Muhtasari - Mwongozo wa Chozi la Heri

Share via Whatsapp


Sura ya kwanza

Sura hii inapoanza, Ridhaa alikuwa amesimama kwa maumivu makali huku mikono kairudisha nyuma ya mgongo wake uliopinda kwa uchungu. Amelitazama wingu la moshi ambalo linamkumbusha ukiwa aliozaliwa nao na ambao anahofia kuwa angeishi na kuzikwa nao. Alipogeuka alitazamana ana kwa ana na moto ambao uliteketeza jumba lake la kifahari.

Walioangamia mle ndani ni Terry (mkewe Ridhaa),bintiye Tila, Mkewe Mwangeka(Lily) na mjukuu wake Becky. Tukio hill linamkumbusha mambo kadha yaliyotokea hapo awali yakiwemo mlio wa kereng'ende na bundi usiku wa kuamkia siku hii ya kiyama. Milio hii ilimtia kiwewe zaidi kwani bundi hawakuwa wageni wa kawaida katika janibu hizi. Alikumbuka akimwambia Terry kuwa milio hii ni kama mbiu ya mgambo ambayo ikilia huenda kukawa na jambo. Terry ambaye kawaida yake ni mcheshi hakunyamaza balI alimwambia Ridhaa kuwa kwake lazima kila jambo liwe na kiini. Terry alishangaa ni vipi daktari mzima alikuja kujishughulisha na mambo ya ushirikina. Terry anamkumbusha mmewe kuwa aliwahi kumwambia kuwa ni vizuri kuiacha mielekeo ya kijadi ambayo huyafifilisha maendeleo. Anazidi kumuuliza hata iwapo jambo likawa atafanya nini? Ndipo Terry anamjuvya kuwa la muhimu ni kumlaani shetani kwani liandikwalo ndilo liwalo. Mazungumzo haya baina ya Terry na mmewe Ridhaa yalikuwa ya mwisho kabisa kutokea Terry akiwa hai. Ridhaa sasa anajutia kuwa angelijua angelitumia kila sekunde za uhai zilizokuwa zimesalia kumuuliza mkewe maswali ambayo sasa yameivamia akili yake. Machozi yalifulika machoni mwake na kuulemaza uwezo wake wa kuona na ndipo moyo wake ukamwonya dhidi ya tabia yake ya kike ya kulia pindi tu akumbwapo na vizingiti ambavyo ni kawaida ya maisha.

Aliyakumbuka maneno ya marehemu mamake kuwa machozi ya mwanamme hayapaswi kuonekana mbele ya majabali ya maisha. Siku hii Ridha hakujali la mama wala la baba; alijiskia kama mpigana masumbwi aliyebwagwa na kufululiziwa makonde bila mwombezi. Alisalimu amri na kuyaacha machozi yamvamie yatakavyo. Katika mito ya machozi ndipo alileta kumbukumbu ya mambo yalivyokuwa usiku ambao uliyatia giza maisha yake. Anakumbuka mayowe ambapo mwenye kuyapiga alimsihi Mzee Kedi asiwauwe kwani wao ni majirani wake. Akamsihi asiwadhuru wanawe wala mume wake.

Baada ya mayowe haya ndipo alisikia mlipuko mkubwa kisha akashikwa na uziwi wa muda uliofuatwa na sauti nyingine ya Mkewe "Yamekwisha". Kumbukumbu hii ilimpa kuzimia na alipozinduka alijipata kalala kando ya gofu la jumba lake lililokuwa linafuka moshi. Alijikongoja hadi kwenye kwenye shamba lililokuwa kando ya nyumba yake alipopaaza sauti na kusema " Familia yangu na mali yote hii kuteketea kwa siku moja?

Aliporudi kulikokuwa sebule ndipo alikumbuka kuwa Mwangeka (kifungua mimba) wake alizaliwa kwenye chumba hiki miaka thelathinl iliyopita. Alishangaa ni vipi Mwangeka aliweza kunusirika mkasa huu na ndipo akawaza kuwa wadhifa aliyopewa kwenda Mashariki ya Kati kudumisha amani ulitokea kuwa wongofu wake. Katika kumbukumbu zake anaukumbuka mjadala mkali baina yake na bintiye Tila kuhusu mafanikio ya baada ya uhuru. Hakuna aliyethubu kuuchangia kwani masuala ya sheria Tila alikuwa ameyamudu kweli. Tila anamuuliza babake maswali magumu ambayo yanamsawiri Mwafrika alivyonyanyaswa na tabaka la juu lililojilimbikizia mali baada ya mzungu kuondoka, likabaki likiukomaza ukoloni mambo leo.

Mwafrika alibaki pasi na chochote cha kumiliki. Tila anasisitiza kuwa wao ni wategemezi si kwa lishe tu, bali pia kwa ajira. Na kazi zenyewe ni vibarua vya kijungu jiko. Tila alishangaa ni kwa nini wao hawajaanza kujisagia kahawa au chai yao. Haihalisi mbegu ziwe zetu, tulikuze zao lenyewe kisha kumpelekea mwingine kwenye viwanda vyake alisage kisha kuja kutuuzia hiyo kahawa au chai kwa bei ya kukatisha tamaa alisisitiza Tila. Ridhaa alikubaliana na mtazamo wa Tila kwani mstakabali wao wa ukuaji kiuchumi uligonga mwamba wakati sheria ya mkoloni ilimpa mzungu kibali cha kumiliki mashamba katika sehemu zinazotoa mazao mengi. Mwafrika akabaki aidha kuwa kibarua au skwota ambaye maisha yake yalitegemea utashj wa mzungu. Wafrika ambao walibahatika kupata makao yao binafsi walipata sehemu ambazo hazingeweza kutoa mazao mengi, wakawa wakulima wadogo wadogo, maskini wasio na ardhi. Ridhaa anamkumbuka baba Msubili alivyokuwa akisema kuwa jamii yao iligeuka kuwa hazina ya wafanyakazi ambamo Wazungu wangeamua kuchukua vibarua kupalilia mazao yao. 

Ridhaa hakuwa mkaazi asilia wa Msitu wa Heri. Alikuwa Tuata mvua kama walivoitwa walowezi na wenyeji kindakindaki. Ridhaa anasema kuwa hakupachagua mahali hapa ila majaliwa yalitaka awe hapo. Babake alikuwa na wake kumi na wawili. Wake hawa walijaliwa na wana wa kiume ishirini na ndipo ardhi ya mzee Mwimo Msubili ikawa haitoshi kuwalea madume hawa lligawanywa na ikamwia vigumu Mzee Mwimo kuwalisha wana hawa kwani ardhi yake ilitoa zao dogo. Katika ardhi ya Mzee Mwimo mlizuka uhasama, migogoro na uhitaji mkubwa. Jambo hili limfanya mzee mwimo kuwahamishia wake wawili wa mwisho Msitu via Heri au Ughaishu kama walivyopaita wenyeji. Siku hizo ilikuwa rahisi mtu kuwa na shamba mahali kokote katika eneo lililomilikivia na kabila lake kwani umiliki wa mashamba ulitegemea bidii ya mtu.

Mamake Ridhaa alikuwa mke wa mwisho wa Mzee Mwimo. Ridhaa alikuwa mwenye umri wa miaka kumi walipohamia Mlima via Heri na alikuwa bado hajaanza shule. Walipowasili humu hamkuwa na wakaazi wengi na ilimchukua muda kuzoeana na watoto wa majirani ambao waliwaona Ridhaa na nduguze kama waliokuja kuuvuruga utulivu wao.

Ridhaa alipowazia kuhusu jambo hill alielewa fika kuwa hali hii ilizuliwa na wakoloni na kuwarithisha Waafrika. Baba yake, Mwimo Msubili alikwisha kumwambia kabla ya miaka ya Hamsini umiliki wa kibinafsi wa ardhi haukusisitizwa katika jamii yao. Watu walitangamana vyema. Familia zilizotoka kwengine ziliishi miongoni mwao pasi uhasama. Sera mpya ya mkoloni kujumuisha pamoja ardhi iiiyomilikiwa na mtu binafsi na kuuidhinisha umiliki huu kwa hatimiliki, ilivuruga mshikamano wa kijamii.

Sera hii mpya ya umilikaji wa ardhi ilimaanisha kwamba wale waliokosa pesa za kununulia mashamba wangekosa mahali pa kuishi. Wale waliobahatika kuwa na pesa za kununulia mashamba daima walichukuliwa kama wageni wasiopasa kuaminiwa. Ridhaa alikuwa kati ya waathiriwa wa hali hii kwani alitengwa na wenzake siku ya kwanza shuleni katika michezo mbalimbali. Alichokozwa na mwanafunzi mmoja aliyemwita 'mfuata mvua' na kumwambia hakutaka kucheza naye kwani alikuja kuwashinda katika mitihani yote. Jambo hili lilimfanya Ridhaa kulia kwa kite na kumwambia mamake kuwa hangerudi shuleni tena. Mamake alimwambia ni vyema kujifunza kuishi na wenzake bila kujali tofauti za kiukoo na nasaba. Mamake Ridhaa alizungumza na mwalimu naye mwalimu akazungumza na wanafunzi na kuwasisitizia umuhimu wa kuishi pamoja kwa mshikamano. Huu ukawa ndio mwanzo wa maisha ya heri kwa Ridhaa.

Ridhaa alifanya vyema masomoni na kufikia kilelecha cha ufanisi alipohitimu kama daktari. Baadaye aliasi ukapera na akafunga ndoa naye Terry. Alijaliwa na wana ambao waliangamia isipokuwa Mwangeka. Ridhaa anashangaa ni kwa nini Mzee Kedi alimgeuka kwani ndiye aliyemsaidia kupata shamba hilo lake.

Familia zote mbili zilikuwa na mlahaka mwema. Ridhaa ameyafanya mengi mazuri kikijini hadi kikaacha kuitwa Kalahari. Ikawaje aliowatendea hisani wamelipa kwa madhila?

lweje watu waliokula na kunywa pamoja ndio waliomlipulia aila na kuyasambaratisha maisha yake?

Haya maswali yasiyo na majibu yalimsumbua akilini mwake. Alipowaza alianza kuelewa sababu ya vikaratasi kuenezwa kila mahali vikiwatahadharisha kuwa mna gharika baada ya kutawazwa kwa Musumbi- kiongozi mpya. Anaelewa sababu ya jirani kuacha kumtembelea kwake kwa ghafla. Anaelewa sababu ya mke wa jirani kulalamika kuhusu kuuzwa kwa mashamba ya wenyeji kwa wageni. Alielewa kuwa alikuwa mgeni wala si mwenyeji hata baada ya kuishi pale miongo mitano. Katika usingizi alikumbuka habari iliyosomwa katika runinga miaka miinne iliyopita. Habari ilisema kuwa matrekta ya

Baraza ya jiji yalitekeleza amri ya Bwana Mkubwa ambayo ilikuwa ni kwabomoa majumba ishirini katika mtaa wa kifari wa Tononokeni. Ridhaa alitazama picha za majumba yake matatu kwenye mulishi wa runinga yakibomolewa. Majumba haya sasa yamegeuka udongo.Pigo hili la pili aliliona kali zaidi. Alibaki akijiuliza maswali akishangaa ni upi utakuwa mstakabali wake, wa mwanawe Mwangeka na Subira, dada yake Ridhaa aliyeishi maili kumi kutoka pale.

Maswali:

  1. Eleza kwa kifupi hasara ya ukabila.
  2. Ni mambo gani yalifuatia kutawazwa kwa Musumbi ?
  3. Ni mambo gani yalimpata Ridhaa tangu walipohamia Msitu wa Heri?
  4. Wataje, kisha utoe sifa za wahusika waliotajwa katika sura hii.
  5. Onyesha namna mbinu rejeshi ilivyotumiwa katika sura hii.


Sura ya pili

Ni siku kumi tangu kuondoka kwa Kaizari na wenzake na kujipata katika mazingira haya mageni. Si mageni kwani ni mumo humo kwao kwani si ughaibuni wala nchi jirani. Pahali hapa ni kambi au mabanda yaliyosongamana. Waliokuwa nacho na wachochole wote wako pamoja katika kambi hii. Kuna kiasi fulani cha usawa. Japo wanasema kuwa wanadamu huwa sawa kifoni, kuna tofauti katika mandhari wanamofia. Kuna wanaofia zahanati za kijijini na wapo wanaolala maumivu yao yakiwa yamefishwa ganzi katika hospitali za kifahari huku wakiliwazwa na mashine. Kuna wengine ambao hufia kwenye vitanda vya mwakisu vitongojini baada ya kupiga maji haramu(pombe haramu) kama nzi ambao kufia dondani si hasara. Kuna tofauti pia mitindo ya mazishi na hata mavazi ya mwenda zake na wafiwa. Hata majeneza yenyewe huhitilafiana.

