Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Lainaku 1 Joint PreMock Exams 2023

Share via Whatsapp
Maagizo 
  • Jibu maswali yote 
  • Majibu yote ni lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  • Watahiniwa ni lazima wahakikishe kwamba kurasa zote za karatasi hii zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.
  1. UFAHAMU (alama 15)
    Swali la usawa wa kijinsia katika jamii ni jambo ambalo limeleta kero kwa wengi katika jamii kwani waja wengi huchukulia kuwa jinsia ya kiume ina uzito sana kuliko ya kike. Wanaume wengi bado wana mawazo yaliyopitwa na wakati. Wao hufikiri kuwa hata wakati Mungu alipomuumba mwanadamu, aliyeumbwa kwanza alikuwa mwanamme kabla ya mwanamke kuumbwa. Kwa sababu hii isiyokuwa na mashiko, wao hujipendelea na kumdharau mwanamke. Wanawake wengine pia wametingwa katika minyororo ya utamaduni kiasi cha kujiona wanyonge na watumwa wa wanaume.

    Katika jamii nyingi za kiafrika,mtoto mvulana alichukuliwa kuwa mrithi wa mali ya babake na pia mtu ambaye angesaidia kuendeleza jina la familia au ukoo aliotoka. Kwa sababu hii, ilikuwa ni lazima kwa mke kumpata mtoto mvulana. Wengi waliokuwa hawana bahati ya kuwazaa wavulana walitalikiwa au mume kumwoa mke wa pili. Inaaminika kuwa ni kwa sababu hii ndipo suala la ndoa ya wake wengi liliibuka. Mtoto wa kike alileta huzuni katika jamii kwani hakuchukuliwa kama mojawapo wa wanaukoo wowote na wakati wa kuolewa ukifika, basi aondoka.

    Kizazi kipya kinayapa mawazo haya ya kijadi kisogo. Ni yakini kwamba mtoto wa kike ameanza kuonekana kama kiumbe mwenye manufaa mengi. Siku hizi tunawaona wanawake wakiwa na nyadhifa muhimu sana katika jamii, kiasi cha kuwapiku wanaume. Katika shule nyingi na taasisi za juu nchini na ulimwenguni kote, wasichana wamebobea katika masomo na huibuka na alama za kuridhisha katika mitihani. Usawa wa kijinsia kwa hivyo yafaa uonekane katika sekta nyeti ulimwenguni kote.

    Hapo jadi, kazi ambayo mwanamke angefanya na iridhishe ilikuwa tu kazi ya ulezi, usafi wa kijamii pamoja na kumfurahisha mwanamume. Hata hivyo, wazo hili limebadilika kwani wanawake wengi wanafanya kazi tofauti tofauti ambazo hata zingine zilizodhaniwa za kiume. Katika mashirika mengi nchini, huwa tunakumbana na wake wakiwa wakurugenzi. Katika nyadhifa nyingi zinazochukuliwa na wanawake, huwa kuna uwajibikaji wa hali ya juu. Si vyema kutenga kazi kwani kujaribu ni kutenda, na kazi yoyote ile yaweza kufanywa na mtu yeyote.

    Elimu ndiyo uti wa mgongo wa fanaka maishani na ndio ufunguo wa maisha mema. Majukumu mengi wanayopewa watoto wa kike huwafanya wasihudhurie masomo. Jamii nyingi humpendekeza mtoto wa kiume asomeshwe kuliko wa kike.Wazazi wengi wamejipata wakiangamia kutokana na ugonjwa wa ukimwi, na majukumu ya kuchunga familia huachiwa mwana wa kike. Jambo hili huwafanya kutohudhuria masomo na kupata elimu. Inafaa ifanywe jambo la dharura kuwaelimisha wasichana na wavulana, kwani wote ni sawa na yafaa wajitegemee aushini. Ni jambo la kuridhisha kuwaona watoto wa kike pia wakifanikiwa kwa wingi katika masomo. Siku hizi, si nadra kumwona mtoto wa kike amewashinda wengine wa kiume katika masomo, na jambo hili linaonyesha kuwa jamii imezinduka.

    Katika taifa letu, imekuwa ikipiganiwa kuwa katika bunge, idadi ya wanaume itoshane na wanawake. Hii inaonyesha kuwa hata wanawake wana uwezo kisiasa, hata ingawa siasa inasawiriwa kuwa mchezo mchafu. Katika bunge la sasa kuna wanawake kadhaa, na hata wengine wamefanikiwa kupata nyadhifa za uwaziri. Hii inaonyesha kuwa tofauti na miaka ya nyuma,wanawake pia wamezinduka kisiasa. Hata katika nchi ya Liberia, kwa mara ya kwanza kihistoria, kiongozi mwanamke alipigiwa kura na kuwa rais wa nchi hiyo. Mwanamke huyo aliingia katika vitabu vya kihistoria kwa kuwa rais wa kwanza kabisa wa kike barani Afrika. Kwa hivyo ni bayana kuwa kisiasa wanawake wana uwezo katika uongozi.

    Sheria za kitamaduni za kitambo zilikuwa zinamlinda mtoto wa kiume hadi ukubwani. Waliounda sheria zenyewe walikuwa makundi ya wazee waliowapendelea waume kuliko wake. Hata hivyo sheria hizo zimeonyeshwa kisogo hivi sasa kwani sheria zilizoko sasa ni zinazowalinda waja wote pasi na kuzingatia jinsia. Sheria hizo huwa za kumkabili mkosa wala siye mume au mke. Katika katiba ya nchi ya Kenya, mwanamke amepewa nafasi kubwa na wajibu unaomfaa. Jambo hili linampa motisha sana na kumfanya mwanamke ahisi akiwa mmoja miongoni mwa wanajamii.

    Katika kiwango cha kifamilia, yafaa mume na mke washirikiane katika kila jambo. Katika majadiliano yafaa mwanamume amjumuishe mke ili kuwe na usawa katika maafikiano. Hali hii itaepusha migongano na kutoelewana nyumbani. Jamii nzuri yafaa iendeshwe na wazazi wote, na siyo mwanamume au mwanamke pekee.

    Kwa kuhitimisha basi, ni vyema kwa jamii kumchukulia mtoto wa kike kama kiumbe anayefaa heshima, elimu, uongozi, na kufanya maamuzi nyeti yanayoweza kuirekebisha jamii. Kasumba na mielekeo ya jadi imepitwa na wakati. Sheria yafaa ifuatwe ili kumlinda mtoto wa kike au mwanamke.

    MASWALI.
    1. Ni nini maana ya jinsia?                                                                                             (alama 2)
    2. Eleza asili ya mwanamume kumdharau mwanamke.                                                (alama 4)
    3. Toa ushahidi wa kuthibitisha kuwa mwanamke ana uwezo sawa na  mwanamume.  (alama 4)                                                       
    4. Taja mambo matatu yaliyodunisha mwanamke katika jamii.                             (alama 3)
    5. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa katika taarifa .           (alama 2)                                                           
      1. aushini
      2. inasawiriwa
  2. UFUPISHO                          (Alama 15)
    Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.
    Otieno ni profesa wa Kiswahili. Ilivyo ni kwamba aligundua siri ya mafanikio maishani miaka mingi iliyopita. Anaelewa fika kuwa ikiwa mtu anataka kufaulu maishani lazima ajue kuwa ana amali kubwa sana inayomsubiri. Kulingana naye, mtu hana budi kuikabili vilivyo kazi hiyo husika kwa kutumia mbinu mbalimbali ili kuimarisha aushi yake. Ukimuuliza atakueleza kuwa watu wengi ulimwenguni hustawi baada ya kupitia vizingiti vingi. Kila mtu ana wajibu wa kujitahidi kutenda mazuri kuliko anayoyaona. Kwa mujibu wa Otieno, hakuna mtu anayefaa kutosheka na yaliyotendwa na waliomtangulia. Ikiwa kila mwananchi atakuwa na moyo kama huo nchi yetu itaendelea na kuimarika kwa kasi ya ajabu. 

     Ili mtu aweze kupiga hatua maishani, anafaa kutenda mambo kadhaa. Itambidi awe na mlahaka mwema na watu wengine kwani kofi hazilii pasi na viganja viwili. Pia, ikiwa ni kijana au mtoto,itamlazimu awe na ushirikiano na wazazi wake ambao watamwelekeza vyema kitabia. Kwa upande wao, wazazi wanafaa kuwaelewa watoto wao na wawape radhi ambayo hukithiri mali.Pana haja ya watoto kujua wanachohitaji na wawe na shabaha maishani mwao. Wanafaa kujikaza kisabuni ili wapate wanachokitaka na wakatae kujihusisha na maovu kama vile wizi. Ikiwa ni wanafunzi, wanastahili kujikakamua masomoni bila kulazimishwa au hata kubembelezwa. Wanastahili kujua kuwa kulazimishwa na kubembelezwa watekeleze wajibu wao hakuna manufaa yoyote yale. Alipo Otieno, ukimuuliza kuhusu jukumu la watoto la kuhakikisha kuwa maisha ya kesho ni shwari, atakueleza kinagaubaga kuwa mtoto anahitajika kufanya bidii maishani ili kuboresha mustakabali wake; anafaa kujua kuwa asipojifunga kibwebwe kuuboresha mustakabali atapata madhara na atakuwa amechelewa kujaribu kuamsha fikira zake ili kuboresha maisha yake. Kila mtu hasa watoto hawafai kuridhika na kichache wapewacho na wazazi wao ama watu wengine. Hakuna mtu anayefaa kutegemea vitu vya kupewa hata kama ametoka katika jamaa ya wakwasi. Kama ametoka katika jamaa ya matajiri anafaa kujitahidi ili atajirike zaidi. Kwa upande mwingine, ikiwa familia yao ni ya walalahoi, hafai kufa moyo bali anastahili kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha yake; aelewe kuwa bidii huweza kumfanya awapiku wakwasi watajika.

    Watu wote, hasa vijana wanafaa kujua kuwa nidhamu ndicho chimbuko la mafanikio maishani. Hii ina maana kuwa, vijana wana jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wąna heshima ya kiwango cha juu. Kila mtu anastahili kujiamini na kuwapuuzilia mbali wanaojaribu kumvunja moyo. Hakuna mtu anayestahili kutamauka maishani licha ya hali ngumu inayomkabili; yafaa ieleleweke fika kuwa baada ya dhiki faraja. Ni dhahiri shahiri kuwa aghalabu fanaka hutokana na jitihada; bahati ni chudi. Kwa upande wao, wanafunzi hawana sababu yoyote ile ya kuwabeza walimu au wenzao, wajue kuwa mafanikio yao masomoni hutegemea washikadau hawa muhimu. Itawabidi vijana wakubali kukosolewa na kuomba msamaha wa makosa yao. Isitoshe, kila binadamu hafai kuthamini vitu vya anasa kama mavazi ya bei ghali ikiwa hana uwezo wa kuvipata. Wanafaa kuwa wavumilivu kwa kuwa subira huvuta heri na siku moja watapata kila watakacho kulingana na bidii yao. Kulingana na Profesa Otieno, penye nia pana njia na muhimu ni kutokufa moyo.
    Maswali
    1. Fupisha aya ya kwanza kwa maneno 40 .                                         (alama 5, mtiririko 1)
      Matayarisho 
      Jibu
    2. Bila kupotosha ujumbe uliokusudiwa na mwandishi, fupisha aya mbili za mwisho . ( maneno 95-100 ; alama 10, mtiririko 1)
      Matayarisho
      Jibu 
  3. MATUMIZI YA LUGHA                  (Alama 40)
    1. Taja sauti zilizo na sifa zifuatazo:                                                                           (Alama 2)                                                         
      1. Sauti ya wastani na nyuma ya ulimi
      2. Kikwamizo cha ufizi
      3. Hutamkiwa koromeo
      4. Hutamkwa ncha ya ulimi inapojipigapiga haraka kwenye ufizi
    2. Andika wingi wa sentensi :                                                                                    (Alama 2)                                                           
      Tajiri aliweka pesa zake kwenye sefu.
    3. Ainisha viambishi katika neno:                                                                                 (Alama 3)                                             
      AliyemlishA
    4. Andika sentensi moja katika wakati uliopita hali timilifu.                                     (Alama 2)
    5. Jaza mapengo kwa vihisishi mwafaka                                                                       (Alama 2)
      1. …………..……… hivyo ni sawa.
      2. ………………… mlango u wazi.
    6. Tambulisha aina ya vitenzi vilivyotumika katika sentensi hizi.                                (Alama 2)
      1. Kazi hii ni nzuri.
      2. Gari letu lilikuwa linataka kuuzwa.
    7. Andika katika udogo, hali ya wingi.                                                                          (Alama 2)
      Mvulana huyu mdogo ameangushwa na kigari kile.
    8. Dhihirisha matumizi ya na:                                                                                      (Alama 2)
      Kem alitaka kuwa na pesa za kubadilishana nao.
    9. Tofautisha matumizi ya po ya wakati katika sentensi hizi.                                         (Alama 2)   
      1. Alipomwona alimhoji.
      2. Amwonapo humhoji.
    10. Bainisha matumizi ya kiambishi ku.                                                                           (Alama 2)
      Amani atakutengenezea mpini wa jembe kisha aelekee kule kwao.
    11. Tumia vihusishi kudhihirisha hali zifuatazo:                                                       (Alama2)
      1. kiwango
      2. wakati
    12. Ainisha virai katika sentensi:                                                                                    (Alama 2)
      Wiki ijayo watavuna mahindi.
    13. Tumia vitenzi vya silabi moja kutunga sentensi katika kauli zilizoandikwa:      (Alama 2)                               
      1. wa (kauli ya kutendwa)
      2. nya (kauli ya kutendea)
    14. Ainisha yambwa katika sentensi:                                                                            (Alama 3)
      Watoto walimjengea mama yao nyumba kwa  matofali.
    15. Eleza maana mbili zinazopatikana katika sentensi:                                                 (Alama 2)
      Mwalimu alimwambia mwanafunzi kuwa hawataenda nyumbani.
    16. Changanua sentensi ifuatayo kwa matawi:                                                               (Alama 4)
      Yohana ameingia ndani ya chumba hicho.
    17. Eleza matumizi yoyote mawili ya alama ya mkato katika sarufi ya Kiswahili.       (Alama 2)
    18. Tumia visawe vya maneno yaliyopigiwa mstari kuandika tena sentensi ifuatayo.   (Alama 1)
      Shamba hili limelimwa na msichana aliyepewa zawadi jana.
    19. Andika methali moja inayotokana na maelezo yafuatayo:                               (Alama 1)
      Tabia ya kuchelewachelewa kutenda mambo humletea mtu umaskini kwani  yeye hukosa nafasi zote muhimu.                         
  4. ISIMU JAMII
    1. Eleza kwa ufupi jinsi mambo yafuatayo yanavyodhibiti mitindo ya lugha:
      1. mada                                     (Alama 2)
      2. hali ya mtu.                 (Alama 3)
    2. Fafanua sifa zozote tano za sajili ya shuleni.                                                            (Alama 5)

                                                                   MWONGOZO WA KUSAHIHISHA 

  1. Ufahamu
    1. Neno linalotumiwa kurejelea maumbile ya binadamu katika misingi ya  uana-uke au uana-ume.                  (1x2)                     
    2.  
      1. Mungu alimuumba mume kwanza ndipo akamuumba mke.
      2. Mtoto wa kiume alichukuliwa kama mrithi wa mali ya jamii.
      3. Mtoto wa kiume alionekana kama nguzo ya kuendeleza jina la familia au ukoo.
      4. Wanawake wenyewe kujiona wanyonge                                                              (4x1)
    3.  
      1. Wanawake wengi wameweza kufuzu katika masomo yao.
      2. Wanawake wana kazi na nyadhifa kubwa zinazohitaji uwajibikaji mkubwa.
      3. Wanawake wamejiingiza na kufuzu katika siasa.
      4. Wanawake wamenyakua uongozi wa sehemu kadha barani Afrika.                  (4x1)
    4.  
      1. Alionekana kama kiumbe cha kumfurahisha mwanamume
      2. Mlezi wa watoto
      3. Mtu wa kudumisha usafi wa nyumba
      4. Kuwahudumia wazazi walioambukizwa ugonjwa                                               (3x1)
    5.  
      1. maishani                                                                                                                  (1x1)
      2. inachorwa na kuangaziwa au kuchunguzwa kwa undani                                        (1x1)
        Kuadhibu  
        1.  sarufi (s) : Ondoa nusu alama kwa kila kosa litokeapo kwenye kijisemu mahususi mradi tu pana alama nzima,
        2. hijai (h): Ondoa nusu alama hadi upeo wa alama tatu kwa kila kosa litokeapo kwa mara ya kwanza.
  2. UFUPISHO
    1. Aya ya kwanza
      1. Otieno ni Profesa wa Kiswahili/ aligundua siri ya mafanikio miaka mingi iliyopita.
      2. Ikiwa mtu anataka kufaulu maishani, lazima ajue kuwa kuna amali kubwa inayomsubiri na   ni sharti akabiliane nayo kwa kutumia mbinu mbalimbali.
      3. Watu wengi hustawi baada ya kupitia vizingiti vingi.
      4. Kila mtu anafaa kujitahidi kutenda mema zaidi kuliko watangulizi wake.
      5. Moyo wa kujitahidi utaiwezesha nchi kupiga hatua za kimaendeleo kwa kasi.          (4x1)
    2. Aya mbili za mwisho 
      1. Kuendelea maishani kwamhitaji mtu kufanya mambo kadhaa.
      2. Awe na mlahaka mwema na watu wengine.
      3. Vijana na watoto watalazimika kushirikiana na wazazi wao watakaowaelekeza kitabia.
      4. Wazazi waelewane na wanao na wawape radhi.
      5. Watoto wajue wanachohitaji na wawe na shabaha maishani.
      6. Wawajibike kwa kujitahidi ili waepuke maovu na kuboresha mustakabali wao.
      7. Watu wote wasiridhike na wapewacho na wazazi wao au watu wengine.
      8. Ambao jamaa zao ni maskini au matajiri wajitahidi kuboresha hali zao.
      9. Watu wote wanafaa kuwa na nidhamu; kiini cha mafanikio.
      10. Kila mtu anafaa kujiamini na kupuuzilia mbali wanaojaribu kumvunja moyo.
      11. Wanafunzi hawafai kuwabeza walimu  na wenzao madhali mafanikio yao huwategemea.
      12. Vijana wakubali kukosolewa na kuomba msamaha.
      13. Hakuna anayefaa kuthamini anasa.
      14. Muhimu ni kutokufa moyo.                                                                                     (9x1)
                                                         M
                                                        (a) 4
                                                        (b) 9
                                                        (ut) 2 
                                                            15 
        Maelezo
        • Zingatia  idadi  ya maneno  yaliyotolewa  katika  swali.
        • Jibu  liandikwe  kwa  lugha  nathari.
        • Makosa  ya  sarufi  na hijai yaadhibiwe hadi upeo wa makosa 6 (Alama 3) kwa kila mojawapo.
  3. Matumizi ya lugha
      1. /o/
      2. /z/
      3. /h/
      4. /r/                                                     (4 x )
    1. Matajiri waliweka pesa zao kwenye masefu.                                                        (   2/0)
    2.  
      • A/a – nafsi/ nafsi(iii)/ nafsi ya (iii) umoja/ kiima/ mtenda/yeye
      • li - wakati/wakati uliopita
      • ye - kirejeshi
      • m – mtendwa/mtendewa/yambwa
      • ish – kauli
      • a – kiishio/ kimalizio     (3 x 1)
                                                         AU
                       Viambishi awali (a,li,ye,m) viambishi tamati (ish,a)
    3. Maisha yalikuwa yamemwendea vyema.                                                                   (2/0)                                                           
    4.  
      1. Naam!
      2. Karibu!                                                                                                                       (2x1)
                   Tan:  Alama ya hisi lazima iwepo.                                                                           
    5.  
      1. Kitenzi kishirikishi kipungufu/ kitenzi kishirikishi 
      2.  
        • lilikuwa – kitenzi kisaidizi
        • linataka – kitenzi kisaidizi
        • kuuzwa – kitenzi kikuu                                                                                         ( 4 x ½)
    6. Vivulana hivi vidogo vimeangushwa na vigari vile.                                                 ( 2/0)
    7.  
      • na – kihusishi
      • nao – kuunda kirejeshi                 (2 x 1)
    8.  
      1. po – wakati maalumu/wakati unaodhihirika
      2. po – wakati wowote / mara kwa mara/ mazoea                                                      (2x1)                                                           
    9.  
      • ku – nafsi / nafsi ii/ wewe/mtendwa/kitondo/yambwa tendewa
      • ku – mahali kusikodhihirika / kiambishi cha ngeli ya mahali/ kiashiria cha mahali                     (  2 x 1)
    10.  
      1. Viwango   
        • Misri ni mbali kuliko Congo
        • Kaunti zina pesa nyingi zaidi ya kata.
      2. Vya wakati
        • Nitakutumia pesa kabla/ baada ya jua kutua.                                         (2 x 1)
    11.  
      • Wiki ijayo – kirai kielezi
      • watavuna mahindi – kirai kitenzi                       (  2 x 1)
    12.  
      1. Mtoto aliwiwa radhi kwa makosa yale.
      2. Ndege alimnyea / alimnyia msafiri yule.                                                             (  2 x 1)
    13.  
      1. nyumba – kipozi
      2. mama yao - kitondo
      3. matofali – ala                                                                                                         (3 x 1)
    14.  
      1. Walimu hawataenda nyumbani.
      2. Wanafunzi hawataenda nyumbani.                                                                 
      3. Mwalimu na mwanafunzi wake                                                                                 (2x1)
    15.  
                                                      KiswahilimocksQ1   
                                                                                                                                                                              (8x1/2)
    16.  
      1. Hutumiwa kutenganisha maneno, virai na vishazi vilivyo katika mfululizo. Mfano: chungwa, ndizi ,limau na embe ni aina za matunda.
      2. Hutumiwa baada ya kihisishi. Mfano: Pole, sikukusaidia kukuumiza hivyo.
      3. Hutumiwa kutenganisha vishazi huru katika sentensi ambatano. Mfano; Dawa hizi ni       nzuri, na hutibu magonjwa mengi.                                                                                   (2 x 1)
    17.  
      1. shamba – konde,mgunda
      2. zawadi- hidaya, tunu, takrima, tuzo          (2x1/2)                                                                                                     
    18. Ajizi nyumba ya njaa/Ajizi ajizi nyumba njaa                (1 x 1)
      Kuadhibu
      • Hijai  (h): Ondoa  nusu  alama kwa  kila  kosa   litokeapo mara  ya  kwanza  kufikia upeo  wa alama  tatu (makosa 6)
      • Sarufi (s): ondoa  nusu alama kwa kila  kosa  litokeapo   mara ya  ya kwanza  mradi  pana alama  kamili katika  kijisehemu  husika.
  4. ISIMU JAMII
    1.  
      1. mada                                                                             
        • Mazungumzo yoyote yale  hudhibitiwa na mada mahususi.
        • Mada ngumu humlazimisha mzungumzaji kutumia lugha nyepesi/ aweza akabadilisha msimbo ili hadhira yake ielewe.
        • Mada nyingine kama vile za fedha hutumia istilahi mahususi.                                 (2x1)
      2. hali ya mtu                                                                              
        • Mtu mchovu hushindwa kujieleza/ ambaye hajachoka hujieleza kwa ukakamavu.
        • Mgonjwa huenda  akaongea kwa kigugumizi.
        • Aliye na furaha /huzuni kupita kiasi hushindwa kujieleza.
        • Aliye na hamaki huongea kwa mdokezo/ huboboka / hubwaga maneno .                  (3x 1)
    2. Sifa za sajili ya shuleni .
      1. Matumizi ya msamiati maalumu wa kiusomi / kielimu, mfano: vitabu ,maktaba, utafiti, mwalimu, mwanafunzi.
      2. Matumizi ya lugha rasmi hudumishwa katika muktadha rasmi kama vile: katika mazungumzo baina ya mwalimu mkuu na walimu wengine.
      3. Ufunzaji huendeshwa kwa lugha sanifu.
      4. Lugha ya adabu hudumishwa kutegemea wanaoshiriki katika mazungumzo, mathalani, mwalimu hatarajiwi kutumia lugha yenye mzaha anapozungumza na wanafunzi wake.
      5. Ubadilishaji zamu: mwalimu ndiye huelekeza kipindi.
      6. Lugha ya kuhoji; hutumika pale mwanafunzi anapomuuliza mwalimu maswali. Pia, wakati mwalimu anataka taarifa fulani kuhusu mwanafunzi.
      7. Lugha ya kushauri na kuelekeza. Kwa mfano: mwalimu anaweza kutumia lugha ya nasaha kumshauri mwanafunzi kutia bidii.
      8. Lugha isiyohukumu. Hata pale mwanafunzi amekosa mwalimu humwelekeza zaidi badala ya kumhukumu na kumfanya ajihisi mhalifu.
      9. Lugha yenye toni kali; mwalimu anapoonya kuhusu tendo hasi, anaweza kutumia toni kali kumfanya mwanafunzi kuliepuka.                                                                                     (5 x 1)            ( Kutaja ½   mfano/kueleza ½ )
        Kuadhibu
        • S :  Adhibu  kosa  litokeapo kwa  mara ya  kwanza  hadi  upeo  wa alama 2 (makosa 4)
        • H:  Ondoa  nusu maki  kwa makosa  yatokeapo  kwa mara  ya kwanza  hadi upeo  wa alama 2(makosa 4)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Lainaku 1 Joint PreMock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?