Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Royal Exam Series Post Mock Trial Exams 2022

Share via Whatsapp

KISWAHILI
KARATASI YA 2
MATUMIZI YA LUGHA

MAAGIZO

 • Andika jina lako na namba yako ya usajili katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
 • Tia sahihi yako kisha uandike tarehe ya mtihani katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
 • Jibu maswali yote.
 • Majibu yote yaandikwe kwenye nafasi ulizoachiwa katika kijitabu hiki cha maswali.
 • Majibu yote ni lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
 • Usitoe ukurasa wowote kutoka kwenye kijitabu hiki.
 • Karatasi hii ina kurasa 10 zilizopigwa chapa.
 • Watahiniwa ni lazima wahakikishe kwamba kurasa zote za karatasi hii zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.


Maswali 

 1. UFAHAMU (Alama 15)
  Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali

  Wanawake ndio wanaonyanyasika zaidi katika vyombo vya usafiri hasa kwenye mabasi na matatu. Kwa kiasi fulani, kunyanyasika huku hutokana na maumbile, mavazi, watoto na mizigo mbalimbali wanayoibeba. Kwa upande mwingine utakuta kwamba, wafanyakazi karibu wote katika matatu na mabasi ni wanaume na shughuli zao wanaziendesha kama wanaume na sio vinginevyo. Wanaume hawa huendesha mambo zaidi kwa kumjali na kumtetemekea mwanamme na sio mwanamke. Mwanamke anashughulikiwa tofauti iwapo tu yeye mwenyewe ndiye mwenye mali hiyo, ni ya jamaa yake au mpenzi wa wafanyakazi katika matatu hizo. Hali ya vyombo vya usafiri inavyoonekana pia ni kuwa vimeandaliwa zaidi katika kumjali mwanamme na siyo mwanamke au watu wenye tofauti au upungufu fulani mwilini.

  Iwe ni tabia ya utingo au ya madereva au ni hali halisi ya vyombo vilivyoundwa, yote haya ni mambo yanayoweza kubadilishwa endapo tu wanawake watakuwa na sauti moja na kusimama kidete katika kupigania na kutetea kile wanachostahili kukipata katika huduma za usafiri na uchukuzi mijini na nchi nzima kwa ujumla.

  Kama ilivyotajwa hapo juu, kuna tofauti za kimsingi kati ya wanaume na wanawake. Katika jamii inayomjali kila mtu, ni muhimu kwa tofauti hizo kuzingatiwa ili kuhakikisha kuwa kila mwanajamii anapata huduma anayohitaji kwa amani na usalama na bila usumbufu kwake au kwa wale wanaomtegemea. Pamoja na matatizo yote wanayopata wanawake, hakuna chombo kilichojizatiti kutoa sauti ya umoja na kusema kwamba hili au hiki kinachofanyika siyo sawa au siyo haki kwa mwanamke.

  Wakati umefika sasa kwa wanawake wenyewe kujiunga pamoja, kuelimishana na kuanza kupigania haki zao ili wasiendelee kunyanyasika katika vyombo vya usafiri. Ninatoa mifano michache. Wale wanaokwenda safari ndefu wanajua fika adha wanayopata wanawake wakati basi limesimama peupe watu wanatakiwa “wakachimbe dawa.” Kwa mwanamme si kazi. Lakini kwa mwanamke kuna shida,tena siyo kidogo. Je, kwa nini wanawake waendelee kuvumilia haya? Kuna ugumu gani kwa kila basi ya safari ndefu kuwa na choo ndani? Wenye dini zinazodai tohara nao wanasemaje?

  Shida nyingine ni katika kupanda magari haya. Kwenye matatu, ni rahisi (ingawa hatari) kwa mwanamme kupanda gari huku likiwa kwenye mwendo, lakini je, dereva wa matatu anastahili kufanya hivyo kwa mwanamke? Upande wa mizigo hasa kwa wafanyabiashara ni adha tupu kwa wote. Je, nini kifanyike ili kila mtu aweze kufanya biashara yake kwa ustaarabu zaidi? Ni kama kwamba wanawake wamekubali kunyanyaswa kwao ni sehemu ya maisha. Hivi sivyo inavyostahili kuwa. Sote tuna haki sawa kwenye kila aina ya chombo cha usafiri. Tatizo ni pale tunapokubali kugeuzwa mizigo na kubebwa jinsi mbebaji anavyotaka kutubeba. Kama wanawake wana sauti ya pamoja kuhusu maswala haya, nina hakika kuwa tutaanza kuona mabadiliko katika mabasi na matatu zetu.

  Muda wa wanawake kuonekana kuwa ni “washamba” na watu wanaoweza kudanganywa kuwa gari lina viti vya kulala nalo kumbe limejaa tele na bado mtu akapanda umekwisha pita. Huduma yoyote lazima iwe na hadhi ya namna fulani. Na wanaoamua ni hadhi gani huduma hiyo iwe sio wenye basi au matatu bali abiria, maana nauli anayolipa ni kura inayotakiwa kumwezesha kuchagua kilicho bora na sio kilicho duni.

  Ni vyema kuelewa kuwa ni wanawake na sio wanaume waliochangia zaidi kumaliza ubaguzi wa rangi huko Marekani na Afrika Kusini. Wanawake kwa sababu wanafikiriwa kimakosa kuwa legelege ilidhaniwa wasingekubali kususia mabasi na kutembea kwa miguu kama mbinu ya kugomea mfumo uliokuwepo nyakati hizo huko Atlanta na Johannesburg. Hata hivyo, wanawake hao waliyagomea mabasi hayo kwa roho moja na kutembea, wakati mwingine hata masafa ya kilomita ishirini kwa miguu kila siku. Wenye mabasi na serikali wakaonja makali ya mgomo huu na huo ukawa mwanzo wa mabadiliko yaliyosababisha kuzuka kwa siasa zisizovumilia ubaguzi wa rangi katika usafiri na hatimaye katika mustakabali mzima kitaifa. Wanawake wa nchi yetu nao wakitaka wanaweza pia kuanzisha vuguvugu litakalosaidia usafiri na uchukuzi nchini kuwa wa heshima, kistaarabu na unaowajali wanawake, wazee na watoto.

  Maswali
  1. Kwa kurejelea kifungu, fafanua namna tatu mwanamke anavyodhalilishwa.(alama 3)
  2. K una nyakati mwanamke anajipata katika hali nafuu kidogo katika usafiri. Eleza. (alama 1)
  3. Ili kujikomboa na madhila anayokumbana nayo, mwanamke anastahili afanye nini?(alama 4)
  4. Eleza juhudi zilizofanywa na mwanamke kwingine kupambana na dhuluma katika jamii yake. (alama 1)
  5. M wandishi wa kifungu hiki anapendekeza nini kuhusu namna huduma kwa umma zinafaa kutekelezwa. (alama 4)
  6. Eleza maana ya mafungu yafuatayo kama yalivyotumiwa katika kifungu hiki. (alama 2)
   1. katika mustakabali mzima wa taifa
   2. wanatakiwa wakachimbe dawa

 2. UFUPISHO (ALAMA 15)
  Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali

  Kwa hali nyingine, tunaweza kusema kuwa uchafuzi wa mazingira ni uharibifu wa vilevitu vinavyowazunguka binadamu na wanyama maishani mwao. Kuna uchafuzi wa aina mbalimbali na kila uchafuzi humhusu binadamu kwa njia fulani.

  Maendeleo ya viwanda duniani ni sababu mojawapo ya uchafuzi wa hewa. Mitambo katika karakana huwa inatoa moshi mwingi wakati bidhaa zinapotengenezwa. Moshi husambaa eneo kubwa na kuchanganyika na hewa inayovutwa na binadamu. Uchafu hutupwa ovyo ovyo na kuwa hatari kwa afya ya binadamu. Maji machafu huweza kutiririkia mtoni, maziwani na hata baharini. Yale yanayotiririka mitoni na maziwani huchafua maji ambayo hutumiwa na watu wa eneo hilo kwa kunywa, kupika na kunywesha mifugo wao. Yale yanayotiririka baharini huwa ni hatari kwa samaki wanaotegemewa na binadamu kuwa kitoweo muruwa.

  Ongezeko la watu pia ni hali nyingine ya uchafuzi wa mazingira. Halaiki ya watu hufanyauharibifu wa misitu ya asili. Hii ni kwa sababu ya kutaka kuongeza ekari za mashamba. Hili husababisha mmomonyoko wa udongo; hivyo basi kuiacha ardhi bila rutuba yoyote. Katika hali hii, kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa nchi nyingi duniani huzoroteshwa. „„Maisha ya binadamu hutegemea kilimo kwa kila hali kwa hivyo kilimo kinapozoroteka hata uchumi nao huathirika. Kila uchao tunasikia kwamba nchi fulani imekabiliwa na njaa.

  Ufugaji wa wanyama wengi bila mpango maalum pia huharibu mazingira ya asili kama nyasi na vichaka. Watu wengi hufuga ng‟ombe, mbuzi na kondoo. Kwa kuwa hawana mahali maalum pa kuwalisha, huzunguka nao huku na huko kutafuta nyasi na majani ya kuwalisha. Wanyama wanaotangishwatangishwa namna hiyo humaliza majani na nyasi zote na kuacha ardhi tupu ambayo hatimaye huyabisika kwa jua. Ardhi ya namna hii haishiki maji mvua inyeshapo. Nchi iliyoneemeka huweza kuwa jangwa lililo na chungu ya mchanga.

  Watu wanapoongezeka huko mashambani huwabidi wakate misitu ili waanzishe maskani mapya pamoja na mashamba yao. Miti hukatwa bila hadhari na mabiwi ya matawi pamoja na majani huchomwa moto. Jambo la kusikitisha ni kwamba miti hiyo inapokatwa hakuna mingine inayopandwa kuchukua mahali pake.

  Mahitaji ya binadamu ya kuendeleza njia za mawasiliano pia huzusha balaa nyingine. Barabara zinazidi kuongezeka na pia watu wanaozidi kuongezeka pamoja na mazao yao. Kwanza, barabara zinapotengenezwa misitu hukatwa mahali zinapopitia. Pili, wingi wa magari huzidi na baadhi ya hayo magari hutoa moshi unaoharibu hewa.

  Njia kadha wa kadha za kuzuia uharibifu wa mazingira zimependekezwa. Ingawa suluhisho timamu halijafikiwa, serikali nyingi duniani zimo katika harakati za kutafuta suluhisho la uchafuzi huo. Njia mojawapo ni kukomesha ujenzi wa viwanda katika miji mikuu na mahali palipo na watu wengi.Wenye viwanda pia wanahimizwa kufikiria jinsi ya kutupa takataka na maji machafu bila kudhuru afya ya binadamu.

  Watu wakizingatia suala la upangaji wa uzazi na kuwa na familia ndogo ndogo, idadi ya watu haitaongezeka kwa kasi kwa hivyo itakuwa hakuna haja ya kuanzisha makao mapya mara kwa mara.

  Serikali nyingi zimechukua jukumu la kuwaelimisha raia juu ya madhara yanayotokana na uharibifuwa mazingira. Raia wanahimizwa kupanda miti kwa wingi. Aidha, ni jukumu la jamii katika eneo athirika kujenga matuta ya kuzuia mafuriko na kudhibiti mmomonyoko wa udongo.

  Jitihada zinazofanywa kuzuia uchafuzi wa mazingira hukumbana na matatizo. Tatizo kubwa ni fedha za kuendeleza miradi inayopendekezwa. Shida nyingine ni kwamba juhudi zingine huwa zinamwingilia binadamu na mali yake.

