Wahusika na Uhusika - Mwongozo wa Chozi La Heri

Share via Whatsapp


Utangulizi

Mhusika ni mtu katika riwaya au hadithi fulani anayetenda mambo kadha wa kadha, kadri mtunzi wa hadithi au riwaya atakavyo, ili kujenga hadithi yake. Wahusika hutumika kuafikisha maudhui ambayo mtunzi anataka kupitisha kwa msomaji. Kila mhusika huwa na sifa na umuhimu wake katika kazi hii ya ubunifu ya mwandishi.



1. Ridhaa.

Huyu ni mumewe Terry. Ni mhusika mkuu ambaye ana sifa kadhaa.

  1. Mshirikina
    Uk 1,"Anakumbuka mlio wa kereng'ende na bundi usiku wa kuamkia siku hii ya kiyama. Milio hiyo ndiyo iliyomtia kiwewe zaidi kwani bundi hawakuwa wageni wa kikaida katika janibu hizi "
    Pia anamwambia mkewe Terry, "milio hii ni kama mbiu ya mgambo, huenda kukawa na jambo " Kwa hivyo Ridhaa ni mhusika aliyekuwa na imani katika mambo ya ushirikina.
    Uk 2 "Ninashangaa vipi daktari mzima hapo ulipo unajishughulisha na mambo ya ushirikina " Huu ni ushahidi mwingine wa kuonyesha kuwa Ridhaa alikuwa mshirikina.

  2. Mwepesi wa moyo.
    Ridhaa ni mwepesi wa moyo kwani anapopatwa na mawazo ya hapo awali ambayo ni ya kukatisha tamaa, analia kwa urahisi, kinyume na matarajio ya jamii kuwa mwanaume hafai kulia.
    UK 2,"machozi yaliturika uwezo wake wa kuona "
    Uk 3 "Ridhaa mwanangu, mwanamume hufumbika chozi ya mwanamume hayapaswi kuonekana hata mbele ya majabalia ya maisha. Huku ni kujiumbua hasa. Unyonge haukuumbiwa majimbi, ulitunukiwa makoo "

  3. Mwenye bidii.
    Uk 4,"Alikuwa amesafiri kwa shughuli za ujenzi wa taifa, kama alivyoziita safari zake za kikazi " Tunapata kuwa Ridhaa alikuwa ni mwenye bidii za mchwa katika kazi yake ya kila siku aliyoiita 'ujenzi wa taifa'.

  4. Mvumilivu.
    Aliweza kuvumilia matukio yaliyomkumba kijijini mwake, yakiwemo kutotakwa huko, na kufukuzwa, mali yake kuharibiwa na familia yake kuuliwa.
    Anapiga moyo konde kukabiliana na hall hiyo mpya (uk 25).

  5. Mwenye busara
    Ridhaa anapozisikia sauti za hawa ndege, anajua kuwa kuna jambo ambalo lingeweza kutendeka na ambalo si la kupendeza. Pia anamwambia mkewe, uk 2,"wewe endelea kupiga hulu tu, lakini utakuja kuniambia "
    Baadaye tunapata kuona kuwa kuna janga linaloipata familia yake na kwa hivyo, Ridhaa alikuwa na uwezo wa kuhisi kuwa kuna jambo lisilokuwa la kupendeza litakaloifikia jamii yake


2. Terry

Huyu ni mkewe Ridhaa. Aliangamia katika mkasa wa moto.

  1. Mcheshi
    Terry ana sifa moja kuu ya kuwa yeye ni mcheshi.
    Uk 2 "Terry kwa ucheshi wake mwingi wa kawaida, hakunyamaza " Tunaona kuwa ucheshi ulikuwa ni mazoea yake au kawaida yake.

  2. Mwenye busara.
    Anamwambia mumewe, (uk 2) "wewe huishi kufanya tumbo moto!Kila jambo kwako lazima liwe na kiini utakuja kujitia fadhaa bure Anajaribu kumpa ushauri mumewe baada ya kumwona mumewe kuwa mshirikina. (Terry anaiaga dunia pamoja na wanawe, baada ya nyumba yao kuteketezwa)


3. Mzee kedi

Huyu ni jirani yake Terry na Ridhaa. Anaonekana kuwa muuaji.

  1. Katili
    Uk 3,"Uuuui!uuuui!Jamani tusaidieni!Uuuui!Uuuui! Mzee Kedi, usituue, sisi tu majirani!Maskini wanangu!Maskini mume wangu!" 


4. Tila

Huyu ni mwanawe Ridhaa. Anapatwa na janga la moto na kuiaga dunia pamoja na mamake. Jina lake kamili lilikuwa.

  1. Mwerevu
    Alionekana kuwa na sifa ya kuwa mwana mwerevu sana. Baba yake anakumbuka jinsi walivyokuwa wakijadiliana vikali kuhusu mafanikio ya baada ya uhuru, uk 5,"Anakumbuka mjadala mkali aliokuwa nao na bintiye, Tila, kuhusu mafanikio ya baada ya uhuru, mjadala ambao hakuna mmoja katika aila yake aliyethubutu kuuchangia kwani kwenye maswala ya sheria na siasa, hakuna aliyempiku Tila "


5. Becky.

Huyu ni mjukuu wake Ridhaa. Yeye pia anajipata katika janga la moto na kuiaga dunia.



6. Mzee mwimo msubili.

Huyu alikuwa babake Ridhaa. Alikuwa na familia kubwa, yenye madume ishirini; uk 7. Ridhaa akiwemo kati ya madume hao ishirini.

  1. Mwenye busara,
    alihamisha familia yake msitu wa heri, ili kupunguza msongamano nyumbani pake.

  2. mwenye bidii kwani mtu kuilisha familia kubwa namna hiyo si jambo nyepesi. Alikuwa mwenye wake wengi na wana wengi pia.
    -Pia aliwapeleka wanawe shuleni kupata elimu, kama Ridhaa. Uk 10. "Anakumbuka jinsi siku ya kwanza shuleni alivyotengwa na wenzake katika mchezo wao wa kuvuta


7. Mama ridhaa.

Alikuwa mzazi wake Ridhaa wa kike, na mmoja kati ya wake wa mzee Mwimo.

  1. Ni mwenye busara.
    Anamfunza Ridhaa namna ya kuishi na wenzake. Uk11,"Mama Ridhaa alisikiliza malalamishi ya mwanawe akamwambia, 'Mwanangu, ni vyema kujifunza kuishi na wenzako, bila kujali tofauti za ukoo na nasaba. Elimu inapaswa kuwa chombo cha kueneza amani na upendo wala sio fujo na chuki "


8. Selume

  1. Alikuwa mwenye matumaini mengi,
    uk 31,"Selume alitueleza kuwa alikuwa amesikia fununu kuwa upo mradi wa kuwakwamua wakimbizi kutokana na hali hii. Maneno ya Selume yaliwasha mwenge wa tumaini "


9. Billy

Alikuwa mlowezi. Alibagua wengine kwa misingi ya rangi, na kuwadhalilisha wanawake wa Kiafrika, hivyo basi kutafuta mchumba huko kwao ughaibuni.



10. Sally

Alikuwa mchumba wake Billy ambaye Billy alitaka kufunga ndoa naye.

  1. Alikuwa mwenye majivuno na maringo,
    uk 80,"Kipusa akawa ameliona jumba la mpenziwe kama tundu la makinda, akachukua virago na kurudi kwao ughaibuni "


11. Naomi.

Alikuwa mkewe Lunga. Tabia zake zilifananishwa na za Sally aliyemwacha mumewe kwa dharau.

  1. Ni mwenye dharau kwa familia yake,
    kwa jinsi anavyowaacha. Tazama, Uk 81,"Uk 81,"Nimeondoka. Acha nitambae na ulimwengu, huenda nikaambulia cha kukusaidia kuikimu familia. Nasikitika uchungu nitakaokusababishia wewe na wanao. Kwaheri. Naomi "

  2. Ni katili.
    Anaiacha familia yake na kwenda kuizuru dunia uk 84,"Alimlaani mama yake ambaye aliwatelekeza kwa ubinafsi na ukatili mkuu "

  3. Mwenye majuto.
    Baada ya kuwaacha wana wake, anarudi nyumbani baada ya miaka kadhaa na kukuta hali ya huko ikiwa mahame tu. Anakuta kaburi la mumewe tu, likiwa halijafyekewa kwa miaka mingi. Anaanza kazi ya kutafuta walikokwenda wana wake. Kwa bahati nzuri, mwishowe wanapatana na wana wake wakiwa bado hai. Kwa miaka mingi, anaishi kwa majuto ya kuwaacha wana wake (uk 192-193).


12. Lunga

Alikuwa mumewe Naomi.

  1. Mwenye mapenzi kwa mkewe.
    ni kwamba hili linauma na kudhalilisha zaidi kwani Lunga alijisabilia kwa hali na mali kumridhia na kumpendeza mkewe "

  2. Mvumilivu.
    Alijikaza na kuvumilia machungu yaliyomkumba alipoachwa na mpenzi wake Naomi. Uk 81,"lakini mkono wake ulimkataza kujidhalilisha zaidi. Alimeza funda chungu la mate na kuamua kusalimu amri ya usaliti wa Naomi "
    pia alivumilia kuwalea wanawe alioachiwa na mke wake. Uk 81,"mwaka mmoja wa kwanza ulikuwa mgumu mno "

  3. Mlezi mwema.
    ".Lunga ilibidi kuwa baba na mama wa watoto wake, na hilo usilione kama jambo jepesi, Hakuwaacha watoto wake kama alivyofanya mkewe Naomi.


13. Umulkheri (umu)

Ni dadake Dick na Mwaliko.

  1. Ni msomi.
    Tunamwona kuwa anasomea Shule ya upili ya mtende. Uk 82."Ninasomea Shule ya upili ya Mtende "
    Uk 85,"Huenda akapata pa kuishi na hata kuyaendeleza masomo yake!"

  2. Ni mwenye busara
    Anapowakosa ndugu zake, anawatafuta kila mahali, na hatimaye kupiga ripoti kwenye kituo cha polisi kuhusu kupotea kwa watoto wao.

  3. Ni mwenye upendo.
    Anawapenda ndugu zake, na hivyo, anatia bidii kuwatafuta waliko kwenda, kwa kupiga ripoti kwenye kituo cha polisi. Uk 85,"fikra za ndugu zake zilimfanya kuzizima na hata kuishiwa na nguvu "

  4. Mpenda haki.
    Alijitahidi kutafuta haki yake na ndugu zake, na kuamua kuulinda utu wake kwa hali na mali uk 85,"Nitapigana kwa jino na ukucha kuulinda utu wangu. Nitatafuta haki ilikojificha "

  5. Mwenye bidii.
    Tunaona kuwa anaamka asubuhi na mapema kwenda kuitafuta haki yake.
    Uk 85,"Asubuhi moja mbichi ilimpata Umu kwenye kituo cha gari moshi, akiwa amewasili kutoka mlima wa Simba, yu katikati ya mji "

  6. Mpenda Dini.
    Tunapata kuwa Umu aliweza kuhudhuria ibada jijini na wazazi wake kila jumapili. Uk 85,"Kila alipokuja jijini Jumapili alikuwa akaandamana na wazazi wake kwa ubada"

  7. Mwenye huruma na utu.
    Anawahurumia sana vijana wa mtaani, na kutaka kuwasaidia. Anamwomba mamake pesa kidogo aweze kumsaidia kijana mmoja. Uk 86,"Umu alitia mkono ndani ya mfuko wa dangirizi yake, akatoa shilingi mia mbili alizokuwa amedunduliza kutokana na mapeni aliyokuwa akipewa na baba yake kama masurufu, akampa mvulana mmoja ombaomba "


14. Sauna

Ni kijakazi aliyekuwa akiwaangalia Umu, Mwaliko na Dick utotoni wao.

  1. Si mwaminifu
    Kijakazi huyu alitoweka na watoto, kinyume na matarajio ya kuwaangalia wana hao. Uk 84,".ilibainika kuwa wanuna wake walikuwa wametekwa nyara na Sauna"
  2. Katili Anawapeleka watoto aliowateka nyara kwa bibi mmoja ambaye aliwatumia binadamu kama malighafi "


15. Hazina

Huyu alikuwa kijana wa mtaani aliyekuwa akiombaomba mapeni huko barabarani, na alisaidiwa na Umu kwa pesa alizozitumia kununulia mkate. 

