Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Sunrise Pre Mock Exams 2023

Share via Whatsapp
Maagizo 
  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  1. UFAHAMU: (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    “Asante baba, asante mama,” akasema Bahati jioni moja baada ya chajio, “Sijui ilitokeaje kukawa na watu wanaothamini binadamu wenye mahitaji maalumu katika jamii hii. Sitawauliza mlichofanya kunikinga na hukumu ya ukoo ya kuniangamiza; hayo mtakuja kunihadithia siku moja. Ila nataka mjue kwamba kuishi na ulemavu wa aina yoyote ile kuna dhiki kuu. Niliyokabiliana nayo baada ya uamuzi wenu wa kunipeleka shuleni hayawezi kutoshea hata chapisho la kurasa elfu.Si kudhihakiwa na miale ya jua; ngozi yangu inashindwa kuuhimili ukali wake, si kutengwa na marika, si kulazimika kusoma hati za kawaida hadi pale serikali ilipoanzisha sera ya kuhakikisha kwamba matini zote za kiusomi zimeandikwa pia kwa hati ambazo zinaweza kusomwa na wenye changamoto kama yangu, si kubaguliwa kazini....”Bahati alitua, akawatazama wazazi wake kama anayetaka kuona taathira ya maneno yake kisha akaendalea.

    “Msinione kama aliyekosa hisani, ila’ nataka niwaambie kwamba hata uamuzi wenu wa kunitafutia mlinzi kuandamana nami hadi shuleni ulinitia kwenye ngome zaidi.Nilijihisi kama niliyedhulumiwa zaidi katika kule kulindwa! Najua mlikuwa mnachelea kwamba ningekuwa windo rahisi kwa walanguzi wa binadamu ambao wanaamini kwamba viungo vyetu sisi ni dawa ya kutibia ndwele mbalimbali.Hata hivyo, katika kipindi chote hicho nilitamani kwamba mngenifunza mbinu za kujilinda mimi binafsi. Amini usiamini hata nilitamani kwamba ningetekwa nyara, nijadiliane na watesi wangu kuliko kupokwa nafasi ya kubuni mikakati ya kujihakikishia usalama”.

    “Mwanangu Bahati,” alisema mume wangu, “binadamu hawi jagina kwa kuzifuata tamaduni za jamii yake bila kuzichunguza. :haidhuru kwamba ilichukua muda kuyangamua haya'. La muhimu ni kwamba umeweza kuishi kama ndugu zako”.

    Nilimtazama mume wangu kwa macho yaliyokuwa yamepofushwa na dimbwi la machozi. Moyo uliituma akili yangu kurudi nyuma kule -e-e-e- kwenye miereka ya baada ya kuzaliwa kwa Bahati. Asubuhi hiyo ya kipupwe nilishika ujia ulioelekea kwenye msitu uliokuwa karibu na boma la Mzee Kedi, baba mkwe wangu; mgongoni nimeifungia mbeleko ambayo ilikisitiri kitoto changu. Nilitazama nyuma, nikaiona nyumba ambayo mimi na mume wangu tulikuwa tumechanga bia kuijenga.

    “Haya yote nayaacha,” nilijiambia, “nayaacha na mengine mengi. Nawaacha mabinti wangu wawili, namwacha mume wangu, naiacha kazi yangu, nayaacha maisha yangu wala sijuti kwa kuyaacha haya yote. Sina cha kujutia kwani imebidi kuondoka. Jamii yangu imenitema; mimi na mwanangu.Haina nafasi ya mwanangu, kwa hivyo nami nimeamua kwamba haina nafasi yangu kwa vile imesema huu ni mzigo wangu. Ikiwa ukoo umeamua kuwa hatima ya mwanangu huyu ni kuwa kitoweo cha fisi, basi na tuwe sote karamu ya fisi” nilitamatisha kauli yangu kisha nikayarudisha nyuma tena mawazo yangu.

