MKUBWA - Mwongozo wa TUMBO LISILOSHIBA

Share via Whatsapp


Ufaafu wa Anwani Mkubwa

Neno mkubwa linatokana na kivumishi '–kubwa' ambalo lina maana ya kuzidi kwa umbo au kimo; -siyo ndogo. Pia neno hili lina maana '- enye kwisha kukua' au 'kuwa juu'.

Anwani 'Mkubwa' inaafiki kazi hii kwani yafuatayo ni mambo yaliyo wazi zaidi; Msimulizi anatueleza kuhusu mhusika mkuu kazini aliyeitwa Mkubwa. Alikuwa anajihusisha na biashara ya kuuza pweza wa kukaanga. Hii ndiyo biashara iliyompa kipato na faraja.

Mkubwa alipoingia uongozini alikuwa na madaraka makubwa. Alikuwa na uwezo uliozidi. Viongozi walipapata pasipoti za kidiplomasia ziliwawezesha kutosachiwa bandarini wala
kwenye uwanja wa ndege.

Uovu wa Mkubwa ulikuwa umezidi. Aliweza kumwingiza rafiki yake Mkumbukwa kwenye biashara ya kuuza dawa za kulevya. Mkumbukwa aliponaswa na kutiwa ndani kwa kupatikana na mkoba uliojaa dawa hizo alijuta mno. Majuto yake yalikuwa makubwa.

Ushawishi wa Mkubwa ulikuwa umezidi. Aliweza kumtoa Mkumbukwa ndani baada ya siku tatu. Pia alipewa mzigo wake ukiwa katika hali ile ile.

Baada ya Mkumbukwa kutolewa ndani , aliichukia sana biashara ya kuuza dawa. Aliapa na Mola kuwa hatofanya tena biashara hiyo tena.

Mkubwa alipojilaza kwenye kochi na usingizi kumchukua anaota kuwa vijana wameongezeka mjini wanaosinzia ,wengine hali yao imedhoofika sana na wizi umewazidi mitaani.

Mshituko wa Mkubwa ulizidi alipoona kuwa watoto wake wa kiume walikuwa miongoni mwa vijana waliokuwa wameandikwa kwenye nyuso zao 'mla unga' jambo liliomfanya chizi.Dhamira ya Mwandishi

  Mwandishi amelenga kupiga vita biashara haramu ya uuzaji wa dawa za kulevya au “kuuza unga”. Kupitia kwa Mhusika Mkubwa tunagundua kuwa viongozi ndio walanguzi wakuu wa dawa hizi.

Viongozi wawa hawa huwatafuta vijana ambao huzipeleka dawa hizo kwa wateja. Wanaoumia zaidi ni vijana ambao wanaponaswa hutiwa ndani huku walanguzi halisi wakiufurahia uhuru wao nje.Wahusika

Mkubwa

Alikuwa muuzaji wa pweza wa kukaanga kabla ya kuingia kwenye uongozi alikoingilia biashara haramu ya kuuza dawa za kulevya. Ana sifa zifuatazo:

Mwenye bidii

Alikuwa akishughulisha na kazi ya kuuza pweza wa kukaanga na baadaye akauza kipande cha ardhi ili kuingia uongozini.

Mwenye utani

Anamtania utingo kuwa huwa haogi jambo lililomfanya utingo kukimia kwa kuchekwa na abiria.

Ni mtambuzi

Aliweza kuelewa maana ya unga japo hakuwahi tu kuona vituko vyake.

Mwenye utu

Alimpigapiga kijana mbwia unga aliyekuwa ameinama kama kwamba anarukuu na kumuuliza iwapo anaumwa.

Mwenye tamaa ya mali

Alipotanabahi namna viongozi wanavyotajirika kwa kuuza unga , maneno 'unga na utajiri' yalimkaa moyoni kiasi chake kukosa usingizi usiku huo.

Ni maskini

Alikuwa akifanya biashara ya kuuza pweza iliyokuwa na kipato kidogo . vilevile kabla ya kupata uongozi, alikuwa na suruali na shati kipande papa.

Ni fisadi

Baada ya kutia na kutoa, aliamua kufanya biashara haramu ya kuuza dawa za kulevya biashara ambayo huonekana kama ya kishetani. Vile vile alitoa kiasi kikubwa cha pesa ili kuwashawishi wapiga kura kumpendelea na ndipo akaupata ushindi.

Mwenye msimamo dhabiti

Baada ya kuyatia moyoni maneno aliyopewa na kijana yule kuhusu utajiri na unga aliamua kutafuta kwa udi na uvumba na ndipo akamwendea rafikiye kwa jina Mkumbukwa.

Ni msiri

Mwanzoni hakumweleza Mkumbukwa sababu yake kuutafuta uongozi.

Mwenye wasiwasi

Aliogopa kuwa huenda kisomo chake kingemzuia kupata uongozi.

Mkumbukwa

Ni rafikiye Mkubwa aliyejitwika jukumu la kuwarai watu ili wampigie Mkubwa kura.

Rafiki wa dhati

Mkumbwa alimwendea kwa mawaidha baada ya kuamua kuugombea uongozi na ndipo Mkumbukwa akamshauri Mkubwa augombee.

Mkakamavu

Alimweleza Mkubwa bila kupepesa macho wala kugugumizi kuwa pesa na ukaragosi wa chama ndiyo mambo muhimu pale Mchafukoge yatayomwezesha kuupata uongozi.

Mwenye kutimiza ahadi

Alimwambia Mkubwa kuwa akitafuta milioni kumi kisha ampe yeye ataupata uongozi na kuapa kuwa iwapo ataukosa amuue.

Ni mwenye bidii

Baada ya Mkubwa kujaza fomu; alianza kazi ya kuingia /kupita nyumba baada ya nyumba kumtafutia kura mkubwa.

Mwenye busara

Alifahamu fika kuwa ili kufanya kazi vyema ni lazima angemtafuta Bi Kibwebwe (Sada) na kumhusisha katika harakati za kumtafutia Mkubwa kura.

Mwenye majuto

Aliponaswa na askari wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya alijuta kimoyomoyo.

Mwenye kulalamika

Alipotiwa ndani alikuwa akilalamika kupuuzwa kwa haki za mahabusu.

Zoezi

 1. Fafanua sifa za wahusika hawa.
  1. Sada
  2. Vijana wabwia unga
  1. askari


Maudhui

Maudhui ni mengi yaliyomo katika kazi. Haya ni masuala yanayoangaziwa na mwandishi wa kazi husika.

Mwandishi ameangazia maudhui yafuatayo;

Athari za dawa za kulevya

 • Vijana wanaolangua dawa za kulevya(unga) huishi kwa woga huishi kwa mfano yule kijana baada ya kumrushia Mkubwa maneno aliogopa wenyewe wasije wakamwona.
 • Vijana wabwia unga(wanaotumia dawa hizi) hugeuka karakana za matusi. Km yule kijana mbwia unga alimuuliza Mkubwa kijeuri “kwani tunakula kwa babako? Vile vile kijana aliyekuwa kichochoroni alimwita Mkubwa juha
 • Vijana wanaozitumia dawa hizi hugeuka na kuwa mazuzukm kijana mwingine aliyekuwa kichochoroni alikuwa akitokwa na denda mdomoni huku amefumba macho.
 • Vijana wabwia unga huota ndoto za kiajabu – kwa mfano kijana aliyekuwa kichochoroni alimkasirikia Mkubwa kwa kuwa aliikatiza ndoto yake na kumkatizia stimu. Analalamika kuwa Mkubwa aliiangusha ndege yake (katika ndoto) alipomshtua.
 • Viongozi wanaojihusisha katika biashara hii haramu hugeuka matajiri na hatimaye kuliumiza taifa kama anavyorai kijana aliyeandamana na Mkubwa.
 • Wabwia unga husinzia mchana. Hukauka midomo. Hujidunga mili yao ikawa kama jahazi la mtefu. Zaidi ya mno vijana hawa hujitoboa mishipa ya damu ikashabihiana na chungio.
 • Vijana wanaojihusisha na biashara hii haramu huishia kwenye seli. Wanafungwa miaka mingi huku wakuu wao wakiyafurahia maisha yao nje.

