Mzimu wa Kipwerere! summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Mzimu wa Kipwerere!- Yussuf Shoka Hamad

Mtiririko

Mzimu wa Kipwerere unatisha sana.

Mzimu wenyewe ni wa kichaka kidogo kilichojaa aina tofauti ya miti iliyobanana na kusabababisha kiza kinene cha kutisha.

Kitisho cha kwanza ni kichaka hicho kuitwa mzimu.

Pili, kichaka hicho kiko kwenye kiwanja kipana kilichozungukwa na nyumba za wanakijiji.

Jina Kipwerere linatokana na jamaa wa Bw. Msa, aliyesemekana kumpata shetani aliyefichua damu enzi za ujinga.

Alipofariki alizikwa hapo, kisha kichaka hicho kikaota.

Hivyo, kinaaminiwa kutokana na mzimu wa mwanamama huyo aliyejaa nguvu za kimiujiza. 

Kabla ya kufikia ‘mzimu’ huo kutoka pande zote, kumezungukwa na makaburi ya watu maarufu, ambayo lazima uyapite.

Nayo pia yanasemekana kuwa na vizuu na mizuka.

Pia kuna miiko kuhusu msitu huu. 

Mtu haruhusiwi kupita hapo saa sita mchana au majira ya usiku ila wazee wa msitu huo, vinginevyo atatolewa kafara.

Usiku kunaonekana taa ikiwaka.

Msimulizi anapoulizia, anaambiwa ni shetani anawapa watoto wake chakula.

Hili linamtia udadisi.

Pia, wanapita huko na watoto wakicheza na kusikia sauti ya mwanamume na mwanamke kutoka humo msituni, hasa nyakati za usiku mchanga.

Wanapouliza wazee wanaambiwa shetani wa mzimu ana mke, na huzungumza watoto wakilala.

Majibu haya yanamtia kiu zaidi.

Wakati mwingine wanasikia harufu ya mihadarati kama vile sigara na tumbaku.

Wazee wanasema baadhi ya mashetani hutumia mihadarati.

Salihina ni kiongozi wa kijiji na pia mzimu.

Anaongoza shughuli zote na kuomba ruhusa kwa mzimu kama vile tohara, arusi na shughuli.

Ndiye anasemekana kujua siri za mzimu.

Pia anasimamia maadili ya vijana.

Anawakataza kutangamana wavulana na wasichana hata katika michezo.

Wakati mmoja, msimulizi anapokea adhabu ya viboko kumi kwa kusimama karibu na msichana baada ya kucheza.

Utumiaji wa mihadarati ni hatia na pia unasemekana kupigwa marufuku na mizimu.

Hata hivyo, mji wa watawa bado unaongoza kwa usambazaji na utumiaji wa dawa hizi, zinakotoka hakujulikani.

Suala la mzimu badala ya kumtia woga msimulizi, linamtia udadisi na ujasiri.

Anaazimia kujua siri za mashetani.

Anajisogeza karibu na msitu huo kila kuchao hadi siku moja anapoamua kuukaribia.

Anapolala karibu na mzimu, anausikia wimbo ambao husemekana lazima utumiwe kama ufunguo wa kuingia humo.

Unaimbwa na mwanamume na kujibiwa na mwanamke upande mwingine, kisha anaingia mzimuni.

Baada ya muda, harufu ya tumbaku inamjia na sauti zile za chinichini.

Baada ya saa tatu, wawili wale wanaondoka, kila mmoja njia yake.

Msimulizi anaondoka, tayari kurejea keshoye kuingia mzimuni.Keshoye magharibi, msimulizi anafika huku amevaa guo jeupe lililomfunika kabisa.

Anaimba ule wimbo na kuingia.

Kuna giza totoro, hivyo anawasha tochi.

Anamulika na kuona marobota ya bangi, makasha ya tumbaku na unga wa kilevi, pia chang’aa kwenye pipa.

Kuna kitanda cha besera kilichopambwa kwa maua juu na mvunguni.

Anasikia sauti ya mwanamume ikiimba wimbo wa mzimu.

Anazima tochi upesi na kuingia mvunguni.

Baada ya wimbo, wale watu wawili wanaingia. Anajawa na hofu anapogundua sauti ya Salihina.

Wanaanza kwa kutumia vileo.

Bishoo, yule mwanamke, anamweleza Salihina mbinu mpya ya kusambaza mzigo.

Wanachukua ndoo na kusema wanaenda kuchotea shetani wa mzimu maji.

Hakuna anayewasumbua, hata polisi. Ndoo hizo zinajazwa mihadarati badala ya maji.

Salihina anakubali wazo hilo.

Bishoo anamweleza kuwa ana haraka ya kurudi nyumbani kumwuguza mumewe anayeumwa na jino.

Anamwambia kuwa hawatakaa sana.

Salihina anaanza kuimba akimwelekea Bishoo.

Bishoo anasogea na kuchukua kiberiti kuwasha kibatari.

Kwa hofu ya kuonekana, msimulizi anachomoka na kuwashtakia kuwa amewakamata.

Bishoo anaanguka na kuzirai pale pale.

Salihina anatoka mbio lakini mti unamzuia kwa kushika kanzu lake jeupe la bafta.

Anamwomba msimulizi msamaha na radhi akidhani ndiye amemshika.

Msimulizi anaondoka na kuwaacha hapo.

Salihina analilia kitawi kile hadi asubuhi, wanakijiji wanapofika na kushuhudia siri ya mzimu waliouogopa kiasi cha kuuabudu.  

Ufaafu wa Anwani ‘Mzimu wa Kipwerere’ 

Neno ‘Mzimu’ lina maana mbili.

Kwanza, sehemu ambapo hufanyiwa matambiko na ambapo huaminika roho za waliofariki huishi, na kivuli cha mtu aliyeaga ambaye huwatokea walio hai.

Kipwerere ni jina la mwanamke wa enzi za ujinga anayeaminiwa kuwa na nguvu za kimiujiza.

Jina hili linapatiwa msitu ulio katika kijiji hiki.

Kwanza, msitu huo umezungukwa na makaburi pande zote.

Lazima uyapite kabla ya kuufikia.

Makaburi haya yanazikwa watu maarufu.

Ndipo mizimu yao inaishi. 

Msitu huu unapatiwa jina la mzimu kutokana na kutisha kwake.

Una miti mikubwa iliyokua na kubanana, ikafanya kiza kikubwa.

Unaaminika kuwa ulichipuka baada ya Kipwerere kuzikwa hapo.

Mwanamke huyu aliaminiwa kuwa na nguvu za miujiza.

Msitu huu pia unaaminika kuwa makao ya mashetani na mizimu.

Hivyo, watu hawaruhusiwi kupita hapo saa sita mchana na usiku.

Wanaopita hapo wanatishiwa kuwa watatolewa kafara na kuondokea kuwa chakula cha Mzimu wa Kipwerere.

Mzimu huu(msitu) una maajabu yake.

Usiku huonekana mwanga wa taa, na pia husikika mazungumzo ya watu.

Isitoshe, harufu ya tumbaku na vileo vingine hutoka huko.

Majibu ya masuala haya ni kuwa mashetani huzungumza, na pia hutumia mihadarati kama binadamu.

Salihina ndiye kiongozi wa mzimu.

Kila kitu kuhusiana na mzimu lazima ahusishwe.

Anasemekana kuwa ndiye anaweza kuwasiliana na mizimu.

Wakati wa tohara, matambiko na arusi ndiye hutoa maombi kwenye msitu ili mizimu ikubali masuala hayo yaendelee.

Kuingia mzimuni pia kuna masharti yake.

Kuna wimbo ambao yasemekana ndio ufunguo wa kuingia humo, na ambao lazima uimbe ndipo mashetani wakukubalie kuingia.

Msimulizi anausikia kutoka kwa Salihina na Bishoo wanapoimba na kuingia.

Mwishoni, msimulizi anagundua kuwa Salihina ndiye ‘Mzimu wa Kipwerere’!

Ndiye anazungumza huko usiku na mshirika wake, Bishoo.

Ndio wanaowasha taa na kuvuta sigara.

Wanatumia msitu ule kufanya biashara haramu ya usambazaji wa dawa za kulevya.

Sheria zote na imani kuhusiana na msitu huo ni hila tupu.  

Dhamira ya Mwandishi 

Anawasilisha mila na tamaduni zilizopitwa na wakati na imani za kijinga, na jinsi zinavyoweza kutumika kuendeleza uhalifu.

Anadhihirisha unafiki unaotumiwa na viongozi kutekeleza uhalifu na kujinufaisha binafsi.

Anasawiri uozo uliokithiri katika jamii kama vile unafiki na ulaghai, uzinzi na mengine.

Anatoa onyo kwa wanaotumia ujanja kutekeleza uhalifu kuwa siku yao ya kunaswa itafika tu.

Anadhihirisha migogoro iliyopo katika jamii, hasa kati ya wazee na vijana.

Anadhihirisha umuhimu wa kuwa na udadisi na ujasiri kuhusiana na masuala tata ya kijamii.  

Maudhui 

Itikadi na Ushirikina

Ni imani potovu kuhusiana na masuala ya ramli, uchawi, mizimu na masuala ya aina hiyo.

Watu wengi wanatishwa na Mzimu wa Kipwerere kutokana na imani za kishirikina.

Inaaminika kuwa msitu huo ulikua baada ya Kipwerere kuzikwa hapo, mwanamke anayesemekana kupata shetani aliyefichua damu.  

Yasemekana baada ya kuzikwa hapo, mzimu huo unakua.

Pia, anaaminika kuwa alikuwa mwanamke wa miujiza.

Mzimu wa Kipwerere pia una miiko yake.

Watu hawaruhusiwi kupita pale muda wa jua mtikati au jua likishatua.

Pia, hakuna anayeruhusiwa kuingia humo ila wale waitwao wahenga.

Yeyote ambaye angefanya hivyo, basi anasemekana kuwa chakula cha mizimu, na atatolewa kafara. 

Watu pia wanaamini kuwepo kwa mashetani na mizimu.

Watoto wanapochezacheza nja ya msitu ule, wanasikia sauti za chinichini za watu wakiongea.

Wazee wanawaeleza kuwa shetani ana mke na mara nyingi wanapozungumza, watoto wao huwa wamelala.

Taa inayowaka inahusishwa na mashetani hao, sawa na mnuko wa tumbaku na mihadarati mingine.

Msimulizi anajawa na udadisi kuhusiana na mashetani hawa wanaozungumziwa kila mara.

Anaamua kujaribu kuingia msituni na hata ikiwezekana kuwaona kwa macho!

Kwake, ni kweli kwamba mashetani hawa wapo.

Kuna wimbo unaoaminiwa kuwa ufunguo wa kuingia mzimuni.

Anausikia kutoka kwa Salihina na kuuimba kisha kuingia.

La kushangaza ni kuwa hamwoni shetani yeyote anavyotarajia. 

Anagundua kuwa Salihina ndiye anaendesha shughuli zote wanazoshuhudia msituni humo.

Salihina na Bishoo wanatumia itikadi na imani potovu kuchuuza mihadarati.

Bishoo anamweleza mpango wake wa kusafirisha dawa hizo kwa kubeba ndoo wanazodai kuwa wanaenda kuchotea shetani wa mzimu maji.

Hata polisi wenyewe wanawaruhusu!

Ndoo hizo hatimaye zinajazwa ‘mzigo’; mihadarati. 

Mazingira

Hali ya mazingira imengaziwa kwa njia ya kipekee.

Mandhari yanaonyeshwa kwa uwazi wa kupendeza.

Mzimu wa Kipwerere una miti ya aina tofauti, ambayo imemea kwa ukaribu na kufanya kichaka cha kutisha.

Mshonano huo wa miti unafanya muhali kwa miale ya jua kupita au maji ya mvua na kuzua giza totoro mle ndani ya msitu huo.

