo cha afya cha mwanzo mpya
        • Kiini – Ni baada ya kifo cha mmoja wa wagonwa hospitalini hali inayomfanya Meko kutaka kujua iwapo ni yule aliyeletwa usiku
      2. Fafanua umuhimu wa msemaji katika dondoo hili (al. 4)
        Msemaji ni Selume
        1. Amejenga tabia za wahusika kwa mfano utu wa Ridhaa. Anaanzisha kituo cha Afya na kuajiri Selume na Kaizari.
        2. Anaonyesha changamoto katika hospitali za umma. Anashangaa kama alivyovumilia kufanya kazi bila glavu.
        3. Anajenga maudhui ya ufisadi. Dawa zilizotengewa hospitali ziliuzwa na wasimamizi.
        4. Anaendeleza ploti. Kupitia sadfa. Kituo kinakamilika wakati ambapo Selume anajiuzulu, anapata kazi na mkondo wa matukio kubadilika.
        5. Anaonyesha mgogoro unaosababishwa na siasa. Anatengwa na jamaa yake kwa sababu ya kumuunga mwekevu mkono
      3. Kando na maudhui ya elimu eleza maudhui mengine mawili katika dondoo hili (al. 2)
        • Vifo/mauti – wengine waliofariki jana/ tanzia
        • Ulevi – Unywaji wa pombe haramu
    2. Eleza jinsi mwandishi alivyofaulu kutumia mbinu zifuatazo katika kuijenga riwaya hii
      1. Hadithi ndani ya hadithi (al. 5)
        • Usimulizi wa Kairu (uk. 91-93) Unaonyesha dhiki za wakimbizi. Mnuna wa Kairu anafia njiani, kuna msongamano kambini
        • Usimulizi wa Mwanaheri (uk. 93-98) ndio unaonyesha hatima ya familia ya Kaizari; wanarudishwa nyumbani na Mwanaheri na Lime kurudia maisha ya kawaida.
        • Usimulizi wa Zohali (uk. 98-101) kuonyesha matatizo ya vijana. Zahali anashindwa kujidhibiti na kuambulia ujauzito akiwa shuleni.
        • Usimulizi wa chandachema (uk. 101-108) unaendeleza maudhui ya malezi. Analelewa na nyanya baada ya baba yake. Fumba, kumtelekezea huko.
        • Usimulizi wa Pete (uk. 146 – 153) Unaonyesha ukiukaji wa haki za watoto. Mama Pete anaridhia wazo la kumwachisha Pete masomo. Anaozwa kwa Mzee Fungo bila hiari.
        • Hadithi ya Sally kumsaliti Billy inayosimuliwa kama kifani cha Naomi kumsaliti Lunga.
      2. Mbinu rejeshi (al. 5)
        • Ridhaa anakumbuka kupepesa kwa jicho lake la kulia, anguko aliloanguka sebuleni, milio ya bundi iliyomtia kiwewe. (uk. 1)
        • Ridhaa anakumbuka mazungumzo kati yake na Terry mkewe akimuuliza “since when has man ever changed his destiny?” (uk. 2)
        • Ridhaa anakumbuka jinsi mwanawe Mwangeka alivyozaliwa katika chumba chake ambacho kwa sasa kimeteketea. (uk. 4)
        • Ridhaa anakumbuka mjadala kati yake na mwanawe Tila kuhusu mafanikio ya baada ya uhuru.
        • Mwandishi kupitia mbinu rejeshi anatuelez jinsi Ridhaa alivyojipata katika msitu wa Heri.
        • Ridhaa anakumbuka jinsi wanafunzi wenzake walivyomtenga shuleni na kumuita “Mfuata Mvua” (uk. 10)
        • Tetei, mwanaharakati anakumbuka jinsi wanaume walivyotumikishwa katika enzi za kiistimari. (uk. 17)
        • Mja aliyevaa shati lilioandikwa Hitman mgongoni anakumbuka jinsi kila baada ya miaka mitano viongozi huwatumia katika kampeni zao na kushiriki katika njama za viongozi za kuiba kura. (uk. 22)
        • Kupitia kisengere nyuma, mwandishi anatueleza jinsi Mwangeka alivyokutana na Lily Nyamvula mkewe wa kwanza – katika chuo kikuu.
        • Mwangeka anakumbuka jinsi babake alivyomchapa baada ya kumpata yeye na wenzake wakiigiza mazishi ya nduguye Dedan Kimathi. (uk. 60)  5x1=5 (zozote 5)

  6.                                                                        MWONGOZO WA USHAIRI:
                                                                                 SWALI LA LAZIMA 
                                                                                     SWALI LA SITA  
    1. Ni safari ya kupigania uhuru/safari ya kutafuta haki/harakati za kujiendeleza kiuchumi
      Anasema walishikana kwenye safari ya haki. Anataja kuteremsha miliki.   1x2=2
              Kutaja alama 1 ,Kueleza alama 1
    2.  
      • Maelezo ya (maana ya) kinaya yawepo
      • Kinyume cha matarajio
        1. Viongozi wachache waliofika kileleni walijawa na uchoyo, wakaamua kujinufaisha
        2. Walijitengenezea makazi ya raha, wakajinyakulia vyeo wakakaa kufurihiki huku wakiwasahau waliowakweza mamlakani.
        3. Wakawa ndio pekee waliofaidi matunda ya uhuru ambayo yalikuwa yamepiganiwa na wote
          • Viongozi wamefika hadi kuwadharau raia waliowapa hivyo vyeo – wanawatemea mate
          • Raia kupigania uhuru na baadaye kutofaidika kwao (3x1=3)
            (kueleza kinaya/kujitokeza kwa kinaya alama 1)
    3.  
      1. Msuko – Mshororo wa mwisho una mizani chache kuliko mingine/umefupishwa
      2. Ukara – Vina vya kati/ndani vinabadilika vya mwisho/nje vinatiririka  2x1=2
        Kutaja -  1 ½ , kueleza ½ = 1
    4. Wawakilishi/viongozi walijikuta katika hali nzuri sana za maisha ya tamaa ya kujinufaisha ikazidi. Walishiriki sherehe za kila hali hii walisahau wananchi/raia waliowakweza katika nafasi hizo za uongozi, na ambao ndio waliokuwa na nyenzo za kuwafanya kufikia hali yao ya sasa. (alama 4)
    5.  
      1. Inkisari – tukawa’chia – kutosheleza idadi ya mizani
      2. Kufinyanga sarufi – kialeni wadiriki – Wadiriki
                                        kileleni – kuleta urari wa vina
      3. Tabdila – shaki – badala ya shake – kuleta urari wa vina
      4. Msamiati kikale  kialeni – kileleni
        kulipa shairi mapigo ya kimuziki 2x1=2
                 (kutaja – ½  maelezo ½ = 1)
    6.  
      1. Urudiaji wa silabi – ki, ti, to, zo, vi, te
      2. Urudiaji wa maneno – safari – ubeti 1, 3, 7, 8
                                            mbele ya safari – ubeti 7, 8      2x1=2
    7.  
      1. Taswira hisi – shangwe kwetu na fahari. Ubeti 3
      2. Taswira ya mwendo – kwenda safari ya haki. Ubeti 1
      3. Taswira oni – Tukiwa migongo wazi, tukainama kwa shaki. Ubeti 6
                              Wamo wanatema mate. Ubeti 8     2x1=2
    8.  
      1. Takriri/uradidi – safari, tulijizatiti, mbele ya safari
      2. Tashhisi/uhuishi – kijasho kinatuita – Ubeti 5    2x1=2
    9.  
      • Toni ya masikitiko/kuhuzunisha/kuhurumia – safari ilianza kwa dhiki
      • Njaa ikawa thabiti, na kiu kutamalaki
      • Wamo wanatema mate, kwa umati halaiki   1x1=1
                                                                                          (Kutaja ½ kueleza ½ = 1)
  7. Maswali
    1. Hili ni shairi la aina gani? Thibitisha     (al. 2)
      • Shairi huru – halijazingatia kanuni zote za utunzi wa mashairi wa kuzingatia arudhi.
    2. Tambua anayeimba na anayeimbiwa shairi hili     (al. 2)
      • Anayeimba ni mjomba
      • Anayeimbiwa ni mpwawe
    3. Toa ithibati kwenye shairi hili kuthibitisha kuwa msimulizi ana taasubi za kiume    (al. 2)
      • Anaambiwa uoga ukimtikisa huenda ni wa akina mamaye
      • Alichinjiwa fahali ili awe mwanaume
    4. Taja kwa kutolea mifano mbinu zozote nne za uandishi katika shairi hili     (al. 4)
      • Chuku – wao hukatwa kuanzia macheo hadi machweo
      • Takriri – kikali
      • Isitiari – upweke ni uvundo
      • Tashhisi – uoga ukifikia
    5. Taja shughuli zozote mbili za kiuchumi za jamii inayorejelewa katika shairi hili     (al. 2)
      • Wakulima – Atapewa shamba la mahindi
      • Wafugaji – Atapewa mbuzi
    6. Eleza mbinu alizotumia mshairi kutosheleza mahitaji ya kiuarudhi     (al. 4)
      • Tabdila- aamushwe – aamshwe
      • Inkisari – Mme – mwanaume
      • Kuboronga sarufi – Fahali tulichinja-tulichinja fahali
    7. Msamiati ufuatao umetumika kwa maana gani katika shairi hili?     (al. 4)
      1. Mbari – ukoo
      2. Msununu – anayenuna
      3. Ngariba – mtahirishaji
      4. Uvundo – harufu mbaya

                                                                                           SEHEMU E:

                                                                                         HADITHI FUPI

                                                                      Harubu ya maisha Paul Nganga Mutua

                                                    “Naja. Nakamilisha shughuli ndogo hapa kisha nianze safari…”

  1. Weka dondoo hili katika muktadha wake (al. 4)
    1. Maneno haya ni ya kikwai
    2. Anajibu ujumbe wa simu ya Mama Mercy mke wake
    3. Alikuwa ofisini
    4. Ilikuwa usiku wa saa nne na bado alikuwa kazini, hofu ya Mama Mercy ni kuwa Mercy angelala bila babake kufika
  2. Eleza sifa sita za msemaji wa kauli hii (al. 6)
    1.  Mwenye mapenzi kwa familia yake – Mama Mercy alipomwambia kuwa Mercy angelala kabla hajafika, aligushwa na kutoka kasi kazini. Pia mamake alipotamka atume pesa nyumbani alisema angetuma.
    2. Mlezi bora – Anaenda kwa Vaite na kukopa chakula. Anamlisha Mercy. Baada ya kumlisha Mercy, alishindwa kula chakula ilhali Mama Mercy hakula chochote. Hali yake inamfanya kuhisi kulia.
    3. Mwenye mawazo – Amejawa na mawazo hadi anasahau kumpigia mamake simu. Mama anamjulisha juu ya deni ya yule fundi wa nyumba. Atalazimika kuuza mbuzi, kuku n ahata pesa na deni zikose.
    4. Mwenue utu – Anamuombea Nilakosi advansi ilhal yeye anahitaji pesa, badala ya kujiombea yeye mwenyewe
    5. Mwenye bidii – Kuendea msaada kwa Kanisa. Pastor alimpa unga uliowashibisha na wakala wakalala. Pia kufanya kazi kwa bidii haa mshahara unapocheleweshwa
    6. Mvumilivu – Kuvumilia kukosa mshahara, kufokewa na Boss na hata Mama Mercy
  3. Jadili changamoto wanazokumbana nazo waajiriwa kwa kurejelea hadithi hii   (al. 10)
    1. Kuwa kazini hadi saa nane kasorobo za usiku – Kikuni anapigiwa simu na Mama Mercy kuwa Mercy anamsubiri
    2. Usafiri – Usiku hapakuwa na msongamano wa magari barabarani, lakini mchana watu waliotembea kwa miguu, pikipiki na magari yalisongamana
    3. Kukosa pesa za matumizi. Kikwa analazimika kuenda kukopa chakula kwa Vaite. Yeye na mkewe walilala bila kula. Kulala njaa kwake na mama Mercy pia kulitokana na chakula kilichosalia kuwa kidogo na kunuka mafuta taa.
    4. Kazi nyingi ya dharura kazini ya kuandaa vitabu kwa ajili ya kuviwasilisha kwenye wizara. Kutumwa na Bosi kumfanyia kazi za kibinafsi kama kumpeleka mtoto wa Bosi hospitalini.
    5. Ukosefu wa mshahara – kukosa kulipwa mshahara kwa miezi miwili
    6. Uoga – Kuogopa hata kuomba pesa kidogo za matumizi. Hadi Bosi awe kwa ‘mood’
    7. Kutegemewa na jamii – Mama anamjulisha juu ya deni ya yule fundi wa nyumba. Atalazimika kuuza mbuzi, kuku na hata pesa za deni zikoshe kutosha.
    8. Hali mbaya ya kiuchumu – Bei ya mauzo kushuka na hali ya maisha kupanda.
    9. Kutembea kuenda na kurudi kutoka kazini kwa sababu ya kukosa pesa za nauli au mafuta ya kuweka kwa gari
    10. Kufanya kazi kwa ‘contract’ – Nilakosi ambaye mkataba wake unakatika mwezi ujao walitaka kumuachisha kazi sasa.
    11. Kuomba advansi ya elfu tano – Nilakosi
    12. Kufungiwa nyumba na Landlord kwa sababu ua kuksa kulipa nyumba. Sababu ni kukosa kulipwa mshahara.
    13. Kutumwa kufanya kazi za nyumbani na Bosi – kumpeleka mtoto hospitalini akitumia gari la Kampuni.
    14. Kupewa gari na Kampuni lakini kushindwa kuliweka mafuta
    15. Kufokewa na Bosi – Kikwai alipokosa kuja na gari kazini kwa sababu ya kukosa hela za mafuta ya gari, alimfokea na kumuonya kuwa gari ni lazima liwe pale ofisini.
    16. Bosi kukosa kufika ofisini akijua fika kuwa ni mwiso wa mwezi na anafaa kuwalipa wafanya kazi mshahara
    17. Bosi katili ambaye anaweza kumlipa Kikwai mshahara wa miezi miwili na kumwachisha kazi ghafla. Kwa hivyo alikuwa na pesa za kumlipa kila mwezi lakini hakufanya hivyo.
    18. Kuachishwa kazi kwa ghafla na kulazimika kurudisha kila kitu cha kampuni. Analipwa mshahara wake wa miezi miwili.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kapsabet Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?