Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Lainaku II Joint Mock Examination 2023

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Jibu maswali yote .
  • Majibu yote ni lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  1. UFAHAMU  (alama 15)
    Unafiki katika dini pia unadhihirika kupitia injili ya ufanisi ambayo siku hizi inaenezwa kama moto kichakani ikilinganishwa na walivyosisitiza mitume kuwa, watu watubu na kuishi maisha ya utakatifu. Si ajabu kumsikia mchungaji akiitisha shilingi elfu moja ili kupata thibitisho la iwapo jina lako linapatikana katika kitabu cha uzima wa milele. Huu ni unafiki kwa sababu maandiko matakatifu hayakubaliani na hilo. Waumini hujikuta wakinunua miujiza. Viongozi wanafiki huwaambia watoe kiasi fulani cha pesa ili kupona kutokana na magonjwa sugu kama vile ukimwi,saratani, kupinda kwa midomo na kadhalika.

    Nyadhifa katika dini pia huwavutia watu wengi.Utawapata baadhi ya viongozi wa dini wakitumia kila njia kubaki uongozini. Wao huwezah ata kuwanunua wafuasi ili wawapigie kura ama kuwaunga mkono katika kinyang'anyiro cha cheo fulani. Uongozi hutoka kwa Mungu. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wanaohubiri neno hilo la Mungu, utawapata wakiwa na mikutano ya siri ili kuwashawishi waumini kuhakikisha kuwa wamebaki uongozini.

    Haina haja ya kusaza waumini. Baadhi yao pia ni wanafiki. Utawapata wakishiriki kikamilifu katika masuala ya dini, ilhali nia yao ni tofauti. Vijana waliopatikana katika msikiti huko Mombasa wakipewa 'mafunzo va kidini ilhali bunduki na risasi pia zinapatikana mumo humo msikitini, ni mfano wa ulaghai na unafiki katika dini, (iwapo taarifa hizo ni za kweli). Wahubiri waliokuwa wakiendesha mafunzo hayo, ni wanafiki kwa sababu nia yao katika nyumba ya Mungu ilikuwa mbaya ndiposa makabiliano kati yao na polisi ilichukua muda wa saa saba hivi.

    Unafiki pia hujitokeza wakati ambapo baadhi ya viongozi wa dini hutumia dini kama daraja ya kuingia katika ulingo wa siasa. Wao hutumia madhabahu kufanyia kampeni ili kujitosheleza kisiasa. Kupinga maovu ya kisiasa kupitia dini ni sawa. Hata hivyo, kutumia dini kujipatia umaarufu ni kosa la kinafiki.

    Ni ombi langu kuwa dini itatumiwa kulisha kondoo wala si kuwapunja. Maandiko matakatifu yanapigia debe utakatifu katika dini wala si ulaghai na unafiki. Lazima kila muumini atoe zaka na sadaka kama ilivyo katika neno la Mungu. Hata hivyo nafasi hii isitumiwe na viongozi wenye ulafi kuwanyonya waumini wao. Mahali patakatifu ni lazima paheshimiwe wala pasitumiwe kama nyumba ya kupanga mashambulizi na maovu kwa wanadamu wasiokuwa na hatia.
    1. Kipe kifungu hiki anwani mwafaka. (alama 1)
    2. Onyesha msambao wa unafiki katika dini. (alama 4)
    3. Kwa nini waumini wanaonekana kuchanganyikiwa? (alama 2)
    4. Kwa nini injili ya ufanisi imeshamiri kuliko ile ya toba? (alama 2)
    5. Viongozi wengi wa kidini hawataki kung’atuka uongozini. Toa sababu moja. (alama 2)
    6. Waumini wanalaumiwa kwa nini? (alama 2)
    7. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyo tumika katika kifungu. (alama 2)
      1. ulaghai
      2. kuwapunja
  2. MUHTASARI
    Kila niwazapo kisa hiki, machozi hunitoka si haba. Hali ya huzuni ikanikumbatia kusadifu kusononeka. Nikawa sina sinani majibu kwa maswali kochokocho. Ama kweli “majuto ni mjukuu huja kinyume”.

    Katika kijiji chetu cha Kazamwendo, tuliishi pamoja kwa umoja na udugu ukazagaa kotekote. Wanakijiji walisaidiana kwa lolote lile, shida ya mmoja ikawa shida ya wote. Ungewakuta wavyele waliobugia chumvi nyingi wakiwapa nasaha vijana kwa hekima isiyo na kifani. Tabia ya ufuska ikakemewa na maadili ya utu wema yakafunzwa kwa wote. Utovu wa nidhamu ukakashifiwa pasi na maficho wala tasfida.

    Kukaja siku moja akatokea barobaro kutoka mjini. Asili yake ikawa kizungumkuti na hata jina lake halisi halikufahamika. Kila mmoja alimwita jina la utani “Mpanzi”. Ni wazi alikuwa na fedha na alivalia nadhifu. Fauka ya hayo, alipenda anasa sana. Vijana wengi kijijini walimfuata ili angalau wajinasibishe kwake. Miongoni mwa waathiriwa waliovutiwa na Mpanzi alikuwa Maria, mkoi wangu tuliyeishi pamoja tangu utotoni, tukicheza pamoja na hata kusoma shule moja.

    Ushirika wa Maria na Mpanzi ulielekeza mabadiliko makubwa katika tabia yake. Dharau ikachukua nafasi ya heshima, kiburi kikachukua nafasi ya unyenyekevu na aibu akaipa kisogo. Akakataa katakata kutangamana na wanakijiji wenzake akiwaita “washamba”. Kila mtu alistaajabishwa na yale mabadiliko ya kighafla yaliyompata Maria kwa kuwa hapo awali, licha ya kurembeka mithili ya tausi alikuwa na nidhamu ya hali ya juu akiwaheshimu wote na kijiheshimu pia.

    Maji yalizidi unga binti ya watu alipoanza kukwepa nyumbani akienda densini au ukipenda kwenye disko. Huko akatangamanana watu asiowajua walomwingiza katika uraibu wa ulevi na mapenzi haramu. Akabadilisha wanaume kama nguo ili apate fedha za kustarehe kutimiza raha na buraha. Mavazi yakawa minisketi au tumboketi. Akatembea nusu-uchi na wakati mwingine mavazi yakimbana huku akizua ashiki za kifisi mioyoni mwa wanaume. Akafaulu azimo lake na akafuatwa na wengi.

    Waviele walipoona hivyo, wakajaribu kwa juhudi na adili kumnasihi lakini akawa hasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Wakamwachia ulimwengu. Muda hakuisha mwingi Maria akaanza kuugua. Ikaanza kana kwamba ni kikohozi cha kawaida, kisha upele mwilini, afya ikadhoofika kiasi cha nyama kuganda kwenye mifupa.ungemtazama ungefikiri ni kiwiliwili cha mtu. Uchunguzi wa daktari ulibainisha wazi kuwa alikuwa ameambukizwa ugonjwa wa ukimwi. Mtoto wa tatu akalia kwa uchungu na majuto mengi. Akaomba kuwaona wanakijiji wote. Walipoitikia mwito wake aliwaomba msamaha kwa majozi huku akidondoa orodha ndfu ya majina ya watu aliofanya nao mahaba. Kwa sauti hafifu alisema “Taf-taf-adh-ali m-m-mnisamehe, nilidanganywa na mpanzi, nikasusia ushauri wa wazazi wangu. Nikaasi mema niliyopewa. Nawaomba muichukulie hali yangu kama funzo. Msife moyo kwa yote, siku hizi madktari husema ugonjwa huu hauna tiba lakini una kinga. Heri muende mpimwe mjue hali zenye za afya. Msiugue kama mimi ilhali kuna dawa zinazoweza kupunguza makali ya viini vya ugonjwa huu.” Mara pu! Akaanguka chini na kukata roho.

    Hali ya simamzi na majonzi ikakithiri maana ilikuwa dhahiri shairi watu wengi wengi walikuwa wameathirika. Fikira za kufa kwa wazazi na kuwaacha mayatima wachanga katika kijiji ziliwazuga. Siku ya mazishi ukumbi ulijaa hadi pomoni. Jamaa na marafaiki walliwasihi kumpa buriani. Muhubiri aliposimama kuhutubia waombolezaji alitamka “Maandiko yanasema kuna njia panda-njema kwa macho ya mwanadamu yenye hatima ya mauti na njema kwa mtazamo wa Mungu yenye mwisho mzuri. Kila mtu aepukane na uozo na msishiriki ngono kiholela. Waliooa wawe waaminifu ;waache “mipango ya kando.” Sote tuishi kwa kumcha Mungu ili tupone. Wote walisikiza wasia huo kwa umakini na utulivu. Maria alipozikwa, watu walirejea kwao huku wakiungama kuwa “Majuto ni mjukuu huja baadaye”.
    1. Fupisha ujumbe wa aya ya pili, tatu na nne kwa maneno 50. (Alama 7, mtiririko 1)
      Matayarisho
      Jibu
    2. Eleza kwa maneno 60 masuala ambayo mwandishi anaibua katika aya mbili za mwisho. (Alama 8, mtiririko 1)
      Matayarisho
      Jibu
  3. MATUMIZI YA LUGHA (alama40)
    1. Linganisha na ulinganue sauti ny na ng’. (alama 2)
    2. Onyesha shadda katika maneno yafuatayo. (alama1)
      1. chekesha…………………………………………………………………………………………………………
      2. embe……………………………………………………………………………………………………………
    3. Kamilisha majina ya makundi yafuatayo. (alama 2)
      1. …………………………………. cha nyanya
      2. ……………………………….. cha funguo
    4. Andika sentensi upya ukitumia aina za viwakilishi vilivyo katika mabano. (alama 2)
      1. Baadaye……………… walitoa ushahidi .(nafsi)
      2. Bilauri hii ina maji .Bilauri iliyowekwa pale ina maziwa.(Kiwakilishi cha pekee badala ya neno lililokolezwa wino)
    5. Andika katika usemi halisi. (alama3)
      Daktari alitaka kujua matatizo aliyokuwa nayo.
    6. Eleza matumizi ya na katika sentensi ifuatayo: (alama2)
      Walimu na wanafunzi wana nafasi nzuri ya kuwashauri wanafunzi wanaopotoshwa na wenzao.
    7. Andika wingi wa sentensi : (alama 2)
      Wembe ule ni mkali sana.
    8. Bainisha aina za shamirisho na chagizo katika sentensi ifuatayo: (alama 3 )
      Seremala alimtengenezea mwalimu mkuu madawati ishirini juzi.
    9. Tunga sentensi ukitumia neno mpaka kama: (alama 4)
      1. nomino
      2. kitenzi
      3. kielezi
      4. kihusishi
    10. Ainisha viambishi katika neno: (alama 2)
      Tutaonana
    11. Akifisha sentensi ifuatayo. (alama 3)
      mody alitusomea aya mbili kutoka kitabu maisha ya kisiwa cha hazina.
    12. Ainisha virai vilivyopigiwa mstari. (alama 2)
      Mawingu mazito ajabu yalijitandaza kwenye anga.
    13. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao : (alama 3)
      KN(N+RV) + KT(T+RE)
    14. Tumia vishazi vifuatavyo kuunda sentensi kulingana na maagizo. (alama 2)
      Wanasayansi walifanya majaribio .
      Wanasayansi walipata tiba ya ugonjwa huo.(Tumia ka ya kuonyesha tukio moja ni matokeo ya tukio lingine)
    15. Nyambua vitenzi vifuatavyo katika hali uliyopewa kisha uvitungie sentensi: (alama 2)
      1. la (kutendeshana)
      2. panga (kutendeshewa)
    16. Kamilisha sentensi ifuatayo kwa kutumia kinyume cha kitenzi kilichopigiwa mstari. (alama 1)
      1. Mafundi wataezeka……………………. paa la mabati.
    17. Eleza matumizi ya ki katika sentensi ifuatayo: (alama 4)
      Kijakazi na kitoto wamekuwa wakila wakiimba kikasuku.
  4. ISIMUJAMII (Alama 10)
    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.
    Msemaji 1:Wale wanaounga mkono mswada huu wa Finance waseme ndiyo!
    Sauti:Ndiyoooooooo!
    Msemaji 1:Wale wanaopinga mswada waseme laa!
    Sauti: Laaaa!
    Msemaji 1: Waliounga mkono mjadala wameshinda.
    Msemaji 2:Hoja ya nidhamu please!
    Msemaji 1: Mheshimiwa,sheria nambari 200 , kifungu cha 6, yazuia mjadala zaidi.
                      Naomba kuvunja baraza.
    1. Bainisha sajili ya mazungumzo haya. ` (alama 2)
    2. Eleza sifa zozote nne zinazojitokeza katika sajili uliyobainisha katika (a). (alama 4)
    3. Eleza jinsi mazingira hudhibiti mazungumzo: (alama 4)

MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

  1. UFAHAMU (alama 15)
    1. Unafiki/unafiki katika dini 1x1
    2.  
      1. Viongozi wa dini kushiriki katika uzinifu
      2. Injili ya ufanisi kushamiri.
      3. Viongozi kung’angania vyeo kuliko mioyo
      4. Kutumia dini ili kuingia katika siasa 4x1
    3.  
      1. Kutokana na unafiki wa viongozi wao. 1x2
    4. Mwanadamu kwa kawaida anataka maisha yaliyo na ufanisi,utajiri na uponyaji. 1x2
    5. Ili kuendelea kujinufaisha kwa kuwalaghai waumini. 1x2
    6. kukubali kutumiwa kuendeleza azma ya viongozi wanafiki. 1x2
    7.  
      1. udanganyifu/ujanja/uongo/chuku
      2. kuwadanganya/kuwahadaa/kuwaibia/kuwatapeli/kuwapokonya 2x1
        Kuadhibu: Sarufi- ondoa nusu alama kwa kila kosa litokeapo kwenye kijisehemu mahususi mradi tu pana alama nzima
        Hijai – ondoa nusu alama kwa kila kosa litokeapo kwa mara ya kwanza hadi upeo wa alama tatu
  2. MUHTASARI
    1.  
      1. Watu kuishi kwa umoja katika kijiji cha Kazamwendo.
      2. Hali ya kusaidiana
      3. Wazee kuwanasihi vijana kila wakati
      4. Utovu wa nidhamu/ufuska kukemewa
      5. Mjo wa Mpanzi kijijini
      6. Mpanzi kujitokeza kama mpenda anasa
      7. Mpanzi kuathiri vijana wengi akiwemo Maria anayepotoka kitabia    6x1
    2.  
      1. Wavyele kuingilia kati/kumwachia ulimwengu
      2. Maria kuugua
      3. Maria kudhibitishwa kuwa na ugonjwa wa ukimwi
      4. Maria kulia kwa uchungu na majuto mengi
      5. Kuomba kuonana na wanakijiji wote
      6. Kuomba msamaha/kutoa orodha ndefu ya waliofanya mahaba nao
      7. kushauri watu wapimwe ndio walioambukizwa wapate kinga.
      8. Hali ya simanzi kutanda
      9. Mahubiri katika mazishi yalitoa mafunzo kuhusu maisha mema  7x1
                       (a) 6
                       (b) 7
                       (c) 2        
                  M      15-hs-z
        Kuadhibu
        • Zingatia idadi ya maneno uliyoagizwa kuandika kwayo.
        • Jibu liandikwe kwa lugha nathari.
        • Makosa ya hijai na sarufi yaadhibiwe hadi upeo wa makosa sita kwa kila mojawapo.
  3. Matumizi ya lugha   (alama 40)
    1. Sauti ny na ng
      Kulinganisha
      1. nazali
      2. ghuna     2x½=1
        kulinganua
        ny : sauti ya kaakaa gumu
        ng’: sauti ya kaakaa laini 2x½=1
    2.  
      1. ‘ kesha
      2. ‘embe 2x½= 1
    3.  
      1. kichala cha nyanya
      2. kicha cha funguo 2x1=2
    4.  
      1. wao
      2. nyingine 2x1=2
    5.  
      • “Una matatizo gani/yapi/ yepi?”
      • Daktari alitaka kujua. 6x½=3
    6.  
      • na-kiunganishi
      • wana-umilikaji
      • wanaopotoshwa-wakati uliopo
      • na wenzao-uhusiano/mtendaji 4x1/2=2
    7. Nyembe zile ni kali sana. 1x2=2
    8.  
      1. mwalimu mkuu-kitondo
      2. madawati ishirini-kipozi
      3. juzi-chagizo 3x1
    9.  
      1. nomino(N)
        • Mpaka wa Kenya na Somalia umefungwa.
      2. kitenzi(T)
        • Maina anampaka mtoto mafuta.
      3. kielezi(E)
        • Ameenda mpakani.
      4. kihusishi(H)
        • Nitasafiri mpaka kwake. 4X1
    10.  
      • tu-nafsi/nafsi I/nafsi ya I wingi
      • ta-wakati/wakati ujao
      • an-kauli/kutendana
      • a-kiishio/kimalizio 4x½
        ✔                                                         ✔            ✔                     ✔
    11. Mody alitusomea aya mbili kutoka kitabu “Maisha ya Kisiwa cha Hazina .✔”✔ 6x½=3
    12.  
      • mazito ajabu –kirai kivumishi
      • kwenye anga-kirai kihusishi 2x1
    13. Fundi yule hodari alishona vizuri sana. 6x½=3
    14. Wanasayansi walifanya majaribio wakapata tiba ya ugonjwa huo. 1x2=2
    15.  
      • lishana:Maharusi hulishana keki wakati wa kufunga ndoa.
      • pangishiwa:Alipangishiwa nyumba kwa Mwema. 4x½=2     (mnyambuliko ½, sentensi ½)
    16. wataezua  1x1=1
    17.  
      1. kitoto/kijakazi-udogo/kudunisha
      2. wamekuwa wakila-kuendelea kwa kitendo kwa muda
      3. wakila wakiimba- utendo viwili kufanyika wakati mmoja
      4. kikasuku-jinsi/namna kitendo kilivyofanyika 4x1
        Kuadhibu
        • Sarufi - ondoa nusu alama kwa kila kosa litokeapo kwenye kijisehemu mahususi mradi tu pana alama nzima
        • Hijai – ondoa nusu alama kwa kila kosa litokeapo kwa mara ya kwanza hadi upeo wa alama tatu.
  4. ISIMUJAMII (Alama 10)
    1. Sajili ya bungeni/lugha ya bungeni (1x2)
    2.  
      1. Kuwepo kwa msamiati maalumu –mheshimiwa,kifungu
      2. Fomyula /Taratibu maalumu zimetumika wakati wa kujadiliana na kutoa uamuzi.
        Mfano: Wanaounga mkono …ndiyoooooooo!
      3. kunukuu vifungu vya sheria – kifungu nambari 4
      4. kuna kuchanganya ndimi. Mfano: mswada wa finance
      5. wazungumzaji: huelekezwa na spika
      6. uamuzi unatolewa kwa sauti nzito ndiyooooo/laa
      7. lugha hii inaibua hisia/nidaa – laaa!
      8. urasmi umedumishwa katika majadiliano
      9. lugha iliyotumika ni sanifu.
      10. lugha nyenyekevu/heshima imetumika.
      11. matumizi ya msemo – kuvunja baraza        4x1
    3.  
      1. Mzungumzaji huchota msamiati kutoka mahali anapozungumzia. Mfano:Msamiati wa sokoni akiwa sokoni.
      2. Mazingira huathiri uteuzi wa msimbo . Kwa mfano, mazingira rasmi huhitaji lugha rasmi
      3. Mazingira huathiri kiimbo na hata toni. Mfano:kituo cha polisi kidato cha juu
      4. Ishara anazotumia mtu hudhibitiwa na mazingira
      5. Mtu anayeishi katika mazingira magumu hutumia lugha kali /matusi ili kujihami  4x1
        Kuadhibu
        • Sarufi : adhibu kosa litokeapo kwa mara ya kwanza hadi upeo wa alama mbili (makosa 4)
        • Hijai : ondoa nusu maki kwa kila kosa litokeapo kwa mara ya kwanza hadi upeo wa alama mbili ( makosa 4).
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Lainaku II Joint Mock Examination 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?