KISWAHILI KARATASI YA 2 - 2019 KCSE Prediction Questions Set 2

Share via Whatsapp

MAAGIZO:

  • Jibu maswali yote.
  1. UFAHAMU
    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.

    Kama mvulana aliyezaliwa, kulelewa na kukulia kijijini, mtagusano wangu na wanyamapori ni mpana. Pamoja na ndugu zangu tulikuwa tukiwafukuza ndovu walipovamia shamba letu kuharibu mimea, hasa wakati wa usiku kwa kutumia mienge ya mto. Fisi nao hawakuwa wageni machoni petu. Mara kwa mara, walikuwa wakipitia kando kando ya nyumba yetu na tulikuwa tukifurahia sana tulipowafukuza kuelekea mbugani. Nyani na tumbili walikuwa kama ndugu zetu kwani kila mara tulipobakisha chakula tungewarushia.Kwa ufupi, maisha ya ujanani na utangamano na wanyama hawa yalikuwa ya kuridhisha sana. Lakini mvurugiko wa utangamano huu ulianza tu ubinafsi ulipomwingia binadamu.Mbegu hii mbaya ilimgeuza binadamu kuwa katili, hasidi na mchumaji asiyejali madhara ya anakopania kupata lishe lake.

    Wanyama hawa wamegeuzwa kuwa wahasiriwa wa tamaa ya mwanadamu wanauawa kila siku huku mamlaka zilizowajibishwa kuwalinda zikizidi kutepetea na kutojali. Ni fedheha kuu kwa shirika la wanyamapori nchini (KWS) kwani ni kama limeshindwa kuwalinda wanyama hawa hasa ndovu, vifaru na simba. Pembe zao ndizo zimekuwa zikiwaongoza kwa mauti yao, nazo dhana kuwa zinatibu magonjwa kama zinaa na saratani zinachangia pia. 

    Jamii zetu zinapaswa zielimishwe kutangamana na wanyama hawa; si maadui, ni marafiki wazuri. Hadithi za mababu zetu zinapaswa kuibua hisia za kujali miongoni mwetu. Hata kama wanavamia mimea na mifugo yetu, makosa si yao bali ya mamlaka simamizi. Simba anapohisi njaa na ua wa mbuga anayoishi haujatengenezwa ifaavyo, sharti ajitafutie njia ya kujishibisha na watoto wake kama vile walivyotufanyia mama zetu. Tutazilaumu mamlaka hizo, kama KWS, bali si mnyama.

    Kwa hivyo, kwa binadamu razini kuchomoa silaha kusudi kumuua kifaru au ndovu, ni uhayawani - yeye binadamu ndiye amegeuka kuwa mpungufu wa shufaka. Ni kutokana na wanyama hawa ambapo wazungu humiminika nchini kuwatazama, ni sababu yao ambapo nchi hii hupewa tuzo za ulinzi wa mazingira; ni uwepo wao ambapo baadhi ya tamaduni za kikale za jamii zimeendelea kudumu hasa vipera vya fasihi simulizi kama ngano, visaviilini nk. Mbona basi tuwahasi? Mbona tuwavamie viumbe hawa wasiofahamu lolote? Mbona tumejitia hamnazo, hadi kukosa kuona uhai? Huu ndio ustaarabu? Kwa yote naulamu ubepari, na roho ya ubinafsi uliomwingia mwanadamu. Hata hivyo tufikirie kuhusu mustakabali wetu na maisha ya vizazi vijavyo. Turejelee maisha ya kizamani kwa kutowaua wanyama hawa.

    MASWALI
    1. Ipe taarifa hii kichwa mwafaka:- (alama.1)
    2. Eleza uhusiano uliokuwepo kati ya msimulizi na wanyama pori kijijini. (alama 2)
    3. Ni kitu gani kiliharibu uhusiano unaorejelewa katika swali 2? (alama 2)
    4. Mamlaka yanayolinda wanyama hayawajibiki. Thibitisha. (alama 2)
    5. Taja sababu zinazopelekea kuuawa kwa wanyama pori. (alama 2)
    6. Taja faida za wanyama pori. (alama 2)
    7. Mwandishi anapendekeza suluhisho gani kwa tatizo lililozungumziwa katika kifungu? (alama 2)
    8. Eleza maana ya vifungu hivi vya maneno kama vilivyotumika katika taarifa. (alama 2)
      1. Kujitia hamnazo
      2. Kutangamana.

  2. UFUPISHO (Muhtasari) (Alama 15)

    Biashara ya kimataifa ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote ile. Nchi mbalimbali zimekuwa zikitegemea kwa namna moja au nyingine. Kwa mfano, nchi ya Kenya imekuwa ikiuza maua na mboga katika nchi za ng’ambo na kupata fedha za kigeni ambazo hutumiwa humu nchini kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

    Biashara ya kimataifa huziwezesha nchi ambazo hazizalishi bidhaa na hata huduma mbalimbali kupata bidhaa hizo kutoka nchi nyingine zinazohusiana nayo katika biashara. Mathaian, Kenya ni nchi ambayo imekua ikitegemea kilimo lakini hiajaendelea katika sekta ya viwanda. Kenya huagiza bidhaa kama vile vipuri vya magari na hata magari yenyewe kutoka nchi kama vile japan. Nayo Kenya huuza mazao ya shambani kama vile pareto, chai na kahawa ng’ambo. 

    Kupitia kwa biashara ya kimataifa, nchi hupata masoko kwa bidhaa zake. Kwa vile biashara ya kimataifa huziwezesha nchi husika kuzalisha kiasi kikubwa cha bidhaa kuliko mahitaji yake ya nyumbani. Nchi basi hulazimika kutafuta masoko nje ya mipaka yake. Kwa njia hii uchumi wa Nchi huendelea kuimarika.

    Aidha, biashara ya kimataifa huwezesha nchi kupata huduma za kitaaluma ambazo hazipatikani katika nchi husika. Kuna Nyanja za kiuchumi huhitaji wataalamu mahususi. Kwa mfano, katika sekta ya matibabu nchini humu tumepata kwamba kuna baadhi ya magonjwa haya huagiziwa madaktari kutoka ng’ambo au hata kupelekwa ng’ambo kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

    Biashara ya kimataifa hukuza ushurikiano wa kimataifa. Nyakati za majanga ya kimaumbile na hata mengine yanayosababishwa na kutowajibika kwa binadamu, nchi hupata usaidizi kutoka nchi za ng’ambo. Kwa mfano wakati wa mkasa wa bomu wa 1998, Kenya ilipata msaada wa kukabiliana na janga hili kutoka Israeli, Marekani na hata Ujerumani ambako baadhi ya waathiriwa wa mkasa huo walipelekwa kwa matibabu zaidi. Ushirikiano huu wa kimataifa huwezesha wananchi kutoka nchi fulani kwenda kusomea na hata kufanya kazi katika nchi nyingine. Katika miaka ya hivi karibuni wakenya wengi wamekuwa wakienda kusomea vyuo vikuu vya ng’ambo. Wengine wamediriki kupata kazi katika mashirika ya kimataifa katika nchi mbalimbali kama vile afrika kusini, Rwanda, Msumbiji na kadhalika.

    Biashara ya kimataifa husaidia kukuza ushindani kati ya nchi husika. Ushindani huu ni hakikisho la uzalishaji wa bidhaa za thamani bora. Kila nchi itafanya juu chini kuzalisha bidhaa ambazo zinaweza kukubalika katika soko la kimataifa. Pia wananchi wa nchi husika hupata aina tofauti za bidhaa badala ya kutegemea aina moja tu ya bidhaa zinazozalishwa nchini mwao.

    Biashara ya kimataifa huleta ushirikiano wa kisiasa na uelewano zaidi kati ya madola mbali mbali. Mathalan muungano wa nchi za afrika mashariki – Kenya, Uganda na Tanzania, hauchangii tu kuleta manufaa ya kiuchumi bali huleta ushirikiano zaidi wa kisiasa. Ingawa biashara ya kimataifa ina natija, biashara hii huandamana na hasara mbalimbali. Biashara hii imesababisha kuwapo kwa masoko huru ambayo yameleta ushindani mkubwa kwa wafanyibiashara wadogo humu nchini. Baadhi ya wafanyi biashara wamelasimika kufunga biashara zao baada ya kufilisika. Ushuru mkubwa unaotozwa baadhi ya bidhaa zinazoingia nchini huwafanya wananchi wengi kutofaidika kwa bidhaa na huduma kutoka nke. Aidha, kuna uchelewashaji wa bishaa zilizoagizwa. Bidhaa hizi mara nyingi huchukua muda kabla ya kutoka nchini, kwa hivyo wafanyi biashara wengi hulazimika kungojea kupata bidhaa hizi za kuwauzia wateja wao.

    Vilevile, kutokana na biashara ya kimataifa bidhaa duni huweza kupenyezwa katika mataifa yanayoendelea. Pia baadhi ya wafanyi biashara wa kimataifa huchukua fursa hii kulangua dawa mbalimbali za kulevya ambazo huwaathiri vijana wan chi husika. Wengine uhusika katika vitendo vya kigaidi. Kama vile uchomaji wa majengo mbalimbali kwa bomu na mauaji ya wananchi wasio na hatia. Ni kweli kuwa biashara ya kimataifa ina hasara zake. Hata hivyo mhimili mkubwa wa uchumi wa mataifa machanga.

    Maswali
    1. Kwa maneno yasiyozidi themanini eleza umuhimu wa biashara za kimataifa (alama. 7, mtiririko 1)

      Matayarisho/Nakala chafu
      …………………………………………………………………………………………………………
      …………………………………………………………………………………………………………
      Jibu/Nakala safi
      …………………………………………………………………………………………………………
      …………………………………………………………………………………………………………
    2. Kwa maneno yasiozidi 40, eleza ujumbe wa aya ya tatu za mwisho (alam. 6, utiririko 1)

      Matayarisho/Nakala chafu
      …………………………………………………………………………………………………………
      …………………………………………………………………………………………………………
      Jibu/Nakala safi
      …………………………………………………………………………………………………………
      …………………………………………………………………………………………………………
  3.  MATUMIZI YA LUGHA (AL. 40)
    1. Bainisha sifa mbili za kitamkwa kifuatacho /n/. (al. 2)
    2.  Ainisha mofimu katika neno lifuatalo. (al. 3)
      Sikumkaribisha
    3.  Andinka kwa msemo wa taarifa. (al. 3)
      "Maria! Mama! Njoo hapa,’’ Mama akamwita, "Kesho nitaenda Nairobi, kesho kutwa Kisumu na sasa ninaenda huko sokoni.’’
    4. Virai vilivyopigiwa mstari katika sentensi ifuatayo ni vya aina gani. (al. 2)
      Walimu wote hutupatia mtihani mara kwa mara.
    5. Eleza maana mbili zinazopatikana katika sentensi hii. (al. 2)
      Huyu amekuja kutuliza.
    6. Taja sifa mbili za sentensi ya Kiswahili. (al. 2)
    7.  Onyesha matumizi ya -ni katika sentensi hii. Niliyemsaidia ni huyu lakini sasa simameni
      muende uwanjani . (al. 2)
    8. Tumia kihusishi mpaka katika sentensi ili kuonyesha uhusiano wa: (al. 2)
      1. Mahali
      2. Wakati
    9. Nomino zifuatazo ni za ngeli gani? (al. 1)
      1. Mawingu
      2. cheki
    10.  Nyambua vitenzi vifuatavyo katika kauli zilizo kwenye mabano. (al. 2)
      1. Pa (kutendeka)
      2. Pokea (kutendwa)
    11. Andika upya sentensi zifuatazo kwa kuzingatia maagizo (al. 2)
      Hatutaki hizi wala zile (maliza kwa tunazotaka)
    12. Onyesha aina mbili ya shamirisho. (al. 2)
      Kamau alimjengea baba yake nyumba kwa matofali.
    13. Andika sentensi ifuatayo ukizingatia kinyume cha maneno yaliyopigwa mstari (al. 2)
      Mizigo hiyoitatolewa kwenye makasha na kupakiwa taratibu .
    14. Andika katika wingi:
      Nywa (al. 1)
    15. Tafautisha baina ya kiwakilishi nafsi tegemezi na nafsi huru kwa kutolea mifano. (al.2)
    16. Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya mistari. (al.4)
      Mwizi aliyetuibia jana amekamatwa hatimaye.
    17.  Fafanua maana ya kishazi. (al. 1)
    18.  Tofautisha maana baina ya vitate vifuatavyo:
      Randa na landa. (al. 2)
    19. Onyesha aina ya vitenzi katika sentensi ifuatayo.
      Fundi ndiye yule na ndiye atamjengea nyumba. (al. 3)
  4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
    1. Elezea sifa zozote nne za sajili ya siasa. (al. 4)
    2. Eleza tofauti kati ya lahaja na lafudhi. (al. 2)
    3. Fafanua mambo manne ambayo yanaweza kufanywa ili kuendeleza matumizi na ukuaji wa Kiswahili nchini. (al. 4)
Join our whatsapp group for latest updates

Download KISWAHILI KARATASI YA 2 - 2019 KCSE Prediction Questions Set 2.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest