Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - BSJE Mock Exams 2023

Share via Whatsapp
MAAGIZO:
 • Jibu maswali manne pekee.
 • Swali la kwanza ni la lazima.
 • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani; Riwaya,Ushairi, Hadithi Fupi na Fasihi Simulizi.
 • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
 • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili

                                             SEHEMU A: TAMTHILIA: Bembea ya Maisha - T. Arege (ALAMA 20)

 1. “Siwezi kuendelea kuishi hivi. Sasa nimekata shauri. Pombe! Umenichezesha kama mwanasesere kwa muda mrefu. Umeninyima fursa ya kuielewa familia yangu. Hapana! … Lazima nimshukuru kwa vitendo kwa jinsi alivyojitolea kuijenga familia yetu…kwa heri pombe. Buriani.”
  1. Weka dondoo hili katika muktadha wake.                                                              (alama 4) 
  2. Eleza vipengele vinne vya kimtindo alivyotumia msemaji kufanikisha uwasilishaji wa ujumbe. (alama. 4)
  3. Fafanua changamoto ya asasi ya ndoa kwa kuangazia ndoa zilizo katika tamthilia ya Bembea ya Maisha.  (alama 4)       
  4. "...Wakati mwingine mwindaji huwa mwindwa. Hata kijijini wanaishi watu. Watu hao hawakumbwi na dhiki kiasi hiki. Ya nini kung'ang'ana kuyatafuta maisha kama kwamba hayapiti? Maisha ni mshumaa uso mkesha! Ukijiachia sana peupe hata upepo unaweza kuuzima kabla ya kulika hadi nchani.”
   Eleza umuhimu wa msemaji katika kuendeleza ploti ya tamthilia hii. (alama 8)
                                      
                                                      SEHEMU B: RIWAYA, - A Matei: Chozi la Heri
   Jibu swali la 2 au la 3
 2. Jadili ufaafu wa anwani ya riwaya ya Chozi la Heri (alama 20)
 3. “…huenda tusikutane nikiwa hai ila nawausia kwa kauli moja tu, msiache ubinafsi na tamaa kuupweza ubinadamu wenu.
  1. Weka dondoo hili katika muktadha wake.         (alama 4)
  2. Eleza jinsi ubinafsi na tamaa ulivyopweza ubinadamu wa wahusika kwa mujibu wa riwaya ya Chozi la Heri. (alama 8)                     
  3. Kwa kurejelea Pete na Shamsi, jadili mchango wa wahusika hawa katika kujenga maudhui.  (alama 8)

                                                                       SEHEMU C:  USHAIRI
 4. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
  Timothy Arege – Mwili

  Leo kitaka nifike, natamani, ila wauma mwili
  Kwa kazi nihusike, samahani, unahili kimwili
  Napenda nihesabike. makundini, ila huwezi mwili.

  Vitisho pamwe kelele, ninavicha, kwa nafsi na mwili
  Ila ugonjwa utimile, umechacha, na kuudhili mwili
  Msikose simile, magalacha, si gurudumu mwili.

  Vingekuwepo viraka, kuutia, ngeushuruti mwili
  Kifundi kuvipachika, kuingia, hata kuridhi mwili
  Upya ukaungilika, kuvutia, roho na wake mwili.

  Lakini kamwe haiwi, kuvipata, vipande vyake mwili
  Sihofu kupata mawi, sitajuta, kupigania mwili
  Hata kufutwa sikawi, nitakita, kidete nao mwili

  Kazi ninaithamani, ni hakika, akilini na mwili
  Ila kamwe siamini, kusagika, damu jasho na mwili
  Uwele hususani, kioneka, nguvu hitishi mwili
  Maswali
  1. Fafanua mambo ambayo mtunzi anasisitiza katika shairi hili. (alama 8)
  2. Bainisha  mbinu nne ambazo mtunzi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi katika shairi. (alama 4)
  3. Eleza toni ya shairi. (alama 2)
  4. Tambua nafsi nenewa na nafsi neni katika shairi hili ( alama 2)
  5. Bainisha bahari ya shairi hili kwa kurejelea vipande. (alama 1)
  6. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari. (alama 3
 5. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
  KAMA SODOMA!
  Miji yetu kwa yakini, kidogo kama Sodoma!
  Haihitaji makini, kwa mwenye macho mazima
  Utaona walakini, mradi ukitizama
  Wanazini hadharani, wana kwa watu wazima
  Yafanana na Sodoma, miji yetu kwa yakini.

  Miji yetu kwa yakini, kidogo kama Sodoma!
  Wanazini hadharani, wana kwa watu wazima
  Wanatafuna maini, vijana na kina mama
  Hawana haya nyusoni, wameharamisha wema
  Yafanana na Sodoma, miji yetu kwa yakini.

  Miji yetu kwa yakini, kidogo kama Sodoma!
  Hawana haya nyusoni, wameharamisha wema
  Baba na binti ndani, wanacheza lelemama
  Marijali wa mbioni, kujipagaza umama
  Yafanana na Sodoma, miji yetu kwa yakini.

  Miji yetu kwa yakini, kidogo kama Sodoma!
  Marijali wa mbioni, kujipagaza umama 
  Wameikataa dini, toka tumboni mwa mama
  Wadai wataliani, watajirisha mapema
  Yafanana na sodoma, mji yetu kwa yakini.

  Miji yetu kwa yakini, kidogo kama Sodoma!
  Wadai ufirauni, watajirisha mapema
  Hivyo mambo ya kigeni, yametunukiwa dhima
  Uwaonapo fuoni, nusu uchi wa mnyama
  Yafanana na Sodoma, miji yetu kwa yakini.

  Miji yetu kwa yakini, kidogo kama Sodoma!
  Uwaonapo fuoni, nusu uchi wa mnyama
  Watu hawana imani, umezidi uhasama
  Na viongozi wa dini, kuabudu darahima
  Yafanana na Sodoma, miji yetu kwa yakini.

  Miji yetu kwa yakini, kidogo kama Sodoma!
  Na viongozi wa dini, kuabudu darahima
  Wamekeuka yamini, kati yao na Rahima
  Wamemuasi Manani, na kusahau kiyama
  Yafanana na sodoma, miji yetu kwa yakini.

  Miji yetu kwa yakini, kidogo kama Sodoma!
  Wamemuasi manani, na kusahau kiyama
  Ya Illahi tuauni, tuwe watu maamuma
  Tukue katika dini, siku zetu za uzima
  Yafanana na Sodoma, miji yetu kwa yakini.
  Maswali  
  1. Bainisha bahari ya shairi hili ukijikita katika ruwaza zifuatazo  (alama 3)
   1. Mishororo
   2. Maneno
   3. Vina
  2. Eleza muundo wa shairi hili  (alama 4)
  3. Bainisha mbinu zifuatazo za kimtindo  katika shairi hili (alama3)
   1. Tashbihi
   2. Taswira
   3. Tasfida 
  4. Eleza toni ya shairi hili  (alama1)
  5. Bainisha nafsi nenewa katika shairi hili    (alama 1) 
  6. Fafanua dhamira ya mtunzi wa shairi hili  (alama 2)
  7. Fafanua ujumbe wa shairi hili   (alama 4)
  8. Fafanua maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa na mshairi (alama 2) 
   1. Manani 
   2. Marijali   

    SEHEMU YA D: Hadithi Fupi – Mapambazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine – Dw Lutomia
 6. “Poko! Ukiumwa na nyuki haina haja ya kujitwika jukumu la kuharibu mizinga yote ya asali. Hujui faida ya nyuki ulimwenguni? Uliamua kuharibu asali ya nchi. Jadili maudhui ya ukiukaji wa haki za watoto katika hadithi  ya ;
  1. Mapambazuko ya Machweo (alama 10)
  2. Sabina (alama 10)
 7. Siku moja alipokataa katakata kuandamana na mumewe, jungu lilifoka. “Wewe mke sampuli gani usiyetaka kumuunga mkono mmeo?” Haya kaa nyumbani. Kula na kulala tu, hujui jingine. Ona umbo lako sasa, kama nguruwe. Si mke mrembo niliyeoa! Wanawake ni wengi…”
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
  2. Bainisha vipengele vinne vya kimtindo katika dondoo hili (alama 4)
  3. Fafanua nafasi ya mwanamke katika hadithi hii. (alama 12)

                                                                      SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI
 8. Soma kifungu hiki kisha ujibu maswali
  Hapo zamani za kale, Nyani na Mamba walikuwa marafiki wa kufa kuzikana. Watoto wao walipendana na kufaana kama ndugu wa toka nitoke. Familia ya Mamba aliishi mtoni nayo ya Nyani aliishi katika msitu uliokuwa maili thelathini kutoka mtoni. Kila mara marafiki hawa walitembeleana na kusaidiana kwa hali na mali. Kwa vile Mamba alikuwa mvuvi mashuhuri, aliweza kumwauni Nyani na aila yake kwa samaki wa aina mbalimbali. Nyani naye alimpelekea Mamba matunda na nafaka kutoka shambani mwake.

  Urafiki wao ulikita mizizi na kunawiri zaidi wakati Mamba alipokuja kwa Nyani kumposea mwanawe binti. Ukwe uliutilia viungo uhusiano wa Nyani na Mamba wakawa wanagandana kama kupe na mkia wa ng’ombe. Wakatenda mengi pamoja. Wakazungumza ya kupwa na ya kujaa. Hakuna hata mmoja wao aliyeutilia shaka uaminifu wa mwenzake. Wake zao nao walifuata kaida ya maji kufuata mkondo. Walikuwa masahibu wa chanda na pete.

  Msimu mmoja wa mapukutiko ulishuhudia mabadiliko ya kudumu katika maisha ya Nyani na Mamba. Wakati huo, bahari ilichafuka si haba. Kazi ya Mamba ya uvuvi ikaanza kukabiliwa na majabali ya kila aina. Kila mara Mamba alipokwenda uvuvini, alirudi akichekelewa na nyavu zake. Hakuambulia chochote. Njaa ilianza kubisha hodi katika familia ya Mamba. Hali hii ilitishia kuutia ufa urafiki kati ya Mamba na Nyani. Mamba alivamiwa na pepo ambaye hata yeye alishindwa kumfahamu. Kila mara alipomwona. Nyani au watoto wake alitamani kumdakia na kumla mzima mzima. Kadiri alivyojaribu kujiasa dhidi ya fikira hii mbovu ndivyo moyo wake ulivyoendelea kumshauri, “Una njaa bwana, familia yako itaangamia. Je huoni rafiki yako na familia yake wanaweza kuwa kitoweo? Utaendelea kula wishwa hadi lini? Mbona huyo Nyani ambaye anajiita rafiki yako sasa amekata guu humu? Mbona haji tena kukutazama? Hata karafuu alizokuwa akikuletea ameacha kuleta. “Mamba akaanza kumshuku rafiki yake na akasadiki kuwa Nyani alikuwa mla naye tu.

  Usiku mmoja baada ya kula mate na kujilaza kitandani mwake akihesabu nyota, wazo lilimjia. Alikata shauri kumlaghai rafiki yake wa miaka mingi ili apate kujiokoa yeye na familia yake kutoka katika kinamasi cha njaa. Asubuhi yake alikwenda kwa Nyani akiwa amejiinamia kwa jitimai. Alisema, “Rafiki yangu, jana tulipoagana nilipata tanzia. Mjumbe kutoka kijijini aliniarifu kuwa baba yangu ni mgonjwa mahututi. Alisema kwamba baba ananitaka nyumbani upesi,” Habari hizi zilimtia Nyani majonzi makuu. Alimwahidi Mamba kwamba wangeandamana pamoja. Kwa vile Nyani hangeweza kutembea majini, ilibidi abebwe na Mamba. Alipatwa na kichefuchefu na manyezi kila alipotazama bahari iliyojitandaza mbele yao kwa mbwembwe. Hata hivyo, Mamba alimhakikishia kuwa wangefika salama. Naye kwa Imani iliyotokana na urafiki na mazoea ya miaka mingi, alitulia.

  Safari ilikuwa ndefu na yenye machovu yaliyomfanya Nyani kulala mgongoni mwa Mamba. Walipofika kwenye vina vya maji, Mamba aliamua kumpasulia mbarika Nyani. “Rafiki yangu, nimekuwa nikidhani wewe ni rafiki wa dhati, kumbe uzuri wako wa mkakasi? Mimi na wanangu tumetafunwa na njaa kwa miezi kadha sasa huku maghala yako yakishiba na kutapika chakula. Hujadiriki hata siku moja kuja kujua kama nimepata hata senti moja ya kusagia mkunguni. Jana usiku nilipokuwa nikiwazia hali yangu, nilioteshwa katika ndoto kwamba kama ningepata moyo wako na kuula, basi hali ya uhitaji ingeniishia. Moyo wangu unaniuma sana kukufanyia tendo hili, hata hivyo lisilo budi hutendwa.”

  Nyani alipigwa na butwaa nusura moyo wenyewe ujikabidhi kwa Mamba. Hata hivyo, akili yake nyepesi ilifanya kazi. Alimwambia Mamba,”Ndugu yangu, pole sana ikiwa umekuwa unadhani sikujali. Kwa kweli, hata ungeniomba moyo wangu siku hizo ningekupa tu. Unajua tena sisi Nyani, Tumbili na Kima tuna mioyo mingi. Hata hivyo, nasikitika kuwa Mungu alituambia kuwa daima mioyo yetu itakaa mitini. Basi ndugu mpenzi, badala ya kuendelea na safari hii, turudi pale mtini nikupe moyo wangu pamoja na mitatu ya wanangu kusudi uwalishe wanao na mkeo.”

  Mamba akaingia mtegoni. Wakarudi hadi ufuoni. Kwa vile Mamba hakuweza kutoka majini, alibaki ufuoni akimngojea rafiki yake amletee mioyo.

  Mamba alitunga macho yake kwenye ujia alioufuata Nyani akiomba pasitokee lolote la kumchelewesha Nyani. Matumbo yalimnguruma kwa njaa. Roho ikampapa kwa tumaini. Alingoja, akangoja, akangoja... wiki, mwezi, mwaka... Nyani hakurudi. Mamba akajua amepwaguliwa na Nyani. Akaapa kumtafuta kwa udi na ambari. Huo ukawa mwisho wa urafiki kati ya Nyani na Mamba. Hadithi yangu inaishia hapo.
  Maswali 
  1. Tambua kipera cha utungo huu. Thibitisha. (alama 2)
  2. Fafanua  mbinu sita za  kimtindo alizotumia mtambaji wa utungo huu. (alama 6)
  3. Jadili shughuli za kiuchumi na shughuli za kijamii katika jamii hii. (alama 4)
  4. Umepewa jukumu la kutamba ngano hii. Fafanua mambo manane muhimu utakayozingatia ili kufanikisha uwasilishaji wako. (alama 8)

                                                              MWONGOZO WA KUSAHIHISHA 

 1.  
  1.  
   1. Ni maneno ya Yona
   2. Anajiambia
   3. Yuko kwake nyumbani
   4. Yona anajutia matendo yake. Hii ni baada ya yeye kuelewa kuwa mkewe alikuwa muwele kwa kweli na alihitaji usaidizi wake   Zozote 4×1=4   
  2.  
   1. Ritifaa - Yona kuisemesha pombe kana kwamba anasema na mtu. Kwa heri pombe.
   2. Uhaishaji- pombe imepewa sifa za kibidamu, umenichezesha kama mwanaserere..
   3. Uzungumzi nafsia- siwezi kuendelea …
   4. Msemo / nahau- nimekata shauri
   5. Uashiriaji – hivi
   6. Tashbiha – Kama mwanasesere
   7. Nidaa - pombe !        za kwanza 4×1=4
  3. Changamoto za ndoa
   1. Kuelimisha watoto. - Bunju alimsaidia Neema katika kuwaelimisha ndugu zake na kuwajengea wazazi wa Neema nyumba.
   2. Kuwapa ushauri. Sara anamshauri Neema kuhussu namna ya kukabiliana na hali mbalimbali maishani./ bembea inalika
   3. Kukosa watoto. Jamii inawasema Sara na Yona kwa kukosa kizazi katika kipindi cha awali cha ndoa yao.
   4. Malezi ya watoto. Neema na Bunju wanabishana kuhusu majukumu yao kumwelekea Lemi na jinsi ya kumlea. Neema anaonyesha kuridhika na juhudi za Lemi katika elimu ilhali kulingana na Bunju Neema analea unyonge.
   5. Kuendeleza mila na tamaduni za jamii. Yona anamtaka Sara kumwita Neema ampeleke Sara hospitali kwa kuwa fimbo ya mzee hurithi mtoto wa kwanza. Sara anamwambia Neema kuwa utamaduni haumruhusu kulala kwao na Bunju
   6. Kukosa mtoto wa kiume- Yona na Sara kusutwa na jamii kwa kukosa mrithi.
   7. Kuoa mke mwingine- jamii inamshinikiza Yona aoe mke mwingine
   8. Kichapo cha mbwa- Yona kumpiga Sara na kunsababishia dhiki ya kisaikolojia
   9. Ulevi – ulevi wa Yona kumfanya ampige Sara na kumsababishia uwele.
   10. Majukumu ya wanaume na wanawake- Bunju na Neema
   11. Asna kuonyesha hofu katika ndoa- itamnyima uhuru/ ubahili wa Bunju                     Kwanza 4×1=4 
  4. Umuhimu wa Sara katika kujenga ploti
   1. Sara ametumiwa kuonyesha athari ya migogoro katika ndoa. Maradhi ya moyo anayogangua ni tokeo la mzozano baina yake na mumewe Yona.
   2. Kupitia kwake tunaona alivumilia ndoa yake na kufanya juu chini ili wanawe wapate elimu ili kuboresha mustakabali wao.
   3. Aidha, anahakikisha kuwa binti zake Neema na Asna wanapata elimu.
   4. Ni mfano wa wanawake wenye bidii. Hata akiwa hospitalini, akili yake inafikiria mazao yake aliyoyaacha shambani.
   5. Kupitia mazungumzo baina yake na Asna, yanamsawiri Asna kama kijana aliyekengeuka kiasi cha kutotaka kuingia katika ndoa.
   6. Kupitia kwake tunaelezwa kuhusu usuli wa kutopika. Sara anaeleza kuwa kwa sababu ya ugonjwa wake hangeweza kupika.
   7. Sara alisemwa na kutukanwa na wanajamii kwa sababu ya kuwapata watoto wa kike pekee. Hii ilipelekea Yona kuingilia ulevi.
   8. Baadhi ya matukio katika maisha ya wahusika fulani yanaangaziwa katika nyumba yake.  k.m Dina anaangaziwa kama mwenye utu kwani anaenda kumpikia kwa kuwa alikuwa mgonjwa.
   9. Kupitia mazungumzo baina yake na Yona, tunapata kujua kuwa Neema ndiye aliyewasomesha wanuna wake hadi chuo kikuu.
   10. Pia, Sara anatujuza kuwa Neema ndiye aliyewaajiri wafanyakazi nyumbani kwake.
   11. Ametumiwa kuonyesha uwajibikaji wa Neema. Neema anagharamia matibabu ya Sara na pia anampa babake/Yona pesa za kwenda kwa wazee wenzake.
   12. Kupitia kwake tunafahamu kuwa Bunju ndiye aliyemsaidia Neema baada ya kupata ajali na kulipia gharama za hospitali ilhali Bunju hakuwa amemjua Neema.
   13. Kupitia mazungumzo baina yake na Neema na Asna tunapata kujua kuhusu tofauti baina ya hospitali za mjini na kijijini. Huduma za hospitali mjini ni mzuri lakini za kijijini zinalinganishwa na seli na wahudumu hawana mlahaka mwema.
   14. Hatima ya mgogoro baina ya Sara na Yona. Yona anaachana na mila na tamaduni za kutopika kwa Mwanaume.
   15. Anaonyesha jinsi utamaduni ulivyowakandamiza wasichana –Sara anamwambia Asna kuwa siku zao elimu ya wasichana ilifanyiwa bezo na kuwa Sara aliachia darasa la saba.
   16. Kuonyesha mustakabali wa Sara wa kumsamehe,Yona-Yona anamwomba Sara msamaha kwa kuwa hakujua upeo wa ugonjwa wa moyo.    (zozote 8x1=8)
 2. UFAAFU WA ANWANI - Anwani ya Riwaya hii ni Chozi la Heri. 
  • Chozi la heri ni chozi ambalo linatoka wakati mhusika fulani amepata amani, utulivu na usalama/ nafuu.
   1. Mwandishi anatueleza kuwa Ridhaa alipokwenda shuleni siku ya kwanza alitengwa na wenzake kwani hawakuta ashiriki michezo yao. Mamake alimliwaza na kumhakikishia kumwona mwalimu keshoye. Tangu siku hii, huu ukawa ndio mwanzo wa maisha ya heri kwa Ridhaa. Ridhaa alipea kwenye anga ya elimu hadi kufikia kilelecha cha elimu na kuhitimu kama daktari.
   2. Ridhaa alipotoka kwenye Msitu wa Mamba alijiona nafuu kwani wapwa zake- Lime na Mwanaheri walikuwa wamepata matibabu. Dadake Subira alitibiwa akapona. Mwamu wake Ridhaa anajua kuwa Kaizari ni afadhali kwa sababu hakuna aliyemtenga na mmoja kati ya jamaa zake. Ridhaa anapomfikiria Kaizari anajiambia heri nusu Shari kuliko Shari kamili.
   3. Ridhaa aliposikia sauti ya kike ikitangaza, tangazo lile lilimrudiSha katika mandhari yake ya sasa. 
   4. Mwangeka alikuwa akijiuliza iwapo babake amekuwa mwehu kwa kukosa kushirikiana na majirani kuchimba kaburi kuyazika majivu- matone mazito ya machozi yalitunga machorni mwake Mwangeka. Akayaacha yamdondoke na kumcharaza yatakavyo. Moyo wake ukajaa utulivu sasa kwa kujua kuwa wino wa Mungu haufutiki.
   5. Wakati Ridhaa alikuwa akimsimulia Mwangeka misiba iliyomwandama tangu siku alipoondoka kwenda kuweka  amani Mashariki ya Kati, Uk 48
   6. Mwangeka alipokuwa ameketi mkabala na kidimbwi cha kuogelea, mawazo yake yalikuwa kule mbali alikoanzia.  Alipomkumbuka Annatila(Tila) mwili ulimzizima kidogo akatabasamu kisha tone moto la chozi likamdondoka.
   7. Katika Msitu wa Simba kulikuwa na maelfu ya watu waliogura makwao. Kati ya familia zilizoguria humu ni familia ya Bwana Kangata. Kwa Kangata na mkewe Ndarine, hapa palikuwa afadhali kwani hawakuwa na pa kwenda kwa kuwa hata kule walikokuwa wakiishi awali hakukuwa kwao. Uk 57 
   8. Wakati Dick walikutana kisadfa na Umu katika uwanja wa ndege, walikumbatiana kwa furaha. Machozi yaliwadondoka wote wawili na wakawa wanalia kimyakimya. Walijua fika kuwa jaala ilikuwa imewakutanisha na kwamba hawatawahi kutengana tena. Maisha sasa yalianza kuwa ya heri kwao.
   9. Baada ya miaka kumi ya kuuza dawa za kulevya, Dick alifaulu hatimaye kujinasua kutoka kwa kucha za mwajiri wake. Alianza biashara yake mwenyewe ya kuuza vifaa wa umeme. Sasa akaanza kujitegemea kwa kuwa amejiajiri. 
   10. Wakati Neema na Mwangemi walikabidhiwa mtoto wao wa kupanga na Mtawa Annastacia, Mwaliko alimkumbatia Neema na kumwita mama na kumwahidi kuwa ataenda naye. Neema alidondokwa na chozi la furaha na kumkumbatia Mwaliko kwa mapenzi ya mama mzazi. Hili lilikuwa ni chozi la heri .
   11. Dick alimweleza Umu kuwa siku waliokutana katika uwanja wa ndege na wakasafiri pamoja, hiyo ndiyo ilikuwa siku ya heri zaidi kwake.
   12. Dick aliposimulia namna wazazi wake wapya pamoja na Umu walivyomfaa maishani, 
   13. Baada ya Mwaliko kujitambulisha kwa Umu na Dick, umu na Dick hawakungojea amalize. Walikimbia wote wakamkumbatia ndugu yao, 
   14. Mwaliko alimwambia babake kuwa kuja katika hoteli ya Majaliwa kuliwaletea heri kwa kuwa familia yao sasa imepanuka. Sasa amekutana na watu aliokuwa tu anasikia wakitajwa. Maisha sasa ni afadhali.
   15. Dick alitoa shukrani tele kwa Umu kwa kuwa alimpa matumaini kuwa siku moja watampata ndugu yao Mwaliko.
   16. Siku ambayo Mwangeka alimwoa Apondi ilikuwa siku ya heri kwake kwani alimwaga chozi la heri. 10x2 = 20
 3.  
  1.  
   1. Maneno ya Naomi katika uzungumzi nafsia wake.
   2. Kwa wanawe
   3. Mjini alikokuwa amewekeza kwa kufungua biashara ya kuwapigia chapa wanafunzi wa chuo kikuu.
   4. Hii ni baada ya kufutwa kazi na kimbaumbau baada ya kumpitishia makuruhu mengi kama kumpiga na kumkata mshahara kwa kukataa kuhusiana naye kimapenzi.
   5. Naomi alikuwa amejutia kuwaacha wanawe na mume. Alikuwa pia ameshazuru kiambo chake cha zamani na kulifyekea kaburi la Lunga. 4x1
  2.  
   1. Naomi kwa kukataa mabadililiko ya hali ya uchumi baada yake na Lunga kurudishwa mlima wa simba, anawatelekeza wanawe na lunga kwa nia ya kutafuta maisha bora.
   2. Sauna anawaiba watoto wa watu kama Dick na mwaliko ili kujipatia riziki kubwa.
   3. Bi Kangara anafanya biashara haramu ya kulangua binadamu ili kupata riziki. Anamshauri Sauna kuifanya biashara hii ili kuundokea uhitaji.
   4. Bw. Maya kumbaka Sauna ni kuongozwa na ubinafsi huku akaididimiza haki za Sauna.
   5. Wazazi wa Pete na wajomba zake wanaongozwa na ubinafsi wanapomwoza pete ambaye ni mtoto mdogo asiyestahili kuozwa.
   6. Mwanzi kwa kuutaka uongozi wa nchi ya wahafidhina anawachochea vijana kufanya ghasia za baada ya uchaguzi. 
   7. Kedi anaongozwa na hisia za kikabila kuteketeza familia ya Ridhaa.
   8. Wanawake wengine wanawatupa Watoto wao baada ya kujifungua. Riziki immaculata alikuwa ameokotwa kwenye jalala la taka inaposemekana ni kawaida kwa Watoto kutupwa.
   9. Mkewe Satua kullalamika kwa kumpa Chandachema hifadhi kuwa anaongeza msongamano kwenye chumba cha Watoto.
   10. Bwana Tenge anashiriki uasherati na kuishia kuwaathiri wanawe na Chandachema kisaikoljia. xi) Babake Kairu anajihusisha katika mahusiano nje ya ndoa na mamake Kairu na kuishia kumtelekeza kairu.
   11. Bw. Mabavu anaongozwa na tamaa ya ardhi na kulitwaa shamba la babake shamsi kwa kutumia hatimiliki bandia. Shamsi na babake wanakuwa maskwota wahitaji.
   12. Halmashauri ya mikopo ya elimu ya chuo kikuu kuwafadhili wanafunnzi wanaojiweza na kuwaapuza maskini wanaopaswa kupata ufadhili huu. Wanafunzi maskini wanaishia kupitia haali ngumu za maisha na kuingilia ulevi ili kujipurukusha.
   13. Wasimamizi wa hospitali za umma wanashiriki katika ufisadi wa kuuza dawa za hospitali kwenye maduka ya kibinafsi. Hospitali zinaishia kutoa huduma mbovu kwa umma. Zozote 8×1=8
  3.  
   1. Wahusika na maudhui
    Pete Anaenduleza maudhui ya;
    1. Ndoa na changamoto zake
    2. Ukiukaji wa haki za Watoto wa kike
    3. Ubabedume
    4. Nafasi ya mwanamke
    5. Ndoa za mapema
    6. Elimu na changamoto zake
    7. Tohara katika jamii
     Shamsi Anaendeleza maudhui ya;
     1. Ukoloni mamboleo
     2. Ajira na matatizo yake
     3. Elimu
     4. Ulevi na athari zake
     5. Utamaduni zozote 4×1=4
      Aghalabu azungumzie wahusika wote wawili
 4. USHAIRI
  1.  
   1. Ukitaka nifike leo, ninatamani lakini mwili unauma
   2. Naomba radhi sina nguvu za kushiriki kazi
   3. Ninapenda kushirikishwa katika makundi lakini mwili
   4. Mwili hauhitaji kelele na vitisho
   5. Ugonjwa umeharibu mwili
   6. Mwili si kama gurudumu
   7. Hakuna vipuri vya mwili ningetia
   8. Ningekarabati mwili kwa ustadi
   9. Ningeunganisha mwili ili uvutie
   10. Siogopi kupata maovu, sitajuta
   11. Hata nikifutwa kazi nitatunza mwili alama 8x1)
  2.  
   1. inkisari – kitaka, kuvicha, ngeushuruti
   2. kuboronga sarufi – ila wauma mwili
   3. mazda – utimile
   4. tabdila – utimile
   5. ukale - uwele alama (4x1)
  3.  
   1. masikitiko
   2. huzuni
   3. uchungu
   4. majuto      (alama12)
  4.  
   • Nafsi neni – mgonjwa
   • nafsi nenewa- mwajiri/ bosi (alama2x1)
  5. Ukawafi - vipande 3        (alama2)
  6. Ubeti wa mwisho kwa lugha nathari.    (alama 3x1)
   • Ninapenda kazi kwa nguvu na kiakili. Hata hivyo sipendi kumenyeka kuloa jasho la damu. Ugonjwa unapotokea mwili huishiwa na nguvu.
 5.  
  1. (alama3x1)
   1. Mishororo-  takhmisa
   2. Maneno- kikwamba, pindu
   3. Vina- mtiririko
  2. Muundo wa shairi hili  (alama 4x1)
   1. Shairi lina mishororo mitano kila ubeti
   2. Limegawika vipande 2- ukwapi na utao
   3. Vina vyake vinatiririka kila ubeti
   4. Shairi lina kibwagizo- Yafanana na Sodoma, miji yetu kwa yakini
   5. Mshororo mmoja umetumiwa kuanzia kila ubeti
   6. Lina beti 8
  3. Mbinu  za kimtindo  katika shairi hili     (alama3x1)
   1. Tashbihi - Yafanana na Sodoma
   2. Taswira - wanacheza lelemama, Marijali wa mbioni, 
   3. Tasfida  - Wanatafuna maini, kujipagaza umama
  4.  
   1. masikitiko
   2. huzuni
   3. uchungu
   4. majuto       (alama1) 
  5. Bainisha nafsi nenewa katika shairi hili    (alama1)
   Waumini, wasichana na watu
  6. (alama2x1)
   • Kutaka kuonya waumini na watu ili wamheshimu Mungu waache kutembea uchi
   • Kuonya viongozi wa dini waache kupenda pesa.
  7. Ujumbe
   1. Waumini wanafanya uasherati
   2. Watoto pamoja na wazima ni wazinzi
   3. Hawaoni soni
   4. Baba kuzini na mabinti
   5. Wasichana kushika mimba mapema
   6. Wanakataa dini hata wanapozaliwa
   7. Watu kutembea uchi ufuoni
   8. Wanatafuta riziki kwa uzinzi
   9. Watu wamekengeuka, mambo ya kigeni
   10. Viongozi kuabudu pesa (alama 4x1)
  8. (alama2)
   1. Manani  -Mungu
   2. Marijali – wanaume / barobaro 
 6.  
  1. Mapambazuko ya Machweo
   1. Haki ya kuishi/ jasho - hakuna hewa mgodini
   2. Ajira ya watoto - watoto wadogo na vijana kuchimba mchanga na kusomba kwa mikokoteni.
   3. Afya – hakuna miale ya jua kwenye mgodi
   4. Kutishwa na wanyapara - walinzi katili
   5. Mazingira duni
   6. Kuchimba gizani- taa za vibatari
   7. Kulala kwenye mabanda
   8. Kutoruhusiwa kuondoka- walinzi wakali, mbwa wakubwa na nyua za stima
   9. Kukatiziwa masomo- vijana na watoto wadogo
   10. Wanakusanywa barabarani kwa probox ya Makutwa
   11. Kufanywa kuwa watumwa- Sai na Dai 10x1=10
  2. Sabina
   1. Kunyimwa haki ya kusoma- anaambiwa anaharibu mafuta na Yunuke
   2. Kukatiziwa masomo- Nyaboke kuacha shule katika kidato cha pili
   3. Ndoa za mapema – Nyaboke kukataa posa za wanaume/ Sabina kuozwa siku ya kutangaza matokeo
   4. Kufanywa mtumwa- kazi zinazozidi umri wa Sabina/ miaka 14
   5. Mavazi kuu kuu- Sabina kutoka shambani akiwa na rinda kuu kuu
   6. Mateso- matusi ya Yunuke, kumzimia taa, kumkashifu kwa kutouuza maziwa Itumbe
   7. Kuchelewa kufika shule- anafika saa tatu na nusu
   8. Kudhalilishwa – kukama ng’ombe, kuwapeleka malishoni, kuzoa kisonzo, kuuza maziwa asubuhi,kuandaa chajio, kuwafunga ng’ombe zizini
   9. Kutolindwa dhidi ya hatari – watu kuambaa familia ya Nyaboke/ laana
   10. Kudharauliwa na binamu zake Sabina/ Mike ndiye anambebea vitabu wakiwa malishoni.
   11. Kujaribu kumnyima bahati kwa kumwita Mike kuhojiwa na wanahabari.     10x1=10
 7.  
  1.  
   1. msemaji ni Luka
   2. msemewa ni Lilia
   3. nyumbani kwao
   4. Luka alimtaka mkewe kuandamana naye katika kampeni – taswira ya kiongozi anayethamini ndoa na familia ili achaguliwe kuwa gavana, (alama 4x1)
  2.  
   1. Balagha – wewe mke sapuli gani?
   2. Nahau = katakata, unga mkono
   3. Taswira – ona sasa
   4. Tashbiha – kama nguruwe
   5. Masimango – kama nguruwe
   6. Nidaa – niliyeoa!
   7. Mdokezo – wengi… 4x1
  3. Fadhila za punda
   • Mwanamke kutawishwa- lilia anaachishwa kazi ya umeneja na mwishowe kutawishwa.
   • Kukaa nyumbani na kutishwa asidhubutu kutoka nje ya lango.
   • Mwanamke anatishiwa – Lilia anapodhubutu kumshtaki mumewe anakumbushwa kuwa yeye ndiye Gavana na ana uwezo wa kufanya haki kuwa batili na batili kuwa haki.Utajua kichomtoa kanga manyoya.
   • Mwanamke anapokezwa kichapo cha mbwa - Lilia anapokea mapigo kutoka kwa mumewe anapoenda kuripoti kwa polisi.
   • Mwanamke kutusiwa - Lilia anaambiwa amenona kama nguruwe.
   • Mwanamke kudhalilishwa - Lilia annambiwa kuwa ana umbo kama nguruwe kwani kazi yake ni kula na kulala tu.
   • Mwanamke kuendewa kinyume na mumewe katika ndoa-  Luka anasemekana kuwa na kiruka njia ambaye waliandamana naye kila mahali. Lilia anapouliza ni nani anapokea kipigo kinachomlaza kitandani siku mbili.
   • Kuachishwa kazi. Lilia anaachishwa kazi na mumewe ili awe mpokezi wa wageni nyumbani.
   • Ni chombo cha starehe
   • Wasaliti – kunyanganywa bwana
   • Kunyimwa uhuru wa kutangamana
   • Kutohusishwa katika maamuzi ya familia
   • Mwajibikaji – mamake gavana
   • Mwaminifu – Lilia kwa mumewe
   • Mwenye mapenzi ya dhati-  Lilia
   • Mvumilivu- Lilia na mavya wake                         Zozote 12x1= 12
 8. FASIHI SIMULIZI
  1. Ngano ya Usuli – inatueleza kwa nini urafiki wa nyani na mamba ulisambaratika. (ala 1x2
  2. Mbinu za kimtindo
   1. Nahau – kufa kuzikana/Pasulia mbarika
   2. Tashibihi – kufaana kama ndugu wa toka nitoke /kama kupe na mkia wa ng’ombe
   3. Methali – maji hufuata mkondo/ lisilobudi hutendwa
   4. Uhuishi/tashihisi – kuchekelewa na nyavu/njaa kubisha hodi
   5. Mdokezo wa methali – alikuwa mla nawe tu.    Uzuri wako wa mkakasi.
   6. Chuku – maghala yakishiba na kutapika
   7. Takriri – alingoja... akangoja... akangoja
   8. Mdokezo – alingoja .... mwaka...
   9. Dayalojia – kati ya nyani na mamba
   10. Balagha – mbona haji kukuona?
   11. Uzungumzaji nafsia – una njaa bwana, familia yako itaangamia.     (za kwanza 6 x 1 = 6)
  3.  
   • Kiuchumi –
   • Uvuvi – mamba,
   • Kilimo − karafuu, matunda na nafaka,
   • Uwindaji – kukufanya kitoweo, moyo
   • Kijamii − posa ya mwanawe mamba kwa binti wa nyani 4x1
  4.  
   1. Kuhusisha hadhira ili kuundoa ukinaifu 
   2. Uigizaji – matendo ili kusisitiza ujumbe
   3. Kutumia viziada lugha – ishara za uso, mikono
   4. Kutumia maleba yanayoafikiana na hadithi inayowasilishwa
   5. Kubadilisha toni
   6. kiimbo kulingana na ujumbe ninaopitisha
   7. Kuwa mbaraza, kuingiliana vyema na hadhira yangu.
   8. Kuelewa lugha ya hadhira
   9. Kuwa mkakamavu/jasiri
   10. Kuwa mfaraguzi – kubadilisha hadithi
   11. Kuwa mcheshi ili kuchangamsha hadhira yangu.
   12. Kuelewa hadhira  na mahitaji yake
   13. Kutumia sauti inayosikika 
   14. Ubunifu
   15. Nyimbo              (za kwanza  8 x 1 = 8)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - BSJE Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?