Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Cekenas Mock Exams 2022

Share via Whatsapp

MASWALI

 1. SEHEMU YA A :USHAIRI
  LAZIMA.

  Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali
  Kiapo kwao majaji, wanosimamia haki
  Kwa sharia ni magwiji, wahalifu hawatoki,
  Wengi wao ni walaji, kwa rushwa ni mashabiki,
  Kwa rushwa mashabiki.
  Kiapo kwa daktari, wagonjwa hawadhiliki,
  Kazi zao ni dhariri, maradhi hayakwepeki,
  Na wengine ni hatari, bila pesa hutibiki,
  Bila pesa hutibiki.
  Kiapo cha mawaziri, kwa mbwembwe na itifaki,
  Na suti zao nzuri, shingo tai haitoki,
  Na wengi wana dosari, ni kwa mikataba feki,
  Ni kwa mikataba feki.
  Kiapo cha magavana, mikoa kuimiliki,
  Hujifanya ni mabwana, wala hawasogeleki,
  Nayo nchi huitafuna, na kuwa haikaliki
  Na kuwa haikaliki.
  Kiapo cha maraisi, kwa mizinga na fataki
  Na wageni mahususi, hualikwa kushiriki,
  Ikulu wakijilisi, kwa wizi hawashikiki
  Kwa wizi hawashikiki.
  Viapo vya utiifu, kwa sasa havistahiki
  Wanoapa ni wachafu, tena hawaaminiki,
  Biblia misahafu, washikapo unafiki
  Washikapo unafiki
  1. “Dhamira ya shairi hili ni kushtumu ukiukaji wa maadili ya kikazi.” Fafanua. (alama 3)
  2. Eleza namna vipengele vifuatavyo vya kimtindo vilivyotumika katika shairi hili.
   1. Usambamba (alama 2)
   2. Aina za taswira (alama 3)
  3. Bainisha toni katika shairi hili. (alama 2)
  4. Fafanua mbinu mbili alizotumia mshairi kutosheleza mahitaji ya kiarudhi katika shairi hili. (alama 4)
  5. Ainisha bahari kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo; (alama 3)
   1. Mpangilio wa vina
   2. Mizani
   3. Mpangilio wa maneno
  6. Fafanua muundo wa shairi hili. (alama 3)
 2. SEHEMU YA B
  RIWAYA : CHOZI LA HERI – Assumpta Matei
  Jibu swali la 2 au la 3

  ‘‘Nakumbuka asubuhi ya pili baada ya mtafaruku kuanza. Nilikuwa sebuleni na mwanangu tukitazama runinga.’’
  1. Eleza muktadha wa dondoo hii. (alama 4)
  2. Eleza nafasi ya msemaji katika kuwakuza wahusika wengine riwayani. (alama 5)
  3. Tambua mbinu kuu ya kimtindo iliyotumika katika dondoo hili. (alama 1)
  4. Eleza jinsi mbinu uiliyotaja hapo juu (c) ilivyotumika kukuza maudhui riwayani.(alama 10)
   AU
 3. ‘‘Mama mtu alikuwa ameamua kwamba hapa hapamweki tena. Alikuwa amehudumu katika afisi za umma kama mhazili mwandamizi kwa miaka mingi mpaka kazi hii akaiona inamfanya kusinya, hana hamu tena.’’
  1. Eleza umuhimu wa mrejelewa katika kukuza riwaya ya Chozi la Heri. (alama 4)
  2. Huku ukitoa mifano jadili changamoto zinazokumba asasi ya ndoa kwa mujibu wa riwaya ya Chozi la Heri. (alama 8)
  3. Jadili umuhimu wa mandhari katika kuijenga riwaya ya Chozi la Heri kwa kurejelea:
   1. Shule ya Tangamano. (alama 4)
   2. Hoteli ya Majaliwa. (alama 4)
 4. SEHEMU YA C
  TAMTHILIA: P.Kea-Kigogo
  Jibu swali la 4 au la 5
  ‘‘Dalili ya mvua ni mawingu, lazima tuwe macho’’
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
  2. Bainisha vipengele vitatu vya kimtindo. (alama 3)
  3. Fafanua umuhimu wa mzungumzaji katika kuvijenga vipengele vifuatayo vya tamthilia hii.
   1. Ploti (alama 5)
   2. Maudhui (alama 5)
   3. Wahusika wengine (alama 3)
    AU
 5. ‘‘Dunia ni mwendo wa ngisi… ilikuwa haki yangu unilipie karo…
  1. Fafanua muktadha wa maneno haya. (alama 4)
  2. Eleza sifa nne za mzungumzaji. (alama 4)
  3. Thibitisha kwa kutoa mifano kumi na miwili kuwa maisha ya anayezungumziwa yametawaliwa na dhuluma. (alama 12)
 6. SEHEMU YA D
  HADITHI FUPI: Tumbo lisiloshiba na hadithi nyingine.
  Jibu swali la 6 au la 7

  “Hiyo ni dharau ndugu yangu, kwa nini kila siku tunakula sisi kwa niaba ya wengine”.
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
  2. Fafanua sifa za msemaji . (alama 4)
  3. Tathmini vile viongozi wanavyokuwa wabadhirifu. (alama 10)
   AU
 7. Nadhani kicheko chake kiliwaambukiza wenzangu maana vicheko vya nguvu viliwapasuka pamoja. Kama unavyoona, hivi vilikuwa vicheko vya mzaha na utani. Miongoni mwetu sote, Kazu alicheka zaidi. Alicheka kicheko mpaka mbavu zikamtafuna. Na alipocheka basi, alicheka kwa nanma ya ajabu iliyonifurahisha sana. Alicheka huku ameviringa ngumi mbele ya kinywa kama ambaye anazuia hicho kicheko chenye nguvu za kutoa mwangwi uliosafiri robo dunia. Isitoshe, alipocheka namna hiyo, alijirusharusha kitini na kujivuta nyuma kwenye mgongo wa kiti na kuinua miguu yake mpaka soli za viatu vyake zikaonekana. Kumtazama Kazu akicheka ni namna ya kituko. Kila siku nikiwa naye, mimi huhakikisha kwamba namchekesha kwa mzaha huu na ule ili nimwone namna anavyocheka. Hata hivyo, yeye naye hakuwa mchekeshaji mdogo.
  “Aaa, hadithi za kichawi Kazu, ziko kila pahala duniani,” nilimwambia kwa kujitetea. “Unakumbuka mkasa maarufu hapa penu wa chatu lililotambaa kutoka Mashariki hadi Magharibi huku limemeza maelfu ya watu tumboni? Lilisafiri kwa masafa ya zaidi ya kilomita mia tano hivi na kuwatema watu hao huko Magharibi!”
  1. Changanua mbinu za kimtindo katika kifungu hiki. (alama 8)
  2. Fafanua aina nne za taswira kwa kurejela kifungu hiki. (alama 4)
  3. Onyesha Umuhimu wa mandhari ukirejelea clabu Pogopogo (alama 8)
 8. SEHEMU E :FASIHI SIMULIZI
  Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
  Walisema waliosema
  Kitali hakina macho
  Huvizia wapendwa
  Kikafakamia
  Kwenye kinywa kisochoka
  Kwa mara nyingine hasidi
  Ametudhalilisha
  Amewapapu kutisha wanetu
  Majagina kupiga busu la sime
  Jeshi letu sasa ni mateka
  Wasaliti wamewapa mahasimu
  Cheko la kutucheka
  Nii kilio ni kilio ni kilio tangamano
  1. Tambua utanzu na kipera cha kifungu hiki. (alama 2)
  2. Eleza toni ya kifungu hiki. (alama 2)
  3. Eleza sifa sita za kipera kinachorejelewa. (alama 6)
  4. Fafanua majukumu ya kipera hiki katika uwasilishaji wa ngano. (alama 10)


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

 1.        
  1.    
   1. ukiukaji wa maadili ya kikazi
   2. majaji wanaostahili kutetea haki ni walaji rushwa
   3. madaktari hawawajibiki kwa matibabu na kuwa’ magonjwa hayatibiki
   4. madaktari wanakwerida kinyume na kiapo chao kwa kuweka pesa mbele.
   5. Licha ya mbwembwe nyingi za kiapo cha mawaziri, wana mikataba ghushi.
   6. Magavana wanatafuna nchi na kuwa haikaliki.
   7. Viongozi ni wanafiki hawaaminiki.
   8. Maraisi wanashabikia wizi.
   9. Waapaji ni wanafiki Zozote 3 x 1 =3
  2.           
   1.    
    • usambamba
    • Kila ubeti unaanza kwa neno kiapo
    • Sehemu ya utao ya mshororo wa tatu katika kila ubeti inarudiwa katika kimalizio
     alama 2 x 1 =2
   2.    
    • Taswira oni— kiapo cha mawaziri, shingo tai haitoki
    • Taswira sikivu- kwa mizinga na fataki
    • Taswira mwonjo- wengi wao ni walaji alama 3 x 1 = 3
  3. toni katika shairi
   1. Kulalamika- kuna ukosefu wa uwajibikaji kazini
   2. Kushtumu/ kusuta- majaji wanaostahili kutetea haki ni walajirushwa 1×2=2
  4. idhini/ uhuru wa mshairi
   1. Utohozi- feki
   2. Kuboronga sarufi- shingo tai haitoki
   3. Inkisari- wanosimama- wanaosimama alama 2x2=4
  5.      
   1. Mpangilio wa vina- ukara- vina vya nje vinatiririka ilhali vya ndani vinabadilika badilika
   2. Mizani- msuko- kimalizio kimefupishwa
   3. Mpangilio wa maneno- kikwamba- neno kiapo limetumika kuanzia mwanzo wa kila ubeti.
    Pindu- sehemu ya utao ya mshororo wa tatu katika kila ubeti inarudiwa katika kimalizio 3x1=3
  6.      
   1. shairi hili lina beti tano
   2. kila ubeti una mishororo minne
   3. lina pande mbili; ukwapi na utao
   4. kituo kimefupishwa
   5. vina vya nje vinatiririka ilhali vya ndani havitiririki
   6. mizani 16 kwa kila mshororo ila kwa kituo ni nane. Zozote 3x1=3
 2. “Nakumbuka asubuhi ya pili baada ya mtafaruku kuanza. Nilikuwa sebuleni na wanangu tukitazama runinga. (uk.20)
  1.      
   1. Msemaji ni Kaizari
   2. Msemewa ni Ridhaa
   3. Walikuwa katika kambi la wakimbizi.
   4. Kaizari alimsimulia Ridhaa kadhia zilizotokea baada ya uchaguzi (4 x 1= 4)
  2. Msemaji ni Kaizari
   1. Ametumika kuonyesha jinsi ukimbizi ulivyovunja hadhi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha. Anaonekana aking’ang’ania chakula na wakimbizi wengine.
   2. Anawasilisha matatizo yanayowakumba Lime na Mwanaheri kambini. Wao wanapigwa na matone ya mvua kwa kukosa makazi.
   3. Anaonyesha mabadiliko ya kiwajihi yaliyomkumba Subira baada ya kuvamiwa. uk. 16
   4. Ametumiwa kubainisha malalamishi ya Tetci kuhusu ubaguzi unaoendelezwa dhidi ya wanaume.
   5. Ametumiwa kubainisha bidii za Mwekevu. Mwekevu alijitosa kwenye uga wa siasa na kuomba kura kama walivyofanya wanaume.
   6. Ametumiwa kuonyesha ukatili wa kijana aliyevalia shati lililoandikwa ‘Hitman’. Analirushia bomu la petrol gari lililokuwa likipinduka kana kwamba alikuwa akinyunyizia viwavi dawa.
   7. Anaonesha utu wa mhusika Tulia. Tulia alienda kwa nyumba ya Kaizari ili kuwaokoa wakati wa uvamizi.
   8. Ametumia kuonyesha umaskini uliomkumba Makiwa na wenzake katika Mtaa wa Sombera.
   9. Ametumiwa kusawiri tabia ya ufisadi ya Bwana Kute. Bwana Kute anatumia ujanja ili kupata mafungu zaidi ya vyakula vya msaada . zozote 5 x 1 =5
  3.      
   1. Tambua mtindo uliotumika katika dondoo hili. (alama1)
    Mbinu rejeshi: Msimulizi anasimulia matukio yaliyotukia awali. (1×1=1)
   2. Eleza jinsi mbinu uliyotaja katika (c) (i) ilivyotumika kukuza maudhui riwayani. (alamal0)
  4. Kupitia mbinu rejeshi maudhui yafuatayo yanakuzwa:
   1. Ushirikina — Ridhaa anakumbuka matukio kama vile: kupepesa kwa jicho lake Ia kulia kwa muda wa wiki mbili mtawalia, kuanguka kwake bila kuona kilichomkwaa na jeshi la kunguru lililotua katika paa la maktaba yake. Aidha, anakumbuka milio ya kereng’ende na bundi usiku. Matukio hayo yote ni ishara ya mambo mabaya ambayo yangetokea.
   2. Ubabedume — Ridhaa anakumbuka maneno ya marehemu mama yake kuwa unyonge haukutunukiwa majimbi bali makoo (Uk. 3).
   3. Usaliti — Kedi, ambaye alikuwa jirani ya Ridhaa, anamsaliti Ridhaa kwa kuteketeza jumba lake pamoja na jamaa zake.
   4. Uharibifu wa mali — jumba la Ridhaa linateketezwa. Aidha, mahindi katika shamba la Ridhaa yanateketezwa.
   5. Mauaji/ukatili — Terry, Lily Nyamvula, Annatila na Becky wanauawa baada ya nyumba yao kuchomwa moto.
   6. Vita — Mwangeka alikuwa ameenda kudumisha amani katika Mashariki ya Kati.
   7. Ukoloni mamboleo — Hata baada ya uhuru, mmiliki wa mashamba ya Theluji Nyeusi ni mlowezi maarufu. Aidha, Myunani anayamiliki maekari na maekari ya mashamba katika eneo la Kisiwa Bora ambapo wenyeji wamegeuzwa kuwa maskwota.
   8. Utegemezi — Kwa mujibu wa Tila, wenyeji hawana mashamba wanategemea wageni kwa vyakula na ajira.
   9. Udhalimu — sheria za kikoloni zilimpa Mzungu kibali cha kumiliki mashamba katika sehemu zilizotoa mazao mengi. Hali hii iliwalazimu Waafrika kama Msubili kuwa maskwota au vibarua katika mashamba ya wakoloni.
   10. Utumwa — vijulanga vilinyakuliwa kutoka kwenye susu zao, hata vifua havijapanuka; na kupelekwa katika maeneo mbalimbali kufanya kazi.
   11. Upangaji uzazi — Mwimo Msubili alikuwa na watoto wa kiume ishirini. Hivyo, ardhi iligawanywa hadi haingewatosha tena. Aidha, Msubili anakabiliwa na changamoto ya kuwalisha wanawe wengi.
   12. Mgogoro katika familia — Wingi wa vinywa vya kulishwa katika familia ya Msubili ulizua mgogoro, uhasama na uhitaji mkubwa.
   13. Ubaguzi — Ridhaa anatengwa na wanafunzi wenzake kwa kuwa walimwona kama Mfuata Mvua.Hawakumchukulia kuwa, alikuwa mmoja wao.
   14. Elimu — Mamake Ridhaa anatilia mkazo umuhimu wa elimu. Anadai kuwa, elimu inapaswa kuwa chombo cha kueneza amani na upendo.
   15. Uhasama wa kisiasa unasababisha kuvunjika kwa ujirani — Kedi ndiye aliyemtafutia Ridhaa shamba alilolijenga. Aidha, Ridhaa alidhamini masomo ya wapwa wake wawili. Hata hivyo, Kedi anashiriki katika mauaji ya jamaa za Ridhaa.
   16. Vitisho — vikaratasi vilisambazwa kuwatahadharisha akina Ridhaa kuwa, kuna gharika baada ya kutawazwa kwa Musumbi (kiongozi) mpya.
   17. Unyakuzi wa ardhi — baadhi ya mabwanyenye wanajenga majumba mahali ambapo pametengwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara. Mengine yalijengwa chini ya vigingi vya nyaya za stima.
   18. Ufisadi — kuna mabwanyenye ambao wanaonekana wakitoa milungula hadharani.
   19. Ndoa- kwamba si wanawake pekee watesekao katika ndoa. Kuna wanaume ambao wanateseka kutokana na mapigo na dhuluma za kisaikolojia kutoka kwa wake zao (uk.17).
   20. Mabadiliko — wimbi la mabadiliko liliwakumba Wahifidhina kisiasa ambapo mwanamke anachaguliwa kama kiongozi kinyume na ilivyokuwa hapo awali.
   21. Umuhimu wa vyombo vya dola — vyombo vya dola vilitumwa ili kudumisha usalama katika vijiji na mitaa.
   22. Wizi — wengine waliingia katika maduka ya Kihindi, Kiarabu na hata ya Kiafrika na kupora walichoweza kubeba. (Zozote 10 x 1=10)
 3.    
  1. Umuhimu wa mrejelewa; (Annete-mkewe kiriri) (lazima amtaje)
   1. Kielelezo cha malezi mabaya-aliwanyima watoto wake ushirika na babake
   2. Anaonyesha ubinafsi-anahamia ughaibuni na kumwacha mumewe anayeaga dunia kutokana na kihoro
   3. Anaonyesha usaliti anapomwacha mumewe,
   4. Kuonyesha mgogoro katika ndoa
   5. Anyaonyesha ukengeushi anapovutiwa na inchi ya ughaibuni na kuiona bora kuliko nchi yao
   6. Anaonyesha uhusiano uliopo baina ya wazazi na wanao
   7. Anaonyesha madhara ya kuvunjika kwa ndoa
   8. Anachimuza sifa/tabia za Kiriri
    (Zozote 4 x 1 = 4)
  2. Changamoto zinazokumba asasi ya ndoa
   1. Vifo - Terry, Lilly
   2. Ukosefu wa watoto — Mwangemi na Neema
   3. Ukabila/ ukoo — Lucia, Subira, Selume
   4. Wazazi kukataa wanao kuolewa — Rehema
   5. Ukosefu wa uaminifu — Bw. Tenge
   6. Chuki Pete kuonewa na wake wenza
   7. Vita katika ndoa — mamake Sauna anadhulumiwa na Maya
   8. Migogoro katika ndoa — babake Pete anamkataa Pombe! ulevi — babake mzazi Sauna - Umaskini - Naomi kumwacha Lunga
   9. Upweke — Lunga
   10. Uhasama katika ndoa — Mzee Mwimo
   11. Wazee kuoa wasichana wadogo — mzee Fungo anamuoa Pete
   12. Tofauti za kisiasa — Selume na mumewe
   13. Malezi ya watoto — Annete anaenda ughaibuni na watoto
   14. Ndoa za kujaribisha — Nyangumi na Pete
   15. Kudanganywa — Pete anadanganywa na mwanamme
   16. Wanandoa kutoacha nasaba zao baada ya kuolewa — Naomi Maonevu/ kutengwa -Subira
   17. Usaliti — Billy na Sally (zozote 8×1=8)
  3. umuhimu wa mandhari
   1. shule ya Tangamano
    • Kuonyesha masaibu yanayoikumba familia ya ummu
    • Matatizo wanayokumbana nayo wakimbizi — Kairu
    • Kuonyesha umaskini — familia ya Kairu
    • Ubaguzi wa kiukoo — mamake mwanaheri
    • Matatizo ya vijana wa kike katika umri mdogo — Zohali , Rehema
    • Jukumu la familia kusambaratisha watoto — Chandachema
    • Uwajibikaji wa vijana — Chandachema
    • Nafasi ya dini
    • Ukosefu wa uaminifu katika ndoa uasherati — Bw.Tenge
    • Ukatili wa Bw. Tenge (zozote 4×1=4)
   2. Hoteli ya majaliwa
    • Kukutanisha watoto wa Lunga.
    • Kuonyesha malezi mema — mwangeka na mwangemi
    • Uhafidhina wa babu
    • Taasubi ya kiume ya babu
    • Msamaha — Naomi / watoto wake
     (zozote 4 x 1= 4)
 4.      
  1.    
   1. Msemaji- Kenga
   2. Msemewa - Majoka
   3. Mahali- Ofisini mwa majika
   4. Kenga anamtahadharisha kuwa sharti harakati za Tunu zishughulikiwe kwa haraka 4×1=4
  2.    
   1. Methali — dalili ya mvua ni mawingu
   2. Msemo - tuwe macho
   3. Jazanda/ istiari—mvua(hatari) (3×1=3)
  3. Umuhimu wa Kenga katika kuijenga
   1. ploti;
    • Anachimuza ubadhirifu wa viongozi — anapojaribu kutumia vishawishi kwa Sudi
    • Kupitia kwake tunaona kufumanishwa kwa Ashua na Husda ofisini mwa Majoka.
    • Kupitia kwake tunafahamishwa kuhusu kifo cha Jabali ambacho wahusika walikuwa ni Majoka
    • Yeye pamoja na Majoka wanapanga mauaji ya Chopi
    • Aidha, alihusika katika mpango wa kumuumiza Tunu
    • Mabadiliko — anapojiunga na watetezi na kumuacha Majoka 5×1=5
   2. maudhui;
    • Kuonyesha ubarakala — anafaidika na uongozi wa Majoka
    • Kielelezo cha viongozi badhirifu — wanaponda mali ya umma anapoahidiwa kipande cha ardhi
    • Ushauri mbaya — anampotosha Majoka
    • Ubinafsi — anatumia wadhifa wake kutimiza matakwa ya kibinafsi
    • Anaonyesha mabadiliko —anapojiunga na akina Tunu
    • Ukatili — anahusika katika mauaji ya Jabali 5×1=5
   3. wahusika;
    • Anakuza sifa za Majoka kama katili — wanapopanga naye mauaji ya Jabali
    • Anaonyesha ujinga wa Boza — anamdharau anapochonga kinyago
    • Ujasiri wa Sudi — anapokataa vishawishi vyake 3×1=3
 5.    
  1.    
   1. Ni maneno ya Tunu.
   2. Anamwambia Majoka.
   3. Ofisini mwa Majoka.
   4. Hashima/ mamake Tunu kupigania haki za mumewe wakapata fidia baada ya kifo cha mumewe aliyefanya kazi katika Majoka and Majoka Company. (4×1=4)
  2. Sifa za Tunu
   1. Mwenye utu, anamwambia Siti awachukue watoto wa Sudi awapeleke kwa mamake.
   2. Ni kiongozi mwema- Akiwa na Sudi alionyesha uongozi mwema katika chuo kikuu.
   3. Ni mtetezi wa haki- anamwambia Majoka yeye na watu wake watalipa kil atone la damu.
   4. Ni jasiri- anakabiliana na Mjoka kuhusu kifo cha Jabali.
   5. Ni mwenye shukrani- Anamshukuru Siti kwa kuja kumtembelea.
   6. Ni mtambuzi.
   7. Ni mwenye msimamo dhabiti.
   8. Ni mwenye matumaini. (za kwanza 4×1=4)
  3. Dhuluma ni kitendo cha kumnyima mtu haki au stahiki yake; ni uonevu, ni tendo lisilo na haki. Majoka alidhihirisha dhuluma maishani mwake binafsi na katika uongozi mwake.
   1. Serikali yake hutoza wanabiashara kodi lakini wanafanyia kazi katika mazingira machafu. Uvundo umekithiri. Sudi anasema. “ni jukumu lao kuhakikisha soko ni safi si kukusanya kodi pekee...(uk3.)
   2. Bali na kulipa kodi isiyowaletea huduma yoyote wafanyakazi wa soko wanalalamika kuwa wanadaiwa pesa zaidi . kombe asema kuwa ni lazima wapate chakula na pia wawape wenye nchi kitu kidogo.
   3. Ashua asema mahali wanapofanya kazi wanadaiwa kitu kikubwa au kitu chote.
   4. Utawala wake unawahangaisha wafanyakazi. hawafanyi kazi kwa amani Ashua asema “. . . na kuhangaishwa na wenye nguvu ndiyo hewa tunayopumua...” (uk2) sudi anadhibitisha hilo anapolalamika kwamba, “si haki kuchukua kilicho chetu na kututishatisha’ (uk 3).
   5. Anadhulumu raia kwa kutumia rasilimali za Sagamoyo kujinufaisha pamoja na wachache, wanaomuunga mkono. Wao ndio hula ile keki kubwa, huku raia wakitaabika. Sudi anamwambia Boza, “hapo basi-kijikeki. Kwa nini wewe upate kidogo? Sagamoyo ni kwenu,• sherehe ni zenu... na keki kubwa ni ya kina nani” (Uk 4)
   6. Ni dhuluma pia kwa serikali ya majoka kufunga soko Ia Chapakazi mahali ambapo watu wengi hufanya biashara ili kupata chakula chao cha kila siku.
    vii. Katika kiwanda chake wafanyakazi wanapujwa. Soko la chapakazi lilipofungwa bei ya chakula kwenye kioski cha kampuni ya Majoka and Majoka ikapanda maradufu. Wafanyakazi hawawezi kugharamia chakula. Hili ni dhuluma dhidi ya wafanyakazi. Majoka kuendelea kujitayarisha huh wafanyakazi wake wakiumia(uk 17)
   7. Maandamano yanayokumba jimbo la Sagamoyo , si walimu, si wauguzi, si wafanyakazi wa soko ni ithibati tosha kuwa watu wanadhulumiwa.
   8. Ni dhuluma pia kuwaua watu. k.m alimuua jabali aliyekuwa mshindani wake katika siasa.
   9. Wale vijana watano wa Majoka and Majoka waliuawa wakidai haki yao kwenye maandamano.
   10. Tunu alikuwa auwawe kwa kukashifu vitendo vyak’e vya kidhalimu.
   11. Kingi alionywa kuwa angevunjavunjwa na chatu kwa kukaidi amri ya Majoka ya kuwapiga watu risasi.
   12. Majoka anawaua hata washirika wake wa karibu akihofia kuwa wangetoa siri zake. Kwa mfano Ngurumo aliuawa ilhali alikuwa mfuasi wake sugu. Chopi alipangiwa kuuawa pia kwa kujua ‘mengi’. Hii ni dhuluma iliyozidi. Majoka anasema anaona ziwa kubwa ajabu lililofurika damu... kuna kilio cha ndani kwa ndani na machozi mengi humo yasiyoonekana... (Uk 73) na kwamba mikono yake ilikuwa imefungwa nanga humo damuni.(uk 73).
   13. Serikali yake imewahini wananchi raha, wanaishi kwa hofu. Hashima anakiri kwamba yeye na Tunu wake wanaishi kwa hofu nyingi. Wanaogopa kwamba wanaweza kuvamiwa wakati wowote hasa akitilia maanani kuwa mwanawe nusura auawe. Tunu anapopiga nduru kwa kuota mamake anafikiri wameshambuliwa.
   14. Isitoshe serikali ya majoka inawahangaisha watu kuwatupia vijikaratasi vya kuwashurutisha wahame sagamoyo si kwao. Siti anasema,”jana walitutupia vijikaratasi . . .tuhame Sagamoyo si kwet” (uk 52-53).
    Anaamuru polisi kusambaratisha kikatili maandamano ya raia ambao hawakuwa na hatia. Walikuwa wakidai haki yao tu.
    Zozote 12 x 1 = 12
 6.    
  1.    
   1. Msemaji ni Mbura
   2. Alikuwa anazungumza na Sasa.
   3. Walikuwa kwenye sherehe iliyoandaliwa kwa mzee Mambo. (uk44)
   4. Walikuwa wanazungumza kuhusu ‘kula kwao’ Zozote4×l
  2. msemaji ni Mbura
   1. Ni mzalendo- anafanya kazi kwa bidii katika wizara yake kama njia ya kuonyesha uzalendo. ii. Mwenye tamaa- anajaza sahani kwa chakula na kukila chote.
   2. Mwenye utu- anataka wananchi wale kwa niaba ya viongozi kama vile wao wamekuwa wakila kwa niaba yao.
   3. Ni fisadi- amepokea kazi kwa afisi ya serikali kwa njia isiyo halali.
   4. Mzembe- baada ya kula sahani tatu za vyakula kwenye sherehe analala usingizi mzito badala ya kwenda kazini.
   5. Mtetezi wa haki
   6. Mvumilivu
   7. Mpyaro
   8. Msema kweli. Za kwanza 6×1
  3. Tathmini vile viongozi wanavyokuwa wabadhirifu.
   1. Hulipwa mishahara mikubwa sana na serikali jambo linalochangia ubadhirifu wa mali ya üuma.
   2. Sherehe kubwa za viongozi wa kiserikali huchangia pakubwa ubadhirifu.
   3. Viongozi hutumia raslimali za nchi kwa manufaa yao ya kibinafsi- magari ya serikali.
   4. Raslimali zilizotumiwa katika kuvinunua vyakula na vinywaji vingetumika katika kuendeleza asasi tofauti za kijamii.
   5. Dj na wenzake wanapata mabilioni ya fedha kutokana na kuwatumbuiza wageni katika sherehe kama hizi.
   6. Dj kupata huduma za maji, stima, matibabu bure.
   7. Dj kuuza dawa ambazo zilipaswa kutumika na wananchi katika hospitali
   8. Viongozi wanawachukua baadhi ya watu wao wa karibu na kufanya juu chini kuona kwamba wanajifaidi na mali na raslimali za wananchi pasipo kujitolea jasho kamwe.
   9. Upeperushaji wa matangazo katika vyombo vya habari ya sherehe za kiongozi binafsi ni njia ya kuendeleza ubadhirifu.
   10. Sasa na Mbura wanapoamua kuchukua vyakula kupita kiasi katika sherehe za mzee mambo.
   11. Kuwaajiri viongozi wawili wenye nyadhifa sawa katika sekta moja ya umma.
   12. Vibaraka na vikaragosi kupewa mali ambayo ingewafaidi wananchi.
    Zozote l0×1=10
 7.      
  1.    
   1. Tashhisi/ uhuishi- mbavu zikamtafuna.
   2. Takriri/ uradidi Alicheka.
   3. Chuku- uliosafiri robo dunia.
   4. Utohozi-soli
   5. Nidaa- Magharibi !.
   6. Jazanda- chatu lililotambaa.
   7. Mbinu rejeshi- unakumbuka.
   8. Taswira –kicheko cha kazu/ kuinua mguu . (8×1=8)
  2.    
   1. Taswira oni- ameviringa ngumi.
   2. Taswira sikivu- vicheko vya nguvu viliwapasuka/ mwangwi.
   3. Taswira hisi- mbovu zikamtafuna.
   4. Taswira mwendo- kujirusharusha/ kuinua mguu/ lilisafiri. (4×1=4)
  3.    
   1. Eneo la mkutano wa kina kazu na Bongoa.
   2. Kazu anakutana na mke wa Bogoa- Sakina.
   3. Hali ya kiuchumi ya kazu na wenzake inabainika (club ni maarufu kwa watu wa kipato cha chini).
   4. Tunafahamu alivyofika mjini Bogoa.
   5. Ukatili wa Bi. Sinai unabainika.
   6. Kifo cha wazazi wa Bogoa na Bi Sinai kinaelezwa.
   7. Kutoroka kwa Bogoa kutoka kwa Bi Sinai.
   8. Eneo la burudani. (8×1=8)
 8.    
  1. Tambua utanzu na kipera cha kifungu hiki. (alama 2)
   Utanzu-Ushairi alama 1
   Kipera- Nyimbo za mbolezi alama 1
  2. Eleza toni ya kifungu hiki. (alama 2)
   Huzuni/ uchungu/masikitiko- ni kilio nikilio/ hurizia wapendwa. 1×2
  3. Eleza sifa sita za kipera kinachorejelewa. (alama 6)
   1. Hutofautiana katika jamii moja hadi nyingine kutegemea imani ya jamii kuhusu kifo na hadhi ya waliofiwa.
   2. Huimbwa kwa nia ya kufariji waliofiwa.
   3. Husifu aliyekufa- sifa chanya za aliyekufa.
   4. Hufungamana na muktadha maalum.
   5. Huimbwa wakati wa matanga au wakati wa kuomboleza
   6. Huimbwa kwa toni ya uchungu/ huzuni
   7. Huimbwa kwa mwendo wa taratibu.
   8. Huandamana na ala za muziki. Za kwanza 6×1
  4. Fafanua majukumu ya kipera hiki katika uwasilishaji wa ngano.
   1. Hutumiwa kuwasilisha ujumbe mzito katika hadithi.
   2. Hutenganisha matukio yanayojumuisha hadithi.
   3. Husisimua hadhira na kuiondolea ukinaifu wa masimulizi makavu
   4. Huishirikisha hadhira katika utambaji na uwasilishaji.
   5. Hurefusha hadithi.
   6. Ni kipumuo. Hupunguzia hadhira uchovu.
   7. Huipa hadithi toni fulani mf. Toni ya huzuni.
   8. Huendeleza hadithi.
   9. Huangazia maadili katika hadithi.
   10. Huburudisha jamii
   11. Huchangia kama kitambulisho cha jamii husika. Zozote l0×1=10
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Cekenas Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?