    Nilikumbuka sauti ya muuguzi hospitalini siku ambayo nilijikopoa, “Pongezi Tamasha, Mungu amekutunukia kipusa”. Nilikifunua kitoto changu kilichokuwa kimefunikwa gubigubi, nikakitazama viguu, vikono, uso...kisha, ‘Mungu wangu!’ ikanitoka. “Dadangu, unastahili kumshukuru Mungu,” akasema muuguzi, “wapo wanawake, mimi mwenyewe nikiwemo, ambao hawajawahi kuambulia ujauzito, sikwambii hata kupoteza mimba.Huyu wako ni kiumbe kamili, kasoro yake i kwenye ngozi tu, na hii ni hali ambayo unaweza kukabiliana nayo. Hapa unionapo nimelazimika kumpa mume wangu talaka, mwenyewe alienda kortini akaiomba. Anadai kwamba hatusikilizani. Ila najua kiini cha haya yote ni kutoshika kizazi”.

    Nilimtazama huyo muuguzi kana kwamba hajasema  lolote. Nilimwona kama anayeuona mzigo wangu kuwa kanda la usufi. Huenda huyu muuguzi hakujua kwamba katika jamii yangu watoto wa aina hii ni kama pacha, huaminiwa kuwa nuksi kwa ukoo mzima, kwa hivyo hutupwa. Muuguzi huyu hakujua pia kwamba tayari nilikuwa na watoto wawili wa kike na huo tayari ulikuwa mzigo mkubwa kwangu kwani ilibidi kumhakikishia mavyaa kila mara kwamba hawa pia walikuwa watoto.

    Moyo ulinipa kukumbuka jitimai iliyojiandika usoni mwa mume wangu asubuhi hiyo alipokuja hospitalini. Alikitazama kitoto chetu kana kwamba anaona mzuka. Alinyamaza kwa muda, akashusha pumzi, kisha akanishika kwenye bega na kuondoka kwenye wodi. Machozi yalivunja kingo zake huko yanakohifadhiwa, nikalia kama mfiwa, Mume wangu alirudi tena baada ya siku mbili; anakuja kunipeleka nyumbani.


    “Mke wangu, naomba msamaha kwa kutokuja kuwatazama kwa siku mbili. Ilibidi nishauriane na  ukoo kuhusu tanzia hii.  Inavyoonekana ni kwamba msimamo wa baba na wazee wengine ni ule ule. Wanasema ukoo wa Baulanga haujawahi kupata mtoto wa aina hii, kwamba kumhifadhi mwana huyu kutakuwa kuupaka masizi ukoo. Wahenga hawatakubali tendo hili. Sijui nitakutetea vipi.Nimo kwenye njia panda,” mume wangu alikamilisha uzungumzi wake na kuelekea kwenye afisi ya mhasibu kukamilisha viviga vya kutuondoa hospitalini.

    “Huna haja ya kuniitetea. Sijafanya kosa lolote. Nililofanya ni kujaliwa kiumbe ambaye anaonekana kuwa punguani kwa misingi ya jamii yako. Nitakilinda kitoto hiki hata kifoni,” nilimwambia mume wangu mawazoni.
    1. “Kufanikiwa kwa watu wenye mahitaji maalumu kunategemea jamii.” Thibitisha kwa kutoa hoja sita kutoka aya tatu za kwanza. (alama 6)
    2. Kwa kurejelea aya ya nne hadi ya saba, onyesha jinsi unyanyasaji wa kijinsia unavyoendelezwa katika jamii hii. (alama 3)
    3. “Msimulizi anahimiza. uwajibikaji.” Thibitisha kwa kutoa hoja nne kutoka aya tatu za ‘ mwisho. (alama 4)
    4.  
      1. Andika kisawe cha, ‘hisani’ kwa mujibu wa taarifa. (alama 1)
      2. Eleza maana ya, ‘kuupaka masizi’ kulingana na taarifa. (alama 1)
  2. UFUPISHO (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.


    Wakenya walipoipata katiba mpya waliidhinisha mfumo wa ugatuzi. Katika mfumo huu, mamlaka ya serikali kuu katika uongozi, usimamizi na utumiaji wa rasilimali za nchi hupunguzwa. Kiasi Fulani cha mamlaka hutwaliwa na maeneo ya ugatuzi. Suala hili halikuzingatiwa katika katiba ya awali ambapo mamlaka yote yalikuwa mikononi mwa serikali kuu. Kutokana na upana na wingi wa maeneo, iliiwia vigumu serikali kuu kuhakikisha kwamba kulikuwa na usawa wa kimaendeleo katika sehemu nchini.

    Kwa mujibu wa katiba mpya, serikali kuu haina budi kuyasaidia maeneo yote ya ugatuzi ili yaweze kujinyanyua kiuchumi na kuboresha hali za maisha za wakazi wake. Vilevile ni jukumu la kila eneo la ugatuzi kuweka mikakati madhubuti ili kuchunguza na kubainisha rasirimali zote katika maeneo husika. Hili litasaidia kufumba rasilimali ambazo zinaweza kuchangia katika ustawishaji wa maeneo haya. Maeneo haya pia yanatakiwa kutafuta mbinu zitakazofanikisha uzalishaji na utumiaji wa rasilimali hizi kwa njia endelevu. Mojawapo ya mbinu hizi ni uongezaji thamani katika rasilimali yoyote inayozalisha kwenye eneo mahususi.

    Maeneo mengi  ya ugatuzi nchini humu yanategemea kilimo cha ufugaji kama mhimili wa uchumi. Licha ya kuwa nguzo, kilimo hiki hakijawahi kupigiwa darubini vizuri kwa lengo la kukiimarisha ili kiwanufaishe wenyeji kikamilifu. Aghalabu wafugaji wengi huandama mbinu za jadi za ufugaji ambazo haziwahakikishii ongezeko la mapato.Isitoshe, wafugaji hawa wanakabiliwa na tatizo katika soko la mifugo ambapo wengi hupunjwa na matapeli. Pamoja na haya, baadhi ya wakazi huuza mifugo nje ya nchi wakiwa wazimawazima bila kuwazia matokeo ya kitendo hiki. Si ajabu kuwaona ng’ombe, ngamia, mbuzi na kondoo wakipakiwa kwenye malori na kusafirishwa nje ya nchi. Ukweli ni kwamba jambo hili ni hatari sana, si kwa uchumi wa maeneo husika tu, bali pia kwa Kenya kwa jumla. Hii ni kwa kuwa walionunua mifugo wazimawazima wanaweza kuhiari kutowachinja na badala yake kuwatumia kama mbegu kwani baada ya muda huenda wanaonunua mifugo wakijitosheleza na kukosa kununua mifugo wengine. Hali ikiwa hivyo, maeneo yaliyotegemea soko hili huenda yakalipoteza taratibu, na bila shaka kupoteza natija inayotokana na soko lenyewe.

    Ili kudhibitisha hali hii, itakuwa bora ikiwa viwanda vya kuchinjia mifugo na kupakia nyama vitajengwa katika maeneo haya ya ugatuzi. Hili litawawezesha wakazi kuuza nyama badala ya kuuza mifugo wazimawazima. Fauka ya hayo maeneo haya yatajikinga dhidi ya kupoteza bidhaa zinazotokana na mifugo. Hizi ni kama vile ngozi, kwato na pembe ambazo bila shaka zina natija kuu. Ngozi kwa mfano, ni bidhaa muhimu sana katikasekta ya utengenezaji wa mavazi na mifuko. Viwanda vinavyotumia ngozi kama malighafi vikijengwa katika maeneo haya, wakazi wake watanufaika si haba. Madhalani, viwanda vya kutengenezea viatu, mishipi, mifuko na nguo vikianzishwa,wawekezaji watalazimika kuanzisha viwanda vingine tegemezi. Kathalika, ni dhahiri kwamba bidhaa zinazotokana na ngozi huhitaji kutiwa nakshi. Kuanzishwa kwa viwanda hivi basi kutazua haja ya kuanzishwa kwa viwanda vingine vya kutengeneza rangi, pamoja na maduka ya kuuza bidhaa zenyewe. Isitoshe, gundi ya kugandisha bidhaa hizi itahitajika, hivyo kusababisha haja ya kuanzishwa kwa kiwanda cha gundi. Matokeo ya shughuli hizi zote ni kuzalishwa kwa nafasi anuwaiza kazi kwa wakazi. Hili litakuwa na matokeo zaidi chanya, hususan kwa vijana. Badala ya kushiriki ulevi na burudani zinazowahatarisha, wataweza kujitafutia riziki katika viwanda hivi.

