Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Wahundura Boys Mock Examination 2023

Share via Whatsapp

MAAGIZO:

  • Jibu maswali MANNE pekee.
  • Swali la kwanza ni la LAZIMA.
  • Maswali hayo mengine MATATU yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani; Riwaya, Tamthilia, Ushairi na Fasihi Simulizi.
  • USIJIBU maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Majibu yote LAZIMA yaandikwe kwa lugha ya KISWAHILI.
  • Karatasi hii ina kurasa 7 zilizopigwa chapwa.
  • Watahiniwa ni lazima wahakikishe kwamba kurasa zote za karatasi hii zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.


MASWALI

SEHEMU YA A: Mapambazuko Ya Machweo Na Hadithi Nyingine- Clara Momanyi

SWALI LA LAZIMA

  1. “Mike! Mike! Mike! Njoo! Nilijua utafanya vyema mwanangu…”
    1. Tambua na ueleze toni ya dondoo hili. (alama 2)
    2. Changanua mtindo katika dondoo hili. (alama 2)
    3. Eleza sifa nne za msemaji wa dondoo hili. (alama 4)
    4. Eleza mbinu mbili ulizozitumia kutambua sifa za msemaji wa dondoo hili. (alama 4)
    5. Tambua na ufafanue madhila yanayomsakama mhusika mkuu katika hadithi hii ya “Sabina”. (alama 8)

SEHEMU YA B: RIWAYA
Chozi La Heri-Assumpta K. Matei
Jibu swali la 2 au 3

  1. “Ndivyo tunavyoishi…na usidhani ni kuishi huku…ni kupapatika, kufufurishwa na matumbwe ya maisha…pole ndugu, itabidi usahau mswala kwa hii mbacha.”
    1.  Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Andika mifano mitatu ya sitiari katika dondoo hili. (alama 3)
    3.  Fafanua umuhimu wa anayeambiwa maneno haya katika kuijenga riwaya hii. (alama 3)
    4. Kwa kurejelea hoja kumi za yule anayezungumza, onyesha jinsi raia wa Wahafidhina wanavyopapatika na kufufurishwa na matumbawe ya maisha. ( alama 10)
      AU
  2. . “Lakini…
    Wewe hushangai?
    Kwani wanawashwa
    Na pilipili iliyo
    Kwenye uchango wa mwingine?
    Kwani wasitake kukuli
    Kilichotufanya mimi na wewe
    Kuwa marafiki wa kufa kuzikana?”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Tambua mbinu mbili za kimtindo katika dondoo hili (alama 2)
    3. Eleza sifa nne za msemaji wa maneno haya. (alama 4)
    4. Jadili vyanzo na athari za matumizi mabaya ya vileo na dawa za kulevya kwa mujibu wa diwani ya Chozi la Heri huku ukitolea mifano mwafaka. (alama 10)

SEHEMU YA C: TAMTHILIA
Bembea ya Maisha- Timothy Arege
Jibu swali la 4 au 5

  1. .“…anachukua vidonge vyake na kuvimeza kabla ya kuketi kwenye kochi mpya.”
    1. Weka dondoo hili katika muktadha wake. (alama 4)
    2. Tambua aina za taswira katika dondoo hili. (alama 2)
    3. Eleza umuhimu wa mandhari ya dondoo hili. (alama 4)
    4. Eleza nafasi ya mwanamke ukijikita katika utamaduni wa jamii ya “Bembea ya Maisha”. (alama 10)
      AU
  2.  “ Wakati mwingine maisha haya hukufanya kijisikia kama abiria kwenye gari liendalo kwa kasi. Unatamani dereva apunguze mwendo lakini unakumbuka kuwa safari bado ni ndefu na hutaki kufika ukiwa umechelewa. Basi unatulia japo ndani una wasiwasi, hutulii. Lakini huwezi kushuka maana safari itaganda. Kwa hivyo, unajitahidi tena, japo wakati mwingine unajikuta umetambaliwa na uchovu, shaka na tuhuma.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Changanua mtindo katika dondoo hili. (alama4)
    3. Dhihirisha umuhimu wa mzungumziwa wa maneno haya katika kuijenga tamthilia ya “Bembea ya Maisha”. (alama 6)
    4. Eleza namna maisha yanamfanya mzungumzaji “kujisikia kama abiria kwenye gari liendalo kwa kasi”.(alama 6)

SEHEMU YA D: USHAIRI

Jibu swali la 6 au 7

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
    Jama, Jama, Jamani
    Mbona twabebeshwa mateso hivi
    Mizigo mikubwa ya dhiki kama
    Kwamba hatuna haki ya kusema
    Kukataa ndoa za lazima
    Kukataa kuozwa wazee
    Kukataa kukatishwa masomo
    Kukataa tohara ya lazima

    Jama, Jama Jamani
    Iweje tuteswe mateso haya
    Na watu wasio kuwa hata na haya kama
    Kwamba hatuna haki ya kulalamika
    Kulalamikia kutumikishwa kama mayaya
    Kulalamikia kudhalilishwa kiunyama
    Kulalamikia kutolindwa na sheria

    Jama, Jama, Jamani
    Sasa hii ni awamu nyingine
    Na macho tumeyafungua kabisa
    Tumekataa kudhalilishwa kabisa
    Tumekataa kuteswa kama watumwa
    Tumekataa tohara ya lazima
    Tumekataa kuozwa....... Tumekataa! Tumekataa
    Hii awamu ya ’Haki ya mtoto wa kike’

    Maswali
    1. Taja mambo matatu muhimu yaliyozungumziwa na mshairi kisha ueleze kila moja . (alama 6)
    2. Eleza muundo wa shairi hili (alama 4)
    3. Taja mbinu mbili za lugha alizotumia mshairi kisha ueleze kila moja (alama 4)
    4. Kwa nini mshairi huyu anasema hii ni ’awamu’ nyingine? (alama 3)
    5. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa na mshairi (alama 3)
      1. awamu
      2. kudhalilishwa
      3. Dhiki
        AU
  2. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali yafuatayo
    1. Mkata ni mkatika, harithi hatoridhiwa
      Sina ninalolishika, wala ninalochukuwa
      Mlimwengu kanipoka, hata tone la muruwa!
      Mrithi nini wanangu?
    2. Sina ngo’mbe sina mbuzi, sina konde sina buwa
      Sina hata makaazi, mupasayo kuyajuwa
      Sina mazuri makuzi, jinsi nilivyoachwa
      Mrithi nini wanangu?
    3. Sina kazi sina bazi, ila wingi wa shakawa
      Sina chembe ya majazi, mno nikukamuliwa
      Nakwa’cheni upagazi, ngumu kwenu ku’tuwa
      Mrithi nini wanangu?
    4. Sina sikuachi jina, mkata hatasifiwa
      Hata nifanye la mana, mno mi kulaumiwa
      Poleni wangu sana, sana kwenu cha kutowa
      Mrithi nini wanangu?
    5. Sina leo sina jana, sina kesho kutwaliwa
      Sina zizi sina shina, wala tawi kuchipuwa
      Sina wanangu mi sina , sana la kuacha kuraduwa
      Mrithi nini wanangu?
    6. Sina utu sina haki, mila yangu meuliwa
      Nyuma yangu ili dhiki, na mbele imekaliwa
      N’nawana na miliki, hadi nitakapofukiwa
      Mrithi nini wanangu?
    7. Sina ila kesho kwenu, wenyewe kuiongowa
      Muwane kwa nyinyi mbinu, mwende pasi kupumuwa
      Leo siyo kesho yenu, kama mutajikamuwa
      Mrithi nini wananngu?
      1. Taja mambo yoyote mawili ambayo mtunzi angewarithisha wanawe. (alama 2)
      2. Eleza sababu ya mtunzi kutoweza kuwarithisha wanawe. (alama 3)
      3. Andika ubeti wa nne kwa lugha nathari. (alama 4)
      4. Dondoa mifano miwili miwili ya : (alama 2)
        1. Inkisari
        2. Tabdila
      5. Chambua shairi hili kwa upande wa :
        1. Dhamira (alama2)
        2. Muundo (alama 4)
      6. Eleza maana ya vifungu vifuatavyo kama vilivyotumiwa katika shairi. (alama 3)
        1. Mlimwengu kanipoka
        2. Sina konde sina buwa.
        3. Wingi wa shakawa.

SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI

  1. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali.
    Malaika
    Nakupenda malaika x2
    Ningekuoa malaika...
    Ningekuoa dada...
    Nashindwa na mali sina wee...
    Ningekuoa malaika x2
    Pesa, zasumbua roho yangu x2
    Nami niafanyeje, kijana mwenzio
    Nashindwa na mali sina wee...
    Ningekuoa malaika x2
    1. Ainisha wimbo huu kwa kuzingatia kipengele cha maudhui. (alama 2)
    2. Andika sifa mbili za jamii inayosawiriwa na wimbo huu. (alama 2)
    3. Eleza mikakati sita ambayo mwimbaji angetumia kufanikisha uwasilishaji wa wimbo huu. (alama 6)
    4. Unanuia kutumia mahojiano kukusanya habari kuhusu nyimbo za aina hii.
      1. Eleza manufaa matano ya kutumia mbinu hii. (alama 5)
      2. Eleza changamoto tano za kutumia mbinu hii. (alama 5)


Mwongozo

Swali la 1
Mapambazuko ya machweo:Sabina-Winnie Nyaruri Ogenche

“Mike! Mike! Mike! Njoo! Nilijua utafanya vyema mwanangu…”

  1. Tambua na ueleze toni ya dondoo hili. (al 2)
    • Toni ya furaha- Ombati anamwita mwanawe Mike kushangilia matokeo ya mtihani akidhani ni yake.
  2. Changanua mtindo katika dondoo hili. (al 2)
    • Nidaa- mike!
    • Mdokezo-mwanangu…
  3. Eleza sifa nne za msemaji wa dondoo hili. (al 4)
    • Ni mwenye tamaa. Ananuia kujinufaisha kutoka kwa dadake kupitia kwa mahari yake. Anapoyakosa, anaamua kutumia bintiye, Sabina, kwa kumwoza baada ya darasa la nane ili kupata mifugo.
    • Ni mtamaduni. Anaendeleza mifumo ya kijamii kama vile ubidhaaishaji wa wanawake. Anataka kupata mahari kupitia kwa Nyaboke na anapoyakosa, anaamua kumwoza bintiye, Sabina, katika umri mchanga na kumwandalia sherehe. Anasemekana kumlaani Nyaboke kwa kumkosesha mahari.
    • Ni kigeugeu. Maripota wanapofika kumhoji Sabina, anaungana naye huku akijisifia jinsi alivyomlea na alivyo mwerevu, licha ya kuwa awali anamtelekeza. Anawafukuza waliokuja kumposa Sabina na mifugo wao.
    • Ni mwongo/mzandiki/mnafiki. Anamhadaa mwalimu mkuu kuwa Sabina anapata muda wa kutosha kujiandaa kwa ajili ya mtihani. Anadanganya kuwa Sabina anapenda kazi za shambani hali analazimishwa.
    •  Msaliti- anaisaliti jamaa yake kwa kumwacha Yunuke kumtesa mwana wa dadake Nyaboke.
    • Mbaguzi- anabagua kati ya wana wake na mtoto wa dadake Sabina. Sabina anatumikizwa huku wanawe wakikaa starehe.
      Za kwanza 4x1=4
  4. Eleza mbinu mbili ulizozitumia kutambua sifa za msemaji wa dondoo hili. (al 4)
    Usawiri wa mwandishi
    Maneno ya wahusika wengine
    Maneno yake mwenyewe
    Matendo yake kwa wahusika wengine
  5. Tambua na ufafanue madhila yanayomsakama mhusika mkuu katika hadithi hii ya “Sabina”. (al 8)
    • Kufiwa na mamake Nyaboke na kuachwa mikononi mwa babu na nyaya yake.
    • Babu na nyanyake kufariki akiwa darasa la tano. Hili linamfanya achukuliwe na mjaombake Ombati na Yunuke.
    • Alitumikizwa sana nyumbani kwa mjombake ambako alifanya kazi za kila nui.
    • Anapokea kichapo kutoka kwa Yunuke baada ya kuchelewa kutoka shuleni.
    • Anatusiwa sana Yunuke. Anaitwa baradhuli, kiokote,mjalaana n.k.
    • Kusingiziwa. Subira anasingiziwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume Fulani.
    • Kubaguliwa. Binamu zake wanasomea shule za bweni huku yeye akisomea shule ya kutwa.
    • Kunyimwa nafasi ya kudurusu. Yunuke anazima kibatiri hivyo kumnyima Sabina nafasi ya kumalizia kusoma alichokuwa amebakisha.
    • Kuozwa.mjombake Ombati anapanga kumuoza kwa kijana mwendesha pikipiki hivyo kuzima ndoto yake ya kuemdelea na masomo.
    • Kupuuzwa- yunuke na Ombati waliziona juhudi zake masomoni kama za bure.
    • Kukosa malezi ya wazazi wote. Babake anamringa mimba mamake Nyaboke na kumtoroka.

