Pupa summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Pupa- F. M. Kagwa

Mtiririko

Mwakuona amezaliwa na kulelewa katika mtaa duni na nduguze, ambapo amekumbana na dhiki si haba katika maisha yake.

Wanapatwa na utapiamlo kwa kupungukiwa na chakula na kuwa na nywele za hudhurungi na miguu ya matege.

Hata hivyo, bado ni mtiifu, mcha Mungu na anatia bidii masomoni. 

Jioni moja akitoka shuleni, anamwona bibi fulani akimwangalia kutoka mbali na hatimaye kumsalimu anapomfikia.

Anamwambia kuwa ni wakala wa kampuni fulani mjini ambayo inatafuta vijana wa kudhamini.

Mwakuona anaona hii kama fursa yake ya kupata afueni, hasa anaposikia kuna masomo ya juu.

Wakala huyu anavutiwa na sura ya Mwakuona anapomkagua.

Yuko kidato cha tatu na amebaleghe na kuwa na umbo nzuri.

Wanakubaliana, huku Bi. Mtego akiahidi kumtayarishia pasipoti na visa kwa muda wa wiki moja.

Anampa kijisimu ili wawasiliane, lakini anaonywa kisionekane na yeyote, hata wazazi wake.

Wataambiwa kila kitu kikiwa tayari. 

Mipango inakamilika na Mwakuona anatoka nyumbani kisirisiri, akijiandaa kama anayeenda shuleni.

Anapofika mjini, anabadilisha kwenye choo cha umma na kuvaa mavazi aliyopatiwa na Bi. Mtego baada ya kuvua sare.

Anampigia Bi. Mtego naye anakuja kumchukua.

Anapelekwa katika chumba maalum wanakolainishwa miguu, nywele na kulishwa vizuri na wenzake wanaopatana huko.

Wengine wanaondoka kwa furaha. Wanaandaliwa kwa majuma sita na kubadilika kabisa na kutiwa vipodozi na mapambo.

Mwinamo nako, ametafutwa kila mahali bila mafanikio.

Wazazi hawana picha yake wala hela za kuwalipa polisi. 

Anapoondoka matayarishoni, anakumbuka hajawahi kumwona tena Bi. Mtego wala kuwasiliana naye, na kisimu kilikwishachukuliwa.

Anaendeshwa na dereva lakini kapewa nguo fupi.

Anatarajia kupelekwa uwanja wa ndege, lakini gari linalenga asikojua.

Anajipata kwenye jengo lililoandikwa Chenga-ways, anakopokelewa na watu wanaomjua kwa jina. 

Anaona wanawake wanaotembea mbele ya wanaume nusu uchi, huku wanaume wakiwachagua na kuelekezwa vyumbani.

Wanaume wanalipa na kuwafuata.

Anaambiwa anayemchukua ameamuliwa na hapo anamfuata mwanamapokezi.

Wanapita mapokezi mengine ambapo wasichana wananengua viuno mbele ya wanaume na kunyakuliwa.

Analenga kuona kaunta ya wanaosafiri. Anakutana na msichana waliyekuwa pamoja matayarishoni.

Anataka kumsalimu lakini mwelekezi wake anamzuia. Anaingizwa kwenye chumba na mlango kukomelewa. 

Anampata mwanamume anamsubiri, akimwambia kuwa alimchagua na kumlipia pesa nyingi.

Mwakuona anakumbuka matukio ya awali tangu Bi. Mtego, kutoroka nyumbani, matayarishoni, na sasa hapa alipo.

Anajaribu kupinga hatua za yule mwanamume lakini inambidi kukubali madhara aliyojiletea mwenyewe.

Anaporejeshwa chumbani walimo wenzake, Mashaka, aliyekaa pale kwa muda anamliwaza. 

Anamweleza nia yake ya kutoroka, kutafuta haki na kurudi masomoni.

Mwakuona anaapa kutoroka pale huku akiwalaumu wanaoendesha biashara hii, Bi. Mtego aliyemnasa na serikali iliyofumbia macho hali hii, baadhi ya wateja wakiwa maafisa wa serikali.

Anajilaumu pia kwa kuhadaiwa kwa urahisi.

Ni miezi saba imepita na amepitia mengi.

Leo yuko mbioni kutoroka, na nyuma anaandamwa.

Alifaulu kwa kuomba ruhusa kwenda msalani akawa hajafuatwa.

Anasikia sauti, ambayo inatolewa na bati lililobambatuka na kuacha mwanya.

Anarusha viatu nje na kusikia mtu akikemea kisha vishindo vyake akitoroka.

Anaruka na kufikia mtambaapanya, anapita na kujirusha nje licha ya bati kumkwaruza.

Anafuata njia yenye giza asionekane.

Amekimbia kwa tahriban saa nzima na amechoka kabisa.

Anashindwa kuendelea na kuketi kando ya kijia, kiatu mkononi tayari kujikinga.

Ana malengo matatu makuu.

Kwanza, analenga kufika nyumbani, japo hajui kama watamkubali.

Pili, ni kutafuta kituo cha polisi na kueleza yanayotukia huko Chenga-ways alivyoahidiana na Mashaka, ambaye hajui aliko.

Tatu ni kwenda kwenye kituo cha habari na kusimulia yaliyompata ili watesi wao waanikwe, na labda kuchukuliwa hatua.

Kutoka Chenga-ways, wanamsaka kila mahali baada ya kuona shimo alikotokea na alama za damu.

Wengine wanachunguzwa wasiwe na nia ya kutoroka.

Jua linapochomoza, anakuona nyumbani kwao, Mwinamo kwa mbali.

Ufaafu wa Anwani ‘Pupa’. 

Ina maana ya papara au haraka katika kutekeleza jambo. Ina madhara mengi, mazuri na mabaya.

Kuna methali isemayo kwamba mwenye pupa hadiriki kula tamu.

Mwakuona anapokutana na Bi. Mtego na kusikia nia yake ya kumpeleka ng’ambo kufanya kazi, anamezwa na pupa na kukubali masharti yake mengi bila kuyawazia sana.

Anaiona hii kama fursa yake ya kuwa na maisha mazuri na kusaidia familia yake pia.

 Bi. Mtego anampa simu ambayo anafaa kuificha na kuitoa faraghani.

Haifai kuonekana na yeyote, hata msiri wake wa karibu zaidi wala wazazi wake.

Anaificha kusikoweza kufikika na mikono ya ziada.

Anaposubiri kwa wiki, muda huu anauona kama mwaka kutokana na pupa aliyo nayo kwenda ng’ambo.

Anahiari kuacha hata familia yake na masomo yake. 

Mwakuona anaondoka nyumbani kwa pupa siku ya miadi kwa jitihada tele kufika mjini, anakofaa kukutana na Bi. Mtego.

Anajifichaficha na kuwahadaa watu hadi hatimaye anapofika mjini.

Anabadili sare na kuvaa mavazi aliyopatiwa na viatu, kisha kumpigia simu wakala wake.

Anashangaa kwa nini mhisani wake ndiye anamtumikia.

Hata hivyo, pupa haimruhusu kuchunguza hilo.

Anaona ng’ambo tu! Katika matayarisho, anafanyiwa mengi.

Anatengenezwa nywele na kukandwa kisha kulainishwa ngozi.

Anahudumiwa kwa muda wa majuma sita pamoja na wenzake, huku wakilishwa vyakula vizuri.

Huduma zote hizi ni za bure. Wanarembeshwa zaidi na kuvikwa mapambo ya kila nui.

Haya yote hayamtumi kushuku anachoandaliwa, akili yake inalenga ng’ambo bado.

Muda wote wa matayarisho, hajamwona wala kuwasiliana na Bi. Mtego.

Simu nayo ilikuwa keshachukuliwa.

Hayo hayamtumi kuwa na maswali yoyote.

Hata anapogundua kwamba amevishwa nguo fupi, anawaza labda ndio ustaarabu wa ng’ambo.

Hata anabebwa na dereva wake peke yake. Anatarajia kuona uwanja wa ndege baada ya kutoka hapa. 

Mwakuona anapofika Chenga-ways, anauliza kuhusu safari yake ya ng’ambo.

Vicheko vya wanawake nyuma ya kaunta havimgutushi kuhusu shughuli za huku.

Hata anapoitwa, anainuka kwa furaha na kiherehere kumfuata mwelekezi.

Anatarajia kupelekwa kwenye uwanja wa ndege na kusahau shughuli za pale.

Akilini, imejaa taswira ya ng’ambo.

Mwakuona anapambanukiwa na mambo anapojikuta ndani ya chumba mikononi mwa mwanaume, tena mlango ushakomelewa.

Hana la kujinasua, bali inamlazimu kukubali matokeo. Sasa anagundua jinsi pupa ilivyomziba macho na kumweka hatarini. 

Pupa ya kutoroka inampata Mwakuona, na inatiliwa mkazo na rafiki yake Mashaka, anayemweleza hali iliyomkumba.

Wanakubaliana kuhepa kwa vyovyote vile na kusaka haki kwa ajili yao na pia kwa ajili ya wenzao.

Anamlaumu Bi. Mtego, mwenye Chenga-ways na wateja wa pale, na pia serikali kwa kufumbia macho biashara kama hizi.

Lakini anaapa jambo moja, chuma chao ki motoni! 

Anakumbuka ushauri wa mwalimu wake Bw. Mpevu kuhusu kufanya maamuzi yanayofaa katika maisha yao.

Anashangaa kwa nini hakufuata ushauri wake, msichana wa kidato cha tatu pale alipo, akadanganyika kwa urahisi hivyo.

Anakiri kwamba ni pupa imemwingiza humu na kujilaumu, lakini anaamua kupambana kujitoa.

Anashangaa iwapo wasichana walioandaliwa pamoja hakuna aliyejua yanayowasubiri.

Haikosi nao pupa iliwaziba macho. 

Pupa inamwezesha kutoroka Chenga-ways.

Anaingia msalani usiku wa manane na kutoka kwa haraka kupitia kwenye tundu lililoachwa na bati lililobambatuka.

Licha ya kufaulu, anakwaruza na kuvuja damu.

Anatoka na kutafuta viatu alivyotangulia kutupa nje na kupata kimoja.

Anakichukua na kutoka mbio.Anapitia upembe wenye giza asionekane. 

Japo wamemwandama, bado ana pupa ya kutekeleza maaganao yake na Mashaka.

Anaazimia kufika nyumbani na kuomba msamaha, japo hajui iwapo watampokea.

Anaazimia pia kutafuta kituo cha polisi kutafuta haki, na pia kituo cha habari kuwaanika wale mahasidi.

Kunapopambazuka, anakuona mwinamo kwa mbali.

Kuna tumaini. 

Pupa pia ndiyo inamsukuma Bi. Mtego kumtendea Mwakuona unyama ule.

Anamhadaa kwa ahadi za ng’ambo.

Nia yake ni kunufaika kwa malipo kutokana na biashara hii haramu.

Ana pupa ya kupata hela za haraka. 

Wateja wa Chenga-ways pia wana pupa ya mahaba.

Wanachagua wasichana kati ya wanaocheza densi mbele yao na hata kuwalipia kwa ajili ya huduma zao.

Pupa inawatuma kuwaharibia maisha wasichana kwa kuwakatizia masomo na kuwadhulumu kimapenzi. 

Dhamira ya Mwandishi 

Ananuia kuonya dhidi ya pupa katika maisha na madhara yake.

Anawasilisha dhiki na matatizo yanayowaandama walio katika kimo cha chini kiuchumi.

Anawasilisha ulaghai ulivyokithiri katika jamii na hasara zake.

 Anawasilisha biashara haramu zinazoendeshwa katika jamii na kudhihirisha madhara yake.

Anasawiri masaibu yanayoandama mtoto wa kike katika jamii. 

Anawasilisha umuhimu wa kuwa na fikra pevu za kugundua dalili za hatari inapokuja.  

Maudhui

Umaskini 

Mwakuona amezaliwa katika familia ya kimaskini.

Wanaishi katika mtaa duni wenye nyumba zilizojengwa karibu kwa mabati makuukuu, udongo, mahema makuukuu na hata katoni.

Zinajiinamia na kuwa na thamani ya chini kama wanaoishi huko.

Wakazi wanazaa watoto wengi, huku wakiwa na imani mmoja akifanikiwa, atatoa familia katika umaskini. 

Mwakuona anaona mengi katika maisha yake.

Ana nguo moja ambayo anafua na kungoja ikauke avae.

Wazazi wake wanataabika kuwalisha kila siku.

Yeye na ndugu zakewakubwa wanalazimika kukwangura mabaki na ukoko ili wachanga wapate angaa tonge.

Wanapatwa na utapiamlo na unyafuzi.

Nywele zinageuka hudhurungi na miguu kufanya matege.

Miguu isiyojua viatu inakaukiana na kujaa tekenya. 

Bi. Mtego anatumia umaskini wa Mwakuona kama chambo cha kumnasia.

Anamweleza kuhusu kampuni ambayo inafadhili safari za vijana kwenda ng’ambo na kuwafadhilia masomo.

Hali hii inamtia Mwakuona hamu ya maisha na kuondoka umaskini.

Anakubali rai yake.

Anaona akilini mwake maisha mazuri, vyakula vya kifahari na nguo nzuri.

Anaazimia hata kuhamisha familia yake hadi mtaa wa kifahari na kuelimisha nduguze. 

Umaskini pia unakatiza juhudi na tumaini la wazazi wa Mwakuona kumpata.

Hawajampigisha picha awali kutokana na hali yao.

Isitoshe, hawana hela za kutosha kuwasaidia polisi kumsaka au kamawanavyosema wao, ‘kuwatilia gari mafuta’ .

Wanakata tamaa ya kumwona mwanawe.

Mwakuona anapotoroka Chenga-ways, anashangaa iwapo watamkubali.

Aliondoka maskini wa mali, sasa ni maskini wa kila kitu. 

Tamaa 

Tamaa ndiyo inamwuza Mwakuona na kumtumbukiza kwenye danguro.

Anaelezwa na Bi. Mtego kuhusu kampuni ambayo inawafadhili vijana kufanya kazi na pia kuwagharamia elimu.

Hali hii inamtia Mwakuona mshawasha wa kuishi maisha mazuri.

Anaanza kujiona akiwa na maisha mazuri, akila vyakula vizuri na kuboresha maisha ya aila yake. 

Shughuli zote kutoka Mwinamo, kupelekwa matayarishoni na kufanyiwa maandalizi zinaashiria wazi kwamba hakuna ng’ambo wanayokwenda.

Hata hivyo, tamaa ya maisha mazuri haimpi nafasi Mwakuona kushuku yanyowasubiri. 

Bi. Mtego pia anamnasa Mwakuona kutokana na tamaa.

Anamtumia kama kitega uchumi kwa kumuuza kwenye danguro huko Chenga-ways.

Anamhadaa ili kupata malipo yake. Anapoingia mtegoni, anamkabidhi na kuelekea kunasa mwingine.

Wateja wa Chenga-ways pia wamejawa na tamaa ya mapenzi.

Wanawachagua wasichana miongoni mwa wale wanaocheza mbele yao na kisha kuwalipia kisha kwenda kujiburudisha nao.

Wengine wananyakuliwa bila hiari kama Mwakuona na Mashaka. Bila shaka, mwenye huku amesukumwa na tamaa ya kupata pesa haraka.

Ulaghai

Bi. Mtego anamhadaa Mwakuona kwa ahadi ya kumpeleka kazini ng’ambo na kuyaboresha maisha yake.

Anamwambia kwamba asiwaambie wazazi wake, kuwa watafahamishwa kila kitu wakati atakuwa tayari kuondoka nchini.

Mwakuona anapatiwa simu. Bi. Mtego anamhudumia kwa kila hali hadi anapotimiza azma yake na kumpeleka matayarishoni. 

Mwakuona anapofika kwenye maandalizi, anapatana na wasichana wenzake.

Hapo, wanapata huduma za kipekee.

Wanakandwa mwili na kulainishwa ngozi, huku wakilishwa vyakula vizuri.

Wanafurahia huduma hizi za bure, wakiamini wanaandaliwa kwenda ng’ambo.

Ukweli, hata hivyo, ni kwamba wanatayarishwa kuuzwa kwenye danguro. 

Mwakuona anabebwa na gari lenye dereva akiwa pekee ndani.

Anajihisi kama malkia, bila kujua yanayomsubiri. 

Anapambanukiwa na mambo hatimaye anapojipata kule Chenga-ways, mikononi mwa mwanaume ambaye amemlipia tayari.

Anaishi kule na kupitia mengi hadi anapofaulu kutoroka baada ya miezi saba.

Ufuska/ Ukware/ Uzinzi/ Uasherati. 

Bi. Mtego anamtega na kumwingiza Mwakuona kwenye danguro.

Mwakuona anajiandaa kwenda ng’ambo kama ahadi ilivyosema, lakini anapotolewa kwenye maandalizi, anaelekezwa Chenga-ways ambako biashara ya ufuska inaendeshwa.

Mwakuona anapofika, mwanamapokezi anamwambia kuwa kuna watatu wanaomng’ang’ania.

Mwakuona anafikiri anarejelea waajiri. Anasikia vicheko nyuma ya kaunta.

Hali halisi ni kwamba ni wanaume wanaomng’ang’ania ili wazini naye kwa kuwa ni mrembo sana. 

Mwakuona anawaona wanawake ambao wamevaa nusu uchi wakitembea kwa madaha mbele ya wanaume huku wakiwakagua.

Wanaume wanachagua wanaotaka, ambao wanaelekezwa katika chumba fulani. Wanaume hawa wanalipa na kuelekea kutimiza ashiki zao.  

Anapoelekezwa kwenye chumba chake, anaona wanaume wamekalia viti kama huko alikotoka, wanachagua wasichana kati ya wanaonengua viuno mbele yao, huku wamevaa viguo vinavyoning’inia viunoni. 

Mwakuona anapoelekezwa chumbani mwake, kuna wanume wanaokutana nao, ambao wanageuka tena kumwangalia.

Anakutana na msichana waliyekuwa pamoja maandalizini.

Anataka kumpiga pambaja lakini mwanamapokezi anamzuia.

Msichana yule anamwambia kuwa atajulia huko mbele.

Yeye ashayajua tayari. 

Mwakuona hatimaye anafikishwa kwenye chumba, kuongozwa ndani na mlango kukomelewa.

Anamkuta mwanamume ambaye anamsifia kwa urembo wake na kumweleza kwamba ameshalipa kwa ajili yake.

Mwakuona anajaribu kubisha akisema yeye si kahaba, lakini tayari ashafika kichijioni, hana namna ya kujiopoa. 

Mwakuona anapoondoka pale, machozi hayamkauki machoni.

Mashaka anamweleza yaliyomkuta katika danguro hilo kwa miaka miwili aliyokaa humo.

Wanakubaliana kujiopoa kutoka kwenye ufuska huu. 

Mwakuona anaishi hapo kwa miaka saba na kupitia mengi katika danguro hilo japo hatimaye anafaulu kutoroka. 

Nafasi ya Mwanamke 

Mwanamke amesawiriwa kama bidhaa au kitega uchumi.

Mwakuona anamezwa na tamaa ya maisha mazuri na kuishia kuanguka kwenye mtego wa Bi. Mtego na kuingizwa danguroni.

Bi. Mtego anamtendea haya yote kutokana na tamaa ya kujipatia hela. 

Mwanamke anachukuliwa pia kama chombo cha kumstarehesha mwanamume.

Mwakuona, Mashaka na wasichana wengine wengi wananaswa na kuuzwa kwenye danguro ili kuwahudumia wanaume kimapenzi huko Chenga-ways. 

Mwanamke pia anachukuliwa kama kifaa cha kumpandeza na kumburudisha mwanamume.

Mwakuona na wenzake wanapelekwa katika matayarisho ili kuwapendeza wateja wao.

Wanakandwa miili na kulishwa vizuri hadi wanapoimarika na kisha kupelekwa danguroni.

Huko, anawapata wanawake wanaonengua viuno na wengine kujishaua mbele ya wanaume, ambao wanawanyakua wanaowapendeza. 

Mwanamke anachukuliwa pia kama mtumwa, hasa wa kimapenzi.

Mashaka anamweleza Mwakuona mengi aliyopitia katika maisha yake pale Chenga-ways, ambapo ameishi kwa miaka miwili.

Alitwaliwa bila hiari yake, kama anavyofanyiwa Mwakuona, na bila shaka wasichana wengine wengi.

Mwakuona anapobishana na mwanamume anayemsubiri, anamweleza kwamba hana hiari, yuko mikononi mwake. 

Ufisadi 

Wazazi wa Mwakuona wanapogundua kwamba ametoweka, wanamtafuta bila mafanikio na kuamua kupiga ripoti kwenye kituo cha polisi.

Huko, hawapati msaada, kwani polisi wanawataka ‘kuwawezesha’ kumtafuta, yaani kutoa hongo au ‘kuwatilia gari mafuta’.

Hali hii inazika juhudi zao za kumpata mwanao.

 Mwakuona analaumu serikali kwa kufumbia macho biashara haramu kama inayoendeshwa huko Chenga-ways.

Anasema kwamba baadhi ya wateja huko ni maafisa tajika serikalini.

Kuna sehemu ya serikali ambayo inajua suala hili lakini haichukui hatua.

Bila shaka, kuna wanaotumia biashara hii katika serikali kujinufaisha. 

Migogoro. 

Mwakuona anajipata kwenye mgogoro na mhudumu mmoja anayemwona akitoka msalani kubadilisha mavazi, anapokuja mjini kukutana na Bi. Mtego.

Anataka kujua kwa nini yuko mjini bila sare badala ya kuwa shuleni.

Mwakuona anamjibu kwa ufidhuli kuwa hayo hayamhusu. Mwakuona yuko kwenye mgogoro na mwanamapokezi pale Chenga-ways.

Anataka kujua wakati wa ndege yake kuondoka, kwani yeye anatamani kwenda ng’ambo.

Anapokutana na msichana waliyekuwa pamoja matayarishoni, anataka kumpiga pambaja lakini mhudumu anamzuia.

Anamwelekeza moja kwa moja hadi chumbani mwake. 

Mwakuona pia anagombana na mwanamume anayemsubiri kwenye danguro.

Anamsifia kwa urembo wake na jinsi alivyofanya chaguo bora.

Mwakuona anajaribu kubisha akimwambia kwamba yeye si kahaba, lakini mwanamume huyu anamfokea, akimkumbusha kwamba amelipa hela nyingi kwa ajili yake. Hana namna ya kumhepa. 

Mwakuona anazua mgogoro kule Chenga-ways baada ya kutoroka.

Wanajua ni hatari, na lazima wamtafute asije akamwaga mtama kwenye kuku wengi.

Vyumba vyote vinapekuliwa kuhakikisha hakuna aliye na nia ya kutoroka.

Wanamwandama kwa kila mbinu; kwa magari, kwa baiskeli na hata wengine kwa miguu.

Mwakuona naye amejikunyata kando ya kijia, kiatu mkononi, tayari kujikinga.

Azma yake kuu ni kufika kwa polisi kuripoti yanayoendelea huko na kuwaanika waovu wale kwenye vyombo vya habari. 

Mwakuona pia yuko katika hali ya mgogoro na wazazi baada ya kuondoka bila taarifa.

Sasa hajui iwapo watampokea, japo azma yake kuu ni kurudi nyumbani.

Wazazi wake ni wacha Mungu, haoni kama watamkubali tena alivyo, tambara mbovu, maskini wa utu na mali. 

Dini

Licha ya kuzaliwa katika familia maskini, tunaambiwa kwamba Mwakuona alikuwa mcha Mungu, kama alivyolelewa na kuelekezwa na wazazi wake.

Hata anapoingizwa danguroni, anajuta sana kwa kuwa ni kibiritingoma wa kulazimishwa, anatenda dhambi bila hiari. 

Mwakuona anapofaulu kutoroka, bado hajasahahu suala la dini.

Anamkumbuka na kumwomba Muumba amwepushe na shari, afike asikokujua. 

Mwakuona pia anapania kurejea kwao Mwinamo baada ya kufaulu kutoroka.

Hata hivyo, linalomtatiza ni iwapo wazazi wake watamkubali tena, kwani ni wacha Mungu, naye tayari ni tambara mbovu. 

Maudhui mengine ni pamoja na Udhalimu, Kazi, Familia na Malezi, Unafiki na Ushirikiano. 

Wahusika: Sifa na Umuhimu.

Mwakuona 

Ni msomi.

Kisa hiki kinapoanza, ni mwanafunzi wa shule ya upili, katika kidato cha tatu.

Amesoma kwa taabu kufikia hapo, kwani amezaliwa katika familia ya kimaskini kwenye mtaa wa mabanda.

Ni msiri.

Tunaambiwa kuwa anapopatiwa simu na Bi. Mtego na kuagizwa isionekane na yeyote, kuweka siri si jambo ngumu kwake.

Anaitunza simu ile na kuificha kwa siku saba, isionekane na yeyote.

Anafaulu kuondoka nyumbani bila yeyote kujua wala kushuku lolote.

Ni mwenye pupa.

Anapodokezewa na Bi. Mtego kuhusu mpango wa kazi ughaibuni, anatekwa mara moja.

Anakubali kwa haraka na kutii maagizo yote ya bibi huyu hadi anapojipata matatani.

Ni mcha Mungu.

Tunaelezwa kuwa kama wakaazi wengine wa Mwinamo, Mwakuona ana imani ya kidini.

Hata anapoingizwa danguroni, inamwuma kuwa anatenda dhambi bila hiari.

Ni mwenye mapuuza.

Kuna dalili tosha kwamba Bi. Mtego anamhadaa, lakini anakosa kabisa kuzitia maanani.

Bi. Mtego anamhudumia na kumtaka aweke mipango yote siri, kisha anapoingizwa matayarishoni, bibi huyo anatoweka.

Anakumbuka ushauri wa mwalimu wake aliopuuza akiwa mashakani tayari.  

Ni mkakamavu.

Anaamua kwamba atatoroka kutoka Chenga-ways kwa mbinu zote, na anajikakamua hadi anapofaulu.

Tangu alipoanza mipango ya kutoroka, anaapa kutafuta haki, jambo ambalo anaazimia kufanya. 

Ni jasiri.

Anafaulu kutoroka kwa ujasiri kupitia tundu kwenye msala.

Hata sauti ya mtu anayosikia haimzuii kuhepa.

Anaamua kupitia njia yenye giza, tayari kukumbana na lolote. 

Umuhimu wa Mwakuona. 

Kupitia kwake, dhiki ya maisha kwa vijana wanaozaliwa na kulelewa mitaa duni inadhihirika.

Anawakilisha mashaka yanayomkabili mtoto wa kike katika maisha. 

Kupitia kwake, ukiukaji wa haki unadhihirika na jinsi unavyoendeshwa. 

Ni kiwakilishi cha pupa katika mambo na jinsi inavyoweza kuleta madhara. 

Anawasilisha nafasi ya elimu na umuhimu wake katika kujenga na kuendeleza jamii, pamoja na wasomi binafsi. 

Bi. Mtego

Ni laghai.

Anamdanganya Mwakuona kwa kumwahidi makuu; kufanya kazi ng’ambo na kusoma.

Anampa kisimu ili waweze kuwasiliana.

Hatimaye, anakichukua tena baada ya kutimiza azma yake. 

Ni mjanja.

Anamwambia Mwakuona kuwa wazazi wake wataambiwa kila kitu mambo yakishakuwa tayari.

Anafahamu vyema kuwa wakijua, mipango yake haitaenda vizuri. 

Ni mnafiki.

Anajitia urafiki na Mwakuona kama kwamba ananuia kumsaidia.

Hata hivyo, nia yake ni kumwuza kwenye danguro ili kujinufaisha. 

Ni msaliti.

Anamsaliti Mwakuona kwa kumwingiza katika biashara ya uzinzi bila hiari yake, huku akimdanganya kuwa atampeleka kazini ng’ambo. 

Umuhimu wa Bi. Mtego

Ni kiwakilishi cha wahalifu wanaojitia ufadhili ili kuendeleza maovu yao.

Kupitia kwake, nafasi ya mwanamke katika jamii inadhihirika. 

Kupitia kwake, tunabaini biashara haramu zinavyoendelezwa katika jamii.

Mashaka. 

Ni mwenye huruma.

Amamtuliza Mwakuona, ambaye ameemewa baada ya matukio ya Chenga-ways.

Anamweleza kuwa amepitia mengi pale na kumtaka kunyamaza.

Ni mwenye utu.

Licha ya kuwa amepitia mengi katika makao haya, bado hajapoteza imani.

Anaona uwezekano wa wokovu na kumtaka Mwakuona wajinasue. 

Ni mshauri.

Anamshauri Mwakuona watie bidii na kujitahidi ili waweze kutoroka sehemu ile.

Ananuia kuripoti kwa polisi na pia kutangaza kwenye kituo cha habari.

Umuhimu wa Mashaka

Ni kiwakilishi cha dhiki na matatizo wanayopitia vijana baada ya kutoswa kwenye biashara haramu katika madanguro.

Anawakilisha umuhimu wa urafiki, hasa katika nyakati za taabu.

Anawakilisha nafasi ya mwanamke katika jamii.

Mbinu za Uandishi

Tashbihi 

Nyumba nyingi za kule zilijiinamia ovyo kwa uzee, kama zinazoomba msaada kwa yeyote aliyeziona.

Ungetembea nyumbani kwao, ungedhani u shuleni kwa wingi wa watoto.

Mwakuona aliminywa na maisha mithili ya mjusi aliyebanwa na mchanja kuni katikati ya gogo na gome

....miguu ikiwa myembamba kama ya korongo,

Alikuwa msiri kama kaburi.Japo aliziona siku hizo kama mwaka, 

Nyumbani na shuleni alikuona kama jongoo na mti zilizofaa kutupwa pamoja. 

Nauli aliyoachiwa pamoja na pesa za masurufu alizitunza kama mboni ya jicho lake,

Ili asionekane kama kuku mgeni mwenye kamba mguuni, Bi. Mtego alikuwa amempa viatu vya thamani kiasi na nguo alizoficha hadi sasa. 

Mwakuona alifurahi ghaya kwa kuandaliwa kama malkia kamili.

 ...ngozi ikawa tepetepe kama ya mtoto mdogo,

...simu aliyopewa ilikuwa kama nguo ya kuazima isiyositiri makalio;

Walifuatana...amfuata mhudumu mfano wa kondoo amfuataye mchinjaji kuelekea kichinjioni.

Kila neno alilosema lilikuwa kama msumeno ukatao kuwili,...wakaona hali zao zalingana kama sahani na kawa.

“Dunia ni kama shamba la mahindi, huzaa mahindi na vizimwili.”Chenga-ways kumwachilia ni sawa na kujitia kitanzi.

Alijikunyata pembeni kama kinda aliyenyeshewa kwa kuhofia kufumaniwa kabla ya kujibabadua,

...anahema kama njiwa aliyekimbizwa na mwewe.

Anatetemeka kama kifaranga aliyenyeshewa. 

Tashihisi 

Nyumba nyingi za kule zilijiinamia ovyo kwa uzee, kama zinazoomba msaada kwa yeyote aliyeziona.

Mwakuona aliminywa na maisha…

Si kwamba aliomboleza lakini yaliyomwandama hayakumkubali kutabasamu. 

…hisani ya bibi yule ilimfunika macho, akaona kiwi, akajikuta amenasika.

Jengo la kifahari lenye jina Chenga -ways lilimkaribisha kwa taa za kumemetuka. 

Haya yote yalijibiwa kwa micheko ya wanawake asiowaona nyuma ya kaunta. Ilimdhihaki na kuhanikiza kote. 

Msichana yule…alipoona mwenzake anaelekezwa na wasiwasi umemwandama… 

Mwakuona naye, sasa wasiwasi wautikisa mwili mzima, kajikunyata pale mlangoni, nyayo zimekataa kuelekea aliko yule mwanamume mgeni. 

Kutokana na simanzi iliyomganda, machozi yamekataa kukauka…

Fadhaa na jitimai zilimwandama Mwakuona usiku kucha,Siku zimesonga, imetimia miezi saba. 

Moyo wampapa, damu ikitaka kumsaidia kupambana na hali… Kule matlai, jua linachungulia, mchana wabisha hodi.

Mbali huko, anakuona Mwinamo, bado kwainama mbele ya mitaa jirani ya kifahari.

Istiara.

Mwakuona alikuwa… mwenye heshima na bidii ya mchwa masomoni. 

Mwakuona …akakubali bila masharti, naye mvuvi akajua amekwisha mnasa samaki mkubwa. 

Bi. Mtego alipoona simu ya Mwakuona, akajua ndoano yake imenasa, chambo ki pale pale, angekitoa kinywani mwa samaki na kukitumia kunasia mwingine.

Bi. Mtego yu pale pale, nyangumi mzamisha madau. 

Kila aliyetoka mle alikuwa kivuli cha aliyeingia, amekwishabadilika kabisa…

Kwa Mwakuona, yote haya yalikuwa fumbo. 

Alimwendea mgeni wake kwa kasi, kavaa tabasamu ya chui mchekesha swara,

Anakabiliwa na mwanamume ambaye ni wazi anatokwa na mate ya fisi, yeye ni kingugwa hasa, yu tayari kumhujumu!

Mwanamume Yule alilikaribia windo lake, akamwekelea mkono begani na kujaribu kumrairai…

Bahati iliyoje kwetu sote kupatana!

Mimi mtende, wewe thamani ya hela zangu! Hana la kufanya…

Ni jogoo hapo alipo, baada ya kurushiwa punje za mtama, akazifuata…

Kwanza sharti turudi masomoni… tuwe ngome imara ya kuupinga udhalimu huu. 

Maneno haya yaliyoleta dalili za mwanga gizani yalizibadilisha shake za Mwakuona zikabaki sinasina.

Haya aliyaona kuwa maji yaliyokwisha mwagika, hayazoleki.

Hata kama anajihisi kuwa tambara bovu, ni tambara lao.

Labada watalishona au hata walitumie kutandika mlangoni ua kupangusia nyayo.

Chenga- Ways nako, shughuli zote zimekwama.

Bidhaa muhimu, mhimili wa biashara , umetoweka.

Semi

zilizojengwa kigugu- zilizojengwa kwa ukaribu.

kuzipa tabu kisogo- kuziacha tabu, kuzisahau au kuziondokea.

akaona kiwi-akaona giza.

yalikuwa ya kumtoa nyoka pangoni- yalikuwa ya kuvutia.

Hayakuhusu ndewe wala sikio- hayakuhusu kwa vyovyote vile.

wakitembea mzofafa- wakitembea kwa kujishaua.

alipiga moyo konde- alijikaza, alijikakamua.

asizozilalia wala kuziamkia- zisizomhusu hata kidogo.

kumpiga pambaja- kumkumbatia.

kumtilia chambo- kumshawishi ili kumnasa.

akiambua nyayo- akitembea kwa miguu.

apige unyende- apige duru, atoe kelele.

apige hatua- afanye jambo, afanye uamuzi.

watapigwa kalamu- watafutwa kazi. 

Methali 

Kuzaa mwana si kazi, kazi ni kulea.

Ng’ombe mkubwa ndiye hulalia miba,

Usimwage mtama penye kuku wengi.

Nyumbani na shuleni alikuona kama jongoo na mti zilizofaa kutupwa pamoja(amtupaye jongoo humtupa na mti wake)

Ili asionekane kama kuku mgeni mwenye kamba mguuni(kuku mgeni hakosi kamba mguuni)

Dau la mnyonge haliendi joshi.Kuku wa maskini huliwa na kanu majirani wakiangalia. 

Hayawi hayawi huwa.Ilikuwa sawa na nguo ya kuazima isiyositiri makalio(nguo ya kuazima haisitiri matako)

Cha kuzama hakina rubaniKilichompata ngwena na kiboko ni chicho.

Mbwa hafi maji aonapo ufuo.Nyumbani ni nyumbani.Ng’ombe akivunjika mguu malishoni hujikokota hadi zizini kufaliwa na wenzake wazima. 

Maswali Balagha 

…si mapya na ya thamani bora ameyakumbatia kiganjani? 

Alimwendea alipokuwa, jambo lililomduwaza Mwakuona- iweje anayemsaidia ndiye anayemtumikia?

Nani asingefurahia huduma hii ya kifahari, tena ya bure?

 “Kuning’ang’ania?... mbona hamkufanya uamuzi mapema kuhusu mwajiri wangu?

Ni wa nchi gani? Nasafiria ndege gani?

Safari yangu ni ya saa ngapi? Mshahara wangu ni kiasi gani?” 

“Hii ndiyo kazi ya ng’ambo niliyodanganywa naenda kufanya?”

 Zingali tumboni wala hazimfai tena…

kupigapiga mabawa kutamfaa nini? 

“Dunia ni kama shamba la mahindi…

Utakwendaje kuvuna ukakusanya vizimwili badala ya mahindi na kuvipeleka ghalani?” 

Vipi yeye, mwanafunzi wa kidato cha tatu, asikumbuke ushauri wa shuleni, nyumbani na maabadini, akafanya uamuzi wa busara? 

Mbele kuna pande mbili, wenye giza totoro na kwingine kuna mwangaza.

Afuate njia ipi aepuke zahama? 

Aelekee upande gani afike kule?

Tena akifika, aila yake itampokea?  

Bwana na Bi. Mtondo, wazazi wacha Mungu, watampokea mtoto ajaye akivalia kibiritingoma?

Jamii itamkubali akija mkono tupu baada ya miezi saba?  

Hata kama ni kazi ya ujakazi, aje bila chumvi mkononi, hana hata senti ya kusagia mkunguni?

Hadithi za mengi mabaya aliyopitia zitawafaa nini? 

Walikuwa na mpango kabambe ila sasa mwenzake yu wapi? 

Majazi 

Mwakuona- Binti huyu anayaona mengi katika maisha yake. Anazaliwa katika familia ya kimaskini na kukabiliwa na matatizo chungu nzima. Hatimaye, anahadaiwa na kuingizwa danguroni.  Anapotoroka, anaandamwa na kufikia tamati ya hadithi, hatujui anayaona mengine kiasi gani. 

Mwinamo- ina maana ya kupinda kwenda mbele.  Ni mtaa duni ambao una vyumba vibovu. Mtaa huu ‘umeinama’ kutokana na dhiki ya wanaoishi huko. Tunaambiwa kuwa Mwakuona, “…anakuona

Mwinamo, bado kwainama mbele ya mitaa jirani ya kifahari.” 

Bwana na Bi. Mtondo. Mtondo ni siku baada ya kesho kutwa.  Hawana matumaini ya kuimarika. Wanajishughulisha kupata lishe ya siku, ya mtodo hayawahusu. Fanaka yao haipo leo wala kesho, labda mtondo. Mwakuona wao anapopotea, matuamini yao pia hayapo leo wala kesho. 

Bi. Mtego- ni mbinu inayotumika kunasa. Anamwekea Mwakuona mtego na kumnasa kisha kumtumbukiza kwenye uzinzi. Bila shaka anafanyia wengine hivyo. Anapomtia matayarishoni, anatoweka, bila shaka kuwawekea mtego wengine.

Chenga-ways- Maanake ni nia zisizo wazi. Wanaofikishwa pale wanafanyiwa hivyo kwa kuchengwa. Mashaka anatamani kutoroka lakini njia za kufanya hivyo zinaishia kuwa chenga sana kwake. Mwakuona analazimika kutumia chenga chenga kutoroka, lakini bado kuna chenga kwani anaandamwa kinyama. 

Uwezekano wa kufaulu kutoroka bado ni chenga. 

Kazamoyo- shule anakosomea Mwakuona. Ni shule ya watoto wa maskini ambao wanalazimika kukaza moyo katika maisha yao. Mashaka- ina maana ya taabu anazopitia mtu katika maisha. Msichana huyu amepitia mengi pale

Chenga-Ways baada ya kutoroshwa kama Mwakuona na jitihada zake za kuhepa kutofanikiwa.

Bwana Mpevu- ni mwalimu wa Mwakuona. Ana mawazo mapevu kulingana na ushauri anaowapa. Anawataka wawe wapevu ili wafanye maamuzi ya busara. 

Uzungumzi Nafsia 

Sasa zahitaji tu kupelekwa saluni zioshwe kwa shampuu, zisingwe na kulainishwa kwa kitana moto.

Miguu ikivishwa nguo za kazi na viatu vya mchuchumio, basi! Aliwaza yule wakala.Masomo bila uwezo ni bure!

Aliwaza.Ila alijihimiza, “Chuma chao ki motoni!”Pupa imenitumbukiza katika kisima nilichochimba, sasa naingia mwenyewe

…Mara kwa mara aliwakumbuka aliokuwa nao ‘matayarishoni’.

Waliyajua haya au walikuwa mateka kama mimi? Mbona pasiwe na hata mmoja mwenye hekima atakuramshe, tutunge mbinu za kujinasua?

Koja

Mwakuona alikuwa mtiifu, mcha Mungu, mwenye heshima na bidii ya mchwa masomoni.

 …hisani ya bibi yule ilimfunika macho, akaona kiwi, akajikuta amenasika.

Mwakuona aliposikia matumaini ya utajiri na masomo, alichanganyikiwa, akakubali bila masharti, naye mvuvi akajua amekwisha mnasa samaki mkubwa. 

Msichana wetu aliona vyakula alivyotamani kama pizza, nguo za bei, rangi za kucha na za midomo, wanja machoni, kope na kucha za kubandika, mitindo ya kisasa ya nywele na urembo aina anuwai.

Aliona mashangingi, akaona kasri, akaona ameheshimika katika jamii. 

Kwa akraba yake, aliona akiwanunulia nguo za bei, vyakula aina aina, akaona akiihamishia kwenye mtaa wa kifahari, akiwaelimisha nduguze. 

Asubuhi ya miadi ilikuwa na changamoto si haba- kujiandaa kama aendaye shuleni, chengachenga, kuvizia kwingi, kudanganya huyu na yule ili kufika mjini. 

Kazi ikawa kula na kunywa vinywaji mzomzo, huku miguu ikisuguliwa kwa vifaa maalum vya kielektroniki, kutengenezwa nywele, kulainishwa uso kwa mvuke na mafuta ainaina kisha kusingwa na kukandwa mwili ili ulainike.

Kila aliyetoka mle…amekwishabadilika kabisa- mwili umelainika, ngozi ikawa tepetepe kama ya mtoto mdogo, nyusi zimenyolewa na kuchorwa upya na wasanii maalum wa urembu huku kope ndefu zimepandikizwa kwenye vikawa vilivyopakwa wanja uliofanana na rangi ya midomo. 

Alimwendea mwenzake kwa kasi, kavaa tabasamu ya chui mchekesha swara, mikono kapanua, ataka kumpiga pambaja.

Mwakuona naye, wasiwasi sasa wautikisa mwili mzima, kajikunyata pale mlangoni, nyayo zimekataa kuelekea aliko mwanamume huyu mgeni. 

Akili zake ziliupitia mzingile… tabu za nyumbani, masomo shuleni Kazamoyo, Bi. Mtego, ‘ng’ambo’,chumba cha ‘matayarisho’, mapokezi ya pale alipo na hatimaye zikatua kwenye chumba alimokuwa sasa.

Yule mwanamume… kuusifu urembo wake- umbo lake, urefu, ngozi, nywele na umri! 

Ni jogoo hapo alipo, baada ya kurushiwa punje za mtama, akazifuata, akazidonoa, akazimeza kwa pupa, akanaswa.

Zingali tumboni wala hazimfai tena, kisu chamwelekezea makali shingoni, macho kayatoa pima- kupigapiga mabawa kutafaa nini?

… walisimuliana hali zilizowaleta mle, wakapelekana utotoni, masomoni, wakona hali zao zinalingana

……elimu inawasaidia kupata akili tambuzi, wachuje, watwae vifaavyo na kuacha vibaya.

Aliushika mtambaapanya, akavuta nguvu zake zote na kujinyanyua, akachupa hadi nje. Amekimbia kwa muda wa takriban saa nzima, kalowa jasho chepechepe, anahema kama njiwa anayekimbizwa na mwewe.

Atatafuta kituo cha polisi, labda kwa msaada wa jamii yake, apige ripioti, asimulie yote yanayotendeka Chenga-ways.

Aliamini polisi wangechukua hatua, wawanusuru maskini wenzake na kuiangamiza biashara ile haramu

.…alilenga kutafuta yalipo mashirika ya habari, asimulie yaliyomfika, wahalifu wale waanikwe.

Moyo unampapa, damu ikitaka kumsaidia kupambana na hali, autazame mstakabali wa maisha yake.

Kuchanganya Ndimi

. …aliona vyakula alivyotamani kama pizza…Gari la kifahari lilimjia; atakuwa chauffer- driven, yeye pekee anabebwa back- left, afunguliwa mlango!

“Kuna watatu wanaokung’ang’ania, you are a hotcake.”“Kindly tell me, mbona hamkufanya uamuzi mapema…” 

Kabla ya kuandama chaguo lake, mwanamume angeenda kulipa palipoandikwa Pay here.

Akasikia mmoja… akisema kwa sauti ya furaha,

“Give me this beautiful queen of all slay queens… she’s wow!”

Alitaka kumsalimu ila mwelekezi wake akamwambia, “Not now!” 

Taswira 

Taswira ya mtaa wa Mwinamo, hasa majengo yake yaliyokaribiana yaliyojengwa kwa mabati makuukuu, udongo, mahema na hata katoni na karatasi. 

Taswira ya watoto wa Mwinamo wenye utapiamlo na unyafuzi, nywele za hudhurungi, miguu myembamba yenye tekenya wala isiyovishwa viatu, iliyokaukiana na kuunga matege. 

Taswira ya Mwakuona na wasichana wenzake wanapotoka matayarishoni. Wametiwa vipodozi na mapambo ya kila aina, na kubadilika kuwa wa kuvutia. 

Taswira ya pale mapokezini ya wasichana wanaosakata densi huku wengine wakijishaua mbele ya wanaume wanaowateua watakao. 

Taswira ya Mwakuona na mwanamume anapoingizwa chumbani na mlango kufungwa.

Taswira ya mwanamume yule akimwendea na jinsi Mwakuona anavyomwambaa kwa hofu na jakamoyo tele. 

Taswira ya Mwakuona anapotoroka kutoka Chenga-ways kupitia kwenye tundu msalani, kuvitupa viatu nje, changamoto anazopitia hadi hatimaye kufaulu kutoka humo. 

Taswira ya Mwakuona akitoroka.

Mbele yake anapata njia mbili, moja yenye giza na nyingine mwangaza na kuamua kupitia gizani.

Anakimbia huku amelowa jasho na kupumua kwa nguvu. 

Taswira ya Mwakuona tena mwishoni mwa hadithi; “Mwakuona angali anajikunyata nyuma ya kisiki.

Baridi shadidi inamguguna.

Anatetemeka… Moyo wampapa, damu ikitaka kumsaidia kupambana na hali…

Kule matlai, jua linachungulia, mchana wabisha hodi.

Mbali huko, anakuona Mwinamo, bado kwainama mbele ya mitaa jirani ya kifahari!Kisengerenyuma. 

Mwakuona anapokutana na Bi. Mtego anayempa habari za kampuni inayowaajiri vijana, anakumbuka tabu alizopitia maishani na kuona fursa ya kuziondoka. 

Mwakuona anapotolewa matayarishoni, anakumbuka kuwa hajawahi kumwona Bi. Mtego wala kuwasiliana naye, kwa kuwa hata simu aliyopatiwa ilikuwa kanyakuliwa. 

Mwakuona anapokabiliana na mwanamume katika danguro, anakumbuka matukio yaliyomfikisha hapo kuanzia tabu za nyumbani, masomo shuleni Kazamoyo, Bi. Mtego, ahadi za kwenda ng’ambo, matayarishoni na hatimaye alipo sasa.

Mwakuona na Mashaka wanapatiana hadithi za jinsi walivyotekwa na kutumbukizwa walipo na kuelezana waliyopitia maishani mwao, ikiwemo utotoni mwao na masomoni. 

Mwakuona anajilaumu kwa kuanguka mtegoni mwa Bi. Mtego.

Anakumbuka ushauri wa mwalimu wake, Bwana Mpevu kuhusu kufanya maamuzi ya busara na maonyo aliopatiwa shuleni, nyumbani na maabadini.

Anawakumbuka pia wasichana aliokuwa nao matayarishoni na kushangaa iwapo walijua yaliyowasubiri. 

Akiwa mbioni, Mwakuona anakumbuka makubwa aliyopitia Chenga-ways. Anakumbuka jinsi anavyotoroka baada ya kufaulu kuingia msalani bila kuandamwa, na kufaulu kutorokea kwenye tundu la msala.

Anamkumbuka pia na Muumba wake na kumwomba amwepushe na shari.

Mwakuona pia anakumbuka maagano yake na Mashaka kuhusu kutafuta haki yao na wenzao kwa yeyote atakayefaulu kutoroka, jambo analoazimia kutekeleza. 

Kinaya

Wakazi wa Mwinamo, licha ya kuwa wanazugwa na umaskini, wanakopoa watoto wengi.

Wanaona kuwa wanaweza kupata wa kuwafaa kati yao.

La ajabu ni kuwa hawawazii jinsi watakavyowalisha watoto hao kwa hali hiyo. 

Rai ya Bi. Mtego kuwa Mwakuona asiwajuze wazazi wake haimpigi mshipa.

Ni kinaya kwake kushikilia kuwa wazazi hawafai kujua hadi mipango inapotamatika.

Kwa nini wasijue hali ni mwanao?

Ni wazi kwamba huu ni unafiki lakini Mwakuona hatambui hilo. 

Ni kinaya kuwa Mwakuona haoni dalili zote kuwa Bi. Mtego anamhadaa.

Anayemsaidia bado ndiye anamhudumia, jambo ambalo halimpigi mshipa.

Hata wanapofika kwenye danguro, bado akili yake inamwambia kuwa anaenda ng’ambo wala yanyotukia pale hayamhusu. 

Mwakuona anamwuliza mhudumu kwenye kaunta kuhusu safari yake ya ng’ambo.

Anashangaa kwa nini hawakuamua kuhusu mwajiri wake anapoambiwa kuna watu watatu wanaomng’ang’ania.

Ni wazikwamba haya ni masuala tofauti na kazi ya ng’ambo.

Hawazii haya angaa kujaribu kujinasua.

Ni kinaya kuwa kati ya wasichana wengi waliokuwa matayarishoni, hakuna hata mmoja aliyewaza kuhusu waliyokuwa wakiandaliwa, licha ya dalili kuwa wazi. 

Mwakuona anaondoka nyumbani kwa matumaini makuu ya kuiboresha hali yake na ile ya aila yake.

Ajabu ni kuwa badala yake, anarejea akiwa maskini zaidi, wa mali na utu! 

Sadfa

Mwakuona anakutana na Bi. Mtego kisadfa akitoka shuleni bila kumtarajia. 

Mwakuona anapomfuata mwelekezi kuelekea asikokujua, anakutana kisadfa na msichana waliyekuwa pamoja kwenye ‘matayarisho’ japo hawapatiwi fursa ya kuwasiliana. 

Mashaka na Mwakuona wanakutana kisadfa, baada yake kuhujumiwa kule danguroni.

Wanaishia kuwa na kisa kinacholingana na kuwa marafiki wa kutiana moyo. 

Mwakuona anafaulu kutoroka kisadfa.

Anaenda msalani usiku wa manane bila kuandamwa, kinyume na taratibu.

Isitoshe, inasadifu kuwa choo hicho kiko pembeni na kina bati lililobambatuka, linalompa mwanya wa kuhepea.

Wakati wa kutoroka, anamsikia mtu upande wa pili akikemea kisha vishindo vyake akitoroka.

Hakutarajia kumpata yeyote pale wakati huo. 

Mwakuona anatoroka usiku wa manane na kujaribu kutafuta njia ya kurudi kwao Mwinamo asiijue.

Kunapopambazuka na jua kuchomoza, anakuona Mwinamo kwa mbali.

Taharuki

Kulingana na maelezo ya Bi. Mtego, ni wazi kwamba anamdanganya Mwakuona wala hakuna ng’ambo anakompeleka.

Tunaachwa na hamu ya kujua ni wapi hasa ananuia kumpeleka baada ya hadaa zote. 

Wazazi wa Mwakuona wanakosa tumaini la kumpata mwanao kwa kukosa mbinu ya kumtafuta na msaada wa polisi kukosekana.

Hatujui iwapo wanaendelea kujaribu kumsaka au wanamwacha tu. 

Baada ya kutolewa kwenye ‘matayarisho’, anatarajia gari lielekee kwenye uwanja wa ndege lakini linalenga asikokujua.

Kama Mwakuona amwenyewe, tunasalia na hamu ya kujua wanakoelekea. 

Mwakuona anapokumbana na mwanamume anayemsubiri, anasema kuwa alimchagua yeye kati ya wengi.

Hatujaelezwa vipi alimfahamu, kupitia kwa Bi. Mtego au wakati wa maandalizi.

Isitoshe, mhudumu anasema kuwa kuna watu watatu wanaomng’ang’ania.

Hatujui hao wengine ni wepi, na mbinu gani inatumiwa kuamua atakayemchukua.

 Mwakuona akiwa katika harakati za kutoroka, anasikia sauti inayomtia kiwewe.

Baadaye tunafahamu inatokana na bati lililobambatuka.

Hata hivyo, hatujafahamishwa kwa uwazi ni nani aliyesonya na kutoroka baada yake kutupa viatu nje, tena alikuwa akifanya nini hapo wakati kama huo. 

Mwishoni, tunabaki na maswali tele.

Je, rafikiye Mwakuona, Mashaka, bado yuko kule danguroni?

Atafaulu kutoroka?

Na je, Mwakuona anarejea nyumbani?

Wazazi wake na wakazi wengine wanampokea vipi?

Wanamkubali katika jamii yao? Watamhurumia na kumfariji au kumlaumu na kumfokea?

Na je, anafaulu kutimiza maagano yake na Mashaka?

Iwapo atafaulu kufika kituo cha polisi na hata cha habari kutoa taarifa, wahalifu wale watachukuliwa hatua?

Mashaka, Mwakuona na wenzao watapata haki? N.k 

Jazanda 

Dau tokomevu aghalabu humshawishi mpiga kafi kuelekea kwenye mawimbi.

Dau linapopigwa na dhoruba, kujaribu kuyakumba maji huwa jitihada isiyo na mazao.

Kuangamia hakuwi mbali.

Papa na nyangumi husubiri azamaye azame, wamtie kinywani.

Ni jogoo hapo alipo, baada ya kurushiwa punje za mtama, akazifuata, akazidonoa, akazimeza kwa pupa, akanaswa.

Zingali tumboni lakini hazimfai tena, kisu chamwelekezea makali shingoni, macho kayatoa pima- kupigapiga mabawa kutamfaa nini?

Kuna kufa na kupona na kuliwa na kingugwa.

“Dunia ni kama shamba la mihindi, huzaa mahindi na vizimwili.

Utakwendaje kuvuna ukakusanya vizimwili badala ya mahindi na kuvipeleka ghalani?”

Mbinu nyingine ni kama vile Nidaa, Mdokezo, Tanakali, Takriri na Dayolojia.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Pupa summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?