Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - MECS Pre Mock Exams 2023

Share via Whatsapp

MAAGIZO:

  1. Jibu maswali manne pekee.
  2. Swali la kwanza ni la lazima.
  3. Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani; Riwaya, Tamthilia, Hadithi Fupi na Fasihi Simulizi.
  4. Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  5. Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili
  6. Karatasi hii ina kurasa 7 zilizopigwa chapwa
  7. Watahiniwa ni lazima wahakikishe kwamba kurasa zote za karatasi hii zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.

KWA MATUMIZI YA MTAHINI PEKEE.

Swali

Upeo

Alama

1

20

 

 

20

 

 

20

 

 

20

 

Jumla

80

 



MASWALI

SEHEMU A: SWALI LA LAZIMA (ALAMA 20)
1. USHAIRI
UTU NI NINI?
Utu na ubinadamu, ni kama yai na kuku
Utu ni ile nidhamu, mola aliyokhuluku,
Ubinadamu ni damu, ya utu wa kila siku,
Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake.

Ye yote mwanaadamu, ana asili ya utu,
Ya’ni kwenye yake damu, hakikosi hiki kitu,
Utu sifa maalumu, ya mtu kuitwa mtu,
Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake

Utu ni kiumbe hai, tunacho chaonekana
Utu kamwe haudai, tabia ya kujivuna,
Utu ni ule uhai, ushikao uungwana,
Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake

Utu huweza pimika, kwa hisia ya akili,
Huweza kuhifadhika, kulingana na fadhili,
Utu huweza pendeka, palipo na maadili
Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake

Utu unayo aibu, na tabia ya muhali,
Utu huenda na jibu, la Imani na ukweli,
Utu huiona tabu, tabia ya ujahili,
Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake 

Filosofia ya utu, inapinga ubinafsi,
Utu hautaki kitu, cha upeke wa nafsi,
Utu hauna kiatu, cheupe au cheusi,
Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake.

Utu wa kweli kwa mja, ni wenzake kuwajali,
Utu huiona haja, ya kujua watu hali,
Utu ni kuwa pamoja, kwenye shida mbalimbali,
Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake.

Utu ni ubinaadamu, udugu na wenzi wako,
Utu wote waheshimu, kwa nidhamu na kicheko,
Utu ona mwanadamu, sijitenge peke yako,
Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake

Ingawaje tu dhaifu, katika ubinafsi,
Utu kweli nausifu, ubinadamu halisi,
Utu ni sifa tukufu, iletayo kila nemsi,
Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake

  1. Tambua aina ya shairi hii kwa kutolea ithibati. (alama 2)
  2. Taja sifa tano za mtu mwenye utu kulingana na shairi. ( alama 5)
  3. Tambua mbinu mbili za kimtindo zilizotumiwa na mshairi. (alama 2)
  4. Ainisha shairi hili kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo. (alama 3)
    1. vipande
    2. vina
    3. mpangilio wa maneno
  5. Tambua nafsineni katika shairi. (alama 1)
  6. Tambua mbinu tatu alizotumia mshairi ili kukidhi mahitaji ya kiarudhi. (alama 3)
  7. Andika ubeti wa saba kwa lugha nathari. (alama 4)

SEHEMU B: RIWAYA,
A Matei: Chozi la Heri
Jibu swali la 2 au la 3

2. Jadili mchango wa wazazi na walezi katika kusambaratisha familia katika riwaya ya Chozi la Heri (alama 20)

au

3 Naona wingu kubwa angani likitembea kwa kedi na madaha na kulifunika jua...Mawingu yaliyoshiba yakataka kutapika yanagooka, yanakaribiana, kupigana busu na kusababisha mwanguko wa matone mazito ya mvua; matone yanayoanguka kwenye ngozi laini zą wanangu wakembe... ubavuni mwangu amelala maskini mke wangu... Sijui kama inahalisi kumwita mke wangu.... Siye, siye, siye-e-e-e. Tazama uso wake ulivyovamiwa na majeraha kikwi... Amevimba na kuvimbiana kama dongo la unga ngano baada ya kutiwa hamira. Lakini yeye hana la hamira!

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
  2. Jadili aina nne za taswira katika dondoo hili (alama 4)
  3. Bainisha vipengele vingine vinne vya kimtindo katika dondoo hili (alama 4)
  4. Bainisha toni ya dondoo hili. (alama 2)
  5. Fafanua umuhimu wa mandhari katika dondoo hili (alama 6)

SEHEMU C. TAMTHILIA
T. Arege: Bembea ya Maisha

Jibu swali la 4 au la 5
4."... wakati mwingine mwindaji huwa mwindwa. Hata kijijini wanaishi watu . Watu hao hawakumbwi na dhiki kiasi hiki. Ya nini kung'ang'ana kuyatafuta maisha kama kwamba hayapiti? Maisha ni mshumaa uso mkesha! Ukijiachia sana peupe hata upepo unaweza kuuzima kabla ya kulika hadi nchani.”
Maswali

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama. 4)
  2. Bainisha toni katika kauli hili (alama. 2)
  3. Eleza vipengele vinne vya kimtindo alivyotumia msemaji kufanikisha uwasilishaji wa ujumbe. (alama. 4)
  4. Eleza umuhimu wa msemaji katika kuendeleza ploti ya tamthilia hii. (alama 10)

au

5.

  1. Fafanua umuhimu wa mazungumzo kati ya Luka, Beni na Yona katika kujenga tamthilia ya “Bembea ya Maisha” (alama 10)
  2. "Bembea inapolika na kukatika haiwi mwisho wa michezo.Huungwa na mchezo kuanza tena." Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa kutolea mifano mwafaka tamthiliani. (alama. 10)

SEHEMU YA D
Hadithi Fupi – Mapambazuko Ya Machweo Na Hadithi Nyingine – Dw Lutomia
Jibu swali la 6 au la 7
Kifo cha Suluhu
6. Mume wangu, hebu zivute fikra zako miaka kumi na mitano iliyopita tulipoingia katika mkataba wa ndoa. Kwa nini unataka kujitia hamnazo kuhusu ahadi ulizozitoa? Umesahau namna tulivyohangaika, tukachekwa na watu, tukakosa hata marafiki na hatimaye tukabandikwa majina ya ajabu? Umesahau, mume wangu? Umesahau namna kazi yako ya kuuza makaa ilivyofika hatima ya ghafla baada ya serikali kupiga marufuku ukataji wa miti katika eneo la Dafrao? Naomba ukumbuke. Ninaamini huenda umesahau! Ama cheo chako cha ubunge ulichokipata kwa mbinu nizijuazo mimi kimekulevya na kukufanya uisahau familia yako?

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 5)
  2. Fafanua mbinu za kimtindo zilizotumika katika dondoo hili. (alama 6)
  3. Tambua toni iliyotumika katika dondoo hili. (alama 2)
  4. Fafanua umuhimu wa ujumbe alitoa mnenaji wa maneno haya. Tumia hoja nane. (alama 8)

au
7. “Wewe mke sampuli gani usiyetaka kumuunga mkono mmeo?”
Kwa kurejelea hadithi hii na nyingine zifuatazo, jadili changamoto anazopitia mnenewa pamoja na wahusika wa jinsia yake. (alama 20)
Ahadi ni deni.
Hadithi ya Nipe nafasi

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI
8. Soma kifungu hiki kisha ujibu maswali

Hapo zamani za kale, Nyani na Mamba walikuwa marafiki wa kufa kuzikana. Watoto wao walipendana na kufaana kama ndugu wa toka nitoke. Familia ya Mamba aliishi mtoni nayo ya Nyani aliishi katika msitu uliokuwa maili thelathini kutoka mtoni. Kila mara marafiki hawa walitembeleana na kusaidiana kwa hali na mali. Kwa vile Mamba alikuwa mvuvi msahuhuri, aliweza kumwauni Nyani na aila yake kwa samaki wa aina mbalimbali. Nyani naye alimpelekea Mamba matunda na nafaka kutoka shambani mwake.
Urafiki wao ulikita mizizi na kunawiri Zaidi wakati Mamba alipokuja kwa Nyani kumposea mwanawe binti. Ukwe uliutilia viungo uhusiano wa Nyani na Mamba wakawa wanagandana kama kupe na mkia wa Ng’ombe. Wakatenda mengi pamoja. Wakazungumza ya kupwa na ya kujaa. Hakuna hata mmoja wao aliyeutilia shaka uaminifu wa mwenzake. Wake zao nao walifuata kaida ya maji kufuata mkondo. Walikuwa masahibu wa chanda na pete.
Msimu mmoja wa mapukutiko ulishuhudia mabadiliko ya kudumu katika maisha ya Nyani na Mamba. Wakati huo, bahari ilichafuka si haba. Kazi ya Mamba ya uvuvi ikaanza kukabiliwa na majabali ya kila aina. Kila mara Mamba alipokwenda uvuvini, alirudi akichekelewa na nyavu zake. Hakuambulia chochote. Njaa ilianza kubisha hodi katika familia ya Mamba. Hali hii ilitishia kuutia ufa urafiki kati ya Mamba na Nyani. Mamba alivamiwa na pepo ambaye hata yeye alishindwa kumfahamu. Kila mara alipomwona. Nyani au watoto wake alitamani kumdakia na kumla mzima mzima. Kadiri aalivyojaribu kujiasa dhidi ya fikira hii mbovu ndivyo moyo wake ulivyoendelea kumshauri, “Una njaa bwana, familia yako itaangamia. Je huoni rafiki yako na familia yake wanaweza kuwa kitoweo? Utaendelea kula wishwa hadi lini? Mbona huyo Nyani ambaye anajiita rafiki yako sasa amekata guu humu? Mbona haji tena kukutazama? Hata karafuu alizokuwa akikuletea ameacha kuleta. “Mamba akaanza kumshuku rafiki yake na akasadiki kuwa Nyani alikuwa mla naye tu.
Usiku mmoja baada ya kula mate na kujilaza kitandani mwake akihesabu nyota, wazo lilimjia. Alikata shauri kumlaghai rafiki yake wa miaka mingi ilia pate kujiokoa yeye na familia yake kutoka katika kinamasi cha njaa. Asubuhi yake alikwenda kwa Nyani akiwa amejinamia kwa jitimai. Alisema, “Rafiki yangu, jana tulipoagana nilipata tanzia. Mjumbe kutoka kijijini aliniarifu kuwa baba yangu ni mgonjwa mahututi. Alisema kwamba baba ananitaka nyumbani upesi,” Habari hizi zilimtia Nyani majonzi makuu. Alimwahidi Mamba kwamba wangeandamana pamoja. Kwa vile Nyani hangeweza kutembea majini, ilibidi abebwe na Mamba. Alipatwa na kichefuchefu na manyezi kila alipotazama bahari iliyojitandaza mbele yao kwa mbwembwe. Hata hivyo, Mamba alimhakikishia kuwa wangefika salama. Naye kwa Imani iliyotokana na urafiki na mazoea ya miaka mingi, alitulia.
Safari ilikuwa ndefu na yenye machovu yaliyomfanya Nyani kulala mgongoni mwa Mamba. Walipofika kwenye vina vya maji, Mamba aliamua kumpasulia mbarika Nyani. “Rafiki yangu, nimekuwa nikidhani wewe ni rafiki wa dhati, kumbe uzuri wako wa mkakasi? Mimi na wanangu tumetafunwa na njaa kwa miezi kadha sasa huku maghala yako yakishiba na kutapika chakula. Hujadiriki hata siku moja kuja kujua kama nimepata hata senti moja ya kusagia mkunguni. Jana usiku nilipokuwa nikiwazia hali yangu, nilioteshwa katika ndoto kwamba kama ningepata moyo wako na kuula, basi hali ya uhitaji ingeniishia. Moyo wangu unaniuma sana kukufanyia tendo hili, hata hivyo lisilo budi hutendwa.”
Nyani alipigwa na butwaa nusura moyo wenyewe ujikabidhi kwa Mamba. Hata hivyo, akili yake nyepesi ilifanya kazi. Alimwambia Mamba,”Ndugu yangu, pole sana ikiwa umekuwa unadhani sikujali. Kwa kweli, hata ungeniomba moyo wangu siku hizo ningekupa tu. Unajua tena sisi Nyani, Tumbili na Kima tuna mioyo mingi. Hata hivyo, nasikitika kuwa Mungu alituambia kuwa daima mioyo yetu itakaa mitini. Basi ndugu mpenzi, badala ya kuendelea na safari hii, turudi pale mtini nikupe moyo wangu pamoja na mitatu ya wanangu kusudi uwalishe wanao na mkeo.”
Mamba akaingia mtegoni. Wakarudi hadi ufuoni. Kwa vile Mamba hakuweza kutoka majini, alibaki ufuoni akimngojea rafiki yake amletee mioyo.
Mamba alitunga macho yake kwenye ujia alioufuata Nyani akiomba pasitokee lolote la kumchelewesha Nyani. Matumbo yalimnguruma kwa njaa. Roho ikampapa kwa tumaini. Alingoja, akongoja, akangoja... wiki, mwezi, mwaka... Nyani hakurudi. Mamba akajua amepwaguliwa na Nyani. Akaapa kumtafuta kwa udi na ambari. Huo ukawa mwisho wa urafiki kati ya Nyani na Mamba. Hadithi yangu inaishia hapo.
Maswali

  1. Tambua kipera cha utungo huu. Thibitisha. (alama 2)
  2. Tambua mbinu sita kimtindo alizotumia mtambaji wa utungo huu. (alama 6)
  3. Umepewa jukumu la kutamba ngano hii. Fafanua mambo matano muhimu utakayozingatia ili kufanikisha uwasilishaji wako. (alama 5)
  4. Fafanua umuhimu wa ngano hii katika jamii. (alama 3)
  5. Kwa kutoa hoja nne jadili umuhimu wa maneno yaliyokolezwa rangi katika utambaji wa ngano kama hizi. (alama 4)


MWONGOZO

  1. Swali la lazima
    1. Tambua aina ya shairi hii kwa kutolea idhibati. (alama 2)
      Tarbia – mishororo minne katika kila ubeti
      Kutaja -1
      Kueleza-1
    2. Kwa hoja nne fafanua ujumbe wa mshairi. Taja sifa tano za mtu mwenye utu kulingana na shairi.(alama 5)
      • Mtu mwenye nidhamu
      • Mtu mwenye utu hana tabia ya kujivuna
      • Mtu mwenye utu husema ukweli.
      • Mtu mwenye utu hana ubinafsi
      • Mtu mwenye utu huwajulia wengine hali.
      • Mtu mwenye hushirikiana na wengine.
      • Mtu mwenye utu huwaheshimu wenzake.
      • Mtu mwenye utu huwajali wenzake
      • Mtu mwenye utu hupendeka
      • Mtu mwenye utu ni muungwana. (za kwanza 5x1 = 5)
    3. Tambua mbinu mbili za kimtindo zilizotumiwa na mshairi. (alama 2)
      • Tashbihi – ni kama yai na kuku
      • Takriri/urudiaji – mtu kuitwa mtu.
      • Uhuishi/tashihisi – utu kamwe haudai, utu huiona tabu.
      • Utohozi – filosofia – philosophy
        (za kwanza 2 x 1 = 2)
    4. Ainisha shairi hili kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo. (alama 3)
      • Vipande – mathinawi – migao miwili
      • Vina –ukaraguni – vina vinabadilika katika kila ubeti.
      • Mpangilio wa maneno – kikwamba – neno utu kuanzia katia baadhi mishororo (3x1=3)( akitaja bahari tu atuzwe)
    5. Tambua nafsi neni katika shairi. (alama 1)
      Mshauri – anashauri watu kuwa na utu.
      • Tambua mbinu tatu alizotumia mshairi ili kukidhi mahitaji ya kishairi.(alama 3)
    6. Tambua mbinu tatu alizotumia mshairi ili kukidhi mahitaji ya kiarudhi.
      • Inkisari – yani – yaani, tabu - taabu
      • Kuboronga sarufi – kwenye yake damu – kwenye damu yake, hiki kitu – kitu hiki
      • Msamiati wa kale – mja - mtu
      • Mazda – ubinaadamu – ubinadamu
      • utohozi – filosofia (zozote 3 x1 = 3)
    7. Andika ubeti wa saba kwa lugha nathari. (alama 4)
      • Utu wa kweli wa mtu ni kuwajali wenzake /na kuona haja ya kuwajulia watu hali/. Utu ni kushirikiana na wengine kwenye shida mbalimbali/. Utu wowote wa mtu ni kuwajali wenzake.
        ( asitumie koma, na aondoe uhuru wa mshauri wote, asitumie muundo wa beti) ( 4x 1)
  2.                  
    • Kutoroka - Naomi anawahini wanawe malezi anapomtoroka mumewe kwa kutaka kukimbia umaskini wanaishia kulelewa na kijakazi Sauna/ Subira/Mama yake Pete/ Rehema
    • Wanaendeleza ndoa za mapema - Mama ya Pete anashirikiana na wajomba wake kumwoza mapema licha ya rai ya bibi/nyanya yake kwamba wamwache aendelee na masomo.
    • Wanaendeleza ulanguzi wa binadamu - Sauna anawateka nyara Dick na Mwaliko na kuwatenganisha na Umu.
    • Wanaendeleza ubaguzi - Mavyaa ya Subira anambagua kwa kusema Subira ni msichana wa Bamwezi; anamwita mwizi na kumfanya Subira aondoke.
    • Wanachangia kuvunjika kwa ndoa.- Mavyaa ya Subira anamsimanga Subira hadi Subira anaondoka/Wazazi wake Rehema wanakataa aolowe na Fumba
    • Wanaendeleza mauaji - Subira,mkewe Kaizari anapatikana amejifia chumbani akiwa na chupa ya kinywaji kikali.Wanawe wanakosa malezi yake.
    • Kuwanyima waume zao ushirika wa watoto wao – Mkewe Kiriri anahamia ng’ambo na watoto.
    • Wazazi wake Zohali hawamsaidii binti yao baada ya kupachikwa mimba na kufukuzwa shuleni hawampi ushauri –nasaha wa kumsadia kuikabili hali yake mpya.
    • Amize Lucia wanawakandamiza watoto wa kike, kwa mfano,wanamkataza Kangata kumwelimisha mwanawe Lucia kwa sababu ya kuwa msichana
    • Wanasababisha dhiki za kisaikolojia - Mkewe Kiriri anamwachia Kiriri upweke na kuenda ughaibuni/ Naomi anamwacha Lunga na kusababisha kuugua kwake kisha anafariki/Kaizari.
    • Wanawanyima waume zao haki ya unyumba - Naomi anamwacha Lunga/Annette anamtoroka Kiriri.
    • Kuwanyamazisha wanao / kuwanyima haki ya kusema- k.m Mamake Sauna anamwambia Sauna asimpake Maya tope. Baadaye Sauna anatoroka kwao.
    • Baba Kairu anamtelekeza Kairu kwa kumwacha kulelewa katika maisha ya kimaskini kwa sababu mamake hakujiweza kiuchumi; hii ni kwa sababu alimzaa nje ya ndoa
    • Baba Zohali na mama Zohali wanamdhalilisha na kumsimanga Zohali na kumfanya kijakazi wao.Zohali anaishia kutoroka nyumbani.
    • Fumba anamtelekeza mwanawe Chandachema kwa mamake bila kumpa pesa za matunzo yake. Inawabidi dadaze Fumba kumtumia mama yao pesa za kumtunza Chandachema,
    • Fumba anaoa mke mwingine na kuhamia ughaibuni na kumwacha Chandachema akiteseka katika hali ya umaskini.
    • Babake Kipanga anamkana Kipanga kuwa mwanawe wa kuzaa, hali inayomchochea kutoroka nyumbani na kuanza kunywa pombe, hivyo kuishia kuacha shule.
    • Babake Pete anamkataa Pete kuwa mwanawe akidai kwamba hawafanani. Pete anaishia kulelewa na nyanyake.
    • Wazazi wa Pete wanamkatizia masomo kwa kumwoza kwa Mzee Fungo ili wapate mahari.
    • Mzee Maya anambaka mwanawe wa kambo Sauna na kumpachika mimba.
    • Wazazi wa Mwangemi na Mwangeka wanawahini mwangemi na Mwangeka chakula kama njia ya kuwaadhibu kwa kumuiga babu yao, badala yao ya kuwazungumzia ili kuwaonya dhidi ya kitendo hicho.
    • Mzee Fungo anamfurusha Pete na mwanawe bila kuwazia hatima ya mtoto huyo kwa maana Pete alikuwa angali kikembe katika malezi,
    • Wazazi wengine wanapalilia ukabila miongoni mwa wanao kwa mfano, Lucia anakatazwa na amize kuolewa katika ukoo wa Waombwe
    • Satua anamdhulumu Chandachema akielewa kuwa hana mlezi baada ya kifo cha nyanyake aliyekuwa mleziwe Chandachema anapohamia kwake, anaanza kulalamikia matumizi ya sukari na sabuni hiyo kumfanya Chandachema kumtoroka.
    • Tenge anafanya uasherati / uzinifu machoni pa wanawe, hivyo kuwaachia dhiki za kisaikolojia.
    • Pete anakunywa dawa ya kuulia panya ili afe bila kuwazia maisha ya wanawe wawili wakiwa hai.
    • Zohali anakiuka haki ya mwanawe Nasibu kwa kukataa kumjulisha kuwa ana babu na nyanya.
      (zozote 20 x 1=20)
  3.                    
    1.                          
      • Ni usimulizi wa Kaizari
      • Anawasimulia wakimbizi wenzake / Ridhaa.
      • Yumo kambini / Misitu wa Mamba.
      • Anarejelea hali ya ugeni kule kambini / anarejelea hali ya maumivu ambayo wanawe Lime na Mwanaheri wamo baada ya kubakwa / Hii ni baada ya uchanguzi kufurushwa kwao na kuishia kambini/anarejelea tandabelua ya baada ya uchaguzi. (4x1=4)
    2. Aina za taswira:
      • Taswira oni/ya uoni/mwono - naona wingu kubwa angani likitembea
      • Taswira mwendo - wingu kubwa likitembea
      • Taswira sikivu - sauti ya mawingu yakigooka
      • Taswira mguso - mawingu yanakaribiana, kupigana busu; wingu kulifunika jua; yanayoanguka kwenye ngozi laini za wanangu.
      • Taswira hisi - yakataka kutapika (za kwanza 4x1=4)
    3. Vipengele vya kimtindo;
      • Tashihisi/uhuishi - wingu kubwa angani likitembea kwa kedi na madaha / mawingu yakataka kutapika
      • Urudiaji/Takriri/uradidi- matone; siye;mke wangu/hamira
      • Mdokezo - ngozi Laini za wanangu wakembe.../maskini mke wangu...
      • Tashbihi - amevimba na kuvimbiana kama dongo la unga ngano
      • Nidaa - hana hamira!
      • Nahau/msemo – majeraha kikwi
      • kudumisha sauti – siye-e-e-e
        (za kwanza 4x1=4)
    4. Toni ya uchungu/masikitiko / huzuni (1x2=2)
    5. Umuhimu wa mandhari:
      1. Kuibua maudhui mbalimbali k.m maudhui ya ukatili - jinsi Lime na Mwanaheri walivyabakwa.
      2. Kuchimuza tabia za wahusika – k.m utu wa jiraniye Tulia; tabia za mwanzi kama katili kwani tunaambiwa Selume kuishi na wakimbizi kuliko kwenya kasri la dhuluma za mumewe.
      3. Kuonyesha wakati wa kutukia kwa matukio- tandabelua baada ya uchaguzi
      4. Huchangia kuibua toni na hali ya kijumla – mandhari haya yanaibua toni ya uchungu na masikitiko.
      5. Huibua dhamira ya mwandishi mandhari ya kambi ya wakimbizi yanaibua dhiki za wakimbizi baada ya ghasia za baada ya uchaguzi.
      6. Hutambulisha wahusika - tunabainishiwa wahusika kama Subira, Lime, Mwanaheri, Ridhaa, nk..
      7. Kudokeza migogoro - baina ya wafuasi wa Bi.Mwekevu na mpinzani wake mkuu.
      8. Husaidia kulinganua hali za matabaka- k.m. aliyekuwa waziri, familia ya Bw. Kute
      9. Kuonyesha mahali pa tukio – k.m Lime na Mwanaheri wanabakiwa nyumbani kwao
      10. Huibua taharuki - Kaizari akisimulia jinsi gari lao lilivyoishiwa na petroli taharuki inajengwa.
      11. Kuendeleza ploti – k.m Wakimbizi wanapofurushwa kutoka makwao na kuanza maisha upya katika kambi ya wakimbizi / Msitu wa Mamba.
        (zozote 6x1 = 6)
  4.                              
    1.                          
      • Msemaji ni Sara
      • Msemewa ni Asna
      • Walikuwa nyumbani kwa Asna/servant’s quarter.
      • Sara ana maoni kuwa Asna angehamia kijijini kumsaidia. (4x1=4)
    2. Toni ya kushauri (1x2=2)
    3. Vipengele vya kimtindo:
      • Methali-mwindaji huwa mwindwa
      • Swali ya balagha- ya nini kung’ang’ana kuyatafuta maisha kama kwamba hayapiti?
      • Nidaa- Maisha ni mshumaa uso mkesha!
      • Jazanda/ sitiari- Maisha ni mshumaa uso mkesha( maisha ni mafupi na hayapo daima)
      • Mdokezo - …wakati mwingine
      • Tashihisi / uhuishi - upepo unaweza kuuzima kabla kulika hadi nchani.
      • kweli kinzani – mwindaji – mwindwa
      • msemo/nahau - Maisha ni mshumaa uso mkesha! (za kwanza 4x1 = 4)
    4. Umuhimu wa Sara katika kujenga ploti
      • Sara ametumiwa kuonyesha athari ya migogoro katika ndoa. Maradhi ya moyo anayogangua ni tokeo la mzozano baina yake na mumewe Yona.
      • Kupitia kwake tunaona alivumilia ndoa yake na kufanya juu chini ili wanawe wapate elimu ili kuboresha mustakabali wao.
      • Aidha, anahakikisha kuwa binti zake Neema na Asna wanapata elimu.
      • Ni mfano wa wanawake wenye bidii. Hata akiwa hospitalini, akili yake inafikiria mazao yake aliyoyaacha shambani.
      • Kupitia mazungumzo baina yake na Asna, yanamsawiri Asna kama kijana aliyekengeuka kiasi cha kutotaka kuingia katika ndoa.
      • Kupitia kwake tunaelezwa kuhusu usuli wa kutopika. Sara anaeleza kuwa kwa sababu ya ugonjwa wake hangeweza kupika.
      • Sara alisemwa na kutukanwa na wanajamii kwa sababu ya kuwapata watoto wa kike pekee. Hii ilipelekea Yona kuingilia ulevi.
      • Baadhi ya matukio katika maisha ya wahusika fulani yanaangaziwa katika nyumba yake. k.m Dina anaangaziwa kama mwenye utu kwani anaenda kumpikia kwa kuwa alikuwa mgonjwa.
      • Kupitia mazungumzo baina yake na Yona, tunapata kujua kuwa Neema ndiye aliyewasomesha wanuna wake hadi chuo kikuu.
      • Pia, Sara anatujuza kuwa Neema ndiye aliyewaajiri wafanyakazi nyumbani kwake.
      • Ametumiwa kuonyesha uwajibikaji wa Neema. Neema anagharamia matibabu ya Sara na pia anampa babake/Yona pesa za kwenda kwa wazee wenzake.
      • Kupitia kwake tunafahamu kuwa Bunju ndiye aliyemsaidia Neema baada ya kupata ajali na kulipia gharama za hospitali ilhali Bunju hakuwa amemjua Neema.
      • Kupitia mazungumzo baina yake na Neema na Asna tunapata kujua kuhusu tofauti baina ya hospitali za mjini na kijijini. Huduma za hospitali mjini ni mzuri lakini za kijijini zinalinganishwa na seli na wahudumu hawana mlahaka mwema.
      • Hatima ya mgogoro baina ya Sara na Yona. Yona anaachana na mila na tamaduni za kutopika kwa Mwanaume.
      • Anaonyesha jinsi utamaduni ulivyowakandamiza wasichana –Sara anamwambia Asna kuwa siku zao elimu ya wasichana ilifanyiwa bezo na kuwa Sara aliachia darasa la saba.
      • Kuonyesha mustakabali wa Sara wa kumsamehe,Yona-Yona anamwomba Sara msamaha kwa kuwa hakujua upeo wa ugonjwa wa moyo. (zozote 10x1=10)
  5.                                    
    1.                        
      • Yanaonyesha sifa ya Luka kuwa ni mkarimu -anawakaribisha wenzake kwake nyumbani kwa chakula cha mchana na kinywaji..
      • Kuonyesha mila na utamaduni - Luka anadokeza kuwa kitendo cha kula pamoja kwa wazee kilikuwa kinafanywa na wazee wao kwani mavuno ya kwanza huonjwa na wazee na kutoa baraka. (uk. 58)
      • Yanachimuza ukengeushi - Beni anasema kuwa tatizo la watu siku hizi ni kuzitupa mila zao kabisa. (uk.58) Wajukuu wa Yona hawafahamu lugha yao ya asili. (uk-59)
      • Yanadhihirisha mchango wa dini - Yona anaeleza dini,imechangia watu kuona mila kuwa chafu. (uk.58)
      • Yanaonyesha mabadiliko katika malezi - Yona anaambia wazee wenzake kwa malezi kule mjini yameachiwa kina yaya. (uk.59)
      • Yanaonyesha jinsi mila na tamaduni zilikuwa kandamizi kwani hazikuruhusu mtoto wa kike kuenda shule au kuridhi kitu – kulingana na Luka.(u.k 60)
      • Yanadhihirisha jinsi hao kina Luka walivyomshinikiza Yona kuoa mke mwingine apate mtoto wa kiume.(u.k 60)
      • Yonadhihirisha sifa za Beni jinsi ana wivu kwa watoto wa Yona kwani hataki Luka awataje katika mazungumzo yake.
      • Yanachimuza ufanisi wa watoto wa Yona – Luka anasema walikuwa nyota ya jaha. Neema anarudi kijijini akiwa na gari.
      • Yonaonyesha thamani ya mtoto wa kike ilivyopanda na nafasi yake kupanuka kwani zamani walikuwa wakiwategemea waume zao laikini sasa hali ni tofauti(u.k.60)
      • Yonaonyesha maudhui ya uhafidhina – Luka anamuona Neema kama si wao tena baada ya kuolewa.
      • Yanachimuza hekima ya Luka – Luka anamuuliza Beni kuwa lipi muhimu kati ya tiba au mtu kuja kumpikia mwenzake? (uk.61)
      • Yanaonyesha sifa za Yona hapo awali kuwa alikuwa mualimu mwenye bidii - Yona anasema angefika kazini majira ya alfajiri, kiboko mkononi, siku nzima kazi tu, aliweza kufunga vitabu kwenye baskeli kwenda kuvisahihisha wikendi. (uk. 62)
      • Yanadhihirisha mabadiliko katika nyanja ya elimu - Yona anasema siku hizi huwezi tena kumnyoosha mtoto kwa kiboko. (uk.62)
      • Yanachimuza athari za pombe - jinsi pombe ilivyomfanyaYona kuwa mtumwa akashindwa kuishi bila kulewa (uk62)
      • Yanaonyesha uvumilivu au stahamala za Sara wakati Yona alipokuwa mlevi. Yona anasema Sara alimsaidia kulea na kusomesha watoto na kwamba bila yeye chombo kingezama. (uk-62)
      • Yanaonyesha jinsi Yona alivyoanza kutumia tembo alipokuwa chuoni. Wenzake walimpa mvinyo kumrai kuonja. (uk. 62)
      • Yanadhihirisha uongo wa Beni- kuwa mtoto wake ni fundi wa mitambo na wala si injinia. (uk. 63)
      • Yanaendeleza ploti- tunatambulishwa kuwa Luka,Beni na Yona ni marafiki na walishiriki vileo pamoja. (zozote 10x1=10)
    2.                  
      • Neema nusura apoteze uhai wake katika ajali Lakini Bunju akamnusuru kwa kumpeleka hospitalini.
      • Neema na Bunju baada ya kugombana kuhusu mchango wake Bunju katika matibabu ya Sara, Neema anaamua kumuelewa Bunju hivyo ndoa yao kuendelea vyema.
      • Baada ya changamoto ya kutopata watoto iliyoyumbisha ndoa baina ya Sara na Yona, hatimaye walijaliwa watoto watatu.
      • Maradhi ya moyo yalipomlemea Sara kiasi cha kukata tamaa na maisha, Neema anajitolea kuhakikisha mamaye amepata matibabu murua hivyo kumrejeshea matumaini.
      • Japo Yona na Sara walikosa mwana wa kiume na kusimangwa na wanajamii, mabinti zao wanakuwa wembe masomoni hivyo kuwapa furaha katika ndoa yao.
      • Neema alipoonekana kukata tamaa kutokana na kile alichokiona kuwa ni ubahili wa Bunju, Sara alimpa wasia uliompa nguvu zaidi katika ndoa yake.
      • Yona baada ya kugundua kuwa ulevi wake unaangamiza familia yake, anaapa kutolewa tena na kumhudumia mkewe Sara.
      • Yona na Beni walipotofautiana kuhusu watoto wao,Luka anafaulu kutuliza hali na wazee hawa kuendelea na sherehe zao.
      • Baada ya kumsababishia mkewe maradhi ya moyo,Yona anamwomba Sara msamaha kwa kuwa hakujua upeo wa ugonjwa wa moyo.
      • Mgogoro baina ya Sara na Neema kuhusu Yona unaisha Neema anapogundua upendo wa Yona Kwao anapoacha utamaduni wa kutopika chakula.
      • Mgogoro baina ya Sara na Yona unaisha. Yona anapoachana na mila na tamaduni za kutopika kwa mwanaume.
      • Tatizo la Sara la kushindwa kumpikia mkewe linasuluhishwa na jiraniye Dina anapokuja kumsaidia.
        (zozote 10 x 1=10)
  6.                        
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      • Maneno haya ni ya Bi. Suluhu kwa Bwana Suluhu katika Barua aliyoitoa Abigael mfukoni mwa Bwana Suluhu. Bwana suluhu na Abigael walikuwa wamekwenda kujistarehesha.
    2. Fafanua mbinu za kimtindo zilizotumika katika dondoo hili. (alama 6)
      • nahau/msemo – kujitia hamnazo
      • Balagha – umesahau mume wangu?
      • Takriri/urudiaji – neno umesahau limerudia.
      • Nidaa – naamini huenda umesahau!
      • Uhuishi/Tashihisi – cheo kimekulevya
      • Mbinu rejeshi – Bi Suluhu anakumbuka maisha yao ya awali – m.f tulivyohangaika.
      • Usambamba – tukachekwa tukakosa tukabandikwa
      • Majazi – Dafrao (zozote 6 x 1 = 1)
    3. Tambua toni iliyotumika katika dondoo hili.
      • Toni ya unyenyekevu – naomba ukumbuke.
      • Toni ya mshangao– Bi Suluhu anastaajabu vipi mumewe amesahau maisha yao ya awali. (yoyote 1x2=2)
      • Toni ya huzuni -
    4. Fafanua umuhimu wa ujumbe alitoa mnenaji wa maneno haya. Tumia hoja nane.(alama 8)
      • tunafahamu uhusiano wao – hapo awali Bw. Suluhu alimpenda Bi. Suluhu na kutoa ahadi nyingi kwake. Uhusiano huu umedhoofika sasa.
      • Tunafichuliwa maisha yao ya hapo awali. Walikuwa maskini aliuza makaa kupata riziki.
      • Bwana Suluhu ni Mbunge na alipata cheo chake kwa njia isiyo halali.
      • Tunafichuliwa kuwa Bw. Suluhu ndiye aliyemwangamiza mamake Abigael ili ajifaidi na shamba lake.
      • Tunafahamu kuwa Bw. Suluhu hafanyi maendeleo katika eneo bunge lake kwa sababu anafuja pesa za wananchi kwa kuwalipa wasichana wa vyuo vikuu baada ya kula uroda nao.
      • Tunaambiwa kuwa Bw. Suluhu ana deni la Bw. Ngoma aliyemkopesha pesa za kampeni hivyo akakosa kufanya maendeleo kwa kuwa anatafuta mbinu za kulipa deni hili.
      • Tunafahamishwa kuwa Bw. Suluhu ni mgonjwa. Watu wanazungumza kuhusu kuabiri gari moshi.
      • Bi. Suluhu anahofia Suluhu asimwambukize Abigael nakama
      • Tunafahamishwa kuwa Bw. Suluhu alikuwa mwema hapo awali kwani alisaidia mamake Bi. Suluhu na familia yake.
      • Bi .Suluhu pia anatufahamisha kwamba anaugua msongo wa mawazo uliosababishwa na vitendo vya mumewe vya kihayawani.
      • Kupitia kwa barua hii tunafahamu kuwa Bw. na Bi. Suluhu wana watoto wawili ambao wanaumia kwa sababu ya matendo ya Bw. Suluhu.
        (za kwanza 8 x 1 = 8)
  7.                        
    1. Fadhila za punda
      • Mwanamke kutawishwa, lilia anaachishwa kazi ya umeneja na mwishowe kutawishwa. Anaishia kukaa nyumbani na kutishwa asidhubutu kutoka nje ya lango.
      • Mwanamke anatishiwa – Lilia anapodhubutu kumshtaki mumewe anakumbushwa kuwa yeye ndiye Gavana na ana uwezo wa kufanya haki kuwa batili na batili kuwa haki.Utajua kichomtoa kanga manyoya.
      • Mwanamke anapokezwa vipigo. Lilia anapokea mapigo kutoka kwa mumewe anapoenda kuripoti kwa polisi.
      • Mwanamke kutusiwa: Lilia anaambiwa amenona kama nguruwe.
      • Mwanamke kudhalilishwa. Lilia annambiwa kuwa ana umbo kama nguruwe kwani kazi yake ni kula na kulala tu.
      • Mwanamke kuendewa kinyume na mumewe, katika ndoa, Luka anasemekana kuwa na kiruka njia ambaye waliandamana naye kila mahali. Lilia anapouliza ni nani anapokea kipigo kinachomlaza kitandani siku mbili.
      • Kuachishwa kazi. Lilia anaachishwa kazi na mumewe ili awe mpokezi wa wageni nyumbani.
    2. NIPE NAFASI
      • Wanawake kutosaidiwa katika malezi na waume zao. Mama Kazili hatumiwe pesa na mumewe yeye na watoto wake wanataabika kwa njaa.
      • Mwanamke kutosikilizwa. Wazazi wa mama Kazili wanadinda kusikiliza malalamishi yake kuwa mumewe ana mke mwingine migodini.
      • Kutopatiwa pesa za mahitaji – nyanyake msimulizi anakosa kumpa mamake pesa zinapotumwa na babake.
      • Kufiwa na jamaa zao. Mama Kazili anafiwa na mwanawe Mkhathini wakiwa katika safari yao kwenda Makongeni.
      • Wanawake kulaumiwa/kusingiziwa kusababisha kifo. Mama Kazili analaumiwa kusababusha kifo cha Mkhathini kwa sababu hakuomba ruhusa.
      • Wanawake kuuawa – mwanamke katika kijiji cha Habelo anatoroka na mwishowe maiti yake kufukuliwa na mbwa kondeni mwake. Hii ni baada ya kumuita mumewe mzembe.
      • Wanawake kudhalilishwa – wanawake wanaketi sakafuni nao wanaume wanaketi vitini.
      • Mwanamke kutopewa nafasi ya kujitetea. Mama Kazili ananyamazishwa na Matweba anapojitetea kwa wazee.
      • Kutengwa kwa misingi ya kitaifa. Mama Kazili anaambiwa lazima arudi kwao Swaziland.
      • Mwanamke kuchukuliwa kama mtoto anayetarajiwa kuwa chini ya uelekezaji na utunzi wa mwanamume katika jamii ya Belo.
      • Jamii na serikali imewanyima wanawake uhuru. Wanahitajika kuomba ruhusa kwa kila jambo wanalolihitaji kufanya.
    3. Ahadi ni deni
      • Kutoonana na jamaa zao kwa muda mrefu. Fadhumo anakaa kwa muda wa mihula mitatu bila kuonana na wazazi na jamaa zake.
      • Kufiwa na wazazi, Fadhumo anafiwa na babake katika ajali na mamake pia anafariki baadaye.
      • Kuacha masomo – Fadhumo anaacha masomo yake kwa sababu ya ukosefu wa karo. Anaachia kidato cha pili.
      • Kulazimishwa kuwa kimada. Jamaa ya babake Fadhumo anamwambia kuwa ikiwa anataka kusoma sharti awe kimanda wake.
      • Mwanamke kulazimishwa kuolewa akiwa mchanga Fadhumo anaolewa na Adan akiwa mchanga.
      • Mwanamke kutwikwa majukumu. Fadhumo anajukumika kuwalea na kuwasomesha nduguze ingawa ni mchanga.
      • Mwanamke kufanya kazi kunachukuliwa kama kuzurura. Adan anaulizwa na watu kwa nini mkewe anaenda kazini ilhali anafaa kukaa nyumbani na kutunza nyumba na watoto.
      • Mwanamke kutoruhusiwa kusoma; mjombake Adan anamwambia kuwa masomo yatamfanya mkewe kuwa jeuri.
      • Mwanamke kusingiziwa; mjombake Adan anamwambia Adan kuwa Fadhumo anaweza kutoroka na walimu wake au wanafunzi wenzake (zozote 20 x 1 = 20)
  8. FASIHI SIMULIZI
    1. Tambua kipera cha utungo huu. Thibitisha. (alama 2)
      • Ngano ya Usuli – inatueleza kwa nini urafiki wa nyani na mamba ulisambaratika.
    2. Tambua mbinu sita kimtindo alizotumia mtambaji wa utungo huu. (alama 6)
      • Nahau – kufa kuzikana/Pasulia mbarika
      • Tashibihi – kufaana kama ndugu wa toka nitoke /kama kupe na mkia wa ng’ombe
      • Methali – maji hufuata mkondo/ lisilobudi hutendwa
      • Uhuishi/tashihisi – kuchekelewa na nyavu/njaa kubisha hodi
      • Mdokezo wa methali – alikuwa mla nawe tu.
      • Uzuri wako wa mkakasi
      • Chuku – maghala yakishiba na kutapika
      • Takriri – alingoja... akangoja... akangoja
      • Mdokezo – alingoja .... mwaka...
      • Dayalojia – kati ya nyani na mamba
      • Balagha – mbona haji kukuona?
      • Uzungumzaji nafsia – una njaa bwana, familia yako itaangamia.
        (za kwanza 6 x 1 = 6)
    3. Umepewa jukumu la kutamba ngano hii. Fafanua mambo matano muhimu utakayozingatia ili kufanikisha uwasilishaji wako.(alama 5)
      • Nitahusisha hadhira ili kuundoa ukinaifu
      • Nitatumia uigizaji – matendo ili kusisitiza ujumbe
      • Kutumia viziada lugha – ishara za uso, mikono
      • Kutumia maleba yanayoafikiana na hadithi inayowasilishwa
      • Kubadilisha toni
      • kiimbo kulingana na ujumbe ninaopitisha
      • Kuwa mbaraza, kuingiliana vyema na hadhira yangu.
      • Kuelewa lugha ya hadhira
      • Kuwa mkakamavu/jasiri
      • Kuwa mfaraguzi – kubadilisha hadithi
      • kuwa mcheshi ili kuchangamsha hadhira yangu.
      • Kuelewa hadhira yangu na mahitaji yake
      • Kutumia sauti inayosikika
        (za kwanza 5 x 1 = 5)
    4. Fafanua umuhimu wa ngano hii katika jamii. (alama 3)
      • Hueleza chanzo cha hali Fulani m.f chanzo cha uadui kati ya mamba na nyani
      • Huadilisha – kukashifu tabia hasi kama usaliti
      • Huburudisha watu wanapotambiwa
      • Hukuza ubunifu
      • Huhifadhi na kendeleza utamaduni wa jamii
      • Hukuza ujasiri wa kuzungumza hadharani
      • Hukuza umoja/ushirikiano watu wnapojumuika pamoja kutambiana
      • Huendeleza historia ya jamii kwa kuvitamba kwa vizazi mbalimbali.
      • Huelimisha wanajamii kuwepo kwa funzo
      • Hutumiwa kupitisha muda.
        (zozote 3 x 1 = 3)
    5. Kwa kutoa hoja nne jadili umuhimu wa maneno yaliyokolezwa rangi katika utambaji wa ngano kama hizi.(alama 4)
      • Huashiria mwisho wa utambaji
      • Humpisha mtambaji anayefuata.
      • Huitoa hadhira kwenye ulimwengu wa fantasia hadi ulimwengu halisi.
      • Huwapumzisha/kutuliza hadhira – kwa kutoa suluhisho la mgogoro uliokuwepo katika hadithi.
      • Hutangaza adili na funzo la ngano.
      • Huwapa wasikilizaji changamoto ya kuwa watambaji bora.
      • Hupisha watu kwenye shughuli nyingine.
      • Hutia watu mshawasha wa kusikiliza hadithi nyingine pengine kupitia taharuki inayoibuliwa na fanani

 

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - MECS Pre Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?