Nipe Nafasi summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Nipe Nafasi- Mzamane Nhlapo

Mtiririko

Mamake msimulizi anaamka huku macho yamesharabu wekundu.

Baba yao hawatumii pesa kutoka Afrika Kusini anakofanya kazi migodini.

Mama anaamua waende Makongeni kwa jamaa ya baba badala ya kuwatazama wanawe wafe njaa.

Wanaabiri basi kutoka Habelo, kijiji wanachoishi, mjini Mbote.Wanafikia mwisho wa barabara na kushuka basi.

Wanaipanda Milima ya Maloti huku wakianguka mara kwa mara kwa utelezi, nayo baridi ikiwapiga vilivyo.

Mama anajisemea kuwa lazima arudi kufanya kazi kuwakidhi wanawe.

Baada ya kumaliza milima, mama anataka kumnyonyesha mtoto wao mdogo, Mkhathini, lakini amefariki.

Wanalia kwa kite na kuendelea na safari.

Wanafika kwa jamaa yake baba.

Wanakaribishwa kwa furaha na huzuni sababu ya kifo cha Mkhathini.

Mama ana ujasiri, kwani anajua lawama zinazomsubiri, kuwa haheshimu mumewe na amesababisha kifo cha mwanawe.

Mama anasema amekuja bila ruhusa ya mumewe wala jamaa zake kwa kuwa alijua hawangempa, na pia kuokoa wanawe kufa njaa.

Anataka waishi hapo mwezi au miwili akisaka ajira, hilo pia bila ruhusa.

Maongezi ya mama yanazua minong’ono miongino mwa wanaume, wanaohisi amewakosea heshima.

Baadhi wanadai lazima arudi kwao Swaziland.

Msimulizi anaisikia harufu ya kitunguu kwenye nyumba jirani na tumbo linanguruma, anatamani chakula.

Mama Kazili, hata hivyo, anawaeleza wazi hana nia ya kurudi Swaziland, wala hatalazimishwa.

Anasema kuwa anaielewa vyema Biblia, lakini hila za kumdhalilisha mwanamke zinatiliwa nguvu na serikali inayojidai imechaguliwa na wanawake, kwani wanaume wengi wako Afrika Kusini wakifanya kazi.

Wanaume wanatoka nje mmoja mmoja kujadili suala hilo. 

Msimulizi na nduguze wanapatiwa chakula.

Wanaume wanadai lazima Kazili awaombe msamaha.

Wanawake wa makamo wanamuunga mkono lakini wale wazee wanaona amekosa.

Wa mwisho kuingia amebeba kifurushi cheupe, maiti ya Mkhathini.

Matweba, kaka mkubwa wa Moshe, mumewe Kazili, anasema wana watabaki kwao kama wiki mbili, lakini mama atarudi Habelo keshoye wakazike Mkhathini.

Kazili anasimama kupinga uamuzi huo, ambao huwa wa mwisho.

Anaanguka na kuzimia katikati ya usemi wake.

Richman(Msimulizi) na nduguze wanaondolewa kwa kupiga kelele wanapolia, huku mama akimwagiwa maji kichwani aamke.

Mama anashikilia kuwa lazima aboreshe maisha ya wanawe.

Mwishoni mwa mwaka huo, ni mwalimu wa shule ya msingi bila idhini ya yeyote.

Anakidhi mahitaji ya wanawe.

Ufaafu wa Anwani ‘Nipe Nafasi’

Huu ni wito kutoka kwa wanawake, wakiongozwa na Bi. Kazili kwa wanaume.

Mwanamke anataka kupatiwa nafasi, kwani amekandamizwa sana katika jamii hii.

Mwanamke anapopata nafasi, anawajibika zaidi ya mwanamume.

Kazili anapoona mambo yakienda kombo, anaamua kuchukua hatua mwenyewe bila kumhusisha mumewe kama anavyotakiwa.

Anawachukua wanawe na kufululiza hadi kwa jamaa mmoja wa mumewe wasije wakafa.

Anapopata nafasi, anafanya busara na haki kinyume na mumewe.

Msimulizi anasikia usemi wa mamake wanapopanda Milima ya Maloti.

Anajisemea kuwa atarudi kufanya kazi kuwakimu, na siku hiyo lazima wale chajio.

Mumewe amekosa kuwajibika, hivyo yuko tayari kuchukua nafasi hiyo.

Mama Kazili anamwambia Matweba na wanaume wenzake kwamba aliondoka bila kuomba ruhusa kwa mumewe kwa sababu alijua hangekubaliwa.

Anawajuza kuwa hawezi kukaa tu kuwatazama wanawe wakihangaika kwa njaa, amewaleta wanawe wakae hapo kama miezi miwili akitafuta ajira, bila ruhusa pia.

Anafanya maamuzi mwenyewe.

Wanaume wanahisi kwamba Kazili amewatusi, na kwamba lazima arudi kwao Swaziland kwa kuwakosea heshima.

Hatarajiwi kusema ukweli.

Hata hivyo, anawakumbusha kuwa yeye ni raia halali wa Lesotho kupitia kwa ndoa, na hakuna anayeweza kumlazimisha kurudi Swaziland, hata mumewe.

Zaidi, anaeleza jinsi wanawake wanavyohiniwa nafasi na wadhifa katika jamii kwa kusingizia Biblia, kuwa mwanamke anafaa kuwa mnyenyekevu.

Anachukuliwa kama mtoto ambaye anafaa kuomba ruhusa kwa kila kitu kutoka kwa mumewe.

Hali hii inaendelezwa na chama tawala.

Hata hivyo, yeye yuko tayari kuchukua nafasi ya kuboresha maisha yake na ya wanawe.

Maneno ya Kazili yanasababisha kimya, kwani wanaume hawaamini kwamba mwanamke anaweza kusema mambo kama hayo.

Hajapatiwa nafasi kama hiyo. Isitoshe, wanaume wanaelekea kwenye kraal kutatua masuala hayo.

Ni wanaume tu wanaoruhusiwa huko.

Wanawake hawajapata nafasi hiyo.

Matendo ya Kazili yanalakiwa kwa maoni tofauti huko Habelo.

Wanawake wazee wanaona kuwa amekosea wanaume heshima na anafaa kuomba msamaha, lakini wale wachanga wanaona kuwa amaesema ukweli mchungu.

Wanafaa kupatiwa nafasi pia kuwa na usemi.Maamuzi yanayochukuliwa kwenye kraal huwa ya mwisho yasiyoweza kubatilishwa kwa kuwa wanaume wametawazwa viongozi na Mungu.

Kazili anaagizwa kuwa atarudi alikotoka na kuacha wanawe, kisha abebe maiti ya Mkhathini akasaidiwe kuzika.

Wanaanza kufumukana lakini anapinga maamuzi hayo.

Wengine washaanza kutoka, kwani hawatarajii jibu au neno lolote kuhusu maamuzi yao, hajapatiwa nafasi hiyo, lakini anaichukua. 

Richman(Msimulizi), anashangaa iwapo nia ya mamake ya kuboresha maisha yake na yao itatimia.

Hata hivyo, mamake anatimiza hayo kwani mwishoni mwa mwaka, anaanza kufunza shule ya msingi, bila idhini kutoka kwa yeyote.

Ametwaa nafasi hiyo.  

Dhamira ya Mwandishi.

Kubainisha dhiki wanazopitia wanawake mikononi mwa wanaume katika jamii inayowadhalilisha.

Anatoa mwelekeo kwa wanawake walio katika dhuluma kujikaza kujiondoa humo wenyewe.

Anaelimisha kuhusu nafasi ya wanawake katika familia na jamii kwa jumla.

Anadhihirisha umuhimu wa ujasiri na ukakamavu.

Anawasilisha matatizo ya kijamii na jinsi ya kuyakabili ili kuyashinda.  

Maudhui

Taasubi ya Kiume/ Ubabedume

Kazili anapata fununu kwamba mumewe ana mke mwingine migodini.

Hata hivyo, inaaminika kwamba mwanamume ana uhuru wa kuwa na wake wengi atakavyo, lakini mke mwema hafai kulalamika.

Mume mwenyewe hamtumii pesa na anapozituma kupitia kwa mamake hazimfikii mkewe.

Mama Kazili anapofika kwa Matweba, analaumiwa kwa kuondoka nyumbani bila ruhusa ya mumewe, wala hata kumwambia.

Wanaona huko kama kumdharau mumewe.

Anapotaka ajira, wanasema kuwa hapaswi kuifanya bila idhini kutoka kwa mumewe.

Kazili anaeleza jinsi wanaume wanavyojitukuza kwa kusingizia Biblia, inayosema wanawake wawe wanyenyekevu kwa waume zao.

Wanatakiwa kuwaomba waume zao ruhusa kufanya kila kitu, hata kutembelea familia na marafiki zao.

Wanaume wanaposikia maneno ya Kazili, wanabaki kinywawazi kwa kutoamini.

Wanadai kwamba anafaa kurudi kwa wazazi wake Swaziland kwa kuwakosea heshima.

Wanawake wazee wanaamini kuwa amewakosea heshima wanaume.

Wamepandishwa wadhifa sana kiasi cha kuruhusiwa kuwadhulumu wanawake watakavyo.

Wanaume pia ndio wanaopatiwa wadhifa wa kusuluhisha matatizo ya familia.

Ni wao tu wanaoruhusiwa kwenda kwenye kraal kufanya maamuzi kuhusiana na masuala ya familia.

Wanadai kwamba Mungu aliwapa wadhifa wa uongozi.

Maamuzi yanayotolewa kwenye kraal yanachukuliwa kuwa sheria wala hayafai kubadilishwa.

Matweba anapotoa habari za yale waliyoamua, watu wanaanza kufumukana kwani wanaamini kwamba hiyo ndiyo sheria wala haifai kupingwa.

Msimulizi anaeleza tukio la kijijini Habelo, baada ya mwanamke mmoja kumwambia mumewe ni mzembe kandamnasi.

Wanaume wanaanza kukutana kuelezana jinsi mwanamke huyo alivyokosa heshima.

Anatoweka kijijini na watu wanafikiri aliamriwa kurudi kwao, hadi mbwa wanapofukua mwili wake kondeni mwao.

Mumewe alimuua na kumzika.

Migogoro

Msimulizi anashuhudia migogoro kati ya wazazi wake.

Babake anafanya kazi migodini Afrika Kusini, hali mamake anaishi kijijini Habelo.

Ana mke mwingine huko, na pia hamtumii mama pesa, na anapotuma hazimfikii.

Japo anajua hili, anadai kwamba ameshindwa kuishi na mke anayeshinda kulalamika.

Mama anaamua kuondoka kwenda kwa jamaa ya babake.

Mama na wanawe wanapofika kwa Matweba, mgogoro unazuka.

Mama analaumiwa kwa kuondoka bila ruhusa, lakini anadai kwamba hangekaa tu wanawe wakihangaika, na pia alijua hangeruhusiwa.

Anaeleza kwamba yuko tayari hata kutafuta kazi, kinyume na taratibu.

Kazili pia anazua mgogoro miongoni mwa wanwake.

Wale wazee wanaona kwamba amekosa heshima kwa wanaume, lakini wake wachanga wanahongera juhudi zake.

Maamuzi ya wanaume kwenye kraal yanawazulia mgogoro mwingine na Kazili.

Hakubaliani na maamuzi yao wala hayuko tayari kuyafuata.

Wanajiandaa kufumukana lakini anasema maoni yake kwa ujasiri.

Anaanguka na kuwalazimu kummwagia maji.

Mwishoni mwa mwaka, amekuwa mwalimu wa shule ya msingi bila ruhusa kutoka kwa yeyote.

Msimulizi anaeleza mgogoro uliotukia Habelo miaka miwili awali, baada ya mwanamke mmoja kumwita mumewe mzembe kandamnasi.

Wanaume wanasemezana jinsi alivyokosa maadili kwa wanaume.

Hatimaye anatoweka, na baadaye kubainika mumewe alimuua na kumzika kondeni mwao.

Usaliti

Moshe anamsaliti mkewe na wanawe.

Anamwacha nyumbani peke yake na watoto bila kutuma pesa za matumizi.

Anapotuma zinapitia kwa mamake lakini hazimfikii mkewe.

Licha ya kujua haya, hafanyi lolote kumsaidia.

Anasemekana kuwa na mke mwingine migodini anakofanya kazi.

Serikali tawala pia inawasaliti wanawake.

Licha ya kuwa ndio wanaoiweka mamlakani, kwani waume wengi wanafanya kazi mbali na nyumbani, serikali hiyo inaendeleza mifumo ya dhuluma dhidi ya jinsia ya kike.

Inaendeleza siasa za wanawake kuwanyenyekea waume zao, ambao wanawadhulumu.

Matweba anamsaliti Kazili.

Badala ya kumliwaza kwa kufiwa na mwanawe, anamkemea akidai kuwa ndiye sababu ya kifo chake, kwa kuwa hakumheshimu mumewe.

Anasema kuwa lau angesalia nyumbani, kifo hicho hakingetokea.

Anamtaka kuondoka keshoye na kimba hicho kwenda kukizika.

Baadhi ya wanawake wanamsaliti Kazili.

Anajitolea kwa kila hali kuwapigania kutokana na dhuluma za wanaume, lakini baadhi wanadai kwamba amewakosea heshima wanaume na anafaa kuomba msamaha.

Wako tayari kuendelea kudhalilishwa!

Familia

Uhusiano wa kifamilia hauchukuliwi kwa uzito.

Mumewe Kazili anatuma pesa kwa mamake, ambazo hazimfikii mkewe.

Wanawe wanazidi kutaabika mikononi mwa mama yao.

Msimuliza anaeleza kuwa nyanya yao ndiye anapata pesa na hampi mama, ila baba anajua hili.

Hata hivyo, anasema kuwa inamwia vigumu kuishi na mke anayeshinda kulalamika.Kazili anapoona mambo hayaendi vizuri na wanawe wako hatarini kafariki kwa njaa, anaamua kwenda kwa jamaa ya babake anayeishi Makongeni.

Anaona kwamba huko wanaweza kupata auni ya chakula.

Msimulizi anasema kuwa jamaa ya baba yao anafurahia kuwaona lakini taswira ya Mkhathini aliyefariki inamtia wasiwasi. 

Matweba anataka majibu ya maswali kutoka kwa Mama Kazili kuhusiana na safari yake kuja huko.

Anataka kumkumbusha kwamba hakuolewa kwenye ukoo wa Belo kuua watoto bali ‘kuwatengeneza’.

Matweba ako tayari kusimama mahali pa nduguye aliye kazini Afrika Kusini.

Utamaduni

Japo Kazili anajua kwamba mumewe ana mke mwingine huko migodini anakofanya kazi, hatarajiwi kulalamika kwani utamaduni unamruhusu mume kuwa na wake wengi.

Ndiye pia anatakiwa kufanya kazi na kukidhi familia yake.

Msimulizi anasema kuwa kama mama hangekuwa makini, angekumbushwa kuwa hakutolewa Swaziland aje kuwaua watoto bali kuwatengeneza.

Mwanamke anachukuliwa kuwa kifaa cha uzazi.

Anatarajiwa kuvyaa watoto wengi iwezekanavyo na kuwatunza.

Anatarajiwa pia kuomba ruhusa kutoka kwa mumewe kabla ya kufanya lolote.

Matweba na wanaume wenzake wanamsikiza Kazili.

Tunaambiwa wanasikiza kwa kimya kama kile kinachokuwa katika mahakama yao ya kitamaduni.

Wanaume pia wana sehemu ambayo wanatumia kutoa maamuzi kuhusiana na masuala ya kifamilia kama hayo inayoitwa kraal.

Hapo wanawake hawaruhusiwi.

Maamuzi wanayotoa wanaume yanachukuliwa kuwa sheria.

Tunaambiwa kuwa Matweba na wenzake wanajitahidi kulinda tamaduni za jamii.

Matweba anadai kuwa wanaume ambao hawajapata kazi kwenye migodi wana jukumu la kuhakikisha kwamba familia haisambaratiki.

Wanafaa kuhakikisha kuwa wanawake wanawaheshimu waume zao.

Msimulizi anaeleza kisa cha mwanamke aliyesema mumewe ni mzembe.

Hayo yalionekana kuwa matusi makubwa.

Ilisemekana kuwa amerudi kwa wazazi wake au kuwa ngalile, mwanamke aliyerudi kwa wazazi wake.

Wanagundua baadaye kuwa aliuawa na mumewe na akamzika kondeni mwao.

Hata mama Kazili anapobisha kauli ya wanaume, wanawake wazee wanahisi kwamba anafaa kuomba msamaha.

Msimulizi na ndugu zake wanaandaliwa chakula kitamu cha papasane(aina ya mboga za mwituni) na nyama ya kondoo.

Anasema kuwa jina lake la kupanga, Richman, linatokana na bwana mmoja wa jamaa ya Belo aliyefuga kondoo wengi.

Isitoshe, anasema kuwa anawasikia ng’ombe wakikoroma kwenye kraal.

Ni baadhi ya shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa.

Kazi

Moshe, babake msimulizi anafanya kazi katika migodi huko Afrika Kusini.

Anatakiwa kutumia kazi hiyo kuikimu familia yake. Anatuma pesa kwa mamake muda kwa muda.

Wanaume wengine pia wanafanya kazi katika migodi hiyo hiyo na kuwaacha wake zao nyumbani.

Kazili anamweleza Matweba na wenzake kwamba yuko tayari kutafuta kazi ili kukimi mahitaji yake na ya wanawe.

Mwishoni mwa mwaka, anapata kazi kama mwalimu wa shule ambayo msimulizi anatumaini kuwa itawaboreshea maisha.

Mazingira

Kati ya Makongeni na Habelo, ni umbali wa kilomita arobaini.

Msimulizi, mamake na nduguze wanaabiri basi uchwara mjini Mbote.

Wansafiria basi hilo kwa kilomita thelathini.

Kufikia hapo, haliwezi kuendelea na safari kutoka hapo, ndio mwisho wa barabara.

Wanalazimika kutembea kwa miguu safari ngumu.

Wanakabiliana na majabali na hatari ya utelezi milimani Maloti.

Ni milima mikubwa na myeupe, na theluji imetapakaa kila mahali.

Zaidi, baridi kali  inawapiga. Naposeka, dadake msimulizi anaanguka mara kwa mara na kulowesha nguo zake kwa theluji.

Msimulizi anambeba mgongoni.

Wanaanguka pamoja mara kwa mara.

Mama pia anaanguka mara mbili tatu.

Wanazidi kupambana huku vipande vya theluji bado vikiwapiga nyusoni.

Hali ya mazingira inasababisha kifo cha ndugu yao mdogo, Mkhathini.

Isitoshe, hali ya mazingira inawawezesha wanawe kupata hifadhi.

Kutokana na theluji, Matweba anasema kuwa atawaruhusu wana kukaa kwa wiki mbili tatu hivi, kisha watarudishwa Habelo.

Richman na nduguze wanapata chakula chenye mboga aina ya papasane, inayohimili baridi ya kipupwe. Inafanya vizuri katika mazingira haya.

Ukombozi

Mwanamke yuko katika vita vya kujikomboa kutoka kwa dhuluma za mwanamume na utamaduni unaomdhulumu na kumdhalilisha.

Kazili ndiye anaongoza vita hivi.

Anapoona mumewe amemdhalilisha vya kutosha, anaamua kuondoka.

Hajali kuomba ruhusa kama anavyotakiwa. Anachotilia maanani wakati huu ni maslahi yake na ya wanawe.

Wanapanda milima kwa bidii hadi wanapofika nyumbani kwa Matweba, kakake mumewe.

Kazili anasimama kidete kupinga dhuluma za wanaume kwa wanawake kwa kusingizia Biblia na utamaduni.

Anasema kwamba anataka kuwa mfano kwa wanawake kwamba wanafaa kuchukua hatua wanapoona waume zao hawawajibiki.

Wanawake wa makamo wanakubaliana na rai ya Kazili, licha ya wale wazee kuchukulia haya kuwa madharau na kumtaka kuomba msamaha.

Wako tayari kubadili mkondo huu wa dhuluma dhidi yao.

Mama Kazili anakana maamuzi ya wanaume kwenye kraal ambayo awali yanachukuliwa kuwa sheria isiyoweza kupingwa.

Vitisho vyao kuwa atarudi kwao Swaziland havimshtui. Anawakumbusha yeye ni raia halali wa Lesotho kupitia kwa ndoa.

Anawaambia kuwa atarudi nyumbani kupambana kuboresha maisha yake na ya wanawe.

Mwaka huo ukiisha, anafanya kazi ya ualimu bila ruhusa kutoka kwa yeyote, na wanawe wanapata chakula kila siku.

MabadilikoMama Kazili anaondoka Habelo bila ruhusa kutoka kwa mumewe kama anavyotakiwa.

Yuko tayari kupigania hali yake na ya wanawe.

Hayuko tayari kutawaliwa na mwanamume kama jamii inavyotaka.

Anawajuza haya wazi wazi Matweba na wanaume wenzake.

Wanapomaliza kupanda Milima ya Mailoti na Mkhathini kufariki, mama anaangua kilio.

Wanapofika nyumbani kwa Matweba, hata hivyo, anajua hali inayomkabili.

Sasa yuko makini na uso wake umejaa ujasiri.

Anapozungumza baadaye kupinga maamuzi ya kraal, amerejea sautu ile ile ya milimani.

Kazili anapobisha kauli za wanaume, wanashtuka sana kwani hawajazoea hali hii.

Wamezoea wasemalo ni sheria.

Mwamko wake unaleta msisimko miongoni mwa wanawake wa makamo wanaohisi kwamba hatimaye amesema ukweli unaostahili kusemwa.

Wanahisi kwamba ni wakati wao kusimama kidete kupinga mzigo mzito wa kiuchumi uanowalemea.

Msimulizi anakumbuka usemi wa mama kuwa ataboresha maisha yake na ya wanawe, jambo ambalo anashangaa kama linawezekana.

Hii ni kwa sababu hili linawaziwa kuwa jukumu la wanaume.

Hata hivyo, anaamini mwishoni mwa mwaka, mamake anapopata kazi ya kufunza shule ya msingi, kwani hawakosi chakula.

Kifo/Mauti 

Baada ya kumaliza kupanda Milima ya Maloti, mama anamchukua mtoto wake mchanga, Mkhathini, akinuia kumnyonyesha.

Hata hivyo, mwili wa mtoto huyu umekakamaa, wala hapumui.

Anaangua kilio na kuemdelea na safari huku amebeba maiti hiyo hadi nyumbani kwa Matweba.

Msimulizi pia anakumbuka kisa cha mwanamke wa Habelo aliyetoweka baada ya kumwambia mumewe kandamnasi kwamba ni mvivu.

Hatimaye, anagunduliwa amefariki baada ya mbwa kufukua mwili wake ulioanza kuoza kondeni mwake.

Maudhui mengine ni kama vile Nafasi ya Mwanamke, Dini, Ukatili, Udhalimu, Uwajibikaji na Malezi.  

Wahusika: Sifa na Umuhimu.

Mama Kazili

Ni mkakamavu.

Anapoamua lake, harudi nyuma.

Anaamua kuondoka Habelo bila idhini ya yeyote.

Anawachukua wanawe na kuondoka kuwatafutia chakula.

Anamwambia Matweba kwamba atatafuta ajira bila ruhusa kuwakidhi wanawe na kweli mwishoni mwa mwaka huo, anakuwa mwalimu.

Ni jasiri.

Anawakabili wanaume bila woga.

Anawaambia wazi kwamba wanawadhalilisha wanawake.

Anawaambia kwamba anataka kuwa mfano bora kwa wanawake kuwa wanafaa kusimama kidete kutetea maslahi yao.

Msimulizi anasema kuwa walipofika kwa Matweba, uso wa mamake ulijaa ujasiri wa ajabu.

Ni mwenye bidii.

Anatia bidii katika kusaka ajira hadi anapoipata na kuwa mwalimu wa shule ya msingi.

Yuko tayari kufanya lolote kuboresha maisha yake na ya wanawe.

Mwishowe, wanapata chakula kila siku.

Ni mwajibikaji.

Anapoona mambo yanaenda kombo huko Habelo, anaamua kuondoka kwenda kwa jamaa ya mumewe Makongeni.

Anaelewa kwamba akikawia huko wanawe watakufa njaa.

Ni mkombozi.

Anajitolea kupigania haki za mwanamke katika jamii.

Anaondoka bila ruhusa kwa mumewe na kwenda kwa Matweba kuwatafutia wanawe chakula.

Anawaeleza wanaume waziwazi kuwa wanafaa kuwapa wanawake nafasi kujiendeleza.

Anazua mwamko mpya miongoni mwa wanawake wa makamo.

Umuhimu wa Kazili

Ni kiwakilishi cha dhuluma za jamii dhidi ya jinsia ya kike.

Ni kielelezo cha wanawake jasiri wanaojitolea kwa kila hali kupigania maslahi yao.

Anawakilisha migogoro inayoshuhudiwa katika jamii.Ni kiwakilishi cha ndoa katika jamii na masaibu yake.

Ni kielelezo cha ujasiri na ukakamavu katika maisha

Richman(Msimulizi)

Ni mfadhili.

Wanapofika kwenye Milima ya Maloti, dadake Nopaseka anaona ugumu kukwea kwani anaanguka mara kwa mara.

Anajitolea kumbeba mgongoni, licha ya kuwa wanaanguka mara kwa mara.

Ni mwenye makini.

Anagundua mzozo kati ya wazazi wake na mamake na mkwewe.

Anagundua mabadiliko katika sura ya mamake wakiwa kwenye Milima ya Maloti na nyumbani kwa Matweba.

Anagundua macho ya mamake yamesharabu wekundu kama alikuwa akilia.

Ni mwenye kujali.

Anamjali sana mamake.

Anapomwambia wanaondoka Habelo, anataka kujua wanaenda wapi na kwa nini.

Anaposema mbele ya Matweba na wanaume wengine kisha kuishiwa na nguvu na kuanguka, Richman analia kwa kite akishangaa ikiwa mamake atafariki.

Umuhimu wa Richman.

Anawakilisha matatizo wanayopitia watoto katika ndoa yenye mizozo.

Ni kielelezo cha watoto wanaowajali wazazi wao wakati wa matatizo.

Ni kielelezo cha utu na ubinadamu katika jamii.

Kupitia kwake, madhara ya utamaduni hasa kwa watoto yanabainika.

Matweba

Ni mtamaduni.

Anashikilia kwamba wanawake hawana uhuru wa kufanya maamuzi bila ruhusa ya waume zao.

Anamwambia Kazili kuwa hatamruhusu kumdhalilisha Moshe.

Tunaambiwa kuwa pamoja na wanaume wenzake, wanajitahidi kutunza utamaduni.

Ni dhalimu.

Anataka kumrudisha Mama Kazili Habelo siku inayofuata, huku amebeba maiti ya Mkhathini mgongoni alivyombeba kumleta.

Anataka kukaa na wanawe kwa wiki mbili tatu kisha kuwarudisha.

Ni mfadhili.

Yuko tayari kukidhi mahitaji ya watoto wa kakake Moshe.

Anawapa chakula cha kutosha.

Anasema kuwa atakaa nao kwa wiki mbili kisha kuwarejesha kwa mama yao Habelo.

Ni katili.

Hajali masaibu yaliyompata Kazili huko Habelo.

Anataka kumtwika mzigo wa kurudi huko kumzika Mkhathini.

Anamlaumu kwa kifo chake. Hamwonei huruma kwa kuwa amefiwa na mwanawe.

Umuhimu wa Matweba

Ni kiwakilishi cha wanaume wanaoendeleza unyanyasaji wa wanawake katika jamii.

Anawakilisha utamaduni na nafasi yake katika jamii.

Anawakilisha nafasi ya familia katika kusaidiana maishani.

Moshe(Babake Msimulizi)

Ni mzinzi.

Anamwacha mkewe nyumbani na kuoa mwingine kwenye migodi Afrika Kusini, anakofanya kazi.

Ni mwenye mapuuza.

Anajua kuwa pesa anazotuma kwa mamake hazimfikii mkewe lakini hafanyi lolote.

Anadai kwamba anachoshwa na mkewe kulalamika kila mara.

Ni mtamaduni.

Anadai kwamba ameshindwa na mke ambaye anashinda kulalamika kila mara, hali anamdhulumu.

Anaoa mke mwingine migodini kwa kuwa utamaduni unamruhusu.

Ni mwenye bidii.

Anaondoka kwao Lesotho kwenda hadi Afrika Kusini kufanya kazi katika migodi ili kukidhi mahitaji ya familia yake. 

Ni katili.

Anamtelekeza mkewe na wanawe nyumbani na kuoa mwingine.

Licha ya kujua hela hazimfikii mkewe, hafanyi lolote.

Mkewe analazimika kuranda kwa jamaa kusaka msaada.

Umuhimu wa Moshe.

Ni kiwakilishi cha wanaume wanaodhulumu wanawake katika jamii.

Ni kiwakilishi cha waume wasiojali aila yao.Kupitia kwake, nafasi ya kazi katika kuboresha maisha inadhihirika.

Anawasilisha matatizo na misukosuko iliyopo katika ndoa. 

Mbinu za Uandishi.

Semi

alikata kauli- aliamua.

shughuli ya kuuma meno- shughuli ngumu, ya kung’ang’ana.

baridi shadidi- baridi kali sana.

vilikufa ganzi- vilipoteza hisia sababu ya baridi.

kumeza mafunda machungu- kuhisi uchungu mwingi.

bumbuazi iliyowapiga- mshangao uliowapata.

walikaa tuli- walikaa na kutulia.

kumtia mikononi- kumshambulia kwa vita.

Kumuunga mkono- kukubaliana naye, kusisitiza msimamo wake.

walijishushia pumzi- walipumua kwa nguvu kisha kutulia.

kusimama wima- kujitolea kwa moyo mmoja.

tuliangua kilio- tulianza kulia.

Tashihisi

Baridi ilizidi kututafuna kadri tulivyokazana kupanda Milima ya Maloti…

Mashavu yetu yaliadhibika kwa upepo baridi huku vipande vya theluji vikitupiga kwenye nyuso zetu.

Tulijikaza zaidi kupambana na safari ile ya kilomita kumi.

Ukimya uliotawala unaweza kumithilishwa……sauti yake ikisindikizwa na minong’ono kutoka kwa wanaume waliokuwa pale.

Kundi la ndege… huku wakiimba nyimbo zao kama kwamba hakukuwa na theluji tena.

Sauti yake ilipenya masikio kwa udhabiti wa ajabu.

Kimya kilitawala nyumbani mle… 

…mzigo mkubwa wa kiuchumi ulitishia kuwashinda kuubeba peke yao.

Kimya chao kilitisha.…akatuachia ulimwengu huu katili, usiojali.

Tashbihi

Ukimya uliotawala uliweza kumithilishwa na ule unaotarajiwa katika mahakama zao za kijijini wakati kuna kesi nzito ya kuamuliwa.

Sheria za jamii zinamchukulia mkwanamke kama mtoto anayefaa kuwa chini ya uelekezi na utunzaji wa mwanamume.

Kimya kilitawala nyumbani mle kana kwamba wote walikuwa wamekatwa ndimi.

Mmoja baada ya mwingine… Kiza kiliwafanya kuonekana kama vivuli virefu.

Kinaya

Mosha anajua kwamba mkewe hafikiwi na hela anazotuma.

Hata hivyo, hafanyi lolote, bali anamlaumu kwa kulalamika.

Matweba anamlaumu Kazili kwa kifo cha mwanawe badala ya kumfariji.

Anadai kwamba angemheshimu mumewe na kusalia nyumbani, hayo hayangetokea.

Ajabu ni kuwa huko walikuwa hatarini kufa njaa.

Anatakiwa kuomba ruhusa kwa mumewe na wakwe, ambao ndio kichocheo chake kuondoka.

Kazili anailaumu serikali kwa ajili ya mateso na dhuluma dhidi ya wanawake.

Chama cha Taifa cha Basutoland kinachoendeleza haya kimechaguliwa na wanawake hao, kwani wengi wa waume zao wako kazini kwenye migodi, na wanashabikia chama kingine.

Badala ya kuwatetea wanwake hao, kinawakandamiza.Kazili analaumiwa kwa kuwakosea heshima wanaume, na kumdhalilisha mumewe kwa kuondoka nyumbani bila kumtaariifu.

Ajabu ni kuwa anawaambia ukweli wasiotaka kusikia, na mumewe mwenyewe ndiye anamdhulumu kwa kumtelekeza na kumlazimu kuja huku.

Mama Kazili anapozirai, msimulizi na dadake wanaangua kilio.

Wanaondolewa upesi wakisemekana wanatoa kelele zisizofaa.

Ajabu, hawaoni kama hilo ni tukio la kusikitisha bali wanamwagilia maji kichwani ili aweze kuamka.

Kisengerenyuma/ Mbinu Rejeshi

Wanapofika kwa Matweba, msimulizi anaona mabadiliko katika sura ya mamake.

Anasema kuwa hungejua ni yule yule ambaye muda mfupi uliopita alikuwa ameanguka mara kadhaa na wanawe kwenye theluji.

Msimulizi anakumbuka tukio la awali kijijini Habelo, wakati mwanamke mmoja alimwita mumewe mzembe kandamnasi.

Baada ya muda, mwanamke huyo alitoweka na baadaye kufahamika aliuawa na kuzikwa mbwa walipofukua mabaki ya mwili wake ulioanza kuoza.

Msimulizi anapopatiwa chakula chenye nyama ya kondoo, anakumbuka kuwa jina lake la kupanga, Richman, lilisemekana kutokana na bwana mmoja aliyeishi Makongeni miaka ya 1890, ambaye alifuga kondoo wengi.

Mama anapoeleza msimamo wake akipinga maamuzi ya wanaume kwenye kraal, msimulizi anakumbuka kuwa sauti anayosema kwayo ni ile aliyokuwa nayo wakipanda Milima ya Maloti.

Anapoanguka, anakumbuka anguko lake kwenye milima, tofauti ni kuwa wakati huu hataji jina la babake.

Msimulizi anakumbuka matukio ya siku waliyoenda kwa Matweba na maneno ya mamake.

Anakumbuka hasa usemi wake kuwa kabla ya kufa, anataka awe amepata nafasi ya kuboresha maisha yake na ya wanawe.

Kejeli

…wangemkumbusha kuwa ndugu yao hakumuoa kutoka Swaziland kuwaulia watoto, aliolewa pale ‘kuwatengeneza’ watoto ili kuiendeleza familia ile.

“Na unafikiri unatoa mfano gani kwa wake wengine walioolewa katika familia ya Belo?”

Sasa, nikiwa na nyama ya kondoo sahanini mwangu, niliona kuwa jina lile kweli liliniafiki.…maamuzi hayo yalichukuliwa kuwa matakatatifu kwa maana wanaume walitakaswa viongozi wa familia na mwenyezi Mungu.

Utabeba maiti ya mtoto huyo mgongoni mwako, kama ulivyoibebea kuileta hapa.…tulichukuliwa na kupelekwa kwenye ile nyumba nyingine kwa kusababisha kelele zisizofaa na kuwasumbua watu wazima waliokuwa kule.

Chuku

Hewa ilikuwa baridi shadidi, na iligandisha hata boho za mifupa mwilini… Matweba aliamuru kwa sauti ambayo ingemwogofya simba.

Tumbo langu lilinguruma na mate kunidondoka.

Kwa miaka miwili nilikuwa sijapata kula nyama.

Istiara

Ingawa waume zao walidinda kukiri hili, mzigo mkubwa wa kiuchumi ulitishia kuwashinda kuubeba…

Mbegu aliyokuwa anapanda ilianza kuota mizizi.

Takriri

… kama inavyosema sheria.

Sheria za kijamii…Mmoja baada ya mwingine, walianza kutoka nje, kimyakimya.

Harakaharaka, tulichukuliwa…

Maswali Balagha

“Na unafikiri unatoa mfano gani kwa wake wengine walioolewa katika familia ya Belo?”

“Huyu mwanamke anasoma Biblia kweli? Atajifunza lini kutuheshimu?”

“Ndio. Anaiheshimu Biblia? Anatuheshimu kweli?”

Dayolojia 

Mazungumzo kati ya msimulizi na mamake kabla ya kuondoka Habelo.

Anamweleza mwanawe sababu ya kuondoka huko.

Mazungumzo haya pia yanatuwasilishia matatizo anayopitia Mama Kazili na kujitolea kwake kuboresha hali yake na ya wanawe.

Mazungumzo kati ya Kazili na Matweba.

Yanatusaidia kubaini nafasi ya mwanamke katika jamii na jinsi jamii inavyomdhalilisha na kumtukuza mwanamume.

Uzungumzi Nafsia

Niliyasikia maneno yake, Nitarudi na kufanya kazi ili niweze kuwakimu… leo lazima watapata chajio…

Tanakuzi

… kulikuwa na mchanganyiko wa furaha na huzuni.

Lakabu

Msimulizi ana jina la kupanga, ‘Richman’.Mbinu nyingine ni pamoja na Tadmini, Mdokezo, Koja na Utohozi.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Nipe Nafasi summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?