Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mokasa II Joint Mock Exams 2023

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Jibu maswali yote
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  1. UFAHAMU
    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.

    Basi limemwacha. Basi la abiria ambalo linajuzu kusimama kila kituo rasmi kama hiki. Lime.nwacha kwenye baridi ya mzizimo. Licha ya kujaribu kulisimamisha, dereva mweupe aniejikurup usha kana kwamba hamna kituo rasmi mahali pale cha abiria kusubiri mabasi yanayohudumu kwenye jiji hili. Baridi kama hii kwao Afrika Mashariki hakuwahi kuiona. Lo! Mtu lazima awe na safu ya maguo na viatu vizito kama vya wanajeshi wa nchi kavu ila hazifai kitu kwa sababu bado baridi inapenyeza na kumzizima.

    Alitembea kando ya barabara kwenye kijia cha wapiti-njia huku akinyapianyapia nyapunyapu na kupepesuka kama mlevi. Mara moja akili yake ikamkumbusha siku zake za fahari alipofuatia waragi kwenye kitongoji duni cha Kibuye jijini Kampala, gongo kwenye vichochoro vya Ubungo, Dar-es- Salaam, na chang'aa kwenye fondogoo la Mathare, Nairobi. Zilikuwa siku za heri na faraka, kabla ya kuja kufuatia kisomo cha juu huku wanakoita "majuu." Tangu hapo ameendelea kuwa mwanafunzi mzuri wa chuo cha maisha ya majuu. Amejifunza hakuna mahali kama nyumbani. "Nyumbani ni nyumbani ingawa pangoni," ni methali iliyochukua kina: cha maana kwa kiwango asichowahi kukikadiria alipokuwa kwao.

    Anakumbuka mara ya kwanza alipojikuta darasani yeye peke yake mweusi, kisiwa cheusi kwenye bahari ya weupe. Kama hilo halikutosha, mhadhiri mzungu na wanafunzi darasani walikuwa hawasiti kumsaili kwa maswali ya kumdhalilisha na kumdunisha.

    "Je, kule kwenu watu wanavaaa nguo au wanaternbea rabana?" "Ulivaa nguo ulipotua kwenye uwanja wa ndege wa huku?" "Mbona hamwachi kupigana nchini kwenu?" "Huu weusi wenu unaozidi kiza unatokana na kuangukiwa na lami au kupigwa na mionzi ya jua?” “ Je, mwaishi kwenye miti kama tumbiri?"

    Kile ambacho Fikirini hakuwaambia kimasomaso ni kuwa kachoshwa na kuchushwa na dharau yao, masimbulio na bezo zao. Anaomba tu muda wake wa masomo umalizike, ahitimu arejee nchini mwao. Arudi kwao na kufaidi utajiri na umaskini wao, ajitenge na umaskini wa utajiri wa kule majuu. Hata sheria zao zinamtia hofu. Mara mbili ametozwa faini na polisi mzungu kwa kuvuka barabara huku taa za kuelekeza magari zikiwa zinawaka rangi nyekundu. Huko kwao taa hizi alizisikia tu. Kukaa kwake majuu kumemjuza jela imetengewa watu weusi tu. Wanaume weusi hawapati shahada wanag'ang'ania kula kalenda. Yeye mwenyewe ameepuka jela kimungumungu tu.

    Fikirini anakumbuka kutwa moja alipoingia hoteli akaagiza chakula akala akashiba japo chakula hiki hakipendi. Kila alapo yeye hukumbuka mshumbi wa ugali wa kwao na mlenda, wali wa pilau, matoke na mhogo. Haidhuru, watu wa kwao walisibu walipolonga "Simba akikosa nyama hula nyasi." Alipoondoka kwenda kwenye vyumba vya watu wastaarabu, alikumbana na dharau ya wateja na wahudumu ila mitazamo hiyo haikumshtua. Mama mmoja mweupe alinyanyua simu yake na kubofya huku akimtazama Fikirini kwa jicho la hasama. Alipotoka mkahawani, kufumba na kufumbua polisi walikuwa wamefika na magari yao yakimemetesha taa za kuashiria dharura. Walikuwa wametoa bastola zao walizomwelekeza tayari kwa lolote.
    "Do you speak English?" Walimsaili.
    Sasa polisi gani angejua Kiingereza kuliko yeye mwanafunzi wa uzamifu katika somo la Kiingereza katika chuo kikuu? Hakuwa na kauli. Moyo ulikuwa umemtweta kwa fadhaa, hajui cha kusema wala kufanya. Alikuwa hata hajajibu alipopigwa pingu mikononi na kutoswa ndani ya gari la 911.
    "Ni nani anataka kuona uchi wako?"
    "Bwana polisi sikuelewi?"
    "Someone called to say you are exposing yourself!"

    Hapo ndipo alipotanabahi kwamba hakufunga zipu ya suruali yake. Kama angekuwa kwao Afrika, mtu angefanya hisani ya kumwambia, "Aisee funga duka," badala ya kumwitia polisi. Fikirini alifikishwa mahakamani akashtakiwa kwa kosa la utovu wa adabu kwa kutofunga zipu. Jaji mweusi alimtoza faini ya dola mia mbili zilizokuwa adimu ila zilimwepushia Fikirini kifungo cha miezi sita gerezani! Afikiriapo kuhusu kisa hiki cha zipu, hujiambia hatawahi kuwaambia watu wa kwao hata akilewa gongo, waragi au chang'aa kiasi cha Bahari ya Hindi. Mambo ya aibu kama haya unaweza kuwaeleza ndugu zako nyumbani?

    Maswali
    1.  
      1. Msimulizi wa makala haya alidhamiria nini?       (alama 1)
      2. Onyesha uhalisia wa msemo "Nyumbani ni nyumbani ingawa pangoni" kwa mujibu wa makala haya.    (alama 5)
    2. Eneo alikotoka Fikirini halikuwa limefikia upeo wa ustaarabu. Onyesha kwa mifano mwafaka kutoka kwenye makala.       (alama 4)
    3. Watu wa 'majuu' wana mtazamo hasi kumhusu mtu mweusi. Thibitisha. (alama 3)
    4. Jibu kwa mujibu wa maagizo     (alama 2)
      1. fadhaa (tolea kisawe chake)
      2. adimu (eleza maana)
  2. UFUPISHO
    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.


    Maendeleo ni hali ya watu kuwa na uwezo wa kuishi maisha mazuri, kujidhibiti na kujisimamia katika shughuli zao za kila siku. Hayati Mwalimu Nyerere alisema maendeleo ni kuwepo kwa hali inayowezesha watu kupanga gharama za maisha. Kwa mfano, kuwepo kwa mfumo bora wa elimu, huduma bora za afya, usafiri na utawala bora na utawala bora ni baadhi ya mambo yanayoleta ufanisi katika maisha ya binadamu. Hivyo basi kuwepo kwa miradi, hali au vitu vinavyosaidia binadamu si maendeleo. Aghalabu, vitu hivyo huwa vikwazo vinavyozuia maendeleo na kufanya maisha ya binadamu kuwa magumu.

    Tangu asili na jadi, kikwazo kikubwa cha maendeleo kimekuwa itikadi za kijamii, kisiasa na kiuchumi ambazo zinatenga kazi na mambo fulani, kuwa ya wanaume na mengine kuhusishwa na wanawake. Mathalani, miongoni mwa jamii nyingi za Kiafrika wanawake wanaaminiwa kuwa viumbe duni. Inaaminiwa kuwa mwanamke ana upungufu wa kiakili na nguvu za mwili akilinganishwa na mwanamume. Kwa sababu ya dhana hii hafidhina na potovu, kuna kazi ambazo wanaume hawawezi kuzifanya eti kwa sababu ni za wanawake.

    Katika sehemu za mashambani wanawake hufanya takriban kazi zote za nyumbani zikiwemo za kuchanja kuni, kupika, kulea watoto, kuuguza wagonjwa, kupokea wageni na kuosha. Kazi hizi ni nyingi na humfunga mwanamke nyumbani. Kazi zilizotengewa wanaume ni chache na wao huwa na wakati mwingi wa kupumzika. Kwa mfano, ni nadra kumpata mwanamume wa kijijini akifanya kazi nyumbani baada ya saa kumi za mchana. Wakati kama hizi utawakuta wanaume kwenye vilabu vya pombe, mitaani wakitembea na hata kuzuru boma moja hadi nyingine. Utawakuta sokoni wameketi huku wameandika nne kwa miguu yao wakipiga gumzo. Ukiwauliza baadhi yao watasema ni saa za kupumzika.

    Jambo hili limekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo katika jamii kwa sababu wanaume hutumia wakati mwingi katika starehe badala ya kuzalisha mali.

    Ardhi hiyo ndiyo rasilimali yenye dhamana kubwa kwani ndiyo inayomwezesha mtu kuzalisha mali. Hata hivyo, inasikitisha kuona kwamba wanawake wengi hasa wasioelimika hawana vyeti vya kumiliki ardhi. Hili ni tatizo kubwa kwa sababu panapotokea talaka kati ya mke na mume, mwanamke hurudi nyumbani kwa wazazi wake aghalabu bila kudai chochote.

    Inasemekana kuwa mfumo mzuri wa siasa na uongozi katika jamii hufanikisha maisha mazuri. Vivyo hivyo, siasa mbaya ndicho kiini cha maisha mabaya. Katika mfumo wa siasa na uchumi, idadi kubwa ya wanawake hubaguliwa na wanaume. Mwanamke anayezindua mwenzake dhidi ya siasa mbaya na maonevu aghalabu husemekana amekiuka utamaduni na hataki kudhibitiwa na mwanamume. Jambo hili linawafanya wanawake kuchelea kujitokeza hadharani kupinga uongozi mbaya na maonevu.

    Hata hivyo kuna baadhi ya wanawake waliotia bidii maishani na kuthibitisha kwamba mwanamke ana uwezo sawa na mwanamume. Kwa mfano, nchini Kenya kuna wanawake waliojitokeza kifua mbele wakachaguliwa na hata kuteuliwa katika nyadhifa za uongozi. Wote hawa wana bidii za mchwa na wamestawisha maisha ya wananchi.

    Katika nyanja za michezo, muziki, elimu na sheria, wanawake wamejizatiti na hata kuwashinda wanaume. Kwa mfano, katika michezo ya Olimpiki, timu za wanawake zimekuwa zikishinda nishani chungu nzima.

    Katika elimu, tumewashuhudia wasichana wakiwashinda wavulana katika mitihani. Jambo hili limewawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika masuala kama vile udaktari na uanasheria. Mambo haya ni thibitisho kuwa tunapaswa kuwapa wanawake nafasi sawa na wanaume katika shughuli zote za jamii na ujenzi wa taifa. Ningehimiza wanaume wasiwe na inda na kinyongo dhidi ya wanawake kwani chanda chema huvishwa pete.

    Maswali
    1. Fupisha aya tatu za kwanza kwa maneno yasiyozidi 100.         (alama 9)
      Matayarisho
      Nakala safi
    2. "... kikwazo kikubwa cha maendeleo kimekuwa itikadi za kijamii, kisiasa na kiuchumi." Fafanua kauli hii ukirejelea aya sita za mwisho. (Maneno 60)                    (alama 6)
      Matayarisho
      Nakala safi
  3. MATUMIZI YA LUGHA
    1.  
      1. Linganua sauti zifuatazo:     (alama 1)
        /th/ na /s/
      2. Andika neno linaloanzia kwa kikwaruzo hafifu cha menoni na kuishia kwa irabu ya juu mbele     (alama 1)
    2. Andika neno lenye muundo ufuatao:      (alama 1)
      KIKKIKI
    3. Onyesha panapotiliwa mkazo katika maneno yaliyopigwa mstari:     (alama 2)
      Barabara hii ilijengwa barabara muda mrefu walakini ina walakini.
    4. Jibu inaswali yafuatayo kulingana na maagizo:      (alama 2)
      1. Tafadhali mwalimu, nisamehe. (Geuza ili kuleta dhana ya taarifa.)
      2. Changanua sentensi ifuatayo kwa kielelezo cha matawi. (Bainisha dhima ya sentensi hii)
    5. Fafanua maana inayoibuliwa na viambishi vya upatanisho wa kisarufi katika ngeli ya PA-KU-MU.      (alama 3)
    6. Andika upya sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa.
      Mwanamke yule alitumia nyundo zile kumjengea nyumba ya kifahari.       (alama 2)
    7. Andika neno lenye muundo ufuatao      (alama 2)
      nafsi ya tatu umoja, mzizi wa kitenzi cha asili ya kigeni, kauli ya kutendeshwa, kauli ya kutenda, kirejeshi katika ngeli ya A-WA umoja
    8. Kanusha sentensi ifuatayo katika wakati ujao, hali timilifu.     (alama 2)
      Rais wa Kenya anatoa hotuba yake.
    9. Andika sentensi yenye viambajengo vifuatavyo:          (alama 2)
      nomino ya kawaida, kivumishi kisisitizi cha mbali katika ngeli ya KI-VI, kivumishi cha a-unganifu kinacholeta dhana ya nafasi katika orodha, kitenzi kishirikishi kipungufu, kivumishi cha sifa.
    10. Linganua sentensi zifuatazo.         (alama 2)
      1. Magari yote yatasafishwa.
      2. Magari yoyote yatasafishwa.
    11. Wafanyabiashara watafungua kazi. Amani itapatikana. (Anza kwa kiunganishi cha masharti)          (alama 1)
    12. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya maneno yafuatayo: karibia na karipia.      (alama 2)
    13. Bainisha virai katika fungu tenzi.        (alama 2)
      Wanafunzi wengi wanapaswa kusoma vitabu hivi vyote kila wakati.
    14. Pambanua sentensi ifuatayo kwa njia ya kistari.         (alama 3)
      Mwanafunzi yule aliyekuwa wa kwanza alipewa zawadi ambayo alinunuliwa.
    15. Andika sentensi ifuatayo kwa usemi taarifa:     (alama 3)
      Amani: Salaale! Kwa nini umechelewa?
      Pendo: Nisamehe, nitafika mapema kesho.
    16. Huku ukitolea mifano, eleza matumizi mawili ya alama ya mkwaju.         (alama 2)
    17. Bainisha matumizi ya kiambishi 'O' katika sentensi ifuatayo.       (alama 2)
      Kimondo alinunua mwongozo ulioandikwa vizuri.
    18. Bainisha dhana zilizo mabanoni katika sentensi zifuatazo:
      1. Mji huu ulikuwa safi mno. (kijalizo)        (alama 1)
      2. Jumba lake lilijengwa alivyoagizwa na mhandisi. (kiarifu)        (alama 1)
    19. Tunga sentensi yenye kuonyesha kishazi tegemezi kinachochukua nafasi ya chagizo cha mahali.       (alama 1)
    20. Andika kisawe cha "Enda segemnege".     (alama 1)
    21. Andika upya sentensi ifuatayo kwa kuanzia yambwa tendewa.
      Kitabu kile kizuri kiliandikiwa mwalimu wa Kiswahili.       (alama 1)
  4. ISIMUJAMII
    1. Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.
      Mahakama ya upeo imebatilisha uteuzi wa makatibu wasaidizi wa mawaziri waliokuwa wameteuliwa na rais. Kwa mujibu wa Jaji mkuu Beatrice Kaliku, makatibu hao wanastahili kupunguzwa hadi ishirini na watatu.
      1. Bainisha sajili ya makala haya.    (alama 1)
      2. Fafanua sifa nne za sajili hii.       (alama 4)
    2. Eleza sifa tano za mazungumzo rasmi.         (alama 5)

MARKING SCHEME

  1. UFAHAMU
    1. Msimulizi wa makala haya alidhamiria nini?
      • Kuonyesha jinsi wanafunzi wa kiafrika wanavyodhalilishwa/dharauliwa/wanavyobezwa wanapokwenda ng'ambo kusoma (1x1=1)
    2. Onyesha uhalisia wa msemo " Nyumbani ni nyumbani ingawa pangoni" kwa mujibu wa makala haya.    (alama 5)
      1. Nyumbani kwa kina Fikirini hakuna baridi ya mzizimo kama ile ya majuu
      2. Kule majuu Fikirini anaulizwa maswali ya kumdhalilisha ambayo hangeulizwa kwao
      3. Hapendi chakula cha majuu. Anatamani ugali, pilau, matoke na mhogo wa kwao
      4. Anatazamwa kwa uhasama na wahudumu pamoja na wateja weupe mkahawani jambo ambalo halingetokea kwao.
      5. Anatiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani kwa kutofunga zipu. Ingekuwa kwao, angekumbushwa kufanya hivyo bila tatizo na mtu yeyote.
      6. Jela ja kule majuu ni kama zimejengewa mtu mweusi tu (5x1=5)
    3. Eneo alikotoka Fikirini halikuwa limefikia upeo wa ustaarabu. Onyesha kwa mifano mwafaka kutoka kwenye makala.   (alama 4)
      1. Fikirini anakwenda majuu kusomea shahada ya uzamifu katika Kiingereza
      2. Barabara za kwao mijini hazina taa za kuyaelekeza magari
      3. Kuwepo kwa vitongoji duni kama vile Kibuye,Ubungo na Mathare
      4. Unywaji wa pombe haramu kama vile waragi,gongo na chang'aa zinazouzwa kwenye mitaa duni. (4x1=4)
    4. Watu wa "majuu' wana mtazamo hasi kumhusu mtu mweusi. Thibitisha.      (alama 3)
      1. Kudhani watu weusi hutembea uchi nchini mwao
      2. Kusema eneo la mtu mweusi limejaa fujo
      3. Hawathamini ngozi ya mtu mweusi (weusi wake)
      4. Wana imani kuwa watu weusi wanaishi mitini kama tumbiri. (3x1=3)
    5. Jibu kwa mujibu wa maagizo          (alama 2)
      1. fadhaa (tolea kisawe chake) - wasiwasi/hofu
      2. adimu (eleza maana) – isiyo rahisi kupatikana (2x1=2)
  2. UFUPISHO
    1. Fupisha aya tatu za kwanza kwa meneno yasiyozidi 70.       (alama 9, 1 ut)
      1. Maendeleo ni hali ya watu kuwa na uwezo wa kuishi maisha mazuri, kujidhibiti na kujisimamia katika shughuli zao za kila siku.
      2. Pia ni kuwepo kwa hali inayowezesha watu kupunguza gharama za maisha.
      3. Kuwepo kwa miradi, hali au vitu visivyosaidia binadamu si maendeleo bali huwa vikwazo vinavyozuia maendeleo na kufanya maisha ya binadamu kuwa magumu.
      4. Kikwazo kikubwa cha maendeleo kimekuwa itikadi za kijamii, kisiasa na kuchumi ambazo zinatenga kazi na mambo fulani kuwa ya wanaume na mengine ya wanawake. 
      5. Jamii nyingi za kiafrika zinaamini wanawake ni viumbe duni au inaaminiwa kuwa mwanamke ana upungufu wa kiakili na nguvu za mwili akilinganishwa na mwanaume.
      6. Dhana hii hafidhina huwazuia wanaume kutofanya kazi fulani.
      7. Wanawake hufanya takriban kazi zote za nyumbani k.m kuchanja kuni zinazomfunga nyumbani.
      8. Kazi zilizotengewa wanaume ni chache na wao huwa na wakati mwingi wa kupumzika/Ni nadra kuwapata wakifanya kazi za nyumbani lakini utawakuta kwenye vilabu vya pombe.
    2. “.......................Kikwazo kikubwa cha maendeleo kimekuwa itakadi za kijamii, kisiasa na kiuchumi." Fafanua kauli hii ukirejelea aya sita za mwisho. (Maneno 60) (alama 6, 1 ut)
      1. wanaume hutumia wakati mwingi katika starehe badala ya kuzalisha mali.
      2. Wanawake wengi wasioelimika hawana vyeti vya kumiliki ardhi.
      3. Siasa mbaya ndicho kiini cha maisha mabaya/idadi kubwa ya wanawake hubaguliwa na wanaume.
      4. Mwanamke anayezindua wenzake dhidi ya siasa mbaya na maonevu husemekana amekiuka utamaduni na hataki kudhibitiwa.
      5. Utamaduni unawafanya wanawake kuchelea kujitokeza hadharani kupinga uongozi mbaya na maonevu.
        UTUZAJI
        A-8
        B-5
        UT-2/15
        UTOZAJI
        1. Makosa 6 x 1⁄2h = 3h
        2. Makosa 6 x 1⁄2s = 3s
        3. Maneno ya ziada = Maneno 10-1Z
        4. Ili apate alama 2 za mtiririko,
          • Hoja zote ziwepo
          • Makosa machache ya h/s
          •  Atumie aya moja
          • Atumie viunganishi sahihi.
  3. MATUMIZI YA LUGHA
    1.  
      1. Linganua sauti zifuatazo:      (alama 1)
        /th/na/s/
        /th/hutamkwa menoni ilhali /s/ hutamkwa katika ufizi. 4x1-1
      2. Andika neno linaloanzia kwa kikwaruzo hafifu cha menoni na kuishia irabu ya juu mbele thumni, thamini, thuluthi 1x1=1
    2. Andika neno lenye muundo ufuatao: (alama 1)
      KIKKIKI
      • angika, fungika 1 x 1 = 1
    3. Onyesha panapotiliwa mkazo katika maneno yaliyopigwa mstari: (alama 2)
      Barabara hii ilijengwa barabara muda mrefu walakini ina walakini.
      1. bara'bara/barabara
      2. ba'rabara/barabara
      3. wala'kini/walakini
      4. wa'lakini/ walakini
    4. Jibu maswali yafuatayo kulingana na maagizo:  (alama 2)
      1. Tafadhali mwalimu, nisamehe. (Geuza ili kuleta dhana ya taarifa.)
        Nilimwomba mwalimu anisamehe.
        au
        Nilimwomba mwalimu msamaha. 
          1x1=1
      2. Changanua sentensi ifuatayo kwa kielelezo cha matawi. (Bainisha dhima ya sentensi hii)
        • amri/agizi/elekezi
    5. Fafanua maana inayoibuliwa na viambishi vya upatanisho wa kisarufi katika ngeli ya PA-KU-MU.  (alama 3)
      PA-mahali panapodhihirika
      KU- mahali kusikodhihirika
      MU- ndani ya 
         3x1=3
    6. Andika upya sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa. (alama 2)
      Mwanamke yule alitumia nyundo zile kumjengea nyumba ya kifahari.
      Janajike lile lilitumia majundo Yale kulijengea jumba la kifahari. 2/0
    7. Andika neno lenye muundo ufuatao:        (alama 2)
      nafsi ya tatu umoja, mzizi wa kitenzi cha asili ya kigeni, kauli ya kutendeshwa, kauli ya kutenda, kirejeshi katika ngeli ya A-WA umoja
      mf asafirishwaye  2/0
    8. Kanusha sentensi ifuatayo katika wakati ujao, hali timilifu.
      Rais wa Kenya anatoa hotuba yake.
      • Rais wa Kenya hatakuwa ametoa hotuba yake. 2/0
    9. Andika sentensi yenye viambajengo vifuatavyo:  (alama 2)
      nomino ya kawaida, kivumishi kisisitizi cha mbali katika ngeli ya KI-VI, kivumishi cha a-unganifu kinacholeta dhana ya nafasi katika orodha, kitenzi kishirikishi kipungufu, kivumishi cha sifa.
      Mf. Kitabu kile kile cha kwanza ni bora/kizuri/kipya.
    10. Linganua sentensi zifuatazo.    (alama 2)
      1. Magari yote yatasafishwa.
        • Bila kubakiza/bila kusaza
      2. Magari yoyote yatasafishwa.
        • Bila kuchagua/kutobagua
    11. Wafanyabiashara watafungua kazi. Amani itapatikana. (Anza kwa kiunganishi cha masharti) (alama 1)
      Ikiwa/kama/iwapo amani itapatikana, wafanyaiashara watafungua kazi.
    12. Tunga sentensi moja kutofautisha "karibia" na "karipia" kimaana. (alama 2)
      Mf. Mama alimkaribia na kumkaripia kwa kosa hilo.
      1. Karibia - kwenda karibu
      2. Karipia - kukemea
    13. Bainisha virai katika fungu tenzi.
      Wanafunzi wengi wanapaswa kusoma vitabu hivi vyote kila wakati.        (alama 2)
      wanapaswa kusoma vitabu hivi vyote kila wakati/ wanapaswa kusoma - RT vitabu hivi vyote - RN
      hivi vyote - RV
      kila wakati - RE
    14. Pambanua sentensi ifuatayo kwa njia ya kistari. (alama 3)
      Mwanafunzi yule aliyekuwa wa kwanza alipewa zawadi ambayo alinunuliwa.
      S-KN(N+V+S)+KT(T+N+S)
    15. Andika sentensi ifuatayo kwa usemi taarifa:
      Amani: Salaale! Kwa nini umechelewa?
      Pendo: Nisamehe, nitafika mapema kesho.  (alama 3)
      • Amani alishangaa na kutaka kujua sababu ya Pendo kuchelewa 1⁄2 naye Pendo akamwomba amasamehe/msamaha na kumwambia angefika 1⁄2mapema siku ambayo ingefuata/iliyofuata. 1⁄2
        au
      • Amani alishangaa na kumwuliza Pendo kwa nini alikuwa amechelewa na Pendo akamwomba amasamehe/ msamaha na kumwambia angefika mapema siku ambayo ingefuata/iliyofuata.
    16. Huku ukitolea mifano, eleza matumizi mawili ya alama ya mkwaju. (alama 2)
      1. kuonyesha visawe - mama/Nina
      2. badala ya ama/au - Alitakula ugali/wali.
      3. kuandika kumbukumbu - KUMB/01/2023
      4. kuandika tarehe - 20/02/2023     2x1=2
    17. Bainisha matumizi ya kiambishi "o" katika sentensi ifuatayo.   (alama 2)
      Kimondo alinunua mwongozo ulioandikwa vizuri..
      ulioandikwa - kirejeshi cha ngeli ya U-I umoja
      mwongozo - unominishaji/uundaji wa nomino/tokeo la tendo
    18. Bainisha dhana zilizo mabanoni katika sentensi zifuatazo:
      1. Mji huu ulikuwa safi mno. (kijalizo)     (alama 1)
        safi mno    1/0
      2. Jumba lake lilijengwa alivyoagizwa na mhandisi. (kiarifu)   (alama 1)
        lilijengwa alivyoagizwa na mhandisi 1/0
    19. Tunga sentensi yenye kuonyesha kishazi tegemezi kinachochukua nafasi ya chagizo cha mahali. (alama 1)
      Paka ameingia alimojificha panya.  1/0
    20. Andika msemo wenye maana sawa na " Enda segemnege".
      • Enda mrama/enda tenge/enda upogo 1/0
    21. Andika upya sentensi ifuatayo kwa kuanzia yambwa tendewa. Kitabu kile kizuri kiliandikiwa mwalimu wa Kiswahili.   (alama 1)
      Mwalimu wa Kiswahili aliandikiwa kitabu kile kizuri. 1/0
  4. ISIMUJAMII
    1. Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali. (alama 1)
      Mahakama ya upeo imebatilisha uteuzi wa makatibu wasaidizi wa mawaziri waliokuwa wameteuliwa na rais. Kwa mujibu wa Jaji mkuu Beatrice Kaliku, makatibu hao wanastahili kupunguzwa hadi ishirini na watatu.
      1.  Bainisha sajili ya makala haya.           (alama 1)
        Sajili ya magazetini/matangazo/redioni
      2. Fafanua sifa nne za sajili hii.    (alama 4)
        1. Misamiati hubadilika kutegemea mada mfano saratani katika mada kuhusu afya.
        2. Kuwepo kwa vichwa vifupi vyenye maneno ya kuvutia ili kuleta taharuki na ilhamu ya kusoma. Kwa mfano, 'waziri kizimbani'
        3. Kutia chuku kwa madhumuni maalum
        4. Hutumia lugha ya kueleweka rahisi - hii ni kwa kuwa gazeti husomwa na watu wa viwango tofauti kielimu.
        5. Baadhi ya vichwa vya taarifa hukiuka kanuni za sarufi
        6. Sentensi fupifupi hutumiwa ili kurahisisha usomaji - Watatu kizimbani.
        7. Usemi halisi hutumiwa kuwanukuu wasemaji. Kwa mfano, "Tutapambana na wafisadi," rais asema.
        8. Kuchanganya tarakimu na maelezo - Watu 3 waathirika na mafuriko. ix) Kuchanganya ndimi - maeneo mengi hayaha internet.
        9. Lugha inayoteka hisiya - Suluhu achezwa
    2. Eleza sifa tano za mazungumzo rasmi.    (alama 5)
      1. Msamiati maalum - kutegemea taaluma kwa mfano, daktari, mgonjwa na muuguzi katika muktadha wa hospitalini.
      2. Lugha ya unyenyekevu - samahani mwalimu, nisaidie daftari langu
      3. Lugha sanifu - kwa mfano 'Umeandika insha vizuri' katika muktadha wa shuleni. 
      4. Lugha ya kuhoji na kudadisi - kwa mfano ulikuwa wapi siku usiku wa tarehe nne mwezi wa tano? Katika muktadha wa mahakamani.
      5. Kushirikisha maelezo na hisabati - kwa mfano, meza mbili mara tatu
      6. Kutumia sentensi ndefu ndefu - ili kutoa maelezo kamilifu 
      7. Lugha rasmi hutumika - Bw. Tumbo umeshtakiwa kwa kosa la wizi. 
      8. Lugha ya kuamrisha - kwa mfano polisi anaposema, 'Toa viatu mara moja.
      9. Kuchanganya msimbo - kwa mfano, huyu anaugua mild headache.
        Zozote 5 x 1=5
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mokasa II Joint Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?