Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kassu Jet Joint Mock Exams 2023

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.


MASWALI

SEHEMU A: HADITHI FUPI
YUSSUF SHOKA HAMAD: Mzimu wa Kipwerere

  1. Lazima
    …akikiomba radhi kile kitawi cha mti kilichonasa kwenye kazu yake ya rangi ya udongo iliyoficha kiwingu cha nongo kwa kukosa kuoshwa tangu ainunue! Nikauacha mpambano ule kati ya mzimu na mwenye dhamana ya mzimu ambao sina shaka ulidumu hadi asubuhi pale wanakijiji walipofika kushuhudia siri nzito iliyomezwa na mzimu ule waliokuwa wakiogopa na kuamini kiasi cha kuabudu kwa unyenyekevu na uchaji uliotukuka!
    1. Eleza muktadha wa dondoo. (alama 4)
    2. Fafanua umuhimu wa mandhari katika dondoo hili. (alama 4)
    3. Fafanua mbinu za kimtindo katika dondoo. (alama 4)
    4. Onyesha jinsi itikadi ilivyomwezesha ‘mwenye dhamana ya mizimu’ na wenzake kuwafanya wanakijiji kuogopa na kuamini mzimu wa Kipwerere kiasi cha kuabudu kwa unyenyekevu na uchaji uliotukuka. (alama 8)

SEHEMU B: TAMTHILIA
T. AREGE: Bembea ya Maisha
Jibu swali la 2 au la 3

  1.  
    1. ‘Hizo juu-chini chini-juu ndizo utamu wake. Ni kama maisha kwa jumla. Yana pandashuka ndiyo lakini pandashuka hizo ndizo hutupa kuridhika hatimaye tunapozishinda.’
      Thibitisha kuwa maisha yamejaa pandashuka ukirejelea tamthilia: Bembea ya Maisha (alama 10)
    2. ‘Umenirudisha nyuma kweli katika siku zile za ujana wangu. Asubuhi niko skuli majira ya alfajiri…’’
      1. Eleza mbinu ya kimtindo inayojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)
      2. Fafanua mifano mingine minane (8) ya matumizi ya mbinu hii katika tamthilia (alama 8)

3. “Mwenyewe ona ulivyokonda kama ng’onda!” 

  1. Yaweke maneno haya katika muktadha wake. (alama 4)
  2. Tambua mbinu mbili za lugha katika dondoo hili. (alama 4)
  3. Eleza umuhimu wa msemaji wa maneno haya. (alama 6)
  4. Fafanua umuhimu wa mandhari ya dondoo hili. (alama 6)

SEHEMU C: RIWAYA
A. MATEI: Chozi la Heri
Jibu swali la 4 au la 5

  1.  
    1. Hakiki mtindo wa mtunzi katika kifungu kifwatacho: (alama 8)
      “Suala la polisi na wanajeshi kutatua mizozo midogo midogo kwa makeke na bunduki ni jambo
      ambalo limeanza kupitwa na wakati; ni sawa na kumwua chawa kwa fimbo! Raia wanahitaji
      zaidi ushauri badala ya vipigo. Kutatua tofauti zetu kwa vita ni kama kufukuta moto zaidi, na
      amani tuliyoazimia kupata haipatikani. Vilio vya raia kuhusu kile wanachokiiita extra judicial
      killings vimehanikiza kote. Huenda tusiwe wahusika katika visa hivi. Hata hivyo, ni vyema
      kutahadhari kabla ya hatari. Wakati mwengine, ndugu zangu amani haiji kwa ncha ya upanga!”
    2. “Mwandishi amewasawiri vijana kuwa na nyoyo zilizoshiba wema.” Dhihirisha ukweli wa kauli iliyosisitizwa kwa hoja 12 toshelevu. (alama 12)
  2. “... jua langu li karibu kuchwa... sasa muda umefika. Hutakuwa na lawama duniani hata ahera iwapo utafunga akidi.”
    “... Hata mimi nimeliwazia jambo hili kwa muda. Hata hivyo, moyo wangu umekuwa yabisi, hisia zangu zimekufa ganzi.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Msemaji wa kauli ‘hutakuwa na lawama duniani hata ahera’ kando na kuwa msalihina, ana wasifu gani mwingine kwa mujibu wa dondoo hili? (alama 4)
    3. Jadili jinsi suala la uozo linavyojitokeza kwenye Jumuiya ya Chozi la Heri. (alama 12)

SEHEMU D: USHAIRI
Jibu swali la 6 au la 7

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali
    Ndugu zangu waadhama, leo nawaulizia
    Mlo Embu na Giriama, wote mpate sikia
    Wazima hata vilema, rai zenu nanuia
    Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
    Miezi tisa tamima, tumbo lake nakalia
    Kwa uwezo wa Karima, mama akajizalia
    Ni mdogo sijasema, shida zangu ajulia
    Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
    Mate kwake nimetema, mama hakunichukia,
    Tumbo langu likiuma, kinyesi namtupia
    Chakula hakuninyima, na dawa ya malaria
    Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
    Ni mtu mwenye huruma, tena wa kuvumilia
    Hasa uwe ni yatima, baba amejifilia
    Akufanyia huruma, mradi kutimizia
    Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
    Japo nimpe heshima, sioni kama murua
    Wema wake nikipima, mbali bado huzidia
    Kanipa nyingi huduma, nini nitamlipia?
    Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
    Nikimpa darahima, naona sijatimia
    Unga viazi na nyama, sioni kama fidia
    Zawadi zote kipima, ya kumpa sijajua
    Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
    Kwa heshima yake mama, kwaheri nawapungia
    Naondoka himahima, swali langu nawachia
    Nenda keti huko nyuma, jibu lenu nangojea
    Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
    (Wallah Bin Wallah, Malenga wa Ziwa Kuu)
    Maswali 
    1. Eleza muundo wa shairi hili (alama 4)
    2. Andika bahari zinazojitokeza katika shairi kwa kurejelea:
      1. vina (alama 1)
      2. vipande (alama 1)
      3. mishororo (alama 1)
    3. Kwa kutolea mifano, onyesha mbinu alizotumia mshairi kuzingatia arudhi. (alama 3)
    4. Tambua nafsineni katika shairi hili. (alama 1)
    5. Bainisha mbinu zozote mbili za kimtindo katika shairi hili. (alama 2)
    6. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari (alama 4)
    7. Tambua toni ya shairi hili (alama 1)
    8. Andika maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika shairi (alama 2)
      1. darahima
      2. fidia
  2. Soma shairi lifuatalo kisha uyajibu maswali
    Azali machozi yalilowesha mashavu yangu
    Michirizi yakafanya na mitaro kuchimba
    Chini yakadondoka na mchanga kulowesha
    Utamu wake wa chumvi chumvi niliulamba
    Nikapata hamaniko kuliondoa pasi kufahamu
    Wakati mwingine yalichochea usingizi nikapata amani
    Wakati huo yalikuwa ni maji tu
    Maji, maji yaliyokolea chumvi.

    Leo hii katika makako haya
    Bado ninalia kama mtoto mdogo
    Aliyenyimwa haki yake
    Ingawa hutokea kwa tukizi
    Nalia bado ndiyo ela si kwa sauti tena
    Hulia kubwa ninapofika na kuliziba langu koo
    Fundp hilo chungu huyafungua Masika
    Ya mvua isiyofanya mawingu mazito meusi.

    Hadi leo nimelia vilio vingi
    Vipo niliapo nikiwa na wandani
    Huku tukimenyana na vikombe viloshiba chai
    Vipo niliapo nikiwa pweke
    Nikizongwa na upweke wa chumba changu
    Vilio vya kimnya visivyotaka kuhaniwa
    Ni hivi vilio vya upweke
    Ambavyo vyanituma shairi kuandika
    Hivi vinavyotoka chini moyoni
    Kwenye kiini cha chembe cha moyo.

    Nimetambua kuwa matozi haya hatakauki
    Lau yakapanguswa kwa kitambaa laini cheupe.
    Michirizi yake hukauka lakini chemichemi zake hazikauki.
    Chozi hili lina nguvu zinazozidi kiangazi

    Halichi umri
    Halichi cheo
    Halichi jinsia
    Halichi dini
    Halichi uwezo
    Chozi hili humea katika bonde la wetu unyonge
    Chozi hili huvunja kingo za heshima na staha
    Chozi hili huyeyuka kutoka kitovu cha utu
    Chozi hili halikauki au likiwa,lina siha bado
    Chozi hili ni daraja kati ya mawili yasiyoonekana kwa macho
    Chozi hili lina nguvu kuliko silaha

    Chozi hili litakauka
    Pale moyo utakapokauka
    Na mkono kuzipa
    Hadithi zisizotangazwa za hakina Phili.

    Maswali 
    1. Hili ni shairi la aina gani? Tetea jibu lako. (alama 3)
    2. Chozi halibagui. Kwa mujibu wa shairi hili, eleza ukweli wa kauli hii. (alama 3)
    3. Eleza aina za urudiaji katika shairi hili. (alama 3)
    4. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 1)
    5. Mtunzi wa shairi hili amefaulu kutumia uhuru wake. Fafanua. (alama 2)
    6. Jadili matumizi ya aina zifuatazo za mistari katika shairi hili. (alama 2)
      1. mishata
      2. kifu
    7. Eleza aina zozote tatu za taswira katika shairi hili. (alama 3)
    8. Kwa mujibu wa shairi hili, ni muhimu kulia. Tetea ukweli wa usemi huu huku ukitolea mifano maridhawa. (alama 1)
    9. Eleza matumizi ya vipengele vifuatavyo vya kimtindo katika shairi hili: (alama 2)
      1. chuku
      2. tasfida

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

  1. Mababu zetu waliturithisha heshima, utu, utamaduni wa amani, imani na upendo. Tunatambua nia yao njema ya kuona jamii ikiishi kwa utulivu, umoja, mshikamano na uelewano. Leo hii nyuso zetu zimesawijika. Nyuso zimeinama kwa matokeo mabaya ya kitendo cha ubinafsi, unyama na ukatili cha mmoja wetu. Kama jamii, kama watu wa ukoo wa Shani wa Miramba, tunajitenga na ila hii. Tunamkana Kaliko wa Ndaya. Damu yake si yetu. Tunakemea na kulaani kitendo chake cha ubakaji. Tunalaani umaluuni huu kwa kinywa kipana. Mababu zetu wamemkataa. Mungu wetu mwenye kutaka heri kwa waja wote atuepushe adhabu na ghadhabu yake. Tunaomba dua kwako Mungu wa Mlima mkuu uliovikwa kofia ya theluji na kutukuka. Yalinde mashamba yetu tupate mazao mazuri; ila iliyoingia kwetu isije na kiangazi. Mawindo ya usasi wetu yasitupotelee kutokana na kasoro hii. Tunaomba mito yetu isikauke tusikose kitoweo humo na maji kwa mifugo wetu. Bariki ukoo wetu mtukuka. Tubaki imara kama mwamba. Ukoo wetu ni nyota siku zote. Ndiyo ni nyota! Ukoo wa Shani wa Miramba udumu milele!
    1. Bainisha kipera cha utungo huu na utoe ushahidi wako. (alama 2)
    2. Taja sifa zozote tano za kipera hiki. (alama 5)
    3. Kipera hiki kina nafasi gani kwa jamii? (alama 5)
    4. Mwasilishaji wa kipera hiki anahitajika kuwa wasifu upi ili kukifanikisha? Fafanua kwa hoja tano. (alama 5)
    5. Jamii inayohusishwa kifunguni inajiendelezaji kiuchumi? (alama 3)