Katika kambi la kina Kaizari mipaka ya kitabaka imebanwa. Kwani, hata waliokuwa navyo sasa hivi wanang'ang'ania chakula haswa uji. Hata aliyekuwa waziri wa Fedha miaka mitano iliyopita yumo katika kambi hii aking'ang'ania chakula na wenzake. Mvua kubwa inanyesha na matone mazito kuwaangukia wanawe wakembe wa Ndugu Kaizari-Lime na Mwanaheri. Hana hata tambara duni la kuwafunikia. Ubavuni amelala mke wake Subira. Anaonekana kuwa siye yule Subira wa awali kwani mwonekano wake ni wa kukatisha tamaa amevimba sana baada ya kutendewa unyama na binadamu wengine. Kwa mbali anaonekana Ridhaa, akitafuna kitu fulani kinachofanana na mzizi-mwitu. Ni kinaya Daktari mzima, Mkurugenzi mzima wa Wakfu wa Matibabu nchini kula mzizi!

Kaizari anaanza kusimulia yaliyojiri siku ile baada ya kutawazwa kwa kiongozi mpya. Anasema kuwa baada ya kutawazwa kwa kiongozi mwanamke(wengine waliamini hafai kuongoza) mambo yaliharibika. Watu wakashika silaha kupigania uhuru wao, uhuru ambao walidai hawakupewa wakaupigania. Wakatoa kauli kuwa wanaume watatumikishwa kwa walivyofanywa enzi hizo katika visakale vya jirani GO. Waliona kuwa kiongozi mwanamke atawarudisha pale walikotoka. Walikemea kusumbuliwa walikosumbuliwa kwa miongo mitatu sasa na Affirmative action na a third should be Women. Walikerwa mno na suala Ia jinsia ya kikuchipuza kila mara katika vikao vyao wakalamikia mwa mke kutetewa na vyombo vya habari na wapigania haki. Mwanaharakati mmoja kwa jina la Teitei akazidi kusema kuwa mwanamke kuiongoza jamii nzima itakuwa kukivika kichwa cha kuku kilemba. Bi. Shali alikanusha kauli ya Teitei na kusema kuwa, Mwekevu(kiongozi mwanamke) alijitosa katika siasa na kuomba kura kama wanaume hao wapinzani wake, akastahimili vitisho na matusi kutoka kwa wanaume na kwa hivyo ushindi wake ni zao Ia bidii yake. Mradi wake wa kuchimba visima umewafaidi raia kwenye maeneo kame.

Kaizari aliendelea kumweleza Ridhaa kuwa vita vilianza kati ya kundi lililokuwa linaunga mkono Mwekevu na lililokuwa likiunga mkono mpinzani wake mwanamume. Vita vikachacha baina ya pande zote mbili. Kundi pinzani likidai kuwa haiwezekani mwanamke kushinda uchaguzi huenda aliiba kura na wafuasi wake kuwanunua wanawake ambao ndio wapiga kura wengi. Kundi la mwekevu lilisikika likisema kuwa wakati wa mabadiliko ni sasa na kuwa wanastahili kumpa Mwekevu nafasi. MijadaIa iliyozuka ilizidisha migogoro na hali ya taharuki ikatamalaki. Askari wakatumiwa kudumisha usalama katika vijiji na mitaa. Muda si muda raia walianza kukimbizana na polisi. Katika mchezo huu, watu wengi walipoteza maisha yao. Wengine walipoona kuwa mambo yameharibika waliacha makwao na kukimbia. Mali walioacha nyuma yaliteketezwa. Wakapoteza kila kitu. Wengine waliokuwa jasiri walipora maduka ya Kihindi, kiarabu na hata Waafrika wenzao wakapora walichoweza kubeba kabla ya kupatana na mkono wa utawala. Sura ya nchi ya Wahafidhina ikawa mpya. Misafara ya wakimbizi ikawa kwenye barabara na vichochoro vya Wahafidhina. Mizoga ya watu na wanyama, magofu ya majumba yaliyoteketezwa kwa moto na uharibifu wa mali na mazingira ukashamiri.

Kaizari anakumbuka siku ya pili akiwa sebuleni na wanawe wakitazama runinga mara alisikia kuwa hakuna amani bila kuheshimu mwanamume. Kilichofuatia ni mabarobaro waliobeba picha za mpinzani aliyeshindwa na Mwekevu na wakaanza kughani mkarara uliokuwa ukisema Tawala Wahafidhina tawala, Mwanzi wetu tawala Wahafidhina tawala. Mara hali ilibadilika na wakayazingira magari barabarani na kuanza kuyawasha moto kana kwamba wanayachoma mabiwi ya taka! Vikasikika vilio vya binadamu akiomba kuhurumiwa na binadamu kaini, lakini vilio havikusikika. Magari yakawa yanawaka moto bila kujali binadamu waliokuwamo ndani. Mmoja wa waliokuwa wakitekeleza unyama alisikika akiwaambia wapinzani wao wanyamaze kwani wao ndio wamekuwa wakiwarudisha nyuma miaka yote hiyo kwa kuhadaiwa na vishahada hivyo wanavyopewa vyuoni. Alilalama kuwa wanafunzwa kukariri nadharia bila kuwazia umilisi na stadi za kuwawezesha kujitegemea. Mtu ana digrii tatu na hata baada ya miaka kumi kazi hana. Vijana waliendelea kulamikia kupuuzwa kwao. Mate yamewakauka vinywani wakifunga barua za kutumia maombi ya baadaye ving'ora vilisikika na askari wanaojulikana kama fanya fujo uone wakawa wanawinda vijana hawa. Walimiminiwa risasi vifuani mwao na wote wakaiaga dunia kifo cha kishujaa kwani walijitolea mhanga kupigania uhuru wa tatu. Kaizari alitokwa na machozi na kuwahurumia vijana hawa waliokufa kifo walichoweza kukiepuka. Akaihurumia nchi yake ambayo ilielekea kushindwa kuwahakikishia usalama watu wake.

Baada ya siku nne kwa kina Kaizari kulibishwa hodi, mke wake Kaizari, Subira ndiye alikwenda kuufungua, alisalimiwa kwa kofi kubwa kisha akaulizwa alikokuwa kidume chake kijoga. Walisemekana kuwa wao ndio vikaragosi waliotumiwa na wasaliti wao kuendelea kuwafukarisha. Alikatwa mikato miwili ya sime hata kabla hajajibu lolote, akazirai kwa uchungu. Kisha genge la mabarobaro watano likawabaka mabinti wake Kaizari, Lime na Mwanaheri. Alijaribu kuwaokoa lakini hakufaulu. Mahasimu hao wakaondoka baada ya kuutekeleza unyama huo bila kumgusa Kaizari, auguze majeraha ya moyo. Alijizatiti na kuwapa wanawe na mke wake huduma ya kwanza.

Punde si punde, sauti ya jirani yao Tulia iliita ikiwataka kutoka iwapo walitaka kuishi. Tofauti na majirani wengine, Tulia alimsaidia Kaizari kufunganya na kumsindikiza hadi njia panda. Alimkumbatia na kumwambia kuwa mwenyezi mungu ndiye hupanga na nguvu na mamlaka pia hutoka kwake. Akamjuvya kuwa uongozi mpya umezua uhasama kati ya koo ambazo Zimeishi kwa amani kwa karibu karne moja. Akamshauri aihamishe aila yake kwa muda kwa sababu ya usalama. Akamhakikishia kuwa huo sio mwisho wa kuonana. Huu utakuwa mwanzo wa uzao wa jamii mpya isiyojua mipaka ya kitabaka, jinsia na kikabila. Jirani alipompungia mkono, matwana ya abiria ilikuja nao wakaabiri. Ilikuwa ikiendeshwa kwa kasi kana kwa inakimbizwa. Waliyashuhudia mengi katika safari hii ya shaka kama vile mabasi kuchomwa pamoja na shehena zayo na hata mifyatuko ya risasi.

Hatimaye, gari lilikwisha petroli ikawa sasa ni mtu na malaika wake. Walijitoma msituni, kila mtu na aila yake. Walipata shida kwani chakula kilikuwa adimu. Kulikuwa na changamoto ya maji safi ya kunywa. Walikata miti wakajenga vijumba ambavyo viliezekwa kwa nyasi na kukandikwa kwa udongo. Wengi walipata homa ya matumbo na wengine kuyapoteza maisha yao. Wakimbizi walizidi kuongezeka nayo hali ya maisha ikazidi kuwa ngumu. Idadi kubwa ya wakimbizi ilifanya kuwe na vyoo vya kupeperushwa- yaani sandarusi ambazo hutumiwa kama misalani. Siku za mwanzomwanzo Kaizari hakuweza kutumia misala hii, lakini alisalimu amri na kusema potelea mbali, lisilo budi hutendwa. Lakini kutokana na tishio Ia maenezi ya kipindupindu aliwasihi kuchimba misala kwa jina long drop. Tatizo la njaa pia lilishamiri kwani waliokuwa wamebahatika kubeba nafaka chache walizitoa zikatumiwa na wote, zikaisha. Njaa ikawa inatishia kuwaangamiza wote, lazima wafanye jambo.

Asubuhi ya siku ya kumi na tano Selume(mke wa jirani yao aliyekuwa mpinzani mkuu wa Mwekevu) alipitia kwenye kibanda cha Ndugu Kaizari. Selume alikuja kuwaeleza kuwa alikuwa amesikia fununu kuwa upo mradi wa kuwakwamua Wakimbizi kutokana na hali hii. Shirika la Makazi Bora, lilikuwa limejitolea kuja kuwajengea wakimbizi nyumba bora. Misikiti na makanisa yalikuwa yamekusanya vyakula ili kuwalisha wahasiliwa. Watu walijawa na matumaini. Siku ya ishirini lori kubwa liliingia na watu wakakimbilia chakula kama watoto wafanyavyo. Watu waligawiwa chakula na akina mama( wa Mother's union, woman's Guild na waliokuwa wamepakiwa nyuma ya lori hilo. Msukumano ulianza hadi mlinda usalama mmoja alipojitokeza na kuwasihi kuweka usalama. Watu wengine kama Mzee Kaumu walishangaa walipokuwa hawa wangwana wakati madhila haya yalipowapata. Kwa kuwa tabia ni ngozi, Bwana Waziri Mstaafu aliyekuwa na uzoefu wa kuwaelekeza watu huko wizarani, alisaidia kukigawa chakula. Pia Kaizari na Selume waliitwa kusaidia. Hata hivyo, wengine walitumia ulaghai ( kama familia ya Bwana Kute- diwani wa hapo awali) kupata chakula kingi kuliko familia zingine.

Maswali

  1. Maisha katika mitaa ya mabanda ni kukatisha tamaa. Tetea kauli hii.
  2. Fafanua matatizo wanayoyapitia wakimbizi wa ndani kwa ndani.
  3. Fahali wawili wakipigana, nyasi huumia. Kwa kurejele sura hii, onyesho ukwei wa kauli hii.
  4. Siasa husababisha migogoro katika ndoa. Kwa kurejelea sura hii, tetea kauli hii kikamilifu.


Sura ya tatu

Baada ya kuishi katika msitu wa Mamba kwa miezi sita, Ridhaa, Kaizari na familia yake walibahatika kurudi nyumbani kufuatia mradi wa Operesheni Rudi Kanaani. Asubuhi hii Ridhaa ameketi katika chumba cha mapokezi katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Rubia. Ana hamu kuu ya kumwona Mwangeka akiwa mzima. Ridhaa anakumbuka kuwa siku ya kuhawilishwa kutoka Msitu wa Mamba hakuwa na matumaini ya maisha bora kwani hakuwa na mwenzi wala mtoto wa kuendea. Wengine kama Selume walikuwa wakilia kwa kuwa hawakujua waende wapi kwani mme wake amekwisha kuoa msichana wa kikwao na Babake alimkatalia katakata. Ridhaa alimfariji na kumwomba asilie kwani mwana wake yu hai tena ana kisomo na amehitimu kama mkunga, anaweza kujitegemea. Ndipo Ridhaa akamwahidi warudipo nyumbani, angemtambulisha Selume kwa mkuu wa Idara ya Afya ya Jamii katika Hospitali Kuu ya Tumaini. Leo hii, Ridhaa anapowaza haya, Selume amekwisha kuajiriwa kama muuguzi katika hospitali ndogo iliyojengwa karibu na kambi ya WWHN. Ridhaa anakumbuka mambo mengi kama vile kadhia iliyompoka familia yake ndiyo ilimkutanisha na watu kama Selume ambao angewaita ndugu na kumfanya kusahau msiba wa kuipoteza akraba yake. Kutangamana na wakimbizi kukamfunza thamani ya binadamu. Sasa amejifunza mengi kama vile uzima ni upande mwengine wa mauti. Kwenye Msitu wa Mamba, Ridhaa alipata huduma za ushauri na uelekezaji kutoka kwa wataalamu mbalimbali na akaweza ugonjwa wa shinikizo la damu ambao ulitokana na mshtuko wa kupoteza jamaa yake na mali yake dafrao moja. Hapo alipotoka kwenye msitu alijihisi kiumbe kipya kwani wapwa zake- Lime na Mwanaheri walikuwa wamepata matibabu. Dada yake Subira alitibiwa akapona. Mwamu wake Kaizari- amepona donda lilitokana na kuwaona binti zake wakibakwa. Ridhaa anamwona Kaizari ni afadhali kwani heri nusu Shari kuliko Shari kamili. Asubuhi hii, Ridhaa akiendelea kumngojea Mwangeka hakuweza kusahau jinsi alivyohisi aliporudi tena kwenye ganjo lake siku ile. Anakumbuka kuwa alipozinduka( kutoka kuzirai), alijipata katikati mwa kiunzi cha sebule lililokuwa kasri lake. Eneo hili ndipo wanawe Tila na Mwangeka walipokuwa wadogo walipenda kumkimbilia kila mara alipotoka kwenye shughuli zake za kikazi. Hapo ndipo kijukuu chake kilipozoea kutembea tata na kumwita "bubu" naye alipenda kukirekebisha na kukiambia "sema babuu". Hayo yote hayapo sasa, hata zile pambaja za mkewe Terry na utani wake hamna.

Akiwa yu pale katika kumbukumbu zake, polepole kwenye jukwaa la akili yake kunaanza kuigizwa mchezo wa maisha yake kabla ya dhiki iliyomfika. Anamwona Tila akitoka shuleni na kuuweka mkoba wake juu ya meza. Katika mazungumzo yao inabainika kuwa Tila ana upevu wa mawazo. Waliishi kujadiliana na Mwanawe Tila masuala nyeti kana kwamba walikuwa marika. Tila alijua kuwa Siku moja atakuwa jaji katika mahakama kuu na kuusafisha uozo uliotamalaki humo. Alitamani kuwaonjesha washukiwa waliowekwa rumande kwa miaka mingi utamu wa haki. Lakini sasa Tila hayupo tena, kilichobaki ni kumbukumbu zake.

Ridhaa aliona kuwa utabiri wa mwalimu wa la mabadiliko' ulikuja kutimia kwani viongozi wa awamu ya awali walibwagwa chini na vijana chipukizi. Kinaya ni kuwa wengi walishindwa kabisa kukubali kushindwa hasa yule aliyekuwa akigombea kilelecha cha uongozi. Kulingana naye nafasi hii iliumbiwa mwanamume na kumpa mwanamke ni maonevu yasiyovumilika. Kiongozi huyu alipita kila mahali akitoa kauli ambazo ziliwajaza hamasa wafuasi wake nao wakaanza fujo zilizoangamiza juhudi za miaka hamsini za raia za kuijenga jamii yao. Hatimaye ndege kwa jina PANAMA 79 iliyotarajiwa kufika saa tatu unusu sasa ndio inalikanyaga sakafu. Abiria waliposhuka, Ridhaa na Mwangeka walitazamana kimya. Ridhaa alihisi kana kwamba anauona mzuka wa Mwangeka, hakuamini kuwa angerudi nyumbani akiwa hai.

Hatimaye baada ya shaka kumwondokea, alimkumbatia mwanawe. Mwangeka akajitupa kifuani mwa babake kwa furaha. Ridhaa alimkaribisha Mwangeka nyumbani na kumtaarifu kuwa hakujua kuwa watawahi kukutana akiwa hai. Ridhaa akamjuwa mwanawe yaliyoisibu familia yao. Mwangeka alipomtazama babake akaona kuwa amekonga zaidi na sasa ameshabihi mno babu Mwimo. Baada ya kumbukumbu zake kumkumbusha ya awali Mwangeka alimshukuru babake na kumweleza kuwa alipoipata habari ya machafuko ya baada ya kutawazwa kwa kiongozi, alijawa na kihoro kisicho kifani. Mwangeka amekuwa akifuatilia matukio kwa makini kwani hata kura zilipohesabiwa upya kisha mpinzani wa Mwekevu kukubali kushindwa na kutoa wito kwa raia kusahau yaliyopita, alijua kuwa nchi imepiga hatua moja katika safari ndefu ya kupata afueni kutokana na tufani za baada ya kutawazwa.

Mwangeka aliendelea kuwapa heko vijana wenzake kwa kugundua kuwa wanatumiwa vibaya na viongozi wenye tamaa. Mwangeka akawa sasa anakubaliana na usemi wa Tila kuwa "usi cheze na vijana, wao ni kama nanga. Huweza kuizamisha marikebu " Japo Ridhaa aliyaitikia maneno ya Mwangeka kwa mgoto, alijua kuwa palikuwa na kazi ngumu ya kujenga upya ukuta ambao ufaa wake ulikuwa umepuuzwa. Akawa akawa anakubaliana na sera ya bintiye marehemu, Tila kuwa Vijana wanafaa kuelimishwa zaidi kuhusu amani kwani ndio wengi na ndio mhimili wa jamii yoyote ile. Hatimaye, Ridhaa alishusha pumzi na kumkabidhi mkono mwanawe na kumtaka waende ili akajipumzishe kutokana na adha za anga. Mengine watazungumza baadaye.

Maswali

  1. Fafanua sifa na umuhimu wa Ridhaa.
  2. Mwandishi ametumia mbinu rejeshi katika kuuwasilisha ujumbe wake. Onyesha namna alivyotumia mbinu hii,
  3. Fafanua sifa na umuhimu wa Tila kama zinavyo jitokeza katika sura
  4. Ni masaibu gani Wdhafidhing waliyapitia?
  5. Ni nini umuhimu wa Mwangeka? Rejelea sura hii.


Sura ya nne

Mwangeka ameketi mkabala mwa kidimbwi cha kuogelea nje ya jumba lake la kifahari ambalo yeye aliliona kama makavazi ya kumtonesha donda lililosababishwa na kifo cha mke wake Lily Nyamvula. Siku ile baada ya kutoka kwenye uwanja wa ndege walifululiza moja kwa moja hadi kwenye gofu la baba yake Ridhaa. Majivu yaliyokuwa mabaki ya kilichokuwa kwenye kasri lile yalibaki pale pale. Majivu hayo miili ya mama yake(Terry), wanuna wake, mkewe na mtoto wake. Mwangeka hakuelewa ni kwa nini babake hakuyaondoa mabaki hayo na ni kwa nini hakushirikiana na majirani kuchimba kaburi (mass grave) kuyazika majivu hayo. Baba mtu alimkazia tu macho. Machozi mazito ya machozi yalitunga machoni mwa Mwangeka, akayaacha yamcharaze yatakavyo. Wakati huu hata nyanya yake angekuwapo kumwonya dhidi ya kulia kama msichana angempuuza. Alihitaji kulia ili kuliondoa komango ambalo lilikuwa limefunga mishipa ya moyo wake. Alipolia, moyo wake ulilainika na moyo wake sasa ulijaa utulivu.

Mwangeka akakumbuka methali isemayo wino wa Mungu haufutiki. Hata hivyo alizidi kujiuliza iwapo binadamu aliandikiwa kumpoka binadamu mwenzake uhai. Siku ile baada ya wao kutoka kwenye uwanja wa ndege, Ridhaa alimwelezea Mwangeka mambo yalivyojiri. Alimweleza kuwa maisha yalibadilika pindi tu Mwangeka alipoondoka. Waliandamwa na msiba baada ya mwingine. Mwanzo, Ridhaa akapoteza majumba yake mawili. Miezi mitatu baadaye ami yake Mwangeka aliyeitwa Makaa alichomeka asibakie chochote alipokuwa akiwaokoa watu ambao walikuwa wakipora mafuta kutoka kwenye lori lililokuwa limebingiria. Makaa alizikwa pamoja na mabaki ya wahasiriwa wote katika kaburi moja kwani serikali iliwatayarishia mazishi ya umma. Baada ya Ridhaa kushusha pumzi, aliendelea kumweleza Mwangeka kuwa mambo hayo yote aliyakabili kwa msaada wa wanuna wa Mwangeka, mamake Mwangeka na rnkaza mwanawe. Akaanza kuyajenga upya maisha yake hadi Siku ile ambayo aliitazama familia nzima ikimponyoka.

Daktari Ridhaa amewaokoa wagonjwa wengi kutokana na magonjwa sugu lakini alishindwa kuuzima moto uliokuwa ukiiteketeza nyumba yao. Lakini, hakushindwa kwani hakuwepo tendo lenyewe likitendeka. Alikuwa ameenda kumfanyia majeruhi mmoja upasuaji. Ridhaa alipokuwa akirejea nyumbani akasikia sauti ya kite ya mamake Mwangeka, kisha mlipuko mkali. Yote yakaisha. Hadi hapo, ameyaishi maisha ya kinyama kupigania chakula na wahitaji wenzake. Ameonja shubiri ya kuwa mtegemezi kihali na mali. Lakini katika hayo yote amejifunza thamani ya maisha, udugu na amani.

Alimhurumia Mwangeka ambaye mkasa huo ulimfanya mjane hata kabla ya ubwabwa wa Shingo kumtoka. Baada ya kurejea kwake Mwangeka hakuishi na babake kwa muda mrefu. Mwanzo, hakuweza kustahimili uchungu uliosababishwa na kuamka kila asubuhi kutazama mahali ilipoangamia aila yake. Alimrai babake kila siku akibomoe kiunzi kile cha nyumba lakini babake alikataa katakata. Lilikuwa kaburi la ukumbusho wa familia yake. Sababu ya pili ni kuwa lazima Mwangeka angeyaanza maisha yake upya. Atafute ushauri kutoka kwa wataalamu, auguzie moyo wake mbali na babake. Mwangeka aliporejelea shughuli zake za kawaida kazini alitafuta kiwaja cha kujengea nyumba. Babake akamtahadharisha kufanya uchunguzi kabla ya kuanza ujenzi wenyewe. Baada ya Mwangeka kuhakikisha uhalali wa stakabadhi hii na ite alipata kipande cha ardhi karibu na ufuo wa bahari. Kazi ya ujenzi ilianza na baada takriban mwaka mmoja na nusu akahamia kwake. Hata anapokitazama kidimbwi hiki, mawazo yake yako mbali alikoanza maisha. Anawakumbuka wanuna wake: Kombe, Mukeli na Annatna(Tila). Anapomkumbuka Tila anatabasamu kisha tone moto la chozi linamdondoka. Kumbukumbu ya Annatila inavuta taswira ya mnuna wake mkembe aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka sita wakati ule Mwangeka akiwa na umri wa miaka kumi na miwili tanzia ile ilipowafika.

Katika jamii ya Mwangeka, kifo kilifuatwa na viviga vya aina mbalimbali yakiwemo maombolezi. Basi baada ya kifo cha mtoto huyo majirani walikuja kuifariji familia ya Bwana Ridhaa. Wiki mbili baada ya mazishi ya ndugu yake, Jumamosi moja Mwangeka alimpata Tila na wenzake nyuma ya nyumba wakimngojea. Tila alimvuta na kumnong'oneza kitu sikioni kisha akavuta boksi lililokuwa limetiwa mwanasesere wao kwa jina Dedan Kimathi lakabu waliokuwa wamempa marehemu ndugu yao Dede. Walianza kulia na kuomboleza kifo cha Dedan Kimathi. Wakaimba mbolezi. Katika hali ile ya kuomboleza, watoto hawa hawakujua kuwa baba yao alikwisha kuja dakika thelathini zilizokwisha. Akawa anawatazama watoto hawa wakiigiza mazishi ya ndugu yao Dede. Alibanwa na hasira na kuutwa mshipi wake kutoka kiunoni, akamshika Mwangeka na kumwadhibu vikali. Akamkemea Mwangeka kwa kuwa bendera inayofuata upepo badala ya kuwa kielelezo bora kwa mnuna wake Tila. Mwangeka anapokumbuka kisa hiki anajutia ni kwa nini hakukiomboleza kifo cha Tila. Baada ya kipigo hiki, Mwangeka aliwajibika zaidi akayavalia masomo yake njuga hadi chuo kikuu ambako alisomea uhandisi. Hapo ndipo alipokutana na mke wake Lily Nyamvula. Nyamvula alikuwa akisomea uanasheria. Mwangeka alihitimu masomo yake na kujiunga na kikosi cha wanamaji, jambo hili liliwashangaza wengi.

Maswali

  1. Eleza kwa muhtasari mambo yalivyokuwa Mwangeka aliporudi nyumbani.
  2. Ni kwa nini Mwangeka alimwona Ridhaa(babake kama) mwehu?
  3. Eleza misiba aliyomwandarna Ridha kama iivyoonyeshwa katika sura hii.
  4. Jadili maudhui ya koma yaivyoangaziwo katika sura hii.
  5. Eleza sifa nne za Tila.
  6. 'Kama ningeusikiliza ushauri wa Tausi wangu labda ningeweza kuiokoa aila hii '
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.
    2. Eleza kwa kifupi jambo ambalo aila ya msemaji ilikumbana nalo.
    3. Eleza sifa na umuhimu wa anayeitwa 'Tausi wangu'
  7. Jadili maudhui ya elimu kama yanavyojitokeza katika sura hii


Sura ya tano

Msitu wa Mamba uligeuka kuwa nyumbani kwa maelfu ya watu waliogura makwao bila tumaini la  kurudi. Walijipa moyo na kusema kuwa hata walikokuwa wakiishi hakukuwa kwao, walikuwa maskwota. Wakaamua kula asali na kuyanywa maziwa ya Kanaani hii mpya isiyokuwa na mwenyewe. Matokeo ya maamuzi haya yalikuwa ni kukatwa kwa miti kwa ajili ya kupata mashamba ya kupandia vyakula na kwa ajili ya ujenzi. Kabla ya miaka miwili kuisha, pahali hapa palikuwa pamepata sura mpya- majumba yenye mapaa ya vigae, misitu ya mahindi na maharage, maduka ya jumla, viduka vya rejareja kila mmoja akijibidiisha kufidia kile alikuwa amepoteza.

Familia ya Bwana Kangata ilikuwa miongoni mwa zile zilizoselelea(zilizoishi) kwenye msitu huu. Kwa Kangata na mkewe Ndarine hapa palikuwa afadhali. Awali wakiwa wamelowea katika shamba Ia mwajiri wao aliyekuwa akiishi jijini. Waliishi pale kwa muda mrefu hata watu wakadhani kuwa ilikuwa milki yao. Wengine wakidhani Kangata na familia yake walikuwa akraba ya mwajiri wao. Hata wana wa Kangata walipokwenda shuleni walijisajilisha kwa jina Ia tajiri wa baba yao. Walikuwa wakiitwa Lunga Kiriri, Lucia Kiriri na Akelo Kiriri. Kiriri likiwa jina Ia Mwajiri wa Kangata. Kangata na mwajiri wake walikuwa wamesekuliwa kutoka mtaa wa Matunda katika zile patashika za baada ya kutawazwa. Kiriri aliiaga dunia muda mfupi kutokana na kihoro cha kufilisika na ukiwa aliokuwa ameachiwa na mkewe Annette na wanawe. Walipata Green Card na kuhamia ughaibuni. Hivyo basi, juhudi za Kiriri kumshawishi mkewe asimnyime ushirika wa Wanawe ziliangukia moyo wa Firauni. Mkewe Kiriri alikuwa ashaamua kuwa hapa hapamweki tena. Kazi aliyokuwa akiifanya katika afisi za umma kama mhazili mwandamizi kwa miaka mingi ilikuwa inamfanya kusinyaa, akawa hana hamau akahisi kinyaa. Wanawe walipoenda kusomea Ng'ambo - wafanyavyo wana wa viongozi kwa kuwa wanaiona elimu ya humu kama isiyowahakikishia mustakabali mwema raia wake, yeye alistaafu mapema na kuchukua kibunda cha mkupuo mmoja almaarufu Golden Handshake akachukua Green Card na kuwafuata na kumwacha mume wake akiwa mpweke.

Baada ya wana wa Kiriri kumaliza masomo yao walibakia huko huko Uzunguni kufanya kazi. Walipuuza rai baba mtu za kurudi nyumbani ili kuziendesha baadhi ya biashara zake. Kila mmoja akajishughulisha na mambo yake. Kifungua mimba wa Kiriri kwa jina Songoa alisema kuwa nchi yao haina chochote kumfaa kwa hata walio na shahada tatu bado wanalipwa mshahara mdogo sana, akaona heri awekeze huko mbali aliko na imani nako. Kabla ya kifo chake, Kiriri alikuwa akiibua mijadala nafsi akilini mwake kuhusu Waafrika ambao ni kama waachao mbachao kwa mswala upitao. Akawa anajiuliza maswali mengi kama vile ni nini huwavutia raia kuhamia ughaibuni? Je ni hiyo mishahara minono wanayolipwa? Je, ni hizo kazi za kujidhalilisha za kwenda kuwauguza maajuza waliotelekezwa na aila zao? Au ni zile ndoa kati ya vijana wakembe wa Kiafrika na vikongwe vilivyochungulia kaburi? Kiriri aliendelea kushangaa ikiwa mkewe amegeuka wale wake pindi wafikapo ng'ambo hufunga ndoa na waume wengine kwa kuwa ndio njia pekee ya kuufukuza upweke na kupata riziki au kwa kuta kujikwamua kwenye tope la uhawinde?

Kutokana na uzoefu wake katika kilimo, Kangata alipofika katika Msitu wa Mamba aliweza kuendeleza kilimo chenye natija. Kwa sasa, miaka mitano imepita na Kangata na Ndarine wameipa dunia kisogo. Lucia Kiriri-Kangata ameolewa katika ukoo wa Waombwe ambao awali walikuwa maadui sugu wa ukoo wa Anyamvua. Ndoa hii ilipata pingamizi sana kutoka kwa ukoo mzima lakini kutokana na Msimamo imara wa Kangata ndoa hii ilisimama. Watu wa ukoo wa kina Kangata walishangaa ni kwa nini mwana wao akaozwa kwa watu ambao huvaa nguo ndani nje na pia huzaa majoka ya mdimu ambayo ni machoyo kupindukia. Kangata aliyatupilia maneno ya watu wa ukoo wao kwani Kiriri aliyadhamini masomo ya mabinti zake hata ingawa walikuwa wa ukoo tofauti na wake. Watu wa ukoo wa Kangata walikuwa wakipinga elimu ya msichana na kutoa rai kama kumuelimisha msichana ni kufisidi raslimali. Kangata anashangaa wakati mwanawe ameneemeka na kuishi maisha ya heri ndio wakati jamaa zake wameona tofauti za kiukoo. Hatimaye ukoo wa Kangata ulikubali muungano huu wa ndoa na ukawa umeyeyusha tofauti na chuki iliyokuwa baina yao. Nasaba hizi mbili zikawa sasa zinapikia chungu kimoja.

Naye Akelo Kiriri-Kaango habari yake haijulikani. Baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha nne, alipata kuolewa na dereva wa malori yanayosafirisha bidhaa hadi Zambia. Jina la dereva huyo ni Kaango. Alipomwoa Akelo Kiriri, alimjengea nyumba katika gatuzi la Mbuyuni na tetesi zinasema kuwa walipata watoto wawili. Mmoja kwa jina Ngaire na mwingine Mumbi. Hakuna ajuaye walikopelekwa na misukosuko ya miaka mitano iliyopita. Lunga Kiriri —  Kangata ndiye anaishi katika milki ya babake katika Msitu wa Mamba. Yeye amesomea kilimo. Awali alikuwa ameajiriwa kama afisa wa kilimo nyanjani. Alikuwa akiwaelimisha raia kuhusu mbinu bora za kilimo kama vile watu wasilime karibu na mito, watu wachimbe mitaro kuzuia mmonyoko wa udongo na watu wapande miti inayostahimili ukame. Alikuwa amirijeshi wa uhifadhi wa mazingira. Alipokuwa shuleni ndiye aliyekuwa mwasisi wa chama cha watunza mazingira wasio na mipaka. Kila ijumaa wakati wa gwaride ungemsikia akihutubia wanafunzi wenzake kwa mhemko. Kimondo (mwanafunzi mwenzake Lunga) alikuwa haishi kushangazwa na Lunga kwani mtu akimsikiliza Lunga hangedhani kuwa amekulia mazingira sawa na wale wanyonge ambao uwepo wao huamuliwa na matajiri. Ilishangaza kuwa Lunga hakuwazia kwamba alikolowelea baba mtu palikuwa msitu tu, tajiri wake akapabadilisha.

Babake Lunga haswa ndiye aliyeliendeleza shamba lile. Aliendelea kumuuliza iwapo hajui kwamba umaskini unaweza kuupujua utu wa mtu akatenda hata asivyokusudia kutenda. Lunga hangeweza kujua kwani hajawahi kulala njaa akakosa usingizi kutokana na mkato wa njaa ilhali baba mtu anavuna kahawa katika shamba kubwa Ia Mzungu. Mzungu huyu mwenye shamba akiwa anapata mamilioni ya pesa lakini anawapunja wafanyakazi wake kwa kuwalipa kishahara duni kiasi cha wao kushindwa kuwanunulia wana wao sare mpya. Kimondo anaendelea kumwambia mwenzake Lunga kuwa hajawahi kuamka asubuhi huku anakeng'etwa na tumbo na homa ya matumbo inamwandama. Mwalimu anapokupa barua ili ukatibiwe kwenye kituo cha afya kilichoko ndani ya kijiji ambacho mwenye kahawa amewajengea wafanyakazi, Daktari mwafrika anakataa kukupa huduma kwa kuwa wazazi wako hawajawekewa bima kutokana na kijishahara duni wanacholipwa.

Sasa Lunga ni mkulima stadi. Ametononokea si haba katika msitu huu. Hakumbuki kuwa msitu huu unafaa kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye. Kabla ya shida kumleta hapa mstakabali wa maisha ya Lunga ulitishia kuporomoka. Alikuwa ameipoteza kazi yake ya Ukurugenzi katika kampuni ya Maghala ya Fanaka alikopinga kitendo cha raia kuuziwa mahindi ambayo yalikuwa yameagizwa kutoka ughaibuni. Mahindi ambayo licha ya kuwa na rangi ya njano, yalihofiwa kuwa yameharibika. Yalikotolewa yalisemekana kuwa hatari kwa usalama hata wa panya. Lunga alipopinga uuzaji wa mahindi haya kwa raia vijisababu vilitolewa na vigogo wenye shehena za mahindi haya. Walidai kuyakataa mahindi haya ni kama kuidhinisha kifo cha mamilioni ya raia ambao hawamudu kujinunulia hata kibababa cha unga. Hata hivyo, rai za wakubwa ziliambulia patupu kwani Lunga alikataa katakata. Lunga akawa amehiari kupoteza kazi yake ili kuyaokoa maisha ya wanyonge wasio na hatia. Baada ya mwezi mmoja Lunga akiwa ofisini mwake alitumia barua ya kumstaafisha kwani shirika hili lilikubwa na changamoto ya kifedha na hivyo halmashauri ikachukua hatua ya kupunguza idadi ya wafanyakazi. Lunga alipoisoma barua hii mara mbili alishangazwa na ukosefu wa fadhila wa waajiri wake. Kweli asante ya punda ni mateke. Lunga alipokuja katika Msitu wa Mamba alikuwa na azma ya kumhamisha babake na kuwachia wanyama Edeni pao lakini aliyoazimia siyo aliyotenda. Lunga alipokutana na ekari thelathini na tano za mahindi aliingiwa na tamaa na uchu akausaliti uadilifu wake. Tamaa ya kulima maekari na maekari zaidi ikamkumbatia akakata miti zaidi. Alipoulizwa ilipofia jadhba ya kupigania uhifadhi wa misitu alisema mungu mwenyewe alitupa ulimwengu tuutawale, sio ututawale.

Siku zilivyosonga, mashamba ya Lunga na wenzake yakendelea kutoa mazao mengi nayo jamii ya Msitu wa Mamba ikazidi kupanuka nazo tofauti za kitabaka zikazidi kujionyesha. Kundi Ia kwanza la wakimbizi Ridhaa, Kaizari na Kangata hamkuwa na tofauti kubwa. Mpito wa wakati ukazaa matajiri kama Lunga ambaye alikuwa akiwakumbusha wenzake kuwa alitokana na jadi ya kifahari ya Kiriri. Kulikuwa pia na maskini ambao kupata kwao kulitegemea utashi wa matajiri. Polepole uhasama ulianza kutishia kuisambaratisha jamii ya Msitu wa Mamba. Viongozi nao kwa kuhofia mambo kuharibika, walianza kampeni za kuwaelimisha raia kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani licha ya tofauti zao za kiusuli. Hata hivyo juhudi hazikufua dafu kwani awamu ya kwanza ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ilianza.

Walinda usalama walipokuja kudumisha amani, walitumia bunduki zao na kuwaacha wengi wakiwa wafu nao watoto wakabaki wanawakiwa. Kisa hiki kiliwafungua macho viongozi wakatambua kuwa wakazi hawa walikuwa wakiishi hapa kiharamu. Vyombo vya habari vikatoa wito kwa chama tawala kuwatafutia mahali kwingi, vidonda vya zamani vikanza kutoja damu. Juhudi zao za kuandama ya uamuzi wa kuhamishwa kwao hazikufua dafu. Wachache walifanikiwa kurudi kwao katika awamu ya pili ya Operesheni Rudi Kanaani. Wengine kama Lunga ambaye hakujua kitovu chake hasa walitimuliwa pamoja na familia zao. Baada ya miezi mitatu Lunga aligundua kuwa amerudishwa kwenye Mlima wa Simba ambako inaaminiwa mababu zake walikuwa wamehamia kutoka Kaoleni, siku za biashara ya watumwa. Msitu wa Mamba ulibaki tasa. Mto uliokuwa hapo karibu, ambao ulikuwa umeanza kukauka sasa ulianza kutiririsha maji. Jambo la kushangaza ni kwamba, hata baada ya tangazo kutolewa kuwa msitu huu ni marufuku kwa binadamu, usiku wa manane kulisikika milio ya malori na matrekta yakibeba shehena za mbao, makaa na mahindi. Moshi pia hufuka mle mara kwa mara.

Maswali

  1. Eleza sifa za wahusika hawa: (alama 10)
    1. Lunga
    2. Kimondo
    3. Kangota
  2. "Kuukata mkono niliostahili kuubusu yalinifika ya kunifika "
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili (alama 4)
    2. Eleza namna msemaji alivyoukata mkono aliostahili kuubusu (alama 6)
    3. Fafanua mambo mawili yaliyomfika msemaji (alama 2)
    4. Taja tamathali mbili za usemi ziizotumika katika dondoo
    5. Eleza kwa kifupi namna msemaji alivyobadilika baada ya "yaliyomfika kumfika " (alama 6)
  3. Tofauti za kitabaka huzaa uhasama " Tetea kauli hii kwa Kurejelea sura hii (alama 20)
  4. Fafanua matatizo wanayoyapitia vibarua na familia zao (ala. ma 20)
  5. Mashirika mengi ya kiserikali huendeleza uozo. Tetea kauli hii kwa kurejelea matukio katika sura hii (alama 20)


Sura ya sita

Sura hii inapoanza tunampata Mwalimu Dhahabu akimtaka Umulkheri kuyarudisha mawazo yake darasani. Mwalimu huyu kwa kawaida ni mcheshi. Umu(ufupi wa Umulkheri) aliyarudisha macho yake darasani yakatazamana na ya Mwalimu Dhahabu bila yeye Umu kumwona mwalimu mwenyewe. Tangu Umu kujiunga na shule hii katika kidato cha pili anajihisi kama samaki aliyetiwa kwenye dema. Haya mazingira ni mageni kwake na hakuja hapa kwa hiari. Baridi ya mahali hapa inamsinya kwani si kama kwao ambako kulikuwa na hari. Ukweli ni kuwa Umu alikuwa na kwao ila sag hana. Amebaki kuishi kwa hisani ya mkuu wa shule ya Gamano aliyeshauriwa na Wizara ya Elimu kumsajili Umu na wengine watano. Umu ni mwana wa pili wa Bwana Lunga Kiriri — Kangata. Uongozi ulipoamua kuwahamisha hadi Mlirna wa Simba, Umu alikuwa ndio anajiunga na kidato cha kwanza.

Kule kuhamia Mlima wa Simba hakukumkalia vyema Lunga. Aliona kuwa alikuwa ameyapoteza maisha yake pamoja na ndugu na marafiki zake. Wanawe walikuwa wakisomea katika Shule za kifahari na sasa fidia aliyopewa na serikali haitoshi hata kuwapeleka wanawe katika Shule za watu wa kima wastani. Lunga alipohamia Mlima wa Simba mke wake Naomi naye hakuwekwa na mazingira haya mapya. Asubuhi moja alimtumia Lunga ujumbe na kumtaarifu kuwa ameondoka ili akatambe na ulimwengu na huenda akaambulia Cha kumsaidia Lunga kuikimu familia. Akawaacha Lunga na wanawe. Pigo hili la tatu lilimuuma Lunga sana kwani alijisabilia kwa hali na mali kumpendeza mkewe. Naomi alilipa penzi lake na kumwachia Lunga adha za malezi jambo ambalo Lunga hakustahimili. Mwaka mmoja wa kwanza ulimwia Lunga mgumu mno kwani ilimlazimu Lunga kuwa mama na baba wa watoto wake. Katika hali hii Lunga aliingiwa na wahka na kihoro na hatimaye ugonjwa wa shinikizo la damu ukampata. Kabla ya mwisho wa mwaka huo Lunga alifariki na kuwaacha watoto wake na mikononi mwa kijakazi wao.

Asubuhi moja Umu aliamka na kujipata yu pweke nyumbani mwao. Ndugu zake wawili, Dick na Mwaliko walikuwa wametoweka. Umu alijaribu kumwita kijakazi Sauna kumjuza lakini alisalimiwa na cheko la mwangwi wa sauti yake katika sebule. Umu alimaka, hajui awafuate wapi ndugu zake wakembe. Dick alikuwa darasa la saba naye mwaliko alikuwa katika darasa la kwanza. Picha ya watoto waliotekwa nyara ilimjia Umu akilini mwake ikakifanya kichwa chake kumwanga kwa maumivu. Mwishowe alipiga ripoti katika kituo cha polisi alikoulizwa maswali mengi kuhusiana na kukosekana kwa ndugu zake. Baada ya kuripoti habari hiyo Umu alijizoaoa na kujiendea zake nyumbani. Maisha ya Umu sasa yalichukua mkondo mpya. Siku ile baada ya kuwapigia polisi ripoti, ilibainika wanuna wake walikuwa wametekwa nyara na Sauna kwani hayo ndiyo yalikuwa mazoea ya Sauna. Sauna alikuwa akijifanya mwema kwa waajiri wake ili aaminiwe ili naye apate fursa ya kuwaiba watoto na kuwapeleka kwa bibi mmoja ambaye aliwatumia katika biashara zake na katika ulanguzi wa dawa za kulevya.

Machozi ya uchungu yalimtiririka Umu na hakuamini kuwa nduguze wadogo walikuwa mali ya mtu atakayewatumia kama kitega uchumi. Baada ya kutia na kutoa, aliona kuwa hapo hapamweki tena akaamua kuondoka. Asubuhi moja Umu alifika kwenye kituo cha gari moshi. Sasa yu katikati mwa jiji la Karaha. Woga mkubwa ukamkumbatia kwa kutojua alikokuwa kwani mji huu ni mpya kwake. Hajawahi kutembea hapa peke yake. Hata hivyo, Umu yu tayari kuanza maisha upya katika jiji hili. Hajui vipi lakini penye nia ipo njia. Baada ya kuwaza na kuwazua, Umu alijikokota na kuchukua njia iliyoelekea kushoto. Alipofika Church Road mara moja aliikumbuka njia hii. Aliwahi kupitia pale zama za utukufu wa babake. Anakumbuka akiwapata ombaomba wengi karibu na kanisa Ia Mtakatifu Fatma. Anakumbuka namna alivyomsihi mamake kumpa noti ya shilingi mia moja ili amkabidhi mmoja wa ombaomba wale. Mama mtu alikatalia ombi Ia Umu lakinl hatimaye baada ya Umu kusisitiza mno, mamake alimkabidhi shilingi ishirini naye umu akaongeza mapeni aliyokuwa akipewa na babake na kumkabidhi ombaomba mmoja shilingi 40. Ombaomba huyo alimshukuru na kumwita sistee na kuahidi kuwa siku moja atamsaidia Umu. Leo hii Umu anashangaa iwapo bahati itamvutia usaidizi hata kutoka kwa yule maskini wa Mungu. Akipewa msaada wowote hata kama ni jamvi la kuuweka ubavu wake usiku kwenye mitaa atashukuru. Alielekea kwenye mkahawa mkubwa mkabala mwa kanisa. Aliwaona vijana wengi wa mitaani. Umu akayaangaza macho yake kuona kama atampata rafiki yake. Hakumpata wala hakuona yule aliyekaribiana naye. Alikataa tamaa. Aliamua kuendelea na safari yake, huenda atampata kanisani. Kisadfa, kabla hajatembea hatua chache kutoka pale aliskia sauti ikiita "kipusa". Alipogeuka alimwona yule kijana kazaliwa upya! Nadhifu! Meno meupe! Alijitambulisha kwake Umu kama Hazina.

Serikali ilimwokoa kutokana na kinamasi cha uvutaji gundi na matumizi ya mihadarati. Akapelekwa shuleni akasoma. Walijengewa makao ambapo yeye na wenzake wanaendelea kusaidiwa na kupewa mbinu za kukabiliana na maisha. Hazina alibahatika kujifunza upishi na huduma za hotelini na sasa hivi anafanya kazi kama mhudumu katika hoteli hiyo. Hazina alimwomba Umu waende akanywe chai. Umu alimtazama Hazina huku kaduwaa. Akamfuata hotelini alikokula shibe yake. Alimsimulia Hazina mkasa huku mito ya machozi ikiwatiririka wote wawili. Hazina alimwonea imani umu kwa kuharibikiwa na maisha katika kipindi ambapo anahitaji hifadhi ya wazazi. Umu machozi yake yalikuwa mchanganyiko wa furaha na majonzi. Furaha kwa kuona kuwa rafiki yake amefaulu kujitoa katika hali ya utegemezi. Huzuni kwa sababu anahisi kuwa ndugu zake wawili huenda ndio walichukua nafasi ya Hazina katika mitaa ya miji.

Hazina alimwahidi kuwa atamsaidia. Akampeleka moja kwa moja hadi kwenye makao yao na kumjulisha kwa Julida mama aliyesimamia makao haya. Julida alimkaribisha na kumtaka asijali. Hapo pangekuwa nyumbani mwao kwa muda kisha Julida wangewasiliana na Idara ya Watoto kuhusu suala la ndugu zake Umu. Ndugu zake wangetafutwa na wangepatikana. Mwezi mmoja baadaye, Umu alijiunga na Shule ya Tangamano akajiunga na kidato cha pili ambako alijipata kuwa mgeni. Mwalimu Dhahabu akatambua kwa wepesi unyonge aliokuwa nao Umu. Mwalimu huyu akataka pia kujua usuli wa Umu kutoka kwa mwalimu wa darasa la Umu. Mwalimu huyu wa darasa alipoyahadithia masaibu ya Umu kwa Mwalimu Dhahabu, Bi Dhahabu akawa haishi kumhimiza Umu kuwa jasiri kukabiliana na hali yake hii mpya. Hata hivyo ilimwia vigumu Umu kusahau yaliyopita. Hata hivyo Umu aliendelea kuhimizwa na wenzake ayazoee maisha haya mapya. Siku moja Kairu alimweleza Umu kuwa ana bahati sana kwani yeye hakupitia waliyoyapitia wao.

Wao walitendwa ya kutendwa. Wao walipofurushwa kwao siku hiyo hakujua waendako. Mama akiwa mbele nao kina Kairu nyuma. Mama yao alikuwa amembeba kitindamimba ambaye alijifia mgongoni mwa mamake. Baada ya kuuzika mwili wa ndugu yao, kina Kairu waliendelea na safari wasiojua mwisho wake. Hatimaye nguvu ziliwaisha mama yao akawaashiria kuketi kando ya njia, wakawa wanangojea kifo. Mara waliwajia watu waliokuwa wamevaa mavazi yaliyoandikwa IDR,wakasombwa na kutiwa kambini walikokuwa wamejaa sana watoto kwa watu wazima. Hali hapo ilikuwa ngumu. Miiko ilivunjwa. Waliwmil ia wakawa wanaishi kwa tumaini wakidhani hali itatengenea. Wakatumaini kwamba wangerudi kwao. Lakini kinyume na matarajio, uongozi mpya hukuleta afueni yoyote katika maisha yao. Kilichobadilika ni kuwa walipewa ardhi zaidi ya kujenga mabanda zaidi ili kupunguza msongamano katika mabanda ya awali.

Sasa wako pale pale. Kairu alikwenda pale akiwa darasa la sita na sasa ako kidato cha pili. Wangali wanasubiri kurudi nyumbani ila yeye haoni kama mna nyumbani pema zaidi ya hapo kambini ambako wanaishi bila kujali mtu alikotoka. Kairu alimsihi Umu kuvumilia na kuzingatia masomo kwani ndiyo yatakayomtoa katika lindi hilo la huzuni. Kairu aliendelea kumweleza Umu kuwa ana bahati kupata mfadhili. Yeye Kairu, mzazi wake wa pekee ni mama ambaye ni muuza samaki na baada ya ule mzozo wa ni nani kamiliki Ziwa kuu, biashara yao imedidimia sana. Samaki wamekuwa adimu sokoni na bei yake imepanda. Mamake Kairu hana mtaji wa kuanzisha biashara nyingine kwa kuwa yeye ni maskini. Maisha yamemwia magumu kwani hata karo yake Kairu imembidi amlilie mwalimu mkuu amruhusu alipe kidogokidogo hadi mwisho wa mwaka. Katika mazungumzo ya Kairu inabainika kuwa babake yu hai na ana familia nyingine na kuwa Kairu alizaliwa nje ya ndoa. Umu anapoyaweka masaibu ya Kairu kwenye mizani anaona kuwa anaona msiba wake kuwa mwepesi sasa.

Mwanaheri naye alianza kusimualia na kusema kuwa baada ya kurudishwa nyumbani kutoka Msitu wa Mamba baba yake Mwanaheri- Mzee Kaizari, aliweza kuyajenga maisha yao upya. Akajenga nyumba kufu yao pale kwenye ganjo lao. Yeye na dadake Lime walirudi shuleni mlemle kijijini mwao tu. Ikawa rahisi kuyazoea maisha kwani wanafunzi wenzao waliwapenda sana. Lime alikuwa hodari katika michezo ya kuigiza- ile ya kitoto. Alikuwa mcheshi mno na kutokuwapo kwake shuleni kuliwafanya watoto kumpeza. Mwanaheri alikuwa naye anakipalilia kipaji chake cha kughani mashairi mepesi. Majirani wao nao wakamsaidia baba yao kukabiliana na hali hii mpya ya maisha hata hivyo baba mtu alikuwa na hofu kuwa huenda wangeshambuliwa tena, nao majirani walimhakikishia kuwa hawangeruhusu jambo lolote kuusambaratisha tena udugu baina yao. Kwa hivyo hali ya utulivu ilitawala tena. Uhusiano kati ya marehemu mamake Mwanaheri na mavyaa yake ulikuwa umeingia ufa. Mama mkwe daima alikuwa akimwonea gere mkaza mwanawe kwa kumwona kama aliyekuja kumbwakura mwanawe. Hali hii ikawa imezidishwa na tofauti za kikabila kati ya mamake Mwanaheri na babake. Mamake ametoka kwenye jamii ya Bamwezi. Daima anachukuliwa kama mgeni, si katika boma lao tu, bali katika kijiji kizima. Uhasama ulizidi baada ya vurugu za miaka mitano iliyopita. Nyanya yao akimwona mamake Mwanaheri kama chanzo cha kuharibiwa kwa mali yao, kwamba ndiye aliyewafanya majirani kuwachomea boma lao. Mamake Mwanaheri alidhoofika kiafya kwa majonzi ya kutengwa na wale aliowadhania kuwa wa aila yake. Siku moja waliamka na kupata kibarua juu ya meza dogo iliyokuwa chumbani mwa Mwanaheri. Mwanaheri alipofungua barua hii alipata kuwa mama mtu alihiari kuondoka kwa kubaguliwa, kufitiniwa na kulaumiwa kwa asiyotenda. Mwanaheri aliendelea kuwahadithia wenzake na kusema kuwa baada ya miezi miwili babake alienda kumtafuta mamake kwao asimpate. Baada ya kujuzwa kuwa mama mtu alikuwa ameenda mjini Kisuka kuzumbua riziki, babake Mwanaheri alifululiza mjini kwenda kumtafuta mke wake akiwa menye majuto. Alimtafuta na kumtafuta mwezi baada ya mwezi na alipompata alikuwa amejifia chumbani mwake baada ya kutumia kinywaji kikali. Baba mtu alifanya juhudi na mabaki ya mamake Mwanaheri kuzikwa. Mwanaheri alipomaliza kuhadithia kadhia yake, matone mazitomazito ya machozi yalikuwa yakimdondoka. Umu na Kairu walimwacha autue mzigo wake. Sasa Umu alianza kuhisi mzigo wake ulikuwa mwepesi sana. Mwanaheri aliendelea kuhadithia kuwa mara nyingi mwalimu anapofundisha mawazo yake hutangatanga. Yeye hujiuliza ni kwa nini mamake akakitekeleza kitendo hicho cha ubinafsi. Kwa kuwa maji yamekwishamwagika, sasa ameamua kuufuata ushauri wa Mwalimu Dhahabu wa kuandama elimu kama ya kumwezesha kuleta mabadiliko katika jamii. Mwanaheri anasema kuwa iwapo mamake angefuata mikakati bora zaidi ya kuhusiana na wakwe zake badala ya kukata tamaa, huenda maisha yake Mwanaheri na ndugu zake yangekuwa bora zaidi.

Zohali naye alikuwa akiusikiliza utambaji wa marafiki zake nacho kilio kikawa kinamwandama. Baada ya kuwaza ikiwa atawatolea wenzake dukuduku lake hatimaye aaliamua kuwasimulia. Yeye alikuwa mtoto wa nyumba kubwa. Babake alikuwa mkurugenzi katika Shirika la Utoaji wa Huduma za Simu na mamake alikuwa mwalimu mkuu wa Shule maarufu ya kitaifa. Wazazi wake walikuwa walezi wema. Zohali na nduguze hawakupungukiwa na chochote. Maisha yake Zohali yalianza kwenda tenge alipojiunga na kidato cha pili. Mtafaruku wa kihisia katika umri huo ulimfanya kufanya mambo kwa papara na kutahamaki akawa ameambulia ujauzito. Mwalimu mkuu alimtaarifu dadake Zohali kuwa aikuwa mjamzito na alifaa kurejeshwa nyumbani na akisha kujifungua wazazi wake waweze kumtafutia Shule nyingine. Tima(dadake Zohali) alimaka. Kutoka siku hiyo maisha ya Zohali yalichukua mkondo mpya. Amewahi kulala katika barabara za jiji pamoja na watoto wengine wa mitaani, amewahi kutumia gundi ili kujipurukusha, amewahi kupigana na majitu yaliyokuwa yakitaka kuuhujumu utu wake kwa kumnyanyasa kijinsia. Wakati wenzake waliona siku zake za kujifungua zimekaribia za kujifungua walimpeleka kituo cha Wakfu wa Mama Fatma. Alikuwa ameyapitia mengi. Zohali anamshukuru Mtawa Pacha aliyemwokoa kutokana na kinamasi cha unguliko la moyo. Baada ya Zohali kumweleza kadhia yake, Mtawa Pacha alitikisa kichwa na kumwahidi kwamba baada ya kujifungua angemrejesha shuleni. Sasa hivi anapoongea anafaa kuwa kidato cha nne lakini uzazi na ulezi ulimpotezea miaka yake miwili. Huwa anatamani sana kumwambia Mtawa Pacha ukweli wa mambo kuwa ana wazazi lakini moyo wake hukataa katakata. Atamwambiaje kuwa ana wazazi ilhali waliisha kumkana alipohitaji pendo lao? Anaendelea kusema kuwa madhila aliyoyapitia nyumbani kwao hayaelezeki. Baba yao alisema kuwa hakuwa na pesa za kulipa kijakazi tena. Kazi zote za nyumbani zikawa za Zohali. La kusikitisha zaidi ni, mama mtu ambaye anajua uchungu wa kule mimba hakutoa sauti ya kumtetea. Baada ya Zohali kuyakamilisha masimulizi yake aliyaondoa macho yake kwenye ukuta yalikokuwa yameganda.

Chandachema alifuata kusimulia kadhia yake. Kisa chake kikiwa na mshabaha na kile cha Zohali. Alilelewa na bibi yake aliyefariki Chadema akiwa darasa la kwanza. Habari ilisema kuwa baba yake Fumba alikuwa amehamia Uingereza na familia yake na ni mhadhiri katika Chuo kikuu. Baada ya nyanyake kuiaga dunia, mambo yake Chadema yalijaa giza.

Maswali.

  1. Elezea kwa kifupi madhila aliyoyapata Zohali nyumbani mwao.
  2. Eleza kwa muhtasari kadhia aliyoipata Chandachema tangu kufariki kwa nyanyake.
  3. Mwandishi ametumia mbinu rejeshi kwa mapana no marefu katika sura hii. Fafanua jinsi ilivyotumika kwa kutolea visa vitano kwa muhtasari.
  4. Fafanua maudhui ya malezi kama ya!ivyojitokeza katika suro hii.
  5. Fafanuo sifa za waahusika hawa.
    1. Mwajimu Dhahabu
    2. Umu
    3. Hazina
    4. Kairu
    5. Mvvancheri
  6. Ukabila umechorwa kama sababu ya kuvurugika kwa ndoa. Fafanua.


Sura ya saba

Ni alasiri moja ya joto kali. Mwangeka na Mkewe Apondi wameketi kwenye behewa la nyumba yao. Wameyaelekeza macho yao kwenye kidimbwi ambamo wanao watatu- Sophie, Ridhaa na Umulkheri- wanaogelea. Ukichunguza kwa makini utapata kwamba wawili hawa chochote japo wanatazama. Kila mmoja,  Apondi na Mwanageka, amepotea kwenye ulimwengu wake. Mwangeka anapomtazama Apondi anatabasamu. Kisa cha kukutana kwao kilikuwa kama ifuatavyo: Miaka mitatu ya ujane ilikuwa imemdhihaki Mwangeka. Babake Mwangeka alikuwa akiishi nyumbani kwa Mwangeka kwa muda. Walikuwa wajane wawili waliokomaa. Hitaji la Mwangeka kuwa na mshirika wa kumwondolea ukiwa lilimwandama. Baba mtu alimtaka Mwangeka kuwazia suala hili. Alijua kuwa wakati ndio mwamuzi, ipo siku atakapotokeza hurulaini wake Mwangeka. Ataifungua kufuli kubwa iliyoufunga moyo wake na hiyo itakuwa siku ya kumwaga chozi la heri. Baba mtu akaendelea kungojea kwa matarajio makuu, kila jioni akimchunguza mwanawe kuona kumetokea badiliko lolote.

Siku moja alikutana na Rachael Apondi ambaye alifanya kazi katika Wizara ya Vijana na Masuala ya Kijinsia. Apondi alikuwa na shahada katika masuala ya kijamii. Apondi alikuwa mmoja wa wawasilishaji na ilipowadia zamu yake kuwasilisha aliwasisilisha kwa ustadi wa hali ya juu. Akauteka nyara moyo wa Mwangeka. Apondi alipotoka jukwaani alisindikizwa na makofi ya hadhira yake. Mwangeka akamsindikiza na macho zaidi ya makofi. Moyo wake uliokuwa umejaa barafu ukayeyuka na kutwaa uvuguvugu. Binti huyu alimkumbusha Mwangeka marehemu mke wake Lily. Mwangeka na Apondi walipata kujuana vizuri zaidi wakati wa chamcha. Huu ukawa mwanzo wa usuhuba na uchumba wa mwaka mwaka mmoja ambao kilele chake kilikuwa kufunga ndoa.

Apondi alikuwa mjane wa marehemu Mandu. Mzee Mandu alijifia ughaibuni katika shughuli za kudumisha amani. Kifo chake Mandu kikamwachia Apondi na Sophie mwanawe wa miaka miwili kilio kisichomithilika. Apondi akawa mwoga, akachelea kuhusiana na mwanamume mwingine asije akamwachia ufa wa moyo. Miaka sita baada ya kufiwa ndipo alipokutana na Mwangeka na penzi likazalika, wakapanga kuoana. Alipojifungua mtoto wa kiume alimwita Ridhaa. Ridhaa ni bavyaa yake aliyemkubali katika familia yake licha ya kwamba koo zao ni tofauti. Akawa na furaha tele kwa kuwa Sophie amepata mwenzake naye Baba Ridhaa amepata fidia japo kidogo kwa familia yake iliyoteketea. Mwangeka na Apondi walikuwa wameamua kuwa watoto wao wawili walitosha kukamilisha familia yao. Lakini, ukarimu wao ulifanya kuzaliwa kwa Umulkheri katika familia yao. Baada ya Umu kujiunga na Shule ya Tangamano, mama aliyekuwa akiyasimamia makao ambamo Umu aliishi alishirikiana na mwalimu mkuu wa Tangamano kumtafutia mfadhili. Apondi alikuwa rafiki wa utotoni wa Mwalimu Dhahabu. Alipompigia simu na kumweleza kadhia ya Umu Apondi alikubali kumchukua Umu kama mtoto wake wa kupanga. Baada ya kuwasiliana na Mwangeka, Mwangeka hakuwa na Pingamizi yoyote kuhusu kuwa mlezi wa Umulkheri. Mwange alimwambia mewe kuwa umu ni baraka Mwenyezi Mungu na kuwa Mungu amemfidia mwanaye aliyekufa umu akapata wazazi wapya. Wakawa wanamlipia karo umu mwanzoni alikuwa na shaka lakini baadaye alikuja kuwapenda kwa dhati. Upendo alioupata kwa wazazi hawa wapya uliponya donge chungu lililokuwa moyoni mwake. Akawa sasa yu tayari kumsamehe mamake hapa duniani na ahera. Akawazia pia kumsamehe Sauna. Hata hivyo alibaki kujiuliza maswali mfululizo kuhusiana na walikotokomea ndugu zake.

Maswali

  1. Eleza kwa muhtasari mambo aliyoyazungumzia Apondi katika hotuba yake.
  2. Eleza sifa na umuhimu wa wahusika hawa:
    1. Mwangeka
    2. Apondi
  3. Jadili maudhui ya mapenzi na ndogo kama yanavyojitokeza katika sura hii.
  4. Upendo ni tiba ya moyo ulio na jeraha. Onyesha namna upendo ulivyotekeleza jukumu hilo katika sura hii.
  5. 'ni baraka kutoka kwa mwenyezi Mungu. Mungu amenifidia yule mwanangu aliyekufa "
    1. liweke dondoo hiji katika muktadha wake.
    2. fafanua sifa tatu za mhusika ukionyesha nanna ali baraka kwa msemaji (unaweza kurejelea matukio mengine kwingineko riwayani)
    3. Fafanua umuhimu wa msemaji wa maneno haya.


Sura ya nane

Siku hii Dick alihisi kuwa uwanja wa ndege ulikuwa na baridi na mzizimo kuliko siku nyingine zote. Dick alikuwa akiwaza haya akiwa kasimama katika mlolongo mkubwa wa watu ambao walingoja kuingia kwenye afisi za forodha kukaguliwa. Akawa anakumbuka siku alipoanza kusafiri kwa ndege. Siku hiyo alijawa na kiwewe kwani biashara haramu ya kubeba dawa za kulevya aliyokuwa amejiingiza kwayo ilikuwa imewaingiza wengi kwenye mikono ya polisi, wakatiwa mbaroni. Siku hizo alikuwa mwanagenzi katika uga huu kwani alikuwa na umri wa miaka kumi tu. Zipo siku alipotetemeka karibu ajisaliti lakini hatimaye alizoea kujipa moyo. Sasa miaka kumi ya adha imepita. Alilazimika kukomaa kwa kuwa ulimwengu haukuhitaji mnyonge. Dick alitoswa katika kinamasi cha kuuza dawa za kulevya na Sauna- kijakazi wao. Dick amesafirisha maelfu kwa maelfu ya vifurushi vya dawa hizi. Mwanzoni akawa si mraibu wa dawa hizi lakini ilibidi ajizoeshe kwa usalama wake mwenyewe, kwani mara nyingi alilazimika kuzimeza dawa zenyewe ili kwenda kuzitapika kwenye masoko ya ughaibuni. Jambo hili lilichangiwa na uwepo wa mashine zenye uwezo mkubwa wa kung'amua shehena za dawa zilizofichwa kwenye chupi.

Siku ile baada ya kijakazi Sauna kumwiba Dick alimpelekea baba mmoja tajiri ambaye alijitia kumpeleka shuleni. Kumbe alikuwa amempeleka katika biashara ya kuuza dawa za kulevya. Buda ( lakabu ya tajiri wake Dick) alipoona Dick akitaka kukataa kushiriki biashara hii, alimtishia Dick kuwa angetupwa nje, asingiziwe wizi na bila shaka Dick alijua malipo ya wezi ni kutiwa tairi na kuchomwa moto. Wazo la kupata adhabu ya aina hii lilimtetemesha Dick. Akambuka rafiki yake Lemi alivyofishwa kwa njia hii. Kisa cha Lemi kilimfanya kuunasihi moyo wake kuingilia biashara hii haramu ili mwenye nguvu asije akamtumbukiza kaburini. Akajisemea kuwa huenda siku moja akapata mbinu ya kujinasua. Sababu nyingine iliyomfanya Dick kuingilia biashara hii ni kuwa alihitaji chakula na mahitaji mengine. Akasema potelea mbali kwa lisilo budi hutendwa. Alipojitosa katika biashara hii haramu aliingilia kwa hamasa za ujana. Miaka mitano ya kwanza ikawa imejaa hekaheka kwani alisafiri kwingi na kuona mengi. Akaweza kuchuma pato si haba, pato aliloliona ni halali yake baada ya ulimwengu kumpoka maisha yake.

Hata hivyo asubuhi moja aliamka baada ya kuamua kuwa hakuumbiwa uhalifu, dhamiri yake ikamsumbua na moyo wake kumsuta. Mawazo mengi yakawa yamempitikia akilini na yakamsukuma kuufikia uamuzi wa mkataa, akajinasua kutoka kucha za mwajiri wake huyu. Akaacha biashara ile haramu na kuanzisha biashara ya kuuza vifaa vya umeme. Leo hii amejiajiri. Ashaamua kuufungua ukurasa mpya katika maisha yake. Amekwisha kuhitimu masomo katika Chuo cha ufundi ambako alijifunza teknolojia ya mawasiliano ya simu. Sasa amepanua mawanda yake ya kibiashara. Anauza vifaa vya simu. Husafiri ng'ambo mara kwa mara kununua bidhaa ili kuyauzia mashirika yanayotoa huduma za mawasiliano. Asubuhi hii Dick na kijana mwenzake (mwajiriwa wake) walikuwa katika safari ya kawaida. Alinuiwa kuabiri ndege ya saa moja asubuhi kuelekea ughaibuni ambako alizoea kununua mali yake. Huku akingoja afisi kufunguliwa, mawazo ya nyuma yaliivamia akili yake na akayakunjua maisha yake ya siku za Mlima wa Simba. Akamwazia mama yake kwa masikitiko makuu. Akashanga jinsi ulimwengu unavyoweza kummeza mwanadamu akawacha kuwaazia hata wana wake. Akamkumbuka babake katika dakika ya mwisho ya uhai wake. Maneno yake yalikuwa " wanadamu ni hasidi" ndio waliomsababishia uwele alionao. Dick akiishi, atawaona. Akili yake ikamtuma kumkumbuka Umulkheri- dadake. Anakumbuka alivyomwambia kuwa asijali kwani yeye angewakimu kwa viganja vyake na hawangepungukiwa na chochote. Akawa na maswali chungu nzima kuhusiana na aliko Umu. Wakati Dick alikuwa akiwaza kuhusu familia yake, hakujua kuwa Umulkheri alikuwa nyuma yake kapiga foleni. Anasafiri ng'ambo kwa shahada yake ya uhandisi katika masuala ya kilimo.

Umu, baada ya kuchukuliwa na Mwangeka na Apondi alifanya bidii masomoni na kufuzu vyema katika mitihani yake. Kisadfa, safari ya Umu imekuwa siku hii ambapo Dick anasafiri. Dick aliposikia Mwangeka akimwita Umu na kumtaarifu kuwa ndege i karibu kuondoka, hakuamini. Mazungumzo baina ya Umu na wazazi wake yalimwamsha Dick kutoka lepe lake la muda. Aligeuka na kutazamana ana kwa ana na Umu. Mwanzoni Umu akidhani macho yanamdanganya. Mikono yake ikamwachilia dadake Sophie, moyo wake ukamwenda mbio. Ghafla Dick, alimwita dadake Umu na kumkimbilia. Wakakumbatiana. Wasafiri wote na aila yote ikawatazama kwa mshangao. Machozi yakawadondoka wote wawili na kulia kimyakimya huku wakiambiana kimoyomoyo yote yaliyowakumba. Hatimaye sauti iliita ikitangaza kuwa abiria wa ndege Tumaini waanze kuingia. Walijua kuwa jaala ilikuwa imewakutanisha na hawatawahi kutengana tena.

Maswali

  1. Elezea kwa kifupi namna dawa za kulevya husafirishwa kutoka eneo moja hadi lingine kwa mujibu wa sura hii.
  2. Fafanua sifa za Dick kisha uelezee umuhimu wake.
  3. Dawa za kulevya zina madhara chungu nzima. Tetea kauli hii.
  4. Elezea kwa muhtasari namna Lemi alivyofishwa.
  5. Ni mambo gani yalimsukuma Dick kujiingiza katika biashara haramu ya kuuza dawa za kulevya?
  6. Elezea sadfa ilivyotumika katika sura hii.


Sura ya tisa

Sura hii inaanza kwa Wimbo wake Shamsi. Leo Shamsi anasikika kama amebadilisha wimbo wake kama anawosema Ridhaa japo kwa sauti ya chini. Wimbo huu wa leo unasikika kama wa kiumbe mwenye maumivu zaidi na mapigo yake hasa ni ya mbolezi. Huu wa leo ni tofauti na majigambo yake ya kila siku. Ridhaa alianza kuyaghani majigambo yake Shamsi kwa sauti ya chini kama anayeyatia maneno ya majigambo kwenye mizani. Ridha anamtazama Shamsi akipita kama afanyavyo kila siku. Mtaa anakoishi Shamsi si mbali na hapa, Shamsi na Ridhaa ni majirani. Huu ni mwezi wa tatu tangu Ridhaa kuhamia mtaa wa Ahueni. Ahueni ni mtaa wa raia wenye kima cha juu kiuchumi. Mtaa huu una sura ya mijengo ya kifahari ya ghorofa. Daraja kubwa limeutenga mtaa huu na mtaa wa Kazikeni inakoishi familia ya Shamsi na nyingine za aina yake. Huko maisha ni ya kubahatisha. Huu ni mtaa wamabanda yaliyojengwa kwa udongo na mabati. Mwangeka aliamua kuhamia mtaa wa Ahueni baada ya mjukuu wake wa mwisho kuzaliwa. Aliona ulikuwa wakati wake kuanza kuyajenga maisha yake upya. Maisha ya Mwangeka sasa yalitengenea. Baada ya kuzungumza na mwanawe, Ridhaa alimwomba Mwangeka amruhusu aondoke ili akaanze kuyazoea maisha ya ujane. Aliondoka akiwa na azimio la kukamilisha kukijenga kituo cha afya cha Mwanzo Mpya alichokijenga kwenye ganjo lake. Kituo hicho kingewafaa raia wengi ambao hawangemudu gharama ya matibabu katika hospitali za kibinafsi.

Selume alifanya kazi katika kituo cha afya cha Mwanzo Mpya. Hali katika kituo hiki ni bora kuliko ilivyokuwa katika hospitali ya umma. Huko alikuwa amechoka kutokana na kuwatazama wagonjwa wakifa kwa kukosa huduma za kimsingi huku shehena za dawa zilizotengewa hospitali hii zikiishia kwenye maduka ya dawa ya wasimamizi wa hospitali. Alikuwa amechoshwa na mambo mengi. Katika kituo hiki kipya Selume aliajiriwa kama Muuguzi Mkuu naye Kaizari kama Afisa wa Matibabu. Sasa huu ni mwaka wa tatu tangu kuanza kazi hapa chini ya usimamizi wa Ridhaa ambaye ndiye mkurugenzi. Anawahudumia wagonjwa walio na matatizo aina aina. Kuna mgonjwa mmoja aliuguza majeraha katika mgogoro wa ardhi katika eneo la Tamuchungu. Mwingine aliyejifia ni kijana anayesomea shahada ya uzamili, alikuwa mwathiriwa wa pombe haramu. Mgonjwa mwingine wa kike kwa Jina Tuama alikuwa amejipata katika hali mbaya kwa kukubali kupashwa tohara. Alibahatika kwa kuwa hakuiaga dunia kama wenzake. Tuama anaitetea mila hii ya upashaji tohara kwa wanawake eti haijapitwa na wakati kwani bila tohara mwanamke hubakia kuwa mtoto. Anaendelea kusema kuwa kupashwa tohara hakumaanishi kuacha shule kwani dadake Hazina alipashwa tohara lakini sasa amehitimu shahada kutoka chuo kikuu. Yeye anasema la msingi ni kuwa hakika katika ulengaji shabaha kwenye malengo yako. Mgonjwa mwingine kwa jina Pete aliendelea kupata ahueni. Yeye aliokolewa akitaka kujiangamiza pamoja na kitoto chake. Pete alizaliwa katika kijiji cha Tokasa. Yeye ndiye mtoto wa nne katika familia yenye watoto sita. Alipoutambua ulimwengu tu, alijipata kwa nyanyake mzaa mama. Sababu yake kujipata katika hali hii ni ule mtafaruku uliokuwa umetokea baina ya mamake na babake Pete kisa na maana, Pete hakuwa na mshabaha hata chembe na babake. Mama yake Pete kwa kuchelea kuiharibu ndoa yake akampagaza nyanya mzigo wa malezi. Pete hajadiriki kuonja tamu ya kupendwa na wazazi wake. Alipoanza kupata hedhi maisha yalichukua mkondo mwingine. Alipoingia darasa la saba alipashwa tohara nao wajombake wakapokea posa na baadaye mahari kutoka kwa buda mmoja kwa jina Fungo aliyemuoa kama bibi wa nne. Alipojifungua, akaamua kwa mzee Fungo hakumweki tena. Akaondoka bila kuangalia nyuma. Akaingia jijini kuzumbua riziki. Akapata ajira ya kijishahara duni ambacho hakikutosha kugharamia mahitaji yake yote. Maisha yakazidi kuwa magumu hadi akamzaa mwana wa pili. Kitoto alichonacho zahanatini ni cha tatu na alikipata akiwa katika shughuli za uuzaji pombe. Mambo yalipombainikia kuwa ana watoto watatu kabla ya kufikisha umri wa miaka ishirini na moja, aliona ni heri ajiangamize. Alimwambia jirani yake amchungie watoto kisha akaacha kikaratasi chenye anwani ya bibi yake kwenye kimeza katika chumba chake na kuondoka. Alijiambia kuwa dawa ya panya haingeshindwa kumuua yeye pamoja na kilichomo tumboni na ndipo akamimina kopo la dawa hiyo kinywani. Sasa anapata ahueni katika kituo hiki cha afya.

Kijakazi Sauna anatamani kurudi kitandani alale lakini inambidi amtayarishie Bi. Kangara kiamshakinywa kwani ana miadi ya mapema na mzalendo mmoja jijini. Anapojngia jikoni na kuanza shughuli zake moyo unaanza kumwenda mbio na vipapasio vya akili kusimama wima. Kwa mbali anaskia mbisho hafifu langoni mwa jumba hili. Anapotoka kwenda kuitikia mbisho huu anakumbana ana kwa ana na polisi. Hii ni wiki ya pili tangu Sauna kuwatorosha Dick na Mwaliko. Dick ni mali ya Mzee Buda naye Mwaliko amepelekewa Bi. Kangara awe na mwili kidogo kisha atafutiwe la kufanya. Sauna ashapata ujira wake na yu tayari kuondoka asubuhi ya kuamkia Krismasi. Sauna alipachikwa mimba na babake mlezi. Mamake mzazi alimsaidia kuavya kisha akamwonya dhidi ya kumwambia yeyote kuhusu unyama wa babake. Mamake hakumtaka Sauna kumpaka tope babake. Maneno yale yalimtonesha Sauna kidonda. Mamake alikuwa mjane wa Mzee Kero. Baada ya tendo hili, Sauna aliondoka nyumbani kwani hapakumweka tena. Amewahi kufanya kwenye machimbo ya mawe, amehudumu katika majumba ya kuuza pombe kwa namna zote amefanya mengi. Bi. Kangara ndiye aliyemfunza Sauna mbinu hii mpya ya kuwateka nyara watoto wa waajiri wake na kuwauza. Sasa hii ndiyo siku ya arubaini. Wawili hawa walitiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la kukiuka haki za watoto, wakafungwa miaka saba gerezani na kazi ngumu. Polisi walimchukua Mwaliko katika kituo kimoja cha watoto mayatima ambako aliendelea na masomo yeye na wenzake.

Maswali

  1. Ni ujumbe gani umetamalaki katika wimbo wa Shamsi?
  2. kwa muhtasari ujumbe uliomo katika majigambo aliyoyaghani Ridha. '
  3. Jadili maudhui ya utabaka kama yanajitokeza katika sura hii,
  4. Ni kwa nini Selume aliifurahia hali katika kituo cha afra cha Mwanzo Mpya kinyume na hapo awali a!ipokuwa akifanya katika hospitali ya umma? Elezea.
  5. Pombe haramu ina mathara chungu nzima. Tetea kauli hii kwa mujibu wa sura hii.
  6. Eleza sifa za wahusika hawa:
    1. Selume
    2. Meko
    3. Kipanga
  7. Kupashwa tohara kwa jinsia ya kike kuna hasara nyingi kuliko faida. Tetea kauli hii.
  8. Jadili maudhui ya malezi kama yanavyojitokeza katika sura
  9. Eleza kwa muhtasari masaibu aliyoyapitia Sauna akabadilika kuwa mvunja sheria.


Sura ya kumi

Sura inapoanaza, Mwangemi anamrai Neema asiwe na mawazo finyu kuhusu kupanga mtoto. Anasisitiza kuwa hakuna udhaifu wowote katika kumpanga mtoto. Wamejaribu kupata mtoto kwa muda wa miaka mitano bila mafanikio. Neema amewahi kutunga mimba si mara moja au mbili, amefanikiwa kuilea mimba hadi ikakomaa wakaweza kukipakata kilaika mikononi mwao. Kitoto hicho kiliaga kabla ya juma moja. Mwangemi na Neema walihuzunika kumpoteza mwana. Sio eti Neema hataki kumlea mwana, la hasha, anatamani kukipakata kilaika kiwe chake au cha mwingine. Ni dhamiri yake ambayo humsuta sana akikumbuka nafasi aliyoipoteza aliyopewa na Mungu wakati mmoja ya kumpanga mtoto. Mwangemi alimsihi Neema mke wake asijisulubu kwa kosa ambalo alilitenda kwa kutokuwa na ufahamu bora wa malimwengu. Hayo yamepita. Baada ya Neema kukubali rai ya Mwangemi walienda katika kituo cha watoto cha Benefactor na leo hii wamo afisini. Walikaribishwa na Mtawa Annastacia aliyewataarifu kuwa alilipata ombi lao la kutaka kupanga mtoto kutoka kituo chao. Wakaelezwa kuwa kuna kijana mmoja wa kiume na iwapo wangefaulu katika mahojiano kituo hicho kingewakabidhi mtoto huyo. Mahojiano yalipokamilika Mwangemi na Neema wakaondoka wakitarajia kurudi kumchukua mwanao. Waliporudi afisini mwa Annastacia wana furaha mzomzo kwani walifaulu katika mahojiano na wako tayari kumchukua mwana wao. Mwangemi anahisi kuwa familia yake imekamilika. Kijana huyu alipoletwa Mwangemi alimtulizia macho, kijana huyu ni mrefu na mwembamba, mwenye sura jamali.

Macho yao yalipokutana kijana alitabasamu na kudhihirisha meno meupe pepepe ambayo yalimkumbusha binamu yake Mwangeka. Hapohapo nyoyo zao zikaungana kila mmoja akijisemea kimyakimya, "Haikosi huyu atakuwa rafiki wa dhati " Mwaliko alitambulishwa kwa wazazi wake wapya. Kisha Mtawa Annastacia akamwahidi kuwa atakuwa akienda kumwangalia mara kwa mara. Mwaliko akamtazama Neema kwa hofu iliyojaa mapenzi. Badaye akamkumbatia Neema na kumwambia kuwa atakwenda naye. Chozi la furaha lilimdondoka Neema, akamkumbatia Mwaliko kwa mapenzi ya mama mzazi. Akahisi kama aliyezaliwa upya. Sasa amepata kizazi. Hatachekwa tena na walimwengu eti anazaa watoto wenye upungufu kwa sababu aliavya mimba nyingi akiwa shuleni. Akasema hata kama kitoto hiki si chake kitampa mshawasha wa kufanya kazi zaidi ili kukikimu. Mwaliko alilelewa na Mwangemi na Neema kwa tunu, tamasha na nidhamu. Akainukia kuwa ghulamu mwenye nidhamu ya hali ya juu, akiwaheshimu wazazi na majirani na akiwatii walimu wake. Alipohitimu kidato cha nne alijiunga na Chuo kikuu kusomea shahada ya Isimu na lugha, wazazi wake wakajua kuwa juhudi zao za malezi hazikuambulia patupu. Walikuwa wamechangia katika kumpa tegemeo mwana wa mwenzao. Miaka mitatu imepita sasa tangu Mwaliko kukamilisha masomo yake ya chuo kikuu. Amejisajili kwa shahada ya uzamili katika taaluma ya mawasiliano na kuhitimu. Ameajiriwa na kampuni ya gazeti Tabora kama mhariri katika kitengo cha biashara. Anafanya kazi yake kwa bidii ya mchwa.

Mwaliko alitamani siku ambayo angekutana na ndugu zake, moyoni alihisi kuwa walikuwa hai. Mama Neema aliishi kumkumbusha kuwa siku moja atawaona ndugu zake. Siku moja Mwaliko na baba yake waliamua kwenda kujivinjari. Ilikuwa siku ya kuzaliwa kwa Mwangemi. Mwaliko akaamua kumnunulia babake chamcha. Walienda katika hoteli ya Majaliwa saa sita unusu adhuhuri. Mwaliko alikuwa akiwaza kuhusu waliko ndugu zake lakini hatimaye akamtakia babake siku njema ya kuzaiiwa kwake. Kisadfa familia ya kina Umulkheri walikuwa katika hoteli ii hii wakisherehekea siku ya kuzaiiwa kwake Umu. Umu akawa anawashukuru wazazi wake kwa hisani yao. Dick vilevile akawa anatoa shukrani kwa Mwangeka na Apondi. Mwangemi aliwapata kina Mwangeka wakiwa katika hali ya kutafakari kuhusu hotuba ya Dick. Mwangemi ni binamu yake Mwangeka. Mwangeka alishangaa ni sadfa gani iliyomleta Mwangemi katika maeneo haya. Akamtaarifu ami yake kuwa huwa haji humu ila mwanawe Mwaliko aling'ang'ania kumleta hapa kwa chakula cha mchana. Kisadfa siku hil ilikuwa siku ya kuzaliwa kwa Umu na Mwangemi. Dick na Umu hawakusikia alichokuwa akisema Mwangemi, walimaka kusikia Mwangemi akitaja jina la Mwaliko. Walishangaa iwapo ni sadfa nyingine kuwa Mwangemi ana mtoto mwenye jina kama la ndugu yao mnuna. Walijiuliza maswali chungu " Mwangemi alimwita Mwaliko aje ili amjuze kwa binamu yake Vuuk (lakabu ya Mwangeka). Alipokuja, Umu alimtazama ghulamu huyu kwa tuo akamtambua kuwa ni nduguye Mwaliko. Dick vile alikuwa keshamtambua nduguye. Mwangemi alimkumbusha Mwaliko kile kisa ambacho alimsimulia kila mara kuhusu yeye na Vuuk baada ya kumtambulisha kwa Mwangeka. Mwangeka alicheka kicheko kikubwa na katika kipindi kidogo akayaleta maisha ya kisogoni mbele ya kipaji chake. Wakahadithiana matukio ya utotoni waliyoyafanya pamoja vikiwemo vita vya majogoo nk. Mwangeka akawa amezama katika kisa chake na babu.

Mwangemi aliendelea kumtania Mwangeka kuwa ndiye mhandisi mwenyewe. Yeye ndiye aliyevumbua gari la kwanza la Kiafrika. Mwangemi alipoona amemtonesha kidonda mwenzake na kumbukumbu zake, akatabasamu. Aliendelea kusema na kumjuza kuwa hayo yote yamepita na hiyo ilikuwa ni hatua ya ukuaji, ilibidi waipitie. Alimgeukia Mwaliko na kumtambulisha kwa Mwangeka. Akamweleza kuwa si mwana tu bali ni rafiki yake wa dhati. Maisha yake Mwangemi na Neema yangekuwa tupu bila yeye. Mwangeka na Apondi walipomtazama Mwaliko waliuona mshabaha kati ya Umu, Dick na Mwaliko. Yote yamewabainikia na sasa wanangoja kuhakikishiwa na Umu kuwa huyu ndiye ndugu yao ambaye mamekuwa wakimtafuta msitu na nyika. Moyo wa Mwaliko tayari umemwambia kuwa hawa ni ndugu zake kwa kuwa wameshabihiana na wale watoto walio kwenye picha ambayo baba yao Lunga alipigwa nao kabla ya mauko yake. Picha hii mwaliko ameihifadhi katika buku lake kama kumbukukumbu ya familia yake. Kijakazi Sauna alikuwa amezoea kumwambia kuwa hao ni Umu na Dick. Mwaliko aliinua macho yake na kuwaita Umu na Dick na kuwaambia kuwa ni yeye na kuwa yu hai. Umu na Dick hakumngojea Mwaliko kumaliza. Walimkimbilia wote na kumkumbatia ndugu yao, wakaanza kulia huku wakiliwazana. Sophie na Ridhaa nao walijiunga nao, wote wakakumbatiana na kulizana, wakashikana mikono na kufanya mduara kama ule ufanywao na watoto wakicheza. Ikawa wanaunga udugu upya. Wazazi wakabaki kutazama bila kusema lolote. Umu akawaomba wote kuketi chini, yeye akaketi baina ya wazazi wake wawili kama alivyopenda kufanya kila mara. Akasimulia kwa furaha alivyokuwa akihisi huku akimshukuru Mwangemi kwa kumlea Mwaliko hadi akawa mwana wa kutegemewa. Dick naye hakuchelewa kumshukuru Umu kwa tumaini alilompa kuwa siku moja atamwona ndugu yao. Alimshukuru pia kwa ukarimu wake. Mwaliko naye akasema kuwa kuja kwao pale kulikuwa kwa heri kwani familia yao imepanuka. Tayari amekutana na mabinamu ambao aliskia tu wakitajwa. Tena ikawa heri kwa kuwa mjomba Mwangeka ndiye mzazi na mlezi wa nduguze. Mwangemi akawa anamtazama mwanawe kwa imani na furaha kubwa.

Sasa watajenga uhusiano wao upya na kumtafuta mama yao na kumsamehe. Mwangeka alisema kuwa Naomi(mama yao kina Umu) ana haki ya kujua walipo wanawe. Jambo ambalo Mwangeka hakujua ni kuwa Naomi baada ya kurudi kwao, hakuishi na wazazi wake. Alihamia mjini na kuwa shangingi kwelikweli. Alikumbana na Bwana Kimbaumbau aliyemweka Naomi kimada kwa muda. Bwana huyu alimpitisha Naomi makuruhu yasiyomithilika, kusimangwa, kupigwa na kuadhibiwa. Naomi akawa anajuta sana. Alijuta kumwacha Lunga(mume wake) wakati ambapo alimhitaji zaidi. Sasa hana uso wa kuwatazama wanao. Siku aliyopigwa pute na Kimbaumbau, uchungu wa uzazi ulimtuma kuwatafuta wanawe. Akaenda hadi Mlima wa Simba na kufululiza hadi nyumbani ambapo hapakuwa na mtu, palikuwa mahame. Alifyeka magugu katika kaburi Ia mume wake na kunadhifisha kiambo kisha akaweka koja la maua juu ya kaburi. Kwa kweli amekuwa akiwatafuta wanawe. Hamna kituo Cha polisi ambacho hakubisha hodi. Juhudi hizi hazikuzaa matunda. Kwa sasa hana lolote la kujivunia ila ameanza kuyajenga maisha yake upya. Amefungua kiafisi kidogo karibu na Chuo Kikuu cha Mbalamwezi anakowapigia wasomi kazi zao chapa na kuisarifu miswada yao. Dick alisema kuwa mamake ana haki ya kusamehewa kwani hakuna binadamu aliyemkamilifu. Watashirikiana kumtafuta mama yao. Mwaliko alimwambia baba yake muda wa kufanya hayo upo lakini kwa sasa, la muhimu ni kuwa ndugu zake wako hai. Sasa ni wakati wa kuondoka kuelekea nyumbani kwani ana hamu ya ya kumwambia Young Neema majaliwa yao ya leo.

Maswali

  1. Ndoa bila watoto si kamilifu. Fafanua kwa kurejelea sura hii.
  2. Fafanua ufaafu wa nwani chozi la heri ukirejelea matukio katika sura hii.
  3. Eleza sifa nne za wahusika hawa:
    1. Mwangemi
    2. Neema
    3. Mwaliko
    4. Dick
    5. Umu
    6. Apondi
    7. Mwangeka
  4. Mwiba wa kujidunga hauna kilio. Kwa kumrejelea Naomi, onyesha ukweli wa methai hii.
  5. Onyesha sadfa ilivyojitokeza katika sura hii.  
Join our whatsapp group for latest updates

Download Muhtasari - Mwongozo wa Chozi la Heri.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest