Kiswahili Paper 2 Questions - Maranda High School Mock Exams 2023

Share via Whatsapp

Maagizo

 • Jibu maswali yote.
 • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
 • sawasawa na kuwa maswali yote yamo.
 1. UFAHAMU ( ALAMA 15)
  Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

  Ulikuwa wakati wa jioni jua limepunguza udhia wake na upepo mwanana ulikuwa ukipita na kuzipapasa ngozi zetu mfano wa pamba. Kama ilivyokuwa desturi yetu hapo kijijini, siku hiyo pia tuliketi nje ya nyumba yetu tukafanya duara kulizunguka birika la kahawa. Kila mmoja alichukua glasi akajimiminia kiasi cha kahawa alichotaka na kurudi kuchukua mahali pake kitini.

  Tulipotia fahamu tulipata mazoea haya yamekita mizizi nasi tukawa hatuna budi kuyakumbatia. Hatukuyakumbatia tu bali tuliyakumbatia kwa dhati ya moyo. Vikao hivi havikuwa tu hazina kubwa kwetu bali vilikuwa vya thamani isiyomithilika. Hapa ndipo tulinoleana bongo kwa kupashana habari. Leo hii tumo katika kuzungumzia nguzo kuu za maendeleo, tena maendeleo ya haja ambayo yataibadilisha sura ya mwananchi na nchi. Nahodha wa kikao cha leo anampa msemaji wa kwanza nafasi naye hakusita kushika usukani.

  “Nionavyo mimi, maendeleo yatawezekana ikiwa elimu itaweza kukidhi haja za watu. Sio nadharia tupu ambayo huwezi kuitumikiza ikaleta matokeo. Lazima nchi imwezeshe kila mtu kupata elimu ya msingi ambayo itamsaidia kufikia habari za kimsingi, iwe ni kupitia kwa magazeti au vitabu. Habari hizo zitamfunua macho, akaona na kuhakiki mambo. Wenzangu, jibu ni elimu! Maendeleo yanategemea elimu,” kijana mmoja alisema kwa mhemko.

  Muda wote huo kila mtu alikuwa ametulia. Wapo waliotikisa vichwa kukubaliana naye na wapo waliovitikisa kukataa. Hata hivyo, wapo waliokaa tu kama mawe. Hawakuonyesha ishara yoyote ya kuguswa na maneno yale. Mwendesha mjadala alifanya ishara na mara kijana wa miraba minne aliyekuwa amevalia shati lililompwaya akasimama na kuzungumza kwa sauti nzito.

  “Mtazamo wangu mimi bwana ni tofauti. Ukitazama duniani kote, kila nchi iliyoendelea imewekeza sana viwandani. Uzalishaji wa viwandani ndio dawa mjarabu. Hebu vuta fikra! Kila tunachotumia kuanzia kalamu, kitabu, nguo, msumari, saruji… yaani kila kitu chenye nafasi katika maisha yetu kimepitia hatua za uzalishaji viwandani…” “Si ndiyo hayo! Naona unaniunga mkono aisee! Viwanda huendeshwa kwa elimu au ukipenda maarifa. Na maarifa hayo huja kwa mafunzo ambayo ni elimu,” alifafanua yule kijana wa kwanza.

  “Nipe muda Sudi! Nipe muda nimalizie hoja yangu. Ninachosema ni kuwa elimu bila utumizi wake kuzalisha huduma na bidhaa muhimu haina nafasi kubwa katika maendeleo ya jamii. Elimu si mwisho wa yote bila mwanzo. Elimu inafaa kuzalisha. Na uzalishaji muhimu zaidi ni wa viwandani. Kwa hivyo, nionavyo mimi msisitizo mkubwa zaidi unafaa kuwa katika kutengeneza viwanda na kuvifanya kuzalisha.”

  Jamaa alimaliza mazungumzo yake akatulia na kupiga funda la kahawa. Hapo ndipo mwendesha mjadala alipompa kijana mwingine nafasi naye atoe maoni yake. Kijana huyo mdogo wa kimo na umbo alianza kusafisha koo huku wenzake wakimshangilia. Kwa kawaida kijana huyo alikuwa na mbwembwe nyingi.

  “Bwana Spika,” alianza huku wenzake wakishangilia kwa kila namna. Walipotulia aliendelea, “Mimi najua wapo watakaoniita mjinga hapa lakini naamini miundombinu ni muhimu zaidi. Watu hawawezi kuendelea bila mfumo mzuri wa barabara na reli, usambazaji wa kuridhisha wa umeme, viwanja vya kutosha na bora kwa ajili ya vijana kunoa vipawa vyao…”

  Maneno yake yalifunikwa ghafla na kelele za kumshangilia na kumsifu huyu kijana waliyemwita Sumaku. Hii ilikuwa lakabu waliyompa kwa uwezo wake wa kuelewa mambo kwa wepesi na kwa kujua kuwavutia vijana wenzake maana alijua wapi pa kugonga ili gogo litoe mlio. Alipoona bado wanashangilia aliinua mkono wake wa kushoto juu na kusema, “Basi! Basi, wananchi, sina shaka ujumbe umefika.” Kisha aliketi na kuwaacha wenzake wakiumwa mbavu kwa vicheko.

  Utulivu ulirejea taratibu. Kabla kila mmoja amakinike, mwendesha mjadala alimpa nafasi mzee mmoja aliyekuwa amevutiwa na mazungumzo naye kuchangia. Mzee yule alicheka kidogo, akasafisha koo na kuwapongeza wachangiaji waliomtangulia kisha naye akasema yake.

  “Mambo hayo yote ni kama pacha lakini pekee hayatoshi. Miundomsingi inahitaji watu wa kuitumia, navyo viwanda vinahitaji wafanyakazi. Watu hao wasipokuwepo, vitu hivyo havina maana. Watu wao wanahitaji kuwa na afya bora. Hospitali zinahitaji kuwa katika kiwango cha kutoa huduma za kuridhisha. Zinahitaji wataalamu wasiobabaisha, vyombo vya kisasa vya udodosi na upasuaji, dawa nzuri na mazingira safi kwa ajili ya wagonjwa. Halafu huduma hiyo nzuri iwe inaweza kufikiwa na kila mtu.”

  Alitua kidogo. Sasa kila mtu alikuwa ametulia kama ardhi iliyonyeshewa. Kisha akaendelea, “Pamoja na hayo, ipo haja ya huyo mfanyakazi kupata pa kuweka ubavu wake. Akiisha kuichapa kazi anahitaji kurudi nyumbani. Si nyumbani kwa maana ya mahali pa kupangisha bali nyumbani kwa maana ya mahali pake mwenyewe. Hivyo panahitaji kuwepo mpango wa wafanyakazi kununua nyumba kwa bei nafuu. Mtu si kama ndege anayeweza kuishi mtini na akaamka kushika shughuli zake. Mtu huhitaji makao yake. Haya yote yakifanywa kwa pamoja na kwa ufanisi basi tutakuwa tumeanza kujiandaa kupaa kwa mbawa zetu wenyewe.”

  Alipomaliza kusema alishika njia na kwenda zake bila kutazama nyuma. Sote tulijikuta tunacheka kwa sauti huku tumetabasamu.
  1. Bainisha mambo matatu ambayo yanaleta utangamano baina ya vijana wa jamii hii.    (alama 3)
  2. “Kupata elimu pekee hakutoshi kutoa maendeleo.” Thibitisha kwa hoja mbili kutoka kwenye kifungu. (alama 2)
  3. Kwa kutoa hoja nne, onyesha uhusiano uliopo kati ya nguzo mbalimbali za maendeleo kwa mujibu wa kifungu. (alama 4)
  4. Eleza mambo matatu ambayo yanawachangamsha vijana katika kifungu. (alama 3)
  5. Kauli, “upepo mwanana ulikuwa ukipita na kuzipapasa ngozi zetu,” imetumia mtindo gani wa lugha? (alama 1)
  6. Eleza maana ya ‘tulinoleana bongo’ kwa mujibu wa taarifa. (alama 1)
  7. Andika kisawe cha ‘hoja’ kwa kurejelea kifungu. (alama 1)
 2. UFUPISHO (Alama 15)
  Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.

  Neno teknolojia hutumiwa kuelezea maarifa ya kisayansi yanayosaidia kutekeleza jambo au mambo fulani. Teknolojia hurahisisha kazi anayofanya binadamu maishani mwake. Hali hii hutokana na ukweli kuwa vyombo mbalimbali na mashine atumiazo binadamu ni mazao ya teknolojia. Teknolojia ina historia ndefu kwa kuwa ilianza enzi za kale takriban miaka milioni mbili iliyopita, ambapo binadamu alitumia mawe kama malighafi ya kutengeneza zana zake za kazi. Hii ni baada ya kugundua kuwa mawe yalikuwa na uwezo wa kukatakata na hata kupambana na wanyama hatari.

  Hatua kubwa ya maendeleo ya teknolojia ilianza katika karne ya kumi na nane ambapo Mapinduzi ya Viwanda yalishika kasi. Mapinduzi haya ya Viwanda yalishika kasi huko Ulaya katika nchi kama vile Uingereza na Marekani. Katika kipindi hiki, mashine zilitengenezwa kwa wingi huku viwanda vikiongezeka na kuifanya kazi ya binadamu kuwa nyepesi. Katika siku tunazoishi, teknolojia imekuwa na athari kubwa katika maisha ya binadamu. Nyingi za athari hizi ni chanya. Imeweza kuturahisishia mawasiliano, usafiri, elimu, biashara na kuimarisha kilimo, afya, kiwango cha maisha pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha ajira duniani.

  Ni kutokana na teknolojia ambapo afya ya binadamu imeweza kuimarika. Hali hii imetokana na uvumbuzi wa dawa za kutibu na kuzuia magonjwa mbalimbali. Aidha, mashine za kimatibabu kama vile uyoka, stethoskopu, hadubini miongoni mwa nyingine huwasaidia matabibu kutambua magonjwa mapema iwezekanavyo kabla ya athari za magonjwa haya hazijazagaa mwilini mwa binadamu. Kutokana na uvumbuzi kiteknolojia katika sekta ya matibabu, binadamu ameweza kuishi kwa muda mrefu akiwa na siha bora. ukweli ni kuwa teknolojia imeyazika katika kaburi la sahau, magonjwa yaliyokuwa yakiwaangamiza watu kama surua, ukoma(matana, jedhamu), kifua kikuu na kadhalika.

  Isitoshe, kuimarika kwa mawasiliano ni matokeo mengine ya teknolojia. Vyombo vya mawasiliano kama rununu, kitandazi, wavuti, mdahalisi na baruapepe ni nyenzo za mawasiliano ambazo zimetokana na uvumbuzi wa teknolojia. Kutokana na nyenzo hizi, binadamu wameweza kubadilishana maarifa na kuwasiliana kwa wepesi na upesi zaidi ikilinganishwa na hapo awali ambapo watu walisafiri au kutuma barua ili kuwasiliana na wenzao; hali iliyochukua muda mrefu na hata kuhatarisha maisha ya binadamu.

  Vilevile, kutokana na teknolojia, shughuli za kielimu zimerahisishwa pakubwa. Kwa mfano, uvumbuzi wa mashine za kuchapisha vitabu pamoja na tarakilishi umerahisisha utafiti. Watu hutumia tarakilishi, taraweo,(kiyuweo, kipakatalishi) na hata rukono kufanya utafiti kuhusu masuala ya kielimu. Wao hutumia mtandao ambapo hufanya utafiti wa maswala mbalimbali. Utafiti wa mwanafunzi au hata wanagenzi huweza kutumwa kwa walimu au hata wahadhiri kupitia kwa baruapepe, kukaguliwa na wahusika kutumiwa matokeo yao. Kinyume na ilivyokuwa hapo awali ambapo shule zililalamika kuwapa wanafunzi ripoti za matokeo ya, ripoti hizi zinatumwa moja kwa moja kwa wazazi wanaoyatalii na kujadiliana na wanao namna ya kuyaboresha. kwa kufanya hivi, washikadau wote wanahusishwa ili kuhakikisha kuwa mwanafunzi amenawiri masomoni.

  Manufaa mengine ya teknolojia ya sasa ni uvumbuzi wa vyombo vya usafiri. Vyombo hivi vimerahisisha uchukuzi na usafiri kwa kuwa vinaweza kutegemewa na hufanya kazi kwa kasi bila kuhatarisha maisha ya binadamu. Jambo la kutia moyo ni kuwa vyombo hivi vya usafiri vinaendelea kuongezeka kila uchao kutokana na juhudi za kuvitengeneza kuongezeka. Vyombo hivi vya kisasa ni kama vile meli, magarimoshi ya kisasa, magarikebo, bajaji, ndege, feri na kadhalika.

  Matokeo mengine ya teknolojia ni kuongezeka kwa nafasi za ajira. Nafasi za kazi zimebuniwa kama utangazaji katika redio na runinga, uuzaji wa rununu, uuzaji wa kadihela, uhandisi pale ambapo wahandisi wa vyombo vya kielektroniki huikarabati mitambo ya mawasiliano na hata vyombo vya mawasiliano vilivyoharibika.

  Halikadhalika, kilimo kimeweza kuimarika kutokana na matumizi ya teknolojia. Hali hii imetokana na matumizi ya kuvumbuliwa kwa dawa za kuwaangamiza wadudu wanaoharibu mimea. Matokeo ya hili ni mavuno kochokocho. Mimea inayostahimili kiangazi inazidi kuvumbuliwa hivyo nchi huweza kupamabana na janga la njaa. Wataalamu wa kilimo wameweza kuvumbua mimea inayokua kwa muda mfupi na yenye mavuno tele. Ni kutokana na teknolojia ambapo kilimo kimeimarika pakubwa.

  Usalama umeimarika kutokana na njia mwafaka za kuwadhibiti wahalifu kama vile king’ora na kamera za doria. Vifaa hivi huwafanya wahalifu kuhofia kutekeleza maovu au wizi. Pia kuna vifaa vya kuyakagua magari pamoja na abiria ili kutambua vifaa hatari kama vile vilipuzi na silaha nyinginezo zinazotumiwa kuwaangamiza raia. Hivyo, teknolojia imechangia pakubwa katika udumishaji wa usalama nchini na hata ulimwenguni.

  Michezo mbalimbali ipatikanayo kwenye tarakilishi, kiyuweo na hata rukono ni nyenzo ya burudani kwa binadamu. Binadamu ameweza kuburudika anapocheza au hata kuitazama michezo anuwai kwenye vyombo hivi na hata kufurahia nyimbo na sinema zilizomo kwenye vyombo vya kiteknolojia.

  Fauka ya hayo, biashara imeweza kuimarika madhali kutokana na teknolojia biashara inafanyika haraka na kwa gharama ya chini. Vyombo vya mawasiliano kama vile mtandao, tovuti, rununu na baruapepe vimechangia pakubwa katika uimarishaji wa biashara. Kupitia vyombo hivi, mfanyabiashara anaweza kutangaza, kuuza na hata kuagiza bidhaa kwa wepesi mkubwa.