  1. Mwenye heshima.
    Anamshukuru sana Umu baada ya kumpa pesa za kununua mkate. Uk 86,"Poa sana sistee, we ni mnoma. Siku moja nitakuhelp
  2. Ni msomi.
    Alienda shuleni na kupata elimu. Uk 88,"Nilipelekwa shuleni nikasoma, nina elimu japo akali. Amesomea upishi na huduma za hotelini katika chuo.
  3. Mwenye upendo/urafiki wa dhati.
    Anamwita Umu anapomwona, kwa kukumbuka wema aliomtendea wakati mmoja. Hazina alimpeleka Umu kwenye hoteli na kumpa chakula mpaka akashiba. Aliahidi pia kumsaidia Umu, na akampeleka kwao nyumbani. Uk 89,"Hazina alimwahidi Umu kuwa atamsaidia. Alimpeleka moja kwa moja hadi kwenye makao yao, akamjulisha kwa mama aliyesimamia makao hayo "


16. Julida

Ni mama aliyesimamia makao yaliyokuwa ya wana wa mitaani.

  1. Mwenye utu na upendo
    Anamkaribisha kwa upendo Umu, na kumpa tumaini. Uk 89,"Julida alimgusa Umulkheri begani na kumwambia, 'usijali mwanangu. Hapa patakuwa penu kwa muda "
  2. Mwenye huruma.
    Kwa kumgusa Umu begani, anaonyesha kuwa anamhurumia mwana huyu kwa yaliyomfika.


17. Kairu

  1. Ni mvumilivu.
    Kulingana na jinsi anavyomwambia Umu, inaonekana kuwa yeye ameyapitia magumu, na kuyavumilia. hujapitia tuliyo yapitia. Tulitendwa ya kutendwa "
  2. Ni msomi.
    Ingawa anajipata katika hali ya ufukara uliozidi, mamake anajaribu kuzungumza na mwalimu mkuu baada yake kufukuzwa shuleni kwa ajili ya kukosa karo. Jambo hili linamsaidia kuendeleza masomo yake shuleni kama wanafunzi wengine. Uk 93."Hata karo yangu imebidi amlilie mwalimu mkuu amruhusu alipe kidogo kidogo hadi mwisho wa mwaka "
    Pia tunapata kuwa walipofika huku, Kairu alikuwa katika darasa la sita, na kwa sasa, ako katika kidato cha pili. Hii ina maana kuwa amekuwa akiendeleza masomo yake kwa ufasaha. Uk 92,"nilikwenda hapo nikiwa katika darasa la sita, sasa ni katika kidato cha pili "


18. Mzee kaizari

Alikuwa babake Mwanaheri, na Lime.

  1. Mwenye Busara.
    Aliyajenga maisha ya familia yake upya baada ya kutoka msituni na kurudi nyumbani. Uk 93,"baada ya kurudishwa nyumbani kutoka msitu wa mamba, baba yangu mzee Kaizari aliweza kuyajenga maisha yetu upya "
  2. Mwenye mapenzi kwa familia yake.
    Aliweza kuijengea familia yake nyumba pale ambapo waliishi zamani. Baada ya mkewe kutoweka, tunamwona Mzee Kaizari akitia bidii sana katika kumtafuta kwao na pia mjini. Uk 96,"Baba alikwenda kumtafuta mama kwao asimpate baba alifululiza mjini kumtafuta mama, majuto yamemjaa kifua "
  3. Mvumilivu.
    Anapompata mkewe akiwa ameaga dunia, alivumilia uchungu wa kumpoteza ampendaye, na akamzoazoa na kumzika pamoja na wanawe. Uk 96,"Baba alizoazoa kilichobakizwa na uozo, tukakizika "


19. Mwanaheri

Huyu ni mwanawe mzee Kaizari.

  1. Ni mpenda mashairi.
    Anawaelezea wenzake kuwa alijaribu kupalilia kipawa chake cha kughani mashairi mepesi uk 93.
  2. Ni msomi.
    Anaendeleza masomo yake pamoja na wenzake, akina Kairu.
  3. Ni mvumilivu.
    Anayapitia mambo machungu tangu kuachwa na mamake, mpaka wakati walipomzika katika kaburi la sahau. Barua aliyoiandika mama kabla ya kutoweka ilimtonesha kidonda rohoni mwake.


20. Lime

Ni ndugu yake Mwanaheri, na wote wawili ni wana wake Mzee Kaizari.

  1. Ni msomi.
    Walisoma pamoja na dada yake huko kijijini. Uk 93."mimi na ndugu tulirudi shuleni mle mle kijijini mwetu tu "
  2. Ni hodari katika michezo ya kuigiza.
    Uk 93,"Lime alikuwa hodari katika michezo ya kuigiza -ile ya kitoto "
  3. Mcheshi.
    Alipendwa sana shuleni kwa ucheshi wake. Uk 93,"Alikuwa mcheshi sana, kwa hivyo kutokuwepo kwake shuleni kuliwafanya watoto kumpeza "


21. Kangara.

  1. Mkiukaji haki za watoto.
    Bii kangara anakiuka haki za watoto kwa kuwashika na kuwauza katika madanguro, na kwa matajiri, ili wawe watumishi, na kutumika kama alabiashara haramu. Uk 157,"Bi. Kangara alifanikiwa kupata wasichana wa kuuza katika madanguro, wavulana wa kuwapelekea matajiri ambao walishiriki katika ulaguzi wa dawa za kulevya, na wafanya kazi katika makasri ya matajiri, na katika mashamba ya mikahawa na michai " Uk 158,"mabibi hawa walifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la ukiukaji wa haki za watoto "
  2. Mwanabiashara haramu.
    Anafanya biashara haramu ya kuwauza watoto, na baadaye, anakamatwa na kufungwa gerezani miaka saba ".wakarambishwa miaka saba gerezani na kazi ngumu "


 22. Sauna.

Wanafanya kazi pamoja na Bi. Kangara.

  1. Mlaguzi wa binadamu.
    Wanafanya kazi ya kuwauza watoto pamoja na Bi. Kangara Uk 157,"Hatimaye ulaguzi wa binadamu uligeuka ukawa ngozi yake "
  2. Mwenye bidii.
    Alifanya kazi yake kwa bidii, Uk 157, "Sauna aliianza kazi yake. Ni kazi iliyompa pato kubwa sana, hata akataka kusahau yaliyopita na kuwasamehe walezi wake.
  3. Mtumwa.
    Alifanya kazi chini ya masharti yake Bi. Kangara. Uk 157."Hatimaye, ulanguzi wa binadamu uligeuka kuwa ngozi yake. Na sasa yu tayari kushika tariki kutekeleza utumwa mwingine wa Bi. Kangara "


Maswali tarajiwa kuhusu wahusika.

  1. Mzee Kaizari ni mhusika mwenye manufaa mengi katika jamii. Tetea kauli hii kwa kutolea umuhimu wake kama unavyojitokeza kwenye riwaya hii (alama 20).
  2. Taja sifa kumi za mhusika Ridhaa kama zinavyojitokeza kwenye riwaya hii (alama 20).
  3. Taja umuhimu wa wahusika wafuatao katika kuwasilisha maudhi (alama 20).
    1. Sauna.
    2. Bi. Kangara.
    3. Lime
    4. Umulkheri.
  4. Mhusika Hazina ametumika kudhihirisha maisha ya vijana yalivyo huko mitaani. Kulingana na matukio yanayomkumba mhusika huyu, tolea mapendekezo ambayo yangeweza kufuatwa Hi kuwasaidia vijana wengine kama hawa (alama 20)
  5. Taja sifa zake Umulkheri kama zinavyojitokeza katika riwaya hii (alama 7).
  6. Taja sifa zake Lunga na umuhimu wake katika kupitisha maudhui ya riwaya hii (alama 20).
  7. Mwandishi wa riwaya hutumia wahusika kama vyombo vya kuwasilisha maudhui yake kwa msomaji. Kwa kurejelea riwaya ya Chozi la Heri, eleza maudhui yanayopitishwa kupitia kwa mhusika Ridhaa (alama 20).
  8.  
    1. Ni nini tofauti kati ya mhusika mkuu na mhusika mwingine asiye mkuu (alama 2)
    2. Kwa kurejelea riwaya ya Chozi la Heri, taja wahusika watano wakuu, na watano wasio wakuu (alama 5)
    3. Taja sifa tano za mhusika mkuu yeyote (alama 5)
  9.  
    1. Eleza sifa tano za mhusika Kairu katika riwaya hii (alama 5)
    2. Kairu ametumika na mwandishi kupitisha maudhui yepi? Eleza (alama 10).
  10.  
    1. Mhusika Naomi ametumika na mwandishi katika kuwasilishha maudhui kadhaa kwa msomaji. Kwa kutolea mifano, thibitisha haya (alama 10)
    2. Taja sifa tatu za mhusika Billy (alama 3).
    3. Eleza umuhimu wa mhusika Billy katika kuwasilisha maudhui kwa msomaji (alama 2).
Join our whatsapp group for latest updates

Download Wahusika na Uhusika - Mwongozo wa Chozi La Heri.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest