Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Sunrise Pre Mock Exams 2023

Share via Whatsapp
Maagizo
  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Kila swali lina alama ishirini (20)
  • Maswali hayo mengine yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki: yaani; Ushairi, Tamthilia , Hadithi fupi na Riwaya.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU A: FASIHI SIMULIZI 
Swali Ia Iazima

  1.  
    1. Tofautisha kati ya mighani na maghani.                    (alama 2)
    2. Taja na ueleze ama tatu ya maghani ya kawaida.                                (alama 6)
    3. Eleza sifa za maghani.                                (alama 4)
    4. Kwa kurejelea mifano mwafaka eleza majukumu manane ya nyimbo katika jamii,                               (alama 8)

SEHEMU B: USHAIRI
Jibu swali la 2 au la 3

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
    Ewe hisia!
    Umeniamshia ndoto niloisahau zamani
        nyimbo ya kale
        na mdundo usonivutia
        ila hayawani na mwangu rohoni.

    Tulia sasa tulia
    Hebu tulia ewe hisia ulo mtimani
    Nataka katu kusisimka
             kwa sauti yako laini
    Kwani njia zetu ni
             daima hazioani

    Umesubutu vipi kuniita
          kutoka mwako ngomeni
         ulimosahauliwa tangu zamani
    Basi yawache maombolezi yako yaso maoni,
         yawateke hao mashujaa wa kale
         wafu walo kaburini.

    Hebu tulia, usiniingilie
             Usinihangaishe!
    Kukuandama katu haimkini
    Kwani hata sasa…kwa kukuwaza tu dakika hini
             naona majuto ya mbali moyoni
             kama kwamba nimegawa wangu wakati
             na wazimu, majinuni.
    Basi nenda zako hisia…shuu…hebu tokomea.

    Maswali
    1. Huu ni utungo wa aina gani?           (alama 2)
    2. Huku ukitoa mifano, fafanua sifa zinazoufanya utungo huu kuwa shairi      (alama 5)
    3. Mistari mishata ni nini? Toa mifano kwenye shairi hili.         (alama 4)
    4. Fafanua tamathali za kifasihi katika shairi hili.         (alama 3)
    5. Eleza mbinu tatu alizotumia mtunzi kutosheleza kaida za kishairi.         (alama 6)
  2. Soma shairi lifwatalo kisha uyajibu maswali yanayoliandama:
    Naandika yangu haya, kwa uwezo wa Wadudi,
    Kanipa njema afiya, kumsifu sina budi,
    Nifundishie insiya, hino methali ya jadi,
    Mchama ago hanyeli, huenda akauya papo

    Ago mchama huuya, mbele mambo yakizidi,
    Hurudi pakawa kaya, kupapenda hana budi,
    Kwingi angawayawaya, ago shuruti arudi,
    Mchama ago hanyeli, huenda akauya papo.

    Kule kwetu Mwarakaya, kijiji chetu cha jadi,
    Yalidhihirika haya, bwana mmmoja mkaidi,
    Aloalikwa ulaya, kadhani ‘mepata sudi,
    Mchama ago hanyeli, huenda akauya papo,

    Alidhani hatauya, ‘endapo nchi baidi,
    Na kusema bila haya, kwa inda na ukaidi,
    Kwamba akenda ulaya, harudi kwenya samadi,
    Mchama ago hanyeli, huenda akauya papo.

    Aliranda akitaya, kwa mbwembwe na zake tadi,
    Nguo moto kazitiya, nyumbaye akainadi,
    Kasema vyote ‘ishiya; kurudi sina ahadi
    Mchama ago hanyeli, huenda akauya papo.

    Matusi aliyamwaya, mengi yasiyo idadi,
    Mkewe kamwita yaya, na kudharau abidi,
    Kanena ‘mekata waya’, ng’ambo nenda kufaidi,
    Mchama ago hayeli, huenda akauya papo,

    Ng’ambo alielekeya, kwa vishindo kama radi,
    Kumbe aliyemwendeya, kabambwa kwa ufisadi,
    Vya watu amebugiya, rushwa na kuhepa kodi,
    Mchama ago hanyeli, huenda akauya papo.

    Kombo yakamwendeya, mambo mno yakazidi,
    Akabakia kuliya, nyumbani ataka rudi,
    Nyumba ipi ‘taingiya’, hana tena tabaradi,
    Mchama ago hanyeli, huenda akauya papo

    Maswali
    1. Kwa kutolea ushahidi ufaao shairini, jadili kifupi maswala matatu makuu ambayo mtunzi ameyashughulikia.       (alama 6)
    2. “Mtunzi huyu ni bingwa wa kutumia lugha kupitisha ujumbe.” Tetea.        (alama 4)
    3. Fasiri ujumbe wa mtunzi katika ubeti wa sita.                                                    (alama 4)
    4. Nafsi nenewa katika shairi hili ni nani? Thibitisha.                                            (alama 2)
    5. Zaidi ya tarbia, ungelipangaje tena shairi hili?                                                    (alama 2)
    6. Fafanua msamiati ufwatao kama ulivyotumika shairini:                                   (alama 2)
      1. Baidi
      2. ‘mekata waya’

SEHEMU C: TAMTHILIA: BEMBEA YA MAISHA (Timothy Arege )

Jibu swali la 4 au 5

  1. ”Basi usijipandishe presha bure mama!”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama4)
    2. Ainisha mbinu mbili za kimtindo zilizotumiwakatika dondoo hili. (alama2)
    3. Eleza sifa za msemewa. (alama 4)
    4. Jadili maudhui ya utamaduni kama yanavyojitokeza katika tamthilia nzima.   (alama10)
  2. Katika tamthilia hii Maisha yamesawiriwa kama Bembea. Kwa kutolea mifano mwafaka oanisha kauli hii na wahusika mbalimbali. (alama 20)

SEHEMU D: HADITHI FUPI : MAPAMBAZUKO YA MACHWEO (D.W Lutomia na Phibbia Muthama)

Jibu swali la 6 au 7

  1. ...iwapo penzi hili litatia doa,basi nirudishie mfuko huu kama ishara ya kulitupa penzi langu kama jongoo na mti wake..."
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Fafanua mbinu mbili ambazo zimetumika katika  dondoo hili. (alama 4)
    3. Eleza sifa sita za msemaji wa maneno haya. (alama 6)
    4. Eleza umuhimu wa msemewa wa hadithi hii katika kujenga ploti. (alama 6)
  2. Swala la elimu limepewa kipaumbele katika hadithi ya Sabina. Jadili (alama 20)

SEHEMU E: RIWAYA CHOZI LA HERI : Assumpta Matei 

Jibu swali la 8 au 9

  1. Eleza jinsi maudhui ya ufisadi yalivyoshughulikiwa katika riwaya ya Chozi la Heri.    (alama 20)
  2. .“…liandikwalo ndilo liwalo? Since when has man ever changed his destiny?”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.                       (alama 4)
    2. Bainisha mbinu tatu za kimtindo zinazojitokeza katika dondoo hili.  (alama 6)
    3. Kwa kuzingatia hoja kumi, jadili jinsi ambavyo hali ya, “ liandikwalo ndilo liwalo’’, inavyojitokeza katika Chozi la Heri.    (alama 10)

MARKING SCHEME

SEHEMU A: FASIHI SIMULIZI 

Swali Ia Iazima 1 

  1.  
    • Mighani ni hadithi za mashujaa nayo maghani ni tungo za ushairi ambazo       hutolewa kwa kalima au kwa ujia ya maneno badala ya kuimbwa.
    • Mighani ni kipera cha hadithi ilhali maghani aina ya ushairi
    • Maghani hutumia lugha ya mkato ilhali mighani hutumia lugha simulizi/nathari  (2x1=2)
  2.  
    • Sifo-Ni tungo fupi zinazosemwa katika harusi,vita ,mazishi u.k ili kusifu wahusika ili kudhihirisha uimahiri wa wahusika.
    • Toudozi –Ni tungo za kusifu watu na wanyama.Sifa hizi huwa ni za kistiara zilizokusudiwa binadamu.Husifu tabia na mauinbile.
    • Pembezi -Ni tungo ambazo huwasifu watu mashuhuri ambao wanachangia pakubwa katika jamii husika k.m wakombozi,wanariadha n.k
    • Majigambo/kivungo -Ni tungo za kianaa ambazo mtunzi hujisifu mwenyewe kwa sababu ya uhodari wake katika kazi za kisanii, tukio Fulani kama vita n.k  (3x2=6)
  3.  
    • Hutumia lugha ya mkato.
    • Mishororo huwa na mgao wa vipande.
    • Ni ushairi wa kusemwa wakati wa hafla mbalimbali
    • Hufungamana na kutoa.sifa kwa wahusika.
    • Hufungamana na mila , desturi na utamaduni
    • vipera kama ngano huandamana na ala za muziki.
    • Hutungwa papo hapo na haibadilikibadiliki.
      Zozote (4x1)=4
  4.  
    • Hukuza na kuhifadhi utamaduni wa jamii kupitia kwa tanzu kama tendi.
    • Huelimisha watu kuhusu mambo ya jamii kupitia nyimbo kama za ndoa.
    • Nyimbo hufariji na kuliwaza waliofiwa katika jamii – mbolezi/tahalili
    • Nyimbo huwaha - masisha wana jamii kwa mifano vita, kazi, n.k
    • Nyimbo hukuza lugha na uwezo wa kujieleza wa mhusika.
    • Nyimbo za dini hutumiwa kuabudu Mungu na kuomba heri njema.
    • Kiupitia kwa sifo, tondozi n.k tabia nzuri za wajamii hudumishwa kwa kusifiwa
    • Nyimbo hutumiwa kukashifu maovu katika jamii k.m ufisadi
    • Nyimbo huleta burudani kwa wanajamii kutokana na mahadhi yake.    (Zozote 8x1=8)

USHAIRI
Swali la 2

  1. Ushairi huru/ shairi la kimapinduzi – kwa sababu utungo huu hauzingatii urari wa vina, urari wa mizani n.k.
    Kutaja  - alama 1
    Sababu – alama 1
  2.  
    • Kuwepo kwa mishororo
    • Umegawika katika beti
    • Baadhi ya mishororo inaelekea kuwa na vina
    • Matumizi ya takriri
    • Matumizi ya lugha ya mkato   (5 x 1 = 5 )
  3. Ni mistari isiyokamilika kimaana na huhitaji msomaji kuusoma mstari unaofuata ili kupata maana. Kwa mfano:
    • nyimbo ya kale – ubeti 1
    • na muundo unaovutia – ubeti 1
    • kwa sauti yako laini – ubeti 2
    • daima hazioni – ubeti 2
    • Kutoa maelezo ya mshata – alama 2
      Mifano yoyote miwili – alama 2
  4.  
    • Tashihisi – hisia kupewa uhai
    • Sitiari – ndoto, hisia
    • Tashbihi – majuto ya mbali moyoni kama kwamba …  (zozote 3 x1 = 3)
  5.  
    • Inkisari: niloisahau badala ya niliyoisahau
    • Tabdila: umesubutu badala ya umethubutu
    • Kikale: mtimani badala ya moyoni   (3 x 2 = 6)

Swali la 3

  1. Kwa kutolea ushahidi ufaao shairini, jadili kifupi maswala matatu makuu ambayo mtunzi ameyashughulikia.           (alama 6)
    • Mabadiliko- Bwana aliyealikwa ng’ambo anafikiri maisha yake yameongoka lakini afikapo huko mambo yanamwendea kombo. Inamlazimu kurudi nyumbani alikotoka kwa kiburi akisema kuwa asingerejea.
    • Majuto- Bwana aliyehamia ng’ambo kwa kiburi kikuu anaishia kunyenyekea mambo yanapomharibikia kule.
    • Ufisadi- Mwenyeji wa Bwana anayealikwa ng’ambo anashikwa kwa kushiriki ufisadi.
    • Tamaa na ubinafsi- Bwana anayetoa ualishi wa mwenzake kumzuru ng’ambo anashitakiwa kwa ufisadi na kukwepa kodi hali zinazodhihirisha tamaa.
      Hoja 3 za mwanzo X 2= alama 6
      Tanbihi: Swali hili linatahini maudhui; tathmini majibu mengine ya mtahiniwa
  2. “Mtunzi huyu ni bingwa wa kutumia lugha kupitisha ujumbe.” Tetea.                      (alama4)
    Tanbihi: Swali linatathmini mtindo/mbinu za lugha.
    • Methali- Mchama ago hanyeli, huenda akauya hapo.
    • Takriri- Kibwagizo “mchama ago hanyeli, huenda akauya papo” ni mfano wa uradidi.
    • Kinaya- Bwana anayeenda ng’ambo kwa kiburi analaimika kunyenyekea afikapo huko na kumpata mfadhili wake ameshikwa kwa ufisadi/ alitarajia maisha mema huko na kuishi huko milele lakini hali zinamharibikia.
    • Istiari/jazanda- Samadi katika ubeti wa nne ni kiashiria cha umaskini/kutoendelea.
    • Tashbihi- Ng’ambo alielekeya, kwa vishindo kama radi.
    • Taswira-Tashbiha katika (v) hapo juu inajenga picha ya jinsi Bwana huyu anaondoka kwao kwa vurugu. Pia jazanda ya samadi inatujengea taswira ya umaskini.
    • Nahau- Kombo yakamwendeya.
    • Balagha-nyumba ipi taingiya…
    • Msemo- mekata waya-amekata uhusiano
      Hoja zozote 4X1= alama 4
  3. Fasiri ujumbe wa mtunzi katika ubeti wa sita.                                                         (alama 4)
    • Alitumia lugha chafu sana
    • Akamdunisha mkewe pamoja na wengine wengi.
    • Akasema kuwa amekata uhusiano na kuwa angeenda kufanikiwa kule ng’ambo.
    • Ahamaye hachafui atokapo kwa kuwa huenda akarudi hapo.
      Hoja 4X1= alama 4
  4. Nafsi nenewa katika shairi hili ni nani? Thibitisha.                                              (alama 2)
    • Yeyote anayefanikiwa kuhama alipopazoea.
    • Mtunzi anatahadharisha dhidi ya kutoka alipokuwa akiishi mja kwa dharau/kiburi kwa vile kuna uwezekano wake kurudi hapo.
      Hoja 4X1= alama 4
  5. Zaidi ya tarbia, ungelipangaje tena shairi hili?                                                     (alama 2)
    • Mathnawi-lina vipande viwili katika kila mshororo.
    • Mtiririko-vina vyote vya ndani vinafanana tangu mwanzo hadi mwishi; vya nje vilevile.   Hoja 2X1= alama 2
  6. Fafanua msamiati ufwatao kama ulivyotumika shairini:                                    (alama 2)
    1. Baidi -tofauti
    2. ‘mekata waya’- amekatiza uhusiano

TAMTHILIA (BEMBEA YA MAISHA)

  1.  
    1. Msemaji - Neema
      Msemewa-Sara
      Mahali- Hospitali
      Neema alikuwa akimtuliza Sara baada ya kukasirishwa na Asna aliyesema babake anaweza kuteka maji kisimani.
    2.  
      • Utohozi- presha kutokana na neno la kiingereza pressure
      • Nidaa- mama!
    3.  
      • Mwenye bidi
      • Anayewajibika
      • Mvumilivu
      • Mwenye mapenzi wa dhati kwa wanawe
      • Mtamaduni
      • Mshauri mwema
      • Mwenye busara
      • Mwenye mlahaka mwema
    4.  
      • Mtoto wa kiume anatukuzwa kama mrithi
      • Mtoto wa kwanza ana jukumu la kuwasaidia wazazi wake
      • Sara hawezi kulala kwa Bunju
      • Wazazi hawawezi lala chumba kimoja na wanao
      • Leso hutolewa wakati wa posa
      • Enzi za kitambo elimu ya wasichana haikutiliwa maanani
      • Jamii inashikila utamaduni wa wazee kukutana baada ya mavuno ya kwanza na kutoa baraka
      • Kizazi  cha sasa kimetupa mila zao
      • Mume hafai kufanya kazi za nyumbani (hasa jikoni)
      • Mwanamke hafai kushindana na mwanwmume
  2.  Maisha ya familia ya Sara na Yona yanaleta taswira ya bembea. Mwanzoni, ndoa ya Sara na Yona inaonekana yenye furaha. Hii ina maana kuwa, kama bembea inavyokuwa juu, maisha yao yalikuwa yenye mafanikio na furaha. Maisha yao yanaingiwa na dosari wakati wawili hao wanakosa mtoto baada ya kipindi kirefu katika ndoa. Zaidi ya hayo, wanajaliwa na watoto wa kike watatu. Hawajaliwi na mtoto wa kiume, kinyume na matarajio ya jamii. Wanachekwa, wanasutwa na kukejeliwa.
    • Bembea ya maisha yao inarudi chini. Sara anaanza kuchapwa kichapo cha mbwa na bwana yake Yona. Yona anaidharau familia yake na kuingilia ulevi, ulevi uliomfanya kupigwa kalamu kazini. Sara anasema, japo kuna wakati maisha yanabwagwa na bembea ya maisha, lazima maisha hayo yaendelee. Hata kama kamba, chuma au minyororo ya maisha inakatika, hawana budi kujiinua na kuendelea na maisha (uk. 20-21). Hivyo basi Sara anasimama na familia yake kidete akifahamu kuna siku atafanikiwa na maisha yao yatakuwa mema tena.
    • Maisha ya familia ya Yona yanabadilika kutoka kuwa maisha ya kukosa mahitaji ya kiuchumi. Bembea yao ya maisha ilionekana kuwachini. Baada ya Neema kufanikiwa na kupata kazi, bembea ya maisha yao inakuwa juu. Wanafanikiwa kujengewa nyumba, wanapata wafanyakazi wa kuwasaidia nyumbani na hata kuwa na jiko la gesi la kupikia.
    • Bembea ya maisha ya Neema inaonekana kusukumwa na Bunju mumewe. Kwanza Bunju alimsaidia Neema alipokuwa amepata ajali. Bunju alimtumia flying doctors ili aweze kupata matibabu zaidi (uk.41).
    • Bunju anasaidia kuisukuma bembea ya maisha ya Neema kwa kumsaidia kuwasomesha dada zake. Vilevile, anamsaidia kuwajengea wazazi wa Neema nyumba.
    • Maradhi ya Sara yanaifanya bembea ya maisha ya Sara kuwa kama iliyokatika na kuwa chini. Sara anakosa matumaini ya kuishi na kutamani kufa.
    • Bembea ya maisha ya mjini huwa juu kutokana na maendeleo. Kuna maendeleo ya barabara, magari mengi, majengo mengi na hata sekta ya matibabu imeimarishwa.
    • Watu mjini wanapokea matibabu ya hali ya juu ilhali, bembea ya maisha ya kijijini huwa chini kwa sababu ya kukosa maendeleo hasa katika sekta ya matibabu na barabara nzuri. Sekta ya matibabu ya kijijini inamfanya Neema kumtafutia mamake hospitali ya mjini sababu zile za kijijini hazimpi mtu matumaini ya kutoka akiwa mzima ilhali za mjini zinampa mgonjwa matumaini ya kutoka akiwa buheri wa afya.

HADITHI FUPI (MAPAMBAZUKO YA MACHWEO)

  1. "...iwapo penzi hili litatia doa, basi nirudishie mfuko huu kama ishara ya kulitupa penzi langu kama )ongoo na mti wake...
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      • Haya ni maneno ya Suluhu kwa Abigael kama yanavyokumbukwa na Abigael. Walikuwa katika chumba walichozoea kwenda kuzituliza nafsi zao wakiwa na Suluhu. Aliyakumbuka maneno haya wakati alikuwa amekwisha kichomoa kisu kwenye mfuko alionunuliwa na Suluu huku akitaka kumuua.
    2. Fafanua mbinu mbili ambazo zimetumika katika dondoo hili. (alama 4)
      1. Nahau - tia doa.
      2. Tashbihi - kulitupa penzi langu kama jongoo na mti wake.
    3. Eleza sifa sita za msemaji wa maneno haya. (alama 6)
      • 'Ni muasherati - japo ana mke ana wapenzi wa kando kama Abigael.
      • 'Ni katili alifikiria namna ya kumuangamiza mkewe abaki na Abigael.
      • 'Ni msaliti - anaisaliti familia yake kwa kuitelekeza.
      • .Ni mlezi mbaya- anamwachia mkewe Bi. Suluhu mzigo wa kuwalea watoto wao na kumwambia ni wake pekee.
      • .Ni kiongozi mbaya - haleti maendeleo katika eneobunge lake kw alitumia pesa za umma kuwalipa mabinti wa Chuo kikuu kwa kula uroda nao.
    4. EIeza umuhimu wa msemewa wa hadithi hii katika kujenga ploti. (alam 6)
      • Msemewa ni Abigael.
      • Kupitia kwa Abigael tunaonyeshwa namna Bw. Suluhu alivyokuwa ameoza kitabia kwa kula uroda na mabinti wa Chuo kikuu.
      • Kupitia kwa Abigael tunajua kuwa Bwana Suluhu alikuwa tajiri mwenye mali na pesa nyingi zilizosababisha utovu wa amani kwa mkewe.
      • Kupitia kwa Abigael kuisoma barua ya Bi. Suluhu tunajua kuwa Bwana Suluhu alikuwa ameitelekeza familia yake na kumtwika Bi. Suluhu mzigo wa kuwalea wanawe.
      • Kupitia kwa barua aliyoisoma Abigael, tunajua kuwa Bwana Suluhu alinyakua shamba la mamake Abigael na kumuua.
      • Kupitia kwa Abigael kuisoma barua ya Bi. Suluhu kwa bwanake tunajua Suluhu alikuwa na nakama.
      • KupitiakwaAbigael tunaonyeshwabaadhiyamatatizoyanayowakumba wanafunzi wa Chuo kikuu kama ukosefu wa chakula, uozo wa jamii, utegemezi n.k.
  2. Swala la Elimu limepewa kipaumbele katika hadithi ya sabina. Jadili alama 20
    • Sabina ni mwanafunzi wa darasa la none. Jumapili ya mwisho kabla ya Elimu mtihanai wa kitaifa, Sabina anaonekana mwenye hisia mseto moyoni. (uk. 34)
    • Anawaza kuhusu mtihani huo ambao iwapo angepita ungemwezesha kupata ufadhili katika Shule ya upiti ya bweni. (uk. 34)
    • Anawaza vilevile, iwapo angefeli mtihani huo, hatima yake ingekuwa ipi? (Uk. 34)
    • Sabina anakumbuka maneno ya mwalimu mkuu kuwa mizizi ya elimu ni chungu ila matunda yake ni matamu. (uk. 34)
    • Kauli ya mwalimu mkuu pia inashauri kuwa ikiwa mtu anataka kuonja matunda ya elimu lazima atie bidii. (uk. 34)
    • Sekta ya elimu inakumbwa na changamoto mbalimbali kwa mfano mimba za mapema. Nyaboke - mamake Sabina- alimzaa akiwa kidato cha pili. (Uk. 35)
    • Changamoto nyingine ni kuacha Shule kabla ya kuhitimisha kiwango fulani. Nyaboke anapojifungua anakatiza masomo yake ili kuanza ulezi. (uk. 35)
    • Vilevile baadhi ya desturi potovu za jamii kama kuwaoza wanao mapema huweza kukatiza masomo ya watoto. (uk. 39)
    • Elimu huwahakikishia watu mustakabali mwema maishani. Wazazi wake Nyaboke wanakata tamaa ya maisha mazuri kwa sababu mwanao waliomtegemea kusoma hadi Chuo kikuu anakomea kidato cha pili. (uk. 35)
    • Binamu yake Sabina, Mike, anasomea katika Shule ya msingi ya bweni. Alizoea kubeba vitabu vya kudurusu ambavyo walidurusu na Sabina wakiwa katika kazi yao ya uchungaji. Hii inaashiria tamaa yao ya kutafuta elimu. (Uk. 36)
    • Werevu wa Sabina haukutiwa doa na hali yake ya ujakazi. Kila muhula aliibuka wa kwanza darasani kana kwamba nafasi hiyo ilikuwa imetengwa kwa ajili yake.
    • Mwalimu mkuu anawahutubia watahiniwa ukumbini kama sehemu ya maandalizi kabla ya mtihani wa kitaifa. (uk. 37)
    • Majukumu mengi nyumbani wanayopewa watoto hueza kutatiza masomo yao.
      Kazi ya kuuza maziwa inamfanya Sabina kuchelewa shuleni mara
    • Wanahabari wanamtafuta Sabina hadi nyumbani kwao ili kumhoji kwa kufanya vyema katika mtihani. Anaibuka mwanafunzi wa nane bora nchini. (uk. 39)
    • Kufanya vyema katika mtihani kunafanya kila mtu kujinasibisha na Sabina akiwemo Yunuke na Ombati. (uk. 40)

CHOZI LA HERI

  1. Eleza jinsi maudhui ya ufisadi yalivyoshughulikiwa katika riwaya ya Chozi la Heri.
    • Nyumba za maskini zinapobomolewa Tononokeni, mabwanyenye wanaanza kutoa milungula ili nyumba zao zisibomolewe.
    • viongozi wanapowapoka raia ardhi zao, raia walalamikapo hupozwa roho kwa kuambiwa kuwa kumeundwa tume za kuchunguza kashfa hizo.
    • wakati wa uchaguzi, wanasiasa wanawahonga raia ili wawachague, Papa aliwahonga kwa pesa na unga.
    • Hazina ya Jitegemee inalenga kuwafaidi vijana wa taifa la Wahafidhina lakini ukabila na unasaba unapoliandama hawanufaiki
    • -nyumba zinazolengwa kupewa maskini katika mtaa duni wa Sombera zinachukuliwa na viongozi baada ya ujenzi kukamilika
    • -familia ya Bwana Kute inajigawa na kuwa familia tatu ili wapate msaada mwingi kuliko wakimbizi wengine.
    • Serikali inabomoa majengo ya raia katika mtaa wa Tononokeni na Zari bila kuwafidia.
    • raia wanaiba mafuta ya lori ili wawauzie madereva wa wakubwa au walinda usalama ili wayauze kwingine.
    • madereva wa wakubwa wanafyonza mafuta kwa mirija na kuwauzia wenye magari ya kibinafsi
    • askari wananunua mafuta ambayo yameibiwa na kuyauza kwingine
    • matapeli wanawauzia wananchi wenzao ardhi ya makaburi bila kujali
    • raia matapeli wanauza ardhi zao mara mbili kwa watu wawili tofauti na kutoa hati miliki mbili-halali na bandia
    • viongozi wananyakua ardhi iliyotengewa upanzi wa chakula na kujenga nyumba zao mf. Madhabahu kwenye mlima wa Nasibu yalinyakuliwa ili kujenga hoteli za kitalii.
    • vigogo wanauza mahindi yanayotolewa na mataifa ya nje kama msaada.
    • vigogo wanawalazimisha wataalamu wa maswala ya lishe kuidhinisha uuzaji wa mahindi yaliyoharibika.
    • viongozi wanapasua mbao na kuchoma makaa katika msitu wa mamba baada ya msitu huo kupigwa marufuku.
    • viongozi wanahamisha wakimbizi kutoka msitu wa Mamba na kuanza kuvuna mahindi yaliyopandwa na wakimbizibadala ya kuwaruhusu kuyavuna kabla ya kuwaondoa.
    • Baada ya Fumba kumpachika mimba mwanafunzi wake, aliachishwa kazi kwa muda kisha akahamishwa kwinginehivyo kumsababishia Rehema kutopata haki yake.
    • Baadhi ya walinda usalama wanashirikiana na wahalifuili wagawane mali iliyoibiwa.
    • magari ya vigogo hayaondolewi barabarani na askari licha ya kuwa mabovu.
    • Buda anawahonga askari wanapoenda nyumbani kwake kumtia mbaroni (biashara ya ulanguzi wa mihadarati)
      Tathmini jibu la mwanafunzi.
      Zozote 20x1=10
  2. .“…liandikwalo ndilo liwalo? Since when has man ever changed his destiny?”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. Alama 4
      • Maneno ya Terry
      • Akimwambia Ridhaa
      • Nyumbani kwao
      • Baada ya kugundua kuwa anaamini ushirikina
        Au
      • Ni mawazo ya Ridhaa akikumbuka maneno aliyoambiwa na mkewe Terry
      • Kwa sababu ya  kuamini kuwa milio ya bundi na kereng’ende huashiria jambo Fulani lingefanyika.
      • Yuko kando ya vifusi vya nyumba yake iliyochomwa
      • Baada ya familia yake kuchomewa ndani 4x1 =4
    2. Bainisha mbinu tatu za kimtindo zinazojitokeza katika dondoo hili.     Alama 6
      • Methali-liandikwalo ndilo liwalo
      • Kuhamisha ndimi/msimbo-kauli ya kutumia sentensi nzima kwa lugha nyingine.
         Since when has man ever changed his destiny?
        Tanbihi: mbinu hii si kuchanganya ndimi.Atakayeandika hivi asituzwe.
      • Swali la balagha- “…liandikwalo ndilo liwalo? 
        Since when has man ever changed his destiny?”
        3x2=6
    3. Kwa kuzingatia hoja kumi, jadili jinsi ambavyo hali ya, “ liandikwalo ndilo liwalo’’, inavyojitokeza katika Chozi la Heri. Alama 10.
      • Neema na Mwangemi wanajitahidi kupata mtoto lakini hawafanikiwi na wanaishia kumpanga Mwaliko.
      • Wafuasi wa Mwanzi wanajaribu kushinda ushindi wa Mwekevu lakini wanashindwa.
      • Kaizari anajitahidi kuzuia wahuni wasiwabake binti zake lakini wanamzidi nguvu na kuwabaka.
      • Lunga anajitahidi kumrithia na kumpendeza mkewe Naomi lakini hatimaye anamtoroka na kumwachia Watoto
      • Kiriri anampinga Annette asiende ughaibuni lakini anampuuza na kuhamia huko.
      • Kiriri anawasihi wanawe warudi nyumbani lakini waliendelea kuishi ughaibuni hata baada ya kukamilisha masomo yao.
      • nyanyake Pete anajizatiti kupinga ndoa ya Pete lakini hatimaye Pete anaozwa.
      • Kipanga anataka kuambiwa babake halisi baada ya aliyemdhania kuwa babake kumkana lakini mamake hakumwambia.
      • hata baada ya mabwanyenye kutoa hongo ili nyumba zao zisibomolewe katika mtaa wa Tononokeni, zianbomolewa.
      • Dick anakataa kutumiwa na Buda kulangua dawa za kulevya lakini anamtishia na baadaye kuuza dawa za kulevya.
      • Naomi alimtoroka Lunga kwa sababu ya umaskini lakini anaishia kuteseka Zaidi na baadaye kufa
      • Amize Lucia wanajizatiti kupinga ndoa ya Lucia lakini baadaye Lucia anaolewa.
      • Wanaume wanatishia kumtusi Mwekevu anapojitosa siasani ili kumvunja moyo lakini anavumilia mpaka anachaguliwa kuwa kiongozi wa Wahafidhina.
      • Pete anakunywa dawa ya kuua panya ili afe lakini anapelekwa katika kituo cha afya cha Mwanzo Mpya na kuendelea kuishi.
      • Pete anajaribu kuavya mimba ya mtoto wake wa pili na wa tatu lakini anaishia kuwazaa Watoto hawa.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Sunrise Pre Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?