Swali la 2

“Ndivyo tunavyoishi…na usidhani ni kuishi huku…ni kupapatika, kufufurishwa na matumbwe ya maisha…pole ndugu, itabidi usahau mswala kwa hii mbacha.”

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (al 4)
    Msemaji- kaizari akirejelea mawazo ya Makiwa
    Msemewa- Ridhaa
    Mahali- Msitu wa Mamba
    Wakati- anasimulia alivyoanza kutumia misala/ vyoo vya kupeperushwa kwa kutumia sandarasi baada ya kujuzwa na Makiwa.
    4x1=4
  2. Andika mifano mitatu ya sitiari katika dondoo hili. (al 3)
    Matumbawe ya maisha- maisha ngumu
    Mswala- ya zamani- vyoo alivyozoea kutumia
    Mbacha- mkeka mkuu- vyoo vya kupeperushwa
    Za kwanza 3x1=3
  3. Fafanua umuhimu wa anayeambiwa maneno haya katika kuijenga riwaya hii. (al 3)
    Huyu ni Ridhaa
    • Ni kielelezo cha viongozi waliowajibika kwani anawachimbia wanakijiji wenzake mabomba ya maji. Hata baada ya kutawazwa kwa kiongozi na kuzuka kwa ghasia, anaenda kumhudumia mgonjwa aliyeumia.
    • Ni mhimili mkuu wa mshikamano wa jamii. Anawasaidia wapwa wa Mzee Kedi.
    • Kupitia kwake mwandishi amekuza maudhui ya mapenzi, ndoa, malezi na mengine mengi.
    • Anaonyesha athari za kutokuwa na uthabiti wa kisiasa. Wanaishia kambini ambako wanang’ang’ania chakula na kukosa huduma za msingi.
    • Ni mojawapo ya wahusika wanaojenga ploti ya riwaya. Anasimulia kisa cha kupoteza majumba yake mawili, kuchomeka kwa ndugu yake Makaa na kuangamia kwa familia yake.
    • Anaendeleza sifa za wahusika. Kupitia kwake tunaona ucheshi wa Terry na ukakamavu wa Tila.
      (mwalimu aangazie hoja zingine sahihi za mwanafunzi)
      Zozote 3x1=3
  4. Kwa kurejelea hoja kumi za yule anayezungumza, onyesha jinsi raia wa Wahafidhina wanavyopapatika na kufufurishwa na matumbawe ya maisha. (10)
    *Kupapatika ni kuhangaika.
    • Wanalazimika kuwa wakimbizi katika nchi yao kutokana na vita vya kisiasa. Ridhaa na Kaizari ni wakimbizi katika Msitu wa Mamba.
    • Kule kambini, nyumba zao ni duni, mvua inaponyesha,wananyeshewa k.m. Kaizari anaeleza jinsi matone yanawaangukia wanawe Lime na Mwanaheri.
    • Wanakosa chakula na maji safi ya kunywa kule kambini-Kaizari ala mizizi mwitu.
    • Tunaelezwa kuw baadhi waliugua maradhi kama vile homa ya matumbo.
    • Kuna vifo- tunaelezwa kuwa roho za vitoto zilikuwa zinabwakurwa na magarimoshi wanapoenda haja katika reli.
    • Wanakumbwa na umasikini. Uhitaji wa watu unawafanya kununuliwa kwa vihela vya kushikilia uhai.
    • Mashamba yao yananyakuliwa kule vijijini na wakubwa.-shamsi-mabavu
    • Wanakosa kazi baada ya kuhitimu chuoni n ahata kulaghaiwa na wanasiasa.
    • Wanakosa misaada ya serikali- Hazina ya Jitegemee imejawa na ukabila na unasaba.
    • Wanapitishwa dhiki za kisaikolojia. Mabinti zake Kaizari wanabakwa na mkewe Subira anapigwa na wale mabarobaro.
    • Familia zinavurugika kutokana na tofauti za kisiasa. Selume anaondoka kwake kwa sababu ya kuhitilafiana na wakwe zake kisiasa kwa kumuunga mkono Mwekevu.
    • Wanapoteza mali zao katika harakati za kuhama makwao. Tunaelezwa kuwa mifugo na majumba yaliteketezwa.
      Za kwanza 10x1=10

Swali la 3

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (al 4)
    Msemaji-Shamshi
    Msemewa- chupa yake
    Mahali-Alikuwa njiani akielekea kwake Kazikeni
    Wakati- alikuwa akitoa dukuduku lake kwa mabwanyenye wa mtaa wa Afueni
    4x1=4
  2. Tambua mbinu mbili za kimtindo katika dondoo hili (al 2)
    Balagha-kuzikana?
    Methali- kuwashwa na pilipili iliyo kwenye uchago wa mwingine.
    Msemo- marafiki wa kufa kuzikana
    Ritifaa- chupa
    2x1=2
  3. Eleza sifa nne za msemaji wa maneno haya. (al 4)
    sifa za shamshi
    • Mwenye dharau – anapita akiimba usiku bila kujali kwamba wimbo wake unawasumbua waliolala.
    • mwenye bidii – amesoma hadi chuo kikuu kwa lengo la kumtoa baba yake kwenye umaskini
    • Mwenye kukata tamaa – badala ya kukabiliana na hali mbaya ya kukosa kazi, anaingilia matumizi mabaya ya pombe na kujidhalilisha
    • Mwenye kujigamba – anajisifu kwa kuwa wa kwanza kupata shahada
    • Mtetezi wa haki – yeye na wenzake wanalalamikia mishahara duni
    • Mwenye kulaani – anawalaani waliomsababishia umaskini
    • Ana machungu – analalamikia hali yake ya umaskini kama inavyoashiriwa na wimbo wake ambao una toni ya mbolezi
    • Amekosa kuwajibika – unywaji wa pombe kupindukia unamlazimisha mkewe kumwandama siku ya mshahara ili ajichukulie pesa za matumizi (za kwanza 4x1=4)
  4. Jadili vyanzo na athari za matumizi mabaya ya vileo na dawa za kulevya kwa mujibu wa diwani ya Chozi la Heri huku ukitolea mifano mwafaka.
    • Subira alianza kutumia vileo baada ya kuondoka nyumbani kutokana na kukejeliwa kusimangwa na kukataliwa na mavyaa wake.
    • Subira anaaga dunia na kumwacha Kiazari na uchungu na watoto wake, Lime na Mwanaheri bila mama.
    •  Baada ya Pete kuachwa na Nyangumi anaajiriwa kuuza pombe
    • Pete Anabakwa na mlevi mmoja nishai zikiwa zimemlemea
    • Dick anapouzwa kwa Buda analazimishwa kulagua dawa za kulevya.Wakati mwingine inambidi azimeze na kwenda kuzitapika ughaibuni. Kitendo hiki kinamfanya aanze kuzitumia.
    • Kwa sabau ya hali duni ya maisha vyuoni wanafunzi wanaanza kutumia vileo. Wanaishia kuiaga dunia.
    • Tabia ya Bwana Kero ya kunywa dengelua inafanya kupigwa kalamu na kumfanya kuachwa na bibiye na kuishia kuaga dunia.
    • Kutokana na umaskini, Hazina na watoto wengine ombamba wanatumia gundi
    • Shamsi anaanza kunywa pombe kukabiliana na ulitima na ukosefu wa kazi unaompangaza kwa ndoto zake za ujana kuzima.
    • Buda anaanza bishara ya ulaguzi wa dawa za kulevya kwa sababu ya tamaa za pesa. Anawaingiza vijana kama dick katika biashara hiyo.
    • Umaskini unawafanya wanajamii hawa kujiingiza katika vileo ambavyo vinawafanya kupofuka na kufa
    • Kipanga anapokanwa na babake anaingilia ulevi.
      ( zozote 10 x 1)

Swali la 4

.“…anachukua vidonge vyake na kuvimeza kabla ya kuketi kwenye kochi mpya.”

  1. Weka dondoo hili katika muktadha wake. (al 4)
    Msemaji-mwandishi
    Mrejelewa-Sara
    Mahali- nyumbani kwa Sara
    Wakati- sara ana maradhi kwa hivyo anameza vidonge
  2. Tambua aina ya taswira katika dondoo hili. (al 2)
    Taswira oni- jinsi abachukua vidonge
  3. Eleza umuhimu wa mandhari ya dondoo hili. (al 4)
    Haya ni mandhari ya nyumbani kwa Sara ambayo yanadhihirisha yafuatayo:
    • Malezi-sara anawalea wanawe vyema
    • Mapenzi- sara anampenda Yona
    •  Migogoro- kuna mtafaruku kati ya Yona na Sara.
    • Sifa za Yona kama mlevi, mvivu na mbabedume zinakuzwa.
    • Tunatanguliziwa mhusika Dina kama rafiki wa dhati wa Sara.
    • Utamaduni- Sara anaamini kuwa fimbo ya mzee hurithishwa mtoto wa kwanza.
      Zozote 4x1=4
  4. Eleza nafasi ya mwanamke ukijikita katika utamaduni wa jamii ya “Bembea ya Maisha”. (al 10)
    • Mshichana lazima aolewe. Msichana anafaa kuolewa baada ya kutimiza umri wa kubaleghe.
    • Msichana apewi nafasi ya kupata elimu. Kizazi cha jana hakikudhamini elimu ya mwanamke. Sara anasema elimu kwa mtoto wa kike ilikuwa bezo.
    • Mwanamke anafaa kutii mumewe. Ni utamaduni kwa mke kutunza mumewe. Sara anapoenda mjini, Yona anakosa wa kumtunza.
    • Mke anafaa kuwa mvumilivu kwenye ndoa. Sara anasalia kwenye ndoa yake licha ya madhila aliyopitia.
    • Mwanamke anafaa kuongozwa na mume. Bunju anasema kuwa yeye ni kichwa naye Neema awe shingo.
    •  Zamani mabinti walienda unyagoni na kufunzwa jinsi ya kutunza familiazao na waume zao. Sara alieleza haya.
    • Utamaduni ulikandamiza msichana. Utamaduni wa jadi haukumruhusu mtoto wa kike kwenda shule. Sara anaeleza kuwa hakupata nafasi ya kusoma.
    •  Mwanamke anawekewa laana sisizo na misingi yeyote. Sara anaenda kulala kwa Asna licha ya chumba chake kuwa kidogo.
      Zozote 5x2=10

Swali la 5

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (al 4)
    Msemaji- Neema
    Msemewa-Bunju
    Mahali- sebuleni mwao
    Wakati- hii ni baada ya Buju kumdokezea kuwa hawezi kumsaidia na hela za kumtibu mamake na jinsi ni laana kukaa na wakwe kwa nyumba moja.
    4x1=4
  2. Changanua mtindo katika dondoo hili. (al 4)
    Tashbihi- kijisikia kama abiria kwenye gari liendalo kwa kasi.
    Jazanda/ istiara- safari bado ndefu-maisha bado ni marefu na yana mengi
    Tashihisi-umetambaliwa na uchovu, shaka na tuhuma
    2x2=4
  3. Dhihirisha umuhimu wa mzungumziwa wa maneno haya katika kuijenga tamthilia ya “Bembea ya Maisha”. (al 6)
    Huyu ni Bunju
    • Anaendeleza migogoro katika ndoa. Anatofautiana na mkewe kuhusiana na malezi ya mwana wao Lemi. Anasema mume hafai kutumwa na mkewe.
    •  Anadhihirisha sifa za mkewe Neema kama mkarimu kwa kuwa alitumia mshahara wake kumlipia dadake Asna karo chuoni na kuishi pamoja na Salome kwao nyumbani.
    • Anaendeleza ploti-kupitia mbinu rejeshi, anadokeza alivyompata Neema akiwa mahututi.
    • Anakuza maudhui ya elimu. Anawalipia wanawe karo. Anamlipia shemeji yake Salome karo pia.
    • Anawakilisha wanaume ambao ni wawajibikaji kwani anamjengea babake nyumba, kuwapa chakula, mavazi, kulipia wanawe karo na kumnunulia mkewe gari.
    • Ni kielelezo cha watu watamaduni kwani anadai kuwa mama mkwe hafai kulala kwake kwani ati ni laana.
    • Anatumiwa kuonyesha uhuru ulioko katika ndo za kisasa. Anamruhusu mkewe kutumia mshahara wake apendavyo.
    • Anawakilisha wanaume wababedume. Anaona yeye ni mwanaume na ndiye kichwa cha familia, anastahili heshima, hastahili kupewa majukumu na mkewe kama kumtembeza mtoto wao Lemi.
      6x1=6
  4. Eleza namna maisha yanamfanya mzungumzaji “kujisikia kama abiria kwenye gari liendalo kwa kasi”.
    • Mamake Sara ana amaradhi ya moyo.
    • Hana hela za kutosha kumtibu mamake Sara, anamuomba mumewe usaidizi.
    • Ana kazi nyingi kule kazini-anasema kazi hizo ni kama safari ya ahera.
    • Anakosa muda wa kumlea mwanawe Lemi. Malezi amemuachia yaya Bela.
    • Anakosa muda wa kumpeleka mwanawe matembezini.
    • Wana mivutano katika ndoa na mumewe kuhusu malezi, mila na majukumu.
    • Ana wajibu wa kushughulikia wazazi wake –kuwaajiria wafanyakazi.
      Zozote 6x1=6

Swali la 6

  1. Mambo matatu muhimu yaliyozungumziwa na mshairi na maelezo ya kila moja.
    1. Mateso
      • Mizigo mikubwa ya dhiki
      • Hakuna haki ya kunena
    2. Ndoa ya lazima
      • Kuozwa kwa wazee
      • Kukatishiwa masomo
    3. Tohara
      • Tohara ya lazima
      • Hawaruhusiwi kusema chochote
    4. Sheria
      • Haiwalindi
      • Kudhalilishwa kinyama
    5. Awamu tofauti
      • Wamekataa kudharauliwa
      • Wamekataa kuteswa
      • Wamekataa tohara za lazima.
        Kutaja alama 1
        Kueleza alama 1
        Jumla alama 6
  2. Muundo wa shairi
    1. Ni wimbo ambao haufuati muundo wowote wa ushairi
    2. Ni shairi huru
    3. Halina mpangilio wowote wa kiarudhi
    4. Halina mgao wa mishororo
    5. Halina vina wala mizani
    6. Halina kibwagizo
    7. Lina beti 3
    8. Mishororo si sawa katoka kila ubeti
  3. Mbinu mbili za lugha alizotumia mshairi. Maelezo ya kila moja
    1. Nyimbo-Amezitumia Kwa njia mwafaka ili anase hisia za wasomaji.
    2. Takriri-Amejaribu pia kusisitiza ili kuwekea uzito yale anayozungumzia.
      • Anataka msomaji apate mvuto mzuri kwa lile analolizungumzia. Mfano tumekataa kudhalilishwa, tumekataa kuteswa, tumekataa tohara.
    3. Mdokezo. Mfano Tumekataa kuozwa ...
    4. Tashbihi . mfano ubeti wa pili- Kutumikishwa kama yaya
  4. Sababu za mshairi kusema; ‘hii ni awamu nyingine’
    1. Ulikuwa ukurasa mpya wa maisha.
    2. Kuna mabadiliko ya kuondoa ukandamizaji.
    3. Wanawake wamekataa kuozwa kwa lazima.
    4. Wamekataa kudhalilishwa kabisa
  5. Maana ya maneno
    1. awamu-Kipindi
    2. kudhalilishwa-kukandamizwa/ kudunishwa / kufedheheshwa
    3. dhiki-shida

