Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Bondo Joint Mocks Exams 2022

Share via Whatsapp

Maswali

Maagizo

  • Andika jina lako na nambari yako ya mtihani katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  • Majibu yote sharti yaandikwe kwenye nafasi ulizoachiwa katika kijitabu hiki cha maswali.

1. UFAHAMU: ( Alama 15)
Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.

             Ulikuwa wakati wa jioni jua limepunguza udhia wake na upepo mwanana ulikuwa ukipita na kuzipapasa Ngozi zetu mfano wa pamba. Kama ilivyokuwa desturi yetu pale chuoni, siku hiyo tuliketi karibu na lango kuu la chuo ili kutafiti kazi mradi tuliyokuwa tumepewa darasani. Sehemu hii tuliipenda sana kwa
kuwa kuuchakura mtandao ilikuwa ni bure bora tu ufahamu nywila ya mtandao huo. Mandhari ya sehemu hii pia yaliwavutia wanafuzi wengi katika sehemu hii.
             Tulipotia fahamu, tulipata mazoea haya yamekita mizizi nasi tukawa hatuna budi kuyakumbatia. Hatukuyakumbatia tu, bali tuliyakumbatia kwa dhati ya moyo. Vikao hivi havikuwa tu hazina kubwa kwetu bali pia vilikuwa vya thamani isiyomithilika. Hapa ndipo tulinoleana bongo kwa kupashana habari. Leo hii tumo katika mjadala kuhusu kuhusu mfumo mpya wa elimu CBC tuliopewa darasani kama kazi mradi. Nahodha wa kikundi hiki anampa msemaji wa kwanza nafasi naye hakusita kushika usukani.
             “Nionavyo mimi, mfumo wa CBC unafaa kufutiliwa mbali. Serikali haijajiandaa vilivyo ili kuufanikisha mfumo huu wa elimu. Kwanza, mafunzo waliyopewa walimu ili kuufanikisha mfumo huu kamwe hayatoshi. Nionavyo mimi ni kwamba walimu waliopo ambao idadi yao haitoshi, wanatumia elimu ya mfumo wa 8-4-4 kuufunza ule wa CBC. Itawezekanaje mwalimu apate mafunzo ya wiki moja kisha akawa amefuzu kumwelekeza mwanafunzi? Isitoshe mfumo huu unamhitaji sana mwalimu kutumia teknolojia ya kisasa katika ufunzaji. Usishangae nikikwambia kuwa walimu wengi hawana mafunzo ya kisasa ya kompyuta. Zaidi ya hayo shule nyingi vilevile hazina tarakilishi. Baadhi yazo pia umeme haupo. Baada ya serikali ya uhuru kuahidi kuwapa Watoto vipakatalishi, je jiulize, ni wanafunzi wangapi hivi sasa ambao walipata vipakatalishi hivyo? Kando na hayo, wazazi wengi washalalamika kuhusu gharama kubwa ya vifaa ambavyo walimu huwatuma wanafunzi kuvileta shuleni. Huenda ikawa sababu ya wao kusema kuwa ni heri mfumo huo wa CBC ukaachiwa shule za kibinafsi. Muda huo wote kila mtu pale tulipoketi alikuwa ametulia. Wapo waliotikisa vichwa kukubaliana naye Sumaku na wapo waliotikisa kukataa. Mara kijana mmoja tuliyemwita Sudi alisimama na kuzungumza. mawazo yake sudi ni kama yalikuwa ya kumpinga sumaku.
             “Mtazamo wangu mimi ni kuwa mfumo wa CBC haufai kufutiliwa mbali. Itakuwa hasara kubwa kwa washika dau mbali mbali ambao wameekeza katika mfumo huu. Ikumbukwe kwamba imeigharimu serikali ya Uhuru pesa nyingi katika kujenga madarasa, kuwafunza walimu pamoja kuchapisha vitabu vya mfumo huu. Isitoshe kuutupilia mbali mfumo huu itakuwa sawa nakuwapotezea muda wanafunzi wa darasa la sita ambao kwa miaka sita wamekuwa wakisoma mfumo huu”
             “Nakuunga mkono sumaku, alianza Dida. Kwanza sudi awazie tena udhaifu wa mfumo 8-4-4 ndipo awazie hayo. Kila mwanafunzi katika mfumo huu wa CBC ni mshindi. Hakuna kuwagawa wanafunzi katika makundi ya wajinga na werevu. Isitoshe, katika mtaala huu mpya, hakuna kurudia rudia madarasa kama ilivyo katika mfumo huo wa awali. Vile vile, mtaala wa CBC utawapa wanafunzi wa Kenya matumaini na fursa ya kuimarisha vipawa na uwezo wao. Ikumbukwe kwamba mtaala huu unasisitiza ukuzaji wa talanta za wanafunzi nchini tofauti na ule wa 8-4-4. Pia, CBC humfunza mwanafunzi masomo ambayo tu yatamfaa maishani mwake. Lugha asili za wanafunzi pia zitakuzwa katika mfumo huu mpya. Hivyo basi serikali yake Ruto na Riggy G haina budi kuufanikisha mtaala huu.
Maneno yake Dida yalifunikwa ghafla na kelele za kumshangilia na kumsifu kijana huyu. Alipoona bado wanashangilia, aliinua mkono wake wa kushoto juu na kusema, “Basi ! basi wanafunzi wenzangu, sina shaka ujumbe umeshafika.

  1. Ni mambo yepi yanayoleta utangamano baina ya vijana katika kundi hili chuoni?(alama 3)
  2. Eleza udhaifu wa mfumo wa 8-4-4 kulingana na kifungu hiki. (alama 5)
  3. Jadili manufaa ya mfumo mpya wa elimu kulingana na Makala haya. (alama 5)
  4. Kauli “upepo mwanana ulikuwa ukipita na kuzipapasa Ngozi zetu, “ imetumia tamathali gani ya usemi? (alama 1)
  5. Eleza maana ya “tulinoleana bongo” kwa mujibu wa taarifa. (alama 1)

2. UFUPISHO (Alama 15)
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yafuatayo.
            Bei ghali ya vyakula ni jambo linalowaathiri wakenya wengi kwa hivi sasa. Inasikitisha kupata kwamba bei ya unga wa ugali imepanda hadi sh. 200. Ni wazi kwamba familia nyingi nchini hukosa lishe lao kutokana na kufumka kwa bei ya bidhaa muhimu. Hata hivyo ibainike kwamba nchi isiyowakimu raia
wake kwa chakula ni sawa ng”ombe aliyeshindwa kumnyonyesha ndama wake.
            Kwa muda mrefu, viongozi wamekuwa wakipambana na tatizo la ukosefu wa chakula. Msimu wa kiangazi unapobisha hodi, watu wengi hasa wale wahitaji hupukutika kutokana na mngato wa njaa. Japo serikali na wafadhili hutuma vyakula vya msaada kwa jamii zilizoathirika, chakula hiki huwa kama
nguo ya kuazima, na bila shaka ya kuazima haikidhi haja.
            Mojawapo ya vyanzo vikuu vya uhaba wa chakula ni kiwango cha chini cha uzalishaji na uhifadhi wa chakula chenyewe. Zipo seheu nyingi ambazo ni kame nchini.sehemu hizi hukabiliwa na ukosefu wa maji kwani, ama mvua hainyeshi au inaponyesha haitoshelezi mahitaji ya mimea. Mimea mingi hujikaukia ikiwa michanga na kudhihaki juhudi za wapanzi. Zipo sehemu katika nchi hii ambazo huenda kwa misimu hata mitano bila kupata zao lolote kutoka mashambani.           Hali ikiwa hivi makali ya uhitaji huzidi na wakazi wa sehemu hizi hulazimika kuwa wategemezi kwa majirani na serikali.
Wengine wanapokosa chakula kabisa huazimia kula visivyoliwa. Wanaamwa la mbwa baada ya kukosa la mama. Hali kadhalika japo zipo sehemu zingine ambazo hazina tatizo la ukame, mbinu hasi za kilimo husababisha utoaji wa mavuno haba, hivyo kutojitosheleza kwa chakula. Bilas haka wanapopanda ovyo
wanavuna ovyo. Kuna wakulima ambao hupalilia mmomonyoka wa udongo kwa kulima kando kando ya mito, kupanda zao lile lile katika sehemu ile ile ya ardhi miaka nenda miaka rudi, na kutopanda mimea ambayo hukinga tabaka la juu la udongo dhidi ya kumomonyolewa na maji au upepo. Matokeo ya haya yanaweza kutabiriwa; udongo wenye rutuba huoshwa na mashamba kutwaa utasa ambao huzidisha kuzalisha kwa chakula haba. Wakulima wengine hukaidi wito wa kupanda mimea ambayo hustahimili ukame kama vile mbaazi mihogo, mtama na wimbi. Baadhi ya wakulima hufuga mifugo wengi ambao hushindwa kustahimili kiangazi. Si ajabu kupata kwamba katika baadhi ya maeneo mizoga ya ngombe na hata ngamia imezagaa kote tanuri la kiangazi linapofanya kazi yake.
            Sehemu zingine zimebarikiwa na ukwasi wa chakula. Hata hivyo baadhi ya wakazi wa sehemu hizi hawana mwao kuhusu umuhimu wa lishe bora. Wapo wanaodhani kuwa chakula ni chakula bora tumbo lipate haki. Hawa hula vyakula kama vile viazi, mahindi, na wengine nyama bila kujua wanahiyaji vyakula vyenye virutubisho muhimu, yani wanga, protini , vitamini na madini. Wapo wanaodhani kuwa protini pekee ni nyama. Hawa hula nyama mawio na machweo, matokeo yakiwa kuambulia magonjwa kama vile shinikizo la damu.
            Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula, serikali kupitia wizara husika imeanzisha miradi ya kuhakikisha kuwa kuna uzalishaji wa chakula kwa kiwango cha kuridhisha. Serikali ya Ruto sasa imepunguza bei ya mbolea hadi sh 3500 ili kuwawezesha wakulima kupanda chakula kwa wingi. Visima na mabwawa ya maji pia vitachimbwa katika maeneo kame ili kunyunyuzia mashamba maji. Baadhi ya wakulima wameanza kupanda mimea ambayo inapevuka na kutoa mazao kwa haraka ipo mimea ya kuatika ambayo hutoa matunda baada ya muda mfupi, hivyo kusaidia kupunguza makali ya njaa. Wafugaji wengine wameanzisha miradi ya kufuga kuku wa kututumuliwa. Hawa hukuwa na kukomaa kwa muda mfupi na huweza kutoa nyama na mayai. Wafugaji wa kuku hawa huweza kuwauza kununua aina nyingine ya chakula.
            Wakulima pia wanahimizwa kutumia njia za kisasa za kuzalisha na kuhifadhi chakula.chakula kinapohifadhiwa vyema, hata mvua isiponyesha raia huweza kujitegemea. Ikiwa maghala ya halmashauri za kuhifadhi chakula nchini hayahifadhi chakula mara nyingi hulazimika kuagiza chakula kutoka nje kiangazi kinapojiri. Aidha chakula kisipohifadhiwa vyemahuishia kuharibika na kuhasiri wanaokila ikawa msiba juu ya mwingine.
            Ni muhimu kufahamu kuwajukumu la kupambana na ukosefu wa chakula ni la kila raia. Hali ya kungojea kila mara kulishwa na serikali inatufanya kuwa wategemezi Zaidi. Wadogo wadogo ambao huuza vyakula kwa bei ya chini sana mara tu wanapovitoa mashambani wanapaswa kujiasa dhidi ya mazoea haya na kujua kuwa akiba haiozi. Wanaoishi katika sehemu za vinamasi wasaidiwe kuzitunza sehemu hizi na kuzitumia kwa njia endelevu. Vijana wahimizwe wawaunge wazee mkono kushughulikia kilimo katika sehemu za mashambani badala ya kuhamia mijini kutafuta kazi za ajira ambazo ni haba.

  1. Fupisha ujumbe wa aya tano za kwanza kwa maneno 100. (alama 9, 1 ya mtiririko)
    Matayarisho
    Jibu
  2. Kwa kurejelea aya tatu za mwisho, eleza njia sita za kukabiliana na uhaba wa chakula. (maneno 85)
    (alama 6, 1 ya mtiririko)
    Matayarisho
    Jibu

3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)

  1. Kamilisha jedwali lifuatalo kwa kuandika sauti zifaazo. (alama 3)
     AINA   midomo  meno    ufizi  Mdomo na meno  Kaakaa gumu  Kaakaa laini  koromeo
     Vipasuo            _______  
     Vizuio kwamizwa           _____    
     vikwamizo      _____        
     Ving`ong`o  ____            
     kitambaza      _____        
     kimadende              
     Nusu irabu          _______    
  2. Tofautisha sentensi zifuatazo kimaana. (alama 2)
    1. Andai angelimnywesha babu uji kwa kikombe, babu angelishiba.
    2. Andai angalimnywesha babu uji kwa kikombe, babu angalishiba.
  3. Ikanushe sentensi ifuatayo kwa wingi (alama 2)
    Mwizi alimkata sikio na pua
  4. Tunga sentensi moja itakayodhihirisha kielezi cha namna mfanano. (alama 2)
  5. Ainisha mofimu katika kitenzi kilicho katika sentensi hii. (alama 3)
    Wapenzi hao watanywiana sharubati.
  6.       
    1. Nini maana ya kirai? (alama 1)
    2. Tunga sentensi moja inayodhihirisha kirai kihusishi. (alama 2)
  7. Eleza tofauti za kimatumizi kati ya alama zifuatazo za uakifishaji. (alama 2)
    1. Koloni …………………………………………………………………………………..
    2. Nusu koloni …………………………………………………………………………….
  8. Andika upya sentensi zifuatazo kilingana na maagizo uliyopewa.
    1. Mbuzi walipopotea, mchungaji alikuwa na wasiwasi. (Anza kwa, Kupotea.... (alama 2)
    2. Dereva aliyesababisha ajali alihukumiwa miaka minne na kazi ngumu.
      (Maliza …aliyesababisha ajali. (alama 2)
  9. Tunga sentensi itakayodhihirisha kielelezo kifuatacho cha mstari. (alama 2)
    S-RN(N+V+V)+KT(T+E)
  10. Tunga sentensi moja itakayodhihirisha maana ya vitate rika na lika. (alama 2)
  11. Bainisha vitenzi katika sentensi hii. (alama 3)
    Ndege yu taabani, hata hivyo anajaribu kujinasua.
  12. Onyesha shamirisho na chagizo katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
    Bi. Kerubo alirembeshwa nyusi kwa wanja mweusi.
  13. Andika sentensi ifuatayo katika usemi wa taarifa. (alama 2)
    “Shughuli yangu itamalizika leo,” mama alimwambia baba.
  14. Andika visawe vya; (alama 2)
    1. Rai …………………………………………………………………………………
    2. Azimio …………………………………………..…………………………………
  15. Vumisha neno zuri kwa kulitungia sentensi. (alama 2)
  16. Ainisha vihusishi katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
    Rais alifika mapema kuliko wengine halafu akaondoka.
  17. Tambua matumizi ya kiambishi -ji- katika sentensi (alama 2)
    Jino la jitu hilo lililiwezesha kujilia chakula kingi.
  18. Ikamilishe methali ifuatayo. (alama 1)
    Cha mkufuu…………………………………………………………………………………………
  19. Igeuze sentensi ifuatayo iwe katika mazoea. (alama 1)
    Matunda yanayoiva ndiyo yanayotundwa.

4. ISIMU JAMII (Alama 10)
Tumia kauli ifuatayo kujibu maswali
Haya ng`ara leo, nguo moto moto. Fifty hamsa fifty hamsa fifty hamsa na nyingine. Shati shilingi
hamsini tu. Kuona ni bure…

  1. Kando na sifa zinazojitokeza katika Makala haya taja sifa zingine tano za sajili hii. (alama 5)
  2. Eleza juhudi tano zinazofanywa ili kukikuza Kiswahili nchini Kenya na dunia kwa jumla. (alama 5)

Mwongozo Wa Kusahihisha

  1. UFAHAMU(ALAMA 15)
    1. Mambo yanayoleta utangamano utangamano baina ya vijana katika kundi hili
      • Masomo; wanafunzi hawa walitangamana chuoni kwa madhumuni yamasomo.
      • Haja ya kufanya utafiti kuhusu kazi mradi waliyopewa
      • Kuwepo kwa mtandao wa bure
      • Mandhari ya kuvutia
        (zozote 4*1)
    2. Udhaifu wa mfumo wa 8-4-4
      • Kuwatenga wanafunzi ; wale wanaojua na wale wasiojua.
      • Kuna kurudiarudia baadhi ya madarasa.
      • Hauimarishi talanta/ vipawa vya wanafunzi
      • Baadhi ya masomo anayosoma mwanafunzi hayamfaidi maishani
      • Mtaala huu haukuzi lugha asilia za wanafunzi.
    3. Manufaa ya mfumo wa CBC
      • Huimarisha vipawa/ talanta za wanafunzi
      • Masomo yote anayosoma mwanafunzi humfaa
      • Hukuza lugha asili
      • Hakuna kurudia madarasa
      • Kila mwanafunzi ni mshindi.
    4. Tashisi/ uhuishaji
    5. Tulifahamishana/ tulielimishana
  2.    
    1. UFUPISHO (AlAMA 15)
      • Bei ghali ya vyakula ni jambo linalowaathiri wakenya wengi.
      • Familia nyingi nchini hukosa lishe.
      • Kwa muda mrefu, viongozi wamekuwa wakipambana na tatizo la uhaba wa chakula
      • Chakula kinachotumwa na serikali hakitoshi.
      • Kiwango cha chini cha uzalishaji na uhifadhi ndicho chanzo cha uhaba wa chakula.
      • Zipo sehemu nyingi nchini ambazo ni kame.
      • Wengine wanapokosa chakula kabisa huazimia kula visivyoliwa.
      • Mbinu hasi za kilimo husababisha utoaji wa mavuno haba.
      • Wakulima wengine hukaidi wito wa kupanda mimea inayostahimili ukame.
      • Baadhi ya wakazi hawana mwao kuhusu umuhimu wa lishe bora
    2.  
      • Kupunguza bei ya mbolea hadi sh. 3500.
      • Uchimbaji wa visima na mabwawa ya maji
      • Kupanda mimea inayopevuka na kutoa mazao haraka.
      • Kuanzisha miradi ya ufugaji wa kuku wa kututumuliwa.
      • Kutumia njia za kisasa za kuzalisha na kuhifadhi chakula.
      • Wakulima wajiasi dhidi ya kuuza vyakula kwa bei ya chini.
      • Wanaoishi sehemu za vinamasi wasaidiwe kutunza sehemu hizi.
      • Vijana wahimizwe kuwaunga wazee mkono kushughulikia kilimo mashambani
  3. MATUMIZI YA LUGHA.(ALAMA 40)
    1. Kipasuo cha kaakaa laini /k/ au /g/
      • kizuiokwamizwa cha kaakaa gumu /j/ au /ch/
      • kikwamizo cha ufizi /s/ au /z/
      • kin’gon’go cha midomo /m/
      • kitambaza cha ufizi /l/
      • kiyeyusho cha kaakaa gumu /y/ alama 6*1/2=3
    2. hamisha alama za swali hili hadi kwenye swali la (r) na (t)
    3. Wezi hawakuwakata masikio wala pua. Alama 2/0
    4. kadiria jibu. Mfano
      Rais alitembea kijeshi
    5. watanywiana
      wa-nafsi
      -ta-wakati
      -nyw-mzizi
      -ian-kauli
      -a- kiishio akikosa kimoja atuzwe 21/2
    6. kirai ni
      Neno au fungu la maneno katika sentensi lisilo na uhusiano wa kiima kiarifa / lisilo na maana
      Kisarufi.
      Neno au fungu la maneno katika sentensi ambalo hutambulika kwa kuzingatia neno tangulizi.
    7. Wanafunzi wa mwisho wataadhibiwa. (alama 2/0)
      kadiria.
    8. Koloni hutumiwa-
      Kuorodhesha
      kutenganisha saa na dakika
      katika mazungumzo, kutenga msemaji na maneno yake. (yoyote 1*1)
      Nusu koloni hutumiwa-
      kutenga sentensi na ufafanuzi wake.
      kutenga vishazi huru viwili katika sentensi. (yoyote 1*1)
    9. Kupotea kwa mbuzi kulimpa mchungaji wasiwasi. (alama 2/0)
      Hukumu ya miaka minne na kazi ngumu ilipewa/ ilitolewa kwa dereva aliyesababisha ajali.
    10. Wanafunzi wote maskini walifadhiliwa shuleni. (kn- alama 1, KT alama 1)
    11. sentensi idhihirishe maana zifuatazo;
      rika-kundi la watu wenye umri sawa.
      lika -kuwa katika hali ya kuweza kuliwa au kusagika pole pole hadi kuisha. (alama 2*1)
    12. yu- kitenzi kishikishi
      anajaribu- kitenzi kisaidizi
      kujinasua- kitenzi kikuu (alama 3*1)
    13. nyusi- shamirisho kipozi
      wanja mweusi- chagizo (alama 2*1)
    14. Mama alimwambia baba kuwa shughuli yaje ingemalizika siku hiyo. (alama 4*1/2)
    15. rai- ombi
      azimio-lengo
    16. Madarasa mazuri hupendeza mno. Kadiria, alama 2/0
    17. jino- kuonyesha mwanzo wa baadhi ya nomino katika umoja.
      Jitu- kuonyesha ukubwa wa nomino
      Kujilia-kirejeshi cha mtendaji (alama 3*1)
    18. Rais alifika mapema kuliko wengine halafu akaondoka.
      Kuliko- kihusishi cha kiwango
      Halafu- kihusishi cha wakati
    19. Cha mkufuu mwanafuu ha akila hu, cha mwanafuu mkufuu hu na akila ha. (ala. 1)
    20. Matunda yaivayo ndiyo yatundwayo. (alama 2)
  4. ISIMUJAMII(ALAMA 10)
    1.      
      1. Matumizi ya viziada lugha/ ishara
      2. Matangazo huambatana na picha au michoro
      3. Matumizi ya porojo
      4. Matumizi ya chuku
      5. lugha ya ucheshi
      6. lugha iliyosheheni taswira na tamathali za semi
      7. Lugha yenye kukatizana kauli
      8. Kujinajibisha au kujitambulisha na mteja (hoja za kwanza 5*1=5)
    2. uimarishaji wa kiswahili nchini.
      1. Uchapishaji wa baadhi ya vitabu na magazeti hufanywa kwa Kiswahili. Mfano Taifa leo
      2. Kuna vipindi mbali mbali mbali katika redio na runinga vinavyokuza Kiswahili.
      3. kiswahili kimeingizwa kwenye kompyuta n ahata simu za mkononi
      4. Kiswahili kimefanywa lugha ya taifa nchini Kenya na hata juzi kuteuliwa kule Uganda
      5. Kiswahili hutumiwa kufunzia baadhi ya masomo shuleni.
      6. Kuteuliwa kwa siku ya Kiswahili duniani ni hatua kubwa katika ukuzaji wake.
        Hoja za kwanza 5*1=5
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Bondo Joint Mocks Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?