Sabina summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Sabina- Winnie Nyaruri Ogenche

Mtiririko

Ni Jumapili ya mwisho kabla ya mtihani wa kitaifa kuanza. Sabina anawazia mtihani pamoja na ufadhili wa shule ya bweni unaomsubiri iwapo atafaulu. Hata hivyo, anashangaa itakuwaje akifeli. Anakumbuka maneno ya mwalimu kuwa mizizi ya elimu ni michungu ila matunda ni matamu. Anagutushwa na wito wa Yunuke, na hapo anainuka haraka. Anagundua jua linatua na hivyo kuharakisha kuendea ng’ombe malishoni kuja kuwakama. Anawafunga zizini na kuanza kuandaa chajio. Jumatatu, anaamka na kukama ng’ombe, kupeleka kisonzo shambani na kwenda sokoni kuuza maziwa. Anatoka saa tatu unusu na kuelekea shuleni kwa maandalizi ya mtihani. 

Sabina ana umri wa miaka kumi na minne, japo anaonekana mkubwa kutokana na dhiki. Mamake, Nyaboke, alijifungua akiwa kidato cha pili na kukatiza masomo. Janadume lililomtia uja uzito lilimtelekeza. Sabina anaanza shule katika darasa la kwanza akiwa na miaka saba na anapata matokeo bora. Akiwa darasa la nne, mamake anaugua ugonjwa wa ajabu unaoanza na kipele shingoni. Kinapozidi anapelekwa kwa mganga anayedai kipele hicho ni cha laana. Baadhi ya watu wanasema ni ya babake kwa sababu ya kujifungua nyumbani na kukataa posa ya wanaume, huku wengine wakimshuku Ombati, nduguye kwa kukosa mahari ya dadake. Hatimaye Nyaboke anafariki. 

Sabina anatia bidii masomoni ili kuwafaidi bibi na babu, lakini hao wanafariki akiwa darasa la tano baada ya kujifungia ndani ya nyumba na jiko la makaa likiwaka. Watu wanaanza kuambaa familia yao, na analazimika kuishi kwa mjomba wake, Ombati, na mkewe, Yunuke. Hapa anatwikwa majukumu kamakukama ng’ombe, kuzoa kisonzo, kuuza maziwa, kuwapeleka ng’ombe malishoni na majukumu mengine ya nyumba. Hata binamu zake hawamsaidii bali kumwongezea dhiki, ila Mike anayeandamana naye malishoni hata baada ya kuadhibiwa. Licha ya kazi zote, bado anaibuka wa kwanza darasani kwao. 

Siku ya maandalizi, Sabina anafika amechelewa na kujiunga na wenzake. Mwalimu anawaambia kuwa wanafaa kuwa kwenye chumba cha mtihani saa mbili kasorobo. Atakayechelewa hataruhusiwa kufanya  mtihani. Sabina anatikisa kichwa kama kwa kupinga. Mwalimu mkuu anamwita ofisini na kumwuliza sababu ya kufanya hivyo na pia kuchelewa. Anamweleza majukumu aliyo nayo, na hapo mwalimu anamwandikia barua fulani. Anaporudi nyumbani, Yunuke anamvamia kwani saa mbili zimepita tangu wanafunzi wengine watoke shule. Anamweleza ni barua ilimkawisha huku akijiopoa na kutoroka. Yunuke anamtukana, akidhani ni barua kutoka kwa mwanamume. 

Jumanne saa mbili kasorobo, Sabina yuko ukumbini akisubiri mtihani, hayuko sokoni Itumbe kuuza maziwa. Anafanya mitihani ya siku hiyo kwa furaha na tumaini. Anapofika nyumbani, Yunuka anamkabili kwa kutouza maziwa, lakini anasema aliyauza na kumkabidhi pesa. Yunuke anamtuma shambani kutapakaza kisonzo. Anaporudi anajaribu kusoma kwa mwanga wa kibatari, lakini Yunuke anakizima akimkashifu kwa matusi. 

Ombati anafika nyumbani kwa likizo ya Disemba ili kumwandaa Mike kwa ajili ya shule ya upili, na kumwoza Sabina. Matangazo ya mtihani yakifanywa, Sabina yuko shambani naye Ombati ana mkutano na wanaomwoa Sabina. Maripota wanapofika wakiimba nyimba za kumsifu Sabina, hawaelewi yanayotukia. Wanapomwulizia Ombati mwanawe aliyefanya vyema, anamwita Mike, lakini wanasema wanamtaka Sabina.

Sabina anafika kutoka shambani na rinda lake kuukuu. Wanambeba juu juu na kumshangilia. Ombati anawafurusha waliokuja kumwoa Sabina na mifugo wao, huku akijiunga naye kuhojiwa. Anampa hongera na kuwakaribisha kwa vyakula. Sabina anakumbuka ugumu wa maisha yake, na shughuli zilizomwandama wakati wa mtihani wa kitaifa. Anakumbuka hisani ya mwalimu kuwaandikia wapishi barua ili Sabina awaletee maziwa badala ya kuyauza sokoni. Anauona huo kama mwanzo wa ufanisi wake. Yunuke na Ombati hawataki kumwacha. Mvua inawatawanya na habari za ufanisi wake zinabaki mada kijijini kwa takriban wiki nzima.  

Ufaafu wa Anwani ‘Sabina’  

Mada hii inatokana na jina la mhusika mkuu wa hadithi hii. Ndiye kitovu cha hadithi yenyewe na matukio yote katika kisa hiki yanamzunguka yeye. Inahusu maisha ya Sabina kwa jumla tangu kuzaliwa kwake, kulelewa na mamake Nyaboke hadi anapofariki, kuachwa tena na babu na bibi na hatimaye kudondokea kwenye familia ya Ombati na Yunuke. Huku anapitia dhiki tele na kujikakamua hadi anapofanikiwa hatimaye.  

Dhamira ya mwandishi

Anasawiri matatizo yanayowakumba watoto yatima katika jamii kwa kukosa mteteziKuonyesha jamii inavyomdhulumu mwanamke na jinsi yake kujiendeleza ili kushinda udhalimu huu. Anadhihirisha umuhimu wa bidii katika mambo tufanyayo na matunda yake. Kuwaonya walezi wanaowadhulumu watoto yatima, kwani watoto hao wanaweza kuwa na vipaji vya kipekee vinavyoweza hata kuwafaidi walezi hao.Anadhihirisha nafasi ya elimu katika kujenga na kuendeleza jamii. 

Maudhui

Elimu

Jamii hii ina imani katika usemi wa kuwa elimu ndio ngao ya maisha. Kila mzazi/mlezi anatia bidii kuvumisha elimu katika maisha ya mwanawe. Wanaamini kuwa mwenye elimu atapata mafanikio katika maisha.Nyaboke, mamake Sabina, anasoma hadi kidato cha pili anapoambulia uja uzito. Analazimika kuacha masomo kuingilia ulezi. Hatua hii inawakera wazazi wake na kuwakatiza tamaa, kwani waliamini atasoma ili awe mtu wa maana maishani.Sabina anadhihirisha nafasi ya elimu kwa kutia bidii za mchwa katika masomo. Yuko katika darasa la nane akijiandalia mtihani wa mwisho. Licha ya kazi nyingi anazofanya, bado analazimika kufika shuleni na kuendelea na masomo. Kwa sasa, anajiandalia mtihani, akijua kwamba akifaulu atapata ufadhili katika shule ya upili ya bweni. Sabina anaanza masomo katika shule ya msingi ya Utubora katika darasa la kwanza akiwa na miaka saba kwa sababu ya ushupavu wake. Anaongoza katika darasa lake kwenye mitihani yote. Licha ya kufiwa na mamake, bibi na babu yake, halegezi kamba masomoni. Analazimika kuishi na Yunuke, mke wa mjomba ambaye anamtesa lakini anazidi kufana masomoni.Binamu zake Sabina wanasoma katika shule ya upili ya Golden Heart. Wanaonana na Sabina wakati wa likizo tu. Ombati na Yunuke wanaona juhudi za Sabina kuwa kazi bure, lakini hakati tamaa. Nia yake kuu ni kujiunga na shule ya upili ya bweni.Mwalimu mkuu anamsaidia Sabina kwa kuwaandikia wapishi barua wapokee maziwa yake. Anapata nafasi ya kufika katika mtihani kwa wakati na kuufanya bila tatizo. Matokeo yanapokuja, ndiye wa nane bora nchini. Ombati na Yunuke hawataki kujitenga naye wakati maripota wanapokuja kuwahoji. Kijiji kizima kinajaa habari za ufanisi wake kwa takriban wiki nzima. 

Dhuluma/Udhalimu

Sabina anapitia dhuluma kadhaa katika maisha yake. Hapati muda wa kubarizi. Japo anasubiri mtihani wa kitaifa, analimbikizwa kazi nyingi na Yunuke. Anapoketi chini ya mparachichi kupumzika, anamwita kwa fujo. Analazimika kuinuka haraka kwenda malishoni kuwaleta ng’ombe ili awakame kisha kuanzashughuli ya kuandaa chajio. Asubuhi siku inayofuata, analazimika kuamka mapema, kuwakama ng’ombe, kupeleka kisonzo shambani na kuuza maziwa. Anafika shuleni saa tatu u nusu. Udhalimu unamkumba Sabina tangu akiwa darasa la tano, umri wa miaka kumi na mmoja anapoanza kuishi kwa Ombati. Hatimaye anazoea majukumu yote. Hata binamu zake hawamsaidii wanapokuja likizo bali kumwongezea dhiki. Lao ni kukaa kubarizi huku akitekeleza majukumu yote, lao kumtumatuma. Mike tu ndiye anamsaidia. Sabina anapochelewa kwa mwalimu mkuu, Yunuke anamvamia japo anamwambia ni barua imemchelewsha. Anamtukana akidhani ni barua ya mwanamume na kumcharaza bakora. Hata siku za mtihani, bado anatakiwa kwenda kuuza maziwa kabla ya kwenda kwenye mtihani. Anaporejea siku ya kwanza, Yunuke anamkabili kuhusiana na maziwa, lakini anajiokoa kwa kumpa hela alizoyauza, lakini mara hii shuleni kwa hisani ya mwalimu mkuu.  Ombati anapanga kumwoza Sabina katika umri mchanga ili kupata mahari aliyokosa kwa mamake. Anapokuja likizo ya Disemba, anakutana na wakwe watarajiwa. Bado udhalimu unaendelea, kwani wakati huu Sabina yuko shambani akitapakaza kisonzo. Hata hana habari ya matokeo na ufanisi wake.

Utamaduni

Jamii inategemea ufgaji na kilimo ili kujiendeleza kimaisha. Sabina analazimika kukama ng’ombe wa mjomba wake, kuwapeleka malishoni na kuuza maziwa sokoni kabla ya kwenda shule. Pia anatakiwa kutapakaza kisonzo shambani. Hata maripota wanapofika kumhoji, yuko kazini kwenye shamba.Anarejea bado akiwa na harufu ya samadi. Kuna imani katika uganga na laana. Nyaboke anapopatwa na kipele shingoni, anapelekwa kwa mganga anayesema kuwa kimeletwa na laana. Hasemi ilikotoka. Watu wanakisia ni babake aliyemlaani kwa kuzaa kabla ya ndoa na kukataa wanaume wanaomposa wote. Wengine wanaamini ni Ombati kwa kukosa mahari yake. Hata Nyaboke anapofariki na hatimaye wazazi wake kumfuata, watu wanaanza kuambaa familia hiyo wakiamini wamelaaniwa.Tamaduni za ndoa pia zimesawiriwa. Nyaboke anakataa posa ya wanaume wanaomtaka. Wanawake wanachukuliwa kama raslimali za kuzalisha mahari. Ombati anashukiwa kumlaani Nyaboke kwa kumkosesha mahari anapokataa kuolewa. Isitoshe, Ombati anaamua kumwoza Sabina baada ya mtihani kutokana na visingizio vya Yunuke vya uzinzi. Wakwezewatarajiwa wanakuja na kuleta mifugo, huku wakiandaa sherehe za kumlaki bi arusi wao. Wameandaa mapochopocho lakini yanakatizwa na mjo wa maripota. 

Usaliti

Nyaboke anawasaliti wazazi wake kwa kuambulia uja uzito akiwa katika kidato cha pili. Wamejitolea kwa kila hali kumsomesha huku wakiwa na matumaini yake kuwafaa, yanayowatoka mara anapohimili nakukatiza masomo. ‘Babake’ Sabina naye anamsaliti Nyaboke kwa kumtelekeza baada ya kumpa uja uzito.Yunuke anamsaliti Sabina. Badala ya kumtunza licha ya kujua ni yatima, anamtesa na kumdhalilisha.Anamlazimisha kukama ng’ombe, kupeleka kisonzo shambani na kuuza maziwa kabla ya kwenda shule. Anamfanyisha pia kazi zote za nyumba. Anapojaribu kusoma usiku, anamzimia kibatari anachotumia. Anapofanya makosa madogomadogo, anamcharaza bila huruma na pia kumtukana vibaya, kila mara akimkumbusha kuwa yeye ni ‘kiokote’.Ombati anamsaliti Sabina na Nyaboke pia. Kama mjomba, ni jukumu lake kumlinda na kumtunza Sabina. Badala yake, hafanyi lolote la kumfaa. Anaambia mwalimu mkuu kuwa nyumbani hakuna kazi zozote hali Sabina anatumikishwa sana. Anapanga njama ya kumwoza ili kufidia mahari aliyokosa kutoka kwa mamake, Nyaboke. Huu ni usaliti kwa Nyaboke, ambaye ni dadake. Anafaa kumtunzia mwana.  Binamu zake Sabina pia wanamsaliti. Wanapokuja likizo, wanamzidishia majukumu badala ya kumsaidia. Wanakaa tu na kubarizi huku wakimtumatuma, isipokuwa Mike anayejitolea kwenda naye machungani hata baada ya kuadhibiwa. 

Nafasi ya Mwanamke

Anachukuliwa kama chombo cha kumstarehesha mwanamume. Nyaboke anatiwa uja uzito na janadume ambalo baadaye linamtema na kumwachia mzigo wa malezi peke yake. Mwanamke anachukuliwa kama raslimali ya kuleta mapato kupitia kwa mahari. Nyaboke anapougua kipele kinachosemekana kuwa laana, Ombati anakisiwa kumlaani kwa kumkosesha mahari baada ya kukataa kuolewa. Ili kufidia mahari hayo, anaamua kumwoza bintiye, Sabina, baada ya kukamilisha mtihani. Tayari mifugo wameletwa na sherehe kuandaliwa, lakini zinakatizwa na mjo wa maripota baada ya Sabina kufaulu katika mtihani.Mwanamke pia anachukuliwa kuwa mlinzi wa boma. Ombati anayoyomea mjini na kumwacha mkewe, Yunuke, nyumbani kuwa mlinzi wa mali yao. Yunuke naye anamtumia Sabina kutekeleza majukumu yote ya nyumba kabla ya kumruhusu kwenda shule.  

Ndoa

Ndoa kuu katika hadithi ni ya Ombati na Yunuke, ambao wamejaliwa wana, Mike na wengine. Wawili hawa wanaishi kwa maelewano kama wanandoa kwa kiwango cha kuridhisha. Ombati anachuma riziki kama mume, huku Yunuke akibaki nyumbani kutunza boma kama mke wa boma hilo.Nyaboke anaambulia uja uzito nje ya ndoa na kukataliwa na janadume lililomtia mimba. Hapo anapoteza imani na ndoa na kukataa posa za wanaume wote wanaokuja kumwomba awe mke wao. Hatimaye anafariki bila kuolewa.Ombati anapanga ndoa ya mapema ili kujinufaisha kwa Sabina. Ndoa hii inachukuliwa kama kitega uchumi, ili ajipatie mifugo na hela. Sherehe za kumchukua bi arusi tayari zimepamba lakini zinatibuka maripota wanapokuja na taarifa za kufaulu kwake katika mtihani. 

Kifo/Mauti

Nyaboke anaaga dunia baada ya kuugua kipele shingoni, ambacho kinatunga usaha na kuvimba. Juhudi za mganga wa kijijini anayepelekwa kwake hazizai matunda. Kifo chake ni pigo kubwa kwa Sabina, ambaye anabaki yatima. Anahisi kama amepoteza baba na mama baada ya ‘babake’ kutoweka. Babu na bibi wa Sabina wanafariki kutokana na hewa ya sumu inayotokana na jiko la makaa. Wanajifungia ndani ya nyumba huku jiko likiwaka pembeni, na kupatikana asubuhi wakiwa wafu. Hili ni pigo lingine kwa Sabina, kwani ndio anaotegemea baada ya mamake kufariki. Anadondokea kwa mjombake anapokumbana na dhiki tele.Maudhui mengine katika kazi ni pamoja na Mabadiliko, Migogoro, Utabaka, Familia, Malezi, Ukatili, Tamaa, Uzinzi na Utu.  

Wahusika: Sifa na Umuhimu

Sabina 

Ni mwenye bidii.

Anatia bidii katika masomo na pia katika kazi za nyumbani anazofanya.

Kabla yakwenda shuleni, anatakiwa kukama ng’ombe, kutapakaza kisonzo shambani na kuuza maziwa.

Licha ya yote haya, anafaulu vizuri katika masomo yake.

Ni mtiifu.

Anafuata maagizo ya Yunuke na kumtii bila maswali.

Anatapakaza kisonzo shambani anavyoagizwa na kukama ng’ombe na kuuza maziwa kabla ya kwenda shule.

Anapoitwa na Yunuke, anatoka alipo upesi na kuelekea malishoni kuwaleta mifugo. 

Ni mkakamavu.

Anajitolea kwa kila hali kutimiza azma yake katika elimu.

Baada ya kumaliza kazi zake, anatumia mwanga wa kibatari kusoma japo Yunuke anakizima.

Licha ya kazi zote, bado anafaulu katika masomo yake. 

Ni mwerevu.

Akiwa katika umri wa miaka saba, anaungana na wenzake wanaotoka chekechea kwa wepesi wake wa kuelewa mambo.

Baada ya matokeo kutoka, ndiye mwanafunzi wa nane bora nchini. 

Ni mwenye maono.

Hata baada ya mamamke kufariki, anaazimia kutia bidii ili kuwasaidia babu na bibi.

Azma yake kuu katika siku za usoni ni kuwa daktari.  

Umuhimu wa Sabina 

Ni kiwakilishi cha dhiki ambayo watoto yatima hupitia katika maisha baada ya kuachwa na wazazi wao.

Kupitia kwake, umuhimu wa bidii na matunda yake yanabainika. 

Ametumika kuonyesha umuhimu wa elimu na nafasi yake katika kujenga jamii.

Kupitia kwake, nafasi ya wazazi katika malezi na maisha ya wanao inadhihirika.

Yunuke

Ni katili.

Anamtumikisha Sabina bila huruma.

Anamlazimisha kukama ng’ombe, kupeleka kisonzo shambani na kuuza maziwa kabla ya kwenda shule.

Anapokawia kwenye ofisi ya mwalimu mkuu, anamvamia na kumtandika kwa bakora. 

Ni mpyaro.

Kinywa chake kinadondoka kila aina ya matusi bila haya.

Anamwambia Sabina anaandama wanaume kama mamake na anajua matokeo yake.

Anamwita mjalaana na baradhuli.

Kila mara anamkumbusha kwamba yeye ni ‘kiokote’.

Ni dhalimu.

Anatumia uyatima wa Sabina kumtumikisha nyumbani.

Sabina anafanya majukumu yote ya nyumba huku yeye ameketi tu na kufurisha shingo.

Hata wanawe wanapokuja likizo, hawamsaidii bali kumzidishia dhiki. 

Ni mfitini.

Anamwambia mumewe kuw Sabina ameanza kuwa na tabia za uzinzi na kumfanya kuandaa mipango ya kumwoza katika umri mchanga. 

Umuhimu wa Yunuke

Kupitia kwake, udhalimu unaotendewa matoto mayatima katika jamii unadhihirika.

Ni kiwakilishi cha nafasi ya mwanamke katika jamii. 

Anadhihirisha nafasi ya ndoa na umuhimu wake katika kujenga na kuendeleza jamii

Kupitia kwake, watesi wa wasiojiweza wanapata funzo kuwa wanaowatesa wanaweza kufanikiwa na kuwafaa watesi hao.

Ombati 

Ni mwenye tamaa.

Ananuia kujinufaisha kutoka kwa dadake kupitia kwa mahari yake.

Anapoyakosa, anaamua kutumia bintiye, Sabina, kwa kumwoza baada ya darasa la nane ili kupata mifugo. 

Ni mtamaduni. Anaendeleza mifumo ya kijamii kama vile ubidhaaishaji wa wanawake.

Anataka kupata mahari kupitia kwa Nyaboke na anapoyakosa, anaamua kumwoza bintiye, Sabina, katika umri mchanga na kumwandalia sherehe.

Anasemekana kumlaani Nyaboke kwa kumkosesha mahari. 

Ni kigeugeu.

Maripota wanapofika kumhoji Sabina, anaungana naye huku akijisifia jinsi alivyomlea na alivyo mwerevu, licha ya kuwa awali anamtelekeza.

Anawafukuza waliokuja kumposa Sabina na mifugo wao. 

Ni mwongo/mzandiki/mnafiki.

Anamhadaa mwalimu mkuu kuwa Sabina anapata muda wa kutosha kujiandaa kwa ajili ya mtihani.

Anadanganya kuwa Sabina anapenda kazi za shambani hali analazimishwa. 

Umuhimu wa Ombati 

Anadhihirisha nafasi ya ndoa katika kujenga na kuendeleza jamii.

Kupitia kwake, tunaonyeshwa hali ya utamaduni na nafasi yake katika jamii.

Ni kiwakilishi cha tamaa katika jamii na madhara yake. 

Anadhihirisha nafasi ya mbaidiko wa kijinsia katika jamii.

Nyaboke

Ni mwenye bidii.

Baada ya kujifungua, anaacha shule na kujikaza kumtunza mwanawe.

Anaweza kumlisha na hata kumpeleka shule bila matatizo.

Ni mzinzi.

Anaachia masomo katika kidato cha pili baada ya kuambulia uja uzito.

Ni mwenye msimamo thabiti.

Anapoachwa na babake Sabina, anakosa imani na wanaume na kukataa posa zote anazoletewa na hakuna anayeweza kubadili msimamo wake.

Ni mlezi mwema.

Anamkimu mwanawe peke yake. Anamlisha, kumvisha na hata kumpeleka shule.

Umuhimu wa Nyaboke

Kupitia kwake, changamoto zinazowakumba vijana katika juhudi za kuandama elimu zinadhihirika.

Ni kiwakilishi cha nafasi ya mwanamke katika jamii na matatizo yanayomkumba.

Ni kielelzo ch malezi bora kwa wazazi hata kama kwa taabu kubwa.

Kupitia kwake, masuala ya kitamaduni kama laana, dhuluma na ubidhaaishaji wa wanawake yanadhihirika.

Mwalimu Mkuu

Ni mwenye makini.

Anapohutubu ukumbini, anaweza kubaini Sabina anavyosumbuka akisikia kuhusu sheria za kuchelewa, licha ya kuwa kuna wanafunzi wengi darasani.

Ni mwajibikaji.

Anatekeleza wajibu wake katika shule.

Anawapa wanafunzi maagizo ya mtihani.

Anamwita Sabina kujua linalomsumbua.

Pia, anafuatilia kujua iwapo anapata nafasi ya kudurusu kutoka kwa Ombati.  

Ni mwenye utu.

Anamsaidia Sabina kuwahi chumba cha mtihani kwa kumwandikia barua alete maziwa shuleni badala ya kwenda kuyauza sokoni asubuhi.

Umuhimu Wake

Ni kiwakilishi cha nafasi ya walimu katika maisha ya wanafunzi wao.

Anawakilisha utu na ubinadamu katika jamii na umuhimu wake katika kuiendeleza.

Kupitia kwake, maudhui ya elimu yanadhihirika. 

Mbinu za Uandishi

Tashbihi 

Alianza kwa kuachia tabasamu pana mithili ya msafiri aliyefika salama.

Maswali haya yalimliza yakamwacha akisinasina kama mgonjwa wa mafua.Hakuthubutu kumwendea

…kwani alijua kufanya hivyo ni kama kujipeleka kinywani mwa simba mwenye njaa.

Yunuke alikuwa amejikunjia pembeni huku amefurisha shingo kama kiboko.

Alikimbia kama mwehu hadi nyumbani,Aligutuka kama mtu aliyebumburushwa kutoka ndotoni…

Sabina alinyanyuka mara moja kama askari kanzu.

Miguu ya Sabina ilikufa ganzi, akabaki amesimama kama kisiki.

Kila mtu alijua kuwa kuitwa ofisini mwa mwalimu mkuu kulikuwa sawa na sungura kuitwa pangoni mwa simba.

Semi

Alipigwa na butwaa- alishangaa na kuduwaa.

walikata tamaa- walikosa matumaini.

alijifunga kibwebwe- alitia bidii kutekeleza.

akatangulia mbele za haki- akafariki, akafa.

kulaza damu- kuzembea, kukaa bila kufanya chochote.

haukutiwa doa- haukuathiriwa, haukuwekwa kasoro yoyote.

ilikufa ganzi- ilipoteza hisia.

najipalia makaa- najiletea balaa.

kuchana mbuga- kukimbia,kutoroka. 

nyota ya jaha- bahati nzuri.

Kinaya

Sabina anapowazia kuhusu mtihani, kwanza anaachia tabasamu pana, kisha baada ya hayo, machozi yanaanza kumtiririka.

Mwalimu mkuu anasema kuwa Ombati alimwambia wanampa Sabina wakati wa kutosha kujiandalia mtihani.

Ukweli ni kuwa hapati muda huo.

Analimbikizwa kazi zote nyumbani na hata anapothubutu kudurusu, Yunuke anamzimia kibatari.

Sabina anaporudi nyumbani baada ya siku ya kwanza ya mtihani, Yunuke anamuuliza kama aliona kuraukia shule ndio muhimu kuliko kuuza maziwa.

Kwake, kuuza maziwa ni muhimu kuliko shule!

Sabina anapodurusu, Yunuke anamzimia kibatari huku akisema hana akili za masomo.

Ajabu ni kuwa Sabina mwenyewe anaibuka nambari moja darasani.

Ombati anasema kuwa anashukuru kuwa bintiye amefaulu masomoni.

Ajabu ni kuwa awali, hamchukulii kama bintiye.

Anadai kuwa anapenda kazi za shamba, hali ni kulazimishwa analazimishwa.

Yunuke na Ombati hawataki kumwachilia Sabina hata kwa sekunde baada yake kufaulu katika mtihani.

Awali, hawana shughuli naye hata kidogo bali umuhimu wake mkuu ni kutumika nyumbani.

Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi

Huku Sabina akiwazia mtihani anaosubiri, tunarejeshwa kwa asili yake, ambaye ni mwana wa pekee wa Nyaboke, anayempata akiwa katika kidato cha pili.

Anaachia masomo hapo na kuanza kumlea hadi anapofariki kutokana na kipele shingoni.

Baada ya mama kufariki, Sabina anatia bidii ili kuwasaidia bibi na babu akikua.

Wawili hao pia wanafariki kutokana na hewa ya sumu kutoka kwenye jiko la makaa.

Hatimaye anaishia kwa familia ya Ombati, mjomba wake.

Sabina anatwikwa mzigo wa kutekeleza majukumu yote ya nyumba na anayatekeleza hadi anapozoea.

Binamu zake wakija likizo kutoka shuleni hawamsaidii ila Mike tu.

Bado anaendelea na ubabe wake katika masomo licha ya ujakazi huo.

Wakati akihojiwa, Sabina anakumbuka jinsi Yunuke alivyoishi kumkumbusha kuwa yeye ni ‘kiokote’ kila mara.

Pia, anakumbuka hisani ya mwalimu mkuu ya kumwandikia barua awapelekee wapishi shuleni maziwa badala ya kuyauza, iliyomsaidia kufanikiwa katika mtihani.

Maswali Balagha

Lakini, angefeli je?

Basi kapitia wapi shetani kuchukua roho zao?

Nitafanyaje nifike shuleni kabla ya saa mbili asubuhi?

Kitanifika nini nikifika katika ukumbi huu baada ya mtihani kuanza?

“Uliona kuraukia shule ni muhimu kuliko kuuza maziwa,eh?” 

 “Tangu lini ukaanza kunihadaa…”

TaashiraSabina alipata nafasi ya kumtapikia mwalimu mkuu masaibu yake…(neno ‘kumtapikia’ lina maana ya kumwambia au kumweleza)

Uvundo ulimtoka mwanamke huyo. (‘Uvundo’ hapa lina maana ya lugha chafu, matusi)IstiaraKichwa chake kidogo kilikuwa uwanja wa mawazo ainati…

Chanzo cha laana hiyo kilibaki kuwa fumbo.

Ripoti za Yunuke kwa mumewe kuhusu Sabina alivyobadilika kuwa mumunye la kuharibikia ukubwani…

Methali

Mtaka cha mvunguni sharti ainame.

Kulea mimba si kazi, kazi ni kulea mwana.

Ganga ganga za mganga humwacha mgonjwa na matumaini.

Mtoto wa nyoka ni nyoka.Kuwa mumunye kuharibikia ukubwani.

Tashihisi

Alipigwa na butwaa alipouona wekundu wa jua ukimezwa na vilima vya magharibi.

Alikimbia…akavaa sare yake iliyoshiba viraka vya kila rangi…

Dunia iliamua kumnyesha shubiri pindi tu alipozaliwa. Alikizima kibatari kile na giza kuu likaivaa nyumba.

Chuku

Nyumbani, Yunuke alikuwa amechemka kwa hasira.Kilio cha kwikwi kilimtoka na kuwafanya hata ng’ombe kumsikitikia.

Taharuki

Mwanzo wa hadithi unaibua maswali mengi.

Tunaambiwa kuwa mtihani wa kitaifa unaelekea kuanza, naye Sabina ana hisia mseto na mawazo mengi.

Tunataka kufahamu sababu ya haya yote, ambayo yanatanzuka polepole.

Nyaboke anafariki kutokana na kipele ambacho mganga anasema kuwa kimetokana na laana.

Tunabaki na maswali mengi.

Je, ni kweli kipele hicho kilitokana na laana?

Na ni ya nani?

Ni ya nduguye Ombati au wazazi wake? 

Sabina anaitwa na mwalimu mkuu na kukabidhiwa barua, ambayo hatuambiwi ni ya nini.

Keshoye, yuko miongoni mwa wanafunzi walioketi kwa wakati kusubiri mtihani.

Anaporudi nyumbani, anamkabidhi Yunuke pesa za maziwa na ndoo, japo Yunuke aliambiwa hakuonekana sokoni.

Tunapata jibu hili mwishoni, Sabina anapokumbuka hisani ya mwalimu ya kumwandikia barua apelekee wapishi maziwa badala ya kuyauza sokoni. 

Sadfa

Wakati matangazo ya mtihani yanapofanywa, Sabina yuko shambani.

Familia nzima nayo iko katika harakati za kuandaa mapochopocho kwa ajili ya harusi ya Sabina.

Hivyo, hakuna anayepata taarifa za kufaulu kwa Sabina.

Wakati Ombati na wakwe watarajiwa wa Sabina wanasherehekea ndani ya nyumba, maripota wanawasili na umati ukimwimbia sifa Sabina.

Wote wanashindwa kufahamu kinachoendelea.

Ripota mmoja anamwulizia Ombati mwanawe naye anamwita Mike.

Mwalimu mkuu anaingilia kati kumwuliza aliko Sabina.

Kabla ya kujibu, wakati huo huo anafika Sabina na rinda kuukuu huku harufu ya samadi bado imemtapakaa.

Uzungumzi Nafsia

Nitafanyaje nifike shuleni kabla ya saa mbili asubuhi?

Kitanifika nini nikifika katika ukumbi huu baada ya mtihani kuanza?

Jazanda

Baada ya sherehe na shmra shamra za ushindi wa Sabina, mvua kubwa inaanguka na kuwatawanya watu.

Mvua ni kiwakilishi cha baraka.

Mbinu nyingine ni pamoja na Nidaa, Utohozi, Mdokezo, Dayolojia na Koja.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Sabina summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?