swali la 7

  1.  
    • Makazi mabovu
    • Upagazi
    • Kutothaminiwa
    •  Dhiki
    •  Kufanya kesho ya wengine nzuri
  2.  
    • Ni maskini hohehahe / hana kitu
    • Aliporwa kila kitu.
    •  Hana mifugo.
    • Hana kazi yoyote.
    • Hana sifa / umaarufu.
    • Ana makazi mabovu.
  3.  
    • Sina jina nitakawacha kwani maskini hasifiwi
    •  Hata nikifanya jambo la maana ninalaumiwa tu.
    • Poleni sana wanangu kwa kuwa sina la kuwatolea.
    • Mtarithi nini wanangu?
  4.  
    1.  Inkisari
      • Mana – Maana
      • Meuliwa – Imeuliwa
      • Nitapofukiwa – Nitakapofukiwa.
    2. Tabdila
      • Muruwa - Murua
      • Kutowa -Kutoa
      • Kuchipuwa -Kuchipua
      • Kuiongowa - Kuiongoa
      • Kupumuwa - Kupumua
  5.  
    1. Dhamira
      • Kuwahimiza watu kufanya bidii wakiwa vijana
      •  Kulalamika kwamba maskini hana haki / huonewa / hapewi nafasi.
    2. Muundo
      • Shairi ni aina ya tarbia / unne.Lina mishororo minne katika kila ubeti.
      • Mishororo ya kwanza mitatu imegawika katika sehemu mbili (ukwapi na utao).
      • Kila kipande kina mizani nane na kila mshororo una mizani kumi na sita.
      • Vina vya kati vinatofautiana kutoka ubeti mmoja hadi mwingine, lakini vina vya mwisho ni sawa katika shairi zima katika mishororo ya kwanza mitatu.
      • Shairi hili lina kibwagizo ambacho kimefupishwa.
        Mrithi nini wanangu?
      • Shairi hili lina beti saba.
  6.  
    1. Mlimwengu kunipoka - Mlimwengu kanipokonya.
    2. Sina konde sina buwa - Sina shamba sina chochote.
    3. Wingi wa shakawa – mashaka mengi

Swali la 8

FASIHI SIMULIZI

  1. Ainisha wimbo huu kwa kuzingatia kipengele cha maudhui. (al 2)
    Wimbo wa mapenzi
  2. Andika sifa mbili za jamii inayosawiriwa na wimbo huu. (al 2)
    • Kuna ushirika wa ndoa
    • katika ndoa wanaume hulipa mahali
  3. Eleza mikakati sita ambayo mwimbaji angetumia kufanikisha uwasilishaji wa wimbo huu. (al 6)
    • Kutumia sauti inayosikika
    • Kutumia miondoko ya mwili na ishara zingine
    • Kutumia ala za muziki kama gitaa.
    • Kuhusisha hadhira katika uimbaji.
    • Kubadilisha toni ya uwasilishaji.
      Za kwanza 6x1=6
  4. Unanuia kutumia mahojiano kukusanya habari kuhusu nyimbo za aina hii.
    1. Eleza manufaa matano ya kutumia mbinu hii. (al 5)
      • Hupata habari za kina
      • Sifa za uwasilishaji kama vile toni, ishara za uso na kiimbo hubainika kwa mtafiti.
      • Mtafiti anaweza kurekodi majibu ya mhojiwa au kuyaandika.
      • Mtafiti anaweza kubadilisha maswali kulingana na kiwango cha mhojiwa.
      • Ni rahisi kung’amua wakati unapewa habari ambazo si za kweli.
      • Mhojiwa anaweza kumfafanulia mhojiwa maswali.
        Za kwanza 5x1=5
    2. Eleza changamoto tano za kutumia mbinu hii. (al 5)
      • Mbinu hii huhitaji stadi za mawasiliano za juu zaidi.
      • Urasmi kutokana na na vikao vya mahojiano huenda ukakatiza mawasiliano kati ya mhoji na mhojiwa.
      • Ukosefu wa muda wa kutosha wa mahojiano
      • Mhojiwa huenda asimwamini mtafiti.
      • Kiwango cha mtafiti cha elimu huenda kikawahofisha wahojiwa.
      • Wahojiwa wengine huenda wakampa mtafiti habari za uongo.
        Za kwanza 5x1=5
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Wahundura Boys Mock Examination 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?