  Hata kama teknolojia ina faida tele, inayo madhara hasa pale ambapo baadhi ya watu huitumia kuwaangamiza wenzao kwa mfano, wanapotengeza zana za kiniuklia ambazo hulenga kuwaua watu. Si ajabu kuwaona watu wakipiga zohali na kutekwa na mitandao ya kijamii. Vitendo vya kinyama kama vile ulipuaji wa magari na uavyaji mimba hutokana na maarifa ya kiteknolojia. Pana haja ya binadamu kutawaliwa na utu anapotumia vifaa na vyombo vya teknolojia. Kila mtu anastahili kutumia teknolojia kwa manufaa yake na ya wenzake. Kwa kufanya hivi sote tutaweza kunufaika na kufurahia matunda ya teknolojia.
  1. Fupisha aya tano za mwanzo. (maneno 80-85; alama 7,1 ya utiririko)
   Matayarisho
   Jibu
  2. Bila kupoteza maana, eleza mawazo makuu yanayojitokeza katika aya saba za mwisho. (maneno 90-100; alama 8, 1 ya utiririko)
   Matayarisho
   Jibu
 3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
  1. Andika maneno yenye sifa zifuatazo: (alama 2)
   1. kitambaza, irabu ya chini, irabu ya nyuma wastani
   2. sauti mwambatano ya midomo na meno, irabu ya mbele wastani, kipasuo sighuna cha ufizi, irabu ya nyuma juu
  2. Onyesha muundo wa silabi katika neno lifuatalo: machweo (alama 2)
  3. Weka shadda panapofaa ili kuibua dhana zilizo mabanoni. (alama 2)
   1. Walakini (kasoro)
   2. Ala (kihisishi)
  4. Ainisha mofimu katika maneno yafuatayo: (alama 2)
   1. mtoto
   2. hatukumtembelea
  5. Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya mstari: (alama 2)
   Sisi sote tunacheza uwanjani.
  6. Tunga sentensi moja yenye muundo ufuatao: (alama 2)
   KN(N+RH) + KT(t+E)
  7. Tumia mzizi –w- katika sentensi kama: (alama 2)
   1. Kitenzi kisaidizi
   2. Kitenzi kishirikishi
  8. Akifisha sentensi ifuatayo: (alama 2)
   wanafunzi wameanza kuchambua riwaya ya nguu za jadi nguu alimuuliza jadi
  9. Eleza uamilifu wa nukta pacha katika tungo hili: (alama 1)
   Uraia: Mlokole
   Jinsia: Mume
   Kaunti: Angaza
  10. Andika maana mbili zinazojitokeza katika sentensi ifuatayo: (alama 2)
   Mwema, babake Idi na Asha wameenda Marekani.
  11. Kanusha sentensi ifuatayo: (alama 2)
   Wewe umemaliza kulima shamba ambalo lingalikuwa langu ningalifurahi.
  12. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa: (alama 2)
   Wezi hao waliiba vikapu na ng’ombe.
  13. Andika sentensi ifuatayo upya kwa kufuata maagizo: (alama 1)
   Nafula amemwazima Koech kitabu cha Fasihi. (Anza kwa: Kitabu…)
  14. Bainisha chagizo katika sentensi ifuatayo: (alama 1)
   Mtambo huu umekarabatiwa kwa ustadi mkubwa mno.
  15. Tambua shamirisho katika sentensi ifuatayo: (alama 3)
   Eleza amenunuliwa sare mpya kwa hundi ya shilingi elfu tano na shangazi yake.
  16. Tambua kisha ueleze majukumu ya kisarufi ya virai vilivyokolezwa katika sentensi ifuatayo: (alama 2)
   Shinikizo la mahirimu huhitaji kushughulikiwa kwa makini.
  17. Tunga sentensi moja changamano iliyo na vishazi viwili tegemezi. (alama 1)
  18. Zigeuze sentensi zifuatazo ziwe katika kauli zilizoonyeshwa mabanoni. (alama 2)
   1. Kushiriki katika kipindi hicho kulifanya asifiwe. (wakati uliopo hali ya kuendelea)
   2. Lulu alifurahi. Lulu alimpata mchumba.(Unganisha kuwa sentensi moja katika wakati uliopita hali timilifu)
  19. Nomino zifuatazo zimo katika ngeli gani? (alama 2)
   1. Simanzi…………………………………………………………………………
   2. Nyembe…………………………………………………………………………
  20. Tunga sentensi moja kubainisha maana tofauti za vitate: mbishi na mpishi (alama 2)
  21. Thurea ni kwa nyota, …………………….…..kwa mablanketi ilhali …………………..… kwa wezi. (alama 2)
  22. Hamadi ni kwa kutaka kitu kinusurike,……………………………….ni kwa kukubaliana na jambo. (alama 1)
 4. ISIMUJAMII (ALAMA 10)
  Fafanua sifa kumi za lugha inayotumika katika mazingira ya siasa.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions - Maranda High School Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?