    Juu ya hayo, mfumo wa ugatuzi utayaweza maeneo husika kuongeza thamani, utoaji wa huduma za kijamii na kuitawala kulingana na mahitaji  ya maeneo haya. Ni muhimu hata hivyo kuzingatia kwamba kila eneo la ugatuzi lina upekee wake, navyo vipaumbele hutofautianakulingana na maeneo. Kuna yale ambayo yatasisitiza usalama, mengine ujezi na uimirishaji wa miundomusingi kama vile barabara, vituo vya afya na hata taasisi za elimu. La muhimu ni wakazi wa maeneo husika kubainisha ni lipi litatekelezwa kwanza.

    Kinga na kinga ndipo moto uwakapo. Kufanikiwa kwa mfumo wa ugatuzi kutategemea juhudi za kila mkazi wa eneo husika. Ni muhimu kila mkazi kujiona kuwa mmiliki wa eneo zima la ugatuzi na kuwajibika katika kuliendeleza kwa hali na mali.uwajibikaji huu unajumuisha uteuzi wa viongozi wenye muono mzuri na ambao utawawezesha kuyafikia malengo yao ya kimaendeleo. Hakika, mustakabali na uwepo wa eneo la ugatuzi utakuwa zao la maamuzi ya wanaeneo. Vilevile ufanisi wa maeneo ya ugatuzi utakuwa msingi wa ufanisi wa taifa kwa jumla.
    1. Fupisha ujumbe wa aya tatu za mwanzo kwa maneno 85-90 (alama 8, 1 mtiririko)
      Matayarisho:
      Nakala  safi:
    2. Kwa kutumia maneno 75-80, bainisha masuala ambayo mwandishi anaibua katika aya tatu za mwisho.  (alama7, 1 mtiririko)
      Matayarisho:
      Nakala safi:
  3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
    1. Andika neno lenye sauti zifuatazo:                                                                  (alama 1)
      Kipasuo hafifu cha midomo, irabu ya mbele wastani, kikwamizo sighuna cha ufizi, irabu ya kati chini.
    2. Tunga sentensi moja moja yenye aina zifuatazo za vishazi:                         (alama 2)
      1. Cha nia
      2. Kitegemezi cha wakati
    3. Andika maana ya maneno yaliyopigiwa mstari.                                            (alama 2)
      Walisita kufanya kazi hiyo baada ya saa sita usiku.
    4. Tia shadda:                                                                                        (alama 2)
      1. pekee
      2. alinyongwa
    5. Huku ukitoa mfano, onyesha miundo mitatu ya maneno katika ngeli ya U-I (alama 3)
    6. Tunga sentensi yenye vijisehemu vifuatavyo vya sarufi:                               (alama 2)
      Kiambishi kiwakilishi cha kiima
      Kiambishi kiwakilishi cha wakati
      Yambwa
      Mzizi - dhiki
      Kauli ya kutendesha
      Kiishio
    7. Tumia neno dhahiri kama:                                                                                 (alama 3)
      1. Kitenzi____________________________________________________________
      2. Kivumishi_________________________________________________________
      3. Kielezi___________________________________________________________
    8. Huku ukitoa mifano, eleza miundo mitatu ya silabi za Kiswahili.             (alama 3)
    9. Tofautisha mzizi na shina kwa mifano.                                                           (alama 2)
    10. Nyambua ziba katika kauli ya kutenduka kisha utungie sentensi.              (alama 2)
    11. Bainisha hali zinazorejelewa katika sentensi hizi.                                          (alama 3)
      1. Mwangeka hufika kituoni mapema._________________________________________
      2. Mgonjwa angetibiwa angepona.___________________________________________
      3. Umekuwa nanasi, kutagia mibani? __________________________________________
    12. Andika katika udogo wingi.                                                                               (alama 2)
      Ugwe ulipitishwa juu ya ukuta uliomea uyoga na kufungiwa kwenye makuti.
    13. Onyesha kiarifu katika sentensi hii.                                                               (alama 1)
      Kilimia kimechomoka angani.
    14. Changanua kwa kielelezo cha mstari.                                                             (alama 3)
      Ndege aliruka angani ghafla.
    15. Ainisha Virai vinne katika sentensi ifuatayo.                                                 (alama 2)
      Kicha cha funguo kilikuwa kimepotea jana nikicheza kandanda.
    16. Tunga sentensi kuonyesha matumizi mawili ya nukta mkato.                   (alama 2)
    17. Andika methali yenye maana sawa na jivu usilolilala usilipigie Jibwa.  (alama 1)
    18. Andika upya sentensi ifuatayo ukianza kwa shamirisho kitondo.              (alama 2)
      Kaizari amewakatia ng’ombe majani kwa muundu.
    19. Damka ni kwa rauka, wakati ni kwa_______________oa ni kwa taliki uza ni kwa_______ 
  4. (ISIMUJAMII) (alama 10)
    1. Katika jamii huwa wakati mwingine kuna matumizi ya lugha isiyo ya kistaarabu. Taja mifano mitano ya lugha sampuli hiyo (alama 5)
    2. Taja mambo matano yanayoathiri jinsi tunavyoweza kutumia lugha katika jamii.  (alama 5)

MARKING SCHEME

  1. Majibu -Ufahamu (Alama 15)
    1.  
      • Bahati anapelekwa shuleni
      • Bahati anadhihakiwa na miale ya jua.
      • Bahati ana mlinzi.
      • Bahati na wengine kama yeye kusoma hati za kawaida.
      • Bahati anabaguliwa kazini.
      • Serikali kuhakikisha matini zimeandikwa kwa hati inayoweza kusomwa na walemavu.
      • Wazazi hawamfunzi Bahati mbinu za kujikinga.
      • Walanguzi kuhatarisha maisha ya watoto walemavu.
      • Ukoo kuamua kuangamiza watoto walemavu.
      • Bahati kudhihakiwa na marika.
      • Mama kuamua kumhifadhi Bahati.
    2.  
      • Kuamua kuondoka nyumbani na kuacha mali yake na mumewe.
      • Kuwa mzigo Kwa kuzaa punguani (zezeru).
      • Kulazimika kuacha nyumba aliyochangia kuijenga.
      • Laumiwa kwa kukosa mimba/mtoto.
      •  Kutalikiwa
      • Kupelekwa kortini.
      • Kumsingizia muuguzi kuwa hawaelewani na mumewe.
    3.  
      • Mume kuenda kumuona mkewe hospitalini.
      • Mume kumshika mkewe begani.
      • Mume kuondoka hospitalini bila neno.
      • Mume kurudi hospitalini mara ya pili.
      • Mume kuomba mkewe msamaha.
      • Mume kutokuja hospitalini siku mbili.
      • Mume kushauriana na ukoo.
      • Ukoo kuamua kuangamiza mtoto mlemavu.
      • Mume kumjuza mkewe uamuzi wa ukoo.
      • Mume kulipa gharama ya hospitalini.
      • Make kuamua kumhifadhi mtoto wake.
      • Msimulizi anakashifu mtazamo wa jamii kuhusu watoto walemavu.
    4.  
      1. Hisani - fadhila,wema ,shukrani, tajamela, jamala
      2. Paka masizi - haribu sifa , aibisha , fedhehesha , chafua , tia Soni
  2. MUHTASARI (al.15)
    1.  
      1. Katibu mpya  iliidhinisha mfumo wa ugatuzi ambao hupunguza mamlaka ya serikali kuu katika usimamizi rasilimali.
      2. Eneo la ugatuzi hutwaa kiasi Fulani aha mamlaka.
      3. Ugatuzi utahakikisha usawa wa kimaendeleo nchini kinyume na awali.
      4. Serikali isaidie maeneo yote kujiimarisha.
      5. Maeneo yaweke mikakati ya kutafiti na kubainisha rasilimali zilizomo.
      6. Kuvumbua rasilimali mwafaka kutasaidia ustawi
      7. Kilimo cha ufugaji ni nguzo ya maeneo mengi na kinahitaji kuimarishwa kwa kuaandama mbinu za kisasa za uzalishaji.
      8. Ipo haja ya kujenga viwanda vya kuchinjia mifugo na kupakia nyama.
      9. Baadhi ya wafugaji huhajirika kwa kuliza mifugo wazimawazima.
      10. Wafugaji wengine hutapeliwa.
        Alama=07
        Ut=01
    2.  
      1. Ujenzi wa viwanda vya kuchinjia na kupakia nyama utakinga dhidi ya kupoteza  bidhaa zinazotokana na mifugo.
      2. Kujenga kwa viwanda hivi kunasababisha ujenzi wa viwanda tegemezi
      3. Hili litawezesha kuzalisha nafasi za kazi
      4. Kutakuwa na kuongezea thamani utoaji wa huduma za kijamii na kiutawala.
      5. Kuzalisha nafasi za kazi kwa vijana kutosaidia kuwaadilisha vijana Zaidi.
      6. Kila eneo lina vipaumbele tofauti,wakazi wabainisha kipaumbele chao.
      7. Ugatuzi unahitaji ushirikiano.kila mwanaeneo awajibikie maendeleo ya eneo.
      8. Wanaeneo washiriki kuteua viongozi wenye maono mzuri.
      9. Ufanisi katika maeneo ya ugatuzi utachangia katika ufanisi wa taifa kwa jumla.
        Alama=06
        Ut     =01
        07
  3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
    1. Andika neno lenye sauti zifuatazo:       (alama 1)                                                               
      Kipasuo hafifu cha midomo, irabu ya mbele wastani, kikwamizo sighuna cha ufizi, irabu ya kati chini.
      Pesa
    2. Tunga sentensi moja moja yenye aina zifuatazo za vishazi:     (alama 2)                         
      1. Cha nia
        Ili kufaulu katika mradi huo, itakubidi ufanye bidii. (nia)
      2. Kitegemezi cha wakati
        Tangu Mosi aondoke, hajarudi mpaka leo.
    3. Andika maana ya maneno yaliyopigiwa mstari.     (alama 2)                                             
      Walisita kufanya kazi hiyo baada ya saa sita usiku.
      • Sita-simama kutenda jambo baada ya kuonesha nia ya kutenda au baada ya kuanza.(al 1)
      • Sita-muda/tarakimu kati ya tano na saba.(al 1)
    4. Tia shadda:                                                                                          (alama 2)
      1. pe’kee
      2. ali’nyongwa
    5. Huku ukitoa mfano, onyesha miundo mitatu ya maneno katika ngeli ya U-I (alama 3)
      • M-MI:Mti-miti
      • MW-MI:Mwavuli-Miavuli
      • MU-MI:Muwa-Miwa
    6. Tunga sentensi yenye vijisehemu vifuatavyo vya sarufi:    (alama 2)                                   
      Kiambishi kiwakilishi cha kiima
      Kiambishi kiwakilishi cha wakati
      Yambwa
      Mzizi- dhiki
      Kauli ya kutendesha
      Kiishio
      Kinanidhikisha.
    7. Tumia neno dhahiri kama:  (alama 3)                                                                                     
      1. Kitenzi: Dhihirisha nia yako.
      2. Kivumishi: Habari dhahiri ndio hizo.
      3. Kielezi: Nieleze dhahiri kiini cha habari hizo.
        (Kadiria jibu)
    8. Huku ukitoa mifano,eleza miundo mitatu ya silabi za Kiswahili.                         (alama 3)
      1. Konsonanti moja pekee (K)
        Mtu, mbu,
      2. Konsonanti, Konsonanti, irabu (KKI)
        Mbuzi, ndizi, mbizi, nguo
      3. Konosonanti na Irabu (KI)
        Meza, kula,  kalamu
      4. Irabu pekee (I )
        Ingia, omba, imba
      5. Konsonanti,  Konsonanti , Konsonanti, Irabu (KKKI)
        Ngwena, skrubu, ndwele,
    9. Tofautisha mzizi na shina kwa mifano.  (alama 2)                                                                   
      • Mzizi - ni umbo la msingi la neno . Haligawiki zaidi
      • Shina - sehemu ya neno inayokaa kiambishi tamati.
    10. Nyambua ziba katika kauli ya kutenduka kisha utungie sentensi.                      (alama 2)
      Zibuka
      Mfereji wa majitaka umezibuka na taka zinapita mtaroni.
    11. Bainisha dhana zinazorejelewa katika sentensi hizi.     (alama 3)                                       
      1. Mwangeka hufika kituoni mapema.Mazoea
      2. Mgonjwa angetibiwa angepona. Hali ya masharti
      3. Umekuwa nanasi, kutagia mibani? Hali timilifu
    12. Andika katika udogo wingi.        (alama 2)                                                                                 
      Ugwe ulipitishwa juu ya ukuta uliomea uyoga na kufungiwa kwenye makuti.
      Vijugwe vilipitishwa juu ya vikuta vilivyomea vijoga na kufungiwa kwenye vikuti.
    13. Onyesha kiarifu katika sentensi hii.    (alama 1)                                                                 
      Kilimia kimechomoka angani.
      kimechomoka angani.
    14. Changanua kwa kielelezo cha mstari. (alama 3)                                                                           
      Ndege aliruka angani ghafla.
      S-KN(N)+KT(T+E+E) (S al 1,KN(N) al 1 KT(T+E+E)
    15. Ainisha Virai vinne katika sentensi ifuatayo.        (alama 2)                                                             
      Kicha cha funguo kilikuwa kimepotea jana nikicheza kandanda.
      • Kicha cha funguo-Kirai Nomino(RN)
      • Cha funguo-Kirai husishi (RH)
      • Kilikuwa kimepotea-Kirai Kitenzi(RT)
      • Jana nikicheza-(Kirai Elezi(RE)
      • Kandanda-Kirai Nomino(RN)
      • Funguo-Kirai Nomino(RN)
      • Cha funguo-Kirai vumishi(RV)
        (Zozote 4 *1/2 =alama 2)
    16. Tunga sentensi kuonyesha matumizi mawili ya nukta mkato.    (alama 2)               
      1. kugawa sentensi mbili zinazoweza kujisimamia bila ya viunganishi
        mfano:Wasichana walifuata maagizo waliyopewa; wafulana waliyagomea.
      2. kama kipumziko katika sentensi ndefu
        mfano:Alipochunguza ile hati aliyokabidhiwa na wale wafanya biashara aliona kuwa si nzuri; akaamua kujitenga nayo.
    17. Andika methali yenye maana sawa na jivu usilolilala usilipigie Jibwa          .(alama 1)
      • Usiyoyala usiwawingie kuku.
    18. Andika upya sentensi ifuatayo ukianza kwa shamirisho kitondo.                    (alama 2)
      Kaizari amewakatia ng’ombe majani kwa muundu.
      Ng’ombe wamekatiwa majani na Kaizari kwa muundu.
    19. Damka ni kwa rauka, wakati ni kwa njeo oa ni kwa taliki uza ni kwa nunua            (alama 2)
  4. Isimu jamii
    1.  
      • Lugha hutaja sehemu nyeti za mwili wa binadamu kama vile za uzazi.
      • Kutaja mada pale isipofaa mf. Vifo, magonjwa, upimaji wa kinyesi, makamasi nk. Wakati wa kula.
      • Wanataja vilema ua wenye udhaifu wakiwepo k.v zeruzeru, kipofu, kiziwi.
      • Hutumia maneno ya kimatusi k.v mjinga, pumbavu n.k.
      • Hutumia lugha ya kulaani k.v ninakuombea ufe haraka / ufutwe kazi n.k.
        (Hoja zozote 5 x 1 = 5)
    2.  
      • Hadhira mf. wale anaowazungumzia kama ni watoto akatumia lugha yenye ucheshi.
      • Utungo / matini / muktadha – kama ni mashairi atatumia lugha yenye ukiushi.
      • Tabaka mf. la juu amezoea kiingereza hapendi mf. Kiswahili.
      • Hali – chlokoro wanatumia lugha ya kutisha, mlevi, mgonjwa lugha yake huwa tofauti.
      • Mada – zile ngumu hutumia lugha nzito, zile rahisi hutumia lugha nyepesi.
      • Matilaba mf. Mtu anapotaka wenzake wamuunge mkono atatumia lugha ambayo itawavuta kwake.
      • Umri – kundi la kiumri husababisha vilugha mf. Vijana wana mtindo wao. 
         (Hoja 5 x 1 = 5)

Zingatia makosa ya sarufi kutengemea alama alizopata mwanafunzi katika sehemu
Tahajia mkosa 6.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Sunrise Pre Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?