Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Nginda Girls Mock Examination 2023

Share via Whatsapp

MAAGIZO:

  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani;
    Riwaya, Tamthilia, Ushairi na Hadithi Fupi.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili


MASWALI

SEHEMU A: FASIHI SIMULIZI

Lazima

  1. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali
    Kila kukicha mashaka
    Ni kero hili si huba
    Mimi pendo la viraka, heri demu la mkoba
    Ingawa mno nataka, kuishi nawe muhiba
    Pendo viraka viraka
    Litanishinda kuziba

    Kamwe sitoshughulika
    Nawaje wenye kuziba
    Viumbe wanosifika,kwa fedha, chuma na shaba
    Walostaarabika, si mimi wa tobatoba
    Pendo viraka viraka
    Litanishinda kuziba

    Naapa sitojitweka
    Limenichosha si haba
    Nasomba vyangu viraka, nitie kwenye mkoba
    Sikuye ya kuzinduka, mjinga hawi juba
    Pendo viraka viraka
    Litanishinda kuziba
    1. Huu ni wimbo wa aina gani? Thibitisha. (alama 2)
    2. Eleza sifa tatu za nafsinenewa katika wimbo huu (alama 3)
    3. Bainisha toni ya utungo huu. (alama 1)
    4. Fafanua mbinu nne ambazo nafsineni itatumia kufanikisha uwasilishaji wake. (alama 4)
    5. Eleza mambo ambayo yatapotea wimbo huu ukiandikwa. (alama 6)
    6. Ingawa nyimbo zina faida kwa wanajamii, zina madhara pia.Yaeleze madhara manne. (alama 4)

SEHEMU B: RIWAYA
A. Matei; Chozi la Heri
Jibu swali la 2 au 3

  1. Jadili mchango wa wasomi katika maendeleo ya kijamii kwa kurejelea ‘Chozi la Heri'. (alama 20)
    au
  2. "Kipi kinachompa mama uyabisi wa moyo hata akawaacha wanawe? Umu alijiuliza Fikira za kila aina zilijitoma akilini mwake, akajiona akikabiliwa na tatizo kama la ndugu zake. Alijiona akichukuliwa danadana na majanaume katika madanguro mbalimbali. Wazo hili lilimtia kigegezi, malaika yakamsimama na mwili kumsisimka. Katika hali hii, alifikia uamuzi wa mkataa, kwamba hapo hapamweki tena, atatanga na njia aone jaala itakapomfikisha. "Nitapigana kwa jino na ukucha kuulinda utu wangu. Nitatafuta haki ilikojificha,” alisema Umu.
    1.  
      1. Fafanua aina tatu za taswira katika dondoo hili. (alama 3)
      2. Eleza vipengele vingine vitatu vya kimtindo vinavyojitokeza katika dondoo hili. (alama 3)
    2. Kwa kutolea mifano kumi na minne riwayani ,onyesha jinsi wahusika mbalimbali walivyopigana kwa jino na ukucha kuulinda utu wao na wa watu wengine. (alama 14)

SEHEMU YA C: TAMTHILIA

Timothy Arege: Bembea ya Maisha
Jibu swali la 4 au 5.

  1. Ulevi. Ulevi mwanangu! Gongo liliyamega maadili yake kimyakimya na taratibu uwajibikaji ukawa umemponyoka na kuteleza kama sabuni ya povu jingi na kumwacha na kisomo chake tu.
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Fafanua mbinu nne za kimtindo zilizotumiwa katika dondoo hili. (alama4)
    3. Eleza sifa nne za anayerejelewa . (alama 4)
    4. Jadili umuhimu wa mandhari ya mazungumzo haya. (alama8)
      au
  2.  
    1. Mwandishi wa tamthilia ya Bembea amefaulu kuchora mpaka uliopo kati ya usasa na ukale.Jadili kwa kutoa hoja kumi. (alama 10)
      b)Kuishi mijini kuna adha chungu nzima.Jadili kwa kurejelea tamthilia nzima. (alama 10)

SEHEMU D: USHAIRI

Jibu Swali la 6 au 7.


  1. Nduguni na dada zangu,nisikieni wendani
    Neleze ya moyo wangu,yalo yaniumizani
    Kuhusu ya ulimwengu,ng’onzi chui jifanyani
    Wanasiasa ndu zangu,wanazo hila Chekwa.

    Kila siku twahadawa, kura zetu kuzitaka
    Vitu duni tunapewa,twandanganywa kila mwaka
    Kwa wepesi shawishiwa,hatimaye sahaulika
    Wanasiasa ndu zangu wanazo hila Chekwa

    Watwambia shida zetu,kwazo siku tatatua
    Watwambia kila kitu,kitakuja tengenea
    Maisha ya kila mtu ,waamba tanawiria
    Wanasiasa ndu zangu,wanazo hila Chekwa

    Wao huwa karibuni,kutwahidi nao moyo
    Hali zetu twambiwani,taboreka bila wayo
    Kila kitu waahidini, tafakuri bila nayo
    Wanasiasa ndu zangu .wanazo hila Chekwa

    Lao ajabu ni kuwani, kama lubwi hugeuka
    Kiwapandisha ngazini, daima hutucheka
    Wetu ujinga nambani,hutufanya kusumbuka
    Wanasiasa ndu zangu, wanazo hila Chekwa

    Wakipata na migwisho, waoni tausi huwa
    Maringo yaso na mwisho, nyoyoni huwajawa
    Wanaamba kwa vitisho, wa viongozi kwa kuwa
    Wanasiasa ndu zangu, wanazo hila Chekwa

    Ndu zangu tuzindukeni, twondokee zao hila
    Kiwa humu duniani, wasije nao kutula
    Waadilifu chagueni, tusongozwe nazo hela
    Wanasiasa ndu zangu, wanazo hila Chekwa.

