Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Sukellemo Joint Pre Mock Exams 2023

Share via Whatsapp
Maagizo
  • Jibu maswali manne pekee
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu zilizobaki (hadithi fupi,tamthilia riwaya na fasihi simulizi)
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.

SEHEMU A:USHAIRI

  1. LAZIMA      
    Naikumbuka ,
    siku nilipofika kijijini
    na kumkuta nyanya kaketi chini ya,
    mgunga unaolekeana na machweo,
    akisaga ugoro wake
    na
    kuyaangalia machweo,
    akiwasikiliza nyuni waliokuwa,
    wakiimba kwa msisimko
    kuyaomboleza matanga ya
    magharibi.
    Naikumbuka kauli yake,
    ‘itakuwa lini nasi kuomboleza
    Kifo cha dhiki?

    Naikumbuka sauti ya
    mama alipokuwa akiwinga
    bundi aliyekuwa akiimba
    mbolezi kuucheka umaskini
    kuudhihaki uwezo duni wa wanakijiji.
    Naikumbuka sauti ya mama
    Na swali lake:
    ‘Lini nasi tutawaimbia watutesao
    mbolezi za bundi?

    Naikumbuka siku niliposikika,
    kilio alichokilia ndugu;
    kidole ki lipokatwa na mashine
    ya kutengenezea karatasi
    Sauti yake akilalamika,
    kutolipwa fidia na chozi,
    la kufutwa kazi kwa kutozalisha,kama kabla.
    Ndio na swali lake:
    ‘Lini itakatwa mirija ya
    wanyonyaji wafanyao watu mashine?

    Naukumbuka ukwenzi,
    alioupiga falahi na mkulima,
    aliyepokea pesa ukufi kwa,
    mazao yaliyomlaza nje na kumvunja,
    mgongo akalala hoi,
    nayakumbuka machozi yake ,
    yaliyotiririka na kumkamua
    nguvu akitoa lawama zilizotoka kwa shida
    nililisikia swali lake:
    ‘Lini jasho la upanzi na mavuno
    litawafaidi wachomwa na jua?’
    1. ‘’Shairi hili linakatisha tamaa.’’ Thibitisha kauli hii kwa mifano mitatu kutoka kwenye shairi.      (alama 3)
    2. Fafanua umuhimu wa aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili.(alama 2)
    3. Bainisha nafsineni katika shairi hili.                                                              (alama 2)
    4. Jadili umuhimu wa maswali ya balagha katika shairi hili.                            (alama 2)
    5. Tambua toni ya shairi hili.                                                                              (alama 1)
    6. Bainisha na uoneshe umuhimu wa mistari ifuatayo  katika shairi hili.
      1. Mistari kifu                                                                                   (alama 2)
      2. Mistari mishata                                                                             (alama 2)
    7. Bainisha aina mbili za taswira zinazojitokeza katika shairi hili.                     (alama 2)
    8. Fafanua muundo wa shairi hili .                                                                       (alama 4)

SEHEMU YA .B : HADITHI FUPI 
Jibu swali la  2 au 3

  1. D.W .LUTOMIA                :  Msiba wa kujitakia   
    Wetu ni wetu ,hata akiwa mbaya …ni wetu.hatuna budi kuchagua yeye .lisilobudi hubidi.
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.                                                                            (alama 4)
    2. Fafanua vipengele vya kimtindo katika dondoo hii.                                               (alama 4)
    3. Hiari ya maamuzi ya wahusika mbalimbali yamewaletea madhila anuwai.jadili.(alama 12)
                                                         AU
  2. YUSSUF SHOKA HAMAD        :Mzimu wa Kipwerere     
    “Mbali na vitisho vya aina hii,mzimu wa kipwerere ulikuwa na miiko yake”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.                                                                         (alama 4)
    2. Fafanua sifa za msemaji wa maneno haya.                                                        (alama 4)
    3. Jadili miiko ya mzimu wa kipwerere kwa mujibu wa hadithi.                            (alama 4)
    4. Dondoa vitisho vinavyorejelewa kwa mujibu wa hadithi.                                 (alama 8) 

SEHEMU YA .C.   
BEMBEA YA MAISHA      (Timothy M.Arege)
Jibu swali la 4 au 5

  1. ”Lakini nilivyosema ,mungu hamwachi mja wake..”
    1. Eleza muktadha wa dondoo  hili.   (alama 4)
    2. Tambua sifa tatu za msemewa.   (alama 3)
    3. Eleza umuhimu wa msemaji wa maneno haya katika kukuza vipengele vifuatavyo.
      1. Ploti   (alama 4  )
      2. Maudhui    (alama 4)
    4. Kwa kurejelea tamthilia nzima eleza ukweli wa kauli “mungu hamwachi mja wake”.(alama 5)
                                                      AU
  2. Ukilazwa tayari unakuwa umeonja seli.Hata wahudumu wenyewe hawana mlahaka mwema .amri  na vitisho kama askari.Unashindwa kama uuguze moyo ama ugonjwa.Katika wodi hewa iliyojaaa harufu ya dawa imezagaa,vitanda vimesalimu amri mpaka shiti zikagura.Yaani hali nzima haikupi matumaini ya kutoka ukiwa bora.matumaini yanadidimia .Tumaini lako unaliweka katika sala.
    1. Tambua toni mbili katika kifungu hiki                                                                          (alama 2)
    2. Tambua aina moja ya taswira katika dondoo hili                                                           (alama 2)
    3. Kando na taswira chambua vipengele vingine vya kimtindo                                          (alama 6)
    4. Fafanua namna mandhari ya dondoo hili yalivyochangia kujenga tamthilia ya bembea ya maisha               (alama 10)

SEHEMU YA .D
CHOZI LA HERI   (Assumpta K.Matei)
Jibu swali la 6 au 7

  1. .‘’Amani iwe nanyi.’’
    ‘’Iwe pia nawe.’’
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.                                                  (alama 4)
    2. Onyesha kinyume kinachojotokeza katika kauli iliyopigiwa mstari kwa kuwarejelea   wanaolengwa na maneno haya.            (alama 16)
                                                      AU
  2. .‘’Wanawake ni viumbe wa kushangaza sana.Ya nini kuilea mimba kisha kuja kutupa matokeo ?’
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Eleza umuhimu wa anayeambiwa maneno haya kuijenga riwaya hii. (alama 4)
    3. Kwa kurejelea riwaya hii ,onyesha mchango wa wanawake katika kuzoroteka kwa Maisha yao (alama 12)

SEHEMU YA E
FASIHI SIMULIZI

  1. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali

    Heri ujue mapema
    Nasaba yetu haina woga
    Woga haumei kwetu,humea kwa kina mamaku.
    Tulichinja jogoo na fahali ili uwe mwanaume.

    Ah!kisu cha ngariba ni kikali ajabu.
    Iwapo utatikisa kichwacho.
    Uhamie kwa wasotabiri,
    Ama tukwite njeku.
    Mpwangu kumbuka hili,
    Wananume wa mlango wetu
    Si waoga kwa kisu
    Wao hukatwa mchana hadi usiku
    Wala hawalalamiki.

    Siku nilipokatwa
    Nilisimama tisti
    Nikacheka ngariba kwa tashtiti
    Halikunitoka chozi.

    Iwapo utapepesa kope
    Wasichana wa kwetu na wa mbali
    Wote watakucheka
    Ubaki ukinuna.

    Sembe umepokea
    Na supu ya makongoro ukabugia
    Sema unachotaka
    Usije kunitia aibu

    Maswali
    1. Taja na uthibitishe shughuli zozote za jamii ya wimbo huu.                            (alama 4)
    2. Ni nani mwimbaji wa wimbo huu na anawaimbia nani?                                  (alama 2)
    3. Huu ni wimbo wa aina gani? Thibitisha.                                                           (alama 2)
    4. Mwimbaji wa wimbo huu ana taasubi ya kiume .Thibitisha kauli hii.              (alama 2)
    5. Eleza wajibu wa nyimbo katika jamii.                                                               (alama 6)
    6. Ijapokuwa nyimbo ni nzuri ,zina ubaya wake.Thibitisha kauli hii .                  (alama 4)

MARKING SCHEME 

SEHEMU YA SHAIRI

  1.  
    1. ‘’Shairi hili linakatisha tamaa.’’Thibitisha kauli hii kwa mifano kutoka kwenye shairi.   (alama 3)       
      1. nyanyake nafsineni ameteseka hadi anatamani kukiomboleza kifo cha dhiki.
      2. Umaskini-mama yake nafsineni pamoja na wanakijiji ni maskini
      3. Kuteswa-wanyonge kama mama yake nafsineni wanateswa.
      4. Kuumia kazini-kidole cha nduguye nafsineni kinakatwa na mashini akiwa kazini.
      5. Kutolipwa fidia-nduguye nafsineni anakatika kidole akiwa kazini,lakini kampuni inamnyima fidia.
      6. Kufutwa kazi-nduguye nafsineni analia kwa kufutwa kazi kwa kutozalisha kama awali.
      7. Wakulima kulipwa pesa duni za mazao yao-falahi/mkulima analia kwa kulipwa pesa ukufi kwa mazao yaliyomlaza nje na kumvunja mgongo.
    2. Fafanua umuhimu wa aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili.(alama 2)
      1. Urudiaji wa neno-Neno  ‘naikumbuka ‘ limerudiwa mwanzo  ni mwa kila ubeti.
        Umuhimu :kutilia mkazo linalozungumziwa.
      2. Urudiaji wa mbinu ya lugha-swali la balagha limerudiwa mwishoni mwa kila ubeti.
        Umuhimu:kuonyesha toni ya shairi -toni ya uchungu.
    3. Bainisha nafsineni katika shairi hili.(alama 2)
      • Mtu aliyeshuhudia masaibu waliyoyapitia watu wa familia yake-nyanyaye,mamaye  na nduguye.
    4. Jadili umuhimu wa maswali ya balagha katika shairi hili.(alama 2)
      • Kuonyesha jinsi nyanya yake nafsineni alivyochoshwa na dhiki-’itakuwa lini nasi kuomboleza kifo cha dhiki? ‘’
      • Kuibua toni ya shairi -toni ya uchungu-kwa  mfano,’’itakuwa lini nasi kuomboleza kifo cha dhiki?’’
      • Kudadisi hali/kutaka kufahamu zaidi-’’lini  nasi tutawaimbia watutesao mbolezi za bundi?’’
      • Kuonyesha mshangao wa nafsineni kuhusu unyanyasaji unaoendelezwa dhidi ya wanyonge-’’lini itakuwa mirija ya wanyonyaji wafanyao watu mashine?”
    5. Tambua toni ya shairi hili.(alama 1)
      • Toni ya uchungu-’’lini nasi tutawaimbia watutesao mbolezi za bundi?’’
      • Toni ya kulalamika -’’lini jasho la upanzi na mavuno litawafaidi wachomwa na jua?”
    6. bainisha na uonyeshe umuhimu wa mistari ifuatayo katika shairi hili.
      1. Mistari kifu                                   (alama 2)
        • naikumbuka ,
        • siku milipofika kijijini n.k.
          Umuhimu :inatoa wazo kwa njia thabiti.
      2. Mistari mishata                           (alama 2)
        • na kumkuta nyanya kaketi chini ya ,
        • kuyaomboleza matanga ya
        • naikumbuka sauti ya
        • lini itakatwa mirija ya
          Umuhimu:Hutegemeana ili kuleta maana kamilifu ,kwa hivyo,hujenga muumano wa shairi/hujenga matumaini kwa msomaji ambaye huendelea kuisoma mistari inayofuata kusudi apate ujumbe kamilifu.
    7. Bainisha aina mbili za taswira zinazojitokeza katika shairi hili.(alama 2)
      1. Taswira ya uoni-nyanya akiwa ameketi chini ya mgunga
      2. Taswira sikivu-akiwasikiliza nyuni waliokuwa wakiimba kwa msisimko
      3. Taswira mwendo-nilipofika kijijini
    8. Fafanua muundo wa shairi hili           (alama 4)
      • Lina beti nne
      • Idadi ya mishororo inatofautiana katika kila ubeti
      • Kila mshororo una kipande kimoja isipokuwa ubeti wa tatu,mshororo wa saba wenye vipande viwili.
      • Kiishio ni tofauti katika kila ubeti.mfano
        ubeti 3:wanyonyaji wafanyao watu mashine?
        ubeti 4:litawafaidi wachomwa na jua?’’
      • Vina vinatofautiana katika kila mshororo.
        .………………………………………………………………………...ya
        ….………………………………………………………………………nga
        ….………………………………………………………………………mba
        ….………………………………………………………………………ni
        ….………………………………………………………………………ji
        ….………………………………………………………………………ma
        ….………………………………………………………………………ke
        ….………………………………………………………………………o
        ….………………………………………………………………………ndi
      • Mizani inatofautiana katika kila mshororo-Ubeti 2:
        ………………………………………………………………..…9
        …………………………………………………………………..11
        …………………………………………………………………..11
        …………………………………………………………………..12
        …………………………………………………………………..16
        …………………………………………………………………..11
        .…………………………………………………………………..5
        .………………………………………………………………….15
        .…………………………………………………………………..6
      • Kila kiishio kimekamilika kwa sw ali  la balagha

SEHEMU YA HADITHI FUPI

  1. Wetu ni wetu,hata akiwa mbaya …ni wetu.Hatuna budi kuchagua yeye .Lisilobudi hubidi.
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili                                                                   (alama 4)
      • Ni machoka akikumbuka kauli ya jirani yake zuhura kuwa wanafaa kumchagua mtu wao,awe mzuri au mbaya ,amesoma au la.
      • Machoka ameketi kitako kochini chumbani mwake
      • Baada ya kurejea kutafuta kibarua mchana kutwa bila mafanikio.anajuta kuhusu maamuzi waliyofanya kuchagua viongozi kwa kuegemea nasaba.
    2. Fafanua vipengele vya kimtindo katika dondoo hili                                       (alama 4)
      • Methali-lisilobudi hubidi
      • Mbinurejeshi/kisengera nyuma-machoka anakumbuka kauli ya jirani yake zuhura kuwa wanafaa kumchagua mtu wao ,awe mzuri au mbaya ,amesoma au la.anakumbuka hali ya sintohfahamu kati yake na  zuhura kutokana na misimamo yao hiyo,hali iliyoyeyushwa na dhiki baada ya uchaguzi.
      • Takriri-’’wetu ni wetu,hata akiwa mbaya ni wetu…
      • Kinaya -zuhura anamwambia machoka kuwa wanafaa kumchagua mtu wao,awe mzuri au mbaya.ajabu ni kuwa wao ndio wanateseka chini ya uongozi huo.
      • Hiari ya maamuzi ya wahusika mbalimbali yamewaletea madhila anuwai.Jadili.   (alama 12 )
      • Ugomvi kati ya zuhura na machoka ni msiba wa kujitakia.wanatofautiana kwa kuwa wana misimamo tofauti katika uchaguzi wa viongozi.Ajabu ni kuwa baada ya uchaguzi ,dhiki inawaleta pamoja kwani viongozi wenyewe hawawajibiki kwa vyovyote vile.
      • Kauli ya zuhura ni ithibati kuwa hali yao ni msiba wa kujitakia.anamwambia machoka kuwa wanafaa kumchagua kiongozi kwa ukoo wao hata kama hafai kwa kuwa ni mtu wao.sasa hivi,zuhura anajutia uamuzi wake huo kutokana na dhiki inayomkumba.
      • Machoka anakumbuka shairi la malenga mteule alilowahi kusoma mahali fulani.shairi hili linahusu msiba wa kujitakia.kibwagizo chake ni ‘’msiba wa kujitakia,kweli hauna kilio’’.linaoana na hali ilivyo katika jimbo la matopeni.linaongelea visanga vilivyojaa nchini watu wakifilisika.mtunzi anamwomba Rabana awafungue macho ili waweze kuona.
      • Machoka anapitia hali ngumu kimaisha .ametoka kutafuta kibarua lakini hajaambulia chochote ,hata cha kutia tumboni.wakazi wengine wa jimbo hili pia wanapitia hali ngumu kama hiyo.hali yao ni msiba wa kujitakia ,kwa kuwa wanafanya uchaguzi bila kuzingatia vigezo vinavyofaa kupata kiongozi anayefaa.
      • Wakazi wa matopeni wanaruhusu jimbo lao kugeuzwa ngome ya watu fulani wanaowania uongozi-wanarauka asubuhi na mapema kustahimili jua la mchana ili kuwapigia kura viongozi ,ambao baadaye wanawapuuza na kutojali matatizo yao.
      • Fumo matata anawakumbusha  wakazi wa matopeni  kuwa si busara kuwachagua viongozi kwa kuzingatia  koo,kwani hali hiyo  inaendeleza uongozi mbaya.Hata hivyo ,wanampuuza na kumteua sugu junior kuwa kiongozi.wanazidi kutaabika kutokana na mapuuza yao yao hata baada ya kuonywa.
      • Zuzu matata kukosa uongozi wa matopeni ni msiba wa kujitakia.anapendekezwa na walowezi kutwaa uongozi lakini anasisitiza kuwa lazima sugu senior kwanza aachiliwe kutoka gerezani.anapoachiliwa anakuwa maarufu  kumliko na kutwaa uongozi.Anakosa fursa nyingine ya kutwaa uongozi huo wa kubakia kuwa mpinzani wake hadi kifo chake.
      • Wananchi wanakubali kukandamizwa.wanatengewa upande wa kiwanja  ulio na jua huku viongozi wakitengewa upande wenye  hema  na kuongezewa vinywaji na ulinzi.wanakumbali kukaa  siku nzima wakimsubiri kiongozi wao huku wakiumizwa na jua hilo.
      • Sugu anakosa washirika katika hafla ya kuapishwa,licha ya kuwalipia nauli ya ndege viongozi wa majimbo jirani.Huu ni msiba wa kujitakia ,kwani hatilii maanani maslahi ya wananchi.anataka kuwatumbuiza viongozi kutoka nje kwa fedha za walipa ushuru.hali hii pia inatokana na ushindi wake anaopata kupitia mlango wa nyuma.
        (mtahini akadirie majibu ya mtahiniwa)
  2. ‘’mbali na vitisho vya aina hii ,mzimu wa kipwerere ulikuwa na miiko yake’’
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili                                                         (alama 4)
      1. Ni usimulizi wa  mwandishi
      2. Anasimulia kuhusu hali ya mazingira ya mzimu wa kipwerere
      3. Pia anaeleza sababu za watu kuogopa mzimu wa kipwerere
    2. Fafanua sifa za msemaji wa maneno haya                                         (alama 4)
      • Ni jasiri.badala ya kuogopa kutokana na sifa za mzimu wa kipwerere ,yeye anataka kujua zaidi kuhusu mzimu huo,hata ikigharimu maisha yake!
      • Ni mpelelezi.kila mara ana nia ya kujua kuhusu mzimu unaoogopwa na wanakijiji.anaukaribia kila mara na kutafuta mbinu za kuingia huko wakati mmoja ili kujua kilichopo.
      • ni mdadisi -kina anapopata sifa mpya ya mzimu wa kipwerere ,lazima aulizie kwa wazee.anaulizia sababu ya kuona taa huko usiku ,harufu ya tumbaku kutoka huko na sauti za chini kwa chini zinazosikika.
      • Ni mkakamavu-haachi nia yake ya kuwaona shetani wa mzimu. Licha ya yote anayoambiwa na wazee imani zinazowaogofya,anashikilia msimamo wa kuingia humo hadi anapotimiza azma yake.
      • Ni mwenye akili pevu-anawaza kwa haraka na kutekeleza mawazo.anaposikia watu wakija mzimuni,anazima tochi na kujificha chini ya kitanda.
    3. Jadili miiko ya mzimu wa kipwerere kwa mujibu wa hadithi                     (alama 4)
      • Miiko ya mzimu wa kipwerere ilikuwa ni mambo yaliyopigwa marufuku.
      • Mtu yeyote hakupaswa kupita eneo lile majira ya saa sita mchana na  usiku
      • Watu maalum kama wazee au wenye ushawishi Fulani ndio walioruhusiwa kuenda kwenye kichaka hicho
      • Lazima uimbe wimbo ndipo mizimu wakuruhusu uingie ndani
      • Lazima mizimu ikubali sherehe Fulani kijijini ndipo iweze kufanyika kama vile tohara,arusi na sherehe nyingine
        (mtahini akadirie majibu ya mtahiniwa)
    4. Dondoa vitisho vinavyorejelewa kwa mujibu wa hadithi                            (alama 8)
      • Wanajamii walitishiwa sana kuhusu chanzo cha mzimu huu wa kipwerere. mama mwenye nguvu za miujiza ndiye aliyezikwa hapa.
      • Walipewa vitisho kuwa mashetani ndio walioishi mle ndani
      • Vitisho dhidi ya mapatano ya wake na waume ilikuwa ni kichapo cha mwizi kiliwekwa kuwaogofya wanakijiji wasijue siri zao.
      • Watu walitishiwa kutotumia mihadarati kumbe inasambazwa na viongozi.
      • Kuonekana kwa mwanga wa taa wakati wa usiku mzimuni.
      • Kusikika kwa sauti ya watu-mwanamke na mwanaume wakati wa usiku wa mapema.
      • Harufu kali ya sigara au tumbaku au aina Fulani ya kileo kinachofanana na tumbaku kuhisika mzimuni.
      • Wananchi walihofia kuwepo kwa madhara endapo sherehe yoyote ingeendelezwa bila ya kukubalika kwa sherehe hizo na mizimu.
      • Watu kuhofia kutolewa kafara endapo wangevunja miiko iliyotawala msitu huo.
      • Mzimu kuzungukwa na makaburi ya watu mashuhuri.

SEHEMU YA BEMBEA YA MAISHA -TIMOTHY AREGE

  1. “Lakini nilivyosema, Mungu hamwachi mja wake..”
    1. Eleza mutadha wa dondoo hili                                           (alama4)
      1. Msemaji ni Dina
      2. Msemewa ni kiwa
      3. Nyumbani kwa Dina
      4. Dina anamwelezea Kiwa kuhusu maisha ya Sara na Yona ya awali kama vile walivyosemwa na jamii kwa sababu ya kukawia kupata mtoto lakini Mungu akajibu sala zao kwa kuwapa mtoto.
    2. Tambua sifa tatu za msemewa                                         (alama3)
      • Msemewa ni Kiwa Sifa zake:
      • Mvumilivu ~ Anakula chakula kidogo na anasema hali ya maisha imekuwa ngumu na kupata chakula  kingi ni adimu basi amejifundisha kuvumilia maisha jinsi yalivyo.
      • Amewajibika ~ Anaenda kumwona mamake ili kujua hali yake.
      • Mdadisi ~ Kiwa anamuuliza mama yake maswali mengi kuhusu familia ya Yona..    Mwenye utu ~ Anahimiza Dina aende akamsaidia Sara kwake nyumbani
      • Mwenye heshima ~ Anamheshimu mama yake na kushirikiana naye licha ya pato dogo analopata. Kupitia pato lake dogo, ameweza kubadilisha hali yao ya maisha pale nyumbani na kuinua maisha ya  Dina.
    3. Eleza umuhimu wa msemaji wa maneno haya katika kukuza vipengele vifuatavyo:
      1. Ploti                                                                                                                           (alama4)
        • Kupitia kwake tunatambua Yona hakuwa mlevi awali. Anatusaidia kujua yaliyojiri hadi Yona akawa mlevi chakari
        • Dina ndiye anatujuza maisha ya awali ya Sara yanayotusaidia kuelewa hali ya Sara ya sasa.
        • Kupitia kwake tunapata kujua namna Sara na Yona walivyoanza ndoa yao na kuishi vizuri
        • Kupitia kwa Dina tunatambua Sara na Yona walikosa watoto. Baadaye walisemwa Sana. (ploti)
        • Kupitia kwa Dina tunatambua namna wanajamii walivyoweza kuwasema Sara na Yona (ploti) kwa kukosa mtoto wa kuwarithi
        • Kupitia kwake tunajua kiwango cha maradhi ya Sara kwani Sara hawezi kufanya lolote.
        • Kupitia kwa tunafahamu ukatili wa Yona ~ Dina anasema alikuwa akimpiga Sara kipigo cha mbwa.
      2. Maudhui                                                                                                                           (alama4)
        • maudhui ya ulevi yanachimuzwa kwani Yona alisukumwa na maneno ya watu kwa kukosa mtoto wa kiume.
        • Isitoshe anawapamba wanaume wa kiafrika sifa za ubabedume , anasema wanaume wa kifrika hawawezi kusaidia wanawake hata kukiwa na shida (maudhui ya ubabedume yanajitokeza)
        • Maudhui ya atahri za ulevi~ anaeleza namna ambavyo Yona alikuwa akimpiga mkewe Sara kwa sababu ya kukosa mtoto wa kiume.
        • Maudhui ya utamaduni ~ Yona alikuwa akimpiga Sara kwa sababu ya kukosa mtoto wa kiume kwa sababu jamii ilikuwa inampa sifa mtoto wa kiume .
    4. Kwa kurejelea tamthilia nzima eleza ukweli wa kauli “Mungu hamwaachi mja wake.”  (alama5)
      • Sara na Yona wanakawia kupata mtoto lakini Mungu kwa wakati wake anawabariki na vilaika vyenye  akili pevu.
      • Yona na Sara wanasemwa na wanajamii kwa kukosa mtoto wa kiume lakini kupitia kwa maneno ya Kiwa tunaona ya kwamba hawa mabinti wa Yona wanashinda hata wanaume.
      • Yona na Sara wanamlea Neema kwa taabu na baadaye Neema anafanikiwa kisha kuwasaidia wazazi wake kwa njia mbalimbali kama vile kugharamia matibabu ya mamake Sara.
      • Asna anamwambia Sara kuwa zamani familia ya Dina walikuwa maskini lakini leo wana afadhali.
      • Neema anapopata ajali mbaya anamfanyia mpango na kuleta flying doctors na kumpeleka hospitali japo hakumjua. Isitoshe anagharamia matibabu yake.
      • Dina anamwambia Kiwa kuwa ingawa hali ni ngumu, bado hawajafikia pa kukosa mlo.
                                                                                 AU
  2. Ukilazwa tayari unakuwa umeonja seli. Hata wahudumu wenyewe hawana mlahaka mwema. Amri na vitisho kama askari. Unashindwa kama uuguze moyo ama ugonjwa. Katika wodi hewa iliyojaa harufu ya dawa imezagaa, vitanda vimesalimu amri mpaka shika zikagura. Yaani hali nzima haikupi matumaini ya kutoka ukiwa bora. Matumaini yanadidimia. Tumaini lako unaliweka katika sala.
    1. Tambua toni mbili katika kifungu hiki                                            (alama2)
      • Toni ya kutamauka ~ Yaani hali nzima haikupi matumaini ya kutoka ukiwa bora.
      • Toni ya huzuni ~ Matumaini yanadidimia. Tumaini lako unaliweka katika sala.
    2. Tambua aina moja ya taswira katika dondoo hili                          (alama2)
      • Taswira mnuso ~ hewa iliyojaa harufu ya dawa imezagaa
    3. Kando na taswira chambua vipengele vingine vya mtindo:          (alama6)
      • Utohozi ~ seli, shiti, wodi
      • Tashbihi ~ amri na vitisho kama askari   
      • Nahau ~ vitanda vimesalimu amri
      • Tashihisi ~ vitanda vimesalimu amri, shiti zikagura.
    4. Fafanua namna mandhari ya dondoo hili yalivyochangia kujenga Tamthilia Bembea ya Maisha (alama10)
      • Yanalinganisha huduma duni za afya kijijini na huduma bora za afya mjini.
      • Yanatusaidia kuelewa maudhui ya kutowajibika kupitia wahudumu wa hospitalini za mjini.
      • Yanachimuza maudhui ya uongozi mbaya hospitalini.
      • Yanachangia katika kuonyesha sifa za wahudumu wa hospitalini.
      • Yanachangia katika kuonyesha sifa za wahudumu wa hospitali za nyumbani (wazembe, dhalimu)
      • Yanachimuza matatizo yanayokumba hospitali za mashambani(uchafu, uhaba wa vitanda vizuri, shiti)    Yanajenga mtirirko wa vitushi Sara anapofika hospitalini kupata matibabu.
      • Yanakuza sifa za Asna kama mdaku.
      • Yanajenga sifa za Neema zinazjitokeza ~  mwadilifu. 
      • Yanakuza mtindo kupitia methali na dhihaka.

CHOZI LA HERI

  1. ‘’Amani iwe nanyi’’
    ‘’Iwe pia nawe’’
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.
      1. kauli ya kwanza ni ya kiongozi wa kidini
      2. Kauli ya pili ni ya wakimbizi
      3. Wamo katika msitu wa mamba
      4. Kiongozi wa kidini anawaslimu wakimbizi baada ya kuwaletea chakula cha msaada.              (alama 4)
    2. Onyesha kinyume kinachojitokeza katika kauli iliyopigiwa mstari kwa kuwarejelea wanaolengwa na maneno na maneno haya.
      1. Ukosefu wa chakula -Ridhaa anakula mizizi mwitu huku wengine wakila majani mwitu
      2. Kuishi vibadani-wanaishi kwa vibanda vilivyoezekwa kwa nyasi na kujengwa kwa udongo.
      3. Kupigania chakula-wakimbizi wanapigania chakula .mfano :Kaizari na aliyekuwa waziri wa fedha kitambo wanapigania chakula.
      4. Ukosefu wa maji  safi ya kunywa-wanakunywa maji chafu ya mto wa mamba na wanaanza kuugua homa ya matumbo inayoishia kuwaua baadhi yao.
      5. Ukosefu wa misala -hali hii inasabisha matumizi ya vyoo vya kupeperusha,hivyo kuishia kuchafua mazingira.
      6. Ukosefu wa nguo-vitoto vinacheza nje ya kambi vikiwa uchi.
      7. Kuuguza majeraha ya kuchomewa familia-ridhaa akiwa kambini anauguza jeraha la kuchomewa familia yake
      8. Kuuguza majeraha ya kubakwa-Lime na Mwanaheri wanauguza majeraha ya kubakwa wakiwa kambini
      9. Kufurushwa kwao-wana hasira kwa sababu ya kufukuzwa nyumbani kwao na raia wenzao
      10. Kudhoofika kiafya-umbo la Subira limeumbuka akiwa kambini kutokana na ukatili wa binanadamu wenzake
      11. Kukatizwa masomo -Lime na Mwanaheri wanakosa kuendelea na masomo kwa sababu ya mapingano baina ya makundi mawili ya kisiasa.
      12. Kuuguza jeraha la kuporwa-kaumu anateta kuwa kiduka chake alichokitegemea pamoja na aila yake kiliporwa na kugeuzwa majivu.
      13. Dhiki za kisaikolojia-wakimbizi kama kaizari wana dhiki za kisaikolojia kutokana na kushuhudia wana wake wakibakwa na subira kupata mkato wa sime.
      14. Hali ya kuwa mayatima-watoto wakimbizi hawawezi kuwa na amani kwa sababu walinda usalama wanaotumwa kudumisha usalama ndio wanaohusika katika mauaji ya wazazi wao.
      15. Ukosefu wa vijumba vya kutosha-hii ni kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi  kwa hivyo vijumba kushindwa kuhimili  wakimbizi waliongezeka kila kuchao.
      16. Kutoruhusiwa kuvuna mahindi-Lunga kutoka msitu wa mamba na serikali kabla ya kuvuna mahindi yake.
      17. Kufukuzwa kutoka kambini-baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kukamilika ,serikali inawafurusha wananchi kutoka msitu wa mamba .
        (mtahiniwa ajadili dhiki za wakimbizi kambini zinazowanyima amani)   kwa kila hoja tuza alama moja         (alama 16)
  2. ‘’Wanawake ni viumbe wa kushangaza sana .ya nini kuilea mimba kisha kuja kutupa matokeo yake?’’ (alama 4)
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.
      1. Haya ni maneno ya askari
      2. Anamwambia Neema
      3. Wako kwenye kituo cha polisi
      4. Anazungumzia kisa cha mwanamke aliyejifungua mtoto na kumtupa kisha akaokotwa na Neema na kumpeleka kwenye kituo  cha polisi.
    2. Eleza umuhimu wa anayeambiwa maneno haya katika kuijenga riwaya hii.(alama 4)
      1. Ni kielelzo cha dhiki wanazopitia wanawake wasiokuwa na uwezo wa kujifungua
      2. Neema anaendeleza maudhui ya uwajibikaji kwa kumpanga mwaliko na kumsaidia kujiendeleza kimasomo hadi chuo kikuu
      3. Anatumiwa kuendeleza maudhui ya utu-anakiokota kitoto kilichokuwa kimetupwa kwenye taka na kukipeleka kwenye kituo cha polisi
      4. Ametumiwa kudokeza matatizo yanayowakumba wanandoa .anajifungua kitoto bahati ni kinaaga kwa sababu ya sickle -cell.
      5. Anafunza mbinuishi ya uvumilivu kwani anavumilia kwa miaka kumi na mitano akijaribu kujifungua  ingawa hakufanikiwa
    3. kwa kurejelea riwaya hii,onyesho mchango wa wanawake katika kuzoroteka kwa maisha yao.(alama 12)     
      • Tuama anajipeleka kisiri na kupashwa tohara inayomfanya kupoteza damu nyingi .
      • Pete anakunywa dawa ya kuulia panya ili afe na kuishia kulazwa katika kituo  cha afya cha mwanzo mpya.
      • Sauna na kangara wanashiriki katika biashara haramu ya kuiba na kuuza watoto na kuishia kutiwa mbaroni na kufungwa.
      • Mamake sauna anamwonya mwanaye asiweze kutibua siri ya kutendewa unyama na Maya kwa hivyo kupalilia uovu unaomdhalilisha mwanamke.
      • Mama pete anazorotesha maisha ya pete kwa kumkatizia masomo na kumwoza kwa Fungo.
      • Kangara anawadhulumu wasichana wadogo kwa kuwaiba na kuwauza madanguroni wanakotumiwa na wanaume kama vyombo vya mapenzi.
      • Mavyaa wake Subira anamzoroteshea maisha kwa kumsingizia kuwa mwizi wa mali aliyoitafuta mwenyewe na kumrejelea kama muki.
      • Rehema anayazorotesha maisha ya Chandachema kwa kumtelekeza na kumuachia bibiye hali inayomfanya kuishia kufanya kazi katika shirika la Tengenea.
      • Zohali anawatoroka wazazi wake na kuhamia jijini anakotaabikia sana-anapigana na majitu yanayotaka kumnyanyasa kimapenzi
      • Wanawake wanajidharau-nyanyake Ridhaa anamueleza kua unyonge haukuumbiwa wanaume bali wanawake.
      • Baada ya subira kuhamia mjini Kisuka ,subira anaanza kunywa kinywaji kikali kinachoishia kumuua .
      • Mwekevu anawania uongozi wa wahafidhina ila wenzake wanaostahili kumuunga mkono ili aibuke mshindi wanajitenga naye.
      • Selume anahamia kambini baada ya kuhitilafiana kisiasa na wakweze anakopitia matatizo wanayopitia wakimbizi kama kukosa chakula .
      • Satua jiraniye chandachema anamdhulumu zaidi kwa kulalamikia matumizi mabaya ya sabuni hadi chandachema akaamua kuhama nyumbani kwake.
      • Badala ya kusoma ,Rehema anaanzisha uhusiano wa kimapenzi na mwalimu wake Fumba na kuishia kupachikwa mimba.
        (mtahiniwa ajadili vitendo vibaya vya wanawake vinavyoishia kuwadhuru wao wenyewe au kuwadhuru wanawake wenzao.

SEHEMU YA FASIHI SIMULIZI

  1.  
    1. Shughuli za kiuchumi
      • Ufugaji/wafugaji-anayeimbiwa wimbo alipozaliwa fahali alichinjwa.
      • Ukulima/kilimo-anaahidiwa shamba la migomba na maparachichi
        Mwanafunzi athibitishe 
                                                             (alama 2)
    2. .Ni nani mwimbaji wa wimbo na anamwimbia nani?
      • Mwimbaji-mjomba
      • Anayeimbiwa-mpwa(mtoto wa dadake mwimbaji)              (alama 2)
    3. Huu ni wimbo wa aina gani?Thibitisha
      • Wimbo wa tohara/nyiso-mpwake anatayarishwa kukabiliana na kisu cha ngariba
        Mwanafunzi athibitishe                                           (alama 2)
    4. Mwimbaji wa wimbo huu ana taasubi ya kiume-thibitisha kauli hii
      • Anaona kuwa waoga ni akina mama
      • Anasifu wanaume wa mbari yao kuwa si waoga
      • Akilia atachekwa na wasichana
      • Anaambiwa kuwa ni ‘’Ndume ‘’ akabiliane na kisu      (alama 2)
    5. Nyimbo zina wajibu gani katika jamii
      • Huwatayarisha wanapoenda kupashwa tohara
      • Hukashifu woga na kuhimiza ujasiri
      • Husawiri falsafa ya jamii.wanaume hawaogopi.
      • Huonyesha majukumu mapya ya wanaotiwa jandoni.
      • Hukuza na kuendeleza tamaduni na desturi za jamii
      • Huwaleta wanajamii pamoja
      • Hutumika kama nyenzo ya kuburudisha wanajamii.   (alama 6)
    6. Ijapokuwa nyimbo ni nzuri zina ubaya wake.Thibitisha kauli hii(ubaya wa nyimbo)
      • Huweza kuibua hisia za ukabila na utabaka
      • Hutumika kueneza propaganda /huchochezi baina ya wanajamii.
      • Kuna ukosefu wa maadili katika baadhi ya nyimbo.baadhi huwa na matusi ,vitendo vya ngono n.k
      • Baadhi ya nyimbo huwa ghali /huhitaji kiasi kingi cha pesa kununua au kutoa na kuzirekodi
      • Husabisha uzembe baina ya wanajamii
      • Nyimbo huweza kuwapumbaza watu.    (alama 4)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Sukellemo Joint Pre Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?