Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Form 4 Term 2 Opener Exams 2022

Share via Whatsapp

MAAGIZO KWA MTAHINIWA

  • Jibu maswali manne pekee
  • Swali la kwanza ni la lazima
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani: Tamthilia, Hadithi fupi, Riwaya na fasihi simulizi.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.

Kwa Matumizi Ya Mtahini Pekee.

SWALI

1

2

3

4

5

6

7

8

JUMLA

ALAMA

 

 

 

 

 

 

 

 

 



MASWALI

SEHEMU YA A: USHAIRI

  1. Lazima
    Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali
    Kiapo kwao majaji, wanosimamia haki
    Kwa sharia ni magwiji, wahalifu hawatoki,
    Wengi wao ni walaji, kwa rushwa ni mashabiki,
    Kwa rushwa mashabiki.

    Kiapo kwa daktari, wagonjwa hawadhiliki,
    Kazi zao ni dhariri, maradhi hayakwepeki,
    Na wengine ni hatari, bila pesa hutibiki,
    Bila pesa hutibiki.

    Kiapo cha mawaziri, kwa mbwembwe na itifaki,
    Na suti zao nzuri, shingo tai haitoki,
    Na wengi wana dosari, ni kwa mikataba feki,
    Ni kwa mikataba feki.

    Kiapo cha magavana, mikoa kuimiliki,
    Hujifanya ni mabwana, wala hawasogeleki,
    Nayo nchi huitafuna, na kuwa haikaliki
    Na kuwa haikaliki

    Kiapo cha maraisi, kwa mizinga na fataki,
    Na wageni mahususi, hualikwa kushiriki,
    Ikulu wakijilisi, kwa wizi hawashikiki
    Kwa wizi hawashikiki.

    Viapo vya utiifu, kwa sasa havistahiki
    Wanoapa ni wachafu, tena hawaaminiki,
    Biblia misahafu, washikapo unafiki
    Washikapo unafiki

    Maswali

    1. ’Dhamira ya shairi hili ni kushtumu ukiukaji wa maadili ya kikazi.’’ Jadili. (alama 3)
    2. Eleza namna vipengele vifuatavyo vya kimtindo vilivyotumika katika shairi hili.
      1. Usambamba ( alama 2)
      2. Aina za taswira ( alama 3)
    3. Bainisha toni katika shairi hili. (alama 2)
    4. Fafanua mbinu mbili alizotumia mshairi kutosheleza mahitaji ya kiarudhi katika shairi hili. (alama 4)
    5. Ainisha shairi hili kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo; ( alama 3)
      1. Mpangilio wa vina
      2. Mizani
      3. Mpangilio wa maneno
    6. Fafanua muundo wa shairi hili. (alama 3)

SEHEMU B: RIWAYA YA CHOZI LA HERI ( Assumpta K. Matei)
(Jibu Swali 2 Au 3)

2.

  1. “Sasa anakumbuka vyema. Anakumbuka kupepesa kwa jicho lake la kulia kwa muda wa wiki mbili mtawalia. Anakumbuka anguko ambalo alianguka sebuleni…Anakumbuka mavune yaliyowandama mwili wake na kuunyong`onyeza kwa muda hata pasi na kuudhili kwa kazi yoyote ya haja. Anakumbuka jeshi la kunguru lililotua juu ya paa la maktaba yake… Anakumbuka mlio wa kereng`ende na bundi usiku wa kuamkia siku hii ya kiyama… milio hii ni kama mbiu ya mgambo, huenda kukawa na jambo.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hli. Alama 4
    2. Jadili aina tatu za taswira katika dondoo hili. Alama 3
    3. Bainisha vipengele vingine vitatu vya kimtindo. Alama 3
  2. Kwa kutolea mifano, eleza maudhui kumi yanayopatikana kwenye wimbo wa Shamsi. Alama 10.

3. “ Mama mtu alikuwa ameamua kwamba hapa hapamweki tena. Alikuwa amehudumu katika afisi za umma kama mhazili mwandamizi kwa miaka mingi mpaka kazi hii akaiona inamfanya kusinyaa, hana hamu tena.”

  1. Eleza umuhimu wa mrejerewa katika kukuza riwaya ya Chozi la Heri. Alama 4
  2. Huku ukitoa mifano jadili changamoto zinazokumba asasi ya ndoa kwa mujibu wa riwaya hii. Alama 8
  3. Jadili umuhimu wa mandhari katika kuijenga riwaya hii kwa kurejelea; Alama 8
    1. Shule ya Tangamano
    2. Hoteli ya majaliwa.

SEHEMU YA C: TAMTHILIA YA KIGOGO (Pauline Kea)
(Jibu Swali 4 Au 5)

4. “Huu moyo wangu wa huruma nao…”

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (Alama 4)
  2. Fafanua sifa na umuhimu wa msemaji. (Alama 4)
  3. Onyesha kinyume kinachojitokeza katika dondoo hili. ( Alama 12)

5. Eleza jinsi maudhui yafuatayo yanavyojitokeza katika Tamthilia ya Kigogo

  1. Utabaka (alama 5)
  2. Usaliti (alama 5)
  3. Umaskini ( alama 5)
  4. Dhuluma ( alama 5)

SEHEMU YA D: TUMBO LISILOSHIBA NA HADITHI NYINGINE (Wahariri Dumu Kayanda na Alifa Chokocho)
(Jibu swali 6 au 7)

6. “Wako wapi? Wamepuuzwa tu kulee!Futari kwa niaba.Sikukuu kwa niaba.Harusi kwa niaba.”

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili (alama4)
  2. Tambua mbinu za kimtindo katika dondoo hili (alama 3)
  3. Fafanua sifa za mnenaji ( alama3)
  4. Jadili maudhui yanayojitokeza katika dondoo kwa kurejelea hadithi nzima (alama5)
  5. Kwa kutoa hoja tano jadili ufaafu wa anwani ya hadithi husika. ( alama5)

7.

  1. Eleza jinsi maudhui ya umaskini yanavyojitokeza katika hadithi ya Mapenzi ya Kifaurongo. (alama 4)
  2. Onyesha jinsi unafiki unavyojitokeza katika hadithi, “Shogake Dada ana Ndevu” (alama 4)
  3. Changanua mtindo katika dondoo lifuatalo. (alama 6)
    “Bi. Hamida alitunga donge kifuani mwake. Na donge likaja juu. Likampanda na kumsakama kooni. Kweli? Uongo? Kweli au uongo yale maneno ya binti yake? Labda kweli anamfikiria mambo mabaya binti yake tu. Labda kweli, dhana yake ni mbovu. Bi. Haminda alichanganyikiwa na mambo. Alivutwa huku na huku na nafsi yake yenye chagizo. Upande mmoja sauti yake ya ndani ilikuwa inamtetea Safia, na upande wa pili wa nafsi yake ilikuwa ikimshuku Safia; na sauti zake zote mbili hizo zimo ndani ya kiwiliwili chake zinamvuta yeye mtu mmoja, Bi. Hamida. Hatimaye hakutambua afanye nini.
  4. Hadithi “Tumbo Lisiloshiba imejengwa kijazanda. Thibitisha. (Alama 6)

SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI
8. Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
Ndimi Chesirwo, kijana barubaru,
Ndume na gwiji, la ukoo mtukufu,
Najivunia umahiri, kusakata kandanda.

Tazama umbo langu, guu mithili ya jokovu,
Kifua cha miraba, weusi wa kijungu,
Wenzangu wanienzi, na hata kuduwaa.

Misuli ni tinginya,
Kijijini nasifika,
Wazee kunienzi,
Mabinti kunikabidhi.
Maswali

  1. Tambua utungo huu na uthibitishe jibu lako. (alama 2)
  2. Kwa kurejelea hoja zozote nane, jadili sifa za utungo uliotambua katika (a) (alama 8)
  3.                    
    1. Eleza maana ya maghani. (alama 1)
    2. Taja na ueleze tofauti za aina mbili za maghani. (alama 4)
  4. Eleza jinsi jamii ya kisasa inavyojaribu kuendeleza fasihi simulizi. (alama 5)


MWONGOZO

SEHEMU YA A: USHAIRI
SWALI LA 1(LAZIMA)

  1.                              
    1. ukiukaji wa maadili ya kikazi
      • majaji wanaostahili kutetea haki ni walaji rushwa
      • madaktari hawawajibiki kwa matibabu na kuwa magonjwa hayatibiki
      • madaktari wanakwenda kinyume na kiapo chao kwa kuweka pesa mbele.
      • Licha ya mbwembwe nyingi za kiapo cha mawaziri, wana mikataba ghushi.
      • Magavana wanatafuna nchi na kuwa haikaliki.
      • Viongozi ni wanafiki hawaaminiki.
      • Maraisi wanashabikia wizi.
      • Waapaji ni wanafiki
        Zozote 3
    2. mbinu za kimtindo
      1.  usambamba
        • Kila ubeti unaanza kwa neno kiapo
        • Sehemu ya utao ya mshororo wa tatu katika kila ubeti inarudiwa katika kimalizio
          Alama 2
      2. aina za Taswira
        • Taswira oni- kiapo cha mawaziri, shingo tai haitoki
        • Taswira sikivu- kwa mizinga na fataki
        • Taswira mwonjo- wengi wao ni walaji
          Alama 3
    3. toni katika shairi
      • Kulalamika- kuna ukosefu wa uwajibikaji kazini
      • Kushtumu/ kusuta- majaji wanaostahili kutetea haki ni walaji rushwa
        1*2= 2
    4. idhini/ uhuru wa mshairi
      • Utohozi- feki
      • Tabdila- dakitari
      • Kuboronga sarufi- shingo tai haitoki
      • Inkisari- wanosimama- wanaosimama
        Alama 4
    5. Aina ya shairi
      • Mpangilio wa vina- ukara- vina vya nje vinatiririka ilhali vya ndani vinabadilika badilika
      • Mizani- msuko- kimalizio kimefupishwa
      • Mpangilio wa maneno- kikwamba- neno kiapo limetumika kuanzia mwanzo wa kila ubeti.
      • Pindu- sehemu ya utao ya mshororo wa tatu katika kila ubeti inarudiwa katika kimalizio
        Alama 3
    6.                    
      1. shairi hili lina beti tano
      2. kila ubeti una mishororo mine
      3. lina pande mbili; ukwapi na utao
      4. kituo kimefupishwa
      5. vina vya nje vinatiririka ilhali vya ndani havitiririki
      6. mizani 8, 8 kwa kila mshororo ila kwa kituo n inane.
        Zozote 3

SEHEMU B : RIWAYA YA CHOZI LA HERI (ASSUMPTA K. MATEI)
SWALI LA 2

  1.                      
    1. – maelezo ya mwandishi/ msimulizi
      • Anamrejelea Ridhaa
      • Ridhaa yuko nyumbani kwake/ganjo/gofu lake
      • Anapokumbuka yaliyompta kabla ya kuchomewa nyumba yake
    2. – Taswira mnuso – mavune yaliandama mwili wake
      • Taswira hisi – anguko ambalo alianguka sebuleni
      • Taswira sikivu – mlio wa kereng`ende na bundi
      • Taswira mwendo – jeshi la .ku8nguru kutua juu ya paa
    3.                        
      • Takriri/uradidi – anakumbuka
      • Methali – mbiu ya mgambo ikili a huenda kuna jambo.
      • Tashhisi – mavune yaliuandama mwili wake
  2. Maudhui kwenye wimbo wa Shamsi
    • Kupitia kwa Shamsi maudhui ya umaskini yanakuzwa – umaskini uliwatuma kuwa vibarua.
    • Shamsi anakuza maudhui ya elimu anasema alisoma kwa bidii na kuhitimu elimu ya chuo kikuu
    • Shamsi anawakilisha vijana wanotamauka baada ya kusoma na kukosa ajira. Anajitosa katika unywaji wa pombe haramu
    • Shamsi anakuza maudhui ya utabaka anasema kuna matajiri wanaomtazama wakiwa roshani
    • Kupitia kwake tunapata kuona dhiki wanazopatia wafanyakazi m.f mishahara duni. Kutopandishwa vyeo na kufutwa kazi
    • Anaonyesha athari za uongozi mbaya ukosefu was chakula dawa n.k
    • Anakuza maudhui ya ufisadi licha ya wao kusoma nafasi za kazi zilitwaliwa na ndugu za wenye vyeo “ viganja huoshana aso mwana aeleke jiwe! Hati miliki babdea
    • Anakuza maudhui ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana “Kwani hawakunikabidhi kazi walizoahidi kwenye mabuku?

SWALI LA 3

  1. Umuhimu Wa Mrejelewa ; ( Annete- Mkewe Kiriri)
    • Kielelezo cha malezi mabaya
    • Anaonyesha ubinafsi
    • Usaliti – anapomwacha mumewe
    • Kuonyesha mgogoro katika ndoa
    • Ukengeushi
    • Uhusiano uliopo baina ya wazazi nas wanao
    • Madhara ya kuvunjika kwa ndoa
    • Sifa/ tabia za Kiriri
  2. changamoto zinazokumba asasi ya ndoa
    • Vifo - Teerry, Lily
    • Ukosefu wa watoto – Mwangemi na Neema
    • Ukabila/ ukoo – Lucia, Subira, Selume
    • Wazazi kukataa wanao kuolewa – Rehema
    • Ukosefu wa uaminifu – Bw. Tenge
    • Chuki – Pete kuonewa na wake wenza
    • Vita katika ndoa – mamake Sauna anadhulumiwa na Maya
    • Migogoro katika ndoa – babake Pete anamkataa
    • Pombe/ ulevi – babake mzazi Sauna
    • Umaskini – Naomi kumwacha Lunga
    • Upweke – Lunga
    • Uhasama katika ndoa – Mzee Mwimo
    • Wazee kuoa wasichana wadogo – mzee Fungo anamuoa Pete kama mke wa nne.
    • Tofauti za kisiasa – Seleume na mumewe
    • Malezi ya watoto – Annete anaenda ughaibuni na watoto
    • Ndoa za kujaribisha – Nyangumi na Pete
    • Kudanganywa – Pete anadanganywa na mwanamme
    • Wanandoa kutoacha nasaba zao baada ya kuolewa – Naomi
    • Maonevu/ kutengwa – Subira
    • Usaliti – Billy na Sally
  3. Umuhimu Wa Mandhari
    1. Shule Ya Tangamano
      • Kuonyesha masaibu lyanayoikumba familia ya ummu
      • Matatizo wanayokumbana lnayo wakimbizi – Kairu
      • Kuonyesha umaskini – familia ya Kairu
      • Ubaguzi wa kiokoo – mamake mwanaheri
      • Matatizo ya vijana wa kike katika umri mdogo – Zohali , Rehema
      • Jukumu la familia kusambaratisha watoto – Chandachema
      • Uwajibikaji wa vijana – Chandachema
      • Nafasi ya dini
      • Ukosefu wa uaminifu katika ndo/ uasherati – BW.Tenge
      • Ukatili wa Bw. Tenge
    2. Hoteli Ya Majaliwa
      • Kukutanisha watoto wa Lunga.
      • Kuonyesha malezi mema – mwangeka na mwangemi
      • Uhafidhina wa babu
      • Taasubi ya kiume ya babu
      • Msamaha – Naomi / watoto wake

SEHEMU C: TAMTHILIA YA KIGOGO (PAULINE KEA)
SWALI LA 4

“Huu moyo wangu wa huruma nao…”

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (al4)
    • Haya ni maneno ya majoka
    • Anamwambia kenga
    • Walikuwa ofisini mwa majoka
    • Wanazungumza kuhusu jinsi ya kuwaangamiza wapinzani kama walivyomwangamiza Jabali. (4x1=4)
  2. Fafanua sifa za msemaji (al4)
    MAJOKA
    • Mwenye taasubi ya kiume-Alisema kuwa hababaishwi na mwanamke na alimkemea Kingi kwa kushindwa kukabiliana naye Tunu, mwanamke. Pia anamwita Husda mwanamke, hamheshimu.
    • Mwenye hasira –Alitaka kumpiga Kingi kwa kukaidi amri yake ya kuwapiga watu risasi. Pia alimsukuma Kenga na kuanguka chini. Alikataa salamu za Kenga ati alienda kumuona akivinjari.
    • Mwenye kiburi-Alisema kuwa hawezi kuongea na upepo ilhali kulikuwa na watu wachache.
    • Jasiri – Alipanda jukwaani na kuanza kuwahutubia watu hata baada ya kuambiwa na Kenga kuwa ilikuwa hatari.
    • Mpyaro-Aliwaita Wanasagamoyo wajinga.
    • Ana hisia za ukware- Alisema bado alimpenda Ashua na alikuwa bado amwandama licha ya kuwa tayari alikuwa amemuoa Husda.
    • Mbinafsi –Alishikanisha sherehe za uhuru na za siku ya kuzaliwa kwake ili watu waisherehekee.
    • Fisadi- alisema kuwa hata asipopewa kura hata moja, bado angeshinda. Labda alinuia kuiba kura. Pia alikuwa amemtengea Kenga kipande chake sokoni.
    • Mjinga-Yaonekana haelewi kuna katiba mpya, anaelezwa na Kingi. Hafahamu maana ya safari yake, anamuuliza Babu. Haelewi kuwa kicheko asikiacho ni mwangwi wa kicheko wake. Anadhani ni cha Babu.
    • Mkali-Anamwambia Kingi kuwa amefutwa kazi mara moja. pia anamkaripia Chopi na kumwambia asicheze na chui.
    • Mwenye mamlaka- Alikuwa na walinzi wake waliomfuata alipoenda sokoni. Pia alikuwa na chama chake cha kisiasa.
    • Mwenye moyo mgumu-Baada ya kuenda safari ya kujisafisha nafsi, hakubadilika, aliendelea kuwa katili. Alitaka watu wapigwe risasi.
    • Mkaidi-Alikaidi ushauri wa Babu wa kutenda mema. Aliwaita watu wajinga na wasaliti.
    • Mwenye vitisho/Sauti yake inababaisha. Alimtishia Chopi anapomletea habari ya kifo cha Ngurumo. Anamwambia akishindwa na kazi Kenga angeifanya kumaanisha angepoteza kazi.
    • Mwenye mapuuza-Alipuuza ushauri wa Kenga wa kutoenda sokoni kwa sababu ilikuwa hatari. Afikapo huko, watu walitaka kumpiga na walimkataa kama kiongozi.
    • Muoga-Alimwambia babu asimwache peke yake. Pia alihofia watu waliolilia damu yake na kumhukumu.
      hoja4x1=4
  3. Onyesha kinyume kinachojitokeza katika dondoo hili. ( al 12)
    Tan mtahiniwa aonyeshe kuwa msemaji(majoka) hana huruma…yaani ni katili
    • Anafunga soko la chapakazi
    • Anapanga mauaji ya jabali aliyekuwa mpinzani wake.
    • Akishirikiana na kenga wanapanga kumwangamiza tuni
    • Anapanga kumuua chopi kwa kutotekeleza mpango wa kumwangamiza tu. Wanasema ni lazima aende safari
    • Anamvumanisha ashua na husda katika ofisi yake na hatimaye kusababisha vurugu kati yao
    • Hakumsaidia ashua alipoenda kwake kumuumba msaada watoto walipokuwa hawana chakula
    • Kampuni yake inawanyanyasa wafanyikazi jambo linalopelekea mgomo
    • Wanaompinga /wanaoandamana wanafurushwa na askarai kutokana na amri yake.
    • Ingawa anaungwa mkono na ngurumo, baada ya kifo chake anasema kimba chake kifukiwe juu ya vingine
    • Anaishi na Husda na wakati huo huo anamtamani Ashua. Anamsababishia mkewe dhiki.
    • Anamwambia kenga kuwa navunjwa na chatu. Anaonyesha kuwa katili na huenda akatumia vikosi vyake vya mauaji kumwangamiza
    • Anamfuta kazi Kingi baada ya kukataa kuwafyatulia risasi watu waliokuwa mkutanoni nje ya soko la chapakazi . ni katili
    • Majoka alishika ukosi wa shati lake Kingi akitaka kumpiga. Alimsukuma Kenga akaanguka chini.
      12x1=12

SWALI LA 5
Maudhui

  1. Utabaka
    • Majoka na Kenga ni wa tabaka la juu ilhali wafanyakazi wa sokoni ni wa tabaka la chini
    • Majoka anamiliki mali nyingi huko sagamoyo, kwa mfano- Majoka and Majoka Academy, Majoka and Majoka modern Resort
    • Matajiri kama majoka wanapata huduma bora za kiafya , anaye hata daktari wake huku huduma za afya Sagamoyo zikidorora.
    • Tabaka la juu lina fedha za kuendeleza miradi yao kwa haraka kama vile ujenzi wa hoteli ya kifahari ilhali ni vigumu kwa maskini kupata lishe au kumudu bei ya vyakula
    • Tabaka la juu linatumia tabaka la chini kutimiza malengo yake. Vijana wahuni kwa mfano wanalipwa na wanasiasa ili wamuumize Tunu
    • Tabaka la chini halina vitu vya kimsingi kama mavazi kwa mfano Ashua ilhali Husda ana mavazi mazuri ya kisasa. Sudi ni maskini kiasi kwamba anashindwa kumpa mkewe pesa za matumizi.
      Zozote 5
      Kadiria majibu ya mwanafunzi
  2. Usaliti
    • Majoka anawasaliti wafanyabiashara kwa kuwafungia soko la chapakazi
    • Majoka anawasaliti wafanyakazi kwa kupandisha kodi licha ya hali ngumu ya maisha
    • Majoka anamsaliti Ashua kwa kumpangia njama ya kumkutanisha na mkewe Husda na kufungwa korokoroni
    • Majoka aliwasaliti wanahabari kwa kupanga kuwafungia vituo vya habari kwa kupeperusha habari za maandamano
    • Boza aliwasaliti wafanyakazi wenzakekwa kumuunga mkono Majoka licha ya kuwa aliwafungia soko walikofanyia biashara
    • Boza anawasaliti wenzake kwa kukosa kuwapasha habari kuhusiana na mradi wa kuchonga kinyago
    • Kenga alimsaliti Majoka kwa kuungana na wananchi mambo yanapomharibikia Majoka
    • Uongozi wa Sagamoyo unawasaliti wananchi kwa kuwatupia vijikaratasi wahame Sagamoyo si kwao
    • Serikali ya Majoka inawasaliti walimu na madaktari kwa kuwaongezea mshahara na kisha kupandisha kodi
    • Asiya aliwasaliti wananchi kwa kuwauzia pombe haramu iliyodhuru afya yao na hata kupelekea maafa
      Zozote 5
      Kadiria majibu ya mwanafunzi
  3. Umaskini
    • Wachongaji vinyago walitoka tabaka la chini. Wanakunywa chai ya mkandaa
    • Watoto wa Sudi wanalala njaa. Hii inamlazimu Ashua kwenda kuomba msaada kwa Majoka
    • Mamapima anauza pombe haramu kama njia ya kujipatia riziki
    • Mzee Majoka ana mpango wa kutoa chakula kwa wale wasiojiweza. Hii ni ithibati tosha kuna umaskini katika jimbo la Sagamoyo
    • Soko la Chapakazi linapofungwa wafanyakazi wanahangaika. Soko hili ni la walalahoi ambao walitarajia kuchuma riziki ya kila siku kutoka soko hili.
      Zozote 5
      Kadiria majibu ya mwanafunzi
  4. Dhuluma
    • Majoka napanga njama na Kenga na kumfungia Ashua kwa kisingizio kuwa alizua rabsha ofisini mwake
    • Korokoroni Ashua alipigwa na kujeruhiwa
    • Tunu alivamiwa na wahuni na kuvunjwa muundi wa mguu
    • Majoka na Kenga walipanga njama ambapo jabali aliaga dunia katika ajali ya barabarani.
    • Watu wanaoandamana wanapigwa na polisi na wengine kuuawa.
    • Serikali ya Majoka inafunga soko la Chapakazi ambalo lilikuwa tegemeo la kila siku
    • Hashima anatujulisha kuwa kumekuwa na umwagikaji mwingi wa damu pale Sagamoyo kiasi cha damu kuitia ardhi najisi.
      Zozote 5

SEHEMU YA D: HADITHI FUPI
Tumbo Lisiloshiba Na Hadithi Nyingine( Wah. Dumu Kayanda Na Alifa Chokocho)
SWALI LA 6

  1.                          
    1. Mnenaji – Mbura
    2. Mnenewa – sasa
    3. Wapi – Nyumbani kwa mzee Mambo
    4. Mzee Mambo alikuwa ameandaa sherehe kwa mtoto wake wa kwanza anaingizwa nasari na wa pili ameanza kuota meno
      ( 4 x1 = 4)
  2. Balagha – wako wapi
    Nidaa – wamepuuzwa tu kulee!
    Urudiaji (takriri) kwa niaba
    Kudumisha sauti – kulee!
    Zozote 3 x1 = 3
  3.                            
    • Mlafi – alikula chakula kingi
    • Mtetezi wa haki za wanyonge anasema kuwa kula kwa niaba ya maskini ni dharau.
    • Mwenye busara – anaelewa kuwa shibe ilikuwa ikiwamaliza kwa namna mbalimbali m.f magonjwa n.k
    • Mzalendo anawatetea wanyonge wa nchi yake na kuupanda mchele wa kwao Mbeya
    • Ni mweye utu – anataka wananchi pia wale kwa naiba ya viongozi
    • Ni mtambuzi – anatambua kwamba wananchi wanaendelea kukumbwa na dhiki hukuviongozi wakiendela kujifaidi
      Zozote 3 x1 = 3
  4.                      
    • tabaka la utawala limejawa na ubinafsi – wanakula kwa niaba yaw engine.
    • Mambo anatumia raslimali ya taifa kuandaa sherehe za watoto wake
    • DJ anapata huduma zote za kimsingi kama maji, umeme bila malipo ilhali maskini hulipia yotr
    • DJ anapata dawa za duka lake kutoka kwa bohari ya serikali anasema hajali
    • Mwandishi anasema waliopewa hawapokonyeki
    • Ubinafsi unawamaliza wabinafsi na kuwaletea magonjwa kama saratani, presha n.k
    • Sasa anafurahishwa na tabia yao ya kula kwa niaba ya watu wengine
    • Katika sherehe watu walikula na kurudia tena na tena hadi wengine wakabeba kama Mbura
    • Sasa anasema kuwa walio navyo walikula kwa niaba ya wengine waliopo na watakaozaliwa kwa hivyo kizazi kijacho hakitapata raslimali
    • DJ na wenzake wanachota mabilioni ya serikali katika sherehe
      (Zozote 5 x 1 = 5)
  5.                                
    • Kwa sababu ya kula watu wamepata magonjwa mbalimbali kama presha…
    • Kwa ajili ya kula wameleta vifo kwa kuuana mabomu, risasi na kunyongana
    • Kula kumewafanya wauane kufikiria kimawazo hivyo basi wanabaki nyuma kiamendeleo
    • Shibe inawamaliza kupitia watu kunyang’anyana vitu vinavyoonekana na visivyoonekana kama haki, heshima, utu na uhuru
    • Waliopo wanakula kwa niaba ya wengine waliopo na watakaozaliwa; watakaozaliwa hawatapata chochote ila matatizo ya kulipia mikopo
    • Mzee mambo anaandaa sherehe zisizo na maana kwa taifa lake. Maandalizi haya yanafanywa kwa kutumia raslimali za umma
    • Kwenye sherehe walikula vyakula vya kila aina, vitamu, vichacho, vikali ana baridi, mchele wa basmati. Plastiki matokeo yake ni maradhi ya kila aina na vifo.
      (za kwanza 5 x 1 = 5)

SWALI LA 7

  1. Umaskini katika mapenzi ya kifaurongo
    • wazazi wa Dennis wanafanya vibarua ili kukidhi mahitaji ya familia
    • Dennis akiwa shuleni hakuwa na mavazi ya kuvutia kama wanafunzi wenzake, hana simu na kipatakilishi
    • Chuoni dennis anapika uji mweupe kama chamcha kwa kukosa pesa za kununua chakula
    • Umaskini unamfanya Dennis kuchelea uhusiano wa mapenzi na wasichana chuoni
    • Umaskini unakuwa chanzo cha utengano wa watu. Peninah anamfukuza Dennis kwa ajili ya ukata
    • Dennis anakosa kuajiriwa katika shirika la uchapishaji kwa sababu ni maskini hajulikani. Alama 4
  2. unafiki katika Shogake Dada ana Ndevu
    • Safia anajifanya alivyo mzuri kwa wazazi wake kwa jinsi anavyovalia mavazi yenye staha ndani na nje ya nyumba. Kumbe alikuwa anawapumbaza wazazi wake.
    • Safia anatumia unafiki kwa kutajia wazazi wake masomo ili apate nafasi ya kumleta kimwana nyumbani
    • Kitendo cha Safia kujitia hasira anapoulizwa na mamake kuhusiano na mabadiliko yake ni cha unafiki
    • Swala la Safia kuavya mimba ni la kinafiki. Hakutaka wazazi wake wajue kuwa ulikuwa mjamzito
    • Kimwana ni mnafiki. Anajifanya mwanamke kwa kuvaa buibui ili aweze kukutana na mpenzi nyumbani kwao.
    • Wenye kliniki ambako safia alienda kuavya mimba ni wanafiki.wnatekeleza uovu huu huku wakijua madhara ya kitendo kile
      Zozote 4
      Kadiria majibu
  3. Mtindo
    • Uhuishi- donge likaja juu,
    • Balagha- kweli? Uongo?
    • Takriri- labda kweli
    • Msemo- tunga donge kifuani
    • Taswira- alitunga donge kifuani mwake
    • Taharuki- hakutambua afanye nini
  4. Jazanda kwenye Tumbo Lisiloshiba
    • kiti kulalamika – malalamishi ya maskini kuhusu dhuluma
    • jitu la miraba minne – utajiri/ uwezo mkubwa wa kifedha.
    • Tumbo lisiloshiba – tamaa kubwa ya matajiri
    • Tumbo lisiloshiba – pia ni jiji la kifahari lisilotosheka na maendeleo.
    • Jitu kukalia sehemu ya watu wanne- Tajiri mmoja kunyakua mali za maskini wengi.
    • Mstari mkali wa radi na umweso – uelewa wa wanamadongoporomoka.
    • Meza kuonekana ndogo – matajiri kuwadhulumu maskini kwa kiasi kikubwa.
    • Vyakula mkahawani– mali za watu wa madongoporoka.

SEHEMU YA E - FASIHI SIMULIZI
SWALI LA 8

  1. Tambua utungo huu na udhibitishe jawabu lako. (Alama 2)
    Majigambo/vivugo- mwandishi anajisifu kwa umahiri wake binafsi.
    Kutaja alama 1 kuthibitisha alama 1
  2. Kwa kurejelea hoja zozote nane, jadili sifa za utungo uliotambua kwenye swali la (a). (alama 8)
    Sifa za majigambo
    1. Hutungwa na kuganwa na muhusika mwenyewe.
    2. Hutungwa kwa usanii mkubwa. Anayejigamba hutumia mitindo tofauti au ishara.
    3. Mwenye kujigamba - hujitungia kivugo kufuatia tukio lililowah kuitokea maishani mwake.
    4. Mara nyingi majigambo hutungwa na kuganwa na wanaume.
    5. Husheheni matumizi ya chuku.
    6. Hutolewa kwa nafsi ya kwanza.
    7. Anayejigamba huweza kubeba baadhi ya vifaa vyake vya kazi au vinavyoonyesha jambo analojisifia.
    8. Majigambo yanaweza kutungwa papo kwa hapo.
    9. Anayejigamba huweza kutaja usuli wake wa kinasaba. Anaweza kusifu ukoo wake
    10. Anayejigamba huwa mlumbi.
    11. Maudhui makuu katika majigambo huwa ushujaa.
      (Akikosa (a) , atuzwe 0 katika (b) – Z a kwanza 8 x 1 = 8 athibitishe dai)
  3.                  
    1. Maghani ni nini? (Alama 1)
      Maghani ni ushairi ambao hutolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. 1 x 1 = 01
    2. Taja na ueleze tofauti za aina mbili za maghani unazojua. (Alama 4)
      maghani ya kawaida- tungo za mashairi yenye hubeba masuala ya kawaida; mfano, njaa, mapenzi, elimu nk.
      Maghani simulizi: mashiri ya kihadithi ambayo husimulia sifa za mtu ,mnyama, kitu, historia au tukio fulani.
      Kutaja – alama 2, kutofautisha 2/0
  4. Eleza jinsi jamii ya kisasa inavyojaribu kuendeleza fasihi simulizi. (Alama 5)
    1. Tamasha za kimziki. Wanafunzi hukariri, hugana na kuimba mashairi katika tamasha za muziki
    2. Sherehe za harusi, jando, mazishi na matambiko bado zinaendelezwa na jamii ya sasa.
    3. Utungaji na utegaji wa vitendawili kupitia redio na runinga.
    4. Michezo ya kuigiza katika runinga na redio.
    5. Tamasha za drama hihifadhi utanzu wa maigizo,mazungumzo na ushairi simulizi.
    6. Sarakasi za wasanii huhifadhi kipera cha vichekesho.
    7. Ngoma za kienyeji huchezwa kwenye hafla kama vile harusi au mikutano ya kisiasa.
    8. Wapo watafiti ambao huandika na kuhifadhi rekodi za vipera vya fasihi simulizi.
    9. Utambaji wa hadithi hutambwa na jamii nyingi za kisasa hasa sehemu za mashambani.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Form 4 Term 2 Opener Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest