Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Form 4 Term 3 Opener Exams 2023

Share via Whatsapp
Maagizo
  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili
  1. UFAHAMU    (ALAMA 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yafuatayo


    Mirundiko ya taka pamoja na utaratibu usiofaa wa uzoaji wake ni tishio kubwa kwa siha ya umma pamoja na mazingira. Hii ni kwa kuwa taka huwa ni makaazi ya wadudu waharibifu kama nzi, mbu, kombamwiko na panya ambao hueneza magonjwa na kuharibu vitu vyenye thamani. Maji taka nayo, pamoja na mifuko ya sandarusi huwa ni maskakimu ya wadudu na virusi vinavyoleta magonjwa mbalimbali.

    Mifuko ya sandarusi ina madhara zaidi kwa kuwa huziba mitaro ya maji na kuzuia upitaji wa maji. Madhara hutokeza wakati wa mvua za gharika. Maji hukosa njia yake ya kawaida ambayo huwa imezibwa na mifuko hii. Maji haya husababisha mafuriko ambayo huleta hasara ya mali na wakati mwingine ya uhai. Fauka ya hayo, mifuko hii huwasakama tumboni wanyama, sio wa nyumbani tu bali wa porini na majini.

    Kwa sababu ya hatari zitokanazo na taka, pana haja ya kutafuta njia ya teknolojia ya kuweza kukabiliana na tatizo hili ili kuyatunza mazingira na siha ya umma. Njia mojawapo ya kufanya hivi ni, kuelimisha na kuhimiza umma kuwa na ungalifu katika utumizi wa bidhaa na raslimali ili kupunguza uzalishaji wa taka.

    Matumizi ya bidhaa kwa njia ya ubadhirifu huwa chanzo cha uzalishaji wa taka kwa wingi. Kwa mfano, maji ni raslimali ambayo imeendelea kutumiwa kwa ubadhirifu na hiyo huzalisha maji taka kwa wingi. Raslimali hii inaweza ikatumiwa kwa njia endelevu. Kwa mfano, badala ya kutumia bafu ya manyunyu kuogea mtu anaweza kutumia maji ya karai.

    Watu wengi huchukulia taka kuwa kitu kisicho na manufaa yoyote. Hawajui kuwa kwa kutumia teknolojia endelezi, taka nyingi zinaweza zikageuzwa na kuwa na manufaa mengi. Vijana wadogo mashambani wanahitaji pongezi kwa kuwa na utambuzi wa mifuko ya sandarusi kutengenezea mipira wanayoitumia kuchezea. Hii ni teknolojia endelezi ambayo taka hugeuzwa na kuwa na manufaa.

    Baadhi ya wananchi wenye ubunifu nao wameanzisha miradi ya kuzoa takataka kutoka majumbani mwa watu kwa ada, kisha huzipeleka taka hizi kule zitakakobadisliswha ili ziwe bidhaa za plasitiki kama matangi, mitungi, sapatu na champali. Taka hizi huwa malighafi yakutengenezea bidha zingine. Taka za chupa na chuma nazo huuzwa katika viwanda vinavyozigeuza kuwa na manufaa tena. Taka za karatasi hutumiwa kutengenezea bidha kama vitabu, katoni, shashi za chooni na magazeti. Taka zinaweza pia kugeuzwa kuwa zenye faida kuzitumia kufanyia mboji. Ni muhimu kutambua kuwa si kila aina ya taka inaweza kutumiwa hapa. Taka zinazoweza kufanyiwa mboji ni zile huoza kwa haraka kama vile mabaki ya vyakula, mboga na matunda. Kwa sadfa, hizi ndizo taka zinazozalishwa zaidi siku hizi  na hasa sehemu za mijini na katika maeneo ya biashara kama mikahawa na hospitali.

    Mtu akiwa na nafasi anaweza kuchimba shimo ambalo atafukia taka hizi ili kutengeneza mbolea. Hii ni njia isiyodhuru mazingira na yenye manufaa kem kem. Kwanza hugeuza taka inayoweza kuwa hatari na kuifanya iwe yenye manufaa kwa hivyo hutatua matatizo ya kiafya yanayoweza kutokana na mirundiko ya taka. Mchanga nao hufaidika kupata virutubishi. Mbolea kama hii inaweza ikatumika kukuzia mboga au maua katika bustani. Maji taka, hasa yanayotumiwa kuoshea vyombo, nayo yanaweza kutumika kunyunyizia mashamba madogo ya mboga au bustani za maua. Maji taka haya yanahitaji kutayarishiwa njia mahsusi ya kuyaelekeza katika mashamba haya baaada ya kutumiwa.

    Aghalabu watu wengi wana mazoea ya kuchoma taka. Ni kawaida kupata matanuri ya kuchomea taka katika baadhi ya mitaa, shule na hospitali. Badala ya kupoteza moto huu bure bilashi, inawezekana pakawekwa tangi la chuma ambalo litatumia moto huo kuchemsha maji. Maji haya yanaweza yakatumiwa katika shughuli za nyumbani.

    Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa kuna baadhi ya taka ambazo ni hatari na huenda zisigeuzwe ili kutumika kwa njia yenye faida, taka hizi ni kama vile mikebe au vifaa vingine vyenye kubeba sumu au dawa hatari. Ni bora kuvitupa vifaa hivi katika mashimo marefu au vyoo vya mashimo. Kwa vyovyote vile, ni jambo muhali kwa watu popote wanapoishi kulinda siha yao pamoja na kutunza mazingira. Ulinzi na utunzi huu huhitaji uangalifu mkubwa katika utupaji taka.

    MASWALI
    1. Taka zina madhara chungu nzima kwa binadamu, eleza kwa hoja tano.  (alama 5)
    2. Kuna njia nyingi za kubadilisha taka kuwa na manufaa katika jamii. Thibitisha kwa mujibu wa kufungu. (alama 4)
    3. Taja njia mbili za kuyatunza mazingira (alama 2)
    4. Je, hatima ya taka zisizoweza kuleta manufaa yoyote kwa jamii ni gani? (alama 2)
    5. Andika visawe vya maneno yafuatayo; (alama 2)
      1. Maskakimu
      2. Muhali
  2. UFUPISHO (ALAMA 15) 

    Wanaume wapo katika hatari kubwa ya kupatwa na kansa kuliko wanawake, wataalamu wamebaini. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Kiafya Uingereza, umetaja tofauti za kimaumbile baina ya wanaume na wanawake huchangia wanaume wengi kuathiriwa na kansa. “Kuna tofauti za maumbile kati ya wanaume na wanawake ambazo hufanya wanaume wawe katika hatari zaidi,” unasema utafiti huo uliochapishwa katika jarida la “Cancer”.

    Idadi kubwa ya wanaume pia hujihusisha katika mitindo hatari ya maisha kama vile uvutaji wa sigara, kunywa pombe kupita kiasi na lishe duni ambazo zinawaweka katika hatari ya kupatwa na saratani. Ripoti ya utafiti huo pia inaonyesha kuwa wanawake wana homoni mbili za X ambazo huwa na uwezo wa kuzuia saratani ikilinganishwa na wanaume ambao wana homoni moja ya X pekee.

    Kulingana na Shirika la afya Duniani (WHO), aina za kansa zinazowahaingaisha wanaume zaidi ni kansa ya tezi dume (prostate cáncer), korodani (testicles cáncer), mapafu, koo, kongosho (pancreas), ini na kibofu cha mkojo. Kansa ya koo na mapafu husababishwa na uvutaji sigara na ya ini huletwa na ubugiaji wa pombe kupindukia.

    Wizara ya Afya inakadiria kuwa kansa ya tezi dume huua wanaume elfu moja mia mbili tisini na mbili (1,292) kila mwaka nchini Kenya. Kansa ya mapafu nayo husababisha vifo mia sita sitini na tisa (669). Nchini Kenya kansa huchangia asilimia saba ya vifo vyote kila mwaka.

