KISWAHILI Paper 3 Questions and Answers - KCSE 2022 Past Papers

Share via Whatsapp

SEHEMU A: RIWAYA
A. Matei: Chozi la Heri

 1. Lazima
  1. "... ni vyema kujifunza kuishi na wenzako bila kujali tofauti za ukoo na nasaba. Elimu inapaswa kuwa chombo cha kueneza amani na upendo wala si fujo na chuki. Mwenzako labda ana hofu kwa vile anaona uhuru wake umeingiliwa. Pengine hata ni mzaha tu..."
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili.(alama 4)
   2. Fafanua umuhimu wa mandhari katika dondoo hili. (alama 6)
  2. Jadili mbinu anazotumia msemaji na wenzake wa jinsia yake katika kukabiliana na matatizo wanayokumbana nayo maishani kwa kurejelea riwaya ya Chozi la Heri.  (alama 10)

SEHEMU B: TAMTHILIA

P. Kea: Kigogo

Jibu swali la 2 au la 3.

 1.  
  1. "Kubali pendekezo letu la kufungwa kwa soko... huoni kuwa hii ni fursa nzuri..."
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
   2. Bainisha mbinu moja ya kimtindo iliyotumiwa katika dondoo hili. (alama 2)
   3. Fafanua umuhimu wa mzungumzaji wa maneno haya katika kuijenga tamthilia ya Kigogo.(alama 8)
  2. Kwa kurejelea hoja sita kutoka kwenye tamthilia, jadili namna kufungwa kwa soko kulivyowaathiri Wanasagamoyo. (alama 6)
 2. Tunu: Jukumu la kulinda uhai. Kulinda haki. Kulinda uhuru. Look at the bigger picture man! Hujasahau mafanikio ya mapambano yetu kama viongozi wa chama cha wanafunzi chuoni? Tulikula kiapo Sudi kuzitetea haki za Wanasagamoyo, hata kama ni kwa pumzi zetu za mwisho baada ya kufuzu.
  1. Changanua mtindo katika dondoo hili. (alama 4)
  2. Jadili jinsi Tunu na wenzake walivyochangia kuleta mabadiliko Sagamoyo. (alama 16)

SEHEMU C: HADITHI FUPI

A. Chokocho na D. Kayanda (Wah.): Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine

Jibu swali la 4 au la 5.

 1. K. Wasike: Mapenzi ya Kifaurongo
  1. "Nikawapuuza. Sasa nimekuja kujua walichomaanisha. Maneno yao yamesibu... Mgomba changaraweni haupandwi ukamea."
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
   2. Bainisha toni katika dondoo hili. (alama 2)
   3. Fafanua sifa sita za mhusika anayesema maneno haya. (alama 6)
  2. Kwa kurejelea hadithi ya Mapenzi ya Kifaurongo, jadili suala la unafiki. (alama 8)
 2. E. Kimaliro: Mtihani wa Maisha
  1. Changanua mtindo katika dondoo lifuatalo: (alama 6)
   "Alasiri. Samueli moyo unamtuta. Mtuto wa moyo unakaribia kampasua kidari. Unamzidishia kiwewe. Yupo kwenye foleni ya wanafunzi hapa. Anasubiri kuingia katika ofisi ya mwalimu mkuu ili kuyaona matokeo yake ya mtihani wa kidato cha nne - matokeo ambayo alitegemea yangelikuwa daraja kati yake na ufanisi na uluwa, matokeo ambayo yangemtoa kabisa kwenye hii jela iitwayo shule na kumwezesha kuanza kuishi badala ya kuwepo tu, ili ajitawanye atakavyo. Arambe tamu ya maisha na awe mtu miongoni mwa watu."
  2. Bainisha mbinu mbili zinazoweza kutumiwa kutambua sifa za mhusika Samueli kwa kurejelea hadithi: "Mtihani wa maisha" (alama 4)
  3. "Ingawa baba yao anayaonea fahari mafanikio ya binti zake, aliwaona wanawake tu."
   1. Taja suala linalodokezwa katika kauli hii. (alama 2)
   2. Kwa kurejelea hoja nne, onyesha namna suala ulilotaja (katika swali la c (i) hapo juu) linavyobainika katika hadithi hii. (alama 8)

SEHEMU D: USHAIRI

Jibu swali la 6 au la 7.

 1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

  Viumbe kukumbukana, ni jambo la mana sana,
  Kwa hali kila namna, mambo tukiambizana,
  Hali tukajuliana, hata tusipoonana,
  Ni jambo la mana sana, viumbe kukumbukana.

  Tusipoweza kunena, kunena ana kwa ana,
  Kwa kuwa tumetengana, kwa marefu na mapana,
  Hatuna budi hatuna, ila kuandikiana,
  Ni jambo la mana sana, viumbe kukumbukana.

  Wangwana hukumbukana, kwa hali kila aina,
  Wakawa wanakazana, pasiwe na kutupana,
  Kwa hali hii naona, alama ya kupendana,
  Ni jambo la mana sana, viumbe kukumbukana.

  Wengine hupigiana, simu wanapopezana.
  Papo wakawa wanena, hapo wanasikiana,
  Hii ni moja namna, ya hali kujuliana,
  Ni jambo la mana sana, viumbe kukumbukana.

  Pakiwa njia hapana, ya hizi mbili aina,
  Yani kuandikiana, na simu kupigiana,
  Ipo moja bora sana, nayo ni kwenda onana,
  Ni Jambo la mana sana, viumbe kukumbukana.

  Sipendi kunena sana, neno likakosa mana,
  Ila la kukumbukana, tusiche kuhimizana,
  Ili kesho wetu wana, wakue wakijuana,
  Ni jambo la mana sana, viumbe kukumbukana.
  1. Fafanua mambo sita ambayo mtunzi anasisitiza katika shairi hili. (alama 6)
  2. Bainisha tamathali moja ya usemi iliyotumiwa katika shairi hili. (alama 2)
  3. Eleza mbinu mbili ambazo mtunzi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 4)
  4. Bainisha bahari ya shairi hili ukizingatia vina. (alama 2)
  5. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2)
  6. Andika ubeti wa sita kwa lugha ya nathari (alama 4)
 2. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

  Namna ya kujikinga, kuiepuka balaa,
  Ni wajibu kujitenga, maovu kuyaambaa,
  Kiburi kinywa kuchonga, si vyema si ushujaa,
  Uogopapo balaa, ndipo litakuepuka.

  Kinywa unapo kifunga, kusema ukinyamaa,
  Kamwe huitwi mjinga, wala huitwi kichaa,
  Kinywa unapo kichonga, wajitakia balaa,
  Uogopapo balaa, ndipo litakuepuka.

  Kando unapo jitenga, pembeni kuchuchumaa,
  Jau kwamba wajikinga, na madhara kukuvaa,
  Kuna kicheko kwa mwoga, kwa mshupavu junaa,
  Uogopapo balaa, ndipo litakuepuka.

  Wametabiri wahenga, wazazi walo tuzaa,
  Kuna kicheko kwa mwoga, kwa mshupavu fadhaa,
  Na moto hudai kinga, bila kinga kukomaa,
  Uogopapo balaa, ndipo litakuepuka.

  Katu hazifai shonga, za watu kukuhadaa,
  Japo kwako awe shoga, na mtu mwenye sifaa,
  Ukiliepuka janga, nalo litakuambaa,
  uogopapo balaa, ndipo litakuepuka.

  Beti sita ninatunga, inafaa kunyamaa,
  Japo upakwe mchanga, na majivu na makaa,
  Jifute upone nzuga, la balaa kukuvaa,
  Uogopapo balaa, ndipo litakuepuka.
  1. Fafanua ujumbe wa shairi hili. (alama 6)
  2. Bainisha tamathali mbili za usemi zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 2)
  3. Andika aina nne za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 4)
  4. Eleza mbinu tatu ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 3)
  5. Bainisha toni ya shairi hili. (alama 1)
  6. Andika ubeti wa nne kwa lugha ya nathari. (alama 4)

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

 1. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali.
  Wabalainga na Waserere walikuwa majirani tangu jadi. Hata hivyo, hawakuonana jicho kwa jicho. Walishambuliana na kuibiana mifugo kwa miaka mingi. Siku moja, Wabalainga walipanga vita kwa siri kama ilivyokuwa kawaida yao. Wazee wao walishauriana usiku wa manane, kisha kuwatolea wapiganaji wa jamii hiyo baraka. Kila mpiganaji aliwekewa mkono kwenye kipaji. Mmoja wao aliwekewa mikono miwili. Huyu aliitwa Kulu, kiongozi wa kundi hili. Kulu alikuwa mrefu wa kimo, mwenye vidole virefu, viganja vinene na kifua kipana akilinganishwa na wenzake. Kila alipopumua, hewa kutoka puani mwake ilitikisa majani kwenye miti. Macho yake nayo yalikuwa ya kupenyeza; angekutazama tu ungehisi anakuona hadi moyoni. Hakukosa kwenda vitani kila wakati vita vilipopangwa. Alikuwa chaguo la kijiji kizima.
  Kabla ya vita kuanza, Kulu alivishwa ngozi ya chui na kichwani kachomekwa unyoya wa mbuni. Mikononi kashika mkuki mkubwa uliotetemesha ardhi kila alipousimika. Safari ilianza hadi kwenye uwanja wa vita. Moja kwa moja vita vilianza, kila upande ukitaka kuonyesha ubabe wake. Ghafla bin vuu Kulu alijitoma mbele ya kikundi chake, akavuta pumzi na alipoiachilia, wapiganaji Waserere walipeperuka hewani wakaelea kisha kuanguka chini pu! Wengi wao hawakupumua tena. Walionusurika walivunjika sehemu mbalimbali za mwili. Papo hapo, Kulu alibebwa juu juu na wapiganaji wenzake kusherehekea ushindi wao.
  1.  
   1. Bainisha kipera cha utungo huu. (alama 1)
   2. Toa sababu tano kuthibitisha jibu la (i) hapo juu. (alama 5)
  2. Bainisha vipengele vitano vya kimtindo ambavyo vimetumiwa kufanikisha uwasilishaji wa utungo huu. (alama 5)
  3. Unanuia kuhifadhi tungo za aina hii. Eleza manufaa matano ambayo jamii yako itapata kutokana na hifadhi hiyo. (alama 5)
  4. Unakusudia kutumia mbinu ya kushiriki kufanya utafiti kuhusu tungo za aina hii. Eleza matatizo manne unayoweza kukumbana nayo katika utafiti wako. (alama 4)

MARKING SCHEME

 1.  
  1.  
   1.  
    1. Haya ni maneno ya Mama Ridhaa.
    2. Anazungumza na mwanaye Ridhaa.
    3. Wako nyumbani kwao eneo la Msitu wa Heri.
    4. Mama Ridhaa anamtuliza mwanaye Ridhaa baada ya kufika nyumbani akilalamikia
     kutengwa na kusingiziwa na wenzake shuleni.         4x1 = 4
     (Dondoo limetolewa ukurasa wa 11)
   2.  
    1. Kubainisha migogoro katika riwaya: mgogoro unaosababishwa na wahusika kubaguana; Ridhaa anabaguliwa na wanafunzi wenzake shuleni.
    2. Kufunza kuhusu mbinu chanya za kusuluhisha migogoro. Mama Ridhaa anamshauri Ridhaa kuhusu umuhimu wa kujifunza kuishi na wenzake.
    3. Kuwatambulisha wahusika; Mama Ridhaa na Ridhaa.
    4. Kuchimuza maudhui, kwa mfano, ubaguzi. Ridhaa anabaguliwa akirejelewa kama Mfuata Mvua na wenzake shuleni.
    5. Kutambulisha sifa za wahusika: Mama Ridhaa anabainika kama mhusika
     anayeonyesha uwajibikaji, ni mshauri.
    6. Kuibua dhamira ya mwandishi: Kudhihirisha njia mojawapo ya utatuzi wa migogoro katika jamii.
    7. Kuendeleza ploti. Kwa mfano, kuturudisha nyuma kwenye tukio la awali.
     Hoja 3 x 2=6
     Kutaja 1
     Kufafanua 1
  2. Msemaji ni Mama Ridhaa. Wenzake ni wanawake katika riwaya ya Chozi la Heri
   1. Mama Ridhaa alisuluhisha tatizo la mwanawe kwa kumrejesha shuleni baada ya kutengwa na wenzake; na kudhamiria kuzungumza na mwalimu.
   2. Selume anasulushisha tatizo la kufanya kazi katika mazingira yasiyomridhisha kwa kutafuta ajira katika kituo cha afya cha Mwanzo Mpya; kazi iliyokuwa bora.
   3. Neema kuamua kupanga mtoto (Mwaliko) baada ya kuwa na tatizo la kutoweza kupata mtoto wake mwenyewe.
   4. Umu kupiga ripoti katika kituo cha polisi kuhusu kutoweka kwa ndugu zake.
   5. Umu kuamua kwenda mjini baada ya Sauna kuwatorosha Dick na Mwaliko, ili kuanza maisha upya.
   6. Umu kumweleza Mwalimu Dhahabu kuhusu upweke aliokuwa nao.
   7. Mwalimu Dhahabu kuchukua hatua ya kumshauri Umu, kumhimiza na kisha kumtafutia familia ya kuishi nayo.
   8. Pete, baada ya kuozwa akiwa na umri mdogo na baadaye kuteswa na mumewe, Fungo, aliamua kutoroka ili aziepuke dhuluma za kimapenzi.
   9. Mwekevu, baada ya kujitosa katika siasa, alivumilia matusi, vitisho na hata kutengwa, hatimaye alishinda uchaguzi na kuwa kiongozi wa Wahafidhina.
   10. Selume kuondokea dhiki za wakwe zake kwa kuwa mkimbizi katika Msitu wa Mamba.
   11. Kairu aliamua kuvumilia maisha magumu ili kuyakamilisha masomo yake.
   12. Lime na Mwanaheri waliamua kuendelea na maisha yao hata baada ya kufanyiwa unyama na vijana wenzao.
   13. Apondi kufanya maamuzi ya kuolewa tena baada ya mumewe kuaga.
   14. Zohali kuamua kutoavya mimba na kuendelea na masomo yake baada ya kutoroka kwao.
   15. Wasichana waliopitia hali ngumu na kukutana shuleni wanasimuliana hali zao ili kuliwazana/ kama njia ya kujiliwaza.
   16. Wasichana (Umu, Kairu, Mwanaheri ...) wanahimizana kuhusu njia za kukabiliana na changamoto maishani.
   17. Chandachema kufanya maamuzi ya kurudi shule.
   18. Baadhi ya wanawake kuwatupa Watoto baada ya kujifungua ili kukwepa majukumu ya ulezi. Kwa mfano, mamake kitoto kilichookotwa na Neema.
   19. Baadhi ya wanawake kujihusisha katika ulanguzi wa Watoto. Kwa mfano, Sauna na Bi. Kangara.
   20. Wanawake wengine wanafanya kazi za kujidhalilisha ili kujikimu. Kwa mfano, Pete kuuza pombe kwenye baa.
   21. Baadhi ya wahusika kutafuta msaada ili kujiendeleza maishani. Kwa mfano, Chandachema.
   22. Baadhi ya wahusika kuingilia uraibu wa vileo ili kujituliza. Kwa mfano, Subira. 
   23. Mamake Sauna kumshurutisha Sauna kuavya mimba ili kujikinga na aibu. Hoja 10 x 1-10
 2.  
  1.  
   1.  
    1. Ni sauti ya Mzee Kenga/ Kenga
    2. Sauti hii inasikika mawazoni mwa Majoka.
    3. Majoka yumo ofisini.
    4. Ni baada ya Husda kumfumania Majoka akiwa na Ashua kisha vurugu na fujo kuzuka baina ya Husda na Ashua.
     Hoja 4 x 1 = 4
     (Dondoo limetolewa uk. 28-29)
   2.  
    • Taswira-kufungwa kwa soko.
    • Mbinu rejeshi - kumbukizi za matukio/ mazungumzo mawazoni mwa Majoka.
     Mdokezo
     Hoja 1x2-2
     Kutaja 1
     Maelezo 1
   3.  
    1. Anaendeleza utawala dhalimu wa Majoka. Anawaamuru Sudi, Boza na Kombe kuchonga kinyago (uk. 9). Anachangia kudhulumiwa kisaikolojia kwa Husda na Ashua.
    2. Kupitia kwake tunatambua suala la taasubi ya kiume. Haamini kuwa Sagamoyo imeshawahi kuwa na mashujaa wa kike. (uk.10)
    3. Anachimuza suala la ubadhirifu wa mali ya umma. Anasema kuwa mradi wa kuchonga kinyago umefadhiliwa kutoka nje (uk. 11).
    4. Anaangaza mbinu hasi za utawala kama vile matumizi ya ushawishi/ vishawishi. Anamshawishi Sudi kuchonga kinyago kwa kumwambia kuwa atapokea malipo na jina lake litashamiri (uk. 11). Anawapa akina Boza keki (uk. 14).
     Anaendeleza matumizi ya vitisho. Anamwambia Sudi auchunge sana ulimi wake (uk. 12).
    5. Kupitia kwake tunatambua suala la kuzorota kwa maadili. Anampotosha Majoka anapomwambia akubali pendekezo la kufungwa kwa soko kama fursa ya kulipiza kisasi
     (uk. 29).
    6. Kupitia kwake tunatambua matumizi ya hila. Yeye na Majoka wanapanga njama ya kumtia Ashua kizuizini kwa madhumuni ya kumshinikiza Sudi kuchonga kinyago (uk. 31).
    7. Anachimuza suala la matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Anasifia kitendo cha polisi kuwafurusha na kuwadhulumu waandamanaji (uk. 31).
    8. Anaendeleza suala la ukatili. Anadhamiria kuwakomesha kabisa wapinzani wa Majoka (uk. 33) (uk. 34).
    9. Ndiye anayechochea na kukuza mgogoro kati ya wahusika. Anamchochea Majoka akubali kufungwa kwa soko ili kulipiza kisasi. Wanapanga njama ya kumtia Ashua kizuizini ili kumshinikiza Sudi kuchonga kinyago.
    10. Anaendeleza ploti anaposhiriki vitendo viovu vinavyowachochea wanaharakati kupanga mikakati ya kupinga uovu; hivyo kuchangia maigizo kufikia kilele chake.
    11. Kupitia kwake tunatambua changamoto zinazowakumba wanandoa. Anachangia katika kuvuruga ndoa kati ya Majoka na Husda na ndoa kati ya Ashua na Sudi.
    12. Kuchimuza sifa za wahusika wengine. Sudi kuwa na msimamo thabiti.
    13. Anaendeleza suala la usaliti. Kwa mfano, anapomuasi Majoka kwa kujiunga na kundi la Tunu.
    14. Anaendeleza maudhui ya unasaba katika uongozi. Ana cheo kwa sababu ni binamuye Majoka.
     Hoja 8 x 1 = 8
     Kutaja ½
     Mfano ½
  2.  
   1. Kufungwa kwa soko kulichangia kuwepo kwa maandamano ya wachuuzi.
   2. Kupanda kwa bei ya chakula kwenye kioski cha kampuni maradufu. (uk. 17).
   3. Wafanyibiashara kukosa maeneo ya kuuzia bidhaa zao, hivyo kuendeleza shughuli zao wakiwa nyumbani.
   4. Wanasagamoyo kukosa pesa za matumizi (uk. 18). Ashua anamwambia Majoka kuwa wengi wao walitegemea soko hilo kuyakidhi mahitaji ya jamii zao (uk. 25).
   5. Kufungwa kwa soko kuliwapa wanaharakati (Tunu na Sudi) mshawasha wa kuendelea kupigania haki za wanyonge (uk. 18).
   6. Kuliwanyima wengi wa Wanasagamoyo mtaji.
   7. Kuzikwa kwa matumaini ya wanasagamoyo. Kuliwapoka utu na heshima yao (uk. 25).
   8. Kulichangia matumizi ya vileo na dawa za kulevya. Ngurumo na wenzake walihamia kwa Mamapima na kushiriki ulevi mchana kutwa (uk. 60), (uk. 62).
   9. Kuliwafanya wengi kuwa watumwa wa utawala wa Majoka. Walishawishika kwa wepesi kuunga mkono utawala dhalimu wa Majoka (uk. 59).
   10. Kuumizwa kwa waandamanaji. Baadhi yao hata wanauawa.
    Hoja 6 x 1-6
    Kutaja /1⁄2
    Mfano 1⁄2
 3.  
  1.  
   1. Uradidi- kulinda uhai, kulinda haki, kulinda uhuru.
   2. Kuchanganya ndimi- Look at the bigger picture man!
   3. Mbalagha/ maswali ya balagha- Hujasahau mafanikio ya mapambano yetu kama viongozi wa chama cha wanafunzi chuoni?
   4. Nahau- Tulikula kiapo.
   5. Chuku- kuzitetea haki za Wanasagamoyo hata kama ni kwa pumzi zetu za mwisho. 
   6. Mbinu rejeshi. Tunu kukumbuka walipokula kiapo.
    Hoja 4 x 1= 4
    (Dondo limetolewa uk. 18)
  2.  
   1. Kukataa vishawishi na hongo.
    Sudi anakataa ushawishi wa Kenga kuwa akichonga kinyago atalipwa vizuri pamoja na likizo ya mwezi mzima ughaibuni. Sudi anakataa kula keki iliyoletwa na Kenga (uk. 13).
   2. Kuwazindua wanajamii wenzao. Sudi anamwambia Boza, "Sagamoyo ni kwenu, sherehe ni zenu, ufanisi ni wenu na keki kubwa ni ya kina nani?" (uk 14). Kumfanya Boza atambue kuwa wanadhulumiwa.
   3. Kushiriki katika maandamano. Wachuuzi sokoni wanashiriki katika maandamano yaliyoandaliwa na Tunu na Sudi (uk 16).
   4. Migomo Walimu wanagoma ili kudai haki zao.
   5. Kupinga/kukashifu vitendo viovu - Ashua anakataa kufanya kazi kwenye shule ya Majoka and Majoka Academy Anasema, "Wanafunzi katika shule hizo zako hawafuzu. Wanaishia kuwa makabeji kwa kudungana sumu ya nyoka" (uk. 26).
   6. Tunu na Sudi kuwashirikisha wanaharakati katika maandamano ili kupigania haki za Wanasagamoyo (uk. 32).
   7. Matumizi ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhamasisha umma. Runinga ya Mzalendo ilipeperusha hotuba ya wanaharakati. Pia ilitoa habari kuhusu maandamano yaliyoongozwa na Tunu na Sudi (uk. 37).
   8. Kuukabili utawala na watawala waliopo mamlakani. Tunu anasema, "Mtalipa kila tone la damu mlilomwaga Sagamoyo..." (uk. 43).
   9. Kutokata tamaa. Tumu anaendeleza harakati za kupigania haki za Wanasagamoyo hata baada ya kupigwa (uk. 55).
   10. Kuwepo kwa umoja na ushirikiano baina ya wapiganiaji haki. Siti anamtembelea Tunu baada ya Tunu kuvamiwa (uk. 55). Tunu anamtaka Siti ampeleke kukabiliana na majangili waliomvamia.
   11. Kuandaa mkutano mbele ya soko la Chapakazi siku ya maadhimisho ya uhuru kwa madhumuni ya kuwazindua na kuwakomboa Wanasagamoyo (uk. 59). Tunu anawaalika vijana kwenye mkutano huo.
   12. Kuwasamehe wanaojutia makosa yao na kuomba msamaha. Tunu anampokea Mamapima baada ya Mamapima kuwaomba Wanasagamoyo msamaha kwa maovu aliyowatendea (uk. 92).
   13. Tunu kuwahimiza wenzake. Anamsihi Sudi waendeleze harakati za ukombozi.
   14. Tunu kutishia kuwaleta wachunguzi kutoka nje ili kuchunguza kifo cha Jabali
   15. Tunu kukataa kuozwa kwa Ngao Junior kuliwafanya Waanasagamoyo kumwamini zaidi.
   16. Tunu na wenzake wanasomea uanasheria hivyo kuwazindua Wanasagamoyo.
   17. Ashua kukataa kushiriki mapenzi na Majoka hivyo kudumisha maadili katika jamii.
   18. Sudi kuchonga kinyago cha shujaa halisi (wa kike) hivyo kubadilisha mtazamo wa baadhi ya Wanasagamoyo kuhusu jinsia ya kike.
    Hoja 8 x 2-16
    Kutaja 1
    Mfano 1
 4.  
  1.  
   1.  
    1. Msemaji ni Penina.
    2. Anamwambia Dennis.
    3. Wako nyumbani kwao katika mtaa wa New Zealand.
    4. Ni baada ya Dennis kurejea na kumjuza Penina kuwa hakupata kazi. Penina anajutia kuchumbiwa na Dennis.
     Hoja 4 x 1= 4
     (Dondoo limetolewa uk. 26-27)
   2. Majuto
    Hasira
    Majivuno
    Hoja 1 x 2 = 2
    (Dondoo limetolewa uk. 26)
   3.  
    1. Mwenye huruma - Anamhurumia Dennis anapomwelezea hali yake
    2. Jasiri - Anamkabili Dennis na kumweleza hisia zake.
    3. Mwenye mapenzi ya kuyumbayumba.
    4. Mnafiki - Anasema kuwa penzi lao litadumu ilhali anamfukuza Dennis anapokosa ajira.
    5. Kigeugeu-Anasema hawezi kuolewa na mwanamume asiye na mshahara mkubwa ilhali anaishi na Dennis. Anamgeuka Dennis anapokosa ajira.
    6. Mwenye dharau. - Anapuuza kuwepo kwa Dennis sebuleni. Anamdunisha Dennis. Anamfukuza Dennis kwake kwa dharau.
    7. Mpyoro/ mpyaro/ mwepesi wa kutusi. Anamwambia Dennis aache ubwege.
    8. Asiye mstahimilivu/ hana subira/ hana stahamala. Anachoshwa haraka na ugumu wa hali ya maisha.
    9. Mwenye majuto - Anajutia kutowasikiliza wazazi wake kuhusu kuchumbiwa na Dennis.
     Hoja 6 x 1-6
  2.  
   1. Dennis kusema kuwa hajui lolote kuhusu mapenzi ilhali anamwambia Penina kuwa katika mapenzi kuna kuaminiana, kuheshimiana na kusaidiana (uk. 20).
   2. Penina kusema kuwa anampenda Dennis kwa dhati na angependa wawe wapenzi wa kufaana kwa jua na kwa mvua ilhali anamfukuza Dennis anapokosa ajira (uk. 20, 27).
   3. Penina kukubali kuchumbiwa na Dennis asiyekuwa na lolote kisha kukiri kuwa hawezi kuolewa na mwanamume asiye na kazi yenye mshahara mkubwa.
   4. Afisa aliyemwambia Dennis aingie ofisini anasema kuwa anaamini Dennis ataipata kazi hiyo ilhali hasemi lolote kuhusu tajiriba ya Dennis wakati wa mahojiano.
   5. Penina kusema kuwa amechoshwa na Dennis na kumwambia kuwa alimpenda akidhani kuwa angepata kazi ilhali awali alisema anampenda kwa dhati.
   6. Daktari Mabonga kumwita mwanafunzi kwa jina la heshima na baadaye kumdhihaki kuhusu swali analouliza. Anakashifu majibu ya wanafunzi
    Hoja 4 x 2 = 8
    Kutaja - 1
    Mfano - 1
 5.  
  1.  
   1. Chuku - Mtuto wa moyo kukaribia kumpasua kidari/ Kulinganisha shule na jela.
   2. Taswira 
    • Mtuto wa moyo
    • kuishi badala ya kuwepo
    • foleni ya wanafunzi
   3. Taharuki - Samueli kusubiri kuyapokea matokeo yake ya mtihani.
   4. Tashihisi - matokeo kumtoa katika jela iitwayo shule
   5. Sitiari-shule kuitwa jela, matokeo kuwa daraja/ tamu ya maisha
   6. Nahau-pasua kidari, arambe tamu.
   7. Takriri- matokeo, ambayo
   8. Msemo ame mtu miongoni mwa watu. (viii) Kejeli-shule kuitwa jela
   9. Kinaya- anataka kuwa mtu na hali ni mtu
   10. Utohozi- ofisi
    Hoja 6 x 1-6
    (Dondoo limetolewa uk.131)
  2.  
   1. Ayasemayo mhusika - Samueli anasema, "Mwa...limu... Mwa...limu nimekuja kuchu...chukua matokeo..." Inaashiria kuwa Samueli ni mwoga.
   2. Matendo ya mhusika - kutaka kujitoa uhai - mwenye kutamauka.
   3. Wayasemayo wahusika wengine-maneno ya babake Samueli yanaashiria fadhaa.
   4. Maelezo ya mwandishi/ msimulizi Samueli anaposubiri kuingia ofisini mwa mwalimu mkuu - mwoga- anaingia ofisini jasho likimtoka.
    Hoja 2x2-4
    Kutaja alama 1
    Mifano alama 1
  3.  
   1.  
    1. Taasubi ya kiume
    2. Udhalilishaji wa jinsia ya kike
    3. Kudunushiwa kwa jinsia ya kike
     1x2=2
     (Dondo limetolewa uk. 136)
   2.  
    1. Fahari ya dhati ya babake Samueli ni kumwona mwanawe wa kiume akifua dafu (uk. 136).
    2. Babake Samueli kusadiki kwamba pindi mabinti wakiolewa hana satua tena juu yao na matumizi yao ya fedha zao.
    3. Mtoto wa kiume kuwa mwenye kudumisha jina la ukoo wa babake.
    4. Samueli kushangazwa na dada zake kumshinda.
    5. Ingawa babake Samueli aliyaonea fahari mafanikio ya binti zake, aliwaona wanawake tu.
    6. Mtoto wa kiume ndiye tegemeo la jamii.
     Hoja 4x2=8
 6.  
  1.  
   1. Ni muhimu waja kukumbukana.
   2. Ni muhimu kuwasiliana.
   3. Kujuliana hali hata bila ya kuonana.
   4. Kuandikiana barua iwapo wametengana.
   5. Kupigiana simu.
   6. Kutembeleana ili kuonana.
   7. Kujuana kiukoo.
   8. Kukumbatiana ni ishara ya kupendana.
   9. Ni muhimu waja kusaidiana.
    Hoja 6 x 1=6
  2. Nahau
   • ana kwa ana
   • hatuna budi
   • kujuliana hali
    Hoja 1 x 2-2
    Kutaja alama 1
    Mifano alama 1
  3.  
   • Inkisari mana-maana/ onana-kuonana
   • Kuboronga sarufi - hii ni moja namna - hii ni namna moja
    mambo tukiambizana - tukiambizana mambo
    ili kesho wetu wana -  ili wana wetu kesho
    Hoja 2x2=4
    Kutaja alama 1
    Mifano alama 1
  4. Mtiririko
   Vina vya kati ni 'na'
   Vya mwisho ni 'na'
   Vina vya kati na vya mwisho vinafanana.
   Hoja 1 x 2-2
   Kutaja 1
   Maelezo 1
  5. Anayetoa wasia/ wosia
   Anayewashauri wengine    2x1-2
  6. Sipendi kuzungumza sana, niyasemayo yasikose maana. Tuendelee kuhimizana kuhusu manufaa ya kujuliana hali na kukumbukana ili wana wetu wakue wakifahamiana. Ni muhimu viumbe wakumbukane.
   4x1 = 4
 7.  
  1.  
   1. Ni vyema kuepukana na balaa.
   2. Kunyamaza si ishara ya kuwa mjinga.
   3. Unapotumia maneno vibaya unajitakia balaa.
   4. Kujitenga na balaa ni kujikinga na athari zake.
   5. Watu wenye hekima wametabiri suala la hekima kwa miaka mingi.
   6. Balaa haifai, ni vyema kuiepuka.
   7. Hata ukitukanwa au kuchokozwa ni vyema kutojiingiza katika balaa. (viii) Usihofishwe na maneno ya watu wanaokusudia kukuhadaa.
    6x1 = 6
  2.  
   1. Tanakuzi - kusema ukinyamaa
   2. Tabaini - si vyema, si ushujaa.
   3. Tashihisi - na madhara kukuvaa, uogopapo balaa, ndipo litakuepuka.
   4. Sitiari-japo upakwe mchanga - kuchafuliwa jina.
    2x1 = 2
  3.  
   1. Urudiaji sauti 'a' katika balaa, kuyaambaa.
   2. Urudiaji silabi nga' katika kujikinga, kujitenga, kuchonga.
   3. Urudiaji neno
    • ubeti wa 1-balaa
    • ubeti 3, ubeti 4 - mshupavu
   4. Urudiaji kauli - ubeti 3, ubeti 4 - kwa mwoga
   5. Urudiaji wa sentensi - kibwagizo - uogopapo balaa, ndipo litakuepuka
    4x1 = 4
  4.  
   1. Kuboronga sarufi
    • maovu kuyaambaa- kuyaambaa maovu
    • Kiburi kinywa kuchonga- kinywa kuchonga kiburi
    • Kando unapo jitenga- unapojitenga kando
   2. Kutenganisha maneno - unapo jitenga - unapojitenga
                                          - unapo kichonga - unapokichonga
   3. Inkisari-walotuzaa- waliotuzaa
   4. Tabdila - Jau-Jua
   5. Mazida-kukomaa -- kukoma
    3x1=3
    Kutaja 1⁄2
    Mfano 1⁄2
  5. wosia/ ushauri    1x1 = 1
  6. Wahenga na wazazi wetu wametabiri kwamba kwa mwoga huenda kicheko. Kwa shujaa huenda mahangaiko. Bila ya kuni moto hauwezi kuwaka. Unapojitenga na mabaya hutapatwa nayo.
   4x1-4
 8.  
  1.  
   1. Mighani     1x1 = 1
   2.  
    1. Kuwepo kwa matukio ya kihistoria. Ujirani kati ya Wabalainga na Waserere ulikuwepo tangu jadi.
    2. Kupigwa chuku kwa matukio. Wapiganaji Waserere kupeperuka hewani na kuelea.
    3. Matendo ya mhusika kupigwa chuku. Kulu angeweza kupumua na pumzi yake kutikisa majani ya miti. Mkuki wa Kulu kutetemesha ardhi uliposimikwa.
    4. Maumbile ya nguli si ya kawaida. Kulu alikuwa mrefu wa kimo, mwenye vidole virefu, viganja vinene na kifua kipana.
    5. Kuwepo kwa motifu ya safari. Kulu na wenzake walisafiri hadi kwenye uwanja wa vita.
    6. Kutambuliwa/ kuwepo kwa shujaa wa vita. Kulu alitambuliwa na jamii yake kama shujaa wa vita. Wazee walimwekea mikono miwili kipajini.
     Hoja 5x1=5
  2.  
   1. Nahau - alijitoma mbele
   2. Taswira 
    • wazee wakishauriana usiku wa manane.
    • wapiganaji wakiwekewa mikono. maumbile ya Kulu.
   3. Chuku 
    • maelezo kuhusu maumbile ya Kulu.
    • hewa kutoka pwani mwa Kulu kutikisa majani kwenye miti.
   4. Tashihisi - macho ya Kulu kupenyeza
   5. Sitiari
    • ngozi ya chui - ubabe wa Kulu.
    • unyoya wa mbuni kichwani - kiongozi.
   6. Tanakali za sauti -kuanguka chini Pu!
   7. Tasfida wengi hawakupumua tena.
    5x1=5
    Kutaja 1⁄2
    Mfano 1⁄2
  3.  
   1. Jamii itahifadhi kitambulisho chake kwa kuwa mighani ni kitambulisho chake.
   2. Historia ya jamii itaweza kuhifadhiwa kama kumbukumbu.
   3. Historia ya jamii itaweza kupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
   4. Kung'amua mbinu namna ya kuwatambua mashujaa katika jamii.
   5. Jamii itaweza kukuza uzalendo kwa kuiga wahusika (mashujaa) na matendo ya wahusika.
   6. Kupitisha thamani na amali za jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
   7. Jamii wanajamii wataburudishwa na masimulizi ya tungo hizo.
   8. Kuhimizwa kwa ujasiri na kutokata tamaa miongoni mwa wanajamii kutokana na ujasiri wa wahusika na matendo ya kishujaa.
   9. Kuhimiza ushirikiano miongoni mwa wanajamii.
   10. Kuziba pengo la utafiti.
   11. Kuhifadhi utamaduni.
   12. Kurekebisha mtazamo potovu.
    Hoja 5 x 1 = 5
  4.  
   1. Kutoaminiwa miongoni mwa jamii unayotafitia hivyo kukosa data unayotafitia.
   2. Muda mrefu hutumiwa katika kutafiti.
   3. Mtafiti anaweza kutekwa makini ya yaliyomo hivyo asitafiti vikamilifu.
   4. Changamoto za uchanganuzi wa data ya utafiti wa aina hii
   5. Ni ghali. Mtafiti huenda akahitajika kusafiri mbali, vifaa kuwa ghali au kutokuwepo kwa nguvu za umeme.
   6. Kuwepo kwa changamoto za kitamaduni, mila na desturi ikiwa mtafiti anatafitia jamii yenye utamaduni tofauti na wa mtafiti
    Hoja 4 x 1 = 4
Join our whatsapp group for latest updates

Download KISWAHILI Paper 3 Questions and Answers - KCSE 2022 Past Papers.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?