    Walo walipo neleza, siku yao itafika
    Walotufanya na boza, damu yetu faidika
    Siku zao zitaiza ,safari yao safirika
    Wanasiasa ndu zangu, wanazo hila Chekwa

    Ndu zangu la muhimu, ni kutokufa moyoni
    Duniani kiwa humu, tawaona kilipani
    Liyotendea kaumu, takuja kuyalipani
    Wanasiasa ndu zangu, wanazo hila Chekwa.

    MASWALI
    1. Kwa hoja mbili dhamira ya mshairi katika shairi hili (alama 2)
    2. Fafanua sifa tatu za warejelewa. (alama 3)
    3. Kwa kutolea mifano onyesha mbinu alizotumia mshairi ili kukidhi mahitaji ya kiarudhi. (alama 3)
    4. Tambua nafsineni katika shairi hili. (alama 2)
    5. Ainisha shairi hili kwa kutumia vigezo vifuatavyo. (alama 2)
      1. Vipande
      2. Vina
    6. Fafanua mbinu mbili za kimtindo zilizotumika katika shairi (alama 2)
    7. Andika ubeti wa saba kwa lugha nathari (alama 4)
    8. Eleza toni ya shairi hili. (alama 2)
      au

  2. Unaponyimwa uhuru
    Husemi unavyotaka
    Na kudadisi ya kweli
    Yakini mekandamizwa.

    Unapoliona kosa
    Kwa hofu usiliseme
    Mtu akukosowe
    Nawe usimkosowe
    Ndu yangu mekandamizwa.

    Unapofanywa mjinga
    Usiwe na uamuzi
    Ufanywe kama sanamu
    Na haulizi kwa nini?
    Hakika mekandamizwa.

    Unapoanza kuiga
    Kuiga bila sababu
    Na kushawishika ya kwamba
    Hu lolote hu chochote
    Ndu yangu mekandamizwa.

    Unapofanywa bidhaa
    Uwe mali ya mtu
    Na haulizi kwa nini?
    Hakika mekandamizwa.

    Unapotaka kulewa
    Kulewa ujipumbaze
    Usahau taabu zako
    Fahamu mekandamizwa.

    Unapoanza kuwaza
    Uwaze na uwazue
    Hujui ufanye nini
    Utakapo na kusahau
    Mawazo yakurudie
    Ndu yangu mekandamizwa.

    Unapokata tamaa
    Unapoheshimu mwenzako
    Kwa kile alicho nacho
    Taabu zikulemele
    Yakini mekandamizwa.

MASWALI

  1. Shairi hili ni la aina gani?Toa sababu yako. (alama 2)
  2. Tambua dalili zozote nne za mtu aliyekandamizwa kulingana na mshairi. (alama 4)
  3. Kwa kuotlea mfano, eleza maana ya mshororo mshata (alama 2)
  4. Fafanua mbinu za kimtindo/ kifasihi zilizotumika katika shairi hili. (alama 3)
  5. Onyesha namna mshairi alivyotumia idhini yake katika shairi hili. (alama 2)
  6. Tambua nafsi neni katika shairi hili. (alama 2)
  7. Andika ubeti wa pili kwa lugha nathari. (alama 4)
  8. Onyesha matumizi ya usambamba katika shairi hili. (alama 1)

SEHEMU E: HADITHI FUPI

D.Lutomia na Phibbian Muthama: Mapambazuko ya

Machweo na Hadithi Nyingine.

  1.  
    1. ‘Nipe Nafasi”
      Baridi ilizidi kututafuna kadri tulivyokazana kupanda Milima ya Maloti. Vidole vyangu vya miguuni vilikufa ganzi. Mashavu yetu yaliadhibika kwa upepo baridi huku vipande vya theluji vikitupiga kwenye nyuso zetu.Miili yetu iliathirika;tulihisi njaa na uchovu. Nikatamani tufike kwa jamaa ya baba yetu ambako tungepata angalau mchuzi wa papa kabla ya kulala. Bidii ya mama ilitutia moyo wa kuendelea na safari.
      1. Tambua nafsi ya usimulizi iliyotumika katika hadithi hii na uthibitishe jibu lako. (alama 2)
      2. Eleza umuhimu wa mwandishi kutumia nafsi uliyotaja hapo(i) juu. (alama 2)
      3. Bainisha mbinu mbili za kimtindo zilizotumika katika dondoo hili (alama 2)
      4. “Mamake Msimulizi (Richman) ni kielelezo cha wanawake jasiri””Thibitisha kwa kutolea mifano mwafaka (alama 7)
    2. Hadithi “Toba ya Kalia” inahimiza uwajibikaji. Jadili. (alama 7)


