KCSE 2014 Kiswahili Paper 1 Questions with Marking Scheme

Share via Whatsapp

MASWALI

Maagizo

 1. Andika insha mbili, Insha ya kwanza ni ya lazima
 2. Kisha chagua insha nyingine moja kati ya hizo tatu zilizobakia.
 3. Kila insha isipungue maneno 400.
 4. Kila insha ina alama 20.
 5. Kila insha lazima iandikwe kwa lugha ya Kiswahili. 
 1.  Lazima
  Andika hotuba utakayowatolea wazazi, walimu na wanafunzi kuhusu umuhimu wa ushauri - nasaha katika shule za sekondari.
 2.  Andika insha kuhusu jinsi raia wanavyoendeleza matumizi mabaya ya ardhi.
 3. Andika kisa kitakachodhihirisha maana ya methali: Achanikaye kwenye mpini hafi njaa.
 4. Tunga kisa kinachoanza kwa maneno yafuatayo:
  Mara tu nilipokivuka kizingiti cha lango la nyumba yangu, nilijua kwamba maisha yangu yalikuwa yanachukua mkondo mpya ...

MWONGOZO WA KUSAHISHA

 1. Hii ni hotuba. Vipengele viwili vikuu vya utungo wa aina hii; Maudhui na muundo vizingatiwe.
  1. Muundo
   Vipengele vifuatavyo vya kimuundo vijitokeze:
   1. Utangulizi ambapo mtahiniwa atataja waliohudhuria kwa vyeo kulingana na hadhi. Pia kiini cha hotuba kishughulikiwe hapa.
   2. Mwili - yaliyomo yajadiliwe na yatolewe ufafanuzi.
   3. Hitimisho - ionyeshe msimamo wa hatibu kuhusiana na suala la ushauri - nasaha. Aidha, atoe shukrani kwa hadhira yake na kuiaga.
  2. Maudhui
   Mtahiniwa afafanue hoja zinazoonyesha haja ya kuwepo na ushauri - nasaha shuleni. Baadhi ni:
   1. Huwasaidia wanafunzi kukabiliana na changamoto za kuzoea mazingira ya shuleni hasa endapo mazingira yale ni mageni. Hawa huelekezwa kuhusu namna ya kukubali na kufuata sheria za shule ili wasijihisi kuwa wananyanyaswa
   2. Kushindwa kufikia shabaha alizojiwekea au alizowekewa huwafanya baadhi kuvunjika moyo na kukata tamaa, kabla hawajakata tamaa na kufanya uamuzi usiofaa, wanafunzi hawa wanahitaji msaada wa ushauri - nasaha.
   3. Wanafunzi kama wanajamii wengine, huweza kutatizika kihisia na kifikira, na wakati mwingine huchoshwa na maisha. Ni muhimu huwapa huduma za ushauri nasaha ili kuwaandaa kujidhibiti, na kukabiliana na hali hizi.
   4. Wanafunzi wengi, hasa wanaobaleghe hukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya mwili katika kukua kwao. Wengine huingiwa wa wasiwasi kufedheheka, au kuhuzunika kutokana na hali hizi. Huduma za ushauri
    nasaha zitawasaidia sana kukabiliana na hali hizi kwa njia chanya.
   5. Huwasaidia wanafunzi kukabiliana na shinikizo la marika, na shinikizo kutoka kwa wazazi na wanajamii wengine.
   6. Wanafunzi waliotatizika kiakili na ambao hawawezi wakatatua migogoro inayowakabili kwa njia salama na chanya huwa na ushawishi mkubwa kwa wengine na wasiposaidiwa kwa ushauri nasaha, wanaweza kuwapotosha
    wengine.
   7. Huwaelekeza vijana kuhusu namna ya kufaidika kwa njia za kisasa za mawasiliano bila kupotoshwa na tamaduni za kigeni zinazoandamana nazo.
   8. Ushauri nasaha huisaidia shule kudumisha nidhamu miongoni mwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi.
   9. Wanafunzi huhitaji kuelekezwa kuhusu namna ya kuuratibu muda wao shuleni.