MWONGOZO

SEHEMU A

YUSSUF SHOKA HAMAD: Mzimu wa Kipwerere

  1. Lazima
    …akikiomba radhi kile kitawi cha mti kilichonasa kwenye kazu yake ya rangi ya udongo iliyoficha kiwingu cha nongo kwa kukosa kuoshwa tangu ainunue! Nikauacha mpambano ule kati ya mzimu na mwenye dhamana ya mzimu ambao sina shaka ulidumu hadi asubuhi pale wanakijiji walipofika kushuhudia siri nzito iliyomezwa na mzimu ule waliokuwa wakiogopa na kuamini kiasi cha kuabudu kwa unyenyekevu na uchaji uliotukuka!
    1. Eleza muktadha wa dondoo. (alama 4)
      1. Ni maneno ya msimulizi
      2. Anamrejelea Salihina
      3. Walikuwa katika Mzimu wa Kipwerere
      4. Msimulizi alikuwa amewafumania Bishoo na Salihina katika mzimu na wakati Salihina alipokuwa akitoroka akashikwa na kitawi cha mti hivyo akapiga mayowe akiomba msamaha. 4 x 1 = 4
    2. Fafanua umuhimu wa mandhari katika dondoo hili. (alama 4)
      1. Kubainisha mgogoro katika hadithi – mgogoro uliopo unaotokana na itikadi unaotumiwa na kina Salihina kuwalaghai wanakijiji.
      2. Kuwatambulisha wahusika: Salihina na Bishoo
      3.  Kuchimuza maudhui: unafiki – Salihina anajifanya kuwa mdumishaji wa maadili ilhali yeye ndiye alikuwa akilangua dawa za kulevya.
      4. Kutambulisha sifa za wahusika: Bishoo anabainika kuwa mwongo kwa kuwa anamdanganya mumewe kuwa alikuwa akienda kumwona mtoto mgonjwa ilhali alikuwa anaenda kwa Salihina.
      5. Kuibua dhamira ya mwandishi: Kuonyesha madhara ya ushirikina na itikadi: imani kuhusu Mzimu wa Kipwerere unawatia wanajamii hofu ilhali hakukuwa na mizimu au mashetani yoyote katika kichaka hicho.
      6. Kuendeleza ploti – kusuluhisha taharuki kuhusu kuwepo kwa mashetani katika mzimu kwa kuonyesha kuwa hakukuwa na shetani yeyote ila wajanja kama kina Salihina. Zozote 4 x 1 = 4
    3. Fafanua mbinu za kimtindo katika dondoo. (alama 4)
      1. Tashihisi/uhaishaji - akikiomba radhi kile kitawi cha mti
      2. Taswira - kilichonasa kwenye kazu yake ya rangi ya udongo iliyoficha kiwingu cha nongo kwa kukosa kuoshwa tangu
      3. Nidaa - ainunue!
        uliotukuka!
      4. Kejeli - Nikauacha mpambano ule kati ya mzimu na mwenye dhamana ya mzimu
        4 x 1 = 4
    4. Onyesha jinsi itikadi ilivyomwezesha ‘mwenye dhamana ya mizimu’ na wenzake kuwafanya wanakijiji kuogopa na kuamini Mzimu wa Kipwerere kiasi cha kuabudu kwa unyenyekevu na uchaji uliotukuka. (alama 8)
      1. Kuna itikadi kuhusu chanzo cha kichaka cha Mzimu wa Kipwerere – inaaminika kuwa kichaka hicho kilitokana na kaburi la mwanamke aliyeitwa Kipwerere.
      2. Inaaminika kuwa yeyote aliyekiuka miiko kuhusu kutoingia katika mzimu angetolewa kama kafara kwa mizimu.
      3. Wanajamii wa eneo la Mzimu wa Kipwerere wanaamini kuwa Salihina angeweza kuwasiliana na mizimu. Hivyo, wanapotaka kuandaa sherehe kama vile jando wanamtuma Salihina kuzungumza na mizimu.
      4. Wanajamii wa eneo la Kipwerere kutoruhusiwa kupita kichaka hicho saa sita mchana na usiku wote. Wanajamii hawakupewa sababu zenye mashiko za kuwanyima ruhusa ya kupitia kichaka hicho bali walitishiwa tu kuwa wangetolewa kama kafara kwa mzimu.
      5. Kuamini kwamba taa zilizowaka usiku katika Mzimu wa Kipwerere ziliwashwa na shetani wa mzimu ili kuwapa watoto wake chakula.
      6. Kuamini kwamba mwanamke na mwanamume waliozungumza walikuwa shetani na mkewe. Inadaiwa kuwa waliungumza wakati watoto wao walikuwa wamelala.
      7. Mashetani wanavuta sigara - Kuamini kwamba harufu ya sigara iliyotoka katika mzimu ilitokana na shetani aliyekuwa akivuta sigara.
      8. Kuamini kwamba kulikuwa na wimbo uliokuwa kama ufunguo wa kuingia katika mzimu.
        8 x 1 = 8

SEHEMU B

T. AREGE: Bembea ya Maisha
Jibu swali la 2 au la 3

  1.  
    1. ‘Hizo juu-chini chini-juu ndizo utamu wake. Ni kama maisha kwa jumla. Yana pandashuka ndiyo lakini pandashuka hizo ndizo hutupa kuridhika hatimaye tunapozishinda.’
      Thibitisha kuwa maisha yamejaa pandashuka ukirejelea tamthilia: Bembea ya Maisha (alama 10)
      1. Sara alikuwa buheri wa afya alipoolewa na Yona. Baadaye anapata ugonjwa wa moyo kutokana kupigwa na Yona.
      2. Sara na Yona wanakaa muda mrefu bila mtoto. Wanasimangwa na kudharauliwa na wanajamii. Hata hivyo, wanajaliwa Neema, Asna na Salome
      3. Yona aliyekuwa mwalimu hohari baadaye anafutwa kazi kutokana na ulevi.
      4. Elimu ya mtoto wa kike haikuthaminiwa katika enzi za kina Sara. Sasa inathaminiwa kwa kuwa binti zake Yona wamesoma na kuhitimu.
      5. Sara anapougua na kushindwa kupika, Dina anakuja kumsaidia kupika
      6. Wazazi wa kijijini walijilelea watoto wao na kuwaadilisha kwa mfano, Sara.Wazazi wa sasa kama Neema wanakosa muda wa kutosha na watoto wao kutokana na kazi nyingi.
      7. Yona anatelekeza majukumu yake ya nyumbani baadaye anaepa kumsaidia mkewe katika kazi za nyumbani kama kupika.
      8. Sara anasema kuwa barabara za mjini zilikuwa mbovu. Siku hizi zimesakafiwa na usafiri umekuwa wa haraka.
      9. Watoto wa Dina zamani walikuwa maskini sasa wana afadhali
      10. Sara na Yona wanatengwa kwa kukosa mrithi. Neema anajaza pengo hilo kwa kuusimamia mji wa Yona vizuri.
      11. Sara anapougua Neema anampeleka hospitalini. Anatibiwa na mwishowe
        akapona.
      12. Nduguze Neema (Salome na Asna) wanapokosa karo, Neema anawalipia hivyo kuendeleza masomo yao.
      13. Neema anamtumia baba yake (Yona) pesa za kununua dawa. Hata hivyo, Yona anatumia pesa hizo kwenda kwa wazee wenzake ili asionekane shabiki.
      14. Yona anapofutwa kazi watu wanawatenga na kuwaita maskini wa fedha lakini mwishowe Neema anamsaidia.
      15. Mwanzoni Yona hakuweza kuelewa athari ya ugonjwa wa Sara lakini baadaye anaelewa na kuwa tayari kumsaidia.
      16. Yona alikuwa wa kwanza kuingia chuoni kijijini mwao lakini anamalizia kuwa mlevi hodari jambo linalomfanya kushindwa kufanya kazi.
      17.  Asna anaona kuwa ndoa ina mitihani chungu nzima ambayo haina silabasi mahususi, hata hivyo, Sara anampa ushauri kuwa si ndoa zote zina changamoto na kumtia moyo aolewe.
      18. Zamani Neema alikuwa anaona kuwa baba yake hakuwathamini yeye na wanuna wake lakini baadaye anagundua kuwa baba yao (Yona) anawapenda na kuwathamini.
        Zozote 10 x 1 = 10
    2. ‘Umenirudisha nyuma kweli katika siku zile za ujana wangu. Asubuhi niko skuli majira ya alfajiri…’’ 
      1.  Eleza mbinu ya kimtindo inayojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)
        1. Mbinu rejeshi / Kisengerenyuma – umenirudisha nyuma kweli
          kutaja -1
          kueleza -1
      2. Fafanua mifano mingine minane (8) ya matumizi ya mbinu hii katika tamthilia (alama 8)
        Mifano zaidio ya mbinu rejeshi:
        1. Dina aneleza kuhusu maisha ya awali ya familia ya Yona na Sara ambapo walipata masimango kwa kukosa mtoto.
        2. Yona anakumbuka wakati alipokuwa mwalimu alivyokuwa akibeba vitabu vya wanafunzi kwa baiskeli ili kuvisahihisha wikendi.
        3. Neema anakumbuka namna usafiri wa zamani ulivyokuwa mgumu kabla ya maendeleo ya teknolojia. Safari iliyochukua siku tatu sasa inachukua saa chache tu.
        4. Bunju anasema kuwa zamani Neema alikuwa anamheshimu lakini sasa heshima hiyo imepungua.
        5. Dina anamkumbusha Kiwa namna Yona alikuwa akimtesa na kumpiga Sara hadi anapoteza fahamu.
        6. Bunju alimwachia Neema mshahara wake ili awasaidie wazazi wake na kumwelimisha Asna.
        7. Kupitia kwa mbinu hii, tunapata kujua kwa Salome aliwahi kuishi na familia ya Neema na kwamba alipata ufadhili wa kwenda ng’ambo.
        8. Asna anasema kuwa zamani watoto wa Dina walidharauliwa kwa kuwa maskini, tofauti na alivyo sasa.
        9. Zamani Yona alipenda dini. Baadaye aliacha dini na kuwa mlevi baada ya kushinikizwa na wenzake chuoni.
        10. Sara anakumbuka zamani akiwa angali mzima na afya yake.
        11. Sara anamkumbusha Yona kuwa alipokuwa na afya yake walishirikiana kutafuta riziki ya kuwalea watoto wao.
        12. Sara anakumbuka namna ambavyo Bunju aliokoa maisha ya Neema.
        13. Neema anakumbuka namna Bunju alivyompata barabarani katika ajali mbaya.
          zozote 8 x 1 = 8
  2. “Mwenyewe ona ulivyokonda kama ng’onda!”
    1. Yaweke maneno haya katika muktadha wake. (alama 4)
      1. Haya ni maneno ya Sara. (al. 1)
      2. Anamwambia Asna (al 1)
      3. Walikuwa chumbani mwa Asna kule mjini (al.1)
      4. Baada ya Sara kuona jinsi ambavyo Asna alivyokuwa akikumbwa na changamoto nyingi mjini na kumtaka arudi kijijini naye Asna akakataa kwa kuwa alikuwa ameelimika na kutaka kujitegemea binafsi. (alama 1)
    2. Tambua mbinu mbili za lugha katika dondoo hili. (alama 4)
      Tashbihi – konda kama ng’onda!
      Nidaa -Ng’onda! (kutaja 1, mfano 1= 2x2 = 4)
    3. Eleza umuhimu wa msemaji wa maneno haya. (alama 6)
      Umuhimu wa Sara:
      1. kielelezo cha mlezi bora- anatoa ushauri kwa watoto wake
      2. Anaonyesha uvumilivu. Maradhi yamemfanya akonde sana lakini anavumilia
        • alivumilia mateso ya mumewe Yona
        • alivumilia masimango ya watu alipokuwa hana watoto na alipopata wasichana tu.
      3. Anadumisha utamaduni wa jamii ambapo mwanamke anafaa kumtumikia mumewe
        Kila wakati- nafasi ya wanawake katika jamii.
      4. Anaendeleza maudhui ya ugonjwa
      5. Anaendeleza maudhui ya ndoa
      6. Anaendeleza maudhui ya utiifu- alikuwa mtiifu kwa mumewe Yona
        zozote 6x1 = 6
    4. Fafanua umuhimu wa mandhari ya dondoo hili. (alama 6)
      1. Kuonyesha mkengeuko- Asna amekengeuka
      2. Kuonyesha changamoto za ndoa:
        • kati ya Neema na Bunju
        • Kati ya Sara na Yona
      3. Kuonyesha ushauri nasaha unaotolewa na Sara kwa Asna
      4. Nafasi ya mwanamke katika jamii – wapishi bora
      5. Malezi- Sara alivyowalea watoto wake
      6. Elimu na changamoto zake- Asna kutopata kazi, anaishi kwenye SQ
      7. Kazi- Asna anafanya kazi ya vibarua
      8. Mandhari ya mjini mabadiliko/ mkengeuko- watu wa mjini wanastahabu kukonda ili
        Wapendeze

SEHEMU C

A. MATEI: Chozi la Heri

  1.  
    1. Hakiki mtindo wa mtunzi katika kifungu kifwatacho: (alama 8)
      “Suala la polisi na wanajeshi kutatua mizozo midogo midogo kwa makeke na bunduki ni jambo
      ambalo limeanza kupitwa na wakati; ni sawa na kumwua chawa kwa fimbo! Raia wanahitaji zaidi ushauri badala ya vipigo. Kutatua tofauti zetu kwa vita ni kama kufukuta moto zaidi, na amani tuliyoazimia kupata haipatikani. Vilio vya raia kuhusu kile wanachokiiita extra judicial killings vimehanikiza kote. Huenda tusiwe wahusika katika visa hivi. Hata hivyo, ni vyema kutahadhari kabla ya hatari. Wakati mwengine, ndugu zangu amani haiji kwa ncha ya upanga!” 
      • Taswira oni – polisi na wanajeshi wanasawiriwa kutumia makeke na bunduki kusuluhisha mizozo.
      • Kinaya – polisi na wanajeshi wanaotumainiwa kuwapa wananchi usalama ndio wanaowatishia kwa kuwakabili kwa bunduki na makeke. Pia wanatafuta kuleta amani kwa vita.
      • Tashbiha – ni sawa na kumwua chawa kwa fimbo! Pia, kutatua tofauti zetu kwa vita ni kama kufukuta moto zaidi.
      • Chuku – ni sawa na kumwua chawa kwa fimbo!
      • Taswira hisi – Vilio vya raia kuhusu …extra judicial killings vimehanikiza kote.
      • Taswira sikivu – Vilio vimehanikiza kote.
      •  Kuchanganya ndimi – wanachokiiita extra judicial killings.
      • Methali – ni vyema kutahadhari kabla ya hatari.
      • Jazanda – kumwua chawa kwa fimbo, kufukuta moto,
        Hoja zozote 8X1 =alama 8 
    2. “Mwandishi amewasawiri vijana kuwa na nyoyo zilizoshiba wema.” Dhihirisha ukweli wa kauli iliyosisitizwa kwa hoja 12 toshelevu. (alama 12)
      • Vijana waliotumwa na Masharika yasiyokuwa ya Kiserekali wanawasaidia Mwanaheri na Lime kwa kuwapa ushauri nasaha kambini Msitu wa Mamba. Ushauri huu unawajasirisha kuendeleza na maisha licha ya uchungu waliopitia.
      • Kairu, Chandachema, Mwanaheri na Zohali wanampa Umu motisha ya kuendelea na maisha kwa kumfahamisha changamoto walizozipitia nao.
      • Umu anamsaidia Hazina kwa kumwomba Naomi ampe (Hazina) hela za kununua chakula. Naomi amtupiapo huyu shiling ishirini, Umu anamwongeza shilingi mia mbili alizokuwa amejiwekea kama akiba.
      • Hazina anamsaidia Umu kwa chakula anapofika mjini Karaha asiwe na msaidizi. Baadaye anampeleka kwa Makao ya Mama Julida ambako anapata hifadhi.
      • Apondi anasisistiza haja ya walinda usalama kutumia diplomasia badala ya mtutu wa bunduki kukabiliana na umma mizozo izukapo.
      • Alipokuwa mwanafunzi, Lunga anatetea uhifadhi wa mazingira. Anawakashifu baadhi viongozi kwa unyakuzi wa ardhi hivi kuharibu mazingira.
      • Mwangeka na Apondi wanamchukua Umu kuwa mwana wao wa kupanga hivyo kumpa familia aliyoikosa kwa kutenganishwa na nduguze. Wanayafadhili masomo yake mpaka chuo kikuu hivi kumpa mstakabali mwema maishani.
      • Umu anakuwa kielelezo bora kwa Sophie bintiye Apondi. Kwa mujibu wa Apondi, Umu ndiye mtu wa pekee anayeweza kuzidhibiti hasira za Sophie na amekuwa wa msaada mkubwa kwa kumwelekeza kupitia kipindi kigumu cha kujitambua/ujana.
      • Kwa maneno yake mwenyewe, Dick anakikri kuwa amekuwa kielelezo kwa vijana walioamini kuwa mhalifu hawezi kubadilika. Anaacha kuuza mihadarati na kufwata elimu hivi kuwapa changamoto ya kufwata mkondo huo.
      • Mwangeka anajisajili jeshini ili kulihudumia taifa lake. Uamuzi huu umetokana na mapenzi yake kwa nchi yake na watu wake.
      • Mwangemi na Neema wanampanga Mwaliko hivyo kumpa mapenzi ya familia aliyotenganishwa nao. Isitoshe, wanampa msingi imara maishani kwa mstakabali wake mwema.
      • Neema anamwokota Riziki Immaculata jaani na kumpeleka kwenye kituo cha polisi. Baadaye, pamoja na askari mmoja, wanamwezesha kupata makao katika kituo cha Watoto cha Benefactor.
      • Umu anawatafuta nduguze wanapotoroshwa na Sauna. Anaenda kuripoti kuibwa kwao kituoni kwa mapenzi yake kwao. Hata akosapo msaada alioenda kuutafuta pale, anaapa kuwatafuta baadaye.
      • Waridi anagharamia Masomo ya Chandachema licha ya umaskini uliomzonga. Chandachema anasema kuwa shangazi yake huyu alimlipia karo kwa kidogo alichopata kutoka kwa vikataa alivyokuwa navyo.
      • Watoto wa mitaani wanamsaidia Zohali kipindi cha kujifungua kwake kikaribiapo. Wanampeleka kwa kituo cha Wakfu wa Mama Paulina ambako anasaidiwa kupata salama.
      • Lunga anaupigania umma usiuziwe mahindi hatari. Alipokuwa mkuu wa kitengo cha uhifadhi wa nafaka alipinga mpango wa wakubwa wake kuwauzia Wahafidhina mahindi yaliyokuwa na sumu. Alitenda hivyo licha ya kufahamu kuwa alikuwa akijichongea kikazi.
      • Tila anamweleza Ridhaa kuwa atakapokuwa jaji wa mahakama kuu, angeawatendea haki washukiwa. Kwa mfano, agehakikisha kuwa kesi zilizocheleweshwa mahakamani kwa miaka zimeshughulikiwa upesi kwa manufaa ya wengi waliokuwa wakiozea rumande.
      • Mwalimu Meli anawakuza wanafunzi wake kuwa na mtazamo mpevu maishani. Analihimiza darasa lake Tila kuzingatia usawa wa kijinsia na kujiepusha kuupima uwajibikaji kwa msingi wa kijinsia pekee.
      • Utingo wa matawana moja anamshinikiza Kaizari na familia yake kuyaabiri. Hivi anawasaidia kuepuka uvamizi zaidi kutoka kwa majirani zake.
      • Mwalimu Dhahabu anakuwa tunu kubwa kwake Umu. Ndiye anayefanya mpango wake kupangwa na Mwangeka na Apondi.
      • Umu anawapenda Mwangeka na Apondi na kuwachukulia kama wazazi wake wa kumzaa.
      • Tila anamtahadharisha Kaizari na familia yake waondoke nyumbani kwao kuepuka uvamazi zaidi. Pia, anampa mkono wa udugu licha ya tofauti zao za awali na kumhakikishia kuwa atamchungia mali yake.
        Hoja zozote 12X1=alama 12
  2. “... jua langu li karibu kuchwa... sasa muda umefika. Hutakuwa na lawama duniani hata ahera iwapo utafunga akidi.”
    “... Hata mimi nimeliwazia jambo hili kwa muda. Hata hivyo, moyo wangu umekuwa yabisi, hisia zangu zimekufa ganzi.”
    Riwaya: Chozi la Heri
    “ ... jua langu li karibu kuchwa... sasa muda umefika. Hutakuwa na lawama duniani hata ahera iwapo utafunga akidi.”
    “... Hata mimi nimeliwazia jambo hili kwa muda. Hata hivyo, moyo wangu umekuwa yabisi, hisia zangu zimekufa ganzi.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      1. Kauli ya kwanza ni ya Ridhaa.
      2. Kauli ya pili ni ya Mwangeka.
      3. Walikuwa nyumbani mwa Mwangeka.
      4. Ridhaa alikuwa akimshawishi mwanaye Mwangeka aoe tena baada ya kumpoteza mkewe Lily kwenye kisa cha kuteketezwa moto na jirani yao Mzee kedi
        (Hoja 4x1=4)
    2. Msemaji wa kauli ‘hutakuwa na lawama duniani hata ahera’ kando na kuwa msalihina, ana wasifu gani mwingine kwa mujibu wa dondoo hili? (alama 4)
      1. Mshawishi- alijaribu kwa kila njia kumshawishi Mwangeka aoe tena.
      2. Mwenye matumaini- alikuwa na matumaini makubwa kuwa mwanaye angepata mchumba na aoe tena ili kumwondolea upweke na apate wajukuu.
      3. Mwenye mapenzi ya dhati- walipokuwa wakishiriki mazungumzo haya, alimtazama mwanaye kwa imani na mapenzi makuu huku akitamani angekuwa na kilimbo cha mapenzi angempa ili apate hamu ya kupenda tena.
      4. Ni mshauri mwema- alijua hali ya Mwangeka kubaki mjane katika umri mdogo ingemsumbua sana hivyo akamshauri atafute mke aoe.
      5. Anawajibika- alihamia nyumbani mwa Mwangeka ili kumpa tumaini na kumwondolea upweke baada ya kufiwa na mkewe na mwanaye Becky.
      6. Mtamaduni- alitamani Mwangeka aoe ili aweze kuendeleza ukoo wao na pia apate wajukuu.
        (Hoja 4x1=4)
    3. Jadili jinsi suala la uozo linavyojitokeza kwenye Jumuiya ya Chozi la Heri. (alama 12)
      1. Mauaji- polisi kuwakabili vijana waliokuwa wakiandamana na kuwafyatulia risasi.
      2. Ubakaji- mabarobaro watono wanawashambulia Lime na Mwanaheri nyumbani mwao na kuwabaka. Pete anabakwa akiwa mlevi na kuambulia ujauzito. Bwana Maya alikuwa na mazoea ya kumdhulumu Sauna kimapenzi.
      3. Kutengwa- Mavyaa wake Subira kumchukulia kama mgeni. Anasema msichana wa Bamwezi hubakia kuwa msichana tu hata akiwa na umri wa miaka tisini. Anamwona kama aliyewaletea mkosi.
      4. Kuozwa mapema- Pete anaozwa katika umri mdogo na mamake kwa ushirikiano na wajomba zake.
      5. Kuachishwa kazi- Lunga anafutwa kazi na wakubwa wake kwa kuwatetea wanyonge ambao walitakiwa kuuziwa mahindi yaliyoharibika,
      6. Ulanguzi wa watoto- Bi. Kangara anamwajiri Sauna kwenye matandao wake wa utekaji nyara na ulanguzi wa watoto.
      7. Ulanguzi wa dawa za kulevya- Buda anaendesha biashara ya kulangua dawa za kulevya huku akiwatumia vijana wadogo kama Dick kama mawakala kwenye biashara hii haramu.
      8. Ulaghai- vijana kukubali kutumiwa vibaya na viongozi ili kuiba kura. Wanawadanganya wakonge kuwapigia kura viongozi wasiostahili.
      9. Kutelekeza malezi- Naomi anamwachia mumewe Lunga jukumu la kuwalea wanao. Aidha, Fumba anatelekeza jukumu la kumlea mtoto wake mdogo. Neema anakiokota kitoto kichanga kilichokuwa kimetupwa kwenye jaa la taka na mamake mzazi.
      10. Uzinifu- Bw. Tenge kushiriki mapenzi nje ya ndoa. Pete anahadaiwa na Nyangumi kuwa atamwoa. Anampachika mimba na kumwacha huku akimrudia mkewe halisi. Zohali anashiriki mapenzi angali mwanafunzi na kupachikwa mimba. Fumba anahusiana kimapenzi na mwanafunzi wake na kumtia mimba.
      11. Usaliti- Selume anasalitiwa na mumewe. Anamwacha na kumuoa msichana wa kikwao. Annette na wanawe wanamsaliti Kiriri kwa kuondoka nchini na kumwacha katika ukiwa.
      12. Ufisadi- Buda kuwahonga polisi na maafisa wa forodhani ili aendeleze ulanguzi wa dawa haramu. Hazina ya Jitegemee ilikuwa ikwafaidi ndugu na jamaa wa watu wachache kinyume na malengo yake.
      13. Dhuluma- Mashamba ya wenyeji yananyakuliwa na walowezi hali iliyowaacha bila makao na ardhi ya kulima. Wachache waliokuwa na ardhi hawakuwa na hiari ya kupanda mimea waitakayo. Vilevile, baadhi wa wanaume wananyimwa haki ya unyumba na wake zoa kwa mfano Naomi, Subira na Annette wanaowaacha waume zao.
      14. Ajira ya mapema-watoto walishirikishwa kwenye ajira ya mapema. Kwa mfano Dick aliyetumiwa kulangua dawa za kulevya. Chandachema analazimika kuchuma majani chai ili aweze kujikimu.
      15. Mila potovu- Tuama anakeketwa na kuvuja damu sana. Kuna baadhi ya wanajamii walioichukulia tohara kwa wasichana kama kigezo cha msichana kuolewa.
        (Hoja zozote 12x1=12)

SEHEMU D: USHAIRI

6. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali
Ndugu zangu waadhama, leo nawaulizia
Mlo Embu na Giriama, wote mpate sikia
Wazima hata vilema, rai zenu nanuia
Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
Miezi tisa tamima, tumbo lake nakalia
Kwa uwezo wa Karima, mama akajizalia
Ni mdogo sijasema, shida zangu ajulia
Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
Mate kwake nimetema, mama hakunichukia,
Tumbo langu likiuma, kinyesi namtupia
Chakula hakuninyima, na dawa ya malaria
Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
Ni mtu mwenye huruma, tena wa kuvumilia
Hasa uwe ni yatima, baba amejifilia
Akufanyia huruma, mradi kutimizia
Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
Japo nimpe heshima, sioni kama murua
Wema wake nikipima, mbali bado huzidia
Kanipa nyingi huduma, nini nitamlipia?
Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
Nikimpa darahima, naona sijatimia
Unga viazi na nyama, sioni kama fidia
Zawadi zote kipima, ya kumpa sijajua
Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
Kwa heshima yake mama, kwaheri nawapungia
Naondoka himahima, swali langu nawachia
Nenda keti huko nyuma, jibu lenu nangojea
Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
(Wallah Bin Wallah, Malenga wa Ziwa Kuu)
Maswali

  1. Eleza muundo wa shairi hili (alama 4)
    1.  
      1. shairi hili lina beti saba
      2. kila ubeti una mishororo minne
      3. kila mshororo una vipande viwili
      4. shairi hili lina kibwagizo- Kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
      5. vina vya kati na vya mwisho vinatiririka.
      6. shairi lina mizani kumi na sita katika kila mshororo.
    2. Andika bahari zinazojitokeza katika shairi kwa kurejelea:
      1. vina (alama 1)
        mtiririko -vina vya kati na vya mwisho vinatiririka.
      2. vipande (alama 1)
        Mathnawi - lina vipande viwili kila mshororo.
      3. Mishororo (alama 1) tarbia- shairi lina mishororo minne kila ubeti.
    3. Kwa kutolea mifano, onyesha mbinu alizotumia mshairi kuzingatia arudhi. (al. 3)
      1. kuboronga sarufi-kinyesi namtupia badala ya namtupia kinyesi, leo nawauliza badala ya nawauliza leo.
      2. utohozi- malaria
      3. inkisari- nawapungia badala ya ninawapungia, naona badala ya ninaona, nawaulizia badala ya ninawaulizia, nenda badala ya naenda.
    4. Tambua nafsineni katika shairi hili. (alama 1)
      mtoto/mwana
    5. Bainisha mbinu zozote mbili za kimtindo katika shairi hili. (alama 2)
      1. swali la balagha- kipi cha kumpa mama, iwe ni yake fidia?
      2. tanakuzi- wazima hata vilema.
      3. taswira- kinyesi namtupia, kwaheri nawapungia.
      4. takriri- kipi cha kumpa mama iwe ni yake fidia, heshima
    6. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari (alama 4)
      Mate nimetema kwake na mama hakunichukia. Tumbo langu likiuma namtupia kinyesi. Hakuninyima chakula na dawa ya malaria.kipi cha kumpa mama ili iwe fidia?
    7. Tambua toni ya shairi hili (alama 1)
      Toni ya ushauri/ toni ya shukrani/toni ya furaha-kadiria mifano ya wanafunzi
    8. Andika maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika shairi (alama 2)
      1. darahima-pesa
      2. fidia-malipo

7. Soma shairi lifuatalo kisha uyajibu maswali
Azali machozi yalilowesha mashavu yangu
Michirizi yakafanya na mitaro kuchimba
Chini yakadondoka na mchanga kulowesha
Utamu wake wa chumvi chumvi niliulamba
Nikapata hamaniko kuliondoa pasi kufahamu
Wakati mwingine yalichochea usingizi nikapata amani
Wakati huo yalikuwa ni maji tu
Maji, maji yaliyokolea chumvi.
Leo hii katika makako haya
Bado ninalia kama mtoto mdogo
Aliyenyimwa haki yake
Ingawa hutokea kwa tukizi
Nalia bado ndiyo ela si kwa sauti tena
Hulia kubwa ninapofika na kuliziba langu koo
Fundp hilo chungu huyafungua Masika
Ya mvua isiyofanya mawingu mazito meusi.

Hadi leo nimelia vilio vingi
Vipo niliapo nikiwa na wandani
Huku tukimenyana na vikombe viloshiba chai
Vipo niliapo nikiwa pweke
Nikizongwa na upweke wa chumba changu
Vilio vya kimnya visivyotaka kuhaniwa
Ni hivi vilio vya upweke
Ambavyo vyanituma shairi kuandika
Hivi vinavyotoka chini moyoni
Kwenye kiini cha chembe cha moyo.

Nimetambua kuwa matozi haya hatakauki
Lau yakapanguswa kwa kitambaa laini cheupe.
Michirizi yake hukauka lakini chemichemi zake hazikauki.
Chozi hili lina nguvu zinazozidi kiangazi

Halichi umri
Halichi cheo
Halichi jinsia
Halichi dini
Halichi uwezo

Chozi hili humea katika bonde la wetu unyonge
Chozi hili huvunja kingo za heshima na staha
Chozi hili huyeyuka kutoka kitovu cha utu
Chozi hili halikauki au likiwa,lina siha bado
Chozi hili ni daraja kati ya mawili yasiyoonekana kwa macho
Chozi hili lina nguvu kuliko silaha

Chozi hili litakauka
Pale moyo utakapokauka
Na mkono kuzipa
Hadithi zisizotangazwa za akina Phili.

  1. Hili ni shairi la aina gani? Tetea jibu lako. (alama 3)
    Huru
    Sababu: 
    1. idadi ya mishororo inabadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
    2. idadi ya mizani inabadilika kutoka mshororo mmoja hadi mwingine.
    3. halina usawa vina
      aina- alama 1
      sababu - alama 2 x 1 = 2
  2. Chozi halibagui. Kwa mujibu wa shairi hili, eleza ukweli wa kauli hii. (alama 3)
    1. Halichi umri
    2. Halichi cheo
    3. Halichi jinsia
    4. Halichi dini
    5. Halichi uwezo
      zozote 3 x 1 = 3
  3. Eleza aina za urudiaji katika shairi hili. (alama 3)
    1. urudiaji wa neno- chozi, Halichi, vipo n.k
    2. urudiaji wa sentensi/kishazi - Halichi umri, vipo niliapo nikiwa...
    3. urudiaji wa silabi- kuchimba, niliulamba, vipo, niliapo n.k
    4. urudiaji wa virai - Chozi hili....
      zozote 3 x 1 = 3
  4. Fafanua nafsineni katika shairi hili. (alama 1)
    Mtu wa umri wa makamo - leo hii katika makamo haya. 1×1=1
  5. Mtunzi wa shairi hili amefaulu kutumia uhuru wake. Fafanua. (alama 2)
    1. Inkisari- viloshiba badala ya vilioshiba
    2. kuboronga sarufi/kufinyanga/kubanganga lugha - chini yakadondoka badala ya yakadondoka chini,wetu unyonge badala ya unyonge wetu.
    3. Lahaja - matozi badala ya machozi
      zozote 2 x 1 = 2
  6. Jadili matumizi ya aina zifuatazo za mistari katika shairi hili. (alama 2)
    1. mishata
      ambavyo vyanituma shairi hili kuandika
      fundo hilo chungu huyafungua masika
    2. kifu
      Hadithi zisizotangazwa za akina Phili.
  7. Eleza aina zozote tatu za taswira katika shairi hili. (alama 2)
    1. Taswira mguso /ya kugusa- Azali machozi yalilowesha mashavu yangu.
    2. Taswira onevu/oni/ya kuona- Azali machozi yalilowesha mashavu yangu.
    3. Taswira mwonjo/ya kuonja- utamu wake wa chumvichumvi.
    4. Taswira sikivu - bado ninalia kama mtoto mdogo.
      Zozote 3 x 1 = 3
  8. Kwa mujibu wa shairi hili,ni muhimu kulia. Tetea ukweli wa usemi huu huku ukitolea mifano maridhawa. (alama 1) 
    1. Huchochea usingizi wa mtoto....
    2. Kuondoa upweke....
  9. Eleza matumizi ya vipengele vifuatavyo vya kimtindo katika shairi hili: (alama 2)
    1. chuku
      Chozi hukauka pale moyo utakapokauka.
      Michirizi yakafanya na mitaro kuchimba.
      Fundo hilo chungu huyafungua masika
      1×1=1
    2. tasfida
      Chozi hukauka pale moyo utakapokauka - kufa kwa mtu.
      Aliyenyimwa haki yake - alinyimwa kunyonya titi la mamake.
      1 x 1 =1

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

  1. Mababu zetu waliturithisha heshima, utu, utamaduni wa amani, imani na upendo. Tunatambua nia yao njema ya kuona jamii ikiishi kwa utulivu, umoja, mshikamano na uelewano. Leo hii nyuso zetu zimesawijika. Nyuso zimeinama kwa matokeo mabaya ya kitendo cha ubinafsi, unyama na ukatili cha mmoja wetu. Kama jamii, kama watu wa ukoo wa Shani wa Miramba, tunajitenga na ila hii. Tunamkana Kaliko wa Ndaya. Damu yake si yetu. Tunakemea na kulaani kitendo chake cha ubakaji. Tunalaani umaruuni huu kwa kinywa kipana. Mababu zetu wamemkataa. Mungu wetu mwenye kutaka heri kwa waja wote atuepushe adhabu na ghadhabu yake. Tunaomba dua kwako Mungu wa Mlima mkuu uliovikwa kofia ya theluji na kutukuka. Yalinde mashamba yetu tupate mazao mazuri; ila iliyoingia kwetu isije na kiangazi. Mawindo ya usasi wetu yasitupotelee kutokana na kasoro hii. Tunaomba mito yetu isikauke tusikose kitoweo humo na maji kwa mifugo wetu. Bariki ukoo wetu mtukuka. Tubaki imara kama mwamba. Ukoo wetu ni nyota siku zote. Ndiyo ni nyota! Ukoo wa Shani wa Miramba udumu milele!
    1. Bianisha kipera cha utungo huu na utoe ushahidi wako. (alama 2)
      Maapizo - Kuna maombi maalum kuiepusha jamii na laana kutokana na kitendo cha ubakaji.
    2. Taja sifa zozote tano za kipera hiki. (alama 5)
      1. Hutolewa dhidi ya walioenda kinyume na matarajio ya jamii.
      2. Maombi huelekezwa kwa Mungu, miungu au mizimu.
      3. Hutolewa na watu maalum kwenye jamii k.v wazee, vingozi wa kidini
      4. Huwa na lugha ya kutisha na kutia woga.
      5. Lugha fasaha hutumika kuwasilisha maapizo.
      6. Alitenda uovu huelekezewa laana na mikosi.
      7. Huweza kutolewa kabla ya kula viapo.
      8. Huwasilishwa mahali maalum k.v chini ya miti ‘mitakatifu’, mapangoni, maeneo ya ibada, kando ya mito n.k
      9. Huweza kuandamana na kafara kwa miungu au mizimu.
      10. Kwa baadhi ya jamii, huwasilishwa wakati wakati maalum k..v asubuhi na mapema, jioni jua likitua n.k
      11. Wakati mwingine, aliyeenda kinyume na jamii huhitajika kutoa zawadi kwa mizimu ili asamehewe/atakaswe.
      12. Huwa na masharti makali yanayoelekeza namna ya kutolewa, wanaoshiriki na njia ya kutenda vitendo vinavyoandamana na maapizo.
      13. Yana utendaji/huandamana na matendo maalum k.v kuinua mikono, kutazama juu, kuinama sehemu fulani maalum, kupiga magoti n.k
      14. Kwa baadhi ya jamii kigezo cha umri au jinsia huzingatiwa kwa wanaoshiriki kuwasilisha maapizo k.m wazee wa kiume wa umri fulani(wakongwe)
    3. Kipera hiki kina nafasi gani kwa jamii? (alama 5)
      1. Huonya wanajamii dhidi ya matendo mabaya.
      2. Hutambulisha jamii inayohusika.
      3. Huendeleza mila na utamaduni wa jamii.
      4. Hukuza na kuendeleza umoja na mshikamano wa jamii.
      5. Hupitisha maadili mema kwa wanajamii.
      6. Ni namna ya wanajamii kuonyesha imani yao kuhusu miungu, mizimu n.k
      7. Huonyesha falsafa/msimamo/imani wa jamii kuhusu mambo mbali mbali.
    4. Mwasilishaji wa kipera hiki anahitajika kuwa wasifu upi ili kukifanikisha? (alama 5)
      1. Mjuzi wa lugha/awe mlumbi bora. Atumie lugha fasaha.
      2. Awe na umri unaofaa. Katika jamii nyingi, maapizo huwasilishwa na wazee.
      3. Fanani awe na nafasi/hadhi ifaayo katika jamii husika.m viongozi wa kidini ama watu maalum walioteuliwa
      4. Wakati mwingine avae maleba maalum yanayohitajika k.v mavazi ya kidini
      5. Sauti kakamavu na inayosikika vizuri.
      6. Aweze kutumia ishara na mindoko inayohitajika.
      7. Awe na uelewa mzuri wa utamaduni wa jamii husika.
    5. Jamii inayohusishwa kifunguni inajiendelezaje kiuchumi? (alama 3)
      1. Uvuvi - Mito yao ina kitoweo
      2. Ufugaji wa wanyama - Wana mifugo
      3. Kilimo - Wanatarajia mazao mazuri mashambani
      4. Uwindaji - Wanaombea mawindo
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kassu Jet Joint Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?