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA 

  1.  
    1.  
      1. Wimbo wa mapenzi
        • Mpenziwe hampendi kwa sababu hana pesa/ni maskini. (Kutaja-1, Mifano-1)
    2. sifa za nafsinenewa
      • Mpenda mali (ana tamaa ya mali – hampendi nafsineni kwa sababu hana pesa/mali
      • Msaliti - anasaliti mapenzi aliyo nayo nafsineni.
      • Mwenye mapenzi bandia - anapenda mali/
      • Mwenye dharau/ dhihaka - anamdharau kwa sababu hana pesa/ mali
      • Mwenye tamaa ya mali-pesa (za kwanza 3x1=3)
    3. Toni ya hasira/kutamauka/masikitiko/malalamishi/huzuni/ uchungu/ kuudhika (1x1=1)
    4. Kufanikisha uwasilishaji:
      1. Awe na sauti ya kuvutia.
      2. Aihusishe hadhira
      3. Aigize
      4. Aelewe utamaduni wa jamii husika.
      5. Atumie ishara/ miondoko
      6. Awe mkakamavu /jasiri
      7. Awe mfaraguzi
      8. Abadilishe toni
      9. Awe mbunifu.
      10. Aelewe lugha ya hadhira
      11. Atumie ala
      12. Avae maleba
      13. Awe mcheshi (za kwanza 4x1=4)
    5. Mambo ambayo yatapotea wimbo ukiandikwa
      1. Usemi halisi /usimulizi wa moja kwa moja
      2. Urudiaji wa baadhi ya vipengele /kuongeza vitushi fulani
      3. Viziada lugha/ miondoko/ ishara
      4. Ugizaji/udramatishaji
      5. Ala za muziki
      6. Maleba
      7. Toni ya wimbo
      8. Kauli za pembeni / maoni ya mwimbaji
      9. Ufaraguzi/ kubadilisha muundo wa wimbo
      10. Mtuo wa kidrama/fanani anapotua/kukaa kimya kwa muda
      11. Uhai wa hadhira /upokezi wa hadhira (zozote 6x1=6)
    6. Madhara ya nyimbo;
      1. Baadhi ya nyimbo zinapotosha kv. kusifu dawa za Kulevya / pombe/mapenzi kabla ndoa.
      2. Hutumiwa kueneza propaganda k.m nyimbo za siasa
      3. Baadhi huibua hisia zisizofungamana na maadili ya kijamii k.v. kuwatia watu hofu. Mfano: nyimbo za siasa,vita
      4. Humfanya mtu apuuze mambo mengine muhimu ya kufanya/uzembe
      5. Baadhi yazo hutukuza ukabila/ utabaka k.m nyiso, siasa
      6. Baadhi zinasifu mila na tamaduni ambazo zinadhulumu jamii kv. ukeketaji.
      7. Baadhi zinapunjua maadili ya vijana/ watoto, km waimbaji wakiwa nusu-uchi au kupigana busu hadharani
      8. Baadhi zinatumia lugha ya matusi na kusababisha aibu.
      9. Baadhi yazo zinapoimbwa huhimiza tabia mbaya/ ukosefu wa maadili. km nyiso-
      10. Baadhi huleta usumbufu kwa wanajamii hasa zinapoimbwa usiku. km siasa, nyiso
      11. Baadhi yazo humfanya mhusika akapandura na jadhiba/ hisia kali za Kidini Mfano, nyimbo za dini.
      12. Nyingine ni ghali huhitaji rasilmali ili kufanikisha ( za kwanza 4x1=4)
  2. Riwaya
    Mchango wa wasomi katika maendeleo ya kijamii
    Mifano ya wasomi riwayani.
    • Ridhaa – amehitimu katika taaluma ya udaktari
    • Selume – amehitimu kuwa mkunga na kuajiriwa kama muuguzi
    • Mwangeka – amehitimu katika taaluma ya uhandisi
    • Neema –amehitimu katika taaluma ya uhasibu
    • Mwangemi – ana shahada ya uzamili katika uuguzi
    • Apondi – ana shahada katika taaluma ya masuala ya kijamii
    • Mhandisi Kombo-mwanawe Mzee Kedi, ni mhandisi
    • Lunga- Afisa wa Kilimo nyanjani
    • Hazina –amesomea upishi na Huduma za Hotelini
    • Kaizari- Afisa wa matibabu
    • Naomi – ana stashahada ya uzamili
    • Dick – amesomea Teknolojia ya mawasiliano ya simu
    • Umu- ana shahada ya uhandisi katika musuala ya kilimo.
      1. Ridha anabadilisha eneo la Msitu wa Heri lililokuwa jangwa na kuwa na rangi ya chanikiwiti kutokana na kupanda miti
      2. Ridhaa kumsaidia Selume kupata ajira ya uuguzi baada ya mumewe Mwanzi kumtaliki hivyo kumsaidia kujikimu kimaisha.
      3. Daktari Ridhaa anajenga Kituo cha Afya cha Mwanzo Mpya ili awasaidie raia wasioweza kulipia huduma za matibabu katika hospitali za umma na za kibinafsi.
      4. Apondi anawatahadharisha walinda usalama dhidi ya kufyatua risasi ovyo na kuwaua raia wasio na hatia.
      5. Apondi na Mwangeka kuwasaidia raia maskini wasiojiweza katika eneo gatuzi lao.
      6. Mhandisi Kombo ndiye anayesimamia ujenzi wa jumba la Ridhaa.
      7. Ridhaa anayadhamini Masomo ya wapwaze Kedi.
      8. Ridhaa ana duka analopangisha wafanyabiashara,hivyo kuimarisha uchumi wa taifa.
      9. Apondi anasuta vitendo vya kihalifu kwa kuwalaumu walinda usalama wanaoshirikiana na wahalifu kisha kugawana mali ambazo wameiba.
      10. Selume na Meko wanatoa huduma za matibabu katika Kituo cha Afya cha Mwanzo Mpya/Ridhaa anawasaidia wagonjwa akiwa daktari
      11. Mhandisi Mwangeka anaenda ughaibuni kulikozuka vita ili kudumisha amani
      12. Lunga anapinga raia kuuziwa mahindi yalıyoharibika na viongozi.
      13. Lunga anawaelimisha raia kuhusu mbinu bora za kilimo, hivyo kuimarisha kilimo nchini mwake.
      14. Lunga akiwa shuleni anawahutubia walimu na wanafunzi wenzake na kukashifu uharibifu wa msitu.
      15. Kaizari anawahimiza wakimbizi wenzake kuchimba, misala ili kuzuia uchafuzi wa mazingira. na kuenea kwa magonjwa kama kipindupindu.
      16. Naomi anafungua kiafisi kidogo karibu na Chuo Kikuu cha Mbalamwezi anakowapigia wasomi kazi zao chapa na kuisarifu miswade yao.
      17. Dick anawahimiza nduguze kumsamehe mama yao, Naomi, licha ya kuwatoroka na kuhamia mjini akidai kwamba hakuna binadamu hata mmoja aliyekamilika.
      18. Wasomi katika Chuo Kikuu cha Mbalamwezi wanatoa ajira kwa Naomi kwa kumpelekea kazi zao kupiga chapa na kuisarifu miswada yao.
      19. Apondi na Mwangeka wanamlea Umu kama mwanao na kumsaidia kijiendeleza kimasomo hadi kiwango cha chuo kikuu.
      20. Ridhaa anaikubali ndoa kati ya mwanawe Mwangeka na Rachael Apondi licha ya koo zao kubaidika kama ardhi na mbingu, hivyo kutohoa hisia za kikabila.
      21. Ridhaa anawasaidia wanakijiji wanaoishi kwenye Msitu wa Heri, eneo ambalo ni jangwa kupata maji ya mabomba.
      22. Neema na Mwangemi wanamechukua Mwaliko na kumpanga, hivyo kumpa malezi alıyokosa.
      23. Pia wanamsomesha Mwaliko hadi kiwango cha uzamili katika taaluma. ya mawasiliano na kuhitimu na kuishia kuajiriwa kama mhariri katika Gazeti ya Tabora
      24. Mwalimu Dhahabu anawafunza wanafunzi katika shule ya Tangamano/ Mwalimu Meli anawafunza akina Tila
      25. Dick anapanua mawanda yake ya kibiashara kwa kuuza vifaa vya simu na kuyauzia mashirika yanayotoa huduma za mawasiliano.
      26. Bi. Tamasha, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Kilimo anamsaidia Chandachema kupata elimu na kumtafutia hifadhi
      27. Hazina anamsaidia Umu kwa kumpeleka kwenye makao ya Bi. Julida na kufungua ukurasa mpya wa maisha ya Umu-
      28. Baada ya kusomea shahada ya uzamili katika taaluma ya mawasiliano, Mwaliko anapata ajira kama mhariri katika magezeti ya Tabora,
      29. Wataalamu mbalimbali wanawasaidia wakimbizi pale kambini/ Ridhaa alipokea huduma za ushauri na uelekezaji /kuwahudumia Lime na Mwahaheri (zozote 20x1= 20)
    1. Aina za taswira.
      1. Taswira hisi - uyabisi wa moyo na malaika yakamsimama
      2. Taswira oni - akajiona anakabilina
      3. Taswira mguso - akachukuliwa danadana
      4. Taswira mwendo- atatanga na njia (3 x 1= 3)
    2. Vipengele vya kimtindo:
      1. Swali la balagha - ... akawaacha wanawe ?
      2. Tashihisi/ uhuishi/ uhaishaji - fikra kumwangusha Umu/ haki ilikojificha
      3. Nahau - piga darubini /tia kigegezi
      4. Msemo - pigana kwa jino na ukucha
      5. Chuku - fikra kutaka kumwangusha Umu.
      6. Tashbihi-Kama la ndugu zake (za kwanza 4x1=4)
    3.  
      1. Subira anapochoka kudhulumiwa na mavyaa wake kwa sababu ya tofauti zao za kijamii, anaivunja ndoa yake na kuhamia mjini Kisuka-
      2. Zohali anahama nyumbani kwao na kutorokea jijini baada ya masimango na udhalilishaji kutoka kwa wazazi wake kwa sababu ya mimba.
      3. Zohali akiwa jijini kama mtoto wa kurandaranda anakabili hali ya ukiwa na kuumbuliwa kwa kuvuta gundi.
      4. Zohali akiwa jijini, anakabiliana na wanaume wanaotaka kumnyanyasa kimapenzi kwa kupigana nao.
      5. Chandachema anaondoka kutoka kwa Satua anapomdhulumu na kuhamia katika Shirika la Chai La Tengenea
      6. Chandachema anapotaka kukijua kitovu chake mama yake Rehema ili aende huko, anaanza kukiulizia kutoka kwa majirani zake kama Katini
      7. Chandachema anapogundua kuwa Tenge anamsababishia dhiki za kisaikolojia kwa kuzini na makahaba machoni pake, anahama kwa Tenge na kuanza kulala katikati ya michai, kwa marafiki au wakati mwingine kwenye uchaga sokoni.
      8. Mwangeka na Apondi wanatatua tofauti za kiukoo katika jamii yao kwa kufunga ndoa licha ya kuwa koo zao zilikuwa zimebaidika kama ardhi na mbingu
      9. Licha ya Naomi kuwatoroka Umu, Dick na Mwaliko wakiwa wadogo, Umu anamua kumsamehe baada kuwapata wazazi wapya - Apondi na Mwangeka.
      10. Dick anajinasua kutoka kwenye biashara haramu ya kuuza mihadarati na kuanzisha biashara halali ya kuuza vifaa vya simu.
      11. Dick anakatiziwa masomo yake katika darasa la saba baada ya kutoroshwa na Sauna lakini baadaye anarudi shule anakojifunza Teknolojia ya Mawasiliano ya Simu.
      12. Raia wasiomudu gharama ya matibabu katika hospitali za kibinafsi na za umma wanatatuliwa tatizo hilo na Ridhaa kwa kuwajengea kituo cha Afya cha Mwanzo mpya.
      13. Selume anapokosa glavu za kuwazalishia wajawazito hospitalini anaamua kujinunulia glavu hizo licha ya kuwa alifanya kazi katika hospitali ya umma.
      14. Kipanga anaamua kuacha unywaji wa kangara iliyokuwa imewaua watu sabini baada ya ushauri nasaha katika Kituo cha Afya cha Mwanzo mpya.
      15. Selume anamfunza Tuama madhara ya tohara ya wanawake ili kumshawishi kuiacha.
      16. Mama Pete anapogundua kwamba mtafaruku umetokea katika ndoa yake kwa sababu ya Baba Pete kudai kuwa Pete si mwanawe kwa maana hawafanani, anampeleka Pete kwa nyanyake kulelewa huko.
      17. Pete anapokosa sodo za kutumia anapoingia mwezini, anatumia kanzu kuukuu kufidia upungufu huo.
      18. Pete anatafuta kazi ya kuuza pombe kwenye baa kujikimu kimaisha pamoja na wanawe ili kupata pesa
      19. Baada ya kugundua kwamba Sauna anashikwa na kisulisuli asubuhi, Mama Sauna anampeleka hospitalini anakopimwa na kubainika kuwa yu mjamzito".
      20. Baada ya Sauna kubakwa na kugundua kwamba Maya siye babake halisi, anatoroka nyumbani kwao na kwenda kufanya kazi ya uchimbaji mawe ili kujikimu kimaisha.
      21. Polisi wanapogundua kuwa Sauna na Bi. Kangara wanaiba watoto na kuwauza, wanawatia mbaroni - wanafungwa na kufanya kazi ngumu.
      22. Neema unapokosa kuzaa, anashauriana na mumewe Mwangemi, wanamchukua Mwaliko kutoka kituo cha watoto cha Benefactor kama mwanao wa kupanga
      23. Neema anapomkuta mtoto akiwa ametupwa kwenye jaa, anamwokota na kumpeleka kwenye kituo cha polisi.
      24. Baada ya wazazi wa Cynthia kufa, Neema anamchukua na kuanza kumtunza.
      25. Kimbaumbau anapotaka kumnyanyasa Naomi kimapenzi, kwa sababu amemuajiri kazi, Naomi anakataa.
      26. Wenyeji wa Msitu wa heri wana tatizo la maji kwa sababu eneo hili ni jangwa lakini Ridhaa anahakikisha kwamba kijiji kizima kina maji ya mabomba..
      27. Lucia anapambana na tofauti za kiukoo kwa kukubali kuolewa katika ukoo wa Waombwe licha ya kutoka katika ukoo wa Anyamvua, ukoo uliokuwa maadui sugu wa ukoo wa Waombwe.
      28. Viongozi wafisadi wanapotaka kuwauzia raia mahindi yalıyoharibika, Lunga anasimama kidete na kupinga hali hiyo licha ya kumsababisha kupigwa kalamu.
      29. Lunga anapotorokwa na mkewe Naomi, anamuajiri kijakazi Sauna kumsaidia kuwalea wanawe.
      30. Umu anapogundua kwamba nduguze wameibwa na Sauna anaenda hadi kituo cha polisi kupiga ripoti ili wamsaidie katika kuwatafuta.
      31. Hazina anaomba pesa wapitanjia kama Umu jijini Karaha ili kukabiliana na uhitaji wake wa pesa.
      32. Mama Kairu anaposhindwa kumlipia Kairu karo yote mara moja, anamrai mwalimu mkuu kumruhusu kulipa kidogo kidogo hadi mwisho wa mwaka. ( zozote 14 x 1)
        Swali la nne
  3.  
    1. Msemaji-Sara
      Msemewa- Asna
      Mahali- chumba cha Asna mjini
    2. Sababu-Sara anamweleza Asna jinsi Yona alivyoishia kujipata ulevini. (4x 1 = 4)
      1. Takriri/ urudiaji/uradidi -Ulevi.ulevi, kimya kimya
      2. Nidaa-Ulevi mwanangu!
      3. Uhuishi/ uhaishaji/tashihisi - Gongo liliyamega maadili,uwajibikaji umemponyoka
      4. Istiari/ jazanda - gongo –ulevi
      5. Tashbihi- kuteleza kama sabuni ya povu jingi
      6. Taswira mguso- kuteleza ( za kwanza 4 x 1 =4)
    3. sifa za Yona
      • Katili-anampiga Sara hadi anapoteza fahamu
      • Mwenye taasubi ya kiume- hakuwathamini wanawe kwa kuwa wasichana
      • Mwenye majigambi/majivuno- anajipiga kifua kuwa aliacha rekodi kubwa ya idara chuoni.
      • Mwenye majuto – anajuta kupuuza ugonjwa wa Sara
      • Mwenye bidii- alipokuwa mwalimu alifanya kazi yake kwa bidii
      • Mgomvi- Neema anasema kuwa alipenda kugombana na kulalamika.
      • Mlevi- anakuwa mraibu wa pombe hadi anafutwa kazi. ( za kwanza 4x1=4)
    4. Umuhimu wa mandhari-chumba cha Asna.
      1. kuchimza maudhui ya umaskini- Asna anaishi katika chumba kidogo.Anaketi kitandani huku sara ameketi kwenye stuli .
      2. Sifa za wahusika zinakuzwa katika mandhari hayakama vile Asna –ni mdaku, Bunju kama mkarimu/Sifa za Sara kama vile- kuwa mshauri zinakuzwa –anamshauri kuhusu ndoa.
      3. Athari za ulevi zinaonyeshwa hapa- Yona anafutwa kazi kutokana na ulevi.
      4. Tunafahamishwa sababu za Sara kuwa mgonjwa-vipigo vya mara kwa mara.
      5. Mbinu za kimtindo kama vile Mbinu rejeshi zimekuzwa.
      6. Katika mandhari haya tunafahamishwa kuwa Neema alikuwa hodari masomoni.
      7. kutambulisha wahusika kama vile Bunju – kuwa mkarimu.
      8. Kujenga dhamira ya mwandishi - kwa mfano, maisha ya mjini/ usasa
      9. kukuza ploti-katika mandhari haya tunafahamishwa kuwa Neema alipopata ajali aliokolewa na kutunzwa na Bunju aliyelipa hata ada yake ya hospitali.
      10. kukuza mgogoro – Bunju na Asna/ usasa na ukale/ Asna na Sara
      11. kuonyesha hali za kitabaka – jinsi Asna alivyoishi katika SQ na chumba chake kilivyokuwa kidogo (zozote 8x1=8)
  4. Tofauti za ukale na usasa
    1.  
      1. Elimu ya mtoto wa kike hapo awali haikudhaminiwa lakini sasa inadhaminiwa .Tunaona Sara hakuweza kukamilisha masomo yake alifika darasa la saba lakini Neema amesoma na kuhitimu ana digrii mbili.
      2. Wanawake wa awali walitegemea mifuko ya waume zao lakini siku hizi wanajitegemea kifedha .Neema anategemea mshahara wake kufanya mambo kadha.
      3. Michezo ya watoto zamani haikugharimu chochote.Leo lazima ilipiwe kama Bunju anavyosema.
      4. Mavuno ya kwanza hapo zamani yalionjwa na wazee ili kutoa baraka siku hizi hali hii haizingatiwi.
      5. Watoto wa zamani walilelewa vizuri katika utamaduni na lugha zao asili.Yona anasema kuwa wajukuu wake hata neno moja la lugha yao asili hawajui.
      6. Safari za zamani zilichosha kutokana na barabara bovu, siku hizi usafiri ni mwema kwa sababu barabara zimesakafiwa.
      7. Wanaume hawakuingia jikoni hapo awali sasa wanafanya hivyo tunaona Yona akitayarisha kiamsha kinywa.
      8. Wanawake wa awali waliozwa pindi tu walipobaleghe lakini sasa wanasoma na kujiamulia wakati wao.
      9. Nyimbo za siku hizi si kama za zamani. Watoto wa siku hizi lazima warukaruke .Bela anapoeleza sababu ya Lemi kufika nyumbani akiwa amechelewa.
      10. Zamani wazazi hawangeishi na watoto wao katika nyumba moja lakini sasa wapo wazazi wanaofanya hivyo.
      11. Wanawake wa zamani walidhamini kuwa wanene lakini wa siku hizi wanang’ang’ania kukonda-asemavyo Asna.
      12. Watoto wa kike zamani hawakuruhusiwa kwenda shuleni.Sasa wanakwenda.
      13. Watoto wa zamani waliadhibiwa kwa kiboko shuleni lakini siku hizi huwezi kumnyoosha mtoto kwa kiboko.
      14. Watu wa zamani walikutana wakala na kunywa pamoja hukuna wakibadilishana mawazo lakini siku hizi hawazingatii haya.
      15. Watoto wa kike zamani hawakurithi kitu. Wa sasa wanarithi ( za kwanza 10x 1=10)
    2. Adha za kuishi mjini;
      1. Ada ya juu ya nyumba –Asna anaishi katika servant quarter ingawaje chumba hiki ni kidogo ada yake iko sawa na nyumba ya viumba viwili katika mitaa mingine.
      2. Vyumba vidogo- Sara analinganisha chumba anachoishi Asna na kizimba cha kuku.
      3. Msongamano wa magari- kunaponyesha madereva mjini huingia kimuyemuye na kusababisha msongamano wa magari .Bunju anasema anataka awahi kabla ya msongamano.
      4. Magari ya usafiri ni mabovu –Bela anasema kuwa ni kebe la mabati.
      5. Wafanyakazi mjini kupoteza kazi zao-makampuni yanapopunguza idadi ya wafanyakazi.
      6. Wakazi wa mjini kuchukua mikopo ili kukidhi mahitaji yao- Bunju alichukua mkopo kwa benki kujengea nyumba.
      7. Shule za mjini ni za gharama ya juu-Mina anasomea shule ya bweni ambayo Bunju anahangaika kulipia karo.
      8. Ukosefu wa ajira- Asna amesoma hadi ana digrii lakini hajafanikiwa kupata ajira.
      9. Kuwepo na madeni- Bunju anasema kuwa ana madeni chungu nzima.
      10. Kukosa muda wa kuwa na watoto wao-Neema anakosa wakati wa kumpeleka Lemi out,Bunju vilevile ,hata wakati wa wikendi.
      11. Kupotea kwa nguvu za umeme-Aishipo Asna nguvu za umeme zinapotea.
      12. Wafanyakazi kujihusisha na kazi tofauti ili kuvuta riziki-Madaktari wa mjini wanatoka hospitali moja hadi nyingine ili kupata riziki zaidi. (zozote 10x1=10)

SEHEMU YA D-USHAIRI

  1.  
    1.  
      1. Kuwaonya wananchi dhidi ya kuwachagua wanasiasa wadanganyifu.
      2. Kuonyesha unafiki wa wanasiasa.
      3. Kukejeli viongozi wabinafsi.
      4. Kuwahimiza wananchi kufanya maamuzi ya busara wanapochagua viongozi. ( za kwanza 2x 1 =2)
    2.  
      • Ni vigeugeu-kama lubwi hugeuka
      • Wana maringo- ni kama tausi
      • Waongo- hutoa ahadi za uongo
      • Wasaliti- wanapopata uongozi husahau wananchi na kuwacheka.
      • Wenye vitisho- wanawatishia wananchi. (za kwanza 3x1=3)
    3.  
      1. Inksari- neleze-nieleze yalo- yaliyo yaso-yasiyo, ndu-ndugu, twahadawa- twahadaiwa
      2. Kuboronga sarufi- kama lubwi hugeuka-hugeuka kama lubwi,waoni tausi huiwa –wao huwa tausi
      3. Mazda-waahidini- waahidi, jifanyani- jifanya, yaniumizani- yaniumiza, twambiwani- twaambiwa
      4. Tabdila-zitaiza –zitaisha
      5. Lugha ya kale-Kaumu- watu (zozote 3x1=3)
    4. Nafsi neni- mwananchi aliyechoshwa na tabia za wanasiasa
      Mzindushi- anayewanzindua wananchi wenzake kuhusu viongozi laghai. (1x2=2)
    5.  
      1. Vipande- mathnawi-kila mshororo una vipande viwili (ukwapi na utao)
      2. Vina- ukaraguni –vina vinabadilika kutoka ubeti hadi mwingine.
        (Kutaja 1\2 kueleza ½=1)
    6.  
      1. Tashbihi-kama lubwi
      2. Sitiari-ngazini-uongozini
      3. takriri-watwambia (za kwanza2x1=2)
    7. Ndugu zangu tuzinduke ili tuondokee hila zao humu duniani wasije wakatula.tuwachague walio waadilifu na tusiongozwe na heka kwani wanasiasa wana hila nyingi,
    8. Toni ya kukejeli- mshairi anakejeli tabia za wanasiasa
      Toni ya kuonya – anawaonya wananchi dhidi ya kuchagua viongozi walaghai
      (yoyote 1x2=2)
  2.  
    1. Ni shairi huru- lina idadi tofauti ya mishororo katika beti zake.
      • Lina mishororo mishata ( kutaja 1, maelezo 1)
    2. Dalili za kukandamizwa-Kunyimwa uhuru wa kusema utakalo
      • Mtu kutatafuta ukweli
      • Mtu kutowakosoa wengine ilhali wao wanamkosoa
      • Mtu kutofanya uamuzi wake binafsi.
      • Mtu kuiga bila sababu
      • Mtu kufanywa kama bidhaa
      • Mtu anapoheshimu wengine kwa sababu ya walicho nacho
      • Mtu kulewa ili asahau dhiki zake. ( Za kwanza 4x 1 =4)
    3. mshororo usiojitosheleza kimaana
      Matumizi ya mishororo mishata;
      1. Na kushawishika ya kwamba…
      2. Unapoliona kosa…
        (maana 1, mfano, 1 =2)
    4. Mbinu za kifasihi katika shairi;
      1. Tashbihi - Ufanywe kama sanamu
      2. Takriri- Hu lolote hu chochote
      3. Msemo- uwaze uwazue, unapokata tamaa
      4. Uhuishi-mawazo yakurudie
        (zozote 3x1=3)
    5. Uhuru wa mshairi;
      1. Tabdila-usimkosowe-usimkosoe, zikulemele-zikulemee
      2. Inksari- mekandamizwa-umekandamizwa, ndu-ndugu
        (za kwanza 2x1=2)
    6. Nafsi neni katika shairi-mshauri,
      • mzindushi
        (zozote 1x2=2)
    7. Ubeti wa pili kwa lugha nathari;
      • Mtu anapoliona kosa /na kwa sababu ya hofu asiliseme/ lakini yeye anakosolewa na wengine /basi anafaa ajue amekandamizwa. (4x1=4)
    8. Matumizi ya usambamba ;
      • Unapoanza
      • unapofanywa
      • unapokata
      • unapoliona ( zozote 1x1=1)

sehemu E: Hadithi fupi

  1.  
    1.  
      1. Nafsi ya kwanza
        • Vidole vyangu vya miguuni..
        • Nikatamani tufike kwa jamaa ya baba yetu.....
        • Kututafuna kadri tulivyokazana...nk. (Nafsi-1, Mfano-1)
      2.  Umuhimu wa nafsi ya kwanza:
        1. Msimulizi humleta msomaji karibu na yeye/masafa baina ya msomaji na msimulizi yanaf upishwa.
        2. Msimulizi hudhihirisha hisia zake kwa wasomaji na kuwateka hisia zao
        3. Msimulizi huongezea kisa chake uhalisia ikilinganishwa na kama kisa kingesimuliwa kwa namna ya kuripotiwa
          (zozote 2x1=2)
      3. Mbinu za kimtindo;
        • Tashihisi/uhuishi (uhaishaji- Baridi ilizidi kututafuna/vipande vya theluji vikitupiga
        • Msemo/ Nahau - vilikufa ganzi/ilitutia moyo
        • Taswira - miili yetu iliathirika / tulihisi njaa na uchovu
        • Usimulizi - dondoo lote limesimuliwa
          (za Kwanza 2X1=2)
      4. Mamake msimulizi (Richman) kama kielelezo cha wanawake jasiri;
        • Mama Kazili anapoamua kuwapeleka wanawe Makongeni bila idhini ya mumewe na wakwe zake.
        • Licha ya mumewe kukosa kumtumia pesa kwa zaidi ya mwaka sasa, anajikaza kuwalea wanawe
        • Mama Kazili anatoa dukuduku lake la kutaka apewe nafasi ya Kuikimu familia yaka kwa ukoo wa Belo bila woga
        • Mama Kazili anamweleza Msimulizi waziwazi sababu za kuenda Makongeni baada ya Msimulizi kumuuliza.
        • Vilevile, alianza kufanya kazi kama mwalimu wa shule ya msingi bila ruhusa kutoka kwa mumewe wala ukoo wa Belo.
        •  Anaingiliana vyema na mama aliyemkopesha pesa za nauli ya gari ili kusafiri milimani
        • Aidha, alijibidisha kupanda milima ya Maloti licha baridi na utelezi kuwapeleka wanawe Makongeni wasife njaa
        •  Anamlenga Matweba usoni sawasawa na kumjibu licha ya Matweba kumkemea.
        • Licha ya kumpoteza mwanawe Mkhathini anaendelea na safari huku akiwa amembeba.
        • vilevile, alijua fika kuwa ukoo wa Belo ungem laumu kwa kusababisha kifo cha Mkhathini..
        • Mama Kazili anawaeleza jamaa ya mumewe kuwa yeye ni raia halali wa Lesotho kupitia kwa ndoa na hakuna yeyote anayeweza kumlazimisha kurudi Swaziland ikiwemo mumewe.
        • Anawaeleza wazee kuwa yuwajua Biblia namna mwanamke anapaswa kuwa mnyenyekevu na kuwa sheria za kijamii zinamchukulia mwanamke kama mtoto aliyepaswa kuwa chini ya utunzaji na uelekezi wa mwanaume.
        • Anaikashifu serikali kwa hila kwa kudai kwamba wamechaguliwa na wanawake.
        • Anasema kuwa kabla hajafa, apewe nafasi ya kuyaboresha maisha yake na yale ya mwanawe.
        • Anakataa kuomba msamaha kwa wazee wa ukoo wa kwa Belo kusema kuwa alimaanisha kile alichokisema.
          (zozote 7X 1=7)
    2. Uwajibikaji katika hadithi ‘Toba Kalia’
      1. Jack anawekeza pesa zake zote kwa ajili ya kujiendeleza kimasomo.
      2. Jack anawajibika anapowaunganishia wazazi wa Siri mitambo ili kuwasiliana na mwanao Siri kwa njia ya ‘skype’
      3. Licha ya kuhiniwa nafasi yake katika mashindano na Bwana Kalia, Jack anampa mkewe Kalia zawadi yake ya hundi za shilingi elfu kumi amhifadhie
      4.  Jack anajitengenezea kitanda na kuweka shati lake chini ya mto ili kunyooka .
      5.  Siri anaidhamini lugha ya kwao licha ya kuwa Uchina na hata amewafundisha Wachina wengi lugha ya kwao Kiswahili.
      6.  Siri akiwa Uchina kila mwezi, husoma riwaya mbili, tamthilia mbili na angalau diwani ya mashairi kila baada ya miezi miwili kuendeleza ugwiji wake katika lugha ya Kiswahili
      7.  Bi. Mshewa (Mamake Siri) anafundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Kayole.
      8.  Siri amewafundisha Wachina wengi Kiswahili
      9.  Wadhamini ambao ni wataalamu wa uhandisi kutoka Uchina wanachangia katika elimu kwa kutoa tuzo kila
        mwaka kwa shule za maeneo mbalimbali
      10. Bw. Kalia anakosa kuwajibika anaposhirikiana na Mkurungenzi wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia katika kubadilisha matokeo ya mashindano ya somo la Sayansi.
      11. Wazazi wa Siri hawakutimiza ahadi waliyotoa kwa wazazi wake Jack walipofariki katika ajali ya barabarani kwamba wangemtunza Jack hadi afikie kilele cha masomo yake.
      12. Wazazi wa Siri walikuwa na uwezo wa kumpeleka Jack chuo kikuu bila ufadhili wowote lakini Bw Kalia anampoka Jack aliyefiwa na wazazi
      13. Bi. Mshewa anakosa kuwajibika anapoona Jack anaanza kuimarika katika biashara yake na kumtaka awalipe nusu ya faida ya kila mwezi.
      14. Siri anawajibika anapozungumzia uovu waliomtendea Jack katika runinga ili dunia nzima ipate kujua.
      15. Siri anatoa mshahara wake wa mwaka kufadhili Masomo ya Jack ya chuo kikuu.
      16.  Jane Gatoni anawájibika anapompa Siri fursa ya kumpeperusha siri yake studioni.
      17.  Jack anawajibika katika biashara yake ya kuuza viatu na kuimarika.
      18.  Jack anawajibika anapowasamehe wote katika familia ya Bwana Kalia na kumshukuru Siri kwa kusema ukweli
      19. Bw. Kalia anakosa kuwajibika anapojaribu kumpigia simu Siri kumwonya asipasue mbarika na akatize mahojiano ya runinga.
        (xx) Jack anawajibika anapoiweka siri ya kutomwambia Bwana Kalia mpango wa Siri wa kutoa ujumbe muhimu kwa nchi nzima.
        (zozote 7x1= 7)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Nginda Girls Mock Examination 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?