   10. Ushauri nasaha huwasaidia wazazi kukabiliana na adha za malezi. Mzazi aliye na matatizo ya kuhusiana vyema na mwanawe anaweza kushauriwa kuhusu jinsi ya kumwelewa mwanawe.
   11. Huelekeza wanafunzi kuhusu taaluma au kozi wanazoweza kuchagua baada ya kuhitimu masomo yao.
   12. Humwelekeza mwalimu kuhusu namna ya kuhusiana na wanafunzi.
   13. Ni njia ya kuwasaidia walimu na wanafunzi kukabiliana na majanga kama vile vifo, magonjwa hatari, na kufutwa kazi.
   14. Ushauri nasaha, hasa ushauri marika, huwasaidia wafunzi ambao wanawiwa vigumu kuwatolea wazazi au walezi undani wao, kuwaambia wanafunzi wenzao hivyo kusaidiwa.
  3. Tanbihi
   1. Katika utangulizi, mtahiniwa lazima aonyeshe uelewa wa hadhira, awataje kwa mfuatano ufaao kulingana na vyeo.
   2. Muktadha wa hotuba unaweza kuwa:
    1. siku ya kuwatuza wanafunzi bora shuleni,
    2. siku maalum ya kuwaaga wanafunzi wa kidato cha nne,
    3. siku ya kuwaelimisha wazazi na jamii nzima ya shule kuhusu umuhimu wa ushauri - nasaha; pengine ili kamati ya wazazi iidhinishe kuajiriwa wa afisa wa utuoji nasaha.
   3. Mtahiniwa anaweza kutoa hotuba kuhusu jinsi alivyofaidika kwa ushauri nasaha katika kipindi cha miaka minne aliyokuwa shuleni, bora tu yasiwe masimulizi bali mazungumzo ya moja kwa moja kwa hadhira lengwa.
   4. Anaweza pia kutoa hotuba, pengine kukashifu mielekeo hasi ya wazazi na wanafunzi kuhusu udumishaji wa nidhamu, akaonyesha kwamba tabia ya binadamu huimarishwa zaidi kupitia ushauri - nasaha kuliko matumizi ya nguvu au adhabu kali.
   5. Katika kutathmini, kumbuka kwamba mwanafunzi anaweza kutumia maswali ya balagha ili kuchochea hisia fulani, au kukashifu mwelekeo fulani. Huu unaweza kuhesabiwa kama upekee unaomtofautisha mtahiniwa na wengine wa kiwango cha chini.
   6. Mtindo wa uwasilishaji wa hotuba uzingatiwe. Hatibu azungumze moja kwa moja na hadhira yake. Asitumie mtindo wa masimulizi ila pale tu, pengine anapotoa kisa kifupi kama kielelezo cha mtu aliyefaidika kwa ushauri-nasaha, au mzazi aliyehasirika kwa kutotumia ushauri-nasaha katika malezi.
 2. Hii ni insha ya maoni. Inaweza pia kuwa insha ya maelezo. Vipengele vikuu vya insha ya aina hii: Muundo, maudhui vizingatiwe:
  1. Muundo
   Vipengele vifuatavyo vizingatiwe:
   1. Utangulizi - uangazie hali ya matumizi ya ardhi nchini.
   2. Mwili
    Hapa ndipo yaliyomo / maudhui yanapojadiliwa. Mtahiniwa:
    1. Ajadili hoja ambazo zinadhihirisha namna ambavyo rasilimali za nchi (zinazohusiana na ardhi) zinavyotumiwa vibaya huku akionyesha athari mbaya za hulka hizi.
    2. Aonyeshe mchango wa raia katika uharibifu wa mazingira au matumizi mabaya ya ardhi.
   3. Hitimisho
    Mtahiniwa:
    1. Ajumuishe hoja alizojadili na kuonyesha mwelekeo, msimamo au falsafa yake kuhusiana na matumizi ya ardhi.
    2. Anaweza kutoa wito kwa raia kuepuka mazoea ya kutumia ardhi vibaya.
    3. Anaweza pia kupendekeza njia bora za kutumia ardhi kwa njia endelevu.
  2. Maudhui
   Baadhi ya hoja ni:
   1. kulima kandokando ya mito, hivyo kusababisha mmomonyoko wa udongo
   2. kupanda zao hilo hilo, hivyo kupujua (kudhoofisha) uwezo wa udongo kuzalisha mazao bora
   3. ardhi ambayo imetengewa kilimo kutumiwa kwa ujenzi, hivyo kusababisha kutojitosheleza kwa chakula
   4. kufuga mifugo wengi ambao wanaishia kufa wakati wa ukame, au kusababisha mmomonyoko wa udongo
   5. kutotumia sehemu zenye vinamasi kwa njia endelevu, badala yake wanajenga huko na kusababisha hata kuporomoka kwa majengo
   6. kunyakua ardhi na kutenga katika sehemu zilizotengewa matumizi maalum kama vile maziara namadhabahu
   7. wakulima kutumia kemikali ambazo zinaishia kuua wadudu ambao huchangia kuboresha udongo
   8. wenye viwanda kuelekeza taka zenye kemikali kwenye mashamba na mito na kusababisha vifo vya wanyama na kuharibika kwa mimea
   9. kufyeka misitu kwa ajili ya majengo na kasababisha kuenea kwa jangwa au kupalilia ukame
   10. uwindaji wa wanyama ambao unatishia kupunguza aina za wamyama kama vile ndovu na kifaru
   11. kujenga kwenye sehemu zilizotengewa ujenzi wa barabara hivyo kuathiri ustawishaji wa miundomsingi
   12. kujenga majengo mengi kwenye sehemu ndogo ya ardhi, hivyo kusababisha kusongamana kwa watu
   13. Wawindaji haramu kuchimba vidimbwi vya kuwatilia wanyama sumu. Hili linasababisha vifo vya wanyama na kuzagaa ovyo kwa mizogo. Binadamu wanaweza pia kuumia kwa kutumbukia kwenye vidimbwi hivi
   14. binadamu kukata miti kwa ajili ya samani na nishati, kutopanda mingine, na kusababisha kukosekana kwa aina muhimu za miti.
  3. Tanbihi
   Suala la matumizi mabaya ya ardhi liangaziwa katika upana wake. Mtahiniwa asitarajiwe tu kuzungumzia kilimo, anaweza kujadili aina nyingine za matumizi mabaya ya ardhi au mazin gira.
 3. Hii ni insha ya methali.
  Mtahiniwa abuni kisa kinachodhihirisha maana ifuatayo:
  Mtu anayetia bidii katika jambo gumu huja kupata faida, hata kama faida hiyo ni kidogo. Kisa kinaweza kudhihirisha hali zifuatazo:
  1. Mhusika, kama vile mwanafunzi, aliyejikuta katika mazingira magumu (kwa mfano kusoma, licha ya kufukuziwa karo), akajibidiisha, asikate tamaa, na hatimaye akaja kufaidika.
  2. Mhusika anayejaribu kwa hali na mali kubadilisha mitazamo hasi ya wanakijiji, na kuinua hali zao za maisha na baadaye kufanikiwa.
  3. Mhusika aliyepata pingamizi nyingi kazini, akataka kukata tamaa na kujiuzulu, lakini akajiasa au akaaswa na mwingine, akaamua kufanya kazi kwa ustahimilivu, na hatimaye juhudi zake zikatambuliwa, akapandishwa cheo.
  4. Mhusika kijana aliyehitimu chuoni, akatafuta kazi ya ajira asipate. Baadaye apate mtaji wa kuanzishia biashara ndogo (pengine kupitia Hazina ya Uwezo), apate changamoto nyingi mwanzoni, lakini ajikakamue. Hatimaye mradi wake ufanikiwe, aweze hata kubuni nafasi za kazi kwa vijana wenzake.
  5. Mhusika anaweza kuwa mwenye mahitaji maalum yanayomzuia kujiendeleza, kwa mfano, asiwe na mikono, lakini ajibidiishe, asiuone ulemavu kama kikwazo, na mwishowe kufanikiwa.
  6. Mzazi au mlezi anaweza kuwa na mtoto aliyepotoka, ajaribu kumrekebisha na baadaye mtoto huyu abadilike na hata kumfaa mzazi au jamii pana.
   Tanbihi
   1. Kwa vyovyote vile, lazima kuchanika (kujibidiisha, kuteseka) kujitokeze. Mhusika aonekane akikabiliana na kizingiti fulani, pengine cha kimaumbile au kinachotokana na mazingira anamoishi.
   2. Katika kuchanika huku, tuone juhudi anazotumia kukabiliana na vikwazo vinavyomkabili.
   3. Hatimaye sharti faida ijitokeze. Hapa tunaweza kuona manufaa ya kazi aliyofanya, au namna alivyojitoa kwenye hali ngumu iliyomkabili.
 4. Hii ni insha ya mdokezo inayomhitaji mtahiniwa kuyasanisi mawazo yake na kubuni hadithi inayoafikiana na mwanzo huu.
  Mdokezo unafumbata hali zifuatazo:
  1. Msimulizi anaondoka katika mazingira aliyozoea (kuvuka kizingiti cha lango).
  2. Msimulizi anaanza safari fulani / anaingia katika hali nyingine (maisha kuchukua mkondo mpya).
  3. Msimulizi ana hakika kuwa mustakabali wa maisha yake umebadilika (nilijua).
   Kisa kinaweza kudhihirisha hali kama vile:
   1. Msimulizi amepita mtihani wa darasa la nane na anaelekea shule ya upili ambamo anatarajia maisha yake kuwa tofauti. Aonyeshe mkondo huo mpya wa maisha yake.
   2. Msimulizi amekuwa mjane au mseja kwa muda, ni siku yake ya arusi, anatarajia maisha mapya ya ndoa.
   3. Msimulizi amehitimu masomo ya kidato cha nne, amepata fursa ya kwenda ng’ambo kwa masomo ya chuo kikuu, anajua kuwa maisha yatakuwa tofauti. Anaweza pia kusimulia maisha yake huko ng’ambo ili kuonyesha mabadiliko haya.
   4. Msimulizi amepata kazi ya ajira anaondoka kwao alikozoea na kutarajia mabadiliko.
   5. Msimulizi, baada ya kauli hii, anaweza kuturudisha nyuma, akatumia mbinu rejeshi kuonyesha hali ya maisha yake hapo awali, pengine amekuwa akiishi kwenye mazingira yenye udhalimu, kisha akafikia uamuzi wa kujinasua kwa kuondoka humu.
   6. Msimulizi anaweza pia, baada ya kauli hii, asiturejeshe nyuma, asimulie kisa chake moja kwa moja. aonyeshe namna alivyokuwa ameingojea siku hii kwa hamu, asimulie kuhusu safari yake, adha, furaha ya safari hii hadi anapofika alikoondoka kwenda.
   7. Msimulizi anaweza kuwa kijana mtoro ambaye anayaona maisha ya kwao nyumbani kuwa ya kudhibitiwa. Aamue kuondoka kwao. Hapa tunatarajia msimulizi asimulie, ama maisha yake ya awali, au aonyeshe namna alivyosafiri, na namna hali haikuwa alivyotarajia pengine hapati uhuru aliotarajia, aadhibiwe kwa utoro wake.
   8. Anaweza pia kuwa mwanariadha mashuhuri anayeondoka kwao kwa kinyang’anyiro, pengine mbio, kisha asimulie kuhusu shindano, na jinsi alivyoimbuka mshindi, akapata pato kubwa na kutoka kwenye hali ya umaskini.
    Tanbihi
    1. Mdokezo unaelekeza kwamba kisa kitasimuliwa kwa nafsi ya kwanza.
    2. Hata hivyo, kwa vile msimulizi huenda akakumbana na wahusika wengine, anaweza pia kuchanganya nafsi ya kwanza na ya pili.
    3. Mazungumzo au dayolojia za wahusika zinaweza kujitokeza kulingana na ukomavu wa lugha ya mtahiniwa.
    4. Si lazima mtahiniwa ataje mkondo mpya moja kwa moja.
    5. Si lazima afafanue mabadiliko kwa mapana na marefu. Mtahini atambue mabadiliko yanayojitokeza kisha amkadirie mtahiniwa kwa mujibu wa mwongozo wa kudumu.
Join our whatsapp group for latest updates

Download KCSE 2014 Kiswahili Paper 1 Questions with Marking Scheme.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest