Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Lainaku II Joint Mock Examination 2023

Share via Whatsapp

Maagizo

 • Jibu maswali manne pekee.
 • Swali la kwanza ni la lazima.
 • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki yaani;
 • Riwaya, Ushairi, Hadithi fupi na Fasihi Simulizi.
 • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
 • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU YA A: TAMTHILIA
T.M Arege: Bembea ya Maisha

 1. LAZIMA
  1. Tumbo lenyewe limeshafanya mazoea. Ardhi hiyo ya kulimwa na kuzalisha chakula iko wapi? Hata ingekuwepo mvua yenyewe imefanya ugeni. Imeadimika afadhali wali wa daku. Sasa ni wakati wa kujifunga masombo…
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
   2. Fafanua sifa za msemaji wa maneno haya. (alama 2)
   3. Eleza vipengele vinne vya kimtindo vinavyobainika katika dondoo hili. (alama 4)
  2. Eleza jinsi maudhui ya uwajibikaji yanavyojitokeza katika tamthilia ya Bembea ya Maisha. (alama 10)

SEHEMU B: RIWAYA

A. Matei: Chozi la Heri

Jibu swali la 2 au la 3

 1.  
  1. “Anayeusikiliza wimbo huu anauona mrefu kuliko zile ambazo mja huyu huimba kila siku.”
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
   2. Eleza aina ya “wimbo huu”. (alama 2)
   3. Eleza aina mbili za taswira zinazojitokeza kwenye “wimbo huu”. (alama 4)
   4. Eleza maudhui mbalimbali yanayojitokeza kwenye “wimbo huu”. (alama 10)
 2. “Nakumbuka asubuhi ya pili baada ya mtafaruku kuanza. Nilikuwa sebuleni na mwanangu tukitizama runinga”.
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
  2. Eleza umuhimu wa mandhari ya dondoo hili. (alama 6)
  3. Tambua mbinu kuu ya kimtindo iliyotumika katika dondoo. (alama 2)
  4. Kwa kutolea mifano mwafaka eleza jinsi mbinu uliyotaja hapo juu ilivyotumika kukuza maudhui riwayani. (alama 8)

SEHEMU YA C: USHAIRI

Jibu swali la 4 au la 5

 1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
  Mtu ni afiya yake, ndio uzima wa mtu,
  Mtu ni kuwa na chake, hakuwi ela kwa kitu,
  Mtu ni bahati yake, kupendekeza kwa watu,
  Mtu si fakhari kwake, kuitwa nyama ya mwitu.

  Mtu ni ulimi wake, kunena vyema na watu,
  Mtu ni kijungu chake, kuweka mawe matatu,
  Mtu ni mwenda kwa lake, mtoshwa na kila kitu,
  Mtu si uzuri kwake, kuitwa nyama ya mwitu.

  Mtu ni mwenye nadhari, apimaye kila kitu,
  Mtu ni moyo hariri, mwenye imani na watu,
  Mtu ni alo na ari, shika sana mwana kwetu,
  Mtu si yake fakhari, kuitwa nyama ya mwitu.

  Mtu ni mkono wazi, mtasada kuna watu,
  Mtu ni mwenye maozi, ku oneya kila kitu,
  Mtu ni alo tulizi, asopenda utukutu,
  Mtu si jambo pendezi, kuitwa nyama ya mwitu.

  Mtu ni mwenye ahadi, ndio u’ngwana na utu,
  Mtu ni alo baridi, mbe mbelezi wa watu,
  Mtu ni moyo asadi, aso onewa na mtu,
  Mtu si yake ifadi, kuitwa nyama ya mwitu.

  Mtu niliyo yanena, pima sana ewe mtu,
  Mtu si kujatukana, kukirihi nyoyo watu,
  Mtu nakupa maana, wende nyendo za kiutu,
  Mtu si uzuri sana, kuitwa nyama ya mwitu.
  Maswali
  1. (Jadili ujumbe wa mshairi. (alama 2)
  2. Ainisha shairi kutegema: (alama 2)
   1. Mpangilio wa maneno.
   2. Vina.
   3. Idadi ya mishororo.
   4. Idadi ya vipande.
  3. Eleza mbinu nne za kimtindo ambazo zimetumiwa. (alama 4)
  4. Thibitisha matumizi ya uhuru wa kishairi. (alama 3)
  5. Andika ubeti wa pili kwa lugha tutumbi. (alama 4)
  6. Fafanua nafsi-neni na nafsi-nenewa katika shairi hili. (alama 2)
  7. Kwa kutolea mifano, eleza aina tatu za urudiaji zinazojitokeza kwenye shairi hili. (alama 3)
 2. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
  Nikiwa na njaa na matambara mwilini,
  Nimehudumika kama hayawani,
  Kupigwa na kutukanwa,
  Kimya kama kupita kwa shetani,
  Nafasi ya kupumzika hakuna,
             Ya kulala hakuna,
             Ya kuwaza hakuna,
  Basi kwani hili kufanyika,
  Ni kosa gani lilotendeka,
  Liloniletea adhabu hii isomalilizika?
  Ewe mwewe urukaye juu angani,
  Wajua lililomo mwangu moyoni,
  Niambie pale mipunga inapopepea,
  Ikatema miale ya jua,
  Mamangu bado angali amesimama akisubiri?
  Je nadhari hujitokeza usoni,
  Ikielekea huku kizuizini?

  Mpenzi mama, nitarudi nyumbani,
  Nitarudi hata kama ni kifoni,
  Hata kama maiti yangu imekatikakatika,
  Vipande elfu, elfu kumi, Nitarudi nyumbani,
  Nikipenya kwenye ukuta huu, Nikipitia mwingine kama shetani,
  Nitarudi mpenzi mama…Hata kama kifoni!
  Maswali
  1. Lipe shairi hili kichwa mwafaka. (alama 1)
  2. Tambua nafsi-neni katika shairi hili. (alama 2)
  3. Eleza toni mbili zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 2)
  4. Eleza mambo manne ambayo mshairi analalamikia. (alama 4)
  5. Fafanua dhamira katika shairi hili. (alama 2)
  6. Thibitisha kuwa hili ni shairi huru. (alama 2)
  7. Taja na ufafanue sifa mbili za nafsi neni. (alama 2)
  8. Fafanua mbinu tatu za kimtindo zilizotumika katika ubeti wa tatu. (alama 3)
  9. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa katika shairi hili. (alama 2)
   1. Hayawani
   2. Nadhari

SEHEMU D: HADITHI FUPI

D.W Lutomia na P. Muthama(wah): Mapambazuko ya Machweo na Hadithi nyingine
Jibu swali la 6 au la 7
D.W Lutomia: Msiba wa kujitakia

 1.  
  1. “Wetu ni wetu, hata akiwa mbaya…ni wetu.”
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
   2. Eleza sifa za huyu anayeshikilia msimamo wa “mtu wetu”. (alama 2)
   3. Eleza mbinu mbili za kimtindo zinazojitokeza kwenye dondoo hili. (alama 4)
   4. Kwa kurejelea hadithi “Msiba wa Kujitakia”, eleza misimamo mbalimbali ya mwandishi. (alama 10)

    R.Wangari: Fadhila za Punda
 2.  
  1. Changanua mtindo katika kifungu kifuatacho. (alama 10)
   Alasiri ile, baada ya ibada mbili, mhubiri akawa hoi kwa mavune. Akatamani kufika nyumbani apumzike, kazi ya kuwalisha kondoo wa Mungu si kazi rahisi. Wamefika nusu safari, bintiye katulia kama maji mtungini. Akimtazama kipembe, anamkumbusha marehemu mkewe.Miaka mitatu sasa na dhiki ya kuondokewa haijamwisha. Alihisi ukiwa, akatamani mwenziye.Sasa kazi kukilea kitoto chao, kibinti hiki kilicho mlanda mamake kama shilingi kwa ya pili. Nyumba ilijaa kicheko alipokuwa hai mamake Lilia. Kama si bintiye ambaye ulimi wake hautulii, kihoro kingemvamia labda hata kumvuta kuelekea kaburini. Lakini Lilia, malaika wake, hampi utulivu wa kuwaza sana kuhusu upweke wake. Ilimshangaza sasa kuwa kanyamaza vile. Kumbe kwa muda tu!
  2. Kwa kutolea mifano mwafaka eleza jinsi hadithi “Kila Mchezea Wembe” ilivyotumia kinaya kufanikisha ujumbe wake. (alama 10)

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI


  1. Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
   Ikiwa kweli wewe ni mkaza mwanangu,
   Nami ndimi nilompa uhai mwana unoringia,
   Anokufanya upite ukinitemea mate,
   Chakula kuninyima, wajukuu kunikataza ushirika,
   Mungu na waone chozi langu, wasikie kilio changu,
   Mizimu nawaone uchungu wangu, radhi zao wasiwahi kukupa,
   Laana wakumiminie, uje kulizwa mara mia na wanao,
   Usiwahi kufurahia hata siku moja pato lao,
   Watalokupa likuletee simanzi badala ya furaha,
   Wakaza wanao wasikuuguze katika utu uzima wako!
   1. Tambua aina ya mazungumzo haya na utoe sababu. (alama 2)
   2. Eleza sifa mbili za nafsi nenewa. (alama 2)
   3. Taja na ueleze sifa nne za kipera hiki cha fasihi simulizi. (alama 4)
   4. Unanuia kutumia mbinu ya maandishi kuhifadhi kipera hiki cha fasihi simulizi. Eleza faida na hasara za kutumia mbinu hii. (alama 6)
  2. Eleza faida tatu na hasara tatu za miviga . (alama 6)

MWONGOZO WA USAHIHISHAJI

SWALI LA LAZIMA – Bembea ya maisha

 1.  
  1.  
   1. Maneno ya Kiwa kwa mamake Dina wakiwa nyumbani kwao (Dina)wanajadiliana baada ya Dina kulalamikia hali ya Kiwa kukataa kula chakula alama 4x1
   2.  
    • sifa za Kiwa
    • mwenye utu
    • mweledi/anaelewa
    • mwenye imani kwa mungu
    • mwenye shukrani              (aeleze) kadiria jibu la mwanafunzi (2x1)
   3. Mtindo (4X1)
    • Tashihisi-tumbo kufanya mazoea.
    • Swali la balagha- iko wapi?
    • Tashbihi-imeadimika afadhali wali wa daku.
    • Msemo- kujifunga masombo.
  2. Maudhui ya uwajibikaji
   • Neema anaelimisha dada zake Asna na Salome.
   • Kiwa anafika nyumbani kumjulia hali mamake (Dina).
   • Dina anajitolea kumsaidia Sara anapokuwa mgonjwa.
   • Neema anampeleka mama yake hospitalini.
   • Neema kumfuata mamake kijijini ili kumpeleka hospitalini.
   • Bunju ana mzigo mzito wa majukumu; anayatekeleza yote; kununua chakula, kununulia Neema gari n.k
   • Bunju anamuokoa Neema kutokana na ajali aliyoipata; anagharamia matibabu yake.
   • Neema anatumia mshahara wake kwa matibabu ya wazazi wake.
   • Alipokuwa mwalimu Yona anawaadilisha wanafunzi kwa adhabu ya kiboko.
   • Neema anamrejesha mamake nyumbani baada ya matibabu kwa sababu hali yake haitaki vuta nikuvute za usafiri.
   • Yona hamsaidii mkewe Sara katika majukumu ya nyumbani-hawajibiki.
   • Yona amlazimisha Sara kumwita bintiye Neema aje ampeleke hospitalini-hawajibiki.
   • Mfanyikazi kwa Yona anaondoka kwa kudai kazi ni nyingi.
   • Sara anadai wafanyakazi wa kisasi hiki hawapendi kuchapa kazi.  (10x1)
    Tan: Mtahini anaweza kuonyesha pande zote mbili kuwajibika au kutowajibika.

SEHEMU B: RIWAYA YA CHOZI LA HERI

 1.  
  1.  
   1. Muktadha - Ni maneno/maelezo ya mwandishi/msimulizi akimrejelea Shamsi/wimbo wa Shamsi aliokuwa anauimba usiku wa manane kwa wakaazi wa mtaa wa Afueni unaonyesha matatizo mengi aliyoyapitia maishani. (4x1)
   2. Mbolezi- anasimulia matatizo aliyoyapitia yaliyomwingiza ulevini. (1x2)
   3.  
    • Taswira sikivu- anayeusikiliza wimbo huu…
    • Taswira oni- anauona mrefu…
    • Taswira hisi- Hali ya kutamauka inadhihirika. (2x2=4)
   4. Maudhui kwenye “wimbo huu”.
    • Ulevi na athari zake.
    • Unyakuzi wa ardhi-Bwana Mabavu.
    • Ufisadi- Hatimiliki bandia- Bwana Mabavu.
    • Unyanyasaji- wafanyakazi kulipwa mshahara duni.
    • Umaskini- Jamii ya Shamsi.
    • Ajira- kutawaliwa na ndugu za waajiri.
    • Malezi- Babake Shamsi kumsomesha hadi chuo kikuu.
    • Elimu- ulipaji karo ni muhimu.
    • Uongozi mbaya- Shamsi na wenzake kufutwa kazi bila sababu maalum.
    • Usimamizi mbaya- viongozi kukosa kujenga hospitali na huduma za kimsingi.
    • Mapuuza
    • Tamaa
    • Ubaguzi
    • Tanzia
    • Uwajibikaji
    • Ndoa
    • Utabaka
    • Uzalendo
    • Utamaduni
     Tan: Atoe maelezo mwafaka (Zozote 10x1)
  1. Muktadha: Msemaji ni Kaizari, akiwa katika Msitu wa Mamba(kumbukizi)anakumbuka matukio yalivyokuwa baada ya uchaguzi wa Mwekevu.(vita) (4x1)
  2. Umuhimu wa mandhari (Msitu wa Mamba)
   • Uhitaji wa vitu vya kimsingi: vyoo.
   • Ukatili pale Lime na Mwanaheri wanabakwa.
   • Madhara ya vita baada ya uchaguzi.
   • Matukio kambini, kukosa chakula, vifaa vya matumizi.n.k
   • Utu- mwenye matwana aliwabeba Kaizari na familia yake.
   • Uchafuzi wa mazingira- msitu kufyekwa.
   • Kujenga wahusika k.v Kute.
   • Kuonyesha migogoro ya kifamilia k.v ya Selume.
   • Suluhisho kwa migogoro ile-Selume kuamua kuondoka.
   • Ukosefu wa ajira na hali ya kutamauka.
   • Kuonyesha mahali (Msitu wa Mamba)
   • Kuonyesha nafasi ya mashirika ya kibinadamu. (6x1)
  3. Mbinu kuu ya kimtindo - kisengere nyuma/mbinu rejeshi. (1x2)
  4.  
   • Umaskini- ni vigumu kumudu gharama ya matibabu.
   • Elimu- Mwalimu Meli aliwafunza mifumo ya uzalishaji.
   • Mabadiliko- Asilimia kubwa ya watu walipania kumpigia Mwekevu kura.
   • Nafasi ya mwanamke- Mwekevu alipania kuwa kiongozi.
   • Kifo- Ridhaa anaelezea kuhusu kifo cha Makaa.
   • Vita- Kaizari anasimulia kuhusu ghasia baada ya uchaguzi.
   • Ubakaji- Kaizari anasimulia jinsi alivyoona mabinti zake wakibakwa.
   • Ndoa za mapema- Ndoa ya Pete na Fungo inaelezewa kupitia mbinu rejeshi.
   • Ukatili- Kisa cha Lemi kuteketezwa kinaelezewa kupitia mbinu rejeshi.
   • Ufisadi- Lunga aliachishwa kazi alipokataa kuruhusu mahindi yenye sumu kuuziwa watu.
    Tan: Kadiria jibu la mwanafunzi. (8x1)
 2.  
  1. Ujumbe
   • Umuhimu wa kuwa na utu kwani ni vibaya binandamu kufanya kama wanyama.Utu huonekana kwa matendo mema kama vile kuongea vizuri,kusaidia wengine nk (1x2)
  2. Kikwamba ,ukara,tarbia,mathnawi.(4x1/2)
  3. Mbinu za kimtindo :Takriri (mtu) istiari(mtu ni ulimi) msemo/nahau (mkono wazi)kejeli(kuitwa nyama wa mwitu)(4x1)
  4. Uhuru wa kishairi –Inkisari-alo-aliye,lahaja-maozi-macho,mazida-afiya-afya,kuboronga sarufi-shika sana mwana kwetu –mwana kwetu shika sana.kutenganisha maneno aso penda-asopenda.Kukopa hati kutoka lugha zingine(kh- fakhari), kutenganisha maneno mfano: aso onewa-asoonewa, mbe mbelezi- mbembelezi (3x1)
  5. Tutumbi-mshairi anasema kuwa mtu anajulikana kutokana na ulimi wake na jinsi anavyonena na watu.mtu anafananishwa na kijungu chake kinachowelewa mawe matatu.mtu mzuri ni yule anatosheka na alichonacho.Mshairi anamalizia kwa kushauri kuwa si vizuri mtu kuwa mbaya kwani atakuwa kama mnyama wa mwitu.(4x1)
  6. Nafsi neni-mshauri /anayependa utu/asiyependa fitina.Nafsi nenewa –watu wote /asiye na utu/katili/mwenye fitina(2x1)
  7. Silabi-ke,ke,ke,ke.Neno mtu,mtu.Kirai-kuitwa nyama wa mwitu(3x1)
 3.  
  1. Mama nitarudi/nitarudi/kizuizini(1x1)
  2. Nafsi neni-Mfungwa aliye kizuizini .Anauliza iwapo mama yake angali anasimama na kusubiri akitazama kule kizuizini aliko mtoto wake.(2x1)
  3. Toni mbili
   • masikitiko
   • matumaini-Aeleze.(2x1)
  4.  
   1. Kuachwa njaa
   2. Kufungwa
   3. kufukuzwa
   4. kutopewa nafasi ya kupumzika
   5. kuvalishwa matambara
   6. Kufanyishwa kazi kama mnyama (4x1)
  5. Dhamira ya mwandishi
   • Kulalamikia namna anatumiwa vibaya kizuizini.
   • Anakashifu madhila na mateso ambayo wafungwa hutendewa .
   • Kumpa mamake matumaini kwamba atatoka kizuizini siku moja.(1x2)
  6. Shairi huru
   • Lina mistari mishata na kifu.
   • Idadi ya mishororo katika kila ubeti inabadilikabadilika.
   • Vina vinabadilikabadilika.
   • Idadi ya mizani katika kila mshororo inabadilikabadilika.(2x1)
  7. Sifa za nafsi neni
   • Mwenye kulalamika
   • Mwenye matumaini
   • mwenye mapenzi-Eleza.    (2x1)
  8. Mtindo
   • Takriri-Nitarudi
   • Mdokezo-mama…..
   • Tashbihi-kama shetani
   • Taswira-Ya kizuizini
   • Balagha-akinisubiri? (3x1)
  9.  
   • Hayawani –mnyama/mwenda wazimu
   • Nadhari –Fikira/akili (2x1)

SEHEMU YA D: HADITHI FUPI

 1.  
  1. Kumbukizi ya Machoka kuhusu usemi wa Zuhura aliyesisitiza wamchague mtu wa kabila lao. Yuko chumbani mwake amesimama.Ni jioni, Alikuwa ametoka katika shughuli za kutafuta kibarua akakosa. (4x1)
  2. Sifa za Zuhura
   • Mwenye tamaa-Alipiga kura kwa kutokana na alichopewa.
   • Mjinga- Haelewi viongozi wanaochaguliwa watawasahau.
   • Mwenye matumaini- Anajitia moyo. (2x1)
  3. Mbinu mbili za kimtindo
   • Takriri- Wetu, Wetu.
   • Kinaya- Kudai kuwa wao ni wao hata akiwa mbaya. (2x1)
  4. Falsafa(Msimamo)
   • Ni muhimu kuheshimu maamuzi ya wananchi.
   • Ni muhimu kufuata taratibu za uchaguzi.
   • Ni watu wanaofaa kupiga kura tu wanahitajika kufanya vile (si wafu!)
   • Kuonyesha kuwa watu ambao si chaguo la mwananchi jinsi wao hujaribu kujihalalisha. (Sugu Junior)
   • Ni muhimu viongozi kutumia rasilimali za nchi vizuri si kuzifuja. Mamilioni yanatumika shereheni huku wananchi wakifa njaa.
   • Kutahadharisha raia dhidi ya uongo wa wawaniaji uongozi.
   • Kutahadharisha dhidi ya ubinafsi wa viongozi wetu. Meza zimeandaliwa kwenye hema wananchi wanaachwa kwenye jua.
   • Kuonyesha kilicho na mwanzo huwa na mwisho. Wananchi wanasusia kwenda kwenye sherehe ya kutawazwa kwa kiongozi mpya.
    (Zozote 5x2=10)
 2.  
  1. Mtindo
   1. Mbinu rejeshi/kisengere nyuma- Bintiye anamkumbusha.
   2. Sitiari/jazanda - Kondoo wa Mungu.
   3. Tashbihi - Kutulia kama maji mtungini.
   4. Majazi - Lilia
   5. Chuku - Kihoro kingemvuta kuelekea kaburini.
   6. Msemo - Shilingi kwa ya pili.
   7. Taharuki - Ilimshangaza sasa kuwa kanyamaza vile, kumbe muda tu!
   8. Koja - Kuorodhesha matukio. Lakini Lilia, malaika wake,
   9. Tashihisi - Kihoro kingemvamia.
   10. Usiahi - Muda tu!
   11. Tasfida - Kuelekea kaburini-kufa.  (Zozote 5x2)
  2. Kinaya Kila Mchezea Wembe
   • Ni kinaya kwamba pombe ambayo hunywewa kwa ajili ya starehe iligeuka na kuleta maombolezi kwa kuua watu wengi na kuathiri afya za watu.
   • Ni kinaya Mama Pima kuwekea watu dawa ya kuhifadhi maiti katika pombe. Iweje watu walio hai wanawekewa dawa ya maiti? Tembo anasema kuwa wao walikuwa mizuka, walipaswa kuwa makaburini si hospitali.
   • Ni kinaya kwamba Yule msichana mrembo katika baa aliyekutana na Tembo aliondokea kuwa nyanya kibogoyo mwenye sura ya kutisha. Kumbe usiku alionekana mrembo kama tausi kwa ajili ya kujirembesha.
   • Ni kinaya kwamba Tembo aliridhia kucheza densi naye ili asimvunje moyo huyo “tausi”. Hakumwogopa, asubuhi alipoamka alimwogopa Anji hakutaka kukawia kwake, aliondoka kwa papara.
   • Ni kinaya kwamba mwanzoni Tembo alipojipata katika nyumba ya Anji hakutaka kujua alifikaje hapo,lini na kwa nini lakini alipoamua kuongea, alimuuliza Anji, “kwa nini nipo hapa?”
   • Ni kinaya Tembo kumwita yule ‘tausi’ wa jana nyanya. Anasema “alikuwa anatifua umombo si mchezo nyanyangu huyo.”
   • Ni kinaya kuwa Tembo alijawa na woga na wasiwasi mwingi ilhali mwenyeji wake alikuwa anamhakikishia usalama wake, “Ondoa wasiwasi, you are in very safe hands.”
   • Ni kinaya kuwa Angelica alidai pesa za maintenance ilhali chumba chake hakikuonyesha dalili ya kutunzwa, kijumba cha mabati mabovu, mlango wenye mianya ya kutoshea ngamia na pazia la mlangoni lilikuwa limechanikachanika.
   • Anji pia alidai pesa za lishe bora ilhali afya yake haikuonyesha kama alikuwa akipata lishe bora awali. Alikuwa amekonda na kukondeana, mifupa yahesabika chini ya ngozi yake chakavu.
   • Ni kinaya kwamba Anji alidai malipo ilhali tayari pengine ndiye aliiba pesa za Tembo kutoka kwa pochi na pia simu.
   • Ni kinaya Anji kutoa vitisho, “lipa usichonge viazi” ilhali hakuwa na nguvu yoyote ya mwili ya kumlazimisha Tembo kutenda lolote. Alikuwa na mguu mmoja kwa hivyo Tembo angeamua kutoka nyumbani humo mbio hangempata.
   • Ni kinaya Anji kutarajia angekutana na Tembo tena, natumai tukutane tena hivi karibuni. Tembo ,mwenyewe alikuwa na mshawasha wa kutoka huko mbio na asimwone Anji milele na ndipo nafsini mwake alimjibu Anji, “pengine tukutane ahera”.
   • Ni kinaya kwamba Emmi hakusema chochote mumewe alipofika akitoka kwa Anji, alimwamkua na kumwandalia kiamsha kinywa kinyume na mumewe alivyotarajia. Tembo alitarajia makaripio kama ilivyokuwa ada lakini Emmi siku hiyo akawa mnyamavu.
   • Ni kinaya kwamba Tembo alikuwa amemtoroka au kumhepa Emmi lakini akirudi aliona afadhali ‘kuliwa’ na Emmi ‘zimwi’ ambalo lilimjua, halingemmaliza, alikuwa sasa anamtoroka Angelica, zimwi geni kwake.
   • Ni kinaya kuwa hata baada ya mkufu wa dhahabu kupakwa matope kwa kukanyangiwa chini na viatu vyenye matope, kisha ukatemewa mate, bado watu waliukimbilia, kila mtu akitaka apewe huo mkufu.
   • Ni kinaya kwamba Tembo alikusudia kuwashauri watu dhidi ya hatari za uraibu wa pombe. Alitaka wabadili mwenendo ilhali mwenyewe alionywa kila uchao na watu akakaidi.
   • Ni kinaya Tembo kumsihi kwa dhati Emmi arudi ilhali ndiye alisababisha Emmi na watoto kuondoka. Emmi alimlalamikia kila wakati kuhusu unywaji wa pombe hakumsikia mwishowe alidai talaka.
   • Ni kinaya kwamba Tembo akiwa hospitalini alitaka aletewe watoto awaone afarijike, ilhali alipokuwa mzima alikuwa akiwatelekeza hajui wanakula au kuvaa nini na hata kuwadanganya angewaletea peremende.  (Zozote 10x1)
 3.  
  1.  
   1. Maapizo - mhusika anamuomba Mungu kumwadhibu mkaza mwana wake kwa kumpuuza. (1x2)
   2. Sifa - Nafsinenewa(Mkaza mwana)
    • Mchoyo- Anamnyima chakula mzazi.
    • Mwenye dharau- Anadharau mama mzazi.  (2x1)
   3. Sifa za maapizo (4x1)
    • Hutolewa kwa watu walioenda kinyume.
    • Hutolewa kabla ya kula kiapo.
    • Yanaweza kutolewa na aliyeathirika.
    • Huaminiwa kuwa yataleta maangamizi.
    • Hutumia lugha fasaha.
    • Hutumia lugha yenye ukali. (4x1)
   4. Faida za maandishi.
    • Si rahisi kusahaulika(Data)
    • Hufikia vizazi vingi.
    • Si ghali.
    • Si rahisi data kupotea. (3x1)
     Hasara/Udhaifu
    • Kiimbo, toni, ishara hupotea.
    • Uhai asilia wa fasihi simulizi hupotea.
    • Watafiti kuandika wanayotaka/wanayohitaji.
    • Hadhira hupoteza fursa ya kushirikiana.
    • Huwafikia tu wanaojua kusoma. (3x1)
  2. Faida za miviga
   • Huelimisha wanajamii.
   • Huonyesha matarajio ya jamii kwa vijana.
   • Ni kitambulisho cha jamii.
   • Huendeleza na kuhifadhi utamaduni wa jamii.
   • Hukuza uzalendo.
   • Huhimiza na kukuza umoja wa jamii. (3x1)
    Hasara ya miviga
   • Baadhi ya sherehe hizi zimepitwa na wakati.
   • Baadhi hukinzana na malengo ya kitaifa.
   • Baadhi hujaza watu hofu.
   • Baadhi huhusisha ushirikina.
   • Baadhi ya sherehe hizi hugharimu kiasi kikubwa cha pesa. (3x1)
    Tan:Kadiria jibu la mwanafunzi.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Lainaku II Joint Mock Examination 2023.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?