Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Lanjet Joint Mock Exams 2023

Share via Whatsapp

Maagizo 

  • Jibu maswali yote
  • Maswali yote ni sharti yaandikwe kwa lugha ya kiswahili
  1. UFAHAMU (ALAMA 15)
    Shule Yangu Ya Upili
    Majio yangu katika shule hii ya upili hayakutokea kwa bahati nasibu bali kwa mipango kabambe niliyoianza tangu nikiwa shule ya vichekechea.Nikiwa sitetereki hata kwa wazazi wangu waliponisihi nijiunge na shule nyingine za karibu nikawa sisikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini.Nikawa na ragba ya mkanja nikingoja siku ya kujiunga na shule yenyewe.Kweli majuto ni mjukuu na huja kinyume.

    Nilizaliwa katika aila yenye nafasi iliyotopea na kubobea katika ukwasi uliodhihirika kutokana na mitaa tulikoselelea kwa muda kabla ya baba kuaamua kununua nyumba yake mwenyewe huko upande wa Karen hivyo tukagura kutoka Lunda.Wakatiwa likizo tukawa tunaruka hadi pwani ambako mama yangu alikuwa amemiliki jumba lililokuwa katika ufuo wa bahari lililojengwa katika kipande kisichopungua ekari tatu alilotunukiwa wakati wa nikahi yao na wakwe wa baba yangu.

    Wavyele wangu wakawa wanaendesha magari meusi ya kifahari ingawa sikuwahi kumwona mama akichangamka kuendesha magari yake ya maana,kila macheo ya siku za kazi gari lililoendeshwa na dereva ambaye alimstahi mama hadi akawa anamfungulia mlango wa gari na kuufunga baada ya mama kujitoma katika tumbo la gari lilimjia na kumrejesha kwa wakati.Nikajiunga na shule ya msingi ya kibinafsi ambako nilishughulikiwa kama kikembe.Wengi wa wale tuliosoma nao walikuwa wa tabaka langu na walikuwa wametoka katika kila sehemu nchini Kenya.

    Hayawi hayawi huwa na siku ya kuripoti ikafika.Alfajiri,dereva mmoja akatumwa kwenda hadi Kisumu ili atulaki na kutusafirisha kutoka uwanja wa ndege hadi shule ya upili ambayo ilikuwa yangu ya rohoni.Nasi tukaelekea hadi uwanja wa ndege ili turuke hadi Kisumu.Safari yetu kutoka kitongoji cha kifahari hadi Airport ilikuwa njema,safari yetu tulipoabiri ndege ilikuwa bila bughudha,safari yetu kutoka Kisumu mjini haikuwa na kasoro na tulienda kulingana na mpango.Safari yetu ilikuwa mufti hadi tulipofika katika lango la shule ya kitaifa!Tulipotia ozi tu!!....jamani......jamani nikafa moyo.Labda mama aliweza kubaini mabadiliko ya hisia zangu,nilitamauka, nikawa mchege na kusema kweli niliyoyaona sikuamini.Mvua iliyokuwa imepasua hapo awali ilikuwa imeacha vitua vya maji kwenye vijia vya kutembea vilivyochakaa na kubomoka bila yeyote kuja kuvikarabati.Majengo yalikuwa makongwe yaliyojengwa miaka mia moja iliyopitana yalistahili kuitwa makavazi badala ya pahali pa kumkaribishia mwanafunzi aliyepita kwa alama mia nne na thelathini na tano.Asiye na wake ana Mungu,nikapiga moyo konde lazima nisajiliwe katika shule ya ndoto yangu.Ningewezaje kughairi wazo langu baada ya siku hizo zote za maandalizi tena mbele ya wanuna walioniona kama kielelezo chao tangu walipozaliwa.Nikasajiliwa!

    Sikujua shule ya upili ya kitaifa yaweza kuwa hivi.Kweli mwanafunzi aweza kukosa viatu na hatakushindwa kununua rangi ya kupaka viatu hivyo iwapo amenunuliwa na wahisani?Nilimlaumu nina maana hakunieleza kuwa mtu anaweza kula chakula ambacho mbwa wetu hawezi hata kukiangalia.Nilipoingia katika ukumbi wa chakula nilihisi kitefutefu nusura nichafukwe na moyo. Makapi ya mboga na uchafu usioelezeka ulinikumba,kisha nikapewa kisahani cha plastiki na kupakuliwa kipande cha ugali ambacho bado kilikuwa na unga na kuachiwa hiari ya kukila au kukitupa.Wenzangu wakawa wanakirambatia chakula kwa kasi huku mmoja wao alipoona jinsi nilivyokiangalia changu akanisihi nimpe chote na kukimaliza fyu.Wote walikuwa na furaha kemkem na kuajabia utukufu wa shule iliyotukuka ya kitaifa ila mimi. Baada ya mlo‘rojorojo’,tukaelekea darasani nilikopigwa na mghuma mkubwa. Tulikuwa wanafunzi hamsini na watano katika darasa moja tu! Mwalimu mmoja akaja na kutukaribisha shuleni kisha akatuarifu kuwa atakuwa mwalimu wa darasa letu.Nilipomsikia akinena nusura niishiwe na stahamala,kimombo chake kilinishangaza,hasa matamshi yake yalipungukiwa na kudhihirisha athari za lugha ya asili.Nilihisi kana kwamba ningemrekebisha lakini sikudhubutu.

    Tukafululiza hadi bweni na nikajilaza kitandani chembamba huku mwingine nisiyemjua lakini asiyejua kuwa kuna nguo maalum za kulala akalala uchi katika ghorofa ya juu ya kitanda chetu.Mgeni njoo mwenyeji apone maana baada ya muda wadudu ambao sikuwahi kuwaona aushini mwangu wakaanza kunishambulia. Nikaamka baada ya kumnasa mmoja wa wadudu hawa na kuuliza mmoja wa wenzangu ni wapi wadudu hawa na kwa kutojali hata kidogo,akanieleza kuwa hawana neno bali ni kunguni tu,Sikujua na kwa kweli mama hakuniambia kuwa kuna wadudu wanaotafuna mtu na hunuka fye! Sikulala kwa hofu huku wenzangu wakiforota kwa njia ya kunighasi.Sikuwahi kudhani kuwa watu wengi wanaweza kulala chumba kimoja huku changu kikiwa na hamamu na vifaa vyote muhimu kikibaki bila mtu! Tulisomeshwa na walimu wasiojali kana kwamba tunaelewa au la.

    Hawakushughulika iwapo tulifanya kazi za ziada aula,ndio,hakujali chochote. Kilichonishangaza ni kuwa wanafunzi waliojiunga nasi kutoka shule za umma wenye alama duni waliwapenda na kuelewa haraka walichosomeshwa na hawakujali matamshi yao,labda hawakuyatambua. Hatimaye tukafanya mtihani wa mwisho wa muhula wa kwanza.Nilishangaa ghaya iliponibainikia kuwa aliyetuongoza alikuwa ghulamu mmoja mshamba niliyempuuza tu mvulana kutoka kijijini ambacho singetambua katika ramani ya nchi ambaye hata vitu vya kimsingi vilimpiga chenga.Nikafanya uchunguzi nikatambua mwenzangu alikuwa na alama mia mbili hamsini na tatu akitoka katika darasa la nane. Nilifanikiwa kuwa nambari mia mbili hamsini na tatu kwa jumla ya wanafunzi mia tatu! Tulipofunga kwa likizo ya Pasaka nikaamua kuchukua hatua nyingine: Sitawahi kuhama kutoka shule hii ya upili wala kuwa zaidi ya nambari kumi!
    Maswali
    1. Thibitisha kauli kuwa msimulizi ana msimamo thabiti. (alama2)
    2. Tofautisha jinsi mwandishi alivyofunzwa katika shule ya kibinafsi na shule ya upili.(alama 2)
    3. Taja mambo matatu yanayotuonyesha kuwa msimulizi alilelewa katika aila ya kikabaila kulingana na aya ya pili. (alama3)
    4. Andika masuala matatu yaliyomshangaza katika shule ya upili. (alama3)
    5. Andika tamathali mbili zilizotumika katika kifungu. (alama2)
    6. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumika katika kifungu. (alama3)
      1. Alimstahi
      2. Kughairi
      3. Kunighasi
  2.                                                                      SEHEMU B:UFUPISHO (ALAMA15)
                                                                         Soma kifungu kisha ujibu maswali.
    Ripoti za kila mara kuhusu uharibifu wa pesa za umma katika serikali za kaunti ni za kusikitisha.Kuna mabilioni ya pesa za kulipa ushuru ambazo hufujwa katika serikali kuu,na hivyo basi wananchi wanakosewa sana wanapoona mtindo huu ukiendelea pia katika serikali za kaunti.Wakati katiba ilipopitishwa mwaka wa 2010,Wakenya wengi walikuwa na matumaini mno kwamba ugatuzi ungewatatulia matatizo ambayo walikuwa wakipitia katika tawala zilizotangulia,hasa katika maeneo yaliyotengwa kimaendeleo.

    Miaka tisa baadaye,kuna mafanikio ambayo yamepatikana ila hatua kubwa zaidi inaweza kupigwa katika kuboresha maisha ya kila raia kama mianya inayotumiwa kufuja pesa za umma itazibwa.Wizi huu unaojumuisha pia jinsi magavana wanavyobuni nafasi za kazi zisizo na maana ambazo wakati mwingi hupeanwa kwa jamaa na marafiki wao,ni sharti ukomeshwe mara moja.

    Kuna wananchi wengi ambao tayari wameanza kufa moyo kuhusu umuhimu wa ugatuzi ilhali ukweli ni kwamba hatungependa kurejelea utawala ulio chini ya serikali kuu pekee.Changamoto za ugatuzi zinazosababishwa na ulafi wa viongozi wachache zinatoa nafasi kwa wakosoaji wa mfumo huu wa uongozi kushawishi wananchi na hata wahisani wasishughulike kuchangia katika maendeleo ya kaunti zao.

    Juhudi zozote zile za maendeleo haziwezi kufanikishwa bila ushirikiano kutoka kwa wananchi na wahisani na hivyo basi ni jukumu la viongozi kuonyesha nia ya kutumia mamlaka waliyopewa kwa manufaa ya raia.Tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) kufikia sasa imeonekana kufanya kazi nzuri kwa kuwasaka na kuwashtaki magavana walio mamlakani na wengine walioondoka,kwa kushukiwa kufuja mali za umma.Tungependa asasi zote zinazohusika na masuala ya kupambana na uhalifu, pamoja na wadau wengine katika jamii wenye nia njema kwa wananchi wasifumbie macho maovu yanayotendwa katika kaunti zetu.

    Nchi hii inatawaliwa kwa misingi ya kisheria na hivyo basi hakuna sababu kumhurumia kiongozi yeyote anayekiuka sharia anapokuwa mamlakani kwa msingi wa mamlaka aliyoshikilia.Ni kupitia adhabu kali za kisheria pekee ambapo tutafanikiwa kukomesha uongozi mbaya kwani kama wananchi watakuwa wakisubiri kuwaadhibu wahusika kwa kuwaondoa mamlakani pekee,watakuwa wametoa nafasi ya ufujaji kwa viongozi wapya kila miaka mitano.
    (Kutoka gazeti la Taifa Leo)
    1. Fupisha ujumbe wa aya tatu za kwanza kwa maneno 80. (alama8,1 yamtiririko)
      Matayarisho
      Jibu
    2. Fupisha aya mbili za mwisho kwa maneno 70. (alama7, 1 ya mtiririko)
      Matayarisho
      Jibu
  3.                                                       SEHEMU C: SARUFI NA MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
    1. Andika neno lenye muundo ufuatao; (alama 2)
      Kikwamizo sighuna cha mdomo meno,irabu ya mbele juu,nazali ya midomo,kipasuo ghuna cha midomo na irabu ya nyuma wastani.
    2. Tunga sentensi kwa kutumia kiwakilishi huru cha nafsi ya tatu umoja.(alama 2)
    3. Tambulisha vipashio vitatu vya lugha ya kiswahili.(alama 3)
    4. Tumia neno ‘vibaya’ kama; (alama 2)
      1. Kivumishi
      2. Kielezi
    5. Tunga sentensi moja katika wakati ujao hali endelevu.(alama 2)
    6. Eleza matumizi ya ‘ni’ katika sentensi hii. (alama 2)
      Ingieni darasani mara moja ili niwape zoezi ambalo ni rahisi.
    7. Ainisha vielezi vya namna katika sentensi hii.(alama 2)
      Mzee huyu mkongwe alicheka kijinga huku akila haraka haraka.
    8. Tambua miundo mitatu ya ngeli ya LI-YA. (alama 3)
    9. Bainisha shamirisho na chagizo katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
      Kimani aliukata mti kwa kisu jana asubuhi.
    10. Andika kwa usemi wa taarifa: (alama 2)
      Karani: Njoo nikutume kwa baba yangu.
      Kamau: Sitaki kupita njia ya kwa babu.
    11. Nimenunua dawa ili iwamalize wadudu wanaotusumbua hapa kwetu nyumbani. (alama 2)
      Anza: Wadudu
    12. Andika kwa ukubwa hali timilifu. (alama 2)
      Mtego ulimnasa ndovu huyo.
    13. Bainisha vishazi katika sentensi fuatayo. (alama 2)
      Ingawa alitia bidii masomoni,alifeli mtihani.
    14. Tambua aina mbili za sentensi ukizingatia uamilifu na utoe mfano mmoja kwa kila moja.  N(alama 2)
    15. Taja na utolee matumizi mawili ya mkwaju. (alama 2)
    16. Changanua sentensi hii kwa kutumia kielelezo cha visanduku. (alama 4)
      Waswahili husema chema chajiuza kibaya chajitembeza.
    17. Andika sentensi moja ukitumia kitenzi ulichopewa katika kauli ya kutendewa. (alama 1)
      Ja
    18. Bunda ni kwa noti ,na bumba ni la nyuki ilhali _____________________________ ni kwa karatasi. (alama 1)
    19. Kamilisha methali hii. (alama 1)
      Mfa maji
  4.                                                               SEHEMU D: ISIMU JAMII (ALAMA 10)
        Kibiko: Hujambo dada Cheupe?
        Cheupe: (akikohoa) Sijambo ndugu Kibiko.
        Kibiko: Unaendelea namna gani?
        Cheupe: Niko poa isipokuwa maumivu kidogo ya chest.
        Kibiko: Usijali nitakupa pain relievers utakuwa sawa.
        Cheupe: Asante sana,nashukuru.
    Maswali.
    1. Eleza muktadha wa mazungumzo haya. (alama 2)
    2. Taja na ueleze sifa za lugha iliyotumika katika mazungumzo haya. (alama 8)

                                                               MWONGOZO WA KUSAHIHISHA 

  1. UFAHAMU
    1.  
      • Hatetereki anaposihiwa abadilishe wazo kuhusu shule ya ndoto lake.
      • Uamuzi wa kutohama kutoka shule hii hata baada ya kuona yaliyompata.        (zozote 2x1=2)
    2.  
      • Shule ya binafsi
      • Alitunzwa kama kikembe.
      • Walimu waliomfunza walitamka kimombo kwa njia bora.
      • Shule ya upili.
      • Matamshi ya walimu yaliathiriwa na lugha ya asili.
      • Walimu wasiojali. Uelewa wa wanafunzi wasioshughulika wasipofanyakazi za ziada.     (zozote2x1=2)
    3.  
      • Mitaa walikoishi
      • Uamuzi wa kununua nyumba Karen.
      • Kuruka hadi pwani.
      • Mama yake kumiliki jumba katika shamba la ekari tatu ufuoni.   (zozote3x1=3)
    4.  
      • Mwanafunzi kukosa viatu
      • Chakula duni katika shule hii.
      • Idadi ya wanafunzi katika darasa.
      • Kushambuliwa na wadudu.
      • Kuongozwa na mvulana kwa alama. (zozote3x1=3)
    5.  
      • Uhuishi-Tumbo la gari.
      • Misemo - Ragba ya mkanja.
      • Takriri - Sikujua.
      • Methali - Mgeni njoo mwenyeji apone. (zozote 2x1=2)
    6.  
      •  Alimstahi-Alimheshimu.
      •  Kughairi-badilisha.
      • Kunighasi - kunikasirisha. 3x1=3
  2. UFUPISHO
    1.  
      1. Ripoti za uhalifu wa pesa za umma katika serikali za kaunti ni za kusikitisha.
      2. Mabilioni ya pesa hufujwa katika serikali kuu.
      3. Wananchi wanakosewa mtindo huu ukiendelea katika serikali za kaunti.
      4. Katiba mpya ilipopitishwa wakenya walidhani ingewatatulia matatizo yao.
      5. Miaka tisa baadaye kuna mafanikio ingawa yanaweza kuboreshwa.
      6. Magavana hubuni nafasi za kazi na kupatia marafiki zao. vii)Wananchi wameanza kufa moyo kuhusiana na ugatuzi.
      7. Changamoto za ugatuzi ni ulafi wa viongozi wachache.
      8. Wakosoaji wa ugatuzi huchochea wananchi wasichangie maendeleo katika kaunti zao.     (alama8,1 ya mtiririko)
    2.  
      1. Juhudi za maendeleo haziwezi kufanikishwa bila ushirikiano.
      2. Ni jukumu la viongozi kuonyesha nia ya kutumia mamlaka kwa manufaa ya raia.
      3. Tume ya maadili ya kupambana na ufisadi inafanya kazi nzuri ya kuwashtaki magavana waliofuja mali ya umma.
      4. Asasi zote na washikadau wasifumbie macho maovu.
      5. Nchi inatawaliwa kwa misingi ya kisheria hivyo viongozi wasihurumiwe.
      6. Adhabu kali pekee zitakomesha uongozi mbaya.     (alama7,1 ya mtiririko)
  3. SARUFI
    1. Andika neno lenye muundo ufuatao; (alama 2)
      Kikwamizo sighuna cha mdomo meno,irabu ya mbele juu,nazali ghuna ya midomo,kipasuo ghuna cha mdomo na irabu ya nyuma wastani.
      Fimbo
    2. Tunga sentensi kwa kutumia kiwakilishi huru cha nafsi tatu umoja.(alama 2)
      • Yeye alienda sokoni. (tathmini jibu la mwanafunzi)
    3. Tambulisha vipashio vitatu vya lugha ya kiswahili.(alama 3)
      • Sauti
      • Silabi
      • Neno
      • Sentensi
    4. Tumia neno ‘vibaya’ kama; (alama 2)
      1. Kivumishi
        • Vitabu vibaya vimechomwa. (tathmini jibu la mwanafunzi.)
      2. Kielezi
        • Mtoto huyu amechapwa vibaya. (tathmini jibu la mwanafunzi)
    5. Tunga sentensi moja katika wakati ujao hali endelevu.(alama 2)
      • Mwalimu atakuwa anasoma/akisoma. (tathmini jibu la mwanafunzi)
    6. Eleza matumizi ya ‘ni’ katika sentensi hii. (alama 2)
      • Ingieni darasani mara moja ili niwape zoezi ambalo ni rahisi.
      • Ingieni –kiambishi amrishi wingi
      • Darasani –kielezi cha mahali
      • Niwape –kiambishi nafsi
      • Ni –kitenzi kishirikishi kipungufu.
    7. Ainisha vielezi vya namna katika sentensi hii.(alama 2)
      • Mzee huyu mkongwe alicheka kijinga huku akila haraka haraka.
      • Kijinga - namna mfanano
      • Haraka haraka - namna kikariri
    8. Tambua miundo mitatu ya ngeli ya LI-YA. (alama 3)
      • JI-ME   JINO –MENO
      • JI-MA   JINA –MAJINA
      • O-MA   TUNDA-MATUNDA
    9. Bainisha shamirisho na chagizo katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
      Kimani aliukata mti kwa kisu jana asubuhi.
      • Mti :shamirisho kipozi
      • Kisu :shamirisho ala
      • Chagizo :jana asubuhi.
    10. Andika kwa usemi wa taarifa: (alama 2)
      Karani: Njoo nikutume kwa baba yangu.
      Kamau: Sitaki kupita njia ya kwa babu.
      • Karani alimwita Kamau ili amtume kwa babu yake lakini alimwambia hakutaka kupita njia hiyo ya kwa babu.
    11. Nimenunua dawa ili iwamalize wadudu wanaotusumbua hapa kwetu nyumbani. (alam 2)
      • Anza: Wadudu wanaotusumbua hapa kwetu nyumbani,nimewanunulia dawa ili niwamalize.
    12. Andika kwa ukubwa hali timilifu. (alama 2)
      Mtego ulimnasa ndovu huyo.
      • Jitego/tego limelinasa jidovu/dovu hilo.
    13. Bainisha vishazi katika sentensi fuatayo. (alama 2)
      Ingawa alitia bidii masomoni,alifeli mtihani.
      • Kishazi tegemezi: ingawa alitia bidii.
      • Kishazi huru: alifeli mtihani.
    14. Tambua aina mbili za sentensi ukizingatia uamilifu na utoe mfano mmoja kwa kila moja. (ala 2)
      • Sentensi arifu. Mama alienda sokoni.
      • Sentensi za masharti. Ukinitazama nitalia.
      • Sentensi tatanishi. Alimpigia mpira.
      • Sentensi za rai/ombi. Naomba uniazime simu yako.
    15. Taja na utolee matumizi mawili ya mkwaju. (alama 2)
      • Hutumiwa kuandika tarehe. 5/6/2023
      • Hutumiwa badala ya neno au. Runinga/redio huwavutia na watu wengi.
      • Hutumika katika kumbukumbu.kumb/1/2023
      • Kuonyesha visawe. Mkolwe alinunua friji/jirafu/jokofu.
    16. Changanua sentensi hii kwa kutumia kielelezo cha visanduku. (alama 4)
      Waswahili husema chema chajiuza kibaya chajitembeza.
      KisMocksQ1
    17. Andika sentensi moja ukitumia kitenzi ulichopewa katika kauli ya kutendewa. (alama 1)
      Ja
      • Amina amejiwa gerezani na Yohana. (tathmini jibu la mwanafunzi.)
    18. Bunda ni kwa noti ,na bumba ni la nyuki ilhali burungutu/furushi/bunda ni kwa karatasi. (alama 1)
    19. Kamilisha methali hii. (alama 1)
      • Mfa maji haachi kutapatapa.
  4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
    Kibiko: Hujambo dada Cheupe?
    Cheupe: (akikohoa) Sijambo ndugu Kibiko.
    Kibiko: Unaendelea namna gani?
    Cheupe: Niko poa isipokuwa maumivu kidogo ya chest.
    Kibiko: Usijali nitakupa pain relievers utakuwa sawa.
    Cheupe: Asante sana,nashukuru.
    Maswali.
    1. Eleza muktadha wa mazungumzo haya. (alama 2)
      • Hospitalini/zahanatini.
    2. Taja na ueleze sifa za lugha iliyotumika katika mazungumzo haya. (alama 8)
      • Hutumia sentensi fupi fupi. Mfano hujambo dada Cheupe?
      • Kuchanganya ndimi mfano maumivu kidogo ya chest
      • Lugha haizingatii kanuni za kisarufi. Mfano niko poa.
      • Lugha ya udadisi hutumika.unaendelea namna gani.?
      • Msamiati maalum umetumika. Mfano pain relievers.
      • Lugha ya matumaini imetumiwa. Mfano utakuwa sawa.
      • Lugha ya majibizano- kibiko na cheupe.
      • Lugha ya unyenyekevu hasa kwa upande wa mgonjwa.mfano asante sana,nashukuru.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Lanjet Joint Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?