  Maswali
  1. Fupisha aya sita za kwanza za taarifa uliyosoma kwa maneno 60. (alama 7)
   Nakala chafu
   Nakala safi
  2. Fupisha aya za mwisho tano kwa maneno 50-55 (alama 6)
   Nakala chafu
   Nakala safi

 3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
  1. Andika tofauti moja kati ya sauti zifutazo. (alama 2)
   1. /ny/ na /ng‟/
   2. /g/ na /gh/
   3.  /s/ na /z/
   4. /ch/ na /j/
  2. Aindika kielezi chenye miundo ifuatayo. (alama 1)
   Kipasuo ghuna cha ufizi, irabu ya chini kati, irabu ya mbele juu, nazali ya midomo, irabu ya kati chini
   na tandazwa.
  3.        
   1. Silabi ni nini? (alama 1)
   2. Huku ukitoa mifano, eleza miundo miwili ya silabi za Kiswahili. (alama 2)
   3. Eleza dhima tatu za viambishi tamati mbali na kauli ya kutenda/kiishio. (alama 3)
  4. Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mawili ya kiambishi: -I- (alama 2)
  5. Andika sentensi hii katika ukubwa. (alama 1)
   Kijumba chenyewe kilijengwa karibu na mto.
  6. Taja nomino mbili kutoka ngeli tofauti zinazowakilishwa na kiambishi ngeli kilichopigiwa mstari. (alama 2)
   Itatumika katika sherehe yake.
  7. Badilisha sentensi katika kauli iliyomo kwenye mabano.
   1. Marie alipewa zawadi yake. (tendeka) (alama 1)
   2. Tunga sentensi ukitumia kitenzi kishirikishi kipungufu katika ngeli ya KI-VI. (alama 2)
  8. Yakinisha sentensi ifuatayo katika nafsi ya pili umoja. (alama 1)
   Sitaenda nyumbani kesho.
  9. Tunga sentensi ukitumia nomino dhahania katika ngeli ya U-U kutokana na neno: (alama 2)
   Zusha
  10. Eleza maana mbili zinazojitokeza katika sentensi hii. (alama 2)
   Mama anatupa mtoto.
  11. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao. (alama 2)
   S – KN(N+S)+KT(Ts+T+E)
  12. Akifisha: (alama 4)
   Akionekana mwenye hasira mkurugenzi huyo alishangaa jameni kwa nini wakenya wanaharibu mali hivi hii si siasa bali ni wendawazimu.
  13. Tunga sentensi kudhihirisha masharti yasiyowezekana katika hali timilifu. (alama 2)
  14. Wanne walituzwa na mwalimu. (Tumia kivumishi cha kuorodhesha). (alama 2)
  15. Taja vitenzi vyovyote viwili vyenye asili ya kigeni katika kauli ya kutendea. (alama 2)
  16. Ainisha yambwa katika sentensi; (alama 3)
   Mwanafunzi alitumiwa barua kwa posta.
  17. Unda nomino mbili katika hali ya wingi kutokana na kitenzi hiki. (alama 2)
   Sawidi
  18. Biwi ni kwa taka ........................ni kwa maji na kikuba ni kwa ................... (alama 1)
 4. ISIMU-JAMII (ALAMA 10)

  “Leo hii utashi wetu wa kujitosheleza umetusukumiza ukingoni mwa maisha. Vyakula vyetu sasa vina kemikali hatari kutokana na mizizi ya mimea kufyonza virutubisho vyenye naitrojeni. Virutubisho hivi hustawisha mimea. Hata hivyo, mimea hii tunayoila ina kemikali hatari kwa miili yetu. Kemikali hizi husababisha saratani na hili ndilo tatizo la kijiji hiki.
  1. Bainisha sajili ya makala haya kwa kutoa mfano mmoja kutoka kwenye makala. (alama 2)
  2. Fafanua sifa nyingine nane za sajili hii ambazo zingejitokeza katika makala haya. (alama 8)


Mwongozo Wa Kusahihisha

 1. UFAHAMU
  1.        
   1. Wafanyakazi katika matatu na mabasi ni wanaume na shughulizao wanaziendesha kama wanaume na si vinginevyo.
   2. vyombo vya usafiri vimeundwa kwa kumjali mwanamme na siyo mwanamke au watu wenye tofauti au upungufu Fulani mwilini.
   3.  Katika safari ndefu magari husimama peupe watu waende haja “wakachimbe dawa’ – hali hii haimjali mwanamke.
   4. Kupanda magari wakati gari li katika mwendo (hasa kwenye matatu) – mwanamke hawezi kufanya hivyo.
   5. wanawake kudanganywa kuwa gari lina viti vya kulala nalo limejaa tele.
    (za kwanza 3 x1 = 3)

  2.        
   1. Iwapo mwanamke ndiye mwenye mali hiyo, ni ya jamaa yake au mpenzi wa wafanyakazi katika matatu hiyo.
    (1 x 1 = 1)

  3.       
   1. wanawake wawe na sauti ya umoja na kusema kwamba hili au hiki kinachofanyika siyo sawa au siyo haki kwa mwanamke.
   2. wanawake wenyewe wajiunge pamoja, kuelimishana na kuanza kupigania haki zao ili wasiendelee kunyanyasika katika vyombo vya usafiri.
   3. wanawake wasiendelee kuvumilia kutakiwa kuenda haja peupe ilhali ni vigumu kwao kufanya hivyo.
   4. wanawake waanzishe vuguvugu litakalosaidia usafiri na uchukuzi nchini kuwa wa heshima, kistaarabu na unaowajali wanawake, wazee na watoto.
    (zozote4 x 1 =4)

  4. Marekani, katika mji wa Atlanta, naAfrika Kusini katika mjiwa Johannesburg, wanawake walisusia kupanda magari ya usafiri wa umma na kutembea kwa miguu kwa masafa marefu.
   (1 x 1= 1)

  5. Huduma za umma
   1. kuzingatia tofauti za kimsingi kati ya wanaume na wanawake ili kuhakikisha kuwa kila mwanajamii anapata huduma anayohitaji kwa amani na usalama na bila usumbufu kwake au kwa wale wanaomtegemea.
   2. za kila basi la safari ndefu kuwa na choo ndani yake.
   3. iwe na hadhi ya namna Fulani inayoamuliwa na abiria na wala siyo wenye basi au matatu kwa vile nauli anayolipa ni kura inayotakiwa kumwezesha kuchagua kilicho bora na siyo kilicho duni.
    (zozote4 x 1 =4)

  6.     
   1. siku za usoni za taifa (alama 1/0)
   2. wakaende haja msituni (alama 1/0)

 2. UFUPISHO
  1.  
   1. Viwanda hutoa moshi unaosambaa na kuchafuka hewa.
   2. Uchafu unaotupwa ovyo huhatarisha afya ya binadamu
   3. Maji machafu huchafua maji mitoni,maziwani na baharini
   4. Wanyama wengi huharibu misitu,nyasi na vichaka
   5. Barabara zaidi zinapojengwa miti hukatwa zinapopitia
   6. Magari hutoa moshi unaoharibuhewa
   7. Ongezeko la watu huharibu misitu ya asili kwa kujiongezea ardhi ya makaazi
    (Hoja 7 x 1 =7)

  2.      
   1. Kukomesha ujenzi wa viwanda mijini penye watu wengi
   2. Takataka na maji taka kutupwa bila kudhuru afya ya binadamu
   3. Upangaji wa uzazi usisitizwe kuzuia ongezeko la watu
   4. Raia waelimishwe kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira
   5. Wahimizwe kupanda miti mingi
   6. Kujenga matuta ya kuzuia mafuriko na kudhibiti mmomonyoko wa udongo
    (Hoja 6 x 1 =6)

    Utuzaji
    Sehemu a – 7
    Sehemu b - 6
    Utiririko alalma - 2
    15
    1. Adhabu – ondoa alama moja kwa kila ziada ya maneno 10 baada ya kumtuza
    2. Ondoa alama 1⁄2 kwa kila kosa la hijai na sarufi (6h na 6s) baada ya kumtuza
    3. Anayekosa kuandika matayarisho na jibu kwa haya moja asipewe alama za utiririko

 3. MATUMIZI YA LUGHA (alama 40)
  1. Andika tofauti moja kati ya sauti zifutazo. (alama 2)
   1. /ny/ ni sauti ya kaakaa gumu ilhali /ng’/ ni sauti ya kaakaa laini
   2. /g/ ni kipasuo/kizuiwa ilhali /gh/ ni kikwamizo/kikwamizwa/kikwaruzo
   3. /s/ ni sauti sighuna ilhali /z/ ni sauti ghuna
   4. /ch/ sauti sighuna ilhali /j/ sauti ghuna
    (Atuzwe1⁄2 au0kwakilasehemu 4× 1⁄2 =2)

  2. Andika kielezi chenye miundo ifuatayo. (alama 1)
   Kipasuo ghuna cha ufizi, irabu ya chini, kati, irabu ya mbele, juu, nazali ya midomo, irabu ya kati chini na tandazwa.Daima(alama 1 au 0)
  3.        
   1. Silabi ni nini? (alama 1)
    • Ni tamko moja au pigo moja la tamko au mpigo mmoja wa sauti. (alama 1 au 0)

   2. Huku ukitoa mifano, eleza miundo miwili ya silabi za Kiswahili. (alama 2)
    • I – oa
    • K - mti
    • IK - ah
    • KI – Tuta
    • KKI – kwake
    • KKKI – mbweha
    • KIK – labda
     Za kwanza mbili (muundo1⁄2 ,mfano 1⁄2 )

  4. Eleza dhima tatu za viambishi tamati mbali na kauli ya kutenda/kiishio. (alama 3)
   • Ukanusho – haji
   • Kauliyakutendea – som- e- a
   • Undani/kielezi – darasa-ni / mahali asimama-po
   • Wingi / amrisho – amke-ni, cheze-ni
   • Unominishaji/uzoefu – ushona-ji
   • Kiendelezi – amk-e-ni
   • Wakatiacheza-po
    (Za kwanza 3×1=03)

  5. Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mawili ya kiambishi: -I- (alama 2)
   • Ngeli ya I-I, I-ZI, U-I kwamfano, ilikatwa
   • Ukanusho – kija–siji
    (2×1=02)

  6. Andika sentensi hii katika ukubwa. (alama 1)
   • Kijumba chenyewe kilijengwa karibu na mto.
   • Jumba lenyewe lilijengwa karibu na jito.(alama 1/0)

  7. Taja nomino mbili kutoka ngeli tofauti zinazowakilishwa na kiambishi ngeli kilichopigiwa mstari. (alama 2)
   • Itatumika katika sherehe yake.
   • Nomino yoyote kutoka ngeli ya I-ZI au U-I au I-I
   • Mfano: mikeka, sahani(za kwanza 2×1=02)

  8. Badilisha sentensi katika kauli iliyomo kwenye mabano.
   1. Marie alipewa zawadi yake. (tendeka) (alama 1)
    • Marie alipeka zawadi yake. (atunge sentensi upya kwa kutumia kitenzi alichonyambua(alama 1/0)
   2. Tunga sentensi ukitumia kitenzi kishirikishi kipungufu katika ngeli ya KI-VI. (alama 2)
    • Kitabu ki mezani.(atungesentensi; alama 2/0)

  9. Yakinisha sentensi ifuatayo katika nafsi ya pili umoja. (alama 1)
   Sitaenda nyumbani kesho.
   • Utaenda nyumbani kesho. (alama 1/0)

  10. Tunga sentensi ukitumia nomino dhahania katika ngeli ya U-U kutokana na neno: (alama 2)
   Zusha
   Uzushi – maneno yasiyo ya kweli
   - Hali ya kuzua mambo
   (alama 2×1=02)

  11. Eleza maana mbili katika sentensi hii. (alama 2)
   Mama anatupa mtoto.
   • Mama anamtelekeza mtoto.
   • Mama anamrusha mtoto.
   • Mama ametuzawidi mtoto.
    (Zozote 2×1=02)

  12. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao. (alama 2)
   S – KN(N+Ṥ)+KT(Ts+T+E)
   • Mwalimu aliyetufundisha alikuwa akitembea kitausi.(alama 2/0)

  13. Akifisha: (alama 4)
   • Akionekana mwenye hasira mkurugenzi huyo alishangaa jameni kwa nini wakenya wanaharibu mali hivi hii si siasa bali ni wendawazimu. Akionekana mwenye hasira,mkurugenzi huyo alishangaa, “Jameni!Kwa nini Wakenya wanaharibu mali hivi?Hii si siasa bali ni wendawazimu.”(alama 8× 1⁄2 =04)

  14. Tunga sentensi kudhihirisha masharti yasiyowezekana katika hali timilifu. (alama 2)
   • Angalikuwa amesoma kwa bidii angalikuwa amepita mtihani. (alama 2/0)

  15. Wanne walituzwa na mwalimu. (Tumia kivumishi cha kuorodhesha). (alama 2)
   • Mwanafunzi wane alituzwa na mwalimu.(alama 2/0)

  16. Taja vitenzi vyovyote viwili vyenye asili ya kigeni katika kauli ya kutendea. (alama 2)
   • Samehea, aminia, salimia, hutubia(alama 2/0)

  17. Ainisha yambwa katika sentensi hii; (alama 3)
   Mwanafunzi alitumiwa barua kwa posta.
   • Yambwa tendwa- barua, yambwa tendewa- mwanafunzi, ala- posta(alama 3×1=03)

  18. Unda nomino mbili katika hali ya wingi kutokana na kitenzi hiki. (alama 2)
   Sawidi
   • Miswada, wasawidi (za kwanza 2×1=02)

  19. Biwi ni kwa taka funda ni kwa maji na kikuba ni kwa maua. (alama 1) (alama 2× 1⁄2 =01)

 4. ISIMU-JAMII (ALAMA 10)
  1. Sajili ya kitaaluma/hotuba ya kitaaluma/ mwanasayansi
   1. Msamiati wa kisayansi – saratani, kemikali, virutubisho, nitrojeni
   2. Lugha kavu – usiyoonyesha hisia bali ya kuafiki kile kinacholengwa
   3. Lugha yenye onyo/tahadhari – kemikali hatari kwa miili yetu.
   4. akriri kwa mfano, kemikali
    (Sajili; alama 1, Mfano; alama 1)

  2. Sifa za sajili ambazo zingejitokeza
   1. Lugha shawishii kwa mfano, hili ndilo tatizo la kijiji hiki
   2. Lugha ya maelezo/ maelekezo – jinsi kemikali zinahatarish amaisha
   3. Lugha sanifu inayoeleweka
   4. Kuchanganya ndimi
   5. Kuhamisha ndimi
   6. Matumizi ya takwimu ili kudhihirisha ukweli wa yanayosemwa kwa mfano, asilimia 50%.
   7. Lugha ya adabu / heshima/unyenyekevu
   8. Sentensi ndefu ndefu ili kujieleza kikamilifu
   9. Lugha rasmi - ni ma zingira rasmi
    1 (za kwanza 8×1=08)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Royal Exam Series Post Mock Trial Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest