Ahadi ni Deni summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Ahadi ni Deni- Rayya Timammy

Mtiririko

Fadhumo anajiunga na shule nzuri ya upili.

Anapelekwa na babake mjini na kumnunulia kila anachohitaji.

Wanaagana baada ya Fadhumo kumsisitizia atatia bidii na kufaulu.

Babake anamuaga akisema anarudi kwa raha akijua atatia bidii kwa ajili yake mwenyewe na familia.

Yanaondokea kuwa maneno ya mwisho ya babake.

Wanapanga akae kwa binamu ya babake mjini kupunguza gharama.

Mwishoni mwa muhula wa tatu, babake anaaga kwa ajali.

Kabla ya mwaka wa pili kufika katikati, mamake naye anaaga.

Fadhumo anatamatisha muhula wa pili tu.

Anaacha shule kuwa mlezi wa nduguze kama mwanambee.

Anatafuta jamaa wa kumsaidia.

Mjombake anakubali kumlipia kakake karo.

Jamaa mwingine anataka kumsaidia ila Fadhumo awe kimada wake, lakini anakataa.

Anaolewa na Adan, ambaye anaahidi kuwakimu nduguze.

Anajiahidi kuwa atatamatisha masomo siku moja.

Baada ya miaka sita, anajaliwa wana watatu na kuona haja ya kurejea masomoni.

Anamkumbusha Adan ahadi yake kumsaidia kusoma.

Kiu yake ya elimu iko juu sana.

Adan alidhani ni utoto tu, na anampenda mkewe ambaye anampa furaha katika maisha.

Yuko tayari kutimiza.Anapata mwalimu wa kumfundisha nyumbani bila kuchelewa.

Anafanya mtihani na kupata alama C-.

Anajiunga na koleji ya kufunza watoto wadogo.

Anapata astashahada na kupata kibarua cha kufundisha.

Anaazimia kusomea stashahada.

Watu wanaanza kumtia maneno kuwa mkewe hafai kusoma wala kwenda kazini.

Anayemwudhi zaidi ni mjomba anyetuma ujumbe kuwa anataka kumwona.

Anapoenda, anamwambia kwamba mambo ya mkewe kusoma hataki kuyasikia, kwani atakuwa mjeuri na huenda akamtoroka na hao walimu wake au wanafunzi wenzake.

Anampenda na kumheshimu mjomba lakini hili hawezi kuridhia.

Anajua mkewe hana nia mbaya na yuko tayari kumsomesha hadi atakapo.

Anamtazama njomba kwa huruma na kuondoka, akijua uamuzi moyoni.  

Ufaafu wa Anwani ‘Ahadi ni Deni’

Unapotoa ahadi kwa mtu, umejiweka katika deni ambalo utalipa kwa kutimiza ahadi uliyotoa.

Fadhumo anatoa ahadi kwa babake kuwa atasoma kwa bidii kwa ajili ya kuboresha maisha yake mwenyewe na ya familia wanapoagana mjini.

Mwishoni mwa muhula wa kwanza, babake hata hivyo, anafariki katika ajali ya barabarani.

Mamake anapofariki pia, analazimika kuacha shule kukidhi mahitaji ya nduguze.

Fadhumo anakataa rai ya jamaa anayemtaka kuwa kimada ili aweze kumsaidia na wadogo zake.

Anakubaliwa kuolewa na Adan ili awakidhi ndugu zake.

Hata hivyo, moyoni anajiambia kuwa hata yeye ataandama elimu.

Yuko tayari kutimiza ahadi yake kwa babake, hata ikipita miaka mingapi.

Baada ya kujaliwa watoto watatu baada ya miaka sita kwenye ndoa, anaona muda umefika.

Anamkumbusha mumewe alipomwambia kuwa ana hamu ya kusoma, na kuwa hamu hiyo haijamtoka.

Adan alifikiri kwamba ni utoto na hamu hiyo itaisha, lakini Fadhumo anamkumbusha yalikuwa maagano yake na babake, lazima alipe deni la ahadi aliyotoa.

Adan analazimika pia kutimiza ahadi yake kwa Fadhumo.

Anawakimu nduguze na kuwapeleka shule baada ya kumwoa Fadhumo.

Anapopata hamu ya kuendelea na elimu, yuko tayari kumsaidia kwa kila hali, ili kutimiza ahadi aliyompa.

Fadhumo anaanza masomo licha ya kuwa miaka imesonga.

Licha ya changamoto tele anazopitia, anatia bidii.

Anapata mwalimu wa kumfunza nyumbani ambaye wanashirikiana kwa karibu, hadi anapopata alama ya C- katika mtihani.

Anajiunga na koleji ya kufunza watoto wadogo na kujipatia astashahada inayomwezesha kupata kazi ya kufunza kwenye shule moja.

Hatimaye anajiunga na masomo ya stashahada.

Watu wanaanza kutoa maneno kuhusiana na suala la Fadhumo kusoma na kufanya kazi.

Wanamwambia Adan kuwa amemwacha mkewe kuzurura ovyo.

Wengine wanasema kuwa mkewe hana haja ya kufanya kazi bali akae nyumbani na kutunza watoto.

Hata hivyo, Adan hawezi kuwasikiza kwani yuko katika harakati za kutimiza ahadi aliyotoa.

Mjombake Adan, aliyemlea baada ya babake kuaga pia hatoshi kugeuza msimamo wake.

Anamtumia salamu akamwone, na kumwonya dhidi ya mkewe kusoma na kufanya kazi, eti huenda akamkimbia na hao walimu au wanafunzi.

Anamtaka akomeshe mambo hayo.

Adan anajua hawezi kutimiza hilo.Anamtazama kwa huruma tu, akijua lazima atimize ahadi yake kwa Fadhumo.

Fadhumo pia anatimiza ahadi ya moyo wake.

Jamaa wa babake anapomtaka awe kimada wake ili aweze kumlipia karo anakataa.

Hawezi kukubali kuuza utu wake.

Anahiari kuolewa na Adan badala ya kuwa kimada, wala habadilishi ahadi yake kwa moyo wake anapoolewa.

Anatimiza ahadi ya ndoa kwa kumzalia Adan na kumsaidia kubeba mzigo wa malezi.  

Dhamira ya Mwandishi.

Anawasilisha changamoto wanazopitia wanafunzi katika juhudi za kupata elimu.

Anaonyesha umuhimu wa uvumilivu na kujitolea katika kutimiza azma zetu maishani na jinsi hali hiyo inavyoweza kuleta mafanikio.

Anasawiri matatizo yanayomkumba mtoto wa kike katika jamii iliyojawa na taasubi ya kiume.

Anawasilisha matatizo yanayowakumba watoto mayatima katika jamii.

Anasawiri nafasi ya ndoa na umuhimu wake katika jamii.  

Maudhui

Elimu

Jamii hii inaaminia umuhimu wa elimu.

Babake Fadhumo, licha ya umaskini wake, anampeleka bintiye mjini na kumnunulia vitu anavyohitaji kujiunga na shule ya upili ya kaunti.

Anaachia masomo katika kidato cha pili, muhula wa tatu kwa kukosa karo na pia kuwatunza wadogo zake.

Inamlazimu kuolewa, lakini anasema kuwa bado ataendelea na masomo.

Ili kunata moyo wake, Adan anamwahidi kuwasomesha ndugu zake, ahadi anayoitimiza.

Baada ya miaka sita ya ndoa, anajiunga na shule tena kukata kiu yake ya elimu.

Anapata mwalimu wa kumfunza nyumbani, ambapo hachelewi hata siku moja, hadi anapozoa alama ya C-.

Baada ya masomo hayo, anajiunga na koleji ya mafunzo ya kufundisha watoto wadogo.

Anahitimu na kupata astashahada.

Baada ya kupata kazi hiyo, bado anaandama cheti cha stashahada. 

Watu wanajaribu kumtia maneno Adan kuhusiana na mkewe kusoma lakini hawasikizi.

Wanamtaka amwachishe mkewe masomo.

Mjombake anamwamuru asisikie maneno hayo lakini hamtilii maanani.

Anaondoka kwake akijua hawezi kutimiza hilo.

Nafasi ya Mwanamke.

Jamii hii inaonekana kumkandamiza mwanamke, japo kuna matumaini ya maisha bora kwake.

Mwanamke anawasilishwa kuwa msomi.

Fadhumo anapelekwa na babake mjini kuandaliwa kujiunga na shule ya upili, anayoacha baada ya kufiwa na wazazi.

Hata hivyo, anarejea masomoni miaka sita baadaye na kupata ufanisi mkubwa.

Mwanamke anachukuliwa kama chombo cha starehe.

Jamaa ya babake Fadhumo anataka kujistarehesha na Fadhumo kimahaba ili kuwasaidia nduguze kupata elimu, lakini anakataa.

Mwanamke pia anachukuliwa kuwa mtumishi wa nyumbani.

Watu wanamwambia Adan kuwa hafai kumwacha Fadhumo aendelee na masomo wala kazi bali anafaa kukaa nyumbani ili atunze boma.

Mamake Fadhumo hahusishwi katika kumwandaa kujiunga na shule.

Ni baba anayeandamana naye mjini.Mwanamke pia anaonekana kama kiumbe dhaifu asiyestahili makuu.

Mjombake Adan anamwambia kuwa hafai kumwacha mkewe azidi kusoma, kwamba amesoma vya kutosha.

Anaona kuwa akizidi kusioma atakuwa mjeuri.

Mjombake Fadhumo anakubali kumlipia kakake lakini si yeye.

Umaskini

Babake Fadhumo, Mzee Khalif ni maskini, lakini anajikakamua kumkidhia bintiye mahitaji yote ili ajiunge na shule ya upili.

Anamtaka Fadhumo atie bidii katika masomo ili aweze kujifaa na kuifaa familia yao pia.

Fadhumo anatakiwa kuishi kwa binamu ya babake mjini wakati wa likizo za mihula miwili ya kwanza kuepuka nauli.

Umaskini unamlemea zaidi Fadhumo wazazi wake wanapoaga.

Analazimika kuacha masomo ili kukidhi mahitaji ya nduguze, kwani ndiye mwanambee, na pia kwa sababu ya kukosa karo.

Hali hii inamfanya jamaa wa babake kumtaka awe kimada ili awakimu wadogo zake.

Hata hivyo, umaskini haumfanyi kujidunisha kiasi hicho.

Umaskini ndio unamsukuma Fadhumo kuolewa katika umri mchanga, jambo ambalo hakutaka.

Adan anapotokea kwa nia ya kumwoa, hana hila wala ujanja wa kujitoa.

Anakubali tu Adan anapoahidi kuwasomesha wanuna zake.

Mapenzi na Ndoa.

Ndoa kuu katika hadithi ni kati ya Adan na Fadhumo.

Anamwoa akiwa mchanga ili aweze kuwakidhi wadogo zake baada ya wazazi wao kuaga.

Hata hivyo, anampenda kwa dhati na kumtunza ipasavyo.

Fadhumo na Adan wanajaliwa watoto watatu, na Fadhumo yuko tayari kwa zaidi.

Wanaishi kwa kuelewana kama wanandoa na kusaidiana katika malezi ya wanao.

Fadhumo anafanya suala la malezi kuonekana jepesi na Adan. 

Adan anakubali kumsomesha mkewe baada ya miaka sita nje ya shule.

Rai za watu kuwa anamtelekeza mkewe na huenda akamkalia hazimkatizi kumsaidia.

Hata mjomba wake anaingilia kati kumtaka kukomesha mambo ya mkewe kusoma lakini hayuko tayari.

Mjombake Adan anaonelea kuwa mwanamume ndiye mwenye sauti kwenye ndoa.

Anamtaka Adan akomeshe mambo ya mkewe mara moja kama mwanamume katika boma hilo.

Taasubi ya Kiume/Ubabedume

Mwanamume anaonekana kupaliwa makuu katika jamii hii huku mwanamke akidunishwa.

Khalif anampeleka Fadhumo mjini kumnunulia vitu anavyohitaji kujiunga na shule ya upili.

Mamake Fadhumo hahusishwi katika shughuli hii wala maamuzi kuhusu Fadhumo kwenda nyumbani likizoni.

Jamaa wa babake Fadhumo anamtaka kimapenzi; awe kimada wake ndiposa amsaidie kwa kuwasomesha ndugu zake wadogo.

Suala la kufiwa na wazazi linampa upenyu wa kufuata mkondo huo lakini Fadhumo hampi nafasi.

Mjombake Fadhumo haioni haja ya kuelimisha mtoto wa kike.

Anajitolea kufadhili masomo ya kakake mkuu, kwa kuwa anaona kuwa ndiye afaaye kusoma.

Fadhumo anapozidi kuandamana masomo, watu wanaanza kumtia Adan maneno.

Wanamlaumu kwa kumwacha mkewe azurure huku na huko.

Wanaona kuwa anafaa kumwamrisha atulie nyumbani ili kulea watoto na kutekeleza majukumu ya hapo.

Wanaona kuwa hahitaji kufanya kazi.

Mjombake Adan anamtaka kukomesha suala la mkewe kusoma, kwani anaona kuwa litamfanya kuwa mjeuri asiyemsikiliza mumewe.

Anasema kuwa kama mwanamume katika ndoa yao, Adan hapaswi kukubali upuzi kama huo kuendelea.

Familia na Malezi.

Fadhumo anajaliwa familia inayomwezesha kukua na kusoma.

Babake anampeleka mjini kumnunulia vitu vya kujiunga na shule ya upili.

Pia, binamu wa babake anakubali kuishi naye wakati wa likizo ya mihula ya kwanza miwili.

Wazazi wake wanapofariki, analazimika kuacha shule kuwakidhi nduguze kama mwanambee wa familia.

Mjombake anafadhili elimu ya kakake.

Jamaa wa babake anamtaka kuwa kimada ili awakimu lakini anakataa.

Fadhumo anapata familia yake mwenyewe anapoolewa na Adan.

Anamwoa ili aweze kumsaidia kukidhi mahitaji ya wanuna zake.

Wanajaliwa wana watatu na hata Fadhumo yuko tayari kupata zaidi.

Anawalea wanawe kwa staha na kumfanya Adan ayaone malezi kuwa mepesi kama kanda la usufi.

Mjombake Adan anamwita anapohisi kama mambo hayaendi sawa. Anamtaka kumkomesha mkewe kusoma.

Mjomba huyu ndiye amemlea Adan baada ya babake kufariki.

Hivyo, Adan anamheshimu na kumsikiza, licha ya kuwa hayuko tayari kutekeleza matakwa yake wakati huu.

Kifo/Mauti.

Babake Fadhumo, Mzee Khalif anaangamia kwa ajali ya barabarani na kumwachia ukiwa Fadhumo.

Yuko katika kidato cha kwanza wakati huu, na kifo hiki kinamhuzunisha sana. 

Mamake Fadhumo pia anafariki akiwa katika kidato cha pili na kuwaacha wanawe yatima.

Mauko ya wazazi hawa yanamletea matatizo.

Analazimika kuacha shule kwa kukosa karo na pia kuwakimu nduguze wadogo.

Hatimaye anaolewa na Adan.

Adan anapokwenda kwa mjombawe, anamsikiliza kwa makini kwa kuwa ndiye mlezi wake.

Alimlea na kumsomesha hadi alipofika baada ya babake mzazi kuaga.

Maudhui mengine ni kama vile Uzinzi, Migogoro, Utamaduni na Mabadiliko.  

Wahusika: Sifa na Umuhimu

Fadhumo

Ni msomi.

Anajiunga na shule ya upili maarufu kaunti nzima.

Hata baada ya kuolewa, anarejea masomoni na kujipa vyeti vya astashahada na stashahada.

Ni mkakamavu.

Anaamua kurudi masomoni hata baada ya miaka sita nje.

Anakataa katakata rai ya kuwa kimada kwa jamaa anayemtaka kukidhi mahitaji ya nduguze.

Ni mwenye bidii.

Hata baada ya kuwa nje ya shule kwa miaka sita, anarejea tena masomoni na kutia bidii.

Anatafuta mwalimu wa nyumbani kumsomesha na kujiunga na koleji baada ya kupata alama C-.

Ni mwajibikaji.

Anaacha masomo kuwakidhi wadogo zake wazazi wao wanapoaga.

Anajaribu kila awezalo kutafuta jamaa wa kuwasaidia.

Analazimika kuolewa kwa ajili yao.

Anakidhi majukumu anayotakiwa katika ndoa.

Ni mwenye mapenzi ya dhati.

Anampenda mumewe Adan na anamkidhia mahitaji yote kama mumewe.

Anamwambia kuwa yuko tayari kumpa watoto zaidi.

Umuhimu wa Fadhumo.

Ni kiwakilishi cha elimu na umuhimu na nafasi yake katika jamii ya sasa.

Kupitia kwake, madhila yanayowakumba watoto mayatima, hasa wa kike yanadhihirika.

Ni kielelezo cha bidii na kujitolea katika kutekeleza azma na jinsi hali hiyo huleta mafanikio.

Ni kiwakilishi cha nafasi ya mwanamke katika jamii iliyojaa ubabedume.

Ni kiwakilishi cha asasi ya ndoa na nafasi yake katika jamii.

Adan

Ni mwajibikaji.

Anawajibikia suala la elimu ya mkewe.

Anamsaidia kuandama elimu anayotamani hadi atakapo.

Anatimiza wajibu wake kama mume na kupuuza maneno ya watu.

Ni mfadhili.

Anajitolea kuwakimu nduguze Fadhumo baada ya kumwoa.

Anawasomesha hadi wanapomaliza na kuingilia ya Fadhumo.

Ni mwenye msimamo dhabiti.

Anapoamua kumsomesha Fadhumo, maneno ya watu hayamrudishi nyuma.

Hata mjombake aliyemlea hatoshi kumbadilisha.

Ni mwadilifu.

Anamsikiliza mjombake bila neno kutokana na heshima anayompa.

Japo hakubaliani na matakwa yake, anaondoka bila neno kwa ajili ya adabu.

Ni mpenzi wa dhati.

Anampenda mkewe Fadhumo na yuko radhi kumkidhia mahitaji yake yote na kumsaidia kusoma hadi popote atakapo.

Umuhimu wa Adan

Ni kiwakilishi cha ndoa na nafasi yake katika kujenga jamii.

Ni kielelzo cha wanaume wanaowathamini wanawake licha ya mitazamo hasi ya jamii.

Kupitia kwake, migogoro katika jamii, hasa kwa misingi ya kijinsia inadhihirika.

Anadhihirisha nafasi ya familia na mahusiano yake katika jamii.

Kupitia kwake, umuhimu wa elimu na nafasi yake katika kujenga jamii inadhihirika.

Bwana Khalif(Babake Fadhumo)

Ni mwenye bidii.

Licha ya umaskini wake, anafaulu kumwingiza bintiye katika shule inayofahamika kaunti nzima na hata kumpeleka mjini kumnunulia vitu anavyohitaji kujiunga na shule hiyo.

Ni mshauri.

Anamsisitizia bintiye umuhimu wa kuandama elimu kwa bidii ili iweze kumfaa yeye binafsi na familia yake pia.

Ni mwajibikaji.

Anatekeleza majukumu yake kikamilifu kama baba.

Anampeleka Fadhumo shule na kumkidhia mahitaji yake huko na kumpa ushauri.

Anamtafutia mahali pa kuishi likizoni kutokana na uhaba wa fedha.

Umuhimu wake

Kupitia kwake, nafasi ya wazazi katika maisha ya wanao inadhihirika.

Kupitia kwake, umuhimu wa elimu na nafasi yake katika kujenga jamii inadhihirika.

Anawakilisha pigo la mauti katika jamii na athari zake hasa kwa mayatima.

Mjombake Adan

Ni mtamaduni.

Anashikilia kuwa lazima mume awe mkuu wa familia na aweze kumpeleka mkewe anavyotaka kama kichwa cha uhusiano wa ndoa.

Ni mwajibikaji.

Baada ya babake Adan kufariki, anamlea na kumkimu hadi utu uzimani.

Ni dikteta.

Anapomwita Adan kwake, hampi nafasi ya kutoa habari yake bali anamwamuru akamkomeshe mkewe kusoma.

Ni mbaguzi.

Anabagua kwa misingi ya kijinsia.

Anasema kuwa mwanamke kama Fadhumo hafai kuachiwa kusoma, anafaa kukaa nyumbani na mume ndiye mwenye kusema katika ndoa.

Ni mwenye imani potovu.

Anaonelea kuwa Fadhumo akiendelea kusoma atakuwa mjeuri kwa mumewe, au atoroke na walimu au wanafunzi wenzake. 

Umuhimu wa Mjomba

Ni kiwakilishi cha ubabedume katika jamii na jinsi unavyomkandamiza mwanamke.

Kupitia kwake, nafasi ya utamaduni inadhihirika.

Anadhihirisha matatizo yanayokumba ndoa kutokana na suala la jinsia.

Ni kiwakilishi cha uwajibikaji kwa kumlea Adan baada ya babake kufariki.

Anadhihirisha umuhimu na nafasi ya familia katika maisha.

Ni kiwakilishi cha migogoro kati ya vijana na wazee katika jamii.  

Mbinu za Uandishi

Tashbihi

Maneno hayo yalikuwa kama hirizi aliyoamua kuivaa ili yamwongoze ……mawazo yalikuwa yanampitia akilini mzomzo kama picha kwenye kioo cha runinga.

Masharti magumu aliyoyaona vigumu kuyakubali kwani ni kama kuuza utu wake kwa shetani.

Miaka ilipita kama upepo…Fadhumo… alionekana kama mtoto mdogo aliyekuwa akimtazama mamake kwa hamu kuona kama atakumbuka ahadi aliyotoa ya kurudi na pipi akitoka sokoni.

Basi hapo alifurahi na kama mtoto, akaanza kueleza kwa furaha…

Alishuhudia macho yake yalivyokuwa yanang’aa kama ya mtoto aliyepewa peremende.

Maswali Balagha

Kwa nini aambiwe wakati wa shule?

Kama ni mengine basi si yangesubiri?

“Utoto? Utoto? Lakini si nilikwmbia ni ahadi niliyompa babangu?”

“Mambo mazuri? Unanifanyia utani ama nini?”“Mjomba, mbona sikuelewi?...”

“Yapi haya nasikia mkeo anasoma? Akisoma, atasoma mpaka wapi?

… Kwani nani anayevalia surualikatika ile nyumba? Wewe au yeye? … Kwa nini wewe unakubali? Kwani umemuoa au amekuoa?...Wewe ni simba mwitu au simba wa sarakasi?”

Dayolojia

Mazungumzo kati ya Fadhumo na babake.

Yanaonyesha hali yao ya kiuchumi na pia ushauri wake kwa Fadhumo kuhusiana na elimu.

Mazungumzo hayo yanaondokea kuwa kumbukumbu za daima kwa Fadhumo.

Mazungumzo kati ya Fadhumo na Adan akimweleza nia yake ya kurejea shule, ambayo mumewe anaridhia.

Yanadhihirisha ukakamavu wa Fadhumo na ufadhili wa mumewe pamwe na masuala ya ndoa.

Mazungumzo kati ya Adan na mjombake.

Yanadhihirisha mitazamo yao tofauti kuhusu mwanamke.

Pia yanadhihirisha migogoro iliyopo katika jamii.

Istiara

Alikuwa ndiye taa iliyomulika na kuchangamsha nyumba nzima.…mwalimu mkuu aliweza kusoma wahaka usoni mwake.

Kwa bidii, alifanya ulezi na uzito wote wa ndoa uonekane kanda la usufi.

Semi

maisha ya kijungujiko- maisha ya kutaabika kukidhi mahitaji.

moyo ulikuwa mzito- alikuwa na mawazo tele, aliemewa.

roho ilimruka- alishtuka sana.

yameingia katika kaburi la sahau- yamesahaulika.

ndio mwanzo mkoko unaalika maua- ndio anazidi kuimarika.

akawa roho si yake- akajawa na wasiwasi na kihoro.

Kisengerenyuma/ Mbinu Rejeshi

Fadhumo anakumbuka mazungumzo yake na babake, ambayo yanaishia kuwa maongezi ya mwisho kati yao.

Anayaweka moyoni na kuyakumbuka kila siku.

Baada ya miaka sita katika ndoa, Fadhumo anamkumbusha Adan ahadi yake ya kumrudisha shule aliyotoa wakati wakifunga ndoa.

Anamweleza kuwa hawezi kuacha hamu hiyo kwani ni ahadi aliyompa babake.

Adan anapomtembelea mjombake, tunarejeshwa malezini mwake.

Ni mjomba aliyemlea baada ya babake kuaga.

Tashihisi

Lakini naona wakati ni huu, ukiuacha utakuacha.

Adan alipigwa na mshangao

Methali

Ahadi ni deni.Asojua maana haambiwi maana.Kinaya. 

Jamaa wa babake Fadhumo anamtaka awe kimada wake ili amsaidie kwa malezi ya nduguze.

Ni kinyume kwake kumtaka kimapenzi mtoto wa jamaa wake ili kumsaidia.

Watu wanamwuliza Adan kwa nini mkewe anaenda kazini hali hahitaji kufanya hivyo.

Ni kinaya kwao kusema hivyo hali mkewe huyo amehitimu kwa ajili ya kazi hiyo.

Mjombake Adan anamwita na kumwamrisha akomeshe mkewe kusoma. Ni kinaya kuwa badala ya kumhongera kwa juhudi zake anamkwaza.

Mbinu nyingine ni kama vile Utohozi na Nidaa.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Ahadi ni Deni summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?