Kichaka hiki kiko katikati ya iwanja chenye uwazi cha takriban eka moja.

Pande zote, yanazunguka majumba ya wanakijiji wa hapo.

Katikati ya majumba ya wanakijiji na msitu huo, kuna uwazi mkubwa ambao hautumiwi kwa shughuli zozote za kilimo ila umehifadhiwa kwa ajili ya kuzikwa kwa watu wenye utukufu katika jamii.

Hivyo, kabla ya kuingia msituni lazima upite makaburi hayo. 

Msimulizi anapoingia kwenye msitu, anakumbana na kiza totoro.

Anamulika na kuona kitanda cha besera kilichotandikwa vizuri.

Juu yake kuna asumini na maua ya mlangilangi yanayonukia mahaba.

Chini ya kitanda, kuna chetezo kilichojaa udi wa mawaridi.

Msimulizi anapowashtua washirika wa mzimu, Bishoo anazirai naye Salihina kutoroka lakini anakamatwa na kitawi cha mti, kinachomzuia kukimbia. 

Ulaghai

Salihina anaaminiwa na kuheshimiwa na watu kama mzee wa kijiji na kiongozi wa mzimu.

Anawahadaa wanakijiji kwa kujifanya mtu mzuri mwenye maadili lakini ukweli ni kwamba ni mtu mbaya.

Anamcharaza msimulizi kwa sababu ya kusimama karibu na msichana tu.

La ajabu ni kuwa yeye mwenyewe anazini na mke wa mtu kwenye Mzimu wa Kipwerere. 

Salihina anatumia woga wa watu kuhusiana na Mzimu wa Kipwerere kujinufaisha.

Anawafanyia maombi na kuongoza matambiko yote ili yakubalike na mizimu.

Anatoa sheria kali za mizimu ili kuwazuia watu kuingia msituni humo.

Anautumia kuendeleza uzinzi na kuficha shehena za dawa za kulevya. 

Uvutaji sigara na dawa za kulevya ni marufuku katika kijiji hiki.

Hata hivyo, kijiji hiki kinaendelea kuongoza kwa masuala haya.

Haijulikani zianakotoka dawa hizi.

Viongozi kama Salihina ndio wanafaa kuwa katika msitari wa mbele kuwinda wahalifu.

La kusikitisha ni kuwa Salihina mwenyewe ndiye anaendeleza ulanguzi wa dawa hizi kwa ujanja wa kutumia Mzimu wa Kipwerere.

Bishoo anampa Salihina mpango wa kilaghai wanaotumia kulangua dawa zile za kulevya.

Wanakusanya wanawake na kuwapa ndoo wakidai kuwachotea maji shetani wa mzimu.

Watu hawasaili chochote wanaposikia haya, hata polisi.

Ndoo hizi badala ya kujazwa maji zinajazwa mihadarati.

 Bishoo anamwacha mumewe ambaye anaumwa kuja kuzini na Salihina na kuendeleza biashara zao.

Anamwambia Salihina kuwa alimuaga mumewe kuwa ameenda kumwona mtoto wa jirani mgonjwa.

Anataka wamalize biashara zao upesi arudi nyumbani. 

Ulanguzi/Biashara Haramu

Matumizi ya mihadarati yamepigwa marufuku katika kijiji hiki.

Hata hivyo, bado kinaongoza kwa matumizi yake.

Ni suala ambalo linawachanganya wengi, kwani kule zinakotoka dawa hizo ni kitendawili kikubwa.

Msimulizi anapoingia kwenye Mzimu wa Kipwerere, anapata marobota ya bangi, makasha kwa makasha ya tumbaku na mapipa ya chang’aa.

Anagundua biashara haramu ambayo Salihina na washirika wake huendeleza katika msitu huu kwa kisingizio cha mashetani. 

Kwa kuwa ni ulanguzi, Bishoo analazimika kutumia ujanja kusambaza dawa za kulevya. Wanachukua ndoo wakidai kuchotea shetani wa mzimu maji na kuzijaza shehena ile.

Hata hivyo, hatimaye wanafumaniwa na wanakijiji wanajua siri kubwa iliyomezwa na msitu ule. 

Utamaduni

Kuna usimulizi wa visa katika jamii. Jina ‘Mzimu wa Kipwerere’ linatokana na kisa cha mwanamke aitwaye Kipwerere, anayeaminika kuishi enzi za ujahiliya, jamaa ya Bwana Msa aliyepata shetani aliyefichua damu.

Inaaminika kwamba anapozikwa ndipo msitu ule unamea.

Ndio sababu unaaminika kuwa makao ya mizimu na shetani na kuogopwa sana.Jamii hii ina mtindo unaotumika kutekeleza matambiko fulani fulani katika jamii.

Salihina ni mtendaji mkuu wa shughuli za kimila kijijini.

Watoto wanapotaka kutahiriwa, huletwa kando ya mzimu ili Salihina awape Baraka. Kukiwa na arusi, lazima apatikane aombe ruhusa kwa mizimu ili shughuli ziendelee. 

Salihina anakataa katakata watoto wa kiume na kike kutangamana, hata wakati wa kucheza.

Yeyote anakaribia jinsia nyingine anapata adhabu kali. Msimulizi wakati mmoja anajipata amesimama karibu na msichana baada ya mchezo wa mwajificho.

Salihina anapopata habari anampa viboko kumi. Jamii hii pia ina nyimbo zinazotumiwa katika mazingira tofauti.

Msimulizi amewahi kusikia kuwa ili kuruhusiwa kuingia mzimuni, lazima mtu aimbe wimbo fulani ndipo mizimu imruhusu kuingia.

Akiwa kando ya msitu, anausikia wimbo huo ukiimbwa na mwanamume, na baada ya muda unajibiwa na mwanamke.

Anaukariri wimbo huo na hatimaye kuuimba kesho yake kabla ya kuingia mzimuni.

Maudhui zaidi katika hadithi ni pamoja na Unafiki, Uzinzi, Ujinga, Migogoro, Jinsia na Ulevi.  

Wahusika: Sifa na Umuhimu

Msimulizi 

Ni mdadisi.

Kina anapopata sifa mpya ya Mzimu wa Kipwerere, lazima aulizie kwa wazee.

Anaulizia sababu ya kuona taa huko usiku, harufu ya tumbaku kutoka huko na sauti za chini kwa chini zinazosikika. 

Ni jasiri.

Badala ya kuogopa kutokana na sifa za Mzimu wa Kipwerere, yeye anataka kujua zaidi kuhusu mzimu huo, hata ikigharimu maisha yake!

Yuko tayari hata kukutana na shetani wa mzimu ana kwa ana!

Ni mpelelezi.

Kila mara ana nia ya kujua kuhusu mzimu unaoogopwa na wanakijiji.

Anaukaribia kila mara na kutafuta mbinu za kuingia huko wakati mmoja ili kujua kilichopo.

Anakaribia na kuujua wimbo unaodaiwa kutumika kama ufunguo.

Hatimaye anaingia msituni akiwa na tochi kuona kilichomo. 

Ni mkakamavu.

Haachi nia yake ya kuwaona shetani wa mzimu.

Licha ya yote anayoambiwa na wazee na imani zinazowaogofya, anashikilia msimamo wa kuingia humo hadi anapotimiza azma yake.

Ni mwenye akili pevu.

Anawaza kwa haraka na kutekeleza mawazo.

Anaposikia watu wakija mzimuni, anazima tochi na kujificha chini ya kitanda.

Anajua hawawezi kutarajia yuko humo.

Bishoo anapoelekea kuwasha taa, anatokeza na kupiga ukemi, akijua wazi atawashtua.

 Umuhimu wa Msimulizi 

Ni kielelzo cha ujasiri na umuhimu wake katika jamii.

Anadhihirisha migogoro kati ya watoto na wazee hasa kuhusiana na masuala ya utamaduni.

Kupitia kwake, mchango wa watoto katika kujenga na kuboresha jamii unadhihirika.

Anadhihirisha umuhimu wa upelelezi katika kuwafichua wahalifu.

Salihina 

Ni mnafiki.

Anajitia uzuri wa kiuongozi kumbe ni kazi bure.

Anaongoza matambiko ya kijamii na kuwaombea watu Baraka kwa mizimu.

Upande mwingine, analangua mihadarati na kufanya uzinzi kwenye mzimu.

Ni laghai.

Anatumia nafasi yake kama kiongozi kulangua mihadarati.

Anawajaza watu imani ya kuwepo kwa mizimu ili wasiingie msituni, ambamo anaficha shehena za mihadarati. 

Ni dhalimu.

Anawakataza watoto wa kiume na kike kutangamana katika michezo.

Msimulizi anapokezwa viboko kumi bila kuambiwa kosa lake, eti kwa sababu tu alisimama karibu na msichana.

Ni mwenye tamaa.

Tamaa inamsukuma kulangua dawa za kulevya ambazo ni marufuku katika kijiji hiki.

Pia ana tamaa ya kumlaza Bishoo licha ya kujua ana mume. 

Ni mzinzi.

Anakutana na Bishoo msituni ili kupanga mikakati ya ulanguzi.

Zaidi ya hayo, wana ajenda yao ya ‘kusakata rumba’.

Hata wana kitanda mle msituni wanachotumia kutimiza ashiki yao. 

Ni msaliti.

Anasaliti wanakijiji wanaomwamini na kumheshimu kwa kuwaendea kinyume.

Anasaliti utamaduni wa jamii kwa kuutumia kuendeleza uhalifu.

Anamsaliti msimulizi kwa kumpiga bila hatia.

Umuhimu wa Salihina 

Ni kiwakilishi cha uozo uliokithiri katika jamii.

Kupitia kwake, uhalifu unadhihirika na ujanja unaotumiwa kuuendeleza.

Ni kiwakilishi cha mila na itikadi zilizopitwa na wakati na jinsi zinavyoangamiza jamii.

Kupitia kwake, utapeli wa viongozi na watu wanaoaminiwa katika jamii unadhihirika.

Kupitia kwake, mgogoro kati ya watoto na wazee na pia ujadi na usasa unabainika wazi.

Bishoo

Ni laghai.

Anamuaga mumewe kuwa anaenda kumwona mtoto wa jirani ambaye ni mgonjwa, lakini ukweli ni kuwa anaenda kumwona Salihina. 

Ni mjanja.

Anatumia ujanja kulangua dawa za kulevya kwa kudai kuwa ni shughuli za kuwachotea shetani wa mzimu maji.

Ni mzinzi.

Licha ya kuwa ana mume, anahusiana kimapenzi na Salihina kwenye Mzimu wa Kipwerere.

Ni mwoga.

Msimulizi anapochomoka chini ya kitanda na kupiga kelele, anaanguka na kuzirai.

Umuhimu wa Bishoo

Kupitia kwake, uhalifu katika jamii unadhihirika na jinsi unavyoendeshwa.

Ni kiwakilishi cha wanawake na nafasi yao katika kuporomosha jamii.

Kupitia kwake, uozo katika jamii unadhihirika kwa mapana.  

Mbinu za Uandishi.

Tashbihi 

Mzimu wa Kipwerere ukitisha kama samba.

Alikuwa mkubwa…na mkali mithili ya simba jike anayenyonyesha watoto wake.

Kwa bahati mbaya, kuingia kwenye mzimu ule hakukuwa rahisi kama kucheza ngoma ya vanga, mduara au mchiriku.

Nilivaa guo jeupe lililonigubika gubigubi kama maiti.

Nikawa kama dubu tu.Kisha…nikajivurumisha mvunguni mwa kitanda kile chenye matendegu marefu kama miguu ya punda kirongwe.

Nikakaa kimya na kutulia tuli kama ninyolewaye!

Masikio yangu yalivuka kichwa kwa kumwogopa bwana yule, yakawa kama masikio ya sungura aliyeiba mazao shambani.Imani yake kali ilimvuka kama hondowea iliyokatika mpira kwenye mwendo.   

Nilijitokeza mle mvunguni na maguo yangu meupe kama maiti nikaangua mwangwi mkali mfano wa parapanda siku ya kiama.

Maneno yale yalikuwa kama mkuki kwa watu wale wawili niliowashika ugoni.

Istiara

Yaani kile kitendo cha kichaka kile kuitwa mzimu tu kilikuwa homa ya jiji na shetani tosha.

Na hapo…ufike majumbani ambako guo la hofu, hatimaye litakuvuka.

Yakaja kunifika makubwa ya mgeni kuacha chai akanywa masimbi ya chai.

Pia nilitaka nihakikishe kuwa hakuna shetani yeyote kati ya wale wawili, atakayeiona sura yangu…

Semi na Nahau

kukata kiu- kumaliza hamu.

alikuwa mstari wa mbele- alisisitiza zaidi, alikuwa wa kwanza.

Alikataa katakata- alikataa kabisa.

yamepigwa marufuku- yamekataliwa, yameharamishwa. hatua kwa hatua- kwa utaratibu.

Nikaupiga moyo wangu konde- nikajipa ujasiri, nikaamua.

Kufa au kupona- kwa vyovyote vile, lije litakalokuja.ana kwa ana- kuonana kwa macho.

nitatiwa nguvuni- nitakamatwa.kwa mapana na marefu- kwa kiwango kikubwa.

Kinaya

Salihina anampiga msimulizi viboko kumi anapopata habari alisimama karibu na msichana.

Ajabu ni kuwa yeye mwenyewe anashiriki uzinzi, tena na mke wa mtu.

Katika kijiji hiki, yasemekana kuwa kileo chochote aina ya tumbaku ni marufuku na kinaweza hata kugharimu maisha ya mtu.

Kubwia unga na kunywa pombe pia ni makosa ya jinai.

Ajabu ni kuwa kijiji chenyewe bado kinaongoza kwa uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa hizi za kulevya.

Visa vya mizimu na mashetani vinaenea kijijini na kuwatia watu woga.

Kinyume ni kuwa, msimulizi anaingiwa na udadisi badala ya woga, na hata yuko tayari kukutana na mashetani hao ana kwa ana!

Baada ya wale watu wawili wanaoimba kuingia mzimuni, harufu ya tumbaku inatokea.

Msimulizi anasema kuwa hana shauku kwani anajua shetani huvuta sigara.

Ajabu ni kuwa uvutaji huu ni marufuku. Swali kuu ni je, mbona shetani wa mzimu wavute tumbaku hali watu wanakatazwa kuvuta?

Salihina anapoambiwa na Bishoo mpango wa kubeba mihadarati kutoka msituni, anasema kuwa watu watafanya kazi hiyo takatifu kwa uadilifu.

Kinyume ni kuwa si kazi takatifu bali uhalifu na ulaghai. 

Maswali Balagha

Sasa ikiwa kichaka hiki kilipata sifa na cheo cha kuitwa mzimu wenye giza nene ndani, kwa nini kitishe kiasi hicho?

Je, kwa hali hiyo, mtu wa kawaida kichwa mchungwa, ataacha kuogopa?

Kwa nini mashetani wa mzimu wawe wanaogopwa na kila mtu ilhali hawawezi hata kujenga nyumba ya miti na udongo ya kukaa?‘

Rhumba bila kulewa, utalichezaje rhumba?’

Chuku

Woga ambao ukiweza kukupata hapa kwa kujitia hamnazo au kujitia ujabari wa kujipitisha haukuishia kwenye moyo tu, bali ulikuwa woga ulioweza kukutia maradhi hata ya senene,…

Kwa umbile lake hili, ilikuwa yumkini kuamini mle ndani ya kichaka mlikuwa na giza nene kuliko lile giza la kaburini.

Butwaa ambalo kwa hakika liliifanya akili yangu isimame kufikiri kwa muda wa sekunde kadhaa.

Hapo masikio yangu yalivuka kichwa kwa kumwogopa bwana yule…

Taharuki

Mwanzo unatutia hamu ya kujua zaidi.

Tunaambiwa kuwa Mzimu wa Kipwerere unatisha kila mtu, hata wenye ujasiri.

Tunapata hamu ya kujua huu mzimu ni upi, tena kwa nini utishe kiasi hicho.

Msimulizi anapojibiwa kuhusu sifa za shetani, yeye anaingiwa na udadisi na kutafuta upenyu wa kuingia msituni.

Ni hamu kuu kujua iwapo atafanikiwa na iwapo atakutana na shetani hao.

Pia, tuna hamu ya kujua iwapo ni mashetani na mizimu wa kweli walio mle msituni. 

Katika kijiji hiki, tunaambiwa kuwa matumizi ya mihadarati ni marufuku.

Hata hivyo, bado kinaongoza kwa matumizi hayo.

Anayesambaza hajulikani.

Tuna hamu kuu ya kujua anayeshiriki haya. 

Msimulizi anausikia wimbo ukiimba wakati yuko nje ya msitu.

Mwanamume anaanza na kujibiwa na mwanamke.

Tuna hamu kuu ya kujua hawa ni kina nani na wana uhusiano gani na mizimu na mashetani.

Mwishoni pia, tunabaki na maswali kadhaa.

Ni hatua gani ambayo wanachukuliwa Salihina na washirika wake.

Anasema kuwa hayuko peke yake katika hilo.

Anashirikiana na nani? Mumewe Bishoo naye anamchukulia hatua gani, na mengine.

Sadfa

Inasadifu kuwa watoto wanacheza karibu na msitu wanaposikia sauti za chini kwa chini.

Wakati msimulizi yuko kando ya msitu, anawazia jinsi ya kujua wimbo unaosemekana kuwa ufunguo wa kuingia msituni.

Kisadfa, wakati huo huo anausikia ukiimbwa na watu wanaoingia humo baadaye.

Msimulizi hatimaye anafaulu kuingia msituni na kushuhudia yanayotukia humo.

Wakati anapomulikamulika mvunguni mwa kitanda, anausikia wimbo na kujua watu wanakuja.

 Wakati msimulizi akiwa mvunguni mwa kitanda, Bishoo anachukua kiberiti tayari kuwasha taa.

Hili linamlazimisha msimuliza kujitokeza kabla ya kupatikana.Salihina anapotoroka, anakamatwa na tawi la mti kisadfa.

Anafikiri kuwa ni msimulizi aliyemkamata na kuanza kupiga kamsa akimwomba radhi.

Methali

Lisemwalo lipo

Kamba hukatikia pabovu

Nyimbo

Wimbo wa Mzimu wa Kipwerere. Unaimbwa na Salihina na Bishoo kabla ya kuingia msituni.

Unadhihirisha utamaduni wa jamii na pia ulaghai.Wimbo wa kidumbaki anaoimba Salihina wa Rhumba.

Wimbo huu unadhihirisha ashiki yake ya kimapenzi kwa Bishoo.

Koja

Msitu wenyewe ulikuwa wa kichaka kidogo cha miti mseto ikiwemo mibungo, mipera, mipendapendapo, mipo na miti lukuki ya makamo.

Kusini, mashariki, magharibi na kaskazini ya kichaka hiki…

Tabaini

Si mchana si usiku.

Hadithi Ndani ya Hadithi

Hadithi ya Kipwerere, anayesemekana kuwa jamaa wa Bwana Msa aliyepata shetani aliyefichua damu enzi za ujalihiya.

Kisa hiki kinahusiana na Mzimu wa Kipwerere, kwani inaaminika alipozikwa ndipo msitu huo umemea.

Mbinu nyingine ni pamoja na Tashihisi, Utohozi, Kisengerenyuma, Dayolojia, Taswira, Takriri naMdokezo. 

Join our whatsapp group for latest updates

Download Mzimu wa Kipwerere! summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?