    Wagonjwa zaidi ya elfu arobaini na mbili (42,000), wanaougua kansa nchini huenda wakapata afueni baada ya jopokazi maalum kupendekeza kupunguzwa kwa gharama ya matibabu ya ugonjwa huo. Katika ripoti iliyotolea na jopokazi hilo lililoongozwa na Mkuu wa idara ya kupambana na Kansa nchini Mary Nyangasi, linasema kuwa gharama ya matibabu ya kansa nchini ni ghali kiasi kwamba wengi wa wakenya hawamudu.

    “Nchi hii hukumbwa na uhaba wa dawa za kutibu na vifaa muhimu vya matibabu” inasema ripoti hiyo. Gharama ya matibabu nchini hutofautiana kulingana na aina ya kansa na kiwango cha saratani mwilini. Kwa mfano, wagonjwa wanaofanyiwa tibakemia pekee hulipa shilingi 138,200, huku gharama ya wanaofanyiwa upasuaji ikiwa shilingi 128,207. Matibabu ya saratani ya awamu ya kwanza, pili na tatu za saratani ya matiti  katika hospitali za umma ni kati ya shilingi 160,000 hadi shilingi 184,000 huku wanaougua saratani ya mlango wa uzazi wakitozwa kuanzia shilingi 100,000 hadi shilingi 180,000.

    Wagonjwa wanaougua kansa awamu ya tatu, huwa hatarini zaidi kwani huwa imesambaa zaidi mwilini ikilinganishwa na wale wa awamu ya kwanza.

    MASWALI
    1. Fupisha ujumbe muhimu katika aya tatu za kwanza. (maneno 75-80). (alama 7), (1 utiririko).
      Matayarisho
      Jibu
    2. Dondoa hoja kuu katika aya tatu za mwisho. (maneno 80-85). ( alama 8), 1 utiririko
      Matayarisho
      Jibu
  3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
    1. Andika neno lenye muundo ufuatao wa sauti. (alama 1)
      IIKI
    2. Tunga sentensi kwa kutumia nomino katika ngeli ya LI-YA, katika hali ya wingi pamoja na kivumishi kionyeshi cha mbali sana.     (alama 1)
    3. Tunga sentensi kuonyesha viambishi vifuatavyo;
      Nafsi ya kwanza umoja, wakati uliopita, kirejeshi, yambwa, mzizi, kauli ya kutendea, kiishio. (alama 2)
    4. Tambua vitenzi na uonyeshe ni vya aina gani katika sentensi ifuatayo.
      Mwalimu huyu aliyekuwa akizawidiwa juzi ni shujaa. (alama 3)
    5. Nyambua mzizi uliopewa kwa kuzingatia kauli ulizopewa mabanoni. (alama 2)
      1. -l (kutendeka)
      2. -p (kutendewa)
      3. -ti (kutendua)
      4. -fung (kutendama)
    6. Ainisha vielezi katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
      Kura nyingi sana zilipigwa vizuri jana jioni.
    7. Tumia neno ‘kile’ kama kiwakilishi na kama kivumishi.       (alama 2)
    8. Tunga sentensi moja ukitumia  ‘na’ kama kiunganishi na kama kihusishi. (alama 2)
    9. Badilisha maneno yaliyopigiwa mstari kuwa nomino katika sentensi ifuatayo. 
      Alipotangazwa kuwa mshindi alifurahi na kuwashangaza wengi. (alama 3)
    10. Ainisha virai katika sentensi ifuatayo na ueleze ni vya aina gani. (alama 3)
      Viongozi wengi walikuwa wakakamavu sana kabla ya uchaguzi.
    11. Changanua sentensi ifuatayo kwa kutumia visanduku. 
      Baba na Martha wamepewa cheti na mwenyekiti wa kamati. (alama 4)
    12. Bainisha shamirisho katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
      Mbunge aliyepigiwa kura na wananchi amesafiri kwa ndege.
    13. Tunga sentensi yenye mpangilio ufuatao. (alama 2)
      Kiima+ Kivumishi + Kielezi + Kiarifa + Chagizo
    14. Tunga sentensi ifuatayo upya ukitumia ‘o’ rejeshi kuleta dhana ya mazoea.
      Mnyama ambaye alidhoofika ndiye ambaye alitunzwa vizuri. (alama 1)
    15. Ainisha mofimu katika fungutenzi lifuatalo. (alama 3)
      Ameniwia.
    16. Andika kinyume cha maneno yaliyopigiwa mstari. (alama 3)
      Walipachika na kufunga mizigo aliyopakia juu ya lori.
    17. Tunga sentensi yenye kishazi tegemezi ambacho ni kivumishi. (alama 2)
    18. Shumbi ni kwa udongo,……………..kwa chumvi, na …………..kwa mtama. (alama 1)
  4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
    Soma kifungu hiki kisha ujibu maswali yanayofuata.
    Wananchi watukufu, mimi ni ndume. Wale wanaonichokoza waambiwe Kizingo hawaogopi. Wangoje mpaka next general election. Tupatane kwa debe.
    1. Eleza muktadha wa sajili hii. (alama 2)
    2. Tambua mbinu mbili za lugha zilizotumika katika kifungu hiki. (alama 2)
    3. Eleza sifa sita za sajili uliyotambua hapo juu. (alama 6)

MARKING SCHEME

  1. UFAHAMU    (ALAMA 15)
    1.  
      1. Huwa makaazi ya wanyama waharibifu waletao magonjwa
      2. Taka huziba mitaro ya maji na kuzuia maji kupita
      3. Madhara huwa ni mafuriko wakati wa mvua za gharika
      4. Mafuriko husababisha hasara ya mali
      5. Vifo hutokea kupitia mafuriko/ kupoteza uhai
      6. Taka huwasakama tumboni wanyama wa nyumbani, porini na majini (alama 5)
        * sahihisha hoja tano za kwanza
    2. Karatasi za sandarusi hutumiwa kutengeneza mpira
      1. Taka hutumika kama malighafi ya kutengeneza bidhaa zingine, kama vile, bidhaa za plastiki
      2. Taka za karatasi hutengeneza bidhaa kama katoni, vitabu, shashi na magazeti.
      3. Taka ya vyakula hutengeneza mboji au mbolea isiyohatarisha mazingira
      4. Maji taka hasa ya kuoshea vyombo yanaweza kutumika kunyunyuzia mimea
      5. Moto wa kuchoma takataka waweza kutumika kuchemsha maji ya kutumiwa nyumbani (alama 4) * hoja zozote nne
    3.  
      1. Kuelimisha na kuhimiza umma kuwa na uangalifu katika matumizi ya bidhaa ili kupunguza uzalishaji wake.
      2. Kutumia teknojia endelezi au endelevu ili kugeuza taka kuwa ya manufaa. (alama 2) * hoja mbili za kwanza
    4. Hutupwa katika mashimo marefu au vyoo vya mashimo. (alama 2)
    5.  
      1. Maskakimu – Makaazi (alama 2)
      2. Muhali   - muhimu
  2. UFUPISHO (ALAMA 15) 
    1.  
      1. Wanaume wapo hatarini ya kupatwa na kansa kuliko wanawake.
      2. Tofauti za kimaumbile husababisha hali hii.
      3. Wanaume hujihusisha na mitindo hatari na huwa na lishe duni.
      4. Wanawake wana homoni mbili za X zilizo na uwezo wa kuzuia saratani ikilinganishwa na wanaume ambao wana homoni moja ya X.
      5. Kulingana na WHO, kuna aina nyingi za kansa zinazowahangaisha wanaume.
      6. Kansa ya koo na mapafu husababishwa na uvutaji sigara na ya ini ubugiaji wa pombe.
      7. Wizara ya afya Kenya inakadiria kuwa kansa ya tezi dume huua wanaume 1292 kila mwaka.
      8. Asilimia 7 ya vifo vyote huchangiwa na kansa (alama7)(1 ut)
    2.  
      1. Wagonjwa wengi wa kansa huenda wakapata afueni.
      2. Hii ni baada ya jopokazi kupendekeza kupunguzwa kwa gharama ya matibabu ya kansa.
      3. Ripoti ilisema kuwa gharama ya matibabu ya kansa ni Ghali sana
      4. Nchi ina uhaba wa dawa na vifaa muhimu.
      5. Gharama ya matibabu hutofautiana kulingana na kiwango cha saratani.
      6. Gharama ya tiba kemia na upasuaji hutofautiana.
      7. Matibabu ya saratani ya matiti na saratani ya mlango wa uzazi ni Ghali pia.
      8. Wanaougua kansa awamu ya tatu huwa hatarini. (alama 8)(1 ut)
  3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
    1. aibu *kadiria jibu la mwanafunzi 1/0 (alama 1)
    2. Magari yale yalipakwa rangi 1/0  (alama 1)
    3. Nilichokipikia 2/0 (alama 2)
    4. ni-kitenzi kishirikishi kipungufu
      aliyekuwa – kitenzi kisaidizi
      akizawadiwa – kitenzi kikuu 1x3 (alama 3)
    5.  
      1. lika 
      2.  pewa 
      3. toa
      4. fungama ½ x4 (alama 2)
    6.  
      • sana – kielezi halisi
      • vizuri – kielezi cha hali
      • jana jioni – kielezi cha wakati zozote mbili1x2 (al 2)
    7.  
      • Kile kimeraruka – kiwakilishi
      • Kitabu kile kimeraruka – kivumishi   1x2(alama 2)
    8. Juma na Zainabu walinunuliwa viatu na baba.  *kadiria jibu la mwanafunzi   2/0   (ala 2)
    9. Kutangazwa kwake kuwa mshindi kulimpa furaha na kuwapa wengi mshangao. (ala 3)
    10.  
      • Viongozi wengi – kirai nomino (RN)
      • Walikuwa wakakamavu sana – kirai tenzi (RT)
      • Kabla ya uchaguzi  - kirai husishi (RH) 1x3 (alama 3)
    11. Baba na Martha wamepewa cheti na mwenyekiti wa kamati. (alama 4)
                                                                      S    
                     KN                                            KT  
       N  U  N  T  N   H   N   H   N
       Baba  na   Martha   walipewa    cheti    na   mwenyekiti   wa   kamati
    12.  
      • Kura- shamirisho kipozi
      • Wananchi- shamirisho kitondo
      • Ndege- shamirisho ala 1x3 (alama 3)
    13. Jambazi sugu sana lilishikwa jana asubuhi. 2/0 (alama 2)
    14. Mnyama adhoofikaye ndiye atunzwaye vizuri.    1/0 (alama 1) *   
      ‘o’ rejeshi iwe tamati kuleta dhana ya mazoea.
    15.  
      • a - nafsi ya tatu umoja
      • me – hali timilifu
      • ni – yambwa tendewa
      • w - mzizi
      • i – kauli ya kutendea
      • a - kiishio       ½ x6 (alama 3)
    16. Walipachua na kufungua mizigo aliyopakua juu ya lori. 1x3 (alama 3)
    17. Wanafunzi waliokuwa wametia bidii walitunzwa zawadi.   2/0 (alama 2)
    18. Finyo kwa chumvi
      Suke, shuke,, chane, kipeto, shazi, kwa mtama.  ½ x2 (alama 1)
  4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
    1. Muktadha wa siasa – msamiati maalum umetumika, kwa mfano, next general election.
    2.  
      • Istiara – mimi ni simba
      • Kuchanganya ndimi – Wangoje mpaka next general election.
    3.  
      • Huwa ni lugha ya propaganda
      • Ni lugha ya ucheshi
      • Hutumia chuku
      • Lugha yenye ushawishi
      • Yaweza kuwa na majibizano
      • Ni yenye udanganyifu
      • Imejaa ahadi
      • Ina kudunisha
      • Yaweza kuwa na matusi/bezo
      • Ina majisifu/ majigambo
      • Ina kauli fupi fupi
        *Mifano inaweza kutolewa kwa kifungu au nje ya kifungu, kadiria
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Form 4 Term 3 Opener Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest