Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mangu High School Mock Exams 2022

Share via Whatsapp

MASWALI

 1. Ufahamu(Alama 15)
  Soma makala halafu ujibu maswali yanayofuatia.
  Leo Mwalimu Bidii amerauka kama ada yake kwa ajili ya kutekeleza wajibu wake kwa wanafunzi wake Shuleni Mwera. Anaelewa barabara kwamba mchapuko wa ghafla wagonjwa la korona kule Uchina, ulitikisa na kuvuruga dunia nzima katika nyanja zote za maisha ya binadamu. Miongoni mwa nyanja zilizoathiriwa zaidi ni elimu ambayo huongoza nyanja zingine za maisha. Awali, taasisi zote za elimu zilifungwa kama hatua muhimu ya kudhibiti msambao wa uwele huu. Baadaye afueni ilipodhihiri, na ushauri kutolewa na wataalamu wa afya, mataifa mbalimbali yalibuni taratibu za kurejelewa kwa shughuli za masomo katika taasisi zote. Labda marejeleo haya hayakuwa na ugumu kama ilivyokuwa namna ya kufidia na kurejelewa kwa mfumo wa kawaida shuleni. Naam, mwiba uchomeapo ndipo utolewapo na tiba mjarabu ni ile itokayo kwa mwele mwenyewe. Wizara ya elimu nchini iliratibu mihula upya na kuvuruga 'mazoea. Hii ni hatua iliyowasababishia bughudha washikadau wote; sio walimu, wazazi, wauzaji na wanafunzi. Sijui mizani gani iliyotumiwa kupima, lakini watu wengi walihisi kwamba ni walimu waliokumbwa na usumbufu mkubwa zaidi. Iliwabidi walimu wafarague na kuongeza ubunifu wao ili kukamilisha mitaala ya masomo katika muda mfupi kuliko ule ulioratibiwa na wakuzaji mitaala. Mathalani, vipindi vilianza mapema kuliko kawaida yake na kuendelea hadi kupita saa kumi jioni na kuzima michezo ya baada ya madarasa. Mwalimu Bidii hakuwa na budi ila kujitoma ndani ya kinyang'anyiro hiki kwa vile hakupenda kuachwa nyuma. Hii ndiyo sababu ilimfanya kurauka kila siku. Lakini leo matarajio yake ya kuwahi kipindi cha saa kumi na mbili alfajiri yanaelekea kuyeyuka na kutokomea mithili ya theluji inavyoyeyuka na kugeuka kuwa maji yanayateremka kutoka milimani kufaidi walio mabondeni na kuviacha vileleta vya milima na kiu. Usiku uliopita ilikunya kidindia ungedhani ilikuwa mashindanoni. Barabara iliyotamani kutiwa sakafu tangu nchi ijinyakulie uhuru hadi sasa ikanyonya, ikameza na kutapika maji yakaloa kote. Wajuao chuku ya lugha walisema kilichozaliwa barabarani kilikuwa mama ya tope wala sio tope tu. Tazamo hili lilikejeli ile pikipiki aina ya 'Honda' aliyokuwa ameitumia Mwalimu Bidii kwa miongo miwili u nusu sasa pikipiki aliyonunua baada ya kuomba mkopo kutoka kwenye chama cha ushirika cha akiba na mikopo baada ya miaka mitatu ya ajira. Ilimchukua miaka mitano kulipia mkopo wake. Ilikuwa dhahiri tangu aiguse barabara hii kwamba alikuwa anajenga nyumba ya karata. Utelezi wa barabarani uliongezwa na magurudumu yaliyolika meno na kubwagwa chini halikuwa tukio lililokuwa ng'ambo ya utendekaji kamwe. Mara mojamoja ilimbidi Mwalimu Bidii kusalimu amri. Si hoja kwamba hakupiga hatua za maana kupunguza kitalifa cha kilomita kumi baina ya shule na nyumba yake ya kukodisha. Muda huu wote manyunyu ya mvua yalikuwa yanaendelea kudondoka ni kama yalikuwa na kinyongo na mzalendo huyu aliyejitolea sabili kuhudumia nchi yake. Alizidi kupambana akihema kama punda aliyebandikwa mzigo uliozidi uwezo wake akijaribu kuelekeza chombo chake kisiende pewa topeni. Kwa kweli hakuenda popote heri ule mfano wa simulizi ya Sofokile kumhusu mbingirisha mwamba kuupandisha kwenye mlima ulioteleza. Ingawa alishindwa kuukwea mlima, angaa angerudi nyuma sio kama mwalimu. Mwalimu alisakamwa kabisa; mbele na nyuma hakukuendeka!
  Mbele yake kidogo alimwona mtu aliyemjua akiwa amevua viatu na kuvishika mikononi ili alikabili tope barabarani. Huyu alikuwa afisa wa maabara kwenye Zahanati ya Nafuu iliyokuwa karibu na Shule ya Mwera. Muala Mutia alipambana na hali yake bila kutazama nyuma aone dhiki alizokuwa anapitia mwalimu. Aliogopa kuchelewa kupokezwa zamu na mwenzake aliyehudumu usiku huo. Hakupenda nuksani za asubuhi ambazo Kechi angemzulia lau angechelewa hata kwa dakika chache tu. Kechi alikuwa mbali sana na ungwana na wenzake kazini waliepuka kumkorofisha kwani hakuna neno ambalo ulimi wake haungelitaja faraghani na hadharani. Hakuwa na kaba ya ulimi. Kama alikuwa na marafiki, achana na wandani, hawakujulikana pale zahanatini. Mutia aliambaa shari ili imwambae. Lakini leo ilikuwa muhali kwani hangeweza kukamilisha umbali wa kilomita tisa kwa miguu katika nusu saa iliyosalia kabla ya muda wa kupokezwa zamu. Na hakika lisilo budi mja muungwana hupatana nalo wala hapingani nalo.
  Hatua kadhaa mbele yake alimpata yule mchuuzi anayewasambazia maziwa zahanatini amebwagwa chini na pikipiki yake na mitungi ikafunguka na kurembesha barabara kwa maziwa yaliyokuwamo. Kiplimo, jamaa aliyestawisha kilimo cha ufugaji katika Kijiji cha Kaplel, leo ameambulia hasara. Atarejea nyumbani mikono mitupu. Alisakama pale matopeni hadi Mutia alipomfikia na kuinua pikipiki iliyokuwa imeumbana mguu wake wa kulia asitoke.
  "Hawa viongozi wetu wanahujumu maendeleo yetu kabisa! Mbona miaka hii yote barabara hii haijabandikwa lami?" Kiplimo akamaka baada ya kusimama.
  Mutia akamkumbusha, "Lakini si ni nyinyi mna mazoea ya kukubali visenti vichache wakati wa uchaguzi ili kuwachagua wanafiki hawa? Kisha kuna wengine ambao husema "Tunachagua mtu wetu', 'mtu wetu' ambaye sasa hana mwao kuhusu kero tunazopitia! Na wengine kama yule jirani yetu upande wa kusini haendi kupiga kura akidai kuwa kura yake moja haiwezi kuleta tofauti yoyote. Ni janga tumelichuma wakati wa uchaguzi sasa tuvumilie kulila. Wajua tangu kale, mwiba wa kujidunga huambiwi pole."
  Mwalimu Bidii naye, baada ya kughairi nia, alikuwa ameegesha 'Honda' yake kando ya kigingi cha ua uliozingira shamba la yule mkwasi ambaye wengi hawakumjua ila walimsikia tu, akawa anamfuata Mutia akitumainia usaidizi wake. Alipowakaribia na kusikia malumbano yao, akatupa nukuu aliyowahi kuisikia kwa mtu asiyemkumbuka, "Choices have consequences!" Wale wawili wakaitikia kama ngonjera, "Ni kweli mwalimu!"
  1. Mikakati ya kukamilisha mitaala ya masomo iliwaathiri washikadau kwa namna mbalimbali. Taja athari tatu kwa wanafunzi. (alama 3)
  2. Orodhesha changamoto nne zinazowatanza wahusika katika kutekeleza shughuli zao katika makala haya. (alama 4)
  3. Thibitisha ukweli wa kauli kwamba uamuzi una athari zake kwa kurejelea matukio matatu kuwahusu wananchi kama inavyosimuliwa katika kifungu hiki. (alama 3)
  4. Nakili kisawe cha 'bughudha kutoka kifunguni. (alama 1)
  5. Andika visawe vya nahau zifuatazo:
   1. aliyejitolea sabili .............
   2. kisiende pewa ................
  6. Bila kukanusha, eleza maana ya 'Hakuwa na kaba ya ulimi.' (alama 1)
  7. Andika methali moja inayoasa kuhusu ulimi. (alama 1)
 2. Ufupisho
  Fupisha kifungu hiki kulingana maagizo yanayotolewa mwishoni mwake.
  Katika karne ya kumi na tisa bara la Afrika lilivamiwa na nchi za Ulaya kama vile Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji, Italia, Ureno na kadhalika na kutwaliwa. Uingiliaji huu haukuhusu Afrika pekee bali mataifa mengine katika ule ulioitwa ulimwengu usiostaarabika kama India. Kwa mujibu wa wanahistoria, Uingereza ndilo taifa lililojitwalia idadi kubwa ya nchi za ulimwengu chini ya mfumo wa kiutawala ulioitwa ukoloni labda kwa sababu kwamba Uingereza ni taifa lililokuwa limefikia ustawi mkubwa katika Ulaya nzima wakati huo. Bila shaka huu ulikuwa muktadha uliostahili matumizi ya usemi kuwa mwenye nguvu hupishwa na mataifa mengine ya Ulaya hayakuwa na budi ila kuipisha Uingereza ijilimbikizie mataifa ya ulimwengu na kuyaweka chini ya kwapa zake. Jambo lingine lililoiwezesha Uingereza kuyapiku mataifa mengine ya Ulaya katika kujipakulia koloni ulimwenguni ni kwamba Waingereza walitakadamu katika uvumbuzi wa vyombo vya usafiri wa majini na kwa hivyo waliweza kuzuru nchi za ulimwengu kwa wepesi zaidi na katika kipindi kifupi. Licha ya Uingereza kuwa katika nafasi bora ya kutwaa koloni ulimwenguni, mataifa mengine ya Ulaya hayakusubiri kugawiwa bali hayo pia yaling'ang'ania kumega sehemu fulani ya koloni. Huu mng'ang'anio ulikuwa kinyang'anyiro halisi ambacho kilimithilishwa na watu wanaogawana kipande cha mkate au nyama; kila mmoja akijikatia kadiri ya uwezo wake na makali ya kisu chake.
  Uvamizi huu ulidhihirika kupitia utwaliwaji wa mamlaka ya kiutawala katika mataifa yaliyoathiriwa na kuwekwa chini ya himaya ya taifa husika kutoka Ulaya. Mtindo huu ulikinzana na tawala asilia za jamii mbalimbali za Kiafrika zilizokuwa na falme zao ambazo zilisambaratishwa baada ya kuangikwa kwa bendera ya taifa husika kutoka Ulaya. Hakukuwa na fursa ya kutathmini namna kila jamii katika kila eneo ilivyoendesha serikali yake chini ya viongozi wao mbalimbali. Usishangae kusikia kwamba Wazungu wengi waliipuuzilia mbali hii mifumo ya kiutawala au hata kudai kwamba wenyeji hawakuwa na mfumo wowote wa kujitawala. Uhasama uliokuwepo baina ya jamii tofauti pamoja na upekee wa mila na tamaduni zao zingine, ni mambo yaliyoangaziwa kwa kurunzi kali zaidi na kupuuza ukweli kwamba Waafrika walikuwa na mifumo mbalimbali ya kujiongoza.
  Bara la Afrika lilikatwakatwa katika vipande mbalimbali na kugawiwa mataifa tofautitofauti ya Ulaya. Walibuni mipaka kiholela na kuwatenganisha watu wa jamii moja wakajipata kwenye nchi mbili tofauti. Si ajabu kwamba hata katika visa vya kidhalimu watu wa familia moja walitenganishwa kwa kuwekwa katika nchi mbili tofauti. Aidha, hata watu wa ukoo mmoja walitawanywa kimakusudi na kupelekwa katika maeneo mengine ya kijiografia yaliyoitwa nchi. Kadhalika, hata kuna maboma ambayo yalipigwa mpaka katikati na kumega sehemu moja kuitupa katika nchi tofauti na nyingine. Na kwa kweli asiyekujua hakudhamini. Watu walioathirika na tendo hili la kiholela waliona ugumu mkubwa kutii mipaka ya aina hii na kunao waliokaidi mipaka na kuendelea kutagusana na kutangamana na jamaa zao kokote walikopelekwa.
  Tahakiki za wanahistoria hudai kwamba uvamizi wa Wazungu katika bara la Afrika, kwa kiwango cha juu zaidi uliletwa na msukumo wa kutaka kunyakua maliasili kochokocho iliyojaa
  katika maeneo mengi. Madini kama chuma, makaa, shaba, almasi, dhahabu na mengine mengi yalijaa tele na viwanda vilivyokuwa vimestawishwa kutokana na Mageuzi ya Kiwanda ya Karne ya 19 vilihitaji mali ghafi na madini kwa wingi. Afrika illikuwa na hazina ya hiyo mali ghafi na ilifaa kutwaliwa bila pingamizi. Njia ya pekee ya kujihakikishia kuwepo mfululizo kwa bidhaa hii ilikuwa kuziweka nchi hizi chini ya himaya za serikali zao za Ulaya. Sina shaka walielewa msemo kwamba pavumapo palilie nao wageni wavamizi iliwabidi walilie bara lenye maliasili nyingi sana.
  Licha ya majilio ya Wazungu barani Afrika kuangaziwa kwa uhasi, ni kweli kwamba kuna mambo mengi mazuri ambayo hayangetokea lau hawangalikuja. Ustawishaji wa miundomsingi, hasa njia, uliwezesha maeneo ya ndani kufikiwa bila bughudha nyingi. Ikumbukwe kwamba njia ya reli ya Kenya - Uganda, iliyojengwa mwanzoni mwa karne ya ishirini ilirahisisha kufanywa kwa shughuli katika maeneo ya ndani ya nchi. Kuna taasisi za matibabu, shule na vyuo vya mafunzo anuai katika taaluma mbalimbali vilivyojengwa na wakoloni. Hata viongozi wa kwanza baada ya nchi hizi kurejeshewa utawala wao, walisomea kwenye taasisi hizi. Mgala muue na haki yake mpe kwani ni stahili yake.
  1. Kwa maneno kati ya 80-90, andika hoja muhimu katika aya mbili za kwanza. (alama 8)
  2. Fupisha aya za tatu, nne na tano ukizingatia athari hasi za ukoloni, kichocheo cha chake na manufaa ya ukoloni barani Afrika. (maneno 50) (alama 6)
 3. Matumizi ya Lugha (Alama 40)
  1. Andika maneno yenye vitamkwa vya sifa zifuatazo: (alama 2)
   1. kikwamizwa sighuna cha kaakaa gumu, irabu ya nyuma juu, kikwamizwa ghuna cha kaakaa laini, irabu ya nyuma juu, kilainisho na irabu ya mbele juu
   2. nazali ya midomoni, irabu ya mbele kati, nazali ya menoni na irabu ya nyuma wastani
  2. Taja sifa zinazoonyesha usawa baina ya kila jozi ya sauti hizi.
   1. /m/ na /w/
   2.  /t/ na /ch/
  3. Eleza maana mbili zilizo katika sentensi:
   Usijadili mtihani unaoendelea wakati huu.
  4. Tumia wingi kuandika sentensi zifuatazo.
   1. Mkulima alilima ucheu ili kujiandaa kwa msimu wa upanzi wa nafaka.
   2. Shauri lake liliniepusha na janga la uwele hatari unaosambaa haraka.
  5. Onyesha katika sentensi moja matumizi mawili ya ritifaa (*) katika lugha.
  6. Zingatia maagizo katika mabano mwishoni mwa kila sentensi kuziandika upya.
   1. Wangia alipata mafunzo murua chuoni. Wangia ni stadi katika Kifaransa. (Unganisha ukianzia: Mafunzo...)
   2. Sherehe nyingi zilifanywa ili kuadhimisha ushindi wa Pute. (Tumia vitenzijina badala ya eno yaliyopigiwa mistari.)
   3. Mari alinunua simutamba mpya kwa shilingi elfu kumi na kumtunza mwanafunzi bora. (Anza na shamirisho ala.)
  7. Ainisha mofimu katika maneno yafuatayo:
   1. katika (kitenzi).
   2. achaguliwaye..
  8. Tunga mfano mojamoja wa sentensi kwa kila muundo.
   1. S-KN (0)+KT(Ts+T+H+N)
   2. S-KN (W+V)+KT(t+N+V)
  9. Bainisha kiima, kiarifu na chagizo katika sentensi hii. Mhandisi shupavu atakagua ujenzi wa ghorofa hatua kwa hatua.
  10. Eleza matumizi ya kiambishi -o katika sentensi ifuatayo: Waliofanikiwa walifanya makadirio mazuri. (alama 1)
  11. Tambua kisha ainisha nomino katika sentensi hii: Mashabiki wengi walipiga vigelegele Kocha Manoa alipotaja kikosi cha wachezaji wake. (alama 1)
  12. Vishazi tegemezi vina dhima za kivumishi na kielezi. Tunga sentensi mojamoja kuonyesha kila dhima.
   1. kivumishi:
   2. kielezi:
  13. Onyesha maana mbili za neno 'bunda' kwa kutungia sentensi mbili tofauti.
  14. Kwa kutumia sentensi moja, onyesha miundo miwili ya virai husishi.
  15. Akifisha.
   siku ya kiswahili duniani iliadhimishwa na wengi ilifana
  16. Jaza mapengo kwa maneno yanayostahili.
   Kinza ni kwa pinga na tambua ni kwa......ilhali nata ni kwa (alama 2)
  17. Onyesha katika sentensi maana ya nahau: 'shika shokoa".
  18. Kasura aligundua kwamba Ogina alikuwa na uwezo mwingi wa kukabili Somo la Hisabati na akaamua kwenda mara kwa mara kupewa ushauri na Ogina hata akaimarika.Taja methali inayoweza kutumiwa kuafiki muktadha wa Karusa
  19. Kwa kuzingatia maana, sentensi ifuatayo inaweza kuwa katika aina mbili. Zitaje. Mkiondoka wawiliwawili, mtafika haraka. .
 4. Isimujamii (Alama 10)
  1. Eleza sifa tano za lugha ambayo wewe kama mnyapara wa kiwanda cha kusaga miwa cha Kimatuni utatumia ukiwahutubia wafanyakazi walio chini yako. (alama 5)
  2. Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali. (alama 5)
   "Polepole, Mama Mercy! Unajua si kupenda kwangu. Tena si hali itakayodumu milele. Baada ya siku chache tu, tutakuwa tumekamilisha mradi huo wenye dharura. Kisha tutakuwa na muda wa kila kitu. Hili, Mama Mercy, ni kile tunaita bad coincidence... nimebanwa na kazi. Unanielewa...?
   "Dadii...njaa...sana!" Fafanua sifa tano za lugha inayotumika katika huu muktadha wa familia. (alama 5)


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

 1. SWALI LA KWANZA: UFAHAMU (ALAMA 15)
  1. Athari za mikakati ya kukukamilisha mitaala kwa wanafunzi
   1. Vipindi vya masomo vilianza mapema sana (alfajiri).
   2. Vipindi vya masomo viliendelea na kupita saa kumi jioni.
   3. Wanafunzi walikosa muda wa kushiriki michezo ya baada ya madarasa. (hoja 3 x 1 = alama 3)
  2. Changamoto za katika kutekeleza shughuli zao
   1. Hali ya barabara ni mbovu. Haijabandikwa lami.
   2. hali ngumu ya hewa. - Kuna manyunyu ya mvua na baridi.
   3. kulazimika kukanyaga ardhi mbichi (matope) kwa miguu kavu - Mutia amevua viatu ili aweze kupita matopeni.
   4. Vyombo vya usafiri viko katika hali duni. Pikipiki ya Mwalimu Bidii ina magurudumu yaliyoisha kwani hayana meno.
   5. mwendo mrefu kufika mahali pa kufanyia kazi - Kilomita kumi ni mwendo mrefu. (hoja 4 x 1 = alama 4)
  3. Ithibati kwamba uamuzi una athari zake kwa kuwazingatia wananchi
   1. Walihongwa ili kuwachagua viongozi.
   2. Waliwachagua viongozi kwa kuzingatia uhusiano; watu wao.
   3. Hawakushiriki katika kupiga kura kuwachagua viongozi wao. (hoja 3 x 1 = alama 3)
  4. Kisawe cha bughudha kutoka kifunguni
   usumbufu (msitari wa mwisho katika aya ya kwanza)
  5. Visawe vya nahau
   1. aliyejitolea mhanga
   2. kisiende upogo/mrama/fyongo
  6. Maana ya 'Hakuwa na kaba ya ulimi pasipo kukanusha
   Angesema lolote.
  7. Methali inayoasa kuhusu ulimi
   Ulimi hauna mfupa.
 2. SWALI LA PILI: UFUPISHO (ALAMA 15) 
  1. Hoja katika aya mbili za kwanza
   1. Katika karne ya kumi na tisa Afrika ilivamiwa na Ulaya na kutwaliwa.
   2. Mataifa mengine yaliyodhaniwa kwa hayajastarabika yaliingiliwa.
   3. Uingereza ilijitwalia nchi nyingi kwa sababu ilistawi zaidi ya mataifa mengine ulimwenguni. 
   4. Waigereza ndio walitakadamu vyombo vya usafiri wa majini.
   5. Mataifa mengine ya Ulaya pia yaling'ang'ana kumega (kupata) koloni ulimwenguni.
   6. Uvamizi ulidhihirika kupitia utwaliwaji wa mamlaka katika mataifa yaliyoathiriwa.
   7. Mtindo huu ulikinzana na tawala asilia za Kiafrika.
   8. Falme zilisambaratishwa.
   9. Hawakutathmini jinsi kila jamii iliendesha serikali yake chini ya viongozi wake/ Walipuuza mifumo ya kiutawala ya wenyeji/ Walidai kuwa wenyeji hawakuwa na mfumo wa utawala.
   10. Uhasama baina ya jamii na upekee wa mil ani mambo yaliyoangaziwa kuliko mifumo mbalimbali ya kujiongoza ya Waafrika.
  2. Ufupisho wa aya ya tatu, nne na tano
   Aya ya 3 - Athari hasi
   1. Walibuni mipaka kiholela na kutenganisha jamii moja.
   2. Watu wa familia moja walijipata katika nchi tofauti.
   3. Watu wa ukoo mmoja walitawanywa na kupelekwa katika nchi tofauti.
   4. Kuna maboma yaliyopigwa mpaka katikati.
    Aya ya 4 - Kichocheo
    Uvamizi uliletwa na kutaka kunyakua maliasili iliyojaa barani Afrika.
    (hoja 1 x 1 = alama 1)
    Aya ya 5 - Manufaa
    1. Miundomsingi ilistawishwa.
    2. Maeneo ya ndani ya bara la Afrika yaliweza kufikika.
    3. Taasisi mbalimbali zilijengwa na wakoloni.
     (hoja 2 x 1 = alama 2)
     jumla - 15
 3. SWALI LA TATU! MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
  1.    
   1. shughuli
   2. meno (2 x 1 = alama 2)
  2.    
   1. /m/ na /w/ - midomoni/ mahali pa (ala za) kutamkia
   2. /t/na/sh/-sighuna/hafifu/ hali ya nyuzisauti (glota)
  3. Maana za sentensi tata
   1. Mtihani ndio unaendelea wakati huu.
   2. Mjadala kuhusu mtihani usiendelee wakati huu.
    Tanbihi: Utata unatokana na kielezi wakati huu' ambapo kinaweza kurejelea chochote kati ya vitenzi viwili kwenye sentensi hiyo katika nyakati tofauti. (2 x 1 = alama 2)
  4. Kubadili tungo katika wingi
   1. Wakulima walilima cheu ili kujiandaa kwa misimu ya upanzi wa nafaka.
   2. Mashauri yao yalituepusha na majanga ya ndwele hatari zilizosambaa haraka.
    (Akikosea popote katika kila sentensi apewe alama 1)
  5. Matumizi mawili ya ritifaa katika lugha kwa sentensi moja
   1. maneno yenye king'ong'o cha kaakaa laini
   2. herufi/sauti zilizodondoshwa/zilizobanwa katika matamshi ya neno/ufupishaji
    Mfano: Wao 'takuwa waking'ang'ania mpira.
    Tanbihi: Lazima sentensi itumiwe katika jibu.
  6. Kuandika sentensi upya kwa mujibu wa maagizo
   1. Mafunzo murua aliyopata chuoni yamemfanya Wangia kuwa (awe) stadi wa (katika) Kifaransa.
   2. Kusherehekea kwingi kulikofanywa kulikuwa kunaadhimisha kushinda kwa Pute. (1 x 2 = alama 2)
   3. Shilingi elfu kumi zilitumiwa na Mari kununua simutamba mpya na kumtuza mwanafunzi bora.
  7. Mofimu katika maneno
   1. katika-kat- mzizi, -ik- kauli na-a
    kiishio
   2. achaguliwaye -a- shamirisho, -chagu- mzizi, -liw- kauli, -a- mzizi na -ye kirejeshi
    (5 alama 2, akipata 1-2, alama 2, 3-4 alama 1)
  8. Sentensi zenye miundo iliyopo
   1. Haendi kuungana na wanasiasa.
    Ts T H N
    (Sentensi sahihi 1/0)
   2. Hilo lako lina magurudumu mapya.
    W  V  t  N   V
    (Sentensi sahihi yenye viungo vyote 2/0)
  9. Kubainisha viungo katika sentensi
   Mhandisi shupavu atakagua ujenzi wa ghorofa hatua kwa hatua. 
   kiima     kiarifu      chagizo
  10. Kueleza matumizi ya kiambishi -o katika maneno Waliofanikiwa-kirejeshi, makadirio - unominishaji (2 x 2 = alama 1)
  11. Kutambua na kuainisha nomino katika sentensi
   mashabiki - kawaida, vigelegele - dhahania, Kocha Manoa-pekee/halisi/maalum, kikosi cha wachezaji - jamii/kundi/makundi
   (kutambua 3 x 1⁄2= alama 11⁄2, kuainisha 3 x 1⁄2 alama 11⁄2, jumla alama 3)
  12. Dhima za vishazi tegemezi
   1. kivumishi - Gari lililonunuliwa limewasili.
   2. kielezi - Walilima wakishirikiana
    (mfano sahihi katika sentensi 2 x 1 = alama 2)
  13. Kutunga sentensi mbili kutumia kitawe 'bunda'
   1. Furushi la vitu kama karatasi, noti: Mwalimu amebeba bunda la karatasi za watahiniwa.
   2. Anguka/kosa kitu: Wanafunzi waliobunda ktika mtihani walikuwa wazembe.
    (Sentensi sahihi 2 x 1 = alama 2)
  14. Sentensi moja yenye miundo miwili ya virai husishi
   Mtoto wa shule ameketi karibu bustanini.
   H+N   H+E
   (2 x 1 = alama 2)
  15. Kuakifisha
   Siku ya Kiswahili Duniani iliadhimishwa na wengi. Ilifana.
   Au
   Siku ya Kiswahili iliadhimishwa na wengi; ilifana.
   (herufi kubwa alama 1, viakifishi alama 1; jumla alama 2)
  16. Kinza ni kwa pinga na tambua ni kwa jua (elewa/fahamu) ilhali nata ni kwa gandama (shika/jamidi/ganda).
   Tanbihi: Ni visawe vinavyolengwa.
   (2 x 1⁄2= alama 1)
  17. Kutunga sentensi kuonyesha maana ya nahau 'shika shokoa'.
   Maana: Lazimisha mtu kufanya jambo
   Mfano: Mwalimu aliwashika shokoa wanafunzi wazembe wakajibu maswali. (sentensi sahihi 1 x 1 = alama 1/0)
  18. Methali inayoafiki muktadha
   Mtegemea nundu haachi kunona. (1 x 1 alama 1/0)
  19. Kuainisha sentensi kulingana na maana zilizomo
   Mkiondoka wawiliwawili, mtafika haraka.
   1. masharti
   2. sisitizi/kariri
   3. arifu/taarifa
 4. SWALI LA NNE: ISIMUJAMII
  1. Sifa za sajili ya Viwandani
   1. msamiati teule - kutaja bidhaa zinazozalishwa kama sukari
   2. kuchanganya ndimi - Kiingereza na lugha za kieneo, duty, boiler
   3. sentensi ndefu katika kutoa taratibu na masharti kazini
   4. maswali yanayohitaji majibu moja kwa moja ili kutaka kujua ukweli kuhusu suala fulani
   5. maswali ya balagha - Ukichelewa kazini, unataka nini?
   6. lugha ya maagizo/uamrishaji - Mtu yeyote asipige simu wakati wa kazi!
   7. ukali - Hakuna kubembelezana tena!
   8. kurejelea sehemu za sheria, katiba au mkataba wa kuajiriwa
   9. kauli kamilifu kwa sababu ni lazima kueleweka bila utata
   10. utohozi-meneja, mashine, trakta
   11. misimu - Sitaki mtu aniletee!
   12. kutozingatia sarufi/lugha legevu - Baadhi ya wafanyakazi huenda hawana kisomo kingi.
    (hoja 5 na mifano ambatani x 1 = 5)
  2. Sifa za sajili ya mazungumzo ya nyumbani baina ya wanandoa katika dondoo
   1. unyenyekevu kuashiria mapenzi - Polepole Mama Mercy!
   2. Lugha yenye ahadi - ...tutakuwa na muda wa kila kitu
   3. kutotaja jina halisi mwenza na badala yake kutumiamajina ya watoto - Mama Mercy
   4. maswali elekezi- Unanilewa...?
   5. kukata kauli - Mama Mercy anamkatiza mwenzake kwa kusema ana njaa.
   6. kulumbana - Wahusika wote wawili wanazungumza.
   7. kubadili mada ghafla-Mama Mery amwita Dadii na kusema ana njaa.
   8. kuchanganya ndimi - bad coincidence
   9. kauli fupi ambazo sio sentensi - maneno ya Mama Mercy
    (hoja 5 na mifano ambatani x 1 = 5)

ADHABU
Ondoa nusu alama kwa kila kosa linalotokea huku ukiweka upeo wa jumla ya makosa ya kuadhibiwa katika kila moja ya maswali hayo manne yaani, Ufahamu, Ufupisho, Matumizi ya Lugha na Isimujamii.
Adhabu kwa makosa ya sarufi na hijai katika kila swali itekelezwe kwa lengo la kumhadharisha mtahiniwa kwamba ni sharti azingatie kanuni za kuandika na sarufi bora ili kuyawezesha mawasiliano kamilifu kwa njia ya maandishi. Hata hivyo, adhabu isiwe na lengo la kumtia hofu mtahiniwa hadi aogope kuandika majibu kwa mtihani. Aidha, adhabu hii itekelezwe mwishoni mwa swali wala sio papo hapo linapotokea kosa. Muhimu zaidi ni kwamba kosa katika kuandika jibu lisiathiri usahihi wa jibu lenyewe.
Huu ndio ukurasa wa mwisho uliochapishwa.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mangu High School Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?