Ufisadi

Ufisadi ni uovu ambao umejitokeza katika hadithi kama ifuatavyo;

 • Pindi tu viongozi wanapopata pasipoti ya kidiplomasia wao hujiingiza katika biashara haramu za kuuza dawa za kulevya. Mkubwa aliweza kupita vizuizi vyote akiwa ameubeba mkoba wenye dawa hizo na hakusachiwa.
 • Mkubwa alipungiana mkono na wale askari ndani ya gari ; pungiano hili lilikuwa na maana yake. Baadaye Mkubwa alifanya mikakati na kumtoa Mkumbukwa ndani alikokuwa amefungiwa. Bila shaka aliwahonga askari wamweke Mkumbukwa huru.
 • Vijana wanaopewa kazi ya kuviuza vidonge vile wanapokamatwa hutiwa magerezani na kuwaacha viongozi walanguzi wakiendeleza shughuli zao. (mwanafunzi aongezee hoja ili kuonyesha namna ufisadi unavyojitokeza)

Uongozi mbaya

Uongozi wa Mkubwa ulikuwa uingozi mbaya kwani;

 • Alishiriki ufisadi- alitumia ushawishi wake kisiasa kumtoa Mkumbukwa ndani na kuuokoa mzigo wake(dawa za kulevya)
 • Alikuwa akiuza dawa za kulevya- sababu kuu ya Mkubwa kujiingiza mamlakani ilikuwa ni utajiri na unga(dawa za kulevya). Alimwingiza Mkumbukwa kinafiki kwenye biashara hii.
 • Viongozi hawasachiwi kwenye viwanja vya ndege na hivyo basi kuwarahishia mipango ya kubeba dawa za kulevya. Idara yauchunguzi imefeli.
 • Idara ya magereza haijukumiki kuwaweka ndani vigogo wanaolangua dawa hizi. Wao huwaweka ndani vidagaa. (mwanafunzi aongezee hoja)

Dhuluma

Vijana mahabusu walio magerezani wanadhulumiwa kama ifuatavyo:

 • Wanalazwa chini kama magunia ya viazi mbatata.
 • Wakiwa mle ndani kwenye vyumba vya mahabusu wananyimwa chakula,hawakogi,hawafui nguo zao,
 • Vijana hawa huhukumiwa kabla na kufungwa pasi kupewa nafasi ya kujitetea
 • Vijana hawa huteswa sana kwani hata chakula wanachokileta jamaa zao huliwa na walinzi wa magereza.
 • Viongozi huwauzia dawa vijana ambao huathirika si haba. (tazama athari za dawa za kulevya)

 

Zoezi

Jadili maudhui yafuatayo kama yanavyojitokeza katika hadithi ya Mkubwa.

 1. Ajira na kazi
 2. Tamaa


Fani

Katika Fani tutashughulikia mbinu za uandishi pamoja na tamathali za usemi.

Ndoto:

Mkubwa aliota alipojilaza kwenye kochi lake. Katika ndoto hii mambo yafuatayo yalijitokeza;

 • Vijana wanaotumia dawa wameathirika mno kwani walikuwa wakisinzia tu.
 • Baadhi ya vijana(wake kwa waume) wamekondeana kana kwamba wanaugua ukimwi au kifua kikuu.
 • Vijana hao walikuwa wac hafu na walikuwa wakivitenda vitendo vichafu vya kihayawani.
 • Watu wengi aliowaona hawakuwa na raha kwani wizi ulikuwa umewazidi. 
 • Nyumba zote zilikuwa zimechanwa nyavu.
 • Vijana aliowaona wote walikuwa wameandikwa kwenye vipande vya nyuso zao “mla unga”
 • Mkubwa aliwaona watoto wake wa kiume miongoni mwa vijana hao.

Tashbihi

Tashbihi zimetumiwa kwa mapana na mwandishi wa hadithi hii.

Mifano michache ya tashbihi ni kama

 • Yule kijana alipita kama umweso…
 • Majumba makubwa yamefumuka kamau yoga…
 • … akipeleka pumzi juu kama mtu aliyepanda…
 • …yalimkaa kama ngoma ya kimanga…
 • Yalitembea kichwani kama damu itembeavyo mwilini…
 • …alilidaka begi la Mkumbukwa kama mwewe anavyodaka kuku…
 • Alipita kama umeme…
 • Mkubwa alikuwa amesimama kama mlingoti wa bendera…
 • Lilikwama kooni kama mtu aliyekuwa anakula vigae…

Mbalagha

Maswali ambayo hayahitaji majibu moja kwa moja yametumiwa mara moja moja na mwandishi kama ifuatavyo;

 • Kwani ulikuwa mwavuli?
 • Wapi?

Onomatopea/tanakali

Mbinu hii imetumika kazini kama ifuatavyo.

 • Popooooooo! Popooooooo! – kuashiria jinsi gari lilivyopiga honi.

 

Utohozi

Mbinu ya kuyaswahilisha maneno ya lugha ya kigeni ili yatamkike na kuandikika kama yale ya Kiswahili.

 • Pasipoti – kutokana na 'passport'
 • Kidiplomasia- kutokana na 'diplomacy'
 • Husachiwi- kutokana na 'search'
 • Profesa- kutokana na 'professor'
 • Begi- kutokana na 'bag'
 • Kiboksi- kutokana na 'box'
 • Presha- kutokana na 'pressure’

Kuchanganya ndimi

Kuna mara kadha ambapo mwandishi amevichopeka vifungu vya lugha ya Kiingereza katika muktadha wa mazungumzo. Kwa mfano;

 • Form four
 • Birthday
 • Brother
 • Sober house

Kinaya

Kinaya ni kinyume na matarajio. Mbinu hii imejitokeza kama ifuatavyo;

 • Ni kinaya kuwa , ili kuwa kiongozi katika eneo la Mchafukoge huhitaji kuwa umesoma kwani cha muhimu ni pesa na kuwa mzalendo kwa chama chako(ukikatwa, damu yako inakuwa rangi ya chama)
 • Ni kinaya kuwawanafunzi wa Profesa walimpa kura Mkubwa ambaye hakuwa na masomo.
 • Ni kinaya kuwa walanguzi halisi wa dawa za kulevya huachwa huru( kama vile Mkubwa)na wanaofungwa ni vijana wanaowafanyia walanguzi hao kazi. (mwanafunzi aongeze hoja)

Takriri

Pia hujulikana ka uradidi. Lengo la kutumia mbinu hii huwa ni kusisitiza ujumbe.

Mifano ya takriri ni kama ifuatayo;

 • Halimezeki, halimezeki…uk 151
 • Hapo hapo!...154
 • Kifo,kifo,kifo…uk 150
 • Unga!unga!...uk 142

Istiara

Tofauti na tashbihi, istiara huwa haitumii maneno ya ulinganisho kama 'kama'. Mbinu hii imetumika kama ifuatavyo.

 • Magereza kuna vitawi vitupu- vijana wanofungwa wameitwa vitawi
 • …wao ni matela tu- vijana wanaowafanyia kazi vigogo kama akina Mkumbukwa wanaitwa matela.
 • …vichwa vya treni huachiwa…- viongozi (vichwa vya treni) huachwa nje wakiendelea na biashara zao haramu.

 

Zoezi

Onyesha namna mbinu hizi zimejitokeza.

 1. Nidaa
 2. Chuku

Maswali ya kudurusu.

 1. “ Usiteketeze umati kama kuni zinavyoteketeza moto. Rudi,rudi kwa Mola wako.”
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili.
  2. Fafanua sifa za msemewa.
  3. Tambua tamathali ya usemi iliyotumika hapo juu
  4. Ni kwa nini msemewa anatakikana kurudi kwa Mola wake?
Join our whatsapp group for latest updates

Download MKUBWA - Mwongozo wa TUMBO LISILOSHIBA.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest