KCSE 2017 Kiswahili Paper 3 with Marking Scheme

Share via Whatsapp

SEHEMU A: FASIHI SIMULIZI

 1. Lazima  (20 marks)

  Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali.

  Walikuja mahasidi, ah, walikuja
  Nyayo zao zikirindima, ah rindima
  Kwa ghamidha ya uadui, oo uadui
  Wali wakibeba sime
  Wali wakibeba mata
  Wali wakibeba mienge
  ya moto kutangazia
  kwao kuwasili

  Walikuja kwa ndimi
  zilohimili cheche
  matusi kutumwaiya
  Hawakujua ya kwamba
  mbele ya mhimili huno wetu
  wao wali vipora.
  Kwenye Mlima wa Sugu, walituvamia
  Aliwakabili Mbwene
  Mwana wa Ngwamba, ee Mbwene
  Aliwakabili Mbwene kwa kitali kikali.
  Wali wametuteka ja samaki kwenye dema
  Wali wamewapukutisha
  wetu mabarobaro
  Aliwakabili Mbwene
  Ee Mbwene, Mwana wa Ngwamba
  Aliwakabili
  kwa hamasa za ujana
  kwa uchungu wa kuumbuliwa
  wa wetu wana.

  Aliwakabili Mbwene
  Nao wakalipiza shambulizi
  kwa kujidai majagina
  walijibwaga uwanjani
  Laiti wangalijua wanajikabidhi
  viganjani mwa Mbwene.
  Aliwakabili Mbwene, ee
  Mwana wa Ngwamba, shujaa asoshindwa
  alipigana kitali
  cha kufa na kupona
  kuiopoa jamii yetu,
  kuirejesha hadhi yetu.
  kuirejesha mifugo yetu
  kuwarejeshea wakulima vikataa vyao
  kuwaokoa vipusa wetu
  nyara waliotekwa, ati walipiza kisasi.

  Aliwakabili Mwana wa Ngwamba
  Aliwakabili Upepo wa Kusi
  Hata kikomo cha mapambano kilipofika
  Wagundi walijua kwamba
  Walikuwa na Mwana, ee Mwana
  Mbwene, ee Mwana wa Ngwamba
  Hakuwa na kifani, ee kifani
  Alipigana nao, ee Mwana wa Ngwamba
  Kwa siku kumi bila tonge wala tone la maji
  Kwetu kukenda kicheko cha wokovu
  Kwao kukenda kilio.
  1. "Huu ni wimbo wa sifa." Thibitisha kauli hii kwa kutoa mifano mitatu kutoka kwenye utungo huu.  (alama 3)
  2. Andika sifa tatu za jamii ya nafsineni katika utungo huu.   (alama 3)
  3. Huku ukitoa mifano, bainisha vipengele vinane vya kimtindo ambapo nafsineni imetumiwa kufanikisha uwasilishaji wa utungo huu.   (alama 8)
  4. Tungo za aina hii zinaendelea kufifia katika jamii yako. Fafanua hoja sita utakazotumia kuishawishi jamii yako kukinga dhidi ya hali hii.   (alama 6)

SEHEMU B: RIWAYA

K. Walibora: Kidagaa Kimemwozea

Jibu swali la 2 au la 3.

 1. "Lakini waliogopa... Waliogopa hata kuwa na uoga."
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili.   (alama 4)
  2. Bainisha tamathali moja ya usemi ambayo imetumiwa katika dondoo hili.   (alama 2)
  3. Kwa kurejelea hoja kumi na nne kutoka kwenye riwaya hii, thibitisha kwamba raia wa Tomoko walistahili kuogopa hata kuwa na uoga.    (alama 14)
 2.  
  1. "Usinivue nguo kwa macho yako wee!"
   Kwa kurejelea hoja kumi na mbili kutoka kwenye riwaya hii, thibitisha kwamba mzungumzaji anastahili kuvuliwa nguo.   (alama 12)
  2. Tathmini umuhimu wa barua ya Ben Bella kwa Mashaka katika kuijenga riwaya hii.    (alama 8)

SEHEMU C: TAMTHILIA

T. Arege: Mstahiki Meya

Jibu swali la 4 au la 5.

 1. Tuyashughulikie ya leo. Kesho, keshokutwa na mtondo hatutakuwepo. Wayatakia nini ya mtondogoo?"
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili.   (alama 4)
  2. Bainisha sifa ya mzungumzaji inayodokezwa na kauli iliyopigiwa mstari.   (alama 1)
  3. Eleza sifa tano za anayeambiwa maneno haya.   (alama 5)
  4. Kwa kurejelea hoja kumi kutoka kwenye tamthilia, onyesha jinsi kutoyataka ya mtondogoo kulivyozorotesha hali ya maisha Cheneo.   (alama 10)
 2. "Ni mgao wa wakubwa kula kwanza na sisi wengine kupigania makombo yanayoanguka chini."
  1. Fafanua sifa tano za mzungumzaji.  (alama 5)
  2. Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa kurejelea hoja kumi na tano kutoka kwenye tamthilia.    (alama 15)

SEHEMU D: USHAIRI

Jibu swali la 6 au la 7.

 1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
  Mwanangu, wenye dhambi vishawishi, vikejeli
  Mwanangu, katu wasikushawishi, binkuli
  Mwanangu, aushi nayo uishi, kama mwali
  Mwanangu sikubali!

  Mwanangu, sherati sikuperembe, kakubali
  Mwanangu, usiwache wakubembe, kwa sali,
  Mwanangu, mithili yao mapembe, ya fahali
  Mwanangu sikubali!

  Mwanangu, wajeuri siwe nao, ni shubili
  Mwanangu usifwate njia zao, pita mbali
  Mwanangu, ujeuri sera yao, mazohali,
  Mwanangu sikubali!

  Mwanangu, waongo usiwasifu, kulihali
  Mwanangu, uongo ubatilifu, si amali
  Mwanangu, ndimi zao hazikifu, si manzili
  Mwanangu sikubali!

  Mwanangu, wafisadi siwe nao, kemikali
  Mwanangu, tamaa ndo utu wao, si Injili
  Mwanangu, wahepe kila uchao, kiakili
  Mwanangu sikubali!

  Mwanangu, wote walio wabaya, wanadhili
  Mwanangu, usije ukawapeya, ikibali
  Mwanangu, katika hino duniya, kaa mbali
  Mwanangu sikubali!
  (J. Kiponda)
  1. Fafanua mambo sita ambayo yanaweza kuzorotesha maadili ya anayelengwa na shairi hili.    (alama 6)
  2. Bainisha tamathali mbili za usemi zilizotumiwa katika shairi hili    (alama 2)
  3. Andika aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili.   (alama 2)
  4. Ainisha shairi hili kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:     (alama 4)
   1. idadi ya vipande katika mishororo.
   2. mpangilio wa maneno katika mishororo
   3. idadi ya mizani katika mishororo.
   4. mpangilio wa vina katika beti.
  5. Andika aina mbili za uhuru wa kishairi zilizotumiwa katika shairi hili.   (alama 2)
  6. Andika ubeti wa tano kwa lugha ya nathari.    (alama 4)
 2. Soma Shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

  Walo nacho hawachi
  mshangao kunitia
  Moyoni watakutia
  pindi waonapo
  we u chambo cha
  kuvutia rasilimali
  huko kwenye vina
  Hawachi
  kukwinamisha
  kukupindisha mgongo
  ndoana umeshika
  kuvulia yao riziki

  Watakwita kwa majina
  ya hadhi
  ya kupembeja
  ya kukwaminisha
  kwamba wenawamu
  wamoja
  hali zenu
  kama sahani na kawa
  wanakwonyesha wao
  mwachumia jungu moja
  yenu matarajio ni mamoja
  watakwahidi halua
  kila tunu watakwashiria
  mradi nyoyo zao zimemaizi
  we u nundu
  ya kukamulia mafuta
  we u ndovu
  wa mti kugonga
  makoma kuangusha
  wafaidi wao

  Mabepari wana mambo
  ukiwa yao makasia
  ya kuliendesha dau lao
  majini lielee
  miamba kulepusha
  Watakusifu
  Watakuchajiisha
  mbele utunge
  machoyo yenye ari
  huku wanakufunga nira
  ja fahali
  mali kuwazalishia
  huku kipato wakupimia
  kwa kibaba
  usipate kukidhi haja
  usipate kujamini
  kuwategemea uzidi.

  Hawa ni wa kuajabiwa
  Watakupa yao kazi
  Mpangilio wa kazi
  wakukabidhi wao
  na malengo wakupe
  La! Hawakupi!
  Wanakuhusisha
  katika kuyavyaza na
  muda wa kuyafikia
  nao mwaafikiana
  ati kuna makubaliano bayana
  ambayo ubatizo wayo ni
  kandarasi ya utendakazi
  Ela we nao mnajua
  ndo kigezo cha kupimia
  wako uwajibikaji
  wako mchango chunguni
  yako thamani
  Na usidhani una hiari ya
  kuamua tapofika
  Watakusukuma
  kufikia yao shabaha
  bila kuwazia
  ujira wanokupa.
  Watakuhimiza
  kutumia chako kipawa
  kuikoza nundu yao mafuta
  Viumbe hawa!
  Mabepari - waajiri.
  1. Eleza mikakati sita inayotumiwa na waajiri kujikuza kiuchumi.     (alama 6)
  2. Bainisha tamathali tatu za usemi zilizotumiwa katika shairi hili.   (alama 3)
  3. Huku ukitoa mifano, bainisha aina mbili za uhuru wa kishairi aliotumia mshairi.   (alama 2)
  4. Andika mifano miwili ya mistari mishata katika shairi hili.   (alama 2)
  5. Bainisha nafsineni katika shairi hili.   (alama 1)
  6. Fafanua toni ya shairi hili.   (alama 2)
  7. Andika ubeti wa tatu kwa lugha ya nathari.   (alama 4)

SEHEMU E: HADITHI FUPI

K. Walibora na S. A. Mohamed (Wah): Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine

 1.  
  1. Tathmini umuhimu wa Lucy katika kuijenga hadithi, "Tazamana na Mauti."     (alama 10)
   "Mizizi ya Matawi" (Ali A. Ali)
  2. "Aaa, bibi yangu namuomba Mungu anisamehe dhambi zangu... 
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili.   (alama 4)
   2. “Jamii ya," Mizizi na Matawi inastahili kusamehewa." Fafanua kwa kutoa hoja sita kutoka kwenye hadithi.(alama 6)


MARKING SCHEME

 1.  
  1.  
   1. Kuonyesha Mbwene kama aliye jasiri-aliwakabili kwa kitali kikali.
   2. Kumrejelea Mbwene kama shujaa asiyeshindwa- hawakujua kwamba mbele ya mhimili huu wetu walikuwa vipora. 
   3. Kumtajaanayesifiwa kwa majina mbalimbali-Mbwene, Mwana wa Ngwamba, Upepo wa Kusi, Mhimili.
   4. Kumsawiri kama bingwa wa kupindukia- Hakuwa na kifani.
   5. Kusifia ushindi//kitali alichopigana. Wagundi walijua walikuwa na  mwana wa Ngwamba/kwetu kukenda kicheko.
    (3x1)
    Kutaja - ½
    Mfano - ½
  2.  
   1. Ni wakulima- kurejesha vikataa. 
   2. Ni wafugaji - kurejesha mifugo.
   3. Utekaji nyara - kuwaokoa vipusa wetu. 
   4. Mazoea ya uchokozi/kupigana vita-walikuja kwa ndimi zilizojaa matusi...aliwakabili Mbwene, nao wakalipiza....
    (3x1)
    Kutaja - ½
    Mfano - ½
  3.  
   1. Matumizi ya vihisishi ili kuibua hisia/kusisitiza ujumbe -ah, ee
   2. Usambamba
    • wali wakibeba sime
    • wali wakibeba mata 
    • wali wakibeba mienge
    • kuirejesha hadhi yetu
    • kuirejesha mifugo yetu
   3. Sitiari- wali vipora 
   4. Tashbihi - ja samaki kwenye dema
   5. Lakabu - Upepo wa Kusi. 
   6. Nahau - cha kufa na kupona -kitali kikali.
   7. Chuku- kupigana (Ngwamba) kwa siku kumi bila kula wala kunywa. 
   8. Tanakuzi - kicheko - kilio
   9. Miundo ngeu ya sentensi/kufinyanga sarufi
    • wetu mabarobaro
    • matusi kutumwaiya
    • wa wetu wana
   10. Inkisari- zilohimili, kukenda.
   11. Taswira-utungo unasawiri picha ya mapigano. 
   12. Matumizi ya mistari mishata ili kuibua taharuki- ya moto kutangazia...
    (8x1)
    Kutaja-½
    Mfano-½
  4. Mtahiniwa aonyeshe umuhimu wa nyimbo za sifa. Baadhi ya hoja ni:
   1. Kuwatambua mashujaa 
   2. Kurithisha utamaduni wa jamii
   3. Ni kitambulisho cha jamii. 
   4. Hutumiwa kuwafunza vijana mbinuishi kama vile ujasiri, kutoa maamuzi yafaayo.... shujaa anahitaji kutoa maamuzi kwa kuzingatia mahitaji ya jamii yake.
   5. Hukuza uzalendo, jamii inaweza kuwatumia wanaosifiwa kama vielelezo vya uzalendo. 
   6. Hupitisha historia ya jamii, hivyo kuwafunza vijana kuhusu kwa mfano, maadui wa jamii zao, vita vilivyopiganwa na mafanikio yaliyofikiwa.
   7. Ni nyenzo ya kurithisha fani yenyewe ya uimbaji.
   8. Hukuza ubunifu. Kadiri vijana wanavyosikiliza nyimbo za aina hii zikiimbwa, ndivyo wanavyojifunza mitindo mbalimbali ya utungaji na uwasilishaji. 
   9. Hutumiwa kuonya dhidi ya matendo hasi kama vile usaliti/buadilisha. 
   10. Ni njia ya kupitisha maarifa, kama vile ya kupigana vita. Mtu kufahamu ni lini atashambulia, ni lini ataepuka shambulizi.
   11. Hukuza utangamano/ushirikiano. Watu wanapoimba nyimbo hizi pamoja hujihisi kuwakundi moja linalomuenzi shujaa mmoja.
   12. Ni njia ya kujiburudisha.
   13. Ni nyenzo ya kupitisha wakati, badala ya kujiingiza kwenye vitendo visivyofaa.
   14. Hupitisha amali na tamaduni za jamii. Desturi za jamii hutajwa katika baadhi ya nyimbo.
    Mtahiniwa anaweza pia kupendekeza njia za kudumisha kipera hiki.
    Baadhi ni:
    1. kuzihifadhi kwenye maandishi
    2. Kuzihifadhi kwenye kanda
    3. Kuzifanyia utafiti
    4. Mashindano ya tamasha za muziki
    5. Kuzifunza shuleni 
    6. Kuwahimiza vijana kuzitunga
     (6x1)
     Kutaja - ½
     Mfano/kueleza - ½

     Tanbihi
     Mtahiniwa anaweza pia kujadili hasara za kutourithisha utungo wa aina hii, akawa anaionya jamii yake dhidi ya kutourithisha.
 2.  
  1.  
   1. Haya ni maneno ya mwandishi/msimulizi.
   2. Yanawarejelea raia ya Sokomoko.
   3. Wanaugulika kwa dhuluma za Mtemi mara tu baada ya kurithi mamlaka kutoka kwa Mzungu.
   4. Wanalalamika kwa minong'ono kwa vile wanaogopa adhabu ya Mtemi.
    (4x1)

    Tanbihi
    Dondoo limetolewa uk. 14.
  2. Chuku - kuogopa hata kuwa na uoga. Woga umepigiwa chuku.
   (1x2)
   Kutaja-1
   Mfano-1
  3.  
   1. Utawala wa mkoloni kunyakua mali ya Waafrika na kuwatelekezea kwenye sehemu duni
   2. Watu kuuawa na Mazungu na kutupwa kwenye Mto Kiberenge
   3. Ukatili wa Mtemi - mauaji ya Chichiri Hamadi na Mama Imani.
   4. Kutumia vyombo vya dola kukabiliana na upinzani. Anawatia Amani, Imani na Matuko Weye korokoni.
   5. Wizi wa mali ya umma - Nasaba Bora kunyakua shamba la Chichiri Hamadi
   6. Utawala wa kiimla-tunaambiwa ulimi wake ulitoa amrisho na cheche za moto (uk. 14)
   7. Matusi - tunaambiwa ulimi wake ulitoa karipio na matusi. (uk. 14)
   8. Kukiuka haki za watoto - Nasaba Bora anakitupa kitoto mlangoni pa Amani.
   9. Kuachiwa majukumu - Nasaba Bora anampagaza Amani ulezi wa mtoto wake.
   10. Upufuju wa maadili - Nasaba Bora kuhusiana kimapenzi na msichana mdogo.
   11. Wizi wa kitaaluma-Majisifu kuiba mswada wa Amani. xii.
   12. Dhiki ya kisaikolojia -- Amani kulazimika kuchimba kaburi la Mtemi angali hai.
   13. Mtemi kumpiga Amani kikatili kwa shutuma ambazo hajathibitsha
   14. Askari kumpiga Mama Imani kikatili na kusababisha kifo chake xv.
   15. Majirani wa Imani kutomtetea anapochomewa nyumba na Mtemi. Kimya chao kinamhuzunisha Imani. xvi.
   16. Serikali kuwatelekezea wazee kamavile Matuko Weye kwenye ugonjwa na umaskini 
   17. Usaliti wa kimapenzi. Michelle kumwacha Major Noon/ Majununi. 
   18. Matumizi mabaya ya dawa. Oscar Kambona anapatikana na bangi, anafungwa. 
   19. Uchochezi - wanafunzi wanamsingizia Amani kwamba kawachochea dhidi ya serikali, anafungwa 
   20. Kutoshughulikiwa kwa watoto wenye mahitaji maalum. Majisifu kuwaona watoto wake kuwa mashizi.
   21. Viongozi kutowahakikishia raia huduma bora za afya. Pesa zilizotengewa ujenzi wa hospitali zinatumiwa vibaya, wanaishia kujenga zahanati.
   22. Nasaba Bora kulipa wema kwa ukatili. Licha ya DJ kumletea barua,
    Nasaba Bora anakataa kumpeleka hospitali anapoumwa na jibwa lake.
   23. Unyanyasaji wa kijinsia Nasaba Bora anamwachia mkewe upweke, ati anakwenda kusuluhisha migogoro ya mashamba. 
   24. Ubakaji - Ben Bella ni mbakaji, ni sugu wa jela. 
   25. Wizi wa mitihani - wazazi wa Fao kumwibia mtihani
   26. Mwalimu Fao kuhusiana kimapenzi na mwanafunzi wake. Anamtunga mimba.
   27. Nasaba Bora kuwatoza raia kodi ili kumpeleka mwanawe ng'ambo
   28. Nasaba Bora kuwafuta wafanyakazi kwa sababu zisizo na msingi kama vile kunadhifisha mazingira
   29. Nasaba Bora na Majisifu kuwalipa wafanyakazi mshahara duni 
   30. Wauguzi kutomtibumtoto wa kina Imani na Amani. Mtoto anakufa. 
   31. Nasaba Bora kumuua paka kikatili
   32. Nasaba Bora kumtaliki mke wake na hali yeye amekuea mzinifu 
   33. Bi Zuhura kutaka kuhusiana kimapenzi na kijana mdogo/ anataka kumhujumu Amani. 
   34. Kuzorota kwa huduma za kiafya- DJ anatoroka kwenye zahanati kutafuta tiba ya kienyeji kwa kukosa matibabu humo. 
   35. Raia kutozwa kodi ili Nasaba Bora ampeleke mwanawwe ng'ambo.
   36. Pesa zilizotengewa ufadhili wa masomo ya watoto maskini kutumiwa kuwasomeshea wa walio nacho kama vile Madhubuti. 
   37. Ufisadi- Mtemi kujitengenezea faili ili apate mali.
   38. Hali duni katika vituo vya kurekebishia tabia. Seli katika afisi ya Mtemi ni choo, Ben Bella analalamikia hali duni huko jela.
   39. Mwalimu Majisifu kushindwa kidhibiti uraibu wake wa dawa licha ya elimu yake
    (14x1=14)
    Kutaja - ½
    Kueleza/mfano - ½
    Tanbihi
    Mtahiniwa abainishe mambo ambayo yanaweza kumfanya mhusika kutotaka kusema
    Au
    Mambo ambayo yanaweza kumfanya mtu kutotaka kuishi Tomoko Sokomoko. Mambo haya yanaweza kuwa ukatili/dhuluma hali mbaya/ duni ya maisha/ kuzorota kwa maaadili/ kutothaminiwa kwa raia/ tamaa na ubinafsi wa wahusika...n.k.
 3.  
  1.  
   1. Dondoo limetolewa uk. 21.
   2. Mtahiniwa aonyeshe mambo ambayo Nasaba Bora ametenda, ambayo ni ya aibu/dhuluma ya kumfanya ashutumiwe.
   3. Kuvua nguo-kuona uozo/kuangaza uovu/kusutwa kwa uovu
    Baadhi ya hoja ni:
    1. Mauaji - Nasaba Bora kumuua Chichiri Hamadi
    2. Uzinzi - Kuhusiana kimapenzi na Lowela.
    3. Kuwafuta wafanyakazi kwa makosa yasiyo na msingi kama vile kunadhifisha mazingira
    4. Kuwapokonya Chichiri Hamadi na Mama Imani shamba.
    5. Kuchoma nyumba ya akina Imani
    6. Kumpiga Amani kikatili
    7. Kudharau watu wenye mahitaji maalum. Anapogundua yule msichana ni kilema anahizika, hamtaki mapenzi tena. 
    8. Kumuua paka kikatili
    9. Kuwatoza raia kodi kumpeleka mwanawe ng'ambo
    10. Kumwachia mkewe upweke; ati anakwenda kusuluhisha migogoro ya mashamba, anashindwa hata kutekeleza majukumu ya unyumba
    11. Kumtupa mtoto wake kibandani mwa Amani
    12. Kumpagaza Amani ulezi 
    13. Kumtafutia mwanawe kazi kwanjia ya kifisadi, kughushi hatimiliki 
    14. Anamwacha mwanamke azalie njiani licha ya rai za mkewe.
    15. Anashindwa hata kusoma hotuba ya rais kwenye sherehe muhimu.
    16. Anachangia matumizi mabaya ya pesa zilizotengewa ujenzi wa hospitali, wanaishia kujenga zahanati. 
    17. Anamlazimisha Amani kumchimbia kaburi angali hai. 
    18. Anashindwa kukabiliana na hali ya ushinde; anajiua/anakufa kifo cha aibu. 
    19. Anashindwa hata kuhusiana na ndugu yake.
    20. Anasahau mafundisho ya kidini ya baba yake.
    21. Uongozi wake unawatelekeza wazalendo kama vile Matuko Weye na Chwechwe Makweche katika ugonjwa na hali duni.
    22. Ufisadi. Anajitengenezea faili ili kupata mali akiwa mkuu katika Wizara ya Ardhi. 
    23. Anamtarajia ndugu yake Majisifu kuandika habari zake kwenye gazeti japo kwa kweli hastahiki.
    24. Anamtaliki mkewe kwa tuhuma ambazo hajathibitisha.
    25. Kutelekeza vituo vya kurekebishia tabia-seli katika afisi yake ni choo cha shimo refu.
     (12 x 1
     Kutaja-½
     Kueleza/ mfano-½
  2.  
   1. Barua ya Ben Bella inaonyesha hali duni katika vituo vya kurekebishia tabia. Anasema aliyopitia yalimfunza kuwa bado Tomoko haijapata uhuru.
   2. Ukiukaji wa haki za wafungwa hajui kinachotokea nje ya kuta za jela.
   3. Kuonyesha maudhui ya mapenzi- anasema alijua bado Mashaka anampenda
   4. Kuonyesha ukosefu wa uwajibikaji wa vijana- yeye na Mashaka wanasuhubiana wakiwa wachanga; shuleni.
   5. Kuonyesha uzinifu wa Nasaba Bora; anahusiana kimapenzi na Lowela. 
   6. Kuonyesha ukiukaji wa haki za kibinadumu; Lowela anaifunga mimba yake bila kujali usalama wa kijusi.
   7. Ndiyo inayoonyesha aliyekitupa kile kitoto mlangoni pa Amani. 
   8. Kuonyesha ukatili wa Lowela-anatoka nyumbani bila kuwajuza wazazi; anakitupa kitoto chake. 
   9. Kuonyesha uthabiti wa moyo wa Ben Bella. Anasema baba mkwe hawezi tena kuwa shemeji, hivyo analazimika kumwacha Mashaka.
   10. Ndiyo kiini cha kuvunjika kwa uchumba wa Ben Bella na Mashaka na kuwehuka kwa Mashaka 
   11. Inabadilisha msuko wa riwaya- Mashaka anashindwa kukabiliana na kutengana kwao, anawehuka na kuacha shule. 
   12. Inachimuza tabia ya Mashaka. Hana uwezo wa kustahimili mazito.
    (8x1)
    Kutaja-½
    Mfano-½
 4.  
  1.  
   1. Ni maneno ya Meya.
   2. Anamwambia Diwani III.
   3. Wamo ofisini mwa Meya. 
   4. Meya amesema wageni watawapa mkopo wa kulipa mishahara. 
   5. Diwani III anasema hili ni suluhisho la sasa lakini ni mzigo kwa watakaobakia. Ndipo Meya anasema haya. (4x1)
    Tanbihi
    Dondoo limetolewa uk. 53.
  2. Mapuuza/kutowazia ya kesho/ukosefu wa uwajibikaji/ubinafsi (1x1)
  3.  
   1. Diwani III ni msema kweli. Anamwambia Meya ukweli kwamba mikopo itakuwa mzigo kwa vizazi vijavyo.
   2. Ni mshauri bora. Anamshauri Meya wabuni mikakati ya kuliinua pato la Baraza
   3. Ni mpiganiaji haki. Anasema kwamba mama mwenye kuuza ndizi analipa kodi hivyo madiwani wanastahili kulipa. 
   4. Ni mnyenyekevu. Anazungumza na Siki/anamsikiliza Siki. Anasema wanawahitaji wafanyakazi.
   5. Ni mwadilifu. Kinyume na madiwani wenzake, anapinga wazo la kuunda kamati za kuhudumu. Anataka Baraza liimarishe pato ili wafanyakazi wote wafikiriwe kwa nyongeza ya mishahara badala ya kuwawazia madiwanitu.
   6. Ni mwenye busara. Anamwambia Meya kuwa migomo itaathiri pato la Baraza 
   7. Ni mtambuzi wa mambo. Kinyume na Meya, anajua kwamba hata kazi za mikono zinahitaji akili; kwamba watu wanahitaji kufunzwa kazi hizo. 
   8. Ni mtiifu. Meya anaponga'ng'ania kwamba mishahara ya madiwani ongezwe, anasema yu radhi kufanya hivyo shingo upande.
   9. Ni mzalendo. Anawazia vizazi vya kesho vya Cheneo; hataki kuviachia mzigo. 
   10. Ni mwenye msimamo thabiti. Anang'ang'ania kwamba Baraza linastahili kubuni mikakati ya kuongeza pato badala ya kuongeza mishahara ya walinda usalama.
    (5x1)
    Kutaja - ½
    Mfano-½
  4. Mtahiniwa aonyeshe athari za mapuuza/kutofanya jambo wakati mwafaka. Baadhi ya hoja ni:
   1. Meya anapuuza umuhimu wa kuwepo kwa dawa hospitalini; raia wanakufa. Dadavuo Kaole.
   2. Meya anapuuza kuboresha elimu; inaishia kuwa duni, anaharibu pesa kuwapeleka wanawe ng'ambo.
   3. Baraza linapuuza malalamishi ya wafanyakazi, linayaona kuwa mkoromowa chura; mgomo unaangusha uongozi wa Meya.
   4. Meya analipagaza Baraza deni kupitia kwa kandarasi, anamwambia mwanakandarasi alipandishe Baraza mahakamani; analifisi Baraza zaidi.
   5. Meya anapuuza mpango wa kimaendeleo wa miaka kumi; Cheneo inaendelea kuwategemea wafadhili.
   6. Kupuuza malalamishi ya wafanyakazi kunalifanya jiji kujaa uvundo; wageni wanaahirisha ziara.
   7. Badala ya kumsikiliza Diwani III kuhusu haja ya kubuni mikakati ya kuinua uchumi wa Baraza, anapanga njia ya kudumisha uzalendo kupitia propaganda, anadhoofisha uongozi wake.
   8. Meya anamfanya Bili kuwa mshauri wake akijua kuwa Bili si mfanyakazi wa Baraza. Bili anaishia kuiba fimbo ya Meya.
   9. Diwani I anatoka na fimbo bila kuwazia madhara yake; Bili anaiiba; wao hawafaidiki.
   10. Raia wanamchagua Meya kila mara wakijua kuwa ni dhalimu; wanakosa mahitaji ya kimsingi kama vile chakula.
   11. Meya anashindwa (anapuuza) haja ya kuwahakikishia watu usalama wa chakula. Wanakula mizizi na matunda mwitu, baadhi wanakufa.
   12. Wanataaluma (Siki)wanachelea kuingia kwenye siasa. Wanajinyima nafasi ya kuuwajibisha uongozi. 
   13. Wanyonge kama vile Dida wamekubali hali zao; Dida anasema kwamba hajali, bora mameya wawepo, naye apate nyumba za kunadhisisha. Wanaendelea kunyanyaswa.
   14. Baraza linampa Meya mamlaka makubwa kikatiba; anaishia kuitumia kuwafurusha wafanyakazi wanaogoma, na kujigawia vipande vya ardhi.
   15. Meya anatumia pesa za mkopo kuagizia mvinyo kutoka ng'ambo, anaishia kulifilisi Baaza.
   16. Meya ananipa mhubiri sadaka bila kuwazia athari; kwamba analifilisi Baraza zaidi. 
   17. Badala ya kutafuta njia za kukomesha mgomo, Meya anasema kuna vijana wasio na kazi. Anaishia kujisababishia kung'olewa mamlakani.
   18. Meya anajigawia viwanja na kumgawia Bili; anaishia kuufanya uongozi wake uchukiwe. Anang'olewa mamlakani.
   19. Baraza linawabagua wafanyakazi. Madiwani wana bima za afya, wafanyakazi wengine hawana. Wafanyakazi wanagoma, Meya anang'olewa mamlakani.
   20. Meya anachochewa na Diwani I na Diwani II kupuuza malalamishi/ migomo ya wafanyakazi, anasema kuna vijana wengi wasio na kazi. Wafanyakazi wanaishia kugoma, uvundo unajaa, Meya anang'olewa mamlakani.
   21. Meya anapuuza Mpango wa maendeleo wa miaka kumi akidai yale ya kimilenia ndiyo muhimu. Cheneo inashindwa kuwatoshelezea raia mahitaji ya kimsingi kama vile chakula; watu wanakufa kwa njaa na ukosefu wa lishe bora
    (10x1)
    Kutaja-½
    Mfano-½
 5.  
  1.  
   1. Beka ni jasiri. Anamwambia Meya kwamba wamekuja kumweleza wala si kujieleza.
   2. Ni msema kweli. Anamwambia Meya kwamba hawataki kucheleweshewa mshahara.
   3. Ni mwenye busara. Anaona haja ya kuwa na akiba ila hawana cha kuweka kwani mshahara ni duni.
   4. Ni mtetezi wa haki. Anamwambia Meya madiwani wamepata nyongeza ila wao wafanyakazi hawana.
   5. Ni mwenye msimamo imara. Anasema kulikotoka pesa za madiwani zao zitoke hukohuko, hakubaliani na Meya.
   6. Ni mwenye mawazo mapevu. Anatambua kuwa kuna ugavi usiofaa wa mali ya umma.
    ( 5 X 1)
    Kutaja-½
    Mfano-½
    Dondoo limetolewa uk. 67
  2. Mtahiniwa aonyeshe namna wanyonge hawatadiki kwa rasilimani za mene huku wenye nguvu wanafaidika. Anaweza pia kuonyesha tofauti za kipato.
   Baadhi ya haja ni:
   1. Nyumba ya Meya inanadhifishwa huku mji umejaa uvundo.
   2. Madiwani kuongezewa mshahara-wafanyakazi hawaongezewi.
   3. Madiwani kutotozwa kodi huku muuza ndizi anatozwa. 
   4. Madiwani wana bima ya matibabu; wafanyakazi hawana.
   5. Madiwani wanaishi kwenye majumba, wafanyakazi wanaishi vibandani.
   6. Kwa Meya kunapikiwa hata mbwa, watu wanakula mizizi na matunda mwitu.
   7. Madiwani wanausafiri, wafanyakazi hawana. 
   8. Meya anajigawia viwanja na kumgawia Bili, wengine hawana. 
   9. Meya anaunda kamati za kulihudumia Baraza ili kuwafaidi wafuasi wake huku wafanyakazi wanakosa hata glavu za kuoshea vyoo. 
   10. Meya anawapeleka wanawe kusomea ng'ambo, wengine wanapata elimu duni. 
   11. Meya anampeleka mkewe kuzalia ng'ambo, wengine wanapata huduma hafifu za kiafya; zahanati haina hata dawa ya kuua vijasumu. Mtoto anakufa kwa kula chakula kibaya.
   12. Meya anampa mhubiri sadaka na hali hawaongezei wafanyakazi mshahara.
   13. Meya, Diwani I na Diwani II wanajilipa ovataimu na hali hawana hata pesa za kuwaongezea wafanyakazi mshahara. 
   14. Meya na madiwani wanapanga njama za kujidumisha mamlakani bila kupanga lolote la kumfaidi raia wa kawaida. Diwani III anawaambia hayo.
   15. Bili,kwa sababu ya akili yake, ameiba fimbo. Meya na madiwani I na II hawafaidiki kutokana na ukosefu wao wa busara.
   16. Waridi anawatarajia wagonjwa kulipia matibabu na hali jamaa yake anapokufa anajiuzulu.
   17. Katiba inampa Meya mamlaka makubwa; madiwani wanalazimika kuuwajibikia uongozi wa Meya kwa kukubaliana na baadhi ya maamuzi hata kama si ya haki.
   18. Meya anatumia entertainment vote yake kujiburudisha yeye na Bili na hali wagonjwa wanakufa kwa ukosefu wa dawa.
   19. Meya anafanikisha kufidiwa kwa mwanakandarasi ili yeye pia afaidike, na hali Baraza halina hata vifaa vya kimsingi vya wanaosafisha mji.
    (15 x 1)
    Kutaja-½
    Mfano-½
 6.  
  1.  
   1. Kufuata ushawishi wa wenye dhambi
   2. Kuandamana na washerati 
   3. Kuandamana na wajeuri 
   4. Kuwasifu waongo
   5. Kuandamana na wafisadi 
   6. Kuwapa nafasi watu wabaya/kuandamana na wabaya 
   7. Kukubali kupembejwa na washerati 
   8. Kufuata njia za wajeuri/kuathiriwa na wajeuri
    (6 x 1)
    Kutaja-½
    Mfano-½
  2.  
   1. Tashbihi 
    • kama mwali
    • kiakili
    • mithili yao mapembe ya fahali
   2. Sitiari
    • ni shubili
    • Kemikali
    •  si Injili
     (2x1)
     Kutaja-1
     Mfano-1
  3.  
   1. Urudiaji wa neno-mwanangu.
   2. Urudiaji wa sentensi/kishazi - mwanangu sikubali
   3. Urudiaji wa silabi -ngu, li
    (2 x 1)
    Kutaja-1
    Mfano-1
  4.  
   1. Idadi ya vipande - Ukawafi - vipande, 3 katika kila mshororo
   2. Mpangilio wa maneno - Kikwamba - neno, mwanangu kuanzia kila mshororo.
   3. Idadi ya mizani - Msuko - kibwagizo ni kifupi. 
   4. Mpangilio wa vina - ukara. Vina vya kati vinabadilika, vya nje vinatiririka
    (4 x 1)
    Kutaja-½
    Mfano-½
  5.  
   1. Inkisari
    • sikuperembe. Wasikuperembe
    •  siwe—usiwe
    • ndo-ndio
   2. Lahaja
    • usifwate - usifuate
    •  hino-hii
    • duniya-dunia 
   3. Udondoshaji maneno
    • ujeuri sera yao - ujeuri ni ndio) sera yao.
     (2 x 1)
     Kutaja-½
     Mfano-½
  6. Mwanangu usiandamane na wafisadi kwani wao ni mfano wa kemikali. Utu wao unaongozwa (wao wanaongozwa na tamaa wala si injili/dini. (Mwanangu) Usikubali kuandamana nao; waambie (wahepe) kila siku.
   (4 x 1)
 7.  
  1.  
   1. Kumthamini mfanyakazi waonapo ana uwezo wa kuwazalishia riziki
   2. Kuwafanyiza kazi ngumu/kwa muda mrefu - kukupindisha mgongo
   3. Kumsifu kiongo-watakwita kwa majina 
   4. Kujinasibisha na wafanyakazi - kumwonyesha mfanyakazi wao ni wamoja; kwa faida ya pamoja.
   5. Kumhadaa mfanyakazi kwa zawadi
   6. Kumshawishi/kumhimiza kuendelea na kazi
   7. Kulipa pato duni/kumpimia kipato
   8. Kumwaminisha wanaweka malengo pamoja ili kuvuta uaminifu wake mfanyakazi
   9. Kumtengenezea kandarasi ya kazi
   10. Kumsukuma ili kufikia shabaha.
    (6 x 1)
  2.  
   1. Sitiari 
    • u chambo
    • ndoana- nyenzo ya kufanyia kazi
    • u nundu
    • u ndovu
    • ukiwa yao makasia
    • dau- nchi
    • miamba matatizo 
   2. Tashbihi
    • kama sahani na kawa.
    • ja fahali
   3. Kinaya - kusifu kiongo, ujira duni kwa kazi nyingi.
   4. Taswira (Taswira mwendo)
    Kukupindisha mgongo- kutesa/kufanyiza kazi nyingi. Picha ya mtu anayeinama/anayeumia.
   5. Tashtiti - shairi zima linawafanyia tashtiti waajiri.
    (3 x 1)
    Kutaja-½
    Mfano-½
  3.  
   1. Inkisari 
    • walo - walio
    • ndo-ndio 
   2. Kufinyanga sarufi
    • ndoana umeshika - umeshika ndoana
    • yenu matarajio - matarajio yenu
    • makoma kuangusha - kuangusha makoma 
    • yao kazi- kazi yao
    • yako thamani- thamani yako
     (2x1)
     Kutaja-½
     Mfano-½
  4.  
   1. We u chombo cha
   2. Kwamba we na wao mu
   3. Watakwonyesha wao
   4. Katika kuyavyaza na
   5. Ambayo ubatizo wake ni
   6. Na usidhani una hiari ya
    (2 x 1)
  5. Mzindushi/mlalamishi mtetezi wa haki/mwajiriwa/mfanyakazi.
   (1 x 2)
   Kutaja - 1
   Mfano-1 
  6. Ya kukashifu/ya uchungu (Na usidhani una hiari ya kuamua ...)
   (1 x 2)
   Kutaja -1
   Maelezo/mfano-1
  7. Ukiwa ndiwe chombo cha kuyafanikisha mambo/ malengo ya mabepari, watakusifu na kukuhimiza uendelee kufanya kazi kuwazalishia mali. Hata hivyo wanakupa ujira mdogo ili usikidhi/ usitosheleza haja zako. Uendelee kuwategemea
   (4x 1)
 8.  
  1. Umuhimu wa Lucy
   1. Anaonyesha ukengeushi - anatamani London kwa kupenda ya fahari yaliyopo
   2. Kuonyesha ndoto ambazo vijana wanazo na ambazo zinawaporomosha- ndoto yake ya London inamsababishia kifo.
   3. Kuendeleza maudhui ya elimu, hafanyi vyema katika mtihani wa kidato cha sita.
   4. Kuendeleza dhamira/suala la uhamiaji ng'ambo. Anatafuta sababu za kumpeleka ng'ambo, anaishia kujifunga kwa mzee mgonjwa ili kukidhi haja yake.
   5. Kuonyesha maudhui ya ubinafsi - anamsaidia Mzee Crusoe ili afaidike. Anapomsaidia hapo sinema, Crusoe anamwahidi zawadi
   6. Kuonyesha kuendeleza maudhui ya tamaa; hataki riziki, anataka muluki.
   7. Kulinganua maishaya Uingereza na huku; serikali ya huko inashughulikia/inawakidhi wasio na kazi.
   8. Kuendeleza maudhui ya ndoa. Anaolewa na Crusoe ili afaidike kwa mali yake.
   9. Kuujenga msuko (ploti) wa hadithi.Kuhudhuriasinema kwake kunabadilisha mkondo wa hadithi. Anaolewa na Crusoe, anaenda London.
   10. Kupitia kwake mwandishi anamjenga mhusika Crisoc. Anaonyesha uwajibikaji wa Crusoe. Anataka kumrithisha kihalali kabla hajafa.
   11. Anaendeleza maudhui ya unafiki. Anasema yeye ni mwanamke mwenye bahati sana ili kumshajiisha Crusoe amrithishe.
   12. Filamu anayotazama inamdokezea/ inamtabiria msomaji yatakayotokea.
   13. Kuonyesha matatizo yanayowakumba vijana. Ukosefu wa nafasi za kazi na matarajio yaliyokiuka mipaka yanamfanya kumhadaa Crusoe kwa mapenzi 
   14. Kunyesha maudhui ya uwajibikaji. Anampa dawa Crusoe kule kwenye sinema.
    (10 x 1)
    Kutaja-½
    Mfano-½
  2.  
   1.  
    1. Ni maneno ya Bi. Kudura.
    2. Anamwambia Bimkubwa. 
    3. Wamo nyumbani mwa Bimkubwa.
    4. Bimkubwa amemuuliza kama ana mwana. 
     4x 1)
     Dondoo limetolewa uk. 115.
   2. Mtahiniwa afafanue makossa ambayo jamii hii imetenda/ Aonyeshe udhaifu wa wahusika mbalimbali katika jamii hii Aonyeshe kwa nini jamii inastahili kusamehewa. Baadhi ya hoja ni: 
    1. Bimkubwa kutomwambia Sudi usuli wake.
    2. Bimkubwa kumwambia Sudi kwamba mumewe alikufa na kumwaminisha kuwa alikuwa na baba.
    3. Bimkubwa anamsababishia Sudi dhiki ya kisaikolojia kwa kutomwambia usuli wake. 
    4. Bi. Kudura anakitupa kitoto chake.
    5. Bi Kudura kutomtafuta mtoto wake awali. 
    6. Sudi alihusiana na Waridi Ulaya lakini amemsahau.
    7. Kupata watoto nje ya ndoa - Bi. Kudura anamzaa Sudi nje ya ndoa.
    8. Mapuuza - vijana kutoona faida ya ujana na kuuthamini (Bi. Kudura anajutia haya).
    9. Japo Bimkubwa alimlca Sudi vyema, hatujaonyeshwa iwapo alimrithi kihalali.
    10. Bi. Kudura anaishi na Sudi kwa muda bila kumwambia yeye ndiye mama yake hadi pale anapoulizwa na Bimkubwa na kuona aibu.
     (6 x 1)
     Kutaja-½
     Mfano-½
Join our whatsapp group for latest updates

Download KCSE 2017 Kiswahili Paper 3